You are on page 1of 41

YALIYOMO

UTANGULIZI .............................................................................................vii

REJEA ........................................................................................................... ix

1. Maana ya familia kisheria ni nini? ............................................................ 1

2. Familia imegawanyika katika makundi mangapi? .................................... 1

3. Makundi hayo ni yapi? ............................................................................... 1

4. Kundi la kijadi limegawanyika katika makundi mangapi? ....................... 1

5. Kundi la kisasa la kifamilia ni lipi? ........................................................... 2

6. Kuna aina ngapi za familia? ...................................................................... 2

7. Ndoa ni nini? .............................................................................................. 2

8. Maana ya ndoa chini ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 iliyofanyiwa


marekebisho mwaka 2019 imetafsiriwaje? ............................................... 3

9. Ili kuwe na uhalali wa ndoa chini ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971


inapaswa kuzingatia vigezo gani? ............................................................. 3

10. Ni kesi zipi zinazohusishwa na maana ya ndoa chini ya sheria hii? ....... 3

11. Ikitokea mzazi au mlezi amemchagulia mtoto mwenza wake, sheria


inasemaje? ................................................................................................. 3

12. Ili ndoa iwe halali, ni mambo gani yanapaswa kuzingatiwa? ................. 3

13. Je, kabla ya muislamu kufunga ndoa anatakiwa afuate taratibu zipi? .... 5

i
14. Je, kwa upande wa wakristo wanatakiwa kufuata taratibu zipi wakati
wa kufunga ndoa? ...................................................................................... 6

15. Je ndoa isipofuata utaratibu wote ulioelezwa hapo juu itakuwa halali? . 6

16. Dhana ya ndoa ni nini? ............................................................................ 6

17. Mazingira gani yanayoonyesha kuwepo kwa dhana ya ndoa? ................ 6

18. Nani mwenye uwezo wa kupinga kuwa hakuna ndoa bali kuna dhana ya
ndoa? .......................................................................................................... 7

19. Mtu yeyote mwenye kupinga kuwa hakuna ndoa bali kuna dhana ya
ndoa anapaswa kuwa na ushahidi gani? .................................................... 7

20. Je, kwa ndoa zinazofungwa kimila ambazo hazihitaji kufanyika kwa
sherehe wala hakuna cheti cha ndoa kinachotolewa, sheria inasemaje ? . 7

21. Mtu anayesema kuwa wanaodhaniwa kuwa hawana ndoa halali wana
ndoa halali, anapaswa kuwa na ushahidi gani? ......................................... 7

22. Ni matokeo gani ya kuwa na ndoa dhania? ............................................. 8

23. Je, makosa yapi wayafanyayo watu wanapokuwa wanaishi kidhana ya


ndoa? .......................................................................................................... 8

24. Nani mwenye mamlaka ya kubatilisha ndoa? ......................................... 8

25. Je, mmojawapo kati ya wanandoa anaweza kubatilisha ndoa bila


kwenda mahakamani? ............................................................................... 9

ii
26. Ni mambo gani ambayo mahakama itayazingatia wakati wa
kubatilisha/kutengua ndoa iliyo batili toka mwanzo wa ufungaji wa ndoa
hiyo? .......................................................................................................... 9

27. Ndoa iliyofungwa halali inaweza kubatilishwa na mahakama, endapo


kutatokea mambo gani? ........................................................................... 10

28. Je, ni jambo gani litapelekea mahakama kutobatilisha ndoa iliyofungwa


halali hata kama kukitokea jambo linalopelekea kubatilishwa kwa ndoa
hiyo? ........................................................................................................ 12

29.Ni muda gani wa kuomba mahakama ibatilishe ndoa? .......................... 12

30.Ni madhara gani ambayo yatatokea endapo mahakama itabatilisha


ndoa? ........................................................................................................ 12

31. Je, ni mambo gani yatapelekea mtu kuweka pingamizi la zuio la


kuomba mahakama ibatilishe ndoa? ....................................................... 13

32. Je, pindi ndoa inapofungwa, wanandoa wana haki na wajibu gani? ..... 13

33. Haki za wanandoa kwa watoto ni zipi? ................................................. 15

34. Je, ndoa inapovunjika au wazazi wanapotengana, kisheria watoto


wanapaswa kukaa na nani? ..................................................................... 15

35. Je, maslahi ya watoto ni kama yapi?. .................................................... 15

36. Je, ni kesi zipi zingine zinazohusu ndoa ambazo mtu anaweza kupeleka
mahakamani? ........................................................................................... 16

iii
37. Mahakama inapofanya tathmini ya kutoa adhabu au fidia kwa mtu
aliyezini nje ya ndoa, itazingatia mambo gani?. ..................................... 17

38. Kesi za ndoa hupelekwa mahakama zipi?. ..................................... 17

39. Je, inawezekana kesi kupelekwa mahakama ya mwanzo kabla wahusika


hawajaanzia kwenye bodi ya usuluhishi ya ndoa? .................................. 17

40. Je, endapo bodi ya usuluhishi imesuluhisha wanandoa kitu gani


kitaendelea? ............................................................................................. 18

41. Endapo bodi ya usuluhishi itashindwa kusuluhisha mgogoro huo, ni


hatua gani zitafuata? ................................................................................ 18

42. Kwa nini Cheti kutoka bodi ya usuluhishi ya ndoa ni muhimu? .......... 18

43. Je, endapo mahakama itaamua kusikiliza maombi ya mwanandoa


mwenye kesi ya ndoa bila cheti kutoka bodi ya usuluhishi wa ndoa,
maamuzi hayo yatakuwa na nguvu kisheria? .......................................... 18

44. Je, kila kesi ya ndoa ni lazima ipitie bodi ya usuluhishi ya ndoa?. ....... 19

45. Je, bodi za usuluhishi za ndoa hupatikana wapi?. ................................. 19

46. Bodi ya usuluhishi ya ndoa inapaswa kuwa na wajumbe wangapi?. .... 20

47. Wajumbe hao ni akina nani? .................................................................. 20

48. Wajumbe hao wanatakiwa wasizidi wangapi?. .................................... 20

49. Bodi ya usuluhishi ya ndoa itakuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za


aina gani?.. ............................................................................................... 20

50. Bodi itatumia utaratibu upi wa kumuita mtu aje ajibu shitaka? ............ 21
iv
51. Endapo mtu aliyeitwa kujibu mashtaka amekataa wito, bodi itafanya
nini?. ....................................................................................................... 21

52. Je, mwanasheria au mtu yeyote anaweza kumwakilisha mtu mwingine


kujibu kesi kwenye bodi ya usuluhishi wa ndoa?. ................................. 21

53. Je, mahakama gani zingine zimepewa mamlaka ya kusikiliza kesi za


ndoa?. ...................................................................................................... 21

54. Kwenye ndoa mtu yeyote anayo haki ya kuomba mahakama imfanyie
mambo yafuatayo; .................................................................................. 22

55. Madhara ya kutengana ni yapi? ............................................................. 24

56. Mtu yeyote anayo haki ya kudai taraka, je mahakama itazingatia sababu
zipi ili iweze kutoa taraka kwa wanandoa? ............................................. 24

57. Endapo mwenza mmoja amefariki na wana ndoa halali, Je, mwenza
aliyebaki anaweza kuolewa au kuoa mtu mwingine bila kuomba
mahakama itoe amri ya kutambua kifo cha mwenza huyo na kubatilisha
ndoa hiyo?. .............................................................................................. 25

58. Kwa nini ni muhimu kuomba mahakama itoe amri ya kutambua kifo
cha mwenza kabla ya kufunga ndoa nyingine? ....................................... 25

59. Ni mazingira gani ambayo mahakama inaweza kuzuia au kutotoa amri


ya taraka kwa wana ndoa?. ...................................................................... 25

60. Ni mahakama pekee yenye mamlaka ya kutoa taraka?. ........................ 26

61. Nini dhana ya taasisi hizi kupewa mamlaka ya kutoa taraka? .............. 27

v
62. Kwa ndoa za kiislamu kuna utaratibu tofauti na ndoa za dini zingine au
ndoa za kimila linapokuja suala la kutoa taraka?.................................... 27

63. Endapo shekhe atataka kutoa taraka kwa wanandoa, atapaswa


kuzingatia mambo gani? .......................................................................... 27

64. Baada ya amri ya taraka ni kuvunjika kwa ndoa. Je, ndoa inapovunjika
nini athari zake? ....................................................................................... 28

65. Mahakama itakua na mamlaka gani baada ya ndoa kuvunjika? ........... 28

66. Mahakama haitogawa au kuuza mali za wataraka hadi pale


kutakapokuwa na mambo yafuatayo; ...................................................... 28

67. Kwenye kugawa mali, mahakama itazingatia mambo gani? ............... 29


68. Kuna maswali yamekuwa yakiulizwa, nani ni mama halali wa mtoto? 29
70. Je, kwa dhana ya kujifungua tu mtoto inatosha kuthibitisha kuwa yeye
ndiye mama halali wa mtoto?.................................................................. 30
71. Nani ni baba halali wa mtoto? ............................................................... 30
72. Nini maana ya dhana ya kisheria ya kwamba huyu ndiye Baba wa
mtoto?. ..................................................................................................... 30
73. Utapingaje mahakamani kuwa wewe si Baba halali wa mtoto? ........... 31
74. Je, ni watu gani wameruhusiwa kuomba mahakama itoe kibali cha
kupima vinasaba (DNA)? ........................................................................ 31
75. Masharti gani yamewekwa kabla ya mtu kutaka kupima vinasaba? ..... 32

vi
UTANGULIZI
Ndoa ni saklamenti kwa upande wa wakristo (Roman catholic), kwa
upande wa waislam ndoa ni mkataba. Kwa upande mwingine ndoa ni
muunganiko kati ya mwanaume na mwanamke waliokubali kuishi
pamoja kwa muda wote wa maisha yao.

Vitabu vya dini na sheria vinathibitisha hilo kuwa ndoa haipaswi


kuvunjika. Pamoja na kwamba ndoa ni agano la milele, lakini kuna
mazingira ambayo wanandoa wanaweza kujikuta hawako pamoja tena.

Migogoro mingi ya ndoa imekuwa ikitokea kwenye jamii zetu na wakati


mwingine wanandoa hao hawajui pa kuanzia linapokuja suala la taraka,
mgawanyo wa mali pamoja na haki za watoto waliopatikana ndani ya
ndoa au nje ya ndoa.

Kijitabu hiki kimeandaliwa kwa kuichambua sheria ya ndoa ya mwaka


1971 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 kwa kuiweka katika
lugha nyepesi ya Kiswahili kwa njia ya maswali na majibu ili kumsaidia
mtu wa kawaida kabisa ambaye hana uelewa wowote kuhusu sheria.
Kwa upande mwingine itakuwa inaguswa sheria ya mtoto ya mwaka
2009 marekebisho ya 2019, kwa sababu kuna mazingira ambayo sheria
hizi zitakuwa zinaingiliana.

vii
Baada ya kupitia jarida hili msomaji atapata uelewa mkubwa kuhusu
nini maana ya ndoa pamoja na mambo mengi yanayohusu ndoa na
baadae atajua utaratibu wa kufuata pindi ndoa yake inapofika mwisho au
kutoendelea tena kwa ndoa hiyo ikiwemo namna mahakama inapaswa
kugawa mali, kuuza, kutoa amri ya taraka na matunzo ya watoto (kama
walipatikana)
Shukrani za kipekee zimwendee Madam Mwasi Mbegu mhadhiri toka
Chuo Kikuu Cha Mt. Agostino Mwanza, yeye ni mtaalam wa sheria ya
ndoa ambaye amechangia kwa kiasi kikubwa mimi kuwa na ufahamu
mpana wa sheria ya ndoa na hatimaye kupelekea kuandaa kijitabu hiki
kwa ajili ya jamii.

ZINGATIA; Mabadiliko ya sheria hii ya ndoa nay a mtoto


yatakayotokea kuanzia mwaka 2025 na kuendelea kwenye baadhi
ya maeneo yatakuwa nje ya yaliyomo kwenye kijitabu hiki.

KUHUSU MWANDISHI; Laban Abas Mapabha

 Ana shahada ya sheria toka chuo kikuu cha Mt. Agostiono


Mwanza
 Stashahada ya Elimu toka chuo cha ualimu cha Mt. Maria
Tabata, Dar es salaam
 Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Inside Community
foundation (ICOM) yenye usajili no.00NGO/R/2820.

viii
REJEA
Dhana” kuamini kuwa jambo fulani au kitu fulani ni sahihi kabla ya
kutokuwa sahihi kwa jambo au kitu hicho.
Ibara” ni maneno yapatikanayo kwenye katiba yaliyotengwa kwa
namba kwa ajili ya ufafanuzi wa jambo fulani la kikatiba
Kifungu” ni maneno yapatikanayo kwenye sheria husika yaliyotengwa
kwa namba kwa ajili ya ufafanuzi wa jambo fulani la kisheria.
Kuasili” kitendo cha kumtunza au kumchukua mtoto ambaye si wako na
kumfanya wa kwako.
No 13” sheria ya mtoto ya mwaka 2009 marekebisho ya 2019.
No 29” sheria ya ndoa ya mwaka 1971 iliyofanyiwa marekebisho
mwaka 2019.

ix
1. Maana ya familia kisheria ni nini?
Maana ya familia kisheria hutofautiana kulingana na jamii na jamii au
koo, pia maana hubadilika kutokana na mambo yanayotokea katika
jamii na maendeleo yake.
Kutokana na sheria ya mtoto ya 2009 inasema familia ni baba, mama,
watoto pamoja na ndugu wa karibu kama Babu, mjomba, shangazi,
binamu, wapwa na wajukuu wanaoishi pamoja.

2. Familia imegawanyika katika makundi mangapi?


 Mawili

3. Makundi hayo ni yapi?


 Kudi la kijadi na Kundi la kisasa

4. Kundi la kijadi limegawanyika katika makundi mangapi?


Makundi matatu ambayo ni;

• Kundi ambalo mwanaume huwa na wake zaidi ya mmoja.


(kifungu cha 9(2) cha no 29)
• Kundi ambalo mwanamke huwa na mume zaidi ya mmoja na
• Kundi ambalo mwanaume huwa na mke mmoja. (kifungu cha 9(3)
cha no 29)

1
5. Kundi la kisasa ni lipi?
Ni kundi ambalo hujipatia familia nje ya utarabu wa kawaida mfano,
mtu mmoja anaweza kumuomba mtu mwingine amzalie mtoto bila hata
kushiriki tendo la ndoa.

6. Kuna aina ngapi za familia? Kuna aina mbili za familia ambazo


ni;
 Familia ambayo huongozwa na Baba kama kichwa cha familia
Familia ambayo huongozwa na Mama kama kichwa cha familia.

7. Ndoa ni nini?
Ndoa haina maana moja, ina maana kulingana na jamii inavyoipa
tafsiri. Pia inategemeana na chaguo la mtu kwa namna ambavyo
angependa kuitafsiri ndoa.

Wahindu wanaitafsiri ndoa kama muungano wa milele baina ya


wanandoa mpaka pale kifo kitakapo watenganisha.
Wakristo huamini ndoa ni tendo la Mungu na kwa waromani katholiki
huamini ndoa ni saklamenti takatifu
Kwa waislam wanaamini ndoa ni mkataba ambao huisha pale ambapo
mwenza mmoja kati yao hana uwezo wa kutimiza majukumu ya kindoa.
Wao wanaamini vyote kuwa ndoa ni tendo la Mungu (ibadat) na ni
tendo la mwanadamu (muamalat)

2
8. Maana ya ndoa chini ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 imetafsiriwaje?
Ni muunganiko wa hiari kati ya mwanaume na mwanamke ambao
wamekubali kuishi pamoja kama mke na mume kwa kipindi cha maisha
yao yote. (kifungu cha 9 cha no 29)

9. Ili kuwe na uhalali wa ndoa chini ya sheria ya ndoa ya mwaka


1971 inapaswa kuzingatia vigezo gani?
• Ndoa ni lazima ifungwe kwa hiari
• Ni lazima iwe kati ya mwanamke na mwanaume
• Wanandoa hao ni lazima wawe wamekusudia kuishi pamoja muda
wa maisha yao yote.

10. Ni kesi zipi zinazohusishwa na maana ya ndoa chini ya sheria


hii?
Ni kesi ambazo mara nyingi wazazi huchukua nafasi ya kuwachagulia
wanandoa watoto bila ya watoto wenyewe kupenda

11. Ikitokea mzazi au mlezi amemchagulia mtoto mwenza wake,


sheria inasemaje?
Ndoa hiyo inakuwa batiri mbele ya macho ya kisheria.

12. Ili ndoa iwe halali, ni mambo gani yanapaswa kuzingatiwa?


• Ni lazima wanandoa wawe na uwezo wa kuoana mfano, wanandoa
wanapaswa kuwa na umri wa miaka 18. (kifungu cha 13 cha no
3
29), isipokuwa sheria imetoa kinga au mbadala kwa wanandoa
ambao wanaoana chini ya umri huo ambapo wanandoa hao
wanapaswa kuomba ridhaa ya mahakama baada ya wanandoa hao
kuruhusiwa na wazazi wao (kifungu cha 13(2) cha no 29)
• Kusiwe na ndoa nyingine iliyokwisha fungwa huko nyuma,
isipokuwa kama ni ndoa inayofungwa kimila au kiislamu, kwa
sababu aina za ndoa hizi zinaruhusu ndoa nyingine kufungwa huku
kukiwa na ndoa nyingine. (kifungu cha 15 cha no 29)
• Isiwe ni ndoa baina ya wana ndugu na ndugu. Sheria imetaja
orodha ya wanandugu ambao hawapaswi kuoana mfano; Babu na
Bibi, Kaka na Dada, Mjomba au shangazi, Wapwa au vitukuu,
wazazi, wake wa wazazi, watoto wa kurithi na kadhalika. (kifungu
cha 14 cha no 29)
• Ndoa ambazo ni tofauti na za kimila ni lazima zitangazwe siku 21
kabla ya kufungwa kwa ndoa. Hii ni muhimu ili kuruhusu
mapingamizi kama yapo.(kifungu cha 23 cha no 29)
• Ndoa lazima iwe na mashahidi walio na umri wa miaka 18 na
kuendelea. (kifungu cha 27 cha no 29)
• Ndoa ifungwe sehemu ya wazi, kama ni ofisini iwe ofisi ya wazi
ya kuruhusu watu kuingia, kama ni kanisani iwe sehemu ya
kuabudu.
• (kifungu cha 28 & 30 cha no 29)

4
• vii. Kama ni muislam na ndoa inayofungwa ni ya mke wa pili na
kuendelea ni lazima mke au wake wa ndoa za awali waweke hiali.
(kifungu cha 38(1) (j) cha no 29).
• Wanaofunga ndoa ni lazima wawepo wote kimwili siku ya kufunga
ndoa. (kifungu cha 38(38)(1)(a) cha no 29)
• Ni muhimu wanandoa kufanya sherehe. Mfano;
• Ndoa ya bomani au ya kiserikali sherehe ishuhudiwe na msajiri
wa ndoa wa halmashauri ambayo ndoa ilifungiwa.
• Ndoa ya kimila, hii itasherehekewa kimila.
• Ndoa ya kikristo, isherehekewe katika kanisa wanakoabudu
wanandoa na ifungwe na mtu ambaye ana cheti au mamlaka ya
kufungisha ndoa.(kifungu cha 30(1) cha no 29)
• Ndoa ya kiislam, hii itasherehekewa kwa mujibu wa taratibu na
imani za kiislam. Sherehe au ndoa itafungwa na KADHI au afisa
ambaye ni muislam.(kifungu cha 23(3)(a) na 30(3) cha no 29)

13. Je, kabla ya muislamu kufunga ndoa anatakiwa afuate taratibu


zipi?
• Mwanaume apeleke pendekezo la nia ya kuoa kwenye familia
anapotoka mwanamke
• Mwanaume alipe MAHR, ambayo huwa kimfumo wa fedha,
thamani au kitu.

5
14. Je, kwa upande wa wakristo wanatakiwa kufuata taratibu zipi?
• Kila dhehebu la kikristo lina utaratibu wake kuhusu hatua za
kufuata kabla ya ndoa.
• Ndoa ifungwe na padre au mchungaji aliyepewa kibali au mamlaka
ya kufungisha ndoa. (kifungu 23(3) (b) cha no 29).

15. Je ndoa isipofuata utaratibu wote ulioelezwa hapo juu itakuwa


halali?
 Hapana, itakuwa batiri

16. Dhana ya ndoa ni nini?


Ni hali ya mume na mke au mume na wake kuishi pamoja kwa
kudhania kuwa wana ndoa halali kumbe si ndoa halali.

17. Mazingira gani yanayoonyesha kuwepo kwa dhana ya ndoa?


Ni pale ambapo;
• Wanandoa hawakuwahi kufanya sherehe ya ndoa
• Hawana cheti cha ndoa
• Watu wamekuwa wakiishi pamoja kama mume na mke kwa zaidi
ya kipindi cha miaka 2.
• Watu hao wamekuwa wakichukuliwa na jamii wanayoishi kama
mume na mke na wamepata hadhi hiyo kwa kipindi cha miaka 2 au
zaidi. (kifungu cha 160 (1) cha no 29).

6
18. Nani mwenye uwezo wa kupinga kuwa hakuna ndoa bali kuna
dhana ya ndoa?
Ni mtu yeyote mwenye mashaka na ndoa hiyo.

19. Mtu yeyote mwenye kupinga kuwa hakuna ndoa bali kuna
dhana ya ndoa anapaswa kuwa na ushahidi gani?
• Anapaswa kuthibitisha kuwa watu hao wanaodhani wana ndoa
halali hawakuwahi kufanya sherehe ya ndoa na hawana cheti cha
ndoa.
• Kama ni ya kiislam haijafuata utaratibu wa kiislam
• Kama ni ya kikristo haijafuata utaratibu wa kikristo
• Kama ni ya kiserikali haijafuata utaratibu wa kiserikali
• Kama ni ya kimila haijafuata utaratibu wa kimila

20. Je, kwa ndoa zinazofungwa kimila ambazo hazihitaji kufanyika


kwa sherehe wala hakuna cheti cha ndoa kinachotolewa, sheria
inasemaje ?
 Sheria itaangalia utamaduni wa jamii au kabila husika.

21. Mtu anayesema kuwa wanaodhaniwa kuwa hawana ndoa halali


wana ndoa halali, anapaswa kuwa na ushahidi gani?
Anapaswa kuonyesha kuwa watu hao walifuata taratibu zote za ndoa
kutokana na aina ya ndoa mfano, kimila au jadi, kikristo na kiislam

7
22. Ni matokeo gani ya kuwa na ndoa dhania?
• Endapo mkitengana mahakama haitatoa taraka
• Mali mlizopata kwa aina hiyo ya ndoa zitagawanywa kwa misingi
ya matunzo ya mwanamke na watoto tu. (kifungu cha 160(2) cha
no 29)

23. Je, makosa yapi wayafanyayo watu wanapokuwa wanaishi


kidhana ya ndoa?
• Inapotokea wanataka kuachana watu hao wamekuwa wakiomba
taraka mahakamani badala ya kuomba mgawanyo wa mali kwa
mali walizozipata kipindi cha aina ya ndoa hiyo.
• Wengine hudhani watoto wanaozaliwa ndani ya aina hiyo ya ndoa
hawana haki ya kutunzwa na kupata mali pindi aina hiyo ya ndoa
inapofika kikomo.
• Wanaoishi katika dhana hii ya ndoa hutumia mwanya wa kutaka
kuhalalisha aina hii ya ndoa kama ni ndoa halali.
• Watu hudhani mahakama inatengeneza aina nyingine ya ndoa.

24. Nani mwenye mamlaka ya kubatilisha ndoa?


Mahakama pekee ndiyo yenye mamlaka ya kubatilisha ndoa. (kifungu
cha 98(1) cha no 29)

8
25. Je, mmojawapo kati ya wanandoa anaweza kubatilisha ndoa bila
kwenda mahakamani?
 Hapana hana mamlaka hayo na haya ndiyo makosa ambayo watu
wengi wamekuwa wakifanya. Anamuacha mwenza wake
kinyemela na kufunga ndoa nyingine kabla ya kwenda
mahakamani kuomba mahakama itengue ndoa ya awali kwanza.

26. Ni mambo gani ambayo mahakama itayazingatia wakati wa


kubatilisha/kutengua ndoa iliyo batiri toka mwanzo wa ufungaji
wa ndoa hiyo?
Itabatilisha kwa maombi ya wanandoa au bila maombi kutokana na
sababu zifuatazo;
• Endapo wanandoa wamefunga ndoa iliyokatazwa kisheria mfano,
ndugu na ndugu, umri chini ya miaka 18 na kadhalika. (kifungu
cha 13 & 14 cha no 29)
• Endapo mtu amefunga ndoa ya pili kikristo huku akiwa na ndoa
halali ya kiislam au kimila. (kifungu cha 15 cha no 29)
• Kama ndoa imefungwa na padre au shekhe asiye na kibali cha
kufungisha ndoa huku mmoja au wote kati ya wanandoa hao
wanafahamu hilo.
• Ridhaa haikutolewa na mmoja kati ya wanandoa. (kifungu cha 16
cha 29)

9
• Endapo mmoja kati ya wanandoa hakuwepo eneo la tukio bila
ridhaa ya mashahidi kukubali kutokuwepo kwake.
• Kuwepo kwa mashahidi wasio na sifa. Mfano chini ya miaka 18
• Endapo ndoa hiyo imefungwa kwa mkataba wa muda mfupi au
kwa kipindi cha muda fulani. Maana sheria ya ndoa inatambua
kuwa ndoa ni ya milele.
• Endapo mtu ana ndoa ya kikristo au kiislam baadae akifunga ndoa
nyingine kimila au kikristo. (kifungu cha 38 (1) (a) – (j) cha no
29)
• Endapo ndoa ni ya jinsia moja.(kifungu cha 9(1) cha no 29)
• Kukosekana kwa ridhaa ya mke endapo mume kama ni muislam
anataka kuongeza mke mwingine

Angalizo, mahakama haibatilishi ndoa kwa mawazo ya mwanandoa


mmoja mfano, endapo mwanandoa alidhani anaolewa na tajiri baadae
akakuta ni masikini.

27. Ndoa iliyofungwa halali inaweza kubatilishwa na mahakama,


endapo kutatokea mambo gani?
• Endapo mmoja kati ya wenza si mkamilifu wa viungo mfano hana
sehemu za siri au hawezi kufanya tendo la ndoa.
• Ugonjwa wa akili

10
• Endapo mmoja kati ya wenza anasumbuliwa na magonjwa ya
kuambukiza au ya kurithi kama siko seli
• Endapo mke atazaa na mwanaume mwingine tofauti na mume
wake. Isipokuwa mwanamke hataomba mahakama ibatilishe ndoa
kwa kigezo cha mume wake kuzaa na mwanamke mwingine. Hapa
sheria iliweka upendeleo kwa upande wa mwanaume
• Endapo mmoja kati ya wanandoa atakataa kufanya tendo la ndoa
na mume wake
• Endapo mmoja kati ya wanandoa hajapata ridhaa kutoka kwa
wazazi wake au amri ya mahakama ya kumruhusu kuolewa endapo
yupo chini ya umri wa miaka 18. (kifungu cha 39 (a) i-iv) (b) na
(c) cha no 29)
• Maumbile kuwa makubwa au madogo tofauti na kawaida.
Isipokuwa kama kuna uwezekano wa kufanyiwa upasuaji na tatizo
likaisha haina haja ya kuomba mahakama ibatilishe ndoa hiyo.

11
28. Je, ni jambo gani litapelekea mahakama kutobatilisha ndoa
iliyofungwa halali hata kama kukitokea jambo linalopelekea
kubatilishwa kwa ndoa hiyo?
 Endapo mwanandoa ataendelea kuvumilia mapungufu au kosa la
mwenzake linalopelekea ndoa kuvunjika na asichukue hatua
yoyote ya kuomba mahakama ibatirishe /ivunje ndoa hiyo.

29.Ni muda gani wa kuomba mahakama ibatilishe ndoa?


• Mlalamikaji atume maombi mahakamani ndani ya muda wa
mwaka mmoja tangu kutokea kwa sababu ya kuvunja ndoa.
• Nje ya mwaka mmoja mahakama haitasikiliza maombi hayo
endapo hauna sababu ya msingi ya kutoomba ndani ya mwaka
mmoja.

30.Ni madhara gani ambayo yatatokea endapo mahakama


itabatilisha ndoa?
• Mali zilizopatikana ndani ya ndoa hiyo kabla ya kubatilishwa
zitagawanywa
• Watu hao wanakuwa huru na sheria itawatambua kuwa ni watu
ambao hawajawahi kufunga ndoa.
• (kifungu cha 98 (a) cha no 29)
• iii.Watoto watatambulika kuwa ni watoto halali waliopatikana
ndani ya ndoa kabla ya ndoa hiyo kutenguliwa na mahakama.

12
• Mahakama haitahalalisha vitu ambavyo vilifanyika haramu na
kuharamisha vitu ambavyo vilifanyika halali wakati wa ndoa.
• Maamuzi ya mahakama hayatozuia wanandoa hao kuwa mashahidi
kwa jambo lolote lililofanyika kipindi cha ndoa yao.
• Deni alilokopa mwanaume kipindi cha ndoa kwa ajili ya familia
litalipwa na wote

31. Je, ni mambo gani yatapelekea mtu kuweka pingamizi la zuio la


kuomba mahakama ibatilishe ndoa?
• Endapo mpeleka ombi amepeleka nje ya muda wa kisheria ambao
ni mwaka mmoja. Nje ya mwaka mmoja bila sababu ya msingi
atapoteza sifa za maombi yake kusikilizwa. (kifungu cha 97, 96
(1) (a) (i) cha no 29)
• Endapo mwenza ana ufahamu na tatizo au kosa la mwenzake na
amevumilia kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja bila kwenda
mahakamani kuomba taraka. (kifungu cha 96(a) (ii) cha no 29)
• Endapo mlalamikaji yeye mwenyewe ndiye chanzo cha kutoshiriki
tendo la ndoa. (kifungu cha 96 (a) (iii)

32. Je, pindi ndoa inapofungwa, wanandoa wana haki na wajibu


gani?
• Haki ya kupata kushiriki tendo la ndoa
• Haki ya kuishi pamoja. (kifungu cha 111 cha no 29)
• Haki ya kutumia jina la mwanaume kama ubini wa mwanamke
13
• Haki ya kuomba muishi tofauti bila ya kuathiri haki za watoto.
(kifungu cha 67 cha no 29)
• Haki ya mwanamke kutunzwa na mume wake. (kifungu cha 63(a)
cha no 29)
• Haki ya mwanaume kutunzwa endapo mwanaume huyo amepata
ulemavu au kapoteza kazi. (kifungu cha 63 (b) cha no 29)
• Haki ya kuishi kwenye nyumba ya ndoa pamoja na kushirikishwa
juu ya kuuza nyumba hiyo. (kifungu cha 59 (1) cha no 29)
• Haki ya kumiliki mali. (ibara ya 24 ya katiba ya 1977 na
kifungu cha 56 cha no 29)
• Wajibu wa kila mmoja kuwajibika kwenye makosa ya jinai
• Haki ya wana ndoa kuingia kwenye makubaliano ya kimkataba
ambayo ni ya kibiashara. (kifungu cha 11 cha sheria ya
mkataba)
• Wajibu wa kushitaki au kushitakiwa kila mmoja kivyake. (kifungu
cha 56 cha no 29)
• Wajibu wa kutokuwa shahidi wa mwenzie kwenye makosa ya jinai
isipokuwa yale makosa yahusuyo maadili na ngono kama ubakaji,
kupigana au kuharibu mali ya mwenzie. (kifungu cha 130 cha
sheria ya ushahidi)
• Wajibu wa kutotumia nguvu au kumuadhibu mwenzio. ( Kifungu
cha 66 cha no 29)

14
33. Haki za wanandoa kwa watoto ni zipi?
• Haki ya watoto kuishi na wazazi wote. (kifungu cha 57 cha no 13)
• Haki ya kutunzwa na wazazi wote wawili hata kama wameachana.
(kifungu cha 129 (1) cha no 13)

MUHIMU, ni wajibu wa mwanamke kuwatunza watoto endapo mume


wake amefariki au hajulikani alipo. (kifungu cha 8(1) cha no 13)

34. Je, ndoa inapovunjika au wazazi wanapotengana, kisheria


watoto wanapaswa kukaa na nani?
• Sheria inasema, watoto walio chini ya umri wa miaka 7
wataendelea kukaa na mama yao hadi pale watakapofikisha umri
wa miaka 8 na kuendelea. (kifungu cha 125 (3) cha no 29 na
kifungu cha 26 (2) cha no 13). Isipokuwa endapo kuishi na
mama kunaweza kupelekea hao kukosa mahitaji yao muhimu au
kuathiri makuzi yao, sheria inasema watoto hao watakaa na Baba
badala ya Mama. (kifungu cha 39 (1) cha no 13)
• Kama ni mapacha wasitenganishwe, lakini kama kuwatenganisha
ni kwa ajili ya maslahi yao basi ifanyike hivyo.

35. Je, maslahi ya watoto ni kama yapi?. (Kifungu cha 26 cha no 13)
• Elimu

15
• Chaguo lao la ni mzazi gani ambaye wamemchagua kuishi naye na
lifanywe na mtoto mwenye umri wa miaka 8 na kuendelea.
(Kifungu cha 125(2) cha no 13)
• Maoni ya mahakama kuwa ni mzazi yupi ambaye ana uwezo wa
kuwatunza watoto yatazingatiwa.
• Kuwatembelea wazazi wote wanapotaka kufanya hivyo.

36. Je, ni kesi zipi zingine zinazohusu ndoa ambazo mtu anaweza
kupeleka mahakamani?
• Kesi ya kuomba fidia endapo mtu amevunja ahadi ya kukuoa au
kuolewa. (kifungu cha 69 (1) cha no 29)
• Kesi za kuomba zawadi ulizozitoa kwa mtu ambaye amekataa
kukuoa au kuolewa kukiwa na ahadi kwamba mtakuja kuoana.
(Kifungu no 71 cha no 29)
• Kesi za kuomba haki ya kulipwa fidia endapo mwenza au
mchumba amekamatwa ugoni au kuna ushahidi wa kutosha wa
yeye kufanya uzinzi. (Kifungu cha 72 (1) cha no 29). Isipokuwa
endapo mlalamikaji ndiye aliyepelekea wewe kufanya hivyo, au
endapo maombi ya fidia yameambatanishwa kwenye maombi ya
taraka, hgaiana haja ya kuomba fidia.

16
Angalizo, adhabu hii haitampata mtu aliyeshiriki uzinzi na mke au
mume wa mtu, endapo mtu huyo hakujua au hana taarifa kama mtu
aliyezini naye ameoa au kuolewa.

37. Mahakama inapofanya tathmini ya kutoa adhabu au fidia kwa


mtu aliyezini nje ya ndoa, itazingatia mambo gani?. (kifungu cha
74 cha no 29)
• Utamaduni wa jamii ya wawili waliofanya hicho kitendo, kama
mila zao zinaruhusu haitahesabika kama ni kosa.
• Fidia iwe ya malipo na siyo adhabu
• Ijiridhishe kama mume na mke wanaishi pamoja. Kama walikuwa
wametengana kutakuwa hakuna kosa.

38. Kesi za ndoa hupelekwa mahakama zipi?.


• Huanzia kwenye bodi ya usuluhishi ya ndoa ambazo hupatikana
kwenye vijiji au kata, makanisani au misikitini.
• Baada ya bodi, kesi hupelekwa kwenye mahakama za kawaida.
(kifungu cha 76 cha no 29)

39. Je, inawezekana kesi kupelekwa mahakama ya mwanzo kabla


wahusika hawajaanzia kwenye bodi ya usuluhishi ya ndoa?
(kifungu cha 101 cha no 29)
 Hapana, kesi zote zitaanzia kwenye bodi ya usuluhishi ya ndoa.

17
40. Je, endapo bodi ya usuluhishi imesuluhisha wanandoa kitu gani
kitaendelea?
 Kesi itakuwa imeishia hapo na hakutakuwa na haja ya kwenda
mahakamani tena.

41. Endapo bodi ya usuluhishi itashindwa kusuluhisha mgogoro


huo, ni hatua gani itafuata?
 Bodi itatoa cheti cha kuonyesha kuwa wana ndoa walipitia bodi ya
usuluhishi ya migogoro ya ndoa na mgogoro wao umeshindikana

42. Kwa nini Cheti hicho ni muhimu?


 Ni muhimu kwa sababu hutumika kama kigezo cha kesi yako
kupokelewa kwenye mahakama za kawaida maana bila ya cheti
hicho maombi ya kesi yako hayatapokelewa. (kifungu cha 101
cha no 29)

43. Je, endapo mahakama itaamua kusikiliza maombi ya


mwanandoa mwenye kesi ya ndoa bila cheti kutoka bodi ya
usuluhishi wa ndoa, maamuzi hayo yatakuwa na nguvu kisheria?
 Hapana ni lazima mleta maombi aambatanishe na cheti cha
usuluhishi toka bodi ya usuluhishi ya ndoa.

18
44. Je, kila kesi ya ndoa ni lazima ipitie bodi ya usuluhishi ya ndoa?.
• Hapana, sheria imesema kuna mazingira ambayo si lazima kesi
ipitie bodi ya usuluhishi ya ndoa. Mazingira hayo ni kama
yafuatayo; (kifungu cha 101 cha 29)
• Endapo mleta maombi ana uhakika kuwa, mke au mume hajulikani
alipo
• Endapo mjibu maombi yupo nchi ya nje na hana uwezekano wa
kufika kwenye bodi kwa kipindi cha miezi sita (6)
• Endapo mjibu maombi kwa hiali yake amekataa kufika kwenye
bodi ya usuluhishi ya ndoa
• Endapo mjibu maombi amehukumiwa kifungo cha maisha au
hukumu ya miaka mitano (5) au amewekwa kizuizini kwa muda
unaozidi miezi 6
• Endapo mleta maombi amedai kuwa mjibu maombi anasumbuliwa
na ugonjwa wa akili
• Pale ambapo mahakama itagundua kuwa, kuna mazingira yasiyo
ya kawaida kwa bodi ya usuluhishi ya ndoa kuendelea kusikiliza
maombi hayo.

45. Je, bodi za usuluhishi za ndoa hupatikana wapi?.


(kifungu cha 102 (1) cha no 29)

 Hupatikana katika ngazi ya kata.

19
46. Bodi ya usuluhishi ya ndoa inapaswa kuwa na wajumbe
wangapi?.
 Inapaswa kuwa na wajumbe Sita (6)
(kifungu cha 103 (1) cha no 29)

47. Wajumbe hao ni akina nani?


• Mwenyekiti wa bodi
• Mtu yeyote aliyeteuliwa kuwa mjumbe wa bodi

48. Wajumbe hao wanatakiwa wasizidi wangapi?. (kifungu cha 103


(1) cha no 29)
 Wasipungue wawili na wasizidi watano akiwemo mwenyekiti wa
sita.

49. Bodi ya usuluhishi ya ndoa itakuwa na mamlaka ya kusikiliza


kesi za aina gani?. (kifungu cha 103 (1) cha no 29).
• Kesi ambazo mume au mke ni mkazi wa eneo au kata iliyopo bodi
hiyo na kama ni mume au mke ambaye mume au mke ni mkazi wa
nchi ya nje basi mume au mke awe ni mkazi wa kata iliyopo bodi
hiyo.
• Mume na mke ni lazima wawe wa jamii moja ambako bodi
imeanzishwa au ilipo.

20
ANGALIZO, kesi za kidini zianzie kanisani au msikitini, kesi za
kuanzia kwenye bodi ni zile za ndoa za kijadi au kimila.

50. Bodi itatumia utaratibu upi wa kumuita mtu aje ajibu shitaka?
 Itatumia utaratibu wa wito wa kawaida wa maandishi. (kifungu
cha 104(2) cha no 29)

51. Endapo mtu aliyeitwa kujibu mashtaka amekataa wito, bodi


itafanya nini?. (kifungu cha 104 (3) cha no 29)
 Bodi itaomba mahakama ya mwanzo au wilaya imuandikie wito
wa kuhudhuria kwenye bodi hiyo kwa muda na mahali
palipopangwa kusikilizwa kwa kesi hiyo.

52. Je, mwanasheria au mtu yeyote anaweza kumwakilisha mtu


mwingine kujibu kesi kwenye bodi ya usuluhishi wa ndoa?.
(kifungu cha 104 (8) cha no 29)
 Hapana, sheria imeruhusu ndugu na wanafamilia tu kuambatana
na mjibu maombi kuwepo au kuhudhulia kwenye bodi.
Wanasheria wameruhusiwa kumwakilisha mtu kuanzia
mahakama za mwanzo na kuendelea.

53. Je, mahakama gani zingine zimepewa mamlaka ya kusikiliza


kesi za ndoa?. (kifungu cha 76 cha no 29)
• Mahakama ya rufaa

21
• Mahakama kuu
• Mahakama ya hakimu mkazi
• Mahakama ya wilaya
• Mahakama ya mwanzo.
ANGALIZO, mahakama zote hapo juu zina mamlaka sawa za
kusikiliza kesi za ndoa isipokuwa mahakama ya mwanzo imepewa
mamlaka ya nyongeza ya kusikiliza kesi za ndoa zinazohusisha ndoa za
kijadi au kiislam endapo kesi ya msingi inahusiana na uzinzi.
Pia mahakama hizo zitakuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi zote za
ndoa zenye sifa zilizoanzia bodi ya usuluhishi ya ndoa.

54. Kwenye ndoa mtu yeyote anayo haki ya kuomba mahakama


imfanyie mambo yafuatayo; (kifungu cha 94 (2) (a) to (e))
• Kuomba mahakama ihalalishe au ibatirishe ndoa au sherehe
iliyofanyika au kufungwa nje ya nchi itambulike halali au si halali
ndani ya Tanzania.
• Kuomba mahakama ihalalishe kuwa, wazazi au Babu na Bibi wa
mtuma maombi, walifunga ndoa halali.
• Mahakama itambue kuwa ndoa ya mtuma maombi ilifungwa kwa
sheria za kimila au kiislamu kabla ya kutungwa kwa sheria ya ndoa
ya mwaka 1971
• Kuomba mahakama itambue ndoa iliyoharamishwa kwa sheria za
nje, itambuliwe kuwa ni ndoa halali kwa mjibu wa sheria za
Tanzania.
22
• Kuomba mahakama itoe amri kuwa, mwenza wake anadhaniwa
kuwa amefariki
• Angalizo, endapo mtu anayedhaniwa kuwa amefariki, lakini bado
hajafariki, mtu anayedhani amefariki na hajafariki atapaswa kukata
rufaa kwa muda wa siku 90. (kifungu cha 95 (1) cha no 29).

55. Mmoja kati ya wana ndoa anayohaki ya kuomba Mahakama


itoe amri ya kutengana na mwenza wake, je ni mambo gani
ambayo mahakama itazingatia kabla ya kutoa amri ya
kuwatendanisha?.
(kifungu cha 110 kikisomwa pamoja na 107(2) cha no 29)

Itazingatia kuvunjika kwa ndoa hiyo, sababu zikiwemo;


• Kuzini nje ya ndoa kwa mwenza mmoja na iwe zaidi ya mara moja
• Endapo mwenza mmoja atataka kumlazimisha mwenzie wafanye
tendo la ndoa kinyume na maumbile
• Ukatiri aidha wa kimwili,kiakili na kijinsia.
• Kukataa kushiriki tendo la ndoa
• Kupotea kwa mke au mume kwa zaidi ya miaka mitatu (3)
• Ridhaa ya kutaka kutengana baina ya wenza au kwa amri ya
mahakama
• Kifungo kwa mume au mke kwa zaidi ya miaka 5 na zaidi
• Kuugua akili ambako lazima kuthibitishwe na madaktari wawili
Endapo mmoja kati ya wanandoa atabadili dini au jinsia.

23
56. Madhara ya kutengana ni yapi?
• Huondoa wajibu wa kutimiza majukumu yote ya kindoa
• Ni utengano tu siyo taraka
• Ni makubaliano kati ya wanandoa japo kuna mazingira ambayo
mahakama huamua hivyo
• Haiondoi uwajibikaji wa kuwatunza watoto
• Haizuii mwenza mmoja kuwaona watoto mahali walipo na mzazi
mwenzie
• Kutengana ni kwa muda wanandoa wanaweza kurudiana.
(Kifungu cha 113 (1) cha no 29)

57. Mtu yeyote anayo haki ya kudai taraka, je mahakama


itazingatia sababu zipi ili iweze kutoa taraka kwa wanandoa?
• Kifo cha mwenza mmoja kati yao
• Endapo kuna amri ya mahakama ya kuonyesha kama kuna dhana
ya mume au mke kuwa huenda alikwisha fariki. (kifungu cha 161
cha no 29)
• Endapo kuna amri ya taraka iliyotolewa na mahakama. (kifungu
cha 110 cha no 29)
• Uzinzi
• Ukatili
• Kutelekezwa, ambapo viashilia vya kutelekezwa ni kama
ifuatavyo, kutoonekana kimwili kwa mume au mke, lengo la mume
24
au mke kupotea jumla bila sababu yoyote ya msingi wala ridhaa ya
mume au mke.

58. Endapo mwenza mmoja amefariki na wana ndoa halali, Je,


mwenza aliyebaki anaweza kuolewa au kuoa mtu mwingine bila
kuomba mahakama itoe amri ya kutambua kifo cha mwenza
huyo na kubatirisha ndoa hiyo?.
• Hapana, atatakiwa kuomba mahakama itoe amri ya kuthibitishwa
kwa kifo cha mume au mke wa awali kabla ya kuoa au kuolewa na
mtu mwingine.

59. Kwa nini ni muhimu kuomba mahakama itoe amri ya kutambua


kifo cha mwenza kabla ya kufunga ndoa nyingine?
 Kwa sababu kutofanya hivyo kutasababisha mahakama iendelee
kutambua ndoa ya awali na kutotambua ndoa ya utakayofunga na
mke au mume mwingine.

60. Ni mazingira gani ambayo mahakama inaweza kuzuia au


kutotoa amri ya taraka kwa wana ndoa?.
• Endapo mtuma maombi hana cheti kutoka kwenye bodi ya
usuluhishi wa ndoa cha kuonyesha kuwa kesi yake ilianzia huko.
(kifungu cha 106 (2) cha no 29)
• Endapo ndoa haijavunjika vipande vipande kiasi cha kuweza
kurekebishika
25
• Endapo wana ndoa hawajamaliza miaka miwili toka tarehe ya
kufunga ndoa, isipokuwa kwa sababu ambazo haziwezi kusubiri
muda huo na endapo zitasubili muda wa miaka miwili kuisha mleta
maombi atakuwa ameathirika zaidi. (kifungu cha 100 (2) cha no
29).
• Endapo mleta maombi ndiye mwenye makosa
• Endapo wana ndoa wamekubaliana kuomba taraka kwa ajili ya
kujipatia maslahi yoyote. (kifungu cha 87 cha no 29)
• Endapo wanandoa hao wamewahi kusameheana kwa makosa
yanayopelekea taraka au endapo mmoja wa wenza aliyafumbia
macho makosa ya mwenzake kwa kipindi cha muda wa zaidi ya
mwaka mmoja na wamekuwa wakiishi katika mazingira ya makosa
hayo. (kifungu cha 86 cha no 29)
• Endapo wenza wameambukizana tabia ya kufanya makosa kwa
kulipiziana, mfano uzinzi wa mwanaume ukapelekea na
mwanamke kuzini nje ya ndoa na wakaendelea kuishi hivyo kwa
muda wa zaidi ya mwaka mmoja. (kifungu cha 85 cha no 29)

61. Ni mahakama pekee yenye mamlaka ya kutoa taraka?.


• Hapana, sheria inatambua uwepo wa taasisi zingine zenye
mamlaka ya kutoa taraka, ambazo ni;
• Taasisi za kidini na za kimila au jadi

26
62. Nini dhana ya taasisi hizi kupewa mamlaka ya kutoa taraka?
• Ili kusaidia mahakama kufikia uamuzi sahihi wa kuvunja ndoa
zilizofungwa kwenye taasisi hizo.

63. Kwa ndoa za kiislamu kuna utaratibu tofauti na ndoa za dini


zingine au ndoa za kimila linapokuja suala la kutoa taraka. Je,
utaratibu huo ni upi?
• Mahakama kabla haijatoa taraka lazima ijiridhishe kama wanandoa
ni waislamu
• Mahakama lazima ijiridhishe kama wanandoa hao wamepitia
kwenye bodi ya usuluhishi ya ndoa na bodi hiyo imeshindwa
kutatua mgogoro huo
• Mahakama lazima ijiridhishe kuwa, mwanandoa au wanandoa
wamefanya jambo ambalo ni kinyume na taratibu za dini ya
kiislamu
• Mlalamikaji ni lazima awe ameomba shekhe atoe taraka. (kifungu
cha 107(3) cha no 29)

64. Endapo shekhe atataka kutoa taraka kwa wanandoa, atapaswa


kuzingatia mambo gani?
• Wanandoa sharti wawe waislam
• Endapo anayeomba taraka ni mwanamke, shekhe ataamua
mwanamke huyo alipwe kiwango cha pesa kwa madhara
aliyoyapata.
27
• Endapo anayeomba taraka ni mwanaume, shekhe ataamulu
zitolewe taraka tatu na mwanaume huyo atapaswa kuendelea
mahakamani kwa ajili ya kuomba mahakama itoe amri ya taraka.

65. Baada ya amri ya taraka ni kuvunjika kwa ndoa. Je, ndoa


inapovunjika nini athari zake?
• Wanandoa kwa kila mmoja atakuwa huru na sheria itatambua
kuwa wahusika hawakuwahi kufunga ndoa.
• Mahakama itagawa mali zilizopatikana kwa pamoja kipindi cha
ndoa au
• Mahakama inaweza kuamulu mali za waliokuwa wana ndoa
ziuzwe. (kifungu cha 166 (a) cha no 29)

66. Mahakama itakua na mamlaka gani baada ya ndoa kuvunjika?


• Kutoa amri ya taraka
• Kugawa mali za wataraka
• Kuamulu mali yoyote ya wataraka iuzwe kama ikiona inafaa.
(kifungu cha 114 cha no 29)

67. Mahakama haitogawa au kuuza mali za wataraka hadi pale


kutakapokuwa na mambo yafuatayo;
• Kuwe na taraka
• Lazima kuwe na maombi ya mmoja kati ya wataraka ya kuomba
mgawanyo wa mali
28
• Mali zitakazogawanywa ziwe zile ambazo zilipatikana kwa pamoja
kipindi cha ndoa
Angalizo, endapo kuna mali zilizopatikana kabla ya ndoa, baadae
zikaendelezwa baada ya ndoa, mali hizo nazo zitajumuishwa kwenye
mgao. (kifungu cha 114 (3) cha no 29)

68. Kwenye kugawa mali, mahakama itazingatia mambo gani?


• Itazingatia utamaduni wa jamii ambayo wataraka hao wanatoka
• Kiwango cha mchango wa wataraka hao kwenye kupata mali hizo,
kiwe cha fedha, mali au kazi
• Madeni yaliyokopwa na wataraka wote, haya ni lazima yalipwe
kabla ya mgawanyo au mali inapouzwa ni lazima yalipwe
• Itazingatia mahitaji ya watoto na mgawanyo sawa. (kifungu cha
114 (2) cha no 29)

69. Kuna maswali yamekuwa yakiulizwa, nani ni mama wa mtoto?


• Mama wa mtoto ni ambaye amejifungua mtoto huyo. Hii haina
ubishi, kwa sababu anayejifungua ndiye mama halali maana kuna
uhusiano mkubwa wa maumivu anayopitia wakati wa kujifungua.
• Kwa maendeleo ya teknolojia kuna mazingira ambayo mwanamke
analipwa kwa ajili ya kutunza ujauzito wa mtu mwingine.

29
70. Je, kwa dhana ya kujifungua tu mtoto inatosha kuthibitisha
kuwa yeye ndiye mama halali wa mtoto?.
• Ikitokea kuna mabishano kuhusu mama halali wa mtoto basi mtu
yeyote au kwa amri ya mahakama, itaamuliwa kipimo cha
vinasana yaani DNA.

71. Nani ni baba halali wa mtoto?


• Ili kujua nani baba halali wa mtoto, mambo yafuatayo yanapaswa
kuzingatiwa;
• Uhusiano wa kimaumbile na vinasaba
• Dhana ya kisheria ya kwamba huyu ndiye Baba halali wa mtoto.
Japo dhana hii inaweza kupingwa mahakamani.
• Endapo mtoto ameasiliwa. Baba aliyemuasili ndiye Baba halali wa
mtoto.

72. Nini maana ya dhana ya kisheria ya kwamba huyu ndiye Baba


wa mtoto?.
• Endapo mwanamke aliyeolewa amejifungua mtoto akiwa anaishi
na mwanaume huyo kama mume, mtu huyo atadhaniwa kuwa
ndiye Baba halali wa mtoto
• Endapo mwanamke alitunga mimba kabla ya kutengana na mume
wake, mtoto akizaliwa atatambulika kama ni mtoto wa Baba wa
zamani kabla hawajatengana

30
• Endapo jina la mtoto litakuwa ndio jina lililopo kwenye cheti cha
kuzaliwa cha mtoto
• Baba aliyekutana na mwanamke siku ya tarehe ya kutungwa kwa
mimba, huyo ndiye atakayekuwa Baba wa mtoto.
• Endapo wana ndoa wamefunga ndoa halali chini ya sheria hii
• Endapo Baba amesherehekea kuzaliwa kwa mtoto
• Kutangaza kwa umma kuwa wewe ndiye Baba halali wa mtoto
• Endapo vipimo vya DNA vimethibitisha kuwa, wewe ndiye Baba
halali wa mtoto. (kifungu cha 35 (a) to (e) cha no 13)

73. Utapingaje mahakamani kuwa wewe si Baba halali wa mtoto?


• Kwa kuonyesha ushahidi kuwa siku ambayo mimba ilitungwa
wewe hukuwepo au haukuwa na mwanamke huyo.
• Omba kibari cha mahakama kwa ajili ya kupima vinasaba (DNA)

74. Je, ni watu gani wameruhusiwa kuomba mahakama itoe kibali


cha kupima vinasaba (DNA)?
• Mtoto mwenyewe
• Mzazi
• Mlezi
• Afisa jamii yeyote
• Mtu yeyote mwenye maslahi na kutaka kujua nani mzazi halali wa
mtoto na atapaswa kuomba mahakama impe kibali cha kupima
vinasaba. (kifungu cha 13 cha no 13)

31
75. Masharti gani yamewekwa kabla ya mtu kutaka kupima
vinasaba?
• Vinasaba hupimwa kabla mtoto hajazaliwa
• Mtoto akizaliwa hakuna vipimo vya vinasaba hadi atakapofikisha
umri wa miaka 18. Japo kuna mazingira ambayo sheria au
mahakama itaruhusu kufanyika kwa vipimo vya vinasaba hasa pale
ambapo kutakuwa na ulazima wa kufanya hivyo.
• Vipimo vya vinasaba hufanyika kwa amri ya mahakama

ONYO; kisheria hakuna mtoto haramu. Kumekuwa na tabia ya


kuwanyanyapaa watoto wanaozaliwa nje ya ndoa. Mtoto atakuwa
na haki sawa na watoto waliozaliwa ndani ya ndoa kwa upande
wa Baba.

32

You might also like