You are on page 1of 17

Bwana Yesu asifiwe milele na

milele!
Leo nataka nikushirikishe
sehemu ya tatu, ya somo hili
tunaloendelea nalo wakati huu
wa Pasaka.
Somo hili lina kichwa
kinachosema: NGUVU ZA
MAOMBI KATIKA
KUSHUGHULIKIA MAWAZO NA
FIKRA PINGAMIZI DHIDI YA
MAPENZI YA MUNGU KWAKO.
Naamini ya kuwa, Yesu
alipokuwa Gethsemani
akipambana na mawazo
pingamizi, dhidi ya mapenzi ya
Mungu juu yake, alikuwa
anatufikiria na sisi.
Yesu alipokuwa anajiombea pale
Gethsemani, naamini alikuwa
anatuwazia jinsi
atakavyotutengenezea mazingira
ya kiroho yatakayotuhalalishia
tutumie ushindi wake, juu ya
mawazo pingamizi, ili katika
Kristo na sisi tupate ushindi wetu
dhidi ya mawazo pingamizi juu
ya mapenzi ya Mungu kwetu!
Hebu fikiria ingekuwaje, na sisi
tungefanyaje, kama Yesu
asingeshinda pambano lake
dhidi ya mawazo na fikra
pingamizi, juu ya mapenzi ya
Mungu kwake.
Tunamshukuru Mungu sana, kwa
kumsaidia na kumwezesha Yesu,
kushinda pambano lake lile dhidi
ya mawazo na fikra pingamizi,
juu ya mapenzi ya Mungu kwake.
Biblia inatujulisha ya kuwa, Yesu
aliposulubiwa msalabani, nasi
tulisulubiwa “pamoja” naye
(Wagalatia 2:20). Yesu alipokufa
pale msalabani, nasi tulikufa
“pamoja” naye (Wakolosai 2:20).
Yesu alipozikwa kaburini,
tulizikwa “pamoja” naye
(Wakolosai 2:12).
Tena, biblia inaendelea
kutujulisha ya kwamba, Yesu
alipofufuka, nasi tulifufuka
“pamoja” naye (Waefeso 2:6). Na
Yesu alipoketishwa mkono wa
kuume wa Mungu Baba
Mwenyezi, nasi tuliketishwa
“pamoja” naye (Waefeso 2:6).
Hayo yote ambayo Yesu
ametufanyia, yanakuwa yetu
kihalali, siku tunapompokea Yesu
moyoni kama Bwana na
Mwokozi, na kuupokea wokovu
huu mkuu aliotufanyia.
Hii inatupa kujua ya kuwa ushindi
tunaokuwa nao, ni kwa sababu:
“…katika mambo hayo yote
tunashinda, na zaidi ya kushinda,
kwa yeye aliyetupenda” (Warumi
8:31).
Ndiyo maana biblia inasema;
“hata wakati ule tulipokuwa wafu
kwa sababu ya makosa yetu;
alituhuisha pamoja naye, yaani,
tumeokolewa kwa neema”
(Waefeso 2:5).
Leo, tunapokumbuka kufufuka
kwa Yesu, na maana yake au
faida yake kwetu, tusisahau
uhalali na mbinu za kushinda
pambano dhidi yetu, lililopitia
katika mawazo pingamizi, ili
tusiyafanye mapenzi ya Mungu.
Jambo mojawapo linalotokea
unapookoka, ni Roho wa ufufuo
wa Kristo, kuingia ndani yako, na
“kuifufua” roho yako, iliyokuwa
“imekufa” kwa sababu ya dhambi
(Waefeso 2:5) na unazaliwa
mara ya pili (Yohana 3:3 – 7).
Fahamu hili ya kwamba:
Unapookoka – roho yako
iliyohuishwa pamoja na Kristo
(Waefeso 2:5), inapewa uhalali
na nguvu za kutawala na kumiliki
nafsi yake, na mwili wake, na
ulimwengu, na shetani!
Biblia inatujulisha ya kuwa, kwa
njia ya damu ya Yesu
iliyomwagika msalabani
tumefanyika “ufalme na
makuhani kwa Mungu wetu”; na
kwa sababu hiyo tunatakiwa
kumiliki kiroho na tunatakiwa
kutawala Kiroho “juu ya nchi”
(Ufunuo wa Yohana 5:9,10)
Hii ina maana ya kwamba – roho
yako kwa msaada wa Roho
Mtakatifu, inarudishiwa nguvu za
Mungu za kuongoza, huku
ikimiliki na kutawala!
Njia mojawapo inayotumika
katika ulimwengu wa roho,
kuongoza na, kutawala na,
kumiliki, ni kwa njia ya mawazo
na fikra.
Hii ni kwa sababu, mawazo na
fikra vikipokelewa moyoni mwa
mtu, vina nguvu ya kutengeneza
misimamo ya aina ya maisha ya
mtu. Ndiyo maana imeandikwa
ya kuwa: Maana aonavyo nafsini
mwake, ndivyo alivyo (Mithali
23:7)
Hiki ndicho kilichofanyika katika
bustani ya Edeni, wakati shetani
alipowawekea akina Adamu,
wazo pingamizi katika fikra zao,
na wakaacha kuyafanya mapenzi
ya Mungu (2 Wakorintho 11:3)
Pia, ndicho shetani alichofanya
kwa kushirikiana na mwili, pale
katika bustani ya Gethsemani,
kuachia wazo pingamizi ndani ya
fikra za Yesu, ingawa Yesu
aliyashinda mawazo yale kwa
njia ya
maombi ya muda mrefu
(Mathayo 26:36 – 46).
Wakristo wa Kanisa la Galatia
walipata pambano kama hilo, la
kupewa mawazo pingamizi kwa
kupitia kwenye mapokeo ya dini
yao, yaliyokuwa yanapingana na
mapenzi ya Mungu kwao
(Wagalatia 5:13, 16 – 25).
Mtume Paulo alipoona hali yao
inabadilika, akawauliza maswali
kadhaa yafuatayo:
Enyi Wagalatia msio na akili, ni
nani aliyewaloga, ninyi ambao
Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele
ya macho yenu ya kuwa
amesulubiwa? Nataka kujifunza
neno hili moja kwenu, Je!
Mlipokea Roho kwa matendo ya
sheria au kwa kusikia
kunakotokana na imani? Je!
Mmekuwa wajinga namna hii?
Baada ya kuanza katika Roho,
mnataka kukamilishwa sasa
katika mwili? (Wagalatia 3:1 – 3)
Mtume Paulo akaamua kutumia
mbinu ya
kuwaombea wakristo wa Galatia,
maombi ya mzigo na ya muda
mrefu, “mpaka Kristo aumbike”
ndani yao (Wagalatia 4:19)
Kwa njia ya maombi ya jinsi hii,
mtume Paulo alikuwa anatumia
maombi, kusulubisha miili ya
Wagalatia kiroho pamoja na
mawazo yake (Wagalatia 5:24).
Na pia, kwa njia ya maombi,
Mtume Paulo kwa jinsi ya Kiroho
– alikuwa anausulubisha
“ulimwengu” na mawazo yake
kwa Wagalatia; na alikuwa
anawasulubisha Wagalatia kwa
ulimwengu (Wagalatia 6:14).
Maombi ya jinsi hii ukiyafanya
mara kwa mara, na kwa muda
mrefu, yanakusaidia kupata vitu
vingi, na baadhi yake ni hivi
vifuatavyo:
(i) Utauvua utu wa kale, ili uvae
utu mpya ili ufanane na Kristo
(Waefeso 4:22 – 24 na
Wakolosai 3:9, 10).
(ii) Uvue kiburi, ili ujivike
unyenyekevu wa
Kristo (1 Petro 5:5–8
(iii) Uvue utayari usioletwa na
injili ya amani au neno la Mungu,
ili uvae utayari uletwao na injili ya
amani (Waefeso 6:15).
(iv) Uvue hofu katika mawazo
yako, iliyoletwa na mlango wa
“udhaifu” ulionao, na badala yake
udhaifu ulionao upitishe na
kudhihirisha “nguvu za Mungu”
(2 Wakorintho 13:4 na 2
Wakorintho 12:9, 10, na 1
Wakorintho 1:18).
Ndiyo maana Yesu alipomfufua
Lazaro, alifufuka na akatoka
Kaburini akiwa bado
“amefungwa” miguuni na
mikononi, na uso wake (Yohana
11:44). Yesu akatoa agizo kwa
waliokuwepo pale kaburini, kuwa
wamfungue ili aweze kwenda
zake.
Hii inatupa kujua kuwa ingawa
alikuwa amefufuka, Lazaro
asingeweza kwenda vizuri
alikotakiwa kwenda, pasipo
macho yake, na miguu yake, na
mikono yake kufunguliwa!
Vivyo hivyo, mtu anapookoka,
kuna vitu vinavyoweza kumfunga
Kiroho, na kumzuia asiende
katika mapenzi ya Mungu
ipasavyo.
Kumbuka – kama Mtume Paulo
alivyowafanyia Wagalatia –
maombi ya mzigo na ya muda
mrefu yanaweza kumfungua mtu
toka kwenye vifungo vya
mawazo pingamizi, dhidi ya
mapenzi ya Mungu kwake.
Mungu akubariki sana, na uwe
na sikukuu njema ya Pasaka.

You might also like