MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA),
imezindua klabu ya wanafunzi ijulikanayo kama Sumatra Club itakayotoa mafunzo na mbinu zitakazowawezesha wananfunzi kutambua haki zao katika huduma ya usafiri. Klabu hiyo itaongozwa na kauli mbiu isemayo, Mtetezi wa haki, maslahi na wajibu wa abiria. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa klabu hiyo uliofanyika kwenye viwanja vya sabasaba, mwenyekiti wa Baraza la watumiaji wa barabara na aliyekuwa mgeni rasmi kwaniaba ya mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam, Ayoub Omar amesema kuanzishwa kwa vilabu vya Sumatra mashuleni kutasaidia kutoa elimu kwa wanafunzi ili wajue haki zao katika huduma ya usafiri. Sumatra imeamua kuanzisha vilabu hivi mashuleni ikiwa na lengo la kutoa elimu kwa wanafunzi watambue haki zao katika huduma ya usafiri na wajue namna ya kutatua matatizo wanayokumbana nayo katika vyombo vya usafiri, alisema Omar. Aliongeza kuwa, Kwa muda mrefu wanafunzi wamekuwa wakipata tabu kwenye vyombo vya usafiri na kunyanyaswa na madereva na makondakta wasio waadilifu. Lakini kupitia vilabu hivi watapatiwa mafunzo yatakayowapatia mbinu ya kupambana na changamoto hizo kisheria. Alisema hadi sasa wameshazindua vilabu vya Sumatra katika mikoa nane na mkoa wa Dar Es Salaam ni mkoa wa tisa ambayo tayari wanafunzi wake wataanza kupata mafunzo hayo ya haki ya mtumiaji wa vyombo vya usafiri nchi kavu na majini.
Wanafunzi wamekuwa wanungunikaji kwa muda mrefu lakini sasa
tunataka wawe walalamikaji kwa kufuata sheria na haki walizonazo katika huduma za usafiri. Tunaimani kuwa vilabu hivi vitakuwa suluhisho la wanafunzi kupata tabu na kunyimwa haki zao katika vyombo vya usafiri, alisema Omari. Kamanda wa polisi kikosi cha usalama barabarani Taifa, Johansen Kahatamo amesema jeshi la polisi kwa kushirikiana na Sumatra pamoja na wanafunzi wenyewe wataweza kumaliza changamoto ya usafiri kwa wanafunzi kama vilabu hivi vitasimamiwa vizuri. Tatizo la usafiri kwa wanafunzi litapungua na kuisha iwapo tutasimamia vyema vilabu vyetu. Niwaombe wanafunzi wawe waadilifu na watiifu wa sheria, msiwe chanzo cha vurugu kwenye vyombo vya usafiri. Kuweni watatuzi wa matatizo, alisema Kahatamo. Aliahidi kuwa jeshi la polisi litamshughulikia mtu yeyote atakayevunja sheria au kuwanyanyasa wanafunzi. Mtu atakayevunja sheria lazima tutamshughulikia kwa mujibu wa sheria. Kama wanafunzi mtakumbana na matatizo chukueni namba za magari husika na kuripoti kwa polisi kupitia kwa wazazi wenu. Wazazi wapige namba ya polisi 0682 887722 na jeshi la polisi litachukua hatua za kisheria kufuatilia gari husika, alisema kahatamo. Uanzishwaji wa vilabu hivi imeelezwa kuwa ni moja ya mbinu iliyobuniwa na baraza la watumiaji wa barabara ili kukabiliana na changamoto ya usafiri kwa wanafunzi. Kila mkoa utakuwa na vilabu vyake vya Sumatra kwa utaratibu utakaowekwa na mikoa husika.
Kwa upande wao wanafunzi wameeleza kuridhishwa na uanzishwajki wa
vilabu mashuleni na kusema vitasaidia wao kuthaminiwa katika vyombo vya usafiri kama abiria wengine. Mathias Kondrad mwanafunzi wa kidato cha tano kutoka shule ya sekondari Kibasila amesema, Nimefurahi sana kuanzishwa kwa vilabu hivi, tunaimani nasi sasa tutathaminiwa kama abiria wengine. Tumekuwa tukichelewa shule kwa kukataliwa na hata kupigwa na makondakta ili tusipande magari yao. Lakini sasa hivi tutatumia sheria kudai haki yetu ya msingi kama abiria, alisema Kondrad. Mwisho.