You are on page 1of 3

MAPENDEKEZO KWA DK.

JAKAYA KIKWETE, RAIS WA


JAMHURI YA MAUUNGANO WA TANZANIA KATIKA KIKAO
CHAKE NA WAWAKILISHI WA CHAMA CHA ALBINO
TANZANIA, IKULU, TAREHE 5/3/2015 JUU YA NAMNA YA
KUSAIDIA KUKOMESHA MAUAJI, UKATAJI VIUNGO,
UTEKAJI NA UKATILI DHIDI YA WATU WENYE UALBINO
NA FAMILIA ZAO
Mh. Rais,
Kutokana na kuendelea kushamiri kwa mauaji, ukataji viungo,
utekwaji na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino na familia
zao, Chama Cha Albino Tanzania kina mapendekezo
yafuatayo kwako:
1. Ushughulikiwaji wa kesi zinazohusiana na mauaji, ukataji
viungo, utekwaji na ukatili wa aina hiyo kwa watu wenye
ualbino upewe kipaumbele, kupitia mkakati maalum,
kwamba:
a. Mashauri
yote
ambayo
hayajapelekwa
mahakamani uchunguzi na upelelezi ukamilishwe
mapema na yapelekwe mahakamani;
b. Kesi zilizoko mahakamani zisikilizwe mapema,
kupitia mahakama au utaratibu maalum na kwa
watakaokutwa na makosa hukumu itekelezwe mara
moja;
c. Kuwepo mpango maalum wa kufuatilia kesi hizi,
hasa kupitia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora, ili kutoa msaada wa kisheria ikiwemo kwa
wale ambao hawajaridhishwa na maamuzi ya
mahakama waweze kukata rufaa.
2. Ulinzi shirikishi katika jamii uimarishwe katika ngazi
zote, kuanzia ngazi ya vijiji au mitaa zijengewe uwezo ili
ziwe na mipango maalum ya kutoa ulinzi kwa watu
wenye ualbino kwa kushirikiana na jamii kwani pia wao
ndio wanaowatambua wageni na kupitia wao ni rahisi
hata kupata ushahidi katika kesi mbalimbali. Ni rahisi pia
kupitia kamati hizi kuzitambua kaya zilizoko katika
mazingira ambayo sio salama na kufanya uraghbishi,
ikiwemo kuzihamishia katika makazi salama.

3. Serikali iwe na mkakati maalum, endelevu na shirikishi


wa kuelimisha jamii juu ya ualbino na haki za binadamu
na mpango huu wa elimu kwa jamii uwe na bajeti
maalum ambayo itakuwa vyema kwa kuanzia ijadiliwe
katika bunge lijalo la bajeti;
4. Wahanga wa matukio haya wakiwemo watoto wasaidiwe
ili kuboresha maisha yao na kuwajengea misingi mizuri
ya maisha ya baadae:
a. Watoto walio katika kambi wasaidiwe kupata
mahitaji yao ya msingi kama vile chakula, afya,
malazi na mavazi kupitia serikali;
b. Kambi hizi ziangaliwe kwa namna pana, ikiwa ni
pamoja na kuwapa mafunzo kupitia vyuo
mbalimbali vijana walioishi kwa muda mrefu
kambini ili waweze kujitegemea na pia kupunguza
athari nyingine zinazoweza kutokea,ikiwemo
mimba na udhalilishwaji wa kingono kama
ambavyo imekuwa ikiripotiwa katika taarifa
mbalimbali;
c. Watu wazima wanaoishi katika kambi hizi
wasaidiwe kuishi maisha ya staha, ikiwemo kupata
ajira japo ndani ya kambi hizo hizo ili waweze
kujikimu na kutoa mchango wao kwa kuwatunza
watoto wakati huu ambao hawawezi kurudi
nyumbani;
d. Wale waliopata ulemavu au kujeruhiwa serikali
iwasaidie waweze kujimudu. Kuna ambao maisha
yao yamekuwa ya magumu sana kwa mambo
mengi hivyo kuwa mzigo mzito kwa familia zao
ambazo nazo nyingi ni masikini;
e. Kambi hizi zisichukuliwe kama za kudumu,ila
zijengewe mazingira ya kutoa elimu jumuishi,
kuanzia elimu ya awali;
f. Wahanga na familia zao wapewe ushauri
(counseling) kwani wengi huwa wanaathirika sana
kisaikolojia na hapajawa na mkakati wa
kuwafuatilia.
5. Kwa kuwa mauaji yanayoendelea yanatokana na imani
za kishirikina, na katika matukio waganga wa kienyeji

wanahusika, Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala


pamoja na Sheria ya Uchawi zipitiwe upya, zifanyiwe
maboresho ili kuweza kutofautisha vizuri juu ya aina hizi
za tiba au huduma, na jamii ishirikishwe katika uratibu
wa shughuli za waganga wa tiba mbadala au tiba asili.
6. Kiundwe Kikosi Kazi maalum kufanya uchunguzi wa kina
kubaini wanaotuma na wanaoununua viungo vya watu
wenye ualbino ili washughulikiwe na kuondoa kabisa
jambo hili ambalo limekuwa na kadhia kubwa kwa watu
wenye ualbino, familia zao na jamii na Taifa kwa ujumla.
7. Itengenezwe kanzidata (database) kwa watu wenye
ualbino kote nchini ambayo itakuwa na taarifa
mbalimbali (demographic information), zikiwemo idadi
na mahali (makazi); jinsi na umri; elimu na ajira na; hali
ya saratani ya ngozi, ili kuisaidia serikali na wadau
wengine waweze kupanga na kutekeleza mikakati
mbalimbali ya ulinzi na jinsi ya kuboresha maisha ya
watu wenye ualbino kwa ustawi wa jamii na maendeleo
ya Taifa letu.
8. Tunapendekeza kukawepo na Kamati Maalum ya Kitaifa,
ambayo ni jumuishi, iwe inakutana kwa vipindi maalum
(mara kwa mara) kila mwaka kujadili, kutoa mrejesho na
kuishauri serikali na wadau wengine. Kamati hii iwe chini
ya Ofisi ya Rais au Makamu wa Rais au Waziri Mkuu ili
iwe rahisi kuratibu mambo yake kwa kushirikiana na
Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu. Kwa kuanzia,
kamati hiyo pia ifuatilie utekelezaji wa mapendekezo
haya kama ambavyo utaona yafaa, Mh. Rais.
Mh. Rais tunakushukuru sana kwa kutusikiliza. Mapendekezo
haya na mengine yatakayochangiwa na wadau yatasaidia
kukomesha mauaji na kuwafanya watu wenye ualbino na
familia zao kuishi kwa amani kama watu wengine. Utayari
wetu wa kushirikiana nawe na serikali yetu kama ambavyo
tumekuwa tukifanya wakati wote hauhitaji msisitizo.
______________
Ernest N. Kimaya
Mwenyekiti wa Chama Cha Albino Tanzania

You might also like