Maelezo Binafsi Ya Mhe. Zitto Zubeir Kabwe

You might also like

You are on page 1of 7

MAELEZO BINAFSI YA MHE.

ZITTO ZUBEIR KABWE, MB


KUHUSU UANACHAMA WAKE KATIKA CHAMA CHA
DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) NA HATMA YAKE
KAMA MBUNGE KATIKA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA.
DODOMA, ALHAMISI 19 MACHI 2015.
____________________________________

1)
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa fursa
uliyonipa kutoa maelezo yangu binafsi katika Bunge lako
Tukufu leo. Ninatoa maelezo haya kwa mujibu wa Kifungu
cha 50 (1) cha Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili,
2013 kinachosema kwamba,Mbunge yeyote anaweza, kwa
idhini ya Spika, kutoa maelezo binafsi Bungeni yanayolenga
kufafanua kuhusu jambo lolote linalomhusu na lililoifikia
jamii
2)
Mheshimiwa Spika, Nilijiunga na Bunge lako Tukufu kwa
mara ya kwanza Mwaka 2015 nikiwa na lengo kuu la kupaza
sauti ya vijana kwenye masuala yanayohusu nchi yetu na
kutetea maslahi ya Watanzania hususani Wananchi wa Jimbo
la Kigoma Kaskazini na Mkoa wa Kigoma, na Watanzania kwa
ujumla. Nilichaguliwa na wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa
tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Wananchi wa Kigoma Kaskazini walinichagua tena Mwaka
2010 kupitia tiketi ya CHADEMA.
3)
Mheshimiwa Spika, kupitia fursa ya ubunge niliyopewa
na wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa udhamini wa
CHADEMA, nimejifunza mengi hapa Bungeni na nje ya Bunge
hili. Nimeijua nchi yangu, nimejua siasa na nimejulikana
ndani na nje ya Tanzania. Muhimu zaidi ni kwamba nimepata
fursa adhimu ya kutoa mchango wangu katika kutunga
sheria na sera mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi

yetu. Aidha, nilipata fursa ya kipekee kama Mbunge na


Mwenyekiti wa Kamati zako mbili ya kuisimamia, kuishauri
na kuiajibisha serikali.
4)
Mheshimiwa Spika, Ninawashukuru sana wanachama
wa CHADEMA kwa dhamana mbalimbali walizonipa ndani ya
CHADEMA. Ninawashukuru viongozi wangu na hasa
Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa kunilea
na kuniamini kufanya naye kazi kwa kipindi chote tangu
nilipokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
katika chama na hapa Bungeni. Kama ambavyo nimesema
mara nyingi, CHADEMA imenilea na kunikuza tangu nikiwa
na umri wa miaka 16 na tangu kipindi hicho nimejifunza
mengi.
5)
Mheshimiwa Spika, Nichukue nafasi hii kuwashukuru
sana wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa mapenzi yao na
imani waliyonipa na kuniwezesha kukalia KITI hiki
ninachokalia ndani ya Bunge lako Tukufu. Nashukuru
kwamba juzi nilipata fursa ya kipekee ya kuwashukuru kwa
imani waliyonipa kuwatumikia kwa vipindi viwili mfululizo.
Mola atawalipa wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa imani
kubwa walioionyesha kwangu na kuniwezesha kulitumikia
Taifa langu kwa namna nilivyolitumikia.
6)
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa pamekuwa na
msuguano wa kiuongozi kati yangu na viongozi wangu ndani
ya CHADEMA uliosababishwa na tofauti za kimtazamo juu ya
tafsiri pana ya demokrasia ndani ya chama chetu. Hatimaye
tofauti hizi zilipelekea mwezi Novemba 2013 Kamati Kuu ya
CHADEMA kunivua nafasi zangu zote za uongozi nilizokuwa
nazo. Sikuridhika na maamuzi hayo na hivyo nikaonyesha
kusudio la kukata rufaa katika Baraza Kuu la chama chetu
kama taratibu za kikatiba za chama chetu zinavyotaka.
Bahati mbaya ofisi ya Katibu Mkuu haikunipa fursa hiyo, na

huo ndio ukawa msingi wa mimi kufungua kesi mahakamani


kuweka pingamizi la Kikao cha Kamati Kuu kujadili hatima ya
uanachama wangu hadi pale ofisi ya Katibu Mkuu
itakaponipa fursa ya kukata rufaa katika vikao vya chama.
Yaliyotokea baada ya hapo ni historia, lakini hatimaye
Mahakama Kuu imetoa hukumu yake tarehe 10 Machi 2015.
Katika hukumu hii, nimeshindwa kwa sababu za kiufundi kwa
maelezo kwamba pingamizi letu liliwasilishwa kimakosa.
Pamoja na kwamba hatukuridhika na mwenendo wa jinsi kesi
hii ilivyoamuliwa pamoja na maudhui ya hukumu yenyewe,
ninaheshimu maamuzi ya mahakama na sina mpango wa
kukata rufaa.
7)
Mheshimiwa Spika, katika hali ya kawaida na kwa
mujibu wa katiba ya chama chetu, ilitarajiwa kwamba baada
ya maamuzi ya Mahakama Kuu, Kamati Kuu ingekaa na
kunipa rasmi mashtaka yangu yanayohusu uanachama
wangu, mimi kuitwa kujieleza na hatimaye Kamati Kuu kutoa
uamuzi wake. Hata hivyo, mara baada ya hukumu ya
Mahakama Kuu dunia nzima ilitangaziwa na Mwanasheria
wetu Mkuu, kwa niaba ya chama, kwamba mimi
nimeshafukuzwa na sio mwanachama tena wa CHADEMA.
Baada ya hapo viongozi wangu wametoa matamko
mbalimbali yote yakionyesha kwamba sitakiwi tena katika
chama hiki, pamoja na kwamba hadi ninapoongea hapa leo
sijawahi kukabidhiwa barua yeyote inayonitaarifu kufukuzwa
kwangu katika chama.
8)
Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo ya hapo juu,
ni wazi kwamba uanachama wangu wa kisiasa ndani ya
CHADEMA umeshaondolewa. Ninaweza kuendelea kupigania
uanachama wangu kisheria na kwa kweli nina sababu na
misingi yote kubaki na uanachama wangu kisheria. Lakini
mimi ni mwanasiasa. Sikuja hapa bungeni kwa sababu ya

kushinda kesi mahakamani. Nilichaguliwa na wananchi wa


Kigoma Kaskazini na ninatambua kwamba huwezi kuwa
mbunge bila udhamini wa chama cha siasa. Huu ndio
utaratibu wa kisheria tuliojiwekea. Kwa mujibu wa viongozi
wangu katika chama ni kwamba udhamini wa chama changu
umekwishaondolewa.
9)
Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo ya hapo juu,
ninaomba kukutaarifu wewe na Bunge lako tukufu kwamba
sina mpango wa kuendelea kupigania uanachama wangu wa
CHADEMA katika viunga vya mahakama. Kwa hiyo
ninatangaza rasmi leo kwamba taratibu za kikatiba
zitakapokamilika tu nitaachia uanachama wa CHADEMA,
chama nilichokipenda sana kwa sababu ya kuendelea kukua
kwa tofauti za kiitikadi, kimtazamo na hata kibinafsi kati
yangu na viongozi katika chama changu. Nimeona kuwa
kuendelea kupigania uanachama kisheria ni kutatiza na
kukwaza harakati za mabadiliko hapa nchini katika wakati
ambapo mfumo wa kisiasa unatambua uwepo wa vyama
vingi vya siasa. Kwa kuwa taratibu hizo sijui zitakamilika lini,
natumia fursa hii kuwaaga wabunge wenzangu.
10) Mheshimiwa Spika, vyama vya siasa ni jukwaa muhimu
katika ujenzi wa demokrasia lakini havipaswi kamwe kuwa
juu ya wananchi. Kwa hiyo ni maoni yangu kwamba wakati
sasa umefika wa kukomesha udola na ufalme wa vyama vya
siasa hapa nchini. Mfumo wa siasa ambao unavipa vyama
vya siasa mamlaka ya kisheria ya kukanyaga mamlaka ya
wananchi haupaswi kuendelea katika Karne ya 21 na katika
nchi ambayo inaendeshwa kwa misingi ya demokrasia ya
kuheshimu wananchi. Mimi ninaondoka bungeni sio kwa
sababu wananchi wangu wa Kigoma Kaskazini walionichagua
wametaka niondoke. Siondoki kwa sababu nimeshindwa
kufanya kazi zangu za ubunge. Na kwa kweli siondoki kwa
sababu wanachama wenzangu katika CHADEMA wametaka

niondoke. Ninaondoka kwa sababu mfumo wetu wa kisheria


unavipa vyama vya siasa mamlaka juu ya wananchi na
wapiga kura. Ni matumaini yangu kwamba Bunge lako
tukufu halitaruhusu mfumo huu unaoruhusu vyama vya siasa
kupora mamlaka ya wananchi uendelee. Ni Bunge lako
pekee lenye uwezo wa kukomesha mfumo ambao unatukuza
Parties Power, badala ya Peoples Power.
11) Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali kwamba
vyama vya siasa ni jukwaa. Bahati nzuri nchi yetu inafuata
mfumo wa vyama vingi vya siasa na sasa tuna vyama 22.
Kwa hivyo, wananchi wanaoniunga mkono wasisikitike kwa
maamuzi yangu ya leo. Bado ninayo fursa ya kuwatumikia
kupitia jukwaa lingine ambalo nitaamua katika siku chache
zijazo, na inshala Mungu akitujalia nitarudi tena hapa
Bungeni katika Bunge la 11 kwa nguvu za wananchi.
12) Mheshimiwa Spika, kwa miaka kumi niliyotumikia hapa
Bungeni, si yote niliyoyafanya yalikuwa sahihi, yapo ambayo
niliyakosea kama mwanadamu katika kufanya kazi zangu,
kwa namna yeyote ile naomba radhi Watanzania wote kwa
yote ambayo sikuyafanya kwa usahihi. Mimi ni binadamu,
kiumbe dhaifu, sijakamilika. Ni Mola peke yake aliyekamilika.
13) Mheshimiwa Spika, siwezi kuanza maisha yangu mapya
kisiasa bila ya kulishukuru Bunge lako Tukufu. Kwanza,
Bunge la Tisa chini ya Mzee Samwel Sitta, mzee wa kasi na
viwango! Bado ninakumbuka vizuri jinsi hoja ya Buzwagi
ilivyotikisa Bunge lake na hatimaye kupelekea nchi yetu
kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa uendeshaji
wa sekta ya madini (Sera mpya ya Madini na Sheria mpya ya
Madini ) na hivyo kukuza mapato ya sekta ya madini kutoka
Tshs. 32 bilioni kwa mwaka mpaka Tshs. 450 bilioni kwa
mwaka.

14) Mheshimiwa Spika, ninajivunia kuwa sehemu ya Bunge


la Kumi chini yako, Mama shupavu Anna Semamba Makinda.
Katika Bunge hili nimekuzwa, nimejifunza, nimepambana,
nimefurahi na nimelia ndani ya Bunge hili. Kwa pamoja
tumepigania maslahi ya wananchi wetu kwa juhudi na
maarifa na hivyo kuleta mabadiliko kadhaa. Ni katika kipindi
hiki ambapo wabunge tumekuwa na sauti. Bunge la Tisa
lilijijenga likawa Bunge lenye Meno katika kupambana na
ufisadi. Bunge la Kumi limejenga Bunge lenye Nguvu katika
mfumo wa Bajeti ya nchi yetu. Kupitia Bunge hili tumeweka
misingi ya kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji katika
nchi yetu. Na katika siku za hivi karibuni Bunge la Kumi
litakumbukwa kwa Hoja Maalumu ya Tegeta Escrow
iliyopelekea mfumo wetu wa maadili ya Viongozi kupitia
Baraza la Maadili kuanza kufanya kazi kwa namna ambayo
haijawahi kushuhudiwa katika miaka iliyopita.
15) Mheshimiwa Spika, wajumbe wa PAC ( ambao nimeishi
nao kama familia ) tumekuwa nguzo kubwa ya kujenga
uwajibikaji wa Serikali kwa Bunge na wananchi. Napenda
kuwashukuru kwa dhati kabisa kwa kuniunga mkono na kwa
kunipa ushirikiano kama Mwenyekiti wao. Changamoto na
malezi mliyonipa kwa miaka yote hii yamejenga Mtanzania
mmoja mwenye nia ya dhati ya kuitumikia nchi yake, muda
wowote, wakati wowote na kwa namna yeyote ile bila woga
wala upendeleo. Nawashukuru kwa kujitoa kwenu kwa nchi
yetu na dhamira isiyo na mawaa ya kujenga Taifa imara
zaidi. Pamoja na kwamba ninaondoka Bungeni leo, ninaahidi
kuendelea kuwatumikia wananchi wa Kigoma Kaskazini na
Taifa langu katika kusimamia ukweli, kutetea demokrasia ya
kweli na kupigania maendeleo ya kweli kwa mwananchi wa
kawaida bila ubaguzi wowote.
16) Mheshimiwa Spika, Kwa viongozi na wanachama wa
CHADEMA, najivunia kwa fursa mliyonipa kuwa sehemu ya

Baraza hili la Taifa ambalo leo ninalihutubia kwa mara ya


mwisho kama mbunge wa Kigoma Kaskazini. Inawezekana
tusiweze kuelewana katika masuala ya uongozi, misingi na
itikadi, lakini ninaamini tunapaswa kuelewana na
kukubaliana katika dhamira kubwa ya kuijenga nchi yetu
kuwa Taifa linalojitegemea na lisilo na aina yeyote ya
ubaguzi. Taifa lenye uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira
na kuondoa umasikini, ujinga na maradhi, yaani Taifa la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na ni matumaini yangu
kuwa tutakuwa bega kwa bega katika harakati hizi katika
siku zijazo. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Nafasi hii ya
kihistoria tuliyopewa haihitaji siasa za ubinafsi na unafsi!
Uzalendo wetu utapimwa kwa uwezo wetu wa kuweka tofauti
zetu binafsi pembeni kwa lengo lililo kubwa zaidi yetu.
17) Mheshimiwa Spika, Ninawashukuru tena na tena wana
Kigoma na wananchi wote wa Tanzania ambao kwa ridhaa
yao nimekaa katika viti hivi kwa miaka takribani kumi.
Ninawahakikishia kuwa changamoto nilizokumbana nazo na
ambazo zimenilazimisha leo niondoke bungeni zimechochea
zaidi dhamira, nia na sababu yangu ya kuwatumikia kwa
nguvu zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule. Huu ni
mwanzo mpya.
Mheshimiwa Spika, Asanteni sana na Kwa herini!

You might also like