You are on page 1of 8

MAELEZO BINAFSI YA MHE.

ZITTO ZUBEIR KABWE,


MB KUHUSU UANACHAMA WAKE KATIKA CHAMA
CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) NA
HATMA YAKE KAMA MBUNGE KATIKA BUNGE LA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA.

DODOMA, ALHAMISI 19 MACHI 2015.


____________________________________

1)
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa
fursa uliyonipa kutoa maelezo yangu binafsi katika
Bunge lako Tukufu leo. Ninatoa maelezo haya kwa
mujibu wa Kifungu cha 50 (1) cha Kanuni za Kudumu
za Bunge, Toleo la Aprili, 2013 kinachosema kwamba,

Mbunge yeyote anaweza, kwa idhini ya Spika, kutoa


maelezo binafsi Bungeni yanayolenga kufafanua
kuhusu jambo lolote linalomhusu na lililoifikia jamii

2)
Mheshimiwa Spika, Nilijiunga na Bunge lako
Tukufu kwa mara ya kwanza Mwaka 2015 nikiwa na
lengo kuu la kupaza sauti ya vijana kwenye masuala
yanayohusu nchi yetu na kutetea maslahi ya
Watanzania hususani Wananchi wa Jimbo la Kigoma
Kaskazini na Mkoa wa Kigoma, na Watanzania kwa
ujumla. Nilichaguliwa na wananchi wa Kigoma
Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA). Wananchi wa Kigoma
Kaskazini walinichagua tena Mwaka 2010 kupitia
tiketi ya CHADEMA.

3)
Mheshimiwa Spika, kupitia fursa ya ubunge
niliyopewa na wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa
udhamini wa CHADEMA, nimejifunza mengi hapa
Bungeni na nje ya Bunge hili. Nimeijua nchi yangu,

nimejua siasa na nimejulikana ndani na nje ya


Tanzania. Muhimu zaidi ni kwamba nimepata fursa
adhimu ya kutoa mchango wangu katika kutunga
sheria na sera mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya
nchi yetu. Aidha, nilipata fursa ya kipekee kama
Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati zako mbili ya
kuisimamia, kuishauri na kuiajibisha serikali.

4)
Mheshimiwa Spika, Ninawashukuru sana
wanachama wa CHADEMA kwa dhamana mbalimbali
walizonipa ndani ya CHADEMA. Ninawashukuru
viongozi wangu na hasa Mwenyekiti wetu
Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa kunilea na
kuniamini kufanya naye kazi kwa kipindi chote tangu
nilipokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, katika chama na hapa Bungeni. Kama
ambavyo nimesema mara nyingi, CHADEMA imenilea
na kunikuza tangu nikiwa na umri wa miaka 16 na
tangu kipindi hicho nimejifunza mengi.

5)
Mheshimiwa Spika, Nichukue nafasi hii
kuwashukuru sana wananchi wa Kigoma Kaskazini
kwa mapenzi yao na imani waliyonipa na
kuniwezesha kukalia KITI hiki ninachokalia ndani ya
Bunge lako Tukufu. Nashukuru kwamba juzi nilipata
fursa ya kipekee ya kuwashukuru kwa imani
waliyonipa kuwatumikia kwa vipindi viwili mfululizo.
Mola atawalipa wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa
imani kubwa walioionyesha kwangu na kuniwezesha
kulitumikia Taifa langu kwa namna nilivyolitumikia.

6)
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa
pamekuwa na msuguano wa kiuongozi kati yangu na
viongozi wangu ndani ya CHADEMA uliosababishwa
na tofauti za kimtazamo juu ya tafsiri pana ya
demokrasia ndani ya chama chetu. Hatimaye tofauti
hizi zilipelekea mwezi Novemba 2013 Kamati Kuu ya

CHADEMA kunivua nafasi zangu zote za uongozi


nilizokuwa nazo. Sikuridhika na maamuzi hayo na
hivyo nikaonyesha kusudio la kukata rufaa katika
Baraza Kuu la chama chetu kama taratibu za kikatiba
za chama chetu zinavyotaka. Bahati mbaya ofisi ya
Katibu Mkuu haikunipa fursa hiyo, na huo ndio ukawa
msingi wa mimi kufungua kesi mahakamani kuweka
pingamizi la Kikao cha Kamati Kuu kujadili hatima ya
uanachama wangu hadi pale ofisi ya Katibu Mkuu
itakaponipa fursa ya kukata rufaa katika vikao vya
chama. Yaliyotokea baada ya hapo ni historia, lakini
hatimaye Mahakama Kuu imetoa hukumu yake
tarehe 10 Machi 2015. Katika hukumu hii,
nimeshindwa kwa sababu za kiufundi kwa maelezo
kwamba pingamizi letu liliwasilishwa kimakosa.

Pamoja na kwamba hatukuridhika na mwenendo wa


jinsi kesi hii ilivyoamuliwa pamoja na maudhui ya
hukumu yenyewe, ninaheshimu maamuzi ya
mahakama na sina mpango wa kukata rufaa.

7)
Mheshimiwa Spika, katika hali ya kawaida na
kwa mujibu wa katiba ya chama chetu, ilitarajiwa
kwamba baada ya maamuzi ya Mahakama Kuu,
Kamati Kuu ingekaa na kunipa rasmi mashtaka yangu
yanayohusu uanachama wangu, mimi kuitwa
kujieleza na hatimaye Kamati Kuu kutoa uamuzi
wake. Hata hivyo, mara baada ya hukumu ya
Mahakama Kuu dunia nzima ilitangaziwa na
Mwanasheria wetu Mkuu, kwa niaba ya chama,
kwamba mimi nimeshafukuzwa na sio mwanachama
tena wa CHADEMA. Baada ya hapo viongozi wangu
wametoa matamko mbalimbali yote yakionyesha
kwamba sitakiwi tena katika chama hiki, pamoja na
kwamba hadi ninapoongea hapa leo sijawahi
kukabidhiwa barua yeyote inayonitaarifu kufukuzwa
kwangu katika chama.

8)
Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo ya
hapo juu, ni wazi kwamba uanachama wangu wa
kisiasa ndani ya CHADEMA umeshaondolewa.
Ninaweza kuendelea kupigania uanachama wangu
kisheria na kwa kweli nina sababu na misingi yote
kubaki na uanachama wangu kisheria. Lakini mimi ni
mwanasiasa. Sikuja hapa bungeni kwa sababu ya
kushinda kesi mahakamani. Nilichaguliwa na
wananchi wa Kigoma Kaskazini na ninatambua
kwamba huwezi kuwa mbunge bila udhamini wa
chama cha siasa. Huu ndio utaratibu wa kisheria
tuliojiwekea. Kwa mujibu wa viongozi wangu katika
chama ni kwamba udhamini wa chama changu
umekwishaondolewa.

9)
Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo ya
hapo juu, ninaomba kukutaarifu wewe na Bunge lako
tukufu kwamba sina mpango wa kuendelea kupigania
uanachama wangu wa CHADEMA katika viunga vya
mahakama. Kwa hiyo ninatangaza rasmi leo kwamba
taratibu za kikatiba zitakapokamilika tu nitaachia
uanachama wa CHADEMA, chama nilichokipenda
sana kwa sababu ya kuendelea kukua kwa tofauti za
kiitikadi, kimtazamo na hata kibinafsi kati yangu na
viongozi katika chama changu. Nimeona kuwa
kuendelea kupigania uanachama kisheria ni kutatiza
na kukwaza harakati za mabadiliko hapa nchini katika
wakati ambapo mfumo wa kisiasa unatambua uwepo
wa vyama vingi vya siasa. Kwa kuwa taratibu hizo
sijui zitakamilika lini, natumia fursa hii kuwaaga
wabunge wenzangu.

10) Mheshimiwa Spika, vyama vya siasa ni jukwaa


muhimu katika ujenzi wa demokrasia lakini havipaswi
kamwe kuwa juu ya wananchi. Kwa hiyo ni maoni
yangu kwamba wakati sasa umefika wa kukomesha
udola na ufalme wa vyama vya siasa hapa nchini.
Mfumo wa siasa ambao unavipa vyama vya siasa
mamlaka ya kisheria ya kukanyaga mamlaka ya

wananchi haupaswi kuendelea katika Karne ya 21 na


katika nchi ambayo inaendeshwa kwa misingi ya
demokrasia ya kuheshimu wananchi. Mimi
ninaondoka bungeni sio kwa sababu wananchi wangu
wa Kigoma Kaskazini walionichagua wametaka
niondoke. Siondoki kwa sababu nimeshindwa kufanya
kazi zangu za ubunge. Na kwa kweli siondoki kwa
sababu wanachama wenzangu katika CHADEMA
wametaka niondoke. Ninaondoka kwa sababu mfumo
wetu wa kisheria unavipa vyama vya siasa mamlaka
juu ya wananchi na wapiga kura. Ni matumaini yangu
kwamba Bunge lako tukufu halitaruhusu mfumo huu
unaoruhusu vyama vya siasa kupora mamlaka ya
wananchi uendelee. Ni Bunge lako pekee lenye
uwezo wa kukomesha mfumo ambao unatukuza
Parties Power, badala ya Peoples Power.

11) Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali


kwamba vyama vya siasa ni jukwaa. Bahati nzuri nchi
yetu inafuata mfumo wa vyama vingi vya siasa na
sasa tuna vyama 22. Kwa hivyo, wananchi
wanaoniunga mkono wasisikitike kwa maamuzi
yangu ya leo. Bado ninayo fursa ya kuwatumikia
kupitia jukwaa lingine ambalo nitaamua katika siku
chache zijazo, na inshala Mungu akitujalia nitarudi
tena hapa Bungeni katika Bunge la 11 kwa nguvu za
wananchi.

12) Mheshimiwa Spika, kwa miaka kumi niliyotumikia


hapa Bungeni, si yote niliyoyafanya yalikuwa sahihi,
yapo ambayo niliyakosea kama mwanadamu katika
kufanya kazi zangu, kwa namna yeyote ile naomba
radhi Watanzania wote kwa yote ambayo sikuyafanya
kwa usahihi. Mimi ni binadamu, kiumbe dhaifu,
sijakamilika. Ni Mola peke yake aliyekamilika.

13) Mheshimiwa Spika, siwezi kuanza maisha yangu


mapya kisiasa bila ya kulishukuru Bunge lako Tukufu.
Kwanza, Bunge la Tisa chini ya Mzee Samwel Sitta,
mzee wa kasi na viwango! Bado ninakumbuka vizuri
jinsi hoja ya Buzwagi ilivyotikisa Bunge lake na
hatimaye kupelekea nchi yetu kufanya mabadiliko
makubwa katika mfumo wa uendeshaji wa sekta ya
madini (Sera mpya ya Madini na Sheria mpya ya
Madini ) na hivyo kukuza mapato ya sekta ya madini
kutoka Tshs. 32 bilioni kwa mwaka mpaka Tshs. 450
bilioni kwa mwaka.

14) Mheshimiwa Spika, ninajivunia kuwa sehemu ya


Bunge la Kumi chini yako, Mama shupavu Anna
Semamba Makinda. Katika Bunge hili nimekuzwa,
nimejifunza, nimepambana, nimefurahi na nimelia
ndani ya Bunge hili. Kwa pamoja tumepigania
maslahi ya wananchi wetu kwa juhudi na maarifa na
hivyo kuleta mabadiliko kadhaa. Ni katika kipindi hiki
ambapo wabunge tumekuwa na sauti. Bunge la Tisa
lilijijenga likawa Bunge lenye Meno katika
kupambana na ufisadi. Bunge la Kumi limejenga
Bunge lenye Nguvu katika mfumo wa Bajeti ya nchi
yetu. Kupitia Bunge hili tumeweka misingi ya kujenga
mfumo madhubuti wa uwajibikaji katika nchi yetu. Na
katika siku za hivi karibuni Bunge la Kumi
litakumbukwa kwa Hoja Maalumu ya Tegeta Escrow
iliyopelekea mfumo wetu wa maadili ya Viongozi
kupitia Baraza la Maadili kuanza kufanya kazi kwa
namna ambayo haijawahi kushuhudiwa katika miaka
iliyopita.

15) Mheshimiwa Spika, wajumbe wa PAC ( ambao


nimeishi nao kama familia ) tumekuwa nguzo kubwa
ya kujenga uwajibikaji wa Serikali kwa Bunge na
wananchi. Napenda kuwashukuru kwa dhati kabisa
kwa kuniunga mkono na kwa kunipa ushirikiano kama
Mwenyekiti wao. Changamoto na malezi mliyonipa
kwa miaka yote hii yamejenga Mtanzania mmoja

mwenye nia ya dhati ya kuitumikia nchi yake, muda


wowote, wakati wowote na kwa namna yeyote ile bila
woga wala upendeleo. Nawashukuru kwa kujitoa
kwenu kwa nchi yetu na dhamira isiyo na mawaa ya
kujenga Taifa imara zaidi. Pamoja na kwamba
ninaondoka Bungeni leo, ninaahidi kuendelea
kuwatumikia wananchi wa Kigoma Kaskazini na Taifa
langu katika kusimamia ukweli, kutetea demokrasia
ya kweli na kupigania maendeleo ya kweli kwa
mwananchi wa kawaida bila ubaguzi wowote.

16) Mheshimiwa Spika, Kwa viongozi na wanachama


wa CHADEMA, najivunia kwa fursa mliyonipa kuwa
sehemu ya Baraza hili la Taifa ambalo leo
ninalihutubia kwa mara ya mwisho kama mbunge wa
Kigoma Kaskazini. Inawezekana tusiweze kuelewana
katika masuala ya uongozi, misingi na itikadi, lakini
ninaamini tunapaswa kuelewana na kukubaliana
katika dhamira kubwa ya kuijenga nchi yetu kuwa
Taifa linalojitegemea na lisilo na aina yeyote ya
ubaguzi. Taifa lenye uchumi shirikishi wenye
kuzalisha ajira na kuondoa umasikini, ujinga na
maradhi, yaani Taifa la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Na ni matumaini yangu kuwa tutakuwa
bega kwa bega katika harakati hizi katika siku zijazo.
Yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Nafasi hii ya
kihistoria tuliyopewa haihitaji siasa za ubinafsi na
unafsi! Uzalendo wetu utapimwa kwa uwezo wetu wa
kuweka tofauti zetu binafsi pembeni kwa lengo lililo
kubwa zaidi yetu.

17) Mheshimiwa Spika, Ninawashukuru tena na tena


wana Kigoma na wananchi wote wa Tanzania ambao
kwa ridhaa yao nimekaa katika viti hivi kwa miaka
takribani kumi. Ninawahakikishia kuwa changamoto
nilizokumbana nazo na ambazo zimenilazimisha leo
niondoke bungeni zimechochea zaidi dhamira, nia na
sababu yangu ya kuwatumikia kwa nguvu zaidi kuliko
wakati mwingine wowote ule. Huu ni mwanzo mpya.

Mheshimiwa Spika,

Asanteni sana na Kwa herini!

You might also like