You are on page 1of 7

JUKWAA LA WAHARIRI (TEF), MNAFANYA KOSA LILELILE

LILILOFANYWA NA MAASKOFU WA KKKT NA TEC

Aprili 5, 2018
Dar es Salaam.

Muda mfupi uliopita nimesikiliza Tamko la Jukwaa la Wahariri Tanzania


(TEF) kuhusu hali ya nchi yetu.

Kimsingi TEF walichokifanya hakina tofauti na kile walichokifanya Baraza


la Maaskofu wa Kanisa la Kiinjilisti la Kilutheri Tanzania (KKKT) na
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ambacho ni kuendeleza
wimbo wa ajenda za kisiasa zenye mlengo wa siasa za upinzani.

Huku ni kupotoka kwa hali ya juu sana.

Niliwahi kuhoji huko nyuma juu ya uhalali na uhalisia wa TEF ambao ni


mabosi au viongozi wa waandishi wa habari nikiwemo mimi. Nilihoji hivi
kwa sababu nikiwa mwandishi wa habari mpaka leo sijaelewa na wala
sijaeleweshwa kuhusu Jukwaa la Wahariri ambalo naamini linapaswa kuwa
na uhusiano wa karibu na waandishi wa habari hasa ikizingatiwa mara zote
linazungumza masuala yanayowahusu waandishi wa habari kama
lilivyofanya leo.

Nasema hivyo kwa sababu TEF inatoa matamko ambayo yanabeba sura
kuwa ni matamko ya waandishi wa habari wakati kiuhalisia siamini kuwa
huo ndio msimamo wa waandishi wa habari wa nchi hii.

Nilikuwa nafuatilia mkutano wa TEF, nimemuona Deodatus Balile na


Neville Meena wakiendesha mkutano huu, wametoa hoja nyingi ambazo
kimsingi na kwa ufupi hakuna tofauti na Waraka uliotolewa na Maaskofu wa
KKKT na TEC kabla ya Pasaka.

Kwa bahati nzuri nilipata kusoma barua ya Prof. Kitila Mkumbo


aliyomuandikia Askofu wake Fredrick Shoo. Na katika barua hii kwa usomi
na unyenyekevu mkubwa Prof. Kitila Mkumbo alieleza namna maaskofu
walivyojikwaa katika waraka wao na akatoa ushauri wake kwao.

1
Na mimi pia naomba nifanye hivyohivyo kwenye nyie Maaskofu wangu
yaani Jukwaa la Wahariri na kwa kweli nikulenge wewe Kaimu Mwenyekiti
wa TEF Deodatus Balile ambaye umelisoma tamko la TEF.

Ndugu Balile tamko lenu linatuletea maswali mengi kwenye jamii na hasa
Serikali ambayo ni sehemu muhimu ya kazi zetu za kila siku. Mimi nikiwa
mmoja wa waandishi wa habari ambao hawajashirikishwa na wala
hawajawahi kushirikishwa kwenye masuala ya TEF limenikwaza kwa
sababu wadau ambao nafanya nao kazi kwa karibu ni Serikali ambayo
kimsingi tamko lenu linaituhumu kwa mambo mazito yenye vinasaba vya
siasa za upinzani.

Nilitarajia kwa dhamana ambayo TEF imebeba ingefanya utafiti wa kutosha


kabla ya kuandika tamko hili na kuja kulisoma kwa waandishi wa habari,
nilitarajia waandishi wa habari tungejulishwa kupitia vyama vya waandishi
wa habari wa mikoa (Press Clubs) ama kupitia Umoja wa Vyama vya
Waandishi wa Habari (UTPC) ama ikishindikana kupitia vyombo vyetu vya
habari, kuwa kuna tamko hili zito litatolewa kuhusu sisi.

Badala yake Balile na wenzako akina Neville Meena mmekaa na kwa


mawazo yenu, hisia zenu na malengo yenu mkaamua kuandika
mlichoandika na kisha kwenda kukisoma kwenye mkutano wa vyombo vya
habari, mkibeba sura ya Tamko la Jukwaa la Wahariri wakati ndani yake
mnazungumza kwa niaba ya waandishi wa habari.

Sasa twende hoja kwa hoja, mosi, mnasema kuna sintofahamu katika hali ya
uchumi, mnazungumza hilo kwa kuzingatia nini? Maana takwimu
zinaonesha hali ya uchumi wa nchi yetu ni nzuri? Takwimu za hivi karibuni
zinaonesha kuwa uchumi wetu umepanda na sasa unakua kwa asilimi 7.1
kutoka 6.8, mfumuko wa bei umeshuka hadi asilimia 4.5, nchi yetu ni kati ya
nchi 5 zenye kasi kubwa ya kukua kwa uchumi barani Afrika.

Takwimu za Benki Kuu (BOT) zinaonesha nchi ina akiba ya fedha za kigeni
zaidi ya Bilioni 5 za kutosha kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi 6 na Rais
kasema fedha za kutekelezea miradi mikubwa ya reli, kununua ndege,
barabara, maji, ujenzi wa viwanja vya ndege, elimu bure, kujenga flyover,
kujenga bandari, kununua dawa za hospitali na mengine, zipo. Rais kasema
Serikali ina fedha za kulipa mishahara wafanyakazi na haikopi katika
mabenki ya biashara kama ilivyokuwa zamani. Sasa nyie mnazungumza
sintofahamu ya kutoka wapi?

2
Balile na wenzako mnasema kuna sintofahamu ndani ya jamii kwa sababu
uhuru wa kutoa maoni unaminywa ukiwemo uhuru wa vyombo vya habari,
labda niulize wewe Balile gazeti lako la Jamhuri na mambo mazito
linayoyaandika kila toleo ni mahali gani umeminywa uhuru wako? Au
nimuulize Meena makala anazoandika kila siku kwenye magazeti
mbalimbali likiwemo Mwananchi, na jinsi zinavyoikosoa Serikali ni lini
uhuru wake umeminywa? Au Mwandishi wa habari mkongwe Jenerali
Ulimwengu na vijana wake akina Ezekiel Kamwaga jinsi wanavyotumia
gazeti lao la Raia Mwema kuandika mambo mazito ya kuikosoa Serikali ni
wapi uhuru wao unaminywa? Chukua magazeti ya leo Mwananchi, Tanzania
Daima, Nipashe, Mtanzania kwa kutaja machache soma na angalia kuna
habari ngapi zinaikosoa Serikali, umesikia yameminywa? Ipo mifano mingi.

Nilitarajia wewe Balile kwa elimu yako ya sheria ungekuwa mwalimu pale
ambapo waandishi wa habari wanadhani wana haki ya kuandika chochote tu
bila kutambua kuwa wana wajibu wa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni
mbalimbali zilizopo hapa nchini na pia kuzingatia weledi katika taaluma hii
ya uandishi wa habari.

Ningeelewa zaidi kama TEF katika tamko lenu mngesema pia kuhusu
makosa ya dhahiri ambayo vyombo vya habari vinayafanya na mara kwa
mara tunasoma Mkurugenzi wa Maelezo Dk. Hassan Abbas anavionya na
vinaomba radhi.

Balile na wenzako mnasema vyombo vya habari vinafungiwa na kutozwa


faini. Sasa mlitaka vikikiuka sheria iwaje? Na kama hakutakuwa na adhabu
hizo sheria zimetungwa za nini? Na hapa tuwe wakweli vyombo vya habari
vilivyofungiwa vinafahamika na makosa yake hutajwa. Na kwa sisi
waandishi wa habari tunajuana na tunajua uhalali wa vyombo hivyo
kufungwa, kwa nini hatujiulizi kila wakati ni vyombo vilevile tu?

Hivi Balile na wenzako kwenye TEF mnataka kutuaminisha kuwa Magazeti


ya Mwanahalisi na Mawio hayakustahili kufungiwa? Gazeti la Tanzania
Daima ambalo limemaliza kifungo chake na ambalo Neville Meena aliwahi
kuwa Mhariri wake halikustahili kufungiwa kwa makosa yale?

Hivi Ansibert Ngurumo aliyekuwa Mhariri mmojawapo wa Mwanahalisi na


MAwio na ambaye kwa sasa ametengeneza drama ya kujifanya kakimbilia
uhamishoni nchini Finland ndivyo mnataka waandishi wa habari wa

3
Tanzania tuwe hivyo? Mnakiona anachokifanya Ansibert Ngurumo akiwa
huko Finland au mmefumba macho hamsomi maandiko yake kwenye
mitandao ya kijamii?

TEF mmebeba ajenda nyingine ya siasa za upinzani ambayo hata


Mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA)
Freeman Mbowe kaisema tena jana wakati akitoka rumande Segerea kuwa
demokrasia imezorota, mmepima wapi kuwa demokrasia imezorota?
Kaizorotesha nani? Au mnamhoji nani kiasi cha kutaka Rais Magufuli
akutane na hao mnaosema ni makundi mbalimbali?

Hoja hizi ni za wanasiasa wa upinzani kabisa ambao wanapambana kuingia


Ikulu leo mnataka kuzibeba nyie TEF? Kama ni kukutana na makundi
mbona Rais anakutana nayo? Amekutana na waandishi wa habari na
wakauliza maswali hadi yakaisha, amekutana na wafanyabiashara
wameuliza maswali mpaka yakaisha, hukuna na viongozi wa dini na
huzungumza nao, hukutana na wanasiasa na huzungumza nao na taarifa za
Ikulu zinakuja. Labda mseme mlitaka akutane na akina nani? Na kama ni
hivyo basi muda bado upo, Rais ana miaka miwili na sasa kauanza wa tatu
kati ya miaka mitano ya kuwa kwake madarakani.

Yaani ndugu zangu Wahariri mnatuvalisha joho ambalo waandishi wa habari


hatustahili kabisa. Maanda haya mnayoyaandika ndio nyimbo za vyama vya
siasa vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Watanzania
(UKAWA), nyimbo za akina Mange Kimambi na Evarist Chahali. Yaani
mnafikia mahali mnataka kutuweka waandishi wa habari wa nchi kwenye
kundi moja na Mange Kimambi?

Kwenye tamko lenu mmechukua tukio la mwandishi wa habari kupokonywa


simu na polisi huko Dodoma na Azory Gwanda kupotea kwamba sasa
waandishi wa habari wote hatufanyi kazi kwa amani tumejawa na hofu.
Mimi naomba kuuliza vitendo hivi vya waandishi wa habari kukutana na
matukio ya kunyanyaswa vimeanza leo? Ni wakati gani waandishi wa habari
hawakunyanyaswa? Ni Tanzania tu ndio haya yanatokea? Nadhani majibu
mnayo.

Balile na wenzako TEF mnazungumza kuwa vyama vya siasa vinanyimwa


haki ya kufanya mikutano. Hivi jamani ni mwandishi wa habari gani
kawatuma mtoe tamko hili? Mimi hapa na mkutano wa chama cha siasa
wapi na wapi? Ningeelewa zaidi kama Balile na wenzako mngetumia nguvu

4
zenu kutoa somo kwa wanahabari namna ya kufanya kazi kwa weledi katika
mikutano ya siasa iliyozuiliwa, sasa na nyinyi mmekuwa wanaharakati
mnadai vyama vya siasa vinaminywa, mnataka vikafanye mikutano
isiyoruhusiwa ili mtutume tukaandike habari halafu yatukute yaliyomkuta
Daudi Mwangosi?

Balile na wenzako hapo TEF mnasema hali imekuwa mbaya kwamba


vyombo vya habari sasa vinakosa matangazo ya biashara na mauzo ya
magazeti yameshuka chini. Nilitarajia nyie ndio mngekuja na suluhisho la
namna ya kukabiliana na hali ambapo fedha za matangazo ambazo vyombo
vya habari vilitegemea kupata Serikalini hazipo. Nilitarajia mje mseme sasa
magazeti yetu yatapatikana kwenye App ama katika mfumo ambao
wasomaji watalazimika kulipia ndipo wasome, nilitarajia nyie mtakuja na
msaada wa namna gani matangazo ya televisheni na redio yahamie kwenye
kulipia kama ilivyo kwa Azam Media ili kuwe na kipato cha kuwalipa
waandishi wa habari vizuri?

Mnataka kulazimisha Serikali itoe hela za matangazo? Hivi TEF hamjifunzi


vyombo vya habari vya nchi za wenzetu vinaendeshwaje? Hivi taaluma yetu
si ndio inatufundisha juu ya mgongano wa maslahi, sasa mnapotaka vyombo
vya habari viendeshwe kwa kutegemea Serikali hivyo vyombo vitakuwa na
uhuru gani wa kuikosoa? Labda hili la vyombo vya habari kuidai Serikali
linaweza kueleweka lakini pia sidhani kama ilikuwa sawa kuja kulimwaga
kwenye mkutano na waandishi wa habari kwa sababu wanaoidai Serikali ni
wengi na inawezekana hiki kinachodaiwa na vyombo vya habari ikawa ni
kidogo. Na pia ningetarajia jambo hili litolewe tamko na wamiliki wa
vyombo vya habari sio nyinyi TEF.

Ndugu zangu njooni na solution sio kuja kulalamika. Halafu hebu kuweni
wakweli hata kabla ya nyakati hizi ni wakati gani waandishi wa habari
walikuwa na malipo mazuri na hali nzuri kazini? Tena nyie wenyewe
wahariri ndio mmekuwa wa kwanza kuwashawishi wamiliki wa vyombo vya
habari wawalipe waandishi shilingi 1,750/= kwa habari inayotumwa
gazetini, yaani mwandishi wa habari anaitafuta habari tena kwa kusafiri kwa
gharama kubwa na mwisho wa siku malipo yake ni shilingi 1,750/=, nyinyi
wenyewe wahariri ndio ambao mnapokea habari kutoka kwa waandishi wa
habari ambao hawana mishahara, hawana ajira, hawana mikataba ya kazi na
hata hawana mafao yoyote. Na haya mambo hayajaanza leo.

5
Waandishi wa habari wanafariki dunia, tunaishia kuchangisha fedha ili
kununua hadi chakula cha watu waliopo msibani. Lakini nyie TEF hata siku
moja hatujawaona mkiwabana hao wamiliki wabebe majukumu ya
kuhudumia wafanyakazi wao wanapoumwa ama kifo.

Na niwe mkweli hii tabia ya TEF kukurupuka acheni. Mlikurupuka wakati


wa mgogoro wa Ruge Mutahaba wa Clouds Media na Paul Makonda –
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na mwisho wake ukawa ni aibu na leo
mmekurupuka tena hivyohivyo.

Kwenye mgogoro wa Ruge na Makonda mlipokuruka, na kama kawaida


yenu tukawaona mnaungwa mkono na wanasiasa wa UKAWA na Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na leo tena mnapita humo, mnatufanya
waandishi wa habari wa nchi hii tuonekane ni wapinzani wa Serikali wakati
haya ni mambo yenu nyinyi. Hata habari mnazozipa umuhimu kwenye
nyombo vyenu zinakuwa na mwelekeo huo huo wa kuunga mkono
UKAWA, ndio maana leo mmesababisha waandishi wa habari tunakuwa
wanyonge mbele ya Serikali, hatuaminiki kwa sababu yenu.

Najua baada ya kuandika maoni yangu haya mtakuja kusema sijui katiba ya
TEF na nimeandika takataka lakini nataka niwaambie turudi kwenye misingi
yetu, acheni kutupeleka kwenye mwelekeo unaoharibu taswira ya tasnia hii
ya habari. Msituingize kwenye siasa, hii ni taaluma inayoheshimika duniani
kote. Inawezekana nyie mna maslahi yenu lakini ndani ya tasnia hii tumo
ambao tunategemea kalamu na weledi wetu, msituyumbishe na
msitugombanishe na Serikali.

Na ifike mahali vyombo hivi vinavyowahusu waandishi vipate sura mpya.


Nampongeza sana Mkongwe Teophil Makunga kwa uamuzi wake wa
kujiuzulu uenyekiti wa TEF, inawezekana kuna sababu lakini nadhani ni
muhimu tansia hii ianze kuona demokrasia ya kuwa na sura mpya kwenye
vyombo vinavyosimamia, hapa nina maana ya TEF, Baraza la Habari
(MCT), Umoja wa vyama vya waandishi wa habari (UTPC) na vingine. Sio
kila siku ni wale wale tu akina Meena, Balile na wenzenu. Tunao watu
wengine wazuri.

Mwisho nawaomba viongozi wa Serikali mtambue kuwa tamko lilisomwa


na TEF ni la wahariri wanaounda uongozi wa TEF, halituhusu waandishi wa
habari tulio wengi na ambao tunaendelea kufanya kazi zetu kama kawaida.
Tuendelee kushirikiana kama kawaida kuijenga Tanzania yetu ambayo kwa

6
sasa duniani kote inasifika kwa kuwa na kiongozi Mhe. Rais John Pombe
Magufuli ambaye ni mfano bora wa kuigwa barani Afrika kwa juhudi zake
za kutetea wanyonge, kupigania rasilimali za nchi, kupiga vita rushwa,
kubana matumizi yasiyo ya lazima, kujenga viwanda na kujenga uchumi
imara wa kutupeleka katika kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Mwandishi wa habari niliyetoa maoni haya naishi Dar es Salaam na


nimekuwa katika uandishi wa habari kwa miaka 18 sasa. Sijataka kutaja
jina langu kwa sababu sitaki ninyooshewe kidole na yeyote hasa
ikizingatiwa hulka za jamaa zangu akina Balile, Meena na wenzake
nazijua.