You are on page 1of 18

Kopi zinapatikana MZALENDO.

NET

UMUHIMU WA KURA YA MAONI NA MUSTAKABALI WA

ZANZIBAR

IMETAYARISHWA NA DR. MOHAMED ADAM WA CHUO KIKUU CHA EAST

STROUDSBURG, PENNSYLVANNIA, MAREKANI

NA KUWAKILISHWA KATIKA KONGAMANO LA KURA YA MAONI NA

SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA LILILOTAYARISHWA MUWAZA

IKISHIRIKIANA NA ZANZIBAR LAW SOCIETY, ZANZIBAR LEGAL SERVICES

CENTER NA JUMIKI TAREHE 17-18 JULAI 2010

Maneno ya Msingi (Key words): Kura ya maoni, maamuzi, mustakabali wa

Zanzibar

1.0. UTANGULIZI

Waraka huu lengo lake hasa ni kuzungumzia umuhimu wa kura ya maoni kwa

mustakabali wa nchi ya Zanzibar. Tukilinganisha nchi za Afrika na Marekani (USA) au

Canada au Ulaya kura ya maoni ni mara chache sana kutumika Afrika. Matumaini yangu

utaratibu huu wa kutoa maamuzi kwa kupiga kura ya maoni utaendelea kukua kwa kuwa

ni sehemu ya kutanuka kwa demokrasia iliyoanza kukua tokea mwanzo wa miaka ya

tisiini barani Afrika lakini pia hapa Zanzibar. Waraka huu sio lengo lake kushawishi

yeyote kupiga kura ya ndio au hapana kwenye hoja ya kura ya maoni ya Serikali ya

1
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

Umoja bali ni kuzungumzia umuhimu wa kura ya maoni, na vipi inahusiana na

mustakabali mzima wa nchi ya Zanzibar. Maelezo yamegawiwa katika mtiririko wa

kuchambuwa dhana moja moja kama vile kura ya maoni, mifano mbali mbali ya dunia

inayohusiana na kura maoni, kilicholetea kura ya maoni wakati huu Zanzibar, usimamiaji

wake, umuhimu wa kura ya maoni, na mambo yahusuyo mustakbali wa Zanzibar.

2.0. NINI KURA YA MAONI?

Kwa kuilezea kiutaalamu, Kura ya Maoni (Referendum) humaanisha upigaji kura katika

nchi nzima juu ya jambo maalumu (mara nyingi lenye mvutano baina ya pande mbili au

zaidi) ambalo kupitishwa kwake humaanisha au hupelekea kutatuwa tatizo fulani la

kisiasa ndani ya nchi. Katika ulimwengu wa leo, kura ya maoni ni moja ya njia

zinazokubalika katika kutatua masuala mbali mbali ya kisiasa. Wataalamu wa Sayansi ya

Siasa wanatueleza kuwa ziko aina mbili ya “Kura za maoni” ambazo kwa lugha ya

Kiingereza huzitafautisha kwa maneno tafauti. Kwanza ni ile inayoitwa kwa lugha ya

Kiingereza “initiative”ambayo tafsiri yake ya Kiswahili ni wazo au hoja binafsi au ya

kundi la watu katika kuanzisha hoja ya kura ya maoni. Hii hutafsirika kama ni kura ya

maoni inayoletwa baada ya msukumo wa wananchi wa kawaida wenyewe, kwa mfano,

baada ya wananchi kadhaa kusaini aridhilhali na kupeleka lalamiko lao kwenye Bunge au

Baraza la Wawakilishi, na baadae kudai upigwaji kura ya maoni. Aina ya pili ya Kura ya

Maoni kwa lugha ya Kiingereza inaitwa “Plebiscite”. Hii inamaanisha kuomba kura ya

maoni ifanyike kwa ajili ya kutatuwa suala maalumu la kisiasa linalotanza. Ukweli hasa

badala ya kuziita hizi nia aina mbili ya Kura za maoni, inawezekana kabisa kuziita daraja

mbili tu za kura za maoni. Kwani initiative ni pale ambapo kura ya maoni hupigwa hata

2
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

kabla hapajatokea uvunjwaji wa Sheria au mzozo na hivyo ndio maana ikaitwa hilo jina

la “initiative” (kwa kuwa inanzisha tu wazo au hoja) na hii ya pili ya “Prebiscite”

huitishwa baada ya mzozo kwisha tokea (hasa wa kisiasa) na lengo lake ni kuutatua huo

mzozo uliopo. Na hii ya pili ndio inalingana na hii Kura ya Maoni inayotayarishwa

kupigwa hapa Zanzibar.

Ni vizuri kutafautisha upigaji kura katika uchaguzi mkuu na kura ya maoni.

Upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu na kura ya maoni ni kuwa katika uchaguzi mkuu

mambo mengi ya sera za maendeleo, siasa, uchumi na jamii huchanganywa pamoja na

kujadiliwa wakati wa kampeni na mpigaji kura hutarajiwa kuwa na uwezo wa

kuyachambuwachambuwa mambo hayo mengi ya sera za uchumi, siasa, jamii, ufundi na

muungano na kuyafahamu, na si hayo tu bali, pia pamoja kumfahamu mgombea kabla ya

mpiga kura huyo kufanya uamuzi wa kutia kura yake. Tafauti ni kwamba, Kura ya maoni

hutowa nafasi ya moja kwa moja kwa wananchi kulipigia kura jambo maalumu

linalojieleza kwa uwazi kabisa bila utata au mazonge yoyte ya kufahamika.

3.0 MAPITIO YA KURA ZA MAONI KWA BAADHI YA SEHEMU MBALI

MBALI ULIMWENGUNI.

Kura ya maoni kwa uhakika si jambo geni na zimeshafanywa nyingi sana katika nchi

mbali mbali duniani. Kwahiyo hakuna ukosefu wa mifano duniani ya kuonyesha jinsi

kura za maoni zilivyotumika kutatuwa jambo maalumu la kisiasa. Ndani ya nchi ya

Marekani (USA) kuna jumla ya States 16 (yaani nchi kuminasita) zinazotumia Kura ya

maoni kuamua masuala mbali mbali makuu ya kisiasa katika nchi zao. Pia kwa Bara la

Ulaya, nchi zote ziliomo katika Jumuiya ya Ulaya (European Union) zimefanya kura ya

3
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

maoni katika kuamua aidha wakubali kutumia sarafu na noti ya aina Euro. Na zoezi hilo

kwa kweli limedhihirisha wazi wazi duniani nguvu za wananchi kufanya maamuzi

wenyewe wayatakayo pindipo Bunge na Serikali itawapa fursa hiyo ya kidemokrasia.

Katika baadhi ya nchi maamuzi ya wananchi yalikuwa kinyume na yale

waliyoyapendelea viongozi wa nchi. Inafaa kuangalia mifano zaidi ili kufahamu hoja

mbali mbali zinazopigiwa kura na matokeo yake. Kwa mfano:

• Nchi ya Spain mwaka 1976 walipiga kura ya maoni kubadilisha mfumo wao wa

kisiasa baada ya kifo cha Mtawala dikteta wa nchi hiyo Raisi Franco, na mwaka

1986 walipiga kura ya maoni kuhusu kujiunga na NATO (Jumuiya ya Mashirikiano

ya Kijeshi ya Ulaya na Marekani).

• Denmark pamoja na kuwa ni nchi iliyomo katika Jumuia ya Ulaya, lakini kwa kura ya

maoni kupitia wananchi wao waliamua kujitoa katika suala la kuwa na sarafu ya

pamoja ya Euro.

• Nchi ya Venezuela chini ya Serikali ya Hugo Chavez tokea mwaka 1999 imejiwekea

utaratibu kikatiba unaoruhusu wananchi kupigia kura ya maoni ya kuamuwa aidha

kiongozi aendelee na madaraka yake au aondolewe mradi tu kiongozi huyo ni

mtu aliyechaguliwa kwa kura katika uchaguzi mkuu. Na nafasi hiyo ya kikatiba

na kidemokrasia iliweza kutumiwa mwaka 2004 ambapo baadhi ya watu walidai na

haki ya kikatiba ikatumika kupiga kura ya maoni ya aidha Chavez aendelee na

madaraka au aondoshe na hatima ya matokeo ni kuwa Chavez alinusurika kubaki

madarakani.

4
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

• Nchi ya Puerto Rico ambayo sasa hivi bado ipo chini ya kukaliwa na Marekani,

iliwahi kuendesha kura za maoni mara tatu (katika mwaka 1967,1993 na 1998) ili

WaPuerto Rico waamuwa wenyewe kama wanataka wawe nchi huru au wanataka

wabaki chini ya Marekani kama “Commonwealth”. Matokeo ya kura wananchi

waliamuwa hapana kumaanisha wanataka kuwa chini ya Marekani, uhuru

wakaukataa. Katika jimbo la Quebec huko nchini Canada pia kura ya maoni ilipigwa

1995 ili watu wa Quebec wajitenge na Canada, lakini matokeo ya watu wa Quebec

wengi walipiga kuendelea kubaki katika shirikisho na Canada.

• Nchi kama East Timor(iliyokiwa sehemu ya Indonesia) , Croatia (ilikuwa sehemu ya

Yugoslavia) na Eritrea (ilikuwa sehemu ya Ethiopia) kwa kura za maoni katika nchi

hizo zimekuwa huru.

• Kwa mfano wa karibu yetu hapa Afrika Mashariki ni kura ya maoni ilipigwa Kenya

mwaka 2005 kwa ajili ya kuamua ama kufanya mabadiliko ya Kikatiba au kuiwacha

katiba waliyonayo kuendelea, na matokeo yakawa ushindi ni kwa wale waliotaka

mabadiliko ya Katiba.

Mifano niliyotajwa ni sehemu ya maeneo nyeti ya kisiasa ambayo yamekuwa yakipigiwa

kura na Wazanzibari na viongozi wanafaa kuangalia kwa makini na bila woga vipi

wanaweza kutumia kutanuwa utumizi wa kura ya maoni ikiwa ni sehemu ya kukuza

demokrasia ili kutatua matatizo makuu ya kisiasa lakini pia itasaidia ufanisi na

uwajibikaji katika sekta mbali mbali za kimaendeleo. Zanzibar ya leo na siku za usoni, ili

iweze kuwa imara na mustakabali mzuri basi ni lazima iendelee kukuza demokrasia na

kusaka maendeleo kwa nguvu, hasa tukizingatia katika dunia ya leo iliyojaa ushindani

5
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

wa kibiashara, mafanikio hutegemea mazingira mazuri ya kisiasa, yenye uwazi ya

kidemokrasia, utulivu na umoja ndani ya nchi. Labda nifunge maelezo yangu katika

kifungu hiki kwa kusisitizia kuwa, pamoja na mifano mbali mbali ya kura za maoni

niliyoitaja hapo juu, kura ya maoni inayotakikana kufanyika Zanzibar ni mfano wa aina

yake. Kura hii ya maoni imeletwa kwa ajili umuhimu na ulazima ambao Baraza la

Wawakilishi waliuona wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa baina ya Chama

kitachoshinda uchaguzi na kuvishirikisha vyama vingine vyote vitakavyoshiriki na

kushinda asilimia kubwa ya viti katika uchaguzi kiasi cha kuleta mchuano. Bila shaka,

yeyote anayefuatilia siasa za Zanzibar, ikiwa hayakutokezea mabadiliko makubwa sana

ya kuteteresha moja ya vyama viwili vikubwa vyenye ushindani nchini Zanzibar basi

washiriki wakuu wa serikali hii watakuwa CCM na CUF.

4.0. KUTOFAHAMIANA NA MAFAHAMIANO YALIOLETEA HALI YA KUJA

KURA YA MAONI:

Kuanzia miaka ya tisini, karibu nchi zote za Afrika zililazimika kuanzisha demokrasia ya

vyama vingi. Zanzibar pia ilikuwa katika mkumbo huo na kuanza ukuwaji wake wa

demokrasia. Demokrasia ya kweli kawaida huruhusu mabadiliko, hilo haliepukiki na

linaeleweka kwa yeyote mwenye kuifahamu demokrasia. Sio tu kubadilisha vyama

vinavyotawala bali huowa changa moto wa mijadala inayoweza kuleta mabadiliko juu ya

masuala mbali mbali makuu ya kisiasa, ama miundo ya Serikali na mifumo ya utawala,

mabadiliko makubwa ya kikatiba, na kadhalika na kadhalika. Na ni wazi kabisa, kwa

6
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

yeyote yule anayefuatilia siasa za Zanzibar, ataweza kuona kuwa Wazanzibar wa marika

yote ni wana demokrasia halisi wenye kudai mabadiliko ndani ya vyama vyao na nje.

Zanzibar imepitia vipindi vigumu vya kisiasa kabla ya uhuru na baada ya uhuru, na pia

kabla ya demokrasia ya vyama vingi iliyoanza 1992. Kila uchaguzi kuanzia ule wa 1995

ulikuwa na migogoro na vurugu. Pia chaguzi za Zanzibar za mwaka 2000 na 2005

zimeifanya Zanzibar ionekane na dunia mfano wa nchi inayoshindwa kabisa kuendesha

uchaguzi kwa kistaarabu na ustahamilivu bila ya kuwepo na umwagaji wa damu, jambo

ambalo halikubaliki duniani kimataifa na halipendezi hata katika macho ya wananchi

wenyewe nchini.

Ni dhahiri, miafaka kadhaa baina ya vyama vya CCM na CUF na jitihada mbali mbali za

wapatanishi kutoka nje ya nchi na ndani na hata mwisho wake Raisi wa Jamhuri ya

Muungano wa Tanzania, Mhe Jakaya Mrisho Kikwete, wote wameshindwa. kuleta

makubaliano yaliyokamilika kiutekelezaji na mustakabali mwema nchini. Jamii ya

KiZanzibari imeendelea kugawika katikati zaidi kwa kipindi cha karibuni kwa msingi wa

Chama cha CUF na CCM kwa kutaja alau moja ya mgawiko mmoja mkubwa wa kisiasa,

chuki zikaendelea kumea baina ya wananchi hata katika masuala ya jamii, kibinaadamu

na mlahaka (kwa mfano: Kushindwa hata kuzikana, kunyimana huduma za kibiashara na

kusaiidiana baina ya ndugu na majirani waliokuwa na mlahaka mzuri hapo awali) na

zaidi kuzoroteka kwa maendeleo kutokana na wananchi na viongozi wa nchi kukosa

umoja na ushirikiano.

7
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

Professa Issa Shivji katika barua yake ya wazi kwa Mheshimiwa Rais Dk. Amani A.

Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliweka wazi maoni yake

kama aonavyo kwamba sababu kuu ya jitihada zilizokuwa zikifanywa kuleta upatanishi

kutokuzaa matunda ni kuwa wanasiasa wa Zanzibar waliweka maslahi yao ya muda

mfupi mbele ya maslahi ya taifa/jamii (Mzalendo.net, jan 2010). Ni wazi kabisa, katika

hii n’ngwe ya mwisho ya Uraisi wake, Mheshimiwa Amani Karume, uamuzi waliofikia

yeye Raisi Amani Karume (ambaye pia ni kiongozi wa CCM) na, Maalim Seif Sharif

Hamad (Katibu Mkuu wa CUF) kwamba wazungumze na wazizike tafauti zao za kisiasa

kwa maslahi ya taifa la Zanzibar kwa kiasi kikubwa kumechangia kuleta hisia mpya

nchini ya umoja na ushirikiano miongoni mwa Wazanzibar. Tukikubaliana na uchambuzi

wa Professa Shivji basi tendo la Mheshimiwa Amani Karume na Maalim Seif Sharif

kuzika tafauti zao, limeashiria kukubalika na wananchi kuwa viongozi hawa

wametanabahi kuwa maslahi ya taifa wameyapa nafasi yake ya juu yanayostahiki kuliko

yale ya binafsi ya vyeo vya uraisi au uchama.

Makubaliano hayo ndio yaliyokuwa chachu iliyopelekea hata kufika hatua ya kupitisha

Sheria itayoruhusu kuwepo kura ya maoni na kuleta muundo wa Serikali ya umoja

nchini. Hapa ndipo Wanasiasa wa Zanzibar walipoanza kuonesha upevu wa kuelekea

kwenye safari refu ya demokrasia ya kweli, safari ambayo itaweza kulinda mustakabali

wa nchi ya Zanzibar. Katika nchi kadhaa zenye demokrasia duniani, baadhi ya masuala

makubwa ya kisiasa yanapotokezea, si ajabu kabisa kwa viongozi hutoa nafasi kwa

wananchi wenyewe kuamua kwa kura ya maoni. Hiyo ni njia moja ya utanuwaji wa

uga/uwanja wa demokrasia ambao humpa nafasi kila mwananchi kutoa maamuzi katika

suala hilo. Utafiti na maoni mbali mbali yameonyesha kuwa hadi sasa kuna waliotuliza

8
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

vichwa vyao na kutoendekeza ushabiki, woga au uchama wao, na wanasema hii ni nafasi

adimu isiyofaa kuachwa ikapotea. Hao ndio wanaotaka mabadiliko haya yaje. Na kura

nyingi za ndio katika Baraza la Wawakilishi ilikuwa ni sehemu ya uwakilisho wa

mawazo yao. Lakini lazima ikubalike, katika kuleta mabadiliko yoyote makubwa ya

kisiasa ni wazi kuna wale ambao hawatokubaliana na njia hiyo ya kuleta mabadiliko,

aidha wakiwa na njia mbadala au hata ikiwa hawana au wanapenda tu hali iliyopo

iendelee. Pindipo hoja inakubalika na wengi haina maana wale walioikataa au moyo wao

ulikuwa na mashaka na hoja hiyo ya kura kuwa sio wazalendo au ana walakini, ni lazima

kabisa demokrasia inayopevuka au iliopevuka ijenge mihimili ya ustahamilivu. Wana

demokrasia katika kura ya maoni lazima kuheshimu pale hoja inapokubaliwa au

kukataliwa. Pia lazima kuwaheshimu wale walioikataa hoja, ijapokuwa kukataa kwao

hakutokuwa kumeweza kuletea kuzuia mabadiliko. Kizazi kipya ni busara kuandaliwa na

kibadilika ili kuachana na siasa za chuki na uhasama ambazo zinarudisha nyuma

maendeleo na badala yake kuimarisha umoja wa kitaifa. Ili kufikia hatua hiyo, ni lazima

taifa na vyama kutowa kipaumbele kwenye suala la mafunzo juu ya uvumilivu wa kisiasa

na ushindani wa vyama vya siasa. Pindipo hilo litachukuliwa uzito kama ambavyo umoja

wa kitaifa unavyotakiwa upewe uzito, hiyo itakuwa ni dawa ya kuondosha misukosuko,

chuki na uadui uliotawala ndani ya siasa za Zanzibar.

5.0 WAZO LA KURA YA MAONI NA UFUATILIAJI WAKE.

Wazo la kupiga kura ya maoni lilitolewa Januari mwaka huu wa elfu mbili na kumi na

Kiongozi wa Upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Abubakari Khamis Bakari. Mhe.

Bakari aliwasilishwa Barazani mswada uliopendekeza yafanyike mabadiliko katika

9
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

Katiba ya Zanzibar iweze ruhusu kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Mswada

huo ulijadiliwa katika Baraza la Wawakilishi na kupigiwa kuwa na Wawakilishi wote, na

ukapitishwa na wawakilishi hao wote kwa asilimia mia. Ulipitishwa kwa sharti ya

kwamba wapewe nafasi Wazanzibari kwa kutumia kura ya maoni ili waweze kuamua

kama wanataka serikali ya umoja au la.

Wakati akiwasilisha mswada huo, Mhe. Abubakar Kh. Bakari aliilezewa kwa uwazi na

ufasaha kabisa sababu ya kuleta hoja hii ya Serikali ya Umoja ni kwamba hii anaiona ni

njia pekee itakayopelekea kuleta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo sugu la ugomvi wa

kisiasa kila baada ya uchaguzi na pia itawaunganisha wananchi wa Zanzibar (Daily

News, March 30,2010). Lakini tukiangalia dunia nzima, suala la Serikali ya Umoja nalo

sio geni duniani na lishatumika nchi kadhaa kutatuwa mizozo. Serikali za mseto au umoja

wa kitaifa mara nyingi huanzishwa pale inapojitokeza nchi inakuwa na mvutano mkubwa

wa kisiasa baina ya vyama vinavyoshindana au vurumai limetokezea na mara nyengine

hata damu kumwagika. Kwa mfano Kenya au Zimbabwe ni mfano wa nchi damu

zilimwagika ndipo Serikali ya Umoja wa kitaifa ikaundwa. Afrika ya Kusini ni nchi

iliyotokana na mifarakano mikubwa kabla ya uchaguzi wao wa mwaka 1994. Ili

kuepusha mifarakano hiyo kuwa mkubwa nchini baada ya African National Congress

kushinda uchaguzi na kutwaa madaraka ya Serikali na pia katika kuhakikisha

wanaimarisha maslahi ya taifa lao kwanza kuliko ya binafsi na uchama waliunda Serikali

ya Umoja wa Kitaifa. Hili liliendelea kumuwekea nyongeza nyengine kubwa sana ya sifa

ya uongozi Raisi Mandela. Mfano mzuri wa kufuatwa ni wa Afrika ya Kusini zaidi

kuliko wa Zimbabwe au Kenya. Kwani utaratibu walioutumia Afrika ya Kusini ni wa

10
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

kuchukua tahadhari kabla ya athari haijawa kubwa. Inaingia akilini kabisa, ikiwa njia hii

ni tabibu kwa mizozo ya kisiasa, na Zanzibar inao mzozo wa kisiasa kila uchaguzi, basi

inaingilia akilini kabisa kukubali kutumia dawa hii ili kuingalia kama itaitibu Zanzibar.

Tukiachilia mbali Serikali ya umoja wa kitaifa, hata mbinu ya uundwaji serikali za mseto

hutumika sana nchi za ulaya ili kuondoa mivutano na kufanya nchi ziendelee kutawalika,

kuwa na utulivu na wananchi wake wafaidike na sera za maendeleo zinazotekelezwa na

serikali iliyopo madarakani ya mseto. Mfano huu upo kwa nchi nyingi kama vile Israel,

Ujarumani, Italy na hata Australia ambazo zote hizi huwa na serikali za mseto.

Kwa kuendelea kukaa juu ya mstari katika mada hii inayohusu ufuatiliaji wa upigaji kura

ya maoni. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) inabidi ijadiliwe. Kutokana na maelezo

ya Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Bw. Khatib Mwinyichande ( July 13,2010) ni

kwamba Tume ya Uchaguzi Zanzibar imewezeshwa kuendesha shughuli za Upigaji kura

ya Maoni baada ya kuitishwa Sheria ya namba 6 ya mwaka 2010 chini ya maelezo

yaliyomo katika kifungu 3, kijifungu 1. Kwa mujibu wa maelezo ya Bw. Mwinyichande

ni kuwa kifungu hiki ni muhimu sana kwa demokrasia inayoambatana na upigaji kura ya

maoni kwani imeweka “precedence” (kigezo cha msingi kisheria) ambacho kinaweza

kufuatwa kwa suala lolote jengine la kisiasa ikihitajika upigaji kura wa maoni.

imepitishwa kuweza kuiruhusu iweze kusimamia upigaji kura huo”. ikiwa ni pamoja na

kupanga tarehe na kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki.

Kwa mujibu wa muswada huo, ni Wanzibari waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu

la Wapiga kura tu, ndio watakaopiga kura ya kuulizwa ama kujibu ndio au hapana na

11
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

gharama za shughuli hiyo zitabebwa na Wizara ya Fedha. Tume ya Uchaguzi itatumia

majimbo yale yale yaliyopangwa kwa ajili ya uchaguzi mkuu na vituo vile vile katika

kuendesha kura hiyo. Na Tume ya Uchaguzi (ZEC) ndio watakaotangaza matokeo na

kama kutatokea shaka katika matokeo hayo, haitatiliwa maanani na kama ikitokea

matokeo hayo yakafungana (yaani yamekuwa sare), Tume itatangaza tarehe nyingine

katika kipindi cha mwezi mmoja baada ya matokeo hayo, kwa ajili ya upigaji kura

mwingine. Itakuwa ni kosa kwa mtu au taasisi kutangaza matokeo ya kura hizo kabla ya

ZEC na unapendekeza faini ya kati ya Sh milioni moja hadi 10 au kifungo cha miaka

mitatu jela au adhabu zote kwa pamoja. Kwa maelezo ya Mwenyekiti Mwinchande

pindipo patatokea jambo lililokuwa katika uendeshaji wa kura hiyo ya maoni

halikuelezwa katika sheria ya kura ya maoni basi sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1984

(ambayo imefanyiwa marekebisho mara kadhaa kila uchaguzi) ndiyo itafuatwa.

Kura ya maoni inatarajiwa tarehe 31 Julai 2010, na hivi sasa ZEC kupitia msaada ya

Shirika la Umoja wa mataifa la Misaada ya Maendeleo (UNDP) imeweza kufanya

maendeleo ya elimu ya wapiga kura kupitia vikundi na jumuia mbali mbali za katika

mitaa na vijiji. Hizi jumuia ndio zinasaidia hata kusambaza taarifa na karatasi matangazo

au maandishi (posters and leaflets). Ni ZEC yenyewe iliyoandaa na kuendesha kura ya

maoni Julai 31 kwa kutumia wafanyakazi ambao wamewaajiri na wanawapa mafunzo

kwa sasa hivi.

Katika jumla ya haki za mpiga kura hiyo ya maoni ni kwamba, Mzanzibari aliyepiga kura

anaruhusiwa kukata rufaa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar. Uamuzi wa mahakama

hiyo ndio utakuwa wa mwisho na hakuna rufani itakayokubaliwa katika Mahakama ya

Rufani, Lakini kabla ya mtu kukata rufaa dhidi ya matokeo ya upigaji kura huo, atatakiwa

12
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

kwanza kuwa na wapiga kura 10 kutoka kila mkoa visiwani hapa, wanaomuunga mkono

na kulipa Sh milioni tano kwa ajili ya kufungulia kesi siku 30 baada ya matokeo

kutangazwa. Shindikizo langu katika mada hii ni kuwa kuwaelimisha wananchi sio tu

namna ya kupiga kura yenyewe bali pia kuwaeleza ina umuhimu wa Kura hiyo ya maoni

kwa maslahi ya taifa zima la Zanzibar kwa kipindi cha muda mfupi na baadae. Katika

demokrasia yoyote ni wajibu sio tu kuwafanya wapige kura bali wajadili kwa kina na

kuelewa ili wajue faida na hasara za kuwa na muundo huo mpya na faida na hasara za

muundo uliopo. Hili ni muhimu kwani maamuzi ya hao wananchi ikiwa ni kura ya Ndio,

uamuzi huo utawafanya waishi na huo muundo mpya kwa miaka ifuatayo, na

wakaiamuwa kutia kura ya Hapana ama kwa kutokuelewa au kughilibiwa wataendelea

kuishi na mfumo uliopo. Kura ya maoni kwenye nchi mbali mbali huelimisha na

huchangamsha jamii kwa ngoma , nyimbo vifijo kila mtu anapojitahidi kueleza au

kuunga mkono au kukataa hoja. Kwahiyo kuachiwe uhuru wa kutia kampeni.

6.0. KURA HII YA MAONI INA UMUHIMU GANI NA ITASAIDIA NINI

KATIKA MUSTAKABALI WA ZANZIBAR .

a) Kutoa nafasi zaidi ya kutanuka kwa demokrasia: Umuhimu wa kura ya maoni ya

mwaka huu pindipo wananchi watasema ndio au hapana, basi la kwanza kabisa

lililopatikana ni kuwa Zanzibar imeshajijengea utaratibu wa kisheria utaoruhusu kupiga

kura ya maoni kwenye masuala muhimu ya kisiasa, uchumi, kero za muungano au hata

uongozi.

b) Kuwafanya wananchi wafahamu kuwa wanayo sauti katika masuala muhimu ya

kisiasa katika nchi: Pindipo masuala mengi makubwa ya kinchi ambayo hatima yake

13
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

yanawaathiri wananchi kila siku yanafanywa bila ya kuwashirikisha wananchi , basi si

ajabu kuwa na wananchi wanaolalamika na kutoridhika sana na Serikali na viongozi wao.

Na hakuna njia bora ya kuwashirikisha wananchi katika maamuzi inayoizidi hii ya Kura

ya maoni.

c) Kisiasa: Kuondosha siasa za utengano, chuki, ubaguzi, uhasama, ugomvi na visasi

miongoni mwa wananchi na kuleta siasa za umoja, maelewano na mashirikiano (Seif

Sharif hamad, 2010)

d) Kiusalama: Kuondoa khofu na wasiwasi kwa kufuta viashiria vinavyoweza kuwa

chanzo cha fujo na ghasia na ambavyo vingeweza kutumiwa hata na maadui wa Tanzania

kuhatarisha usalama wa nchi na badala yake kuleta hali ya amani na usalama ambayo

inavifanya hata vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi zao katika hali ya utulivu na

ushirikiano na wananchi wote (Seif Sharif hamad, 2010)

c) Kiuchumi: Kuondoa hali iliyokuwepo ya sehemu ya wananchi kujiona

hawashirikishwi au hawapaswi kushiriki katika harakati za ujenzi wa nchi na kuwaleta

pamoja wananchi wote ili kwa pamoja tushiriki katika ujenzi wa Zanzibar mpya(Seif

Sharif hamad, 2010)

d.)Kijamii: Kuondoa hali ya utengano na kutoaminiana miongoni mwa wafuasi wa

vyama tofauti vya siasa na kuwafanya wapendane na washirikiane katika shughuli zote za

kijamii wakijua kuwa wote ni wananchi wa nchi moja (Seif Sharif hamad, 2010). Katika

dunia ya leo, Serikali pekee hazikidhi mahitaji yote ya jamii kwenye huduma za elimu,

14
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

afya, maji safi , umeme na kadhalika. Jamii iliyoshikamana hujikusanya na kusaidiana

kupitia jumuiya zisizo za kiserikali. Ushirikishwaji wa wananchi wa Zanzibari walio

ndani na nje ya nchi katika ujenzi wa taifa utaweza kusaidia hasa maeneo ya huduma za

jamii kuitia jumuia zisizo za Kiserikali.

e) Haja ya kuwa katika Muungano usiodhoofisha mamlaka ya Zanzibar kwa

mujibu wa katiba zote mbili za Muungano na Zanzibar: Zanzibar ilioyo na

viongozi walioshikamana kwa maslahi ya taifa ni Zanzibar imara ndani ya muungano.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari wakati akigombea nafasi ya uraisi kwa

tiketi ya Chama cha mapinduzi, Bw. Muhammad Yussuf Mshamba alieleza kuwa

kuimarisha Muungano haina maana hata kidogo ya kuingiza kila kitu katika orodha

ya mambo ya Muungano. Na kusisitiza kuwa ukweli usiofichika kuwa Muungano

utaimarika zaidi ikiwa hatua za makusudi zitachukuliwa kuyaondoa yale mambo yote

yaliyomo katika orodha ya Muungano ambayo upande mmoja wa Muungano

unaamini kuwa kuendelea kubakia kwake hakuleti faida wala maslahi mazuri kwake

na hivyo kuna muelekeo wa kuuathiri vibaya upande wake. Hili halina mjadala ikiwa

dhana ya kuanzishwa kwa Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar imejengeka

kikweli kweli katika misingi ya usawa, uhuru na upendo tokea hapo awali.

Mustakabali wa Zanzibar utapatikana ikiwa katika kuimarisha misingi ya usawa,

uhuru na upendo utaimarishwa Zanzibar basi ni wazi misingi hiyo ionekane katika

muungano. Kwani hayo ndio yatakuwa maadili ya Wazanzibari. . Kwa mfano tu,

Suala la Mambo ya Nje kweli ni la Muungano, lakini ni wazi masuala ya

Mashirikiano ya Kimataifa kwa Maendeleo (International Development) haya

15
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

yalikuja baadae. Ni masuala mashirikianao ya kimataifa kwa misaada ya maendeleo

ndio mara nyingi tunakuwa na mivutano. Zanzibar inahitaji kuwa na uhuru wa

kutosha kushirikiana na nchi mbali mbali na jumuiya mbali kwa missada ya

maendeleo bila kuingiliwa na SMT. Hii ni sehemu ya mustakabali wa Zanzibar.

f) Haja ya kusimamia imara rasilmali za nchi : Mwananchi mpenda nchi ni yule aliye

imara kulinda mali za nchi. Mwananchi mpenda nchi huwa si mla rushwa na mwenye

kutetea na kuona uchungu pindipo mali ya taifa anaiona inaporwa. Mwananchi

mpenda nchi ni yule anayetaka haki, na mali binafsi za raia mwenzake zilindwe

kama atakavyo zake zilindwe. Nchi yenye raia wasio na hisia na nchi yao huwa

hawajali mali za taifa lao na si walinzi wa raia mwenziwao/wenziwao. Mustakabali

wa Zanzibar utapatikana kuziimarisha hisia hizi. Serikali ya umoja inayo nafasi

kubwa kuzijenga hisia hizi. Masuala kadhaa nyeti yamejitokeza kwa jina la kero za

muungano yanahusu rasilmali za Zanzibar. Zanzibar haina muda wa kupoteza

kwenye mambo ya kutofahamiana wenyewe kwa wenyewe na kushindwa kutumia

wakati wake vizuri kujiimarisha kwenye madai na mijadala inayohusu umilikaji wa

gesi asilia au uchangiaji gharama za muungano na mgawanyo wa mapato

yapatikanayo.

7.0. HITIMISHO:

Mwisho, waraka huu unahitimisha kwa maoni ya kwamba kura ya maoni ni muhimu kwa

vile inaruhusu msimamo wa walio wengi kukubalika kama ndio ridhaa ya wananchi na

ndio uamuzi wa mwisho kinyume na hali ambayo uamuzi ungefanywa na wachache

katika vyombo vya dola. Kwa maana hii basi kura ya maoni inawakilisha matakwa ya

16
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

kweli, inaonyesha matarajio na matamanio ya kweli kabisa ya wananchi wenyewe katika

jamii au nchi. Kura ya maoni inastahiki na ina faida sana pale ambapo kuna masuala

nyeti ya kitaifa kwa ajili ya taifa.

Marejeo (References)

1. Mark N. Franklin, Cees van der Eijk and Michael Marsh, (1995) Referendum

outcomes and trust in government: Public support for Europe in the wake of

Maastricht, West European Politics, Vol 18, 1995

2. Muhammad Yussuf, (2010), Hotuba iliyotolewa kwa waandishi wa Habari na

Bwana Muhammad Yussuf kuelezea azma yake ya kutaka kugombea nafasi ya

Urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi katika ukumbi wa

EACTROTANAL siku ya Alkhamisi tarehe 24 Juni 2010, Zanzibar.

3. Natelson, Robert G. (1999), Are Initiatives And Referenda Contrary To The

Constitution's "Republican Form Of Government"?

4. Norman, A. S1 and Kwadwo, Sarfo Kantanka, (1999), The role of referendum: A

case of Ghana, African Journal of History and Culture (AJHC) Vol. 1 (1), pp.

001-005, May, 2009 -Available online at http://www.academicjournals.org/AJHC

5. UNDP, (2010), Election Support project, Newsletter No. 6, May 2010

6. Gay, Oonagh and Wood Edward, (2000) House of Commons, 2000, The Political

Parties, Elections and Referendums Bill – Referendums and Broadcasting Bill 34

1999-2000

7. Zanzibar: Democracy on Shaky Foundations, Article 191, April 2000

17
Kopi zinapatikana MZALENDO.NET

Marejeo kutoka Mtandaoni

8. Shivji, Issa, 2010, Barua ya wazi kwa Mheshimiwa Rais Karume na Maalim Seif

- http://hakinaumma.wordpress.com/2010/01/

9. Issa Seif Sharif Hamad , 2010, Maridhiano na Mustakbali wa Zanzibar, Januari,

23,2010-http://hakinaumma.wordpress.com/2010/01/23/maridhiano-na-

mustakbali-wa-zanzibar/)

10. http://www.thefreedictionary.com/referendum

11. http:// www.Mzalendo.net

12. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rasimu ya Mswada wa Sheria ya Mabadiliko

ya nane katika Katiba ya Zanzibar ya 1984.

Mahojiano kwa Simu

13. Bw. Khatib Mwinyichande, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, tarehe 13 Julai

2010.

14. Bw. Ramadhan Omar, wa Mwembetanga, 13 Julai 2010

15. Bw. . Zahor Mzee Salum, Miembeni, 6 Julai,2010.

16. Bw. Juma Janja, Kiembesamaki 12 Julai, 2010

18

You might also like