You are on page 1of 4

1

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII







TAMKO LA SERIKALI KUHUSU TETESI ZA KUWEPO
MGONJWA ANAYEHISIWA KUWA NA UGONJWA WA EBOLA
WILAYANI SENGEREMA MKOANI MWANZA

20 Oktoba 2014
Utangulizi

Mnamo tarehe 18 Oktoba 2014, Wizara ilipokea taarifa kutoka Ofisi
ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ya kuwepo kwa mgonjwa
aliyehisiwa kuwa na ugonjwa wa Ebola. Mgonjwa huyu aliyekuwa na
umri wa miaka 17, jinsia ya Kike na mkazi wa kijiji cha Bupandwa
Tarafa ya Kahunda Wilaya ya Sengerema, alilazwa akiwa na dalili za
homa kali, manjano, kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili.

Mgonjwa huyu alilazwa katika Kituo cha Afya Mwangika tarehe 15
hadi 16 Oktoba, 2014 ambapo pia alionekana kuwa vimelea vya
ugonjwa wa Malaria kabla ya kuhamishiwa Hospitali Teule ya Wilaya
ya Sengerema mnamo tarehe 17 oktoba 2014 na kufariki duniani siku
hiyo hiyo muda wa saa 3.30 usiku.

Hata hivyo, mgonjwa huyu hakuwa na historia ya kusafiri kwenda
nchi zilizoathirika na ugonjwa wa Ebola na hakuwahi kupokea mgeni
kutoka nchi hizo ndani ya siku ya 21 zilizopita.
2



Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na;

i. Sampuli ya damu ya mgonjwa kwa ajili ya uchunguzi wa
Kimaabara ilipokelewa tarehe 18 Oktoba, 2014. Matokeo ya
awali dhidi ya magonjwa ya jamii ya ebola yakiwa ni pamoja na
Dengue na Chikungunya yanaonyesha kuwa mgonjwa hakuwa
na magonjwa haya. Uchunguzi wa kimaabara bado unaendelea
na Wizara itatoa taarifa rasmi pindi utakapokamilika.
ii. Mgonjwa alihudumiwa katika chumba maalumu kilichotengwa
ambapo wahudumu pamoja na walioshughulikia mazishi yake
walivaa vifaa kinga (PPE)
iii. Wataalamu pamoja na ndugu waliomhudumia mgonjwa kabla
ya mauti kumfika wametengwa na wapo kwenye uangalizi
maalumu

Mwongozo wa utambuzi wa ugonjwa huu (Standard Case
Definition) unaeleza kwamba ili mgonjwa aweze kuhusiwa kuwa na
ugonjwa wa Ebola anatakiwa akidhi vigezo ifuatavyo:
i. Dalili za awali ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu
ya misuli, kuumwa na kichwa, na kutokwa na vidonda kooni.
Mara nyingi dalili hizi hufuatiwa na kutapika,
kuharisha,kutokwa na vipele vya ngozi, kwa baadhi ya
wagonjwa hutokwa na damu ndani na nje ya mwili
3
ii. Awe amesafiri kwenda sehemu zilizothibitishwa kuwa na
ugonjwa wa ebola ndani ya kipindi cha wiki 3
iii. Kugusa majimaji kutoka kwa mgonjwa, maiti au mnyama
anayehisiwa au kuthibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola.

Hitimisho

Wizara inapenda kuwatoa hofu wananchi kuwa hadi sasa
HAKUNA MGONJWA yeyote aliyethibitishwa kuwa na virusi vya
ugonjwa wa Ebola hapa nchini. Hata hivyo uchunguzi wa kina
wa Kimaabara unaendelea na taarifa itatolewa baada ya majibu
kupatikana

Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu ila kuendelea kuchukua
tahadhari za kuepuka kupata maambukizi ya ugonjwa huu ambazo:-
o Kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho,
kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini
mwa mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola kupitia sehemu
zenye michubuko au vidonda.
o Kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa na dalili
za ugonjwa wa Ebola; badala yake watoe taarifa kwa uongozi
wa kituo cha huduma za Afya kwa ushauri. Wataalam
watasimamia maziko ikiwa itatokea.
o Wananchi waepuke mila na desturi zinazoweza kuchelewesha
kupata huduma muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa wa Ebola.
4
o Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na watoa
huduma za Afya katika ngazi zote pale anapotokea mtu
mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
o Kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za Afya pale mtu
anapohisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
Imetolewa na,

Dkt. Donan Mmbando


KAIMU KATIBU MKUU
20 Oktoba, 2014

You might also like