You are on page 1of 3

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

4 APRILI, 2016
MAAZIMIO YA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA LA CHAMA KATIKA
KIKAO CHAKE CHA TAREHE 2 3 APRILI, 2016 KILICHOFANYIKA MAZSONS
HOTEL, MJINI ZANZIBAR
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la THE CIVIC UNITED FRONT (CUF Chama Cha
Wananchi) limefanya kikao chake cha kawaida kwa siku mbili, tarehe 2 hadi 3 Aprili, 2016
mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama, Mheshimiwa Twaha
Taslima.
Ajenda kuu ya kikao hicho ilikuwa ni Hali ya Kisiasa Zanzibar na mwelekeo wa CUF baada
ya kufanyika kile kilichoitwa uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi, 2016.
Baada ya kupokea na kujadili kwa kina ajenda hiyo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa
limefikia maazimio yafuatayo:
1. Linawapongeza wananchi wote wa Zanzibar kwa ujasiri, uzalendo na ari kubwa
walioionesha kwa kuitikia kwa kiasi kikubwa wito wa chama chao cha CUF wa kuwataka
wasishiriki katika uhuni na ubakaji wa demokrasia uliopewa jina la uchaguzi wa marudio wa
tarehe 20 Machi, 2016. Baraza Kuu la Uongozi limefurahishwa kuona zaidi ya asilimia 80 ya
wapiga kura wa Zanzibar hawakujitokeza kushiriki katika uchaguzi huo haramu na batili, na
hivyo kuudhihirishia ulimwengu kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakina ridhaa ya
wapiga kura hao.
2. Linawapongeza waliokuwa wagombea wa CUF kwa nafasi zote za Urais, Uwakilishi na
Udiwani kwa kuheshimu maamuzi ya Chama na kutoshiriki uchaguzi haramu na batili wa
marudio licha ya njama nyingi zilizokuwa zikifanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
chini ya Mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha, za kulazimisha ushiriki wao. Msimamo wa
wagombea hao umewadhihirishia na kuwathibitishia CCM kwamba tofauti na wao, viongozi
wa CUF hawajali nafasi na vyeo binafsi bali wanachotaka ni kuleta mabadiliko ya kweli kwa
maslahi ya watu wote wa Zanzibar.
3. Linawapongeza kwa namna ya pekee wagombea Urais, Uwakilishi na Udiwani wa vyama
vyengine vya upinzani ambavyo ni UMD, JAHAZI ASILIA, CHAUMMA, UPDP, DP, na
ACT-WAZALENDO, na vile vinavyoshirikiana kupitia UKAWA ambavyo ni CHADEMA,
NCCR na NLD vilivyoungana na wananchi wa Zanzibar kususia uchaguzi haramu na batili
wa marudio na kusimamia maamuzi halali ya wapiga kura waliyoyafanya kupitia uchaguzi
mkuu halali wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
4. Linazishukuru na kuzipongeza jumuiya na taasisi zote za kitaifa na kimataifa pamoja na
nchi rafiki za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo zilikataa kuleta waangalizi wa
uchaguzi katika uchaguzi huo haramu na batili na hivyo kuungana na Wazanzibari katika
kutetea maamuzi yao halali waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu halali uliokuwa huru na wa
haki wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
1

5. Linavishukuru na kuvipongeza vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi pamoja na
waandishi wa habari na wapiga picha kwa jinsi vilivyosaidia kuonesha ulimwengu uchaguzi
mkuu uliokuwa halali, huru na wa haki wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na pia kwa jinsi
vilivyoanika uchafuzi wa tarehe 20 Machi, 2016 hasa kule kuonesha vituo vya kupigia kura
vikiwa havina watu na hivyo kuwasaidia Watanzania na ulimwengu kuujua ukweli ambao
CCM na Tume yao ya Uchaguzi walikuwa wakijaribu kuuficha.
6. Linalaani tabia na mwenendo wa uongo, uzushi, na uvunjwaji wa Katiba, Sheria na
Maadili wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, dhidi ya
matakwa na maamuzi halali ya Wazanzibari waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu huru na wa
haki wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na kitendo chake cha kuiingiza Zanzibar katika dimbwi la
chuki, uhasama, uvunjifu wa haki za binadamu na udhalilishaji wa raia kwa sababu tu ya
kukiridhisha chama chake cha CCM ambacho kimekataliwa na Wazanzibari. Vitendo vya
Jecha Salim Jecha vimeishushia hadhi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na kuichafulia jina
Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mbele ya jumuiya ya kimataifa na
kuonekana haiko tofauti na nchi nyengine za Afrika zisizoheshimu matakwa na maamuzi ya
wananchi katika uchaguzi.
7. Linalaani hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. John Pombe
Magufuli kuleta nguvu kubwa ya vikosi vya ulinzi na usalama kuja kubaka demokrasia
Zanzibar. Baraza Kuu linalaani vikali nguvu kubwa iliyotumiwa na vyombo vya dola dhidi ya
raia wasio na hatia kwa lengo na madhumuni ya kuwatisha na kuwazuia wasitumie haki zao
za msingi kama ibada kwa kuwalazimisha kutotoka nje ya nyumba zao kuanzia saa 2 usiku
wakati muda huo ni muda wa ibada ya sala kwa Waislamu ambao ni asilimia 99 ya wananchi
wote wa Zanzibar. Baraza Kuu pia linalaani mwenendo wa viongozi wa juu wa vyombo vya
ulinzi na usalama wa kutumika waziwazi kisiasa kwa kuegemea upande wa CCM na
kuwakandimiza viongozi na wanachama wa CUF kinyume na maadili ya kazi zao.
8. Linalaani vitendo vya Serikali kuunda makundi ya kiharamia ambayo yamekuwa
yakiwahujumu raia wasio na hatia yakitumia silaha za moto na silaha za kienyeji huku
yakitumia gari za Idara Maalum za SMZ. Baraza Kuu linalaani Jeshi la Polisi ambalo
limekuwa likiyalinda makundi haya na kutochukua hatua zozote dhidi yao licha ya wananchi
wanaohujumiwa kutoa taarifa kwa jeshi hilo. Badala yake, katika matukio mengi Polisi
imewageuzia kibao wananchi waliohujumiwa kwa kuwakamata na kuwaweka ndani. Baraza
Kuu linawataka Wakuu wa Jeshi la Polisi kujirudi, kutekeleza majukumu yao ya kulinda
usalama wa raia na mali zao na na kufuata maadili yao na kuwacha kujifanya ni Idara ya
Polisi ya CCM.
9. Haliyatambui matokeo ya uchaguzi huo haramu na batili, na kwa msingi huo halimtambui
Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar, haliwatambui waliotangazwa kuwa
Wawakilishi na wala haliwatambui waliotangazwa kuwa Madiwani. Baraza Kuu linaungana
na wananchi wa Zanzibar waliokataa kuwapa uhalali watu hao na kwa hivyo halitoitambua
Serikali, Manispaa na Halmashauri za Wilaya zitakazoundwa na watu hao. CUF
haitoshirikiana na Serikali itakayoundwa kwa sababu ni kinyume na Katiba ya Zanzibar,
kinyume na Sheria ya Uchaguzi na haikutokana na ridhaa ya watu. Kwa vyovyote vile,
Serikali itakayoundwa haitakidhi matakwa ya Katiba ya Zanzibar na hivyo CUF haitoshiriki
kwenye uvunjaji wa Katiba ambayo inaeleza kwa uwazi kabisa namna ya kuundwa kwa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
10. Linawataka wananchi wote wa Zanzibar kutumia njia za amani, za kikatiba na kisheria
ambazo zimewahi kutumika katika nchi nyingine duniani kuwakataa watawala waovu na
wasio na ridhaa ya watu waliojiweka madarakani kwa kutumia nguvu na ubakaji wa
demokrasia kwa kutoipa ushirikiano Serikali itakayoundwa na watawala hao.
2

11. Linaendelea kuutambua uchaguzi mkuu uliokuwa halali, huru, wa haki na uliofanyika
katika hali ya amani na utulivu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na pia linayatambua matokeo yake
ambayo yalionesha wazi kwamba chaguo la Wazanzibari ni CUF na Maalim Seif Sharif
Hamad kuiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Kitendo cha zaidi ya asilimia 80
ya Wazanzibari kususia uchaguzi haramu na batili wa tarehe 20 Machi, 2016 kimezidi kuyapa
nguvu maamuzi yao ya tarehe 25 Oktoba, 2015 mbele ya macho ya Watanzania na dunia.
12. Linaendelea kuwataka Wazanzibari kuwa watulivu na kulinda amani iliyopo na
linawahakikishia kwamba CUF inaendelea na juhudi zake za kutafuta haki yao na kusimamia
maamuzi yao waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015 kwa njia za amani na za kidemokrasia.
Njia hizo za amani zimefanikiwa na kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa ambayo
imeanza kuchukua hatua dhidi ya ubakwaji wa demokrasia uliofanyika.
13. Linazishukuru na kuzipongeza nchi washirika wa maendeleo kwa kuchukua maamuzi ya
kuzifutia misaada Serikali za kidikteta za CCM ambazo zimebaka demokrasia na kukanyaga
haki za wananchi wa Zanzibar. Baraza Kuu linatoa wito kwa nchi hizo washirika wa
maendeleo na jumuiya za kimataifa kuchukua hatua zaidi dhidi ya Serikali za CCM na
madikteta wake walioshiriki katika ubakaji wa demokrasia Zanzibar zikiwemo hatua
makhsusi dhidi ya watu makhsusi waliohusika na ubakaji huo wa demokrasia na uvunjaji wa
haki za binadamu katika kipindi hiki.
MWISHO, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linawahakikishia wanachama wake wote na
Watanzania kwa ujumla kwamba chama chao kiko imara na hakitoyumba wala kuyumbishwa
katika kutetea na kupigania haki zao hadi tutakapofanikisha ujenzi wa taifa imara
linalosimamia na kuheshimu utawala wa sheria, haki za binadamu, demokrasia na utu wa
watu wote.
Baraza Kuu linawataka viongozi wa Chama wa ngazi zote watekeleze majukumu yao ya
kichama katika nafasi zao na pia Wabunge na Wawakilishi waliopewa ridhaa na Wazanzibari
tarehe 25 Oktoba, 2015 kuwatumikia wananchi wote katika kutatua matatizo yao kadiri hali
na uwezo wao unavyoruhusu. Mbali na maazimio haya, Maalim Seif Sharif Hamad
atazungumza na wananchi katika siku chache zijazo ili kuwaeleza kwa kina mwelekeo wa
hali ya kisiasa ya Zanzibar na hatua zinazochukuliwa na CUF kuhakikisha maamuzi halali ya
kidemokrasia ya Wazanzibari waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015 yanaheshimiwa.
HAKI SAWA KWA WOTE
Limetolewa na:
BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA
THE CIVIC UNITEDN FRONT (CUF Chama Cha Wananchi)
ZANZIBAR
4 APRILI, 2016

You might also like