Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amezitaka nchi za Maziwa Makuu na
Pembe ya Afrika kuanza utaratibu wa kuziweka alama silaha ndogo ndogo ili kufanikisha azma ya nchi hizo ya kudhibiti tatizo la kuzagaa kwa silaha haramu. Samia ametoa kauli hiyo leo kwenye ufunguzi wa mkutano wa mawaziri wa nchi wanachama wa Taasisi inayopambana na tatizo la Silaha haramu katika nchi za Maziwa Makuu na Pembe ya Afrika (RECSA) uliofanyika leo katika hoteli ya Naura Spring mjini Arusha Alisema utaratibu huo utasaidia kuzitambua silaha hizo zinatoka nchi gani endapo zitakamatwa na kuziharibu zisizokuwa na alama ili zisirudi tena mikononi mwa wananchi na kubainisha kuwa Tanzania tayari imeanza zoezi hilo. "Jambo jingine ambalo nimetilia mkazo ni kuzitaka nchi zetu kuziweka alama silaha ndogo ndogo. Tanzania tumeanza zoezi hili....zoezi hili linasaidia silaha yoyote ikikamatwa, tutajua inatoka nchi gani, kwa hiyo inakuwa rahisi kuziharibu zisizokuwa na alama zisirudi mikononi kwa wananchi," alisema Makamu wa Rais Alisema kuenea kwa silaha ndogo ndogo katika nchi hizo kumechochea makosa mbalimbali ya jinai yakiwamo ugaidi, ujangili, wizi wa kutumia silaha, uharamia na kuwafanya wananchi washindwe kufanya shughuli za maendeleo.
Makamu wa Rais aliueleza mkutano huo kuwa inakadiriwa silaha ndogo
ndogo zipatazo milioni 875 zimezagaa duniani kote na kati ya hizo asilimia 75 zinamilikiwa na raia iwe kihalali ama siyo kihalali ambapo zaidi ya milioni 100 ya silaha hizo zinapatikana Afrika. "Nyingi ya silaha hizo zinaingizwa kwenye soko haramu na kwa hiyo huchangia kudhoofisha amani na usalama, inapunguza upatikanaji wa huduma za jamii na hatimaye ni kurudisha nyuma maendeleo," alisema Samia. Alisema amepata taarifa kuwa watu wasio na hatia wapatao 1,000 wanakufa kila siku na kati ya watu 300,000 na 500,000 wanakufa kila mwaka duniani kote kwa matumizi mabaya ya silaha ndogo ndogo. Aliongeza kusema kuwa nchi zinazotengeneza silaha, hutengeneza kati ya silaha milioni 7 hadi 8 kwa mwaka huku silaha chache zikiharibiwa jambo ambalo linapelekea kuongezeka kwa idadi ya raia wanaomiliki silaha haramu na sambamba na kuzagaa kwa silaha hizo. Aliwataka mawaziri hao kutafuta ufumbuzi wa kudumu na kuweka mikakati itakayowezesha kufichua na kuving'oa vikundi vya watu vinavyoendesha biashara haramu ya silaha ndogo ndogo bila ya kujali hadhi na nafasi walizonazo katika jamii. "Watu watakaobainika kufanya biashara haramu ya silaha washughulikiwe bila ya kuonewa huruma ikiwa ni pamoja na kufikishwa Mahakamani ili haki siyo tu itendeke lakini pia ionekane," alisema Samia. Alisisitiza umuhimu wa kuingiza wanawake katika harakati za kupambana na tatizo la silaha haramu kwa kuwa wanawake ndiyo wanaoathirika zaidi na migogoro ya kivita na wana uwezo mkubwa wa kuleta amani katika nchi zao. Mkutano huo unatarajia kuchagua Mwenyekiti mpya baada ya Tanzania kumaliza muda wake na pia Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo ya RECSA. Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais Dar es salaam 22/4/2016