You are on page 1of 6

Uhuru wa vyombo vya habari nchini

Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Wanadamu wameumbwa kwa hulka na silika ya kuwa na uwezo wa kuwasiliana
miongoni mwao, jamii wanamoishi, taifa na hata ulimwenguni ili waweze kutimiza
nia na azma yao ya kuwasiliana.
Ili mawasiliano hayo yakamilike ni lazima yabebe ujumbe unaokusudiwa
kufikishwa katika jamii.
Ujumbe huo ili uweze kumfikia mlengwa, ni lazima iwepo njia ya kuufikisha
ujumbe huo kwa mlengwa ambao huwasilishwa kwa maandishi (magazeti), sauti
(redio) na picha (TV) pamoja na mitandao ya kijamii kupitia huduma ya inteneti.
Vyombo hivyo vya habari vinahusisha wataalamu ambao kazi yao ni kuhakikisha
jamii inapata ujumbe kwa wakati ili kuweza kujenga, kuboresha na kuimarisha
maisha yao kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.
Vyombo vya habari hakika vimekuwa ndio macho na masikio ya wananchi ili
kufikisha ujumbe unaohusu mambo mbalimbali yanayofanyika ndani na nje ya
nchi.
Tunapoelekea siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari duniani
ambayo huadhimishwa kila mwaka Mei 2 na 3, maadhimisho hayo mwaka huu
yataadhimishwa nchini Finland, ambapo wanahabari wote duniani wataungana
kuwakumbuka wenzao waliofariki dunia walipokuwa wakitekeleza majukumu yao
na kupanga mipango mipya ya namna watakavyoboresha kazi zao ziwe za ufanisi
zaidi.
Tanzania ikiwa miongoni mwa mataifa ya dunia hii, nayo haipo nyuma katika
suala la uwepo wa vyombo vya habari.
Ni dhahiri vyombo vya habari nchini vimekuwa kiungo muhimu katika kisaidia
Serikali kutoa taarifa mbalimbali na ajira hatua ambayo imesaidia kupunguza
tatizo la ajira nchini.

Ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki, Tanzania inayoongoza kwa


kuwa na vyombo vingi vya habari, hali ambayo ni msingi wa kuajiri watu wengi
zaidi katika tasnia hiyo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye ambaye ndiye
mwenye dhamana ya habari nchini anasema Serikali inaunga mkono juhudi
zinazofanywa na vyombo vya habari nchini.
Tulipofika ni pazuri ukilinganisha na tulipotoka, mengi yamefanyika hasa
ukiangalia idadi ya vyombo vya habari nchini na uhuru wa waandishi wa habari
wanavyoanadika na wanavyofikisha ujumbe kwa wasomaji, wasikilizaji na
watazamaji alisema Waziri Nape.
Aidha, Waziri Nape amesema kuwa bado Serikali inakusudia kuboresha mazingira
ya waandishi wa habari ili waweze kufanya kazi zao kwa hali ya uhuru hasa
wanapotimiza majukumu yao ya kiundishi wa habari.
Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambacho
ni chombo kilichoanzishwa kisheria kusimamia sekta za mawasiliano na utangazaji
nchini hadi sasa kuna jumla ya vituo kadhaa vya radio na televisheni
vilivyosajiliwa.
Idadi ya vituo vya redio vilivyosajiliwa nchini hadi sasa ni 123 ambavyo ni sawa
na asilimia 43.4 katika ukanda wa Afrika Mashariki huku miongoni mwa vituo
hivyo vinamilikiwa na makampuni binafsi, taasisi na mashirirka ya dini, jamii na
Serikali ambayo inayomiliki kituo kimoja cha TBC Taifa inayoendeshwa chini ya
Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC), nchini Kenya vipo vituo vya redio 118 sawa
na asilimia 41.7, Uganda 37 sawa na asilimia 13.1, Rwanda vituo vitatu sawa na
asilimia 1.1 wakati Burundi ina vituo vya redio viwili ambavyo ni sawa na asilimia
0.7.
Kwa upande wa vituo vya televisheni, Uganda inaongoza kwa kuwa na vituo vingi
ambavyo idadi yake ni 44 sawa na asilimia 53.6, ikifuatiwa na Tanzania yenye
vituo 24 sawa na asilimia 29.3, Kenya vituo 10 sawa na asilimia 12.2, Rwanda
vituo vitatu ambavyo ni sawa na asilimia 3.7 na Burundi ikiwa na kituo kimoja cha
televisheni ambacho ni sawa na asilimia 1.2

Kwa kuzingatia maslahi ya wananchi na wamiliki wa vyombo vya habari na


wanahabari wenyewe, TCRA imekuwa ikihimiza juu ya ufanisi wa ushindani na
uchumi, kulinda maslahi ya walaji, kulinda uwezo wa fedha na ufanisi wa wagavi.
Pia inahimiza upatikanaji wa huduma zinazosimamiwa kisheria kwa walaji
wakiwemo wenye kipato cha chini na walaji wa vijijini na wa pembezoni, kukuza
mwamko, maarifa na uelewa wa jamii kuhusu sekta zinazosimamiwa ikiwemo
kuzingatia haja ya kulinda na kuhifadhi mazingira, haki na wajibu wa walaji na
wagavi wanaosimamiwa.
Katika kuonesha Tanzania inavyosimamia uhuru wa vyombo vya habari, TCRA ina
jukumu lingine la kusimamia malalamiko na migogoro inayoweza kujitokeza
miongoni mwa wateja wake wakiwemo wamiliki wa vyombo vya habari, wananchi
na kupatia ufumbuzi changamoto hizo.
Aidha, hadi Aprili 22, 2016, Tanzania imekuwa ndio nchi inayoongoza Afrika
Mashariki kwa kuwa na idadi kubwa ya magazeti yaliyosajiliwa ambapo idadi
yake ni 881 licha ya magazeti na majarida mengi kusajiliwa, mengi huchapishwa
mara chache na mengine kutokuchapishwa na kusambazwa baada ya kusajiliwa.
Kwa idadi ya magazeti nchi za Uganda, Rwanda na Burundi yapo magazeti matano
yanayotumika katika nchi hizo wakati Kenya ina magazeti saba ambayo husomwa
na kufikisha ujumbe kwa walengwa katika mataifa hayo.
Wingi huo wa vyombo vya habari nchini imekuwa ishara njema ya kujali uhuru wa
kuanzishwa kwa vyombo vya habari kwa makampuni binafsi, taasisi na mashirika
ya dini pamoja na jamii mbalimbali ili kuweza kuwa ndio namna yao ya kupata
taarifa.
Katika ulimwengu wa leo, uhuru wa habari ni suala la msingi na lina umuhimu
mkubwa katika kutekeleza haki za binadamu katika kutafuta, kupata, kupokea na
kutoa habari ambazo ni muhimu kwa nchi katika kujiletea maendeleo endelevu.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu inawahimiza wanahabari na watu
wote kutambua Kupata Habari ni Uhuru wa Kimsingi: Hii ni haki yako!
ikilinganishwa na kauli mbiu ya mwaka uliyopita ambayo ilisema Achia
uwandishi habari ustawi! Kuelekea upashaji habari bora, usawa wa jinsia na
usalama wa vyombo vya habari katika enzi ya dijitali.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Shirika la Kimataifa
la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Aprili 8, 2016 imebainisha kuwa
katika maadhimisho ya Siku ya vyombo vya habari duniani mwaka huu,
mwandishi wa habari za uchunguzi kutoka Azerbaijan Khadija Ismayilova
amechaguliwa kupokea tuzo ya uandishi wa habari za uchunguzi ijulikanayo
Guillermo Cano inayotolewa na Shirika hilo.
Tuzo hiyo ina thamani ya Dola za Kimarekani 25,000, na imepoewa jina hilo kwa
heshima ya Guillermo Cano Isaza, mwandishi wa habari wa Colombia aliyefariki
Desemba 17, 1986 akiwa kazini.
Jukumu la kuenzi na kutoa tuzo ya heshima kwa waandishi wa habari duniani
linafadhiliwa na taasisi ya Cano Foundation kutoka nchini Colombia na Helsingin
Sanomat Foundation kutoka nchini Finland.
Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano na Habari UNESCO Frank La
Rue anasema "Uhuru wa vyombo vya habari ni muhimu kwa taarifa muhimu na
uwazi ni ambao ni mahitaji ya jamii ya kidemokrasia. Lakini leo tunaona ongezeko
la ghasia na vitisho dhidi ya waandishi ambayo mimi napendekeza nchi zote
duniani kuanzisha utaratibu wa habari na ulinzi kwa ajili ya usalama wa waandishi
wa habari"
Moja ya changamoto za kuweka utaratibu wa usalama wa waandishi wa habari ni
idadi ndogo ya mifano ya taratibu zilizopo ambayo inaweza kuwa somo ili
wengine waweze kujifunza kutokana na taratibu zilizopo.
Masuala muhimu ya kuzingatiwa wakati wa kuanzisha utaratibu huo ni pamoja na
kuwepo kwa makundi matatu ambayo ni wigo wa utaratibu, ushirikishwaji wa
wadau muhimu pamoja na taasisi kubuni na kutathmini hatua ambayo itasaidia
kufikia malengo ya kumlinda mwandishi wa habari.
Akizungumzia maandalizi ya maadhimisho kitaifa ya siku ya Uhuru wa Vyombo
vya habari nchini ambayo yanafanikia jijini Mwanza Mei 2 na 3, mwaka huu,
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho hayo Andrew Marawiti
amesema kuwa yanaendelea vizuri kulingana na ratiba ilivyopangwa.
Katika maadhimisho hayo, Marawiti amesema kuwa Mgeni Rasmi anatarajiwa
kuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Othman Chande ambapo

wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo mada mbalimbali zitawasilishwa na


watoaKuhusu ratiba ya siku mbili za maadhimisho hayo, Marawiti amesema kuwa
zitawasilishwa zikiandamana na majadiliano kwa washiriki wote.
Miongoni mwa washiriki wanaotarajiwa kuwepo katika maadhimisho hayo ni
wadau mbalimbali wa habari wakiwemo viongozi wa Serikali, Mabalozi
wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa,
wamiliki wa vyombo vya habari, waandishi wa habari na wananchi.
Kulingana na takwimu zilizopo, mwandishi wa habari mkongwe nchini, Mzee
Willie Mbunga amesema kuwa Tanzania ina vyombo vingi vya habari
ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo kulikuwa vyombo
vichache vya habari ambavyo ni redio Tanzania Dar es salaam, Tanganyika
Standard, Mambo Leo, Uhuru, Mzalendo na Ngurumo.
Aidha, amesema kuwa changamoto ya baadhi ya watu kujisahau na kuweka
pembeni maadili ya uandishi wa habari ni suala ambalo si la kufumbiwa macho, ni
vema litiliwe maanani ili kukiokoa kizazi cha sasa na kijacho katika kujenga jamii
inayojali na kusimamia maadili ya taaluma na ya jamii.
Katika upashanaji habari, dunia sasa imekuwa sawa na kijiji hasa katika kipindi
hiki cha sayansi na teknolojia ambapo mawasiliano ndio imekuwa nguzo ya kila
kitu.
Awali makala haya yameonesha kuwa ujumbe katika jamiiulifikishwa kwa njia ya
redio, magazeti na TV, zaidi ya vyombo hivyo, mitandao ya kijamii kwa sasa
imekuwa nguzo mahiri na vyanzo vikuu vya habari kwa waandishi wa habari na
wananchi.
Miongoni mwa mitandao hiyo ya kijamii ni pamoja na blog ya Serikali, Michuzi,
fullshangwe, bayana, milardayo, mwamba wa habari, businessmagnetblogs,
mpekuzi, moh Dewji na mitandao mingine.
Mwandishi wa habari Majid Mjengwa ambaye pia ni mwanzilishi na mmiliki wa
blog ya mjengwa anasema Mitandao ya kijamii imekuwa ni eneo la upashanaji
habari linalofanya kazi kama vyombo vingine vya habari.

Ili kufikisha ujumbe kwa jamii, Mjengwa amesema kuwa watu wote wanaofanya
kazi katika mitandao ya kijamii wanapaswa kufuata maadili ya taaluma ya habari
pamoja na sheria na taratibu za nchi husika ili kuondoa mgongano wa maslahi
katika kufikisha ujumbe kwa jamii.
Ni dhahiri haki na wajibu ni vitu ambavyo haviachani, hivyo ni jukumu la kila
mdau wa habari nchini wakiwemo Serikali, waandishi wa habari, wamiliki wa
vyombo vya habari na wananchi kuzingatia sheria, kanuni, taratibu pamoja na
maadili ya jamii.
Hatua hiyo itasaidia kuimarisha na kuhakikisha wadau hao wanakuwa sehemu ya
kujenga uhuru wa vyombo vya habari ambavyo vitakuwa chachu ya kujenga taifa
imara lenye uchumi bora kwa manufaa ya Watanzania ifikapo mwaka 2025.
Mwisho.

You might also like