You are on page 1of 3

1

STATE HOUSE ZANZIBAR


OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar

11.10.2016

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed


Shein amelisisitiza Bunge la Jumuiya ya Afika Mashariki (EALA) kuweka
mikakati imara katika kukuza sekta ya utalii kwa nchi za Jumuiya hiyo kwani
idadi ya watalii wanaoingia kwenye eneo hilo hailingani na vivutio viliopo.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani
Mjini Zanzibar, wakati akizindua Mkutano wa Pili wa Kikao cha Tano cha Bunge la
Tatu la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) unaofanyika Zanzibar.
Amesema kuwa pamoja na kwamba eneo hilo la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
ina vivutio vingi vya utalii, idadi ya watalii wasiozidi milioni 5 wanaoingia katika eneo
hilo kutoka nchi za nje ni ndogo ikilinganishwa na watalii Bilioni moja wanaosafiri kwa
mwaka duniani kote.
Dk. Shein ameongeza kuwa kiasi hicho cha watalii hakilingani na umaarufu pamoja na
vivutio vilivyopo katika eneo hilo la Nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na
kueleza matumaini yake kwamba idadi hiyo inaweza kuongezeka iwapo juhudi za
makusudi zitachukuliwa.
Jumla ya watalii waliotembelea Zanzibar mwaka 2014 walikuwa 311,801 ambapo
lengo letu ni kufikia watalii 500,000 mwaka 2020,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza Miswada inayotarajiwa kujadiliwa katika
kikao cha Bunge hilo ikiwa ni pamoja kuweka Sheria kali zitakazopiga marufuku
biashara haramu ya kusafirisha binaadamu ambayo ni uhalifu na ukiukwaji mkubwa wa
haki za binaadamu.
Akizungumzia kuhusu Mswada wa kudhibiti matumizi ya vifaa vinavyotengenezewa
plastiki ikiwemo mifuko, Dk. Shein alisema kuwa Mswada huo umekuja wakati
muwafaka na kwamba Zanzibar tokea mwaka 2011 imeshaaza kutekeleza kwa vitendo
Sheria ya kupiga marufuku uagiziaji na uzalishaji wa mifuko ya plastiki.

Alisema kuwa uwamuzi wa kupiga marufuku bidhaa hizo Zanzibar ulichukuliwa baada
ya kuona kwamba mifuko hiyo inaharibu mazingira, yakiwemo mazingira ya bahari
pamoja na kuathiri sekta muhimu ya utalii.
Kwa upande wa Mswaada wa Usawa wa Kijinsia na maendeleo, Dk. Shein alisema kuwa
anamatumaini kuwa Mswada huo utatoa njia ya kuinua usawa wa kijinsia na ushiriki wa
wanawake katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Dk. Shein alitoa pongezi kwa uwamuzi wa Bunge hilo kwa kuamua kuifanya Zanzibar
kuwa Makao Makuu ya Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na kueleza kuwa
uamuzi huo ni sahihi kutokana na ukweli kwamba Kiswahili sanifu kinazungumzwa
Zanzibar na kuahidi kutoa kila ushirikiano uanostahiki kufanikisha shughuli za
Kamisheni hiyo.
Ameongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake imechukua
juhudi za makusudi za kukiimarisha Kiswahili kufikia kiwango cha Kimataifa na tayari
imeingizwa kwenye mitaala ya vyuo vikuu kikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha
Zanzibar (SUZA) hadi kufikia kiwango cha Shahada ya Uzamifu.
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuishukuru nchi za Jumuiya hiyo kwa namna
ilivyojali na kushiriki kikamilifu kuwasaidia wananchi wa Tanzania walioathirika
kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, 2016 huko Kagera na kueleza
kuwa hatua hiyo inathibitisha kuwa mashirikiano baina ya nchi wanachama wa
Jumuiya hiyo hayaishii kwenye mikataba laniki imeenda mbali zaidi kwa kujali
ubinaadamu.
Akizungumzia suala zima la changamoto ya ajira ambayo inaikabili nchi zote
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk. Shein alisema kuwa nchi hizo hazina
budi kuondoka zilipo ambapo mchango wa Pato la Taifa katika nchi hizo linakisiwa
kuwa ni asilimia 8.9 ambayo ni kidogo kufikia lengo la asilimia 25 ambayo nchi hizo
zimejiwekea kufikia ifikapo mwaka 2032.
Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina hiostoria ya kuwa ni kitovu kikubwa cha
biashara ambapo ilitumika na wafanyabiashara pamoja na wavumbuzi waliokuwa
wakisafiri katika ukanda wa Afrika Mashariki, hivyo Serikali ya M apinduzi ya
Zanzibar Awamu ya Saba inaamini kwamba inaweza kurejesha hali yake hiyo ya
zamani ambapo hivi sasa imeamua kuimarisha miundombinu ya bandari, viwanja vya
ndege na barabara ili iweze kufikia azima yake hiyo.

3
Kutokana na hatua hiyo, Dk. Shein aliwataka Wajumbe wa Bunge hilo kuwa tayari
kushirikiana na Serikali katika kuifanya Zanzibar kuwa kituo muhimu cha biashara
katika ukanda huo wa Afrika ya Mashariki na Kati.
Dk. Shein ameongeza kuwa maendeleo ya viwanda pekee ndio yatakayowezesha
kuondoa changamoto ya ajira katika eneo hillo.
Nae Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Zubeir Ali Maulid akitoa hutuba
yake alipongeza kwa kufanyika mkutano huo na kueleza kuwa kufanyika mkutano huo
si tu utaimarisha mashirikiano baina ya Mabunge hayo mawili lakini pia, utatoa fursa
zaidi ya pande mbili hizo kujifunza namna ya kuendesha shughili za Bunge kutoka kila
upande.
Mapema Katibu Mkuu wa Bunge la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki Daniel Fred
Kidega alisisitiza suala la amani na utulivu katika eneo la nchi zinazounda Jumuiya
hiyo ili wananchi wake waweze kuendelea na shughuli zao bila ya kuhofia kupoteza
maisha yao.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuisifu Zanzibar na kueleza kuwa kuna uwezekano mkubwa
kuifanya Zanzibar kuwa eneo muhimu la biashara katika ukanda wa Afrika ya
Mashariki na kueleza kuwa inaweza kuwa ni Dubai ya Afrika.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar


Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

You might also like