YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA WAKATI WA UZINDUZI WA TAARIFA YA UCHUNGUZI KUHUSU KUZUIA MATANGAZO YA MOJA KWA MOJA YA SHUGHULI ZA BUNGE. NCHI YETU, BUNGE LETU. JOSAM GARDENS, MWENGE, DAR ES SALAAM 15 NOVEMBA 2016 Ndugu wajumbe wa Bodi ya Baraza la Waandishi wa Habari Tanzania, Ndugu Katibu Mtendaji wa Baraza la Waandishi wa Habari Tanzania, Ndugu waandishi wa habari mliopo, wageni waalikwa, mabibi na mabwana, Aslaam Aleykum, habari za asubuhi.
Napenda kutoa shukrani za dhati kwa niaba ya Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora, na kwa niaba yangu binafsi, kwa mwaliko wenu. Napenda kusema kuwa nimefurahi kushirikishwa katika matukio mawili muhimu katika kazi yenu ya uandishi wa habari, ambayo ni uzinduzi wa Taarifa ya uchunguzi kuhusu zuio la matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge, na pia kuzindua mchakato wa shindano la kutafuta washindi wa Tuzo za waandishi wa habari Mahiri katika maeneo 23, ambayo Baraza na tasnia ya habari kwa ujumla, mmeyaanisha. Madhumuni ya mchakato huu ni kutafuta waandishi wa habari ambao wamejipambanua katika kutoa habari mbalimbali, kupitia vyombo mbalimbali vya habari vilivyopo nchini, yaani kupitia magazeti, runinga, na radio, ama kwa kupitia makala, picha na hata vibonzo katika kufikisha ujumbe kwa jamii. Napenda niseme awali kwamba tasnia ya habari ni kitu muhimu sana katika jamii na nchi yoyote ile, katika kutekeleza majukumu yake. Niseme pia kwamba katika nchi yenye kuamini katika demokrasia, tasnia ya habari ni mojawapo ya nguzo muhimu ya uwepo wa demokrasia ya kweli, kwani huwezesha wananchi kujua kile kinachotokea nchini, na katika jamii wakati wote kupitia uwezo wake wa kuelemisha jamii. Kwa maana hiyo wananchi hupata taarifa nyingi wakiamini kwamba taarifa au habari hizo ni sahihi, na kwamba waandishi wa habari wanafanya kazi yao kwa weledi, na kwa umakini ili kuhakikisha kuwa habari zinazowafikia wananchi zinakuwa zimefanyiwa utafiti, uchunguzi, na uchambuzi wa kutosha. Kwa hiyo ni lazima waandishi wa habari kuwa na vyanzo vya habari vinavyoaminika, na 1
wasitoe habari za uzushi au za kubuni, ili taaluma ya uandishi wa habari
iheshimike. Na huo ndiyo uweledi na umahiri pamoja na kujikita katika maadili ya kazi. Katika misingi muhimu ambayo imetokea kutambulika kama vielelezo vya Utawala Bora ni pamoja na hii ifuatayo, demokrasia, uwajibikaji, uwazi, utawala wa sheria, uheshimu wa mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili ya dola- yaani uhuru wa mahakama, (Judiciary,) uhuru wa Bunge (Parliament,) uhuru wa Mhimili wa Utendaji, yaani serikali (kwa maana ya executive branch,) na uhuru wa vyombo vya habari. Pamoja na misingi hiyo, umuhimu wa mihimili mikuu mitatu ya dola kufanya kazi kwa kujali mipaka ya mhimili mwingine, ndiyo unaojulikana katika dhana ya kikatiba ya utenganifu wa mihimili au heshima baina ya mihimili, (yaani separation of powers.) Katika utendaji wake kila mhimili hufanya kazi kwa kuangalia ukomo wa mipaka yake bila kuathiri utendaji wa mhimili mwingine yaani (checks and balances,) nia ya mfumo huu katika utendaji ni kuhakikisha mhimili mmoja usiwe na nguvu kuliko mhimili mwingine.
Inapotokea kwa mfano mhimili wa serikali (Executive branch) inapovuka
mipaka yake ya sheria na kusababisha uvunjifu wa haki za binadamu basi mhimili wa Mahakama (Judiciary) una uwezo wa kupitia uhalali wa matendo ya serikali au sheria husika na kutolea maamuzi (Judicial Review). Na huu ndio msingi mkubwa wa utawala wa Sheria unaoamini katika kila mtu au taasisi kuwajibika ndani ya sheria (Rule of Law.) Misingi hii ya utawala bora na misingi ya uheshimu wa separation of powers hushabihiana. Ni vigumu kuwa na demokrasia kamilifu iwapo mmoja wapo wa misingi hiyo hautakuwepo. Kama nilivyosema hapo awali katika demokrasia, msingi wowote katika hiyo misingi ikikosekana, lazima kunatokea mapungufu katika mustakabali mzima wa demokrasia. Ingawaje tasnia ya habari si mhimili, lakini imeonekana kuwa ndiyo gundi inayounganisha mihimili hiyo na jamii kwa ujumla, kwa kuwa kila kinachofanyika kwenye mhimili mmoja wapo, na kikabaki ndani bila kutolewa nje kama habari, basi wananchi au jamii haitafahamu kile kinachofanyika huko ndani. Ndiyo sababu katika kila tukio litokeapo, linalohusu habari katika mhimili mmoja wapo, lazima pawepo na wandishi wa habari, wakitumia taaluma yao ili kufikisha ujumbe wa kile kilichotendeka kwa jamii kwa ujumla. Ni kutokana na umuhimu wa tasnia ya habari ndiyo sababu kuna 2
wengine wamediriki hata kuuita mhimili wa nne wa dola au kwa lugha ya
kigeni, the Fourth Estate.
Naamini baada ya kuyasema hayo tutaona ya kwamba, na naamini
tunakubaliana wote kwamba ili tasnia ya habari iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi, upatikanaji wa habari, uenezi wa habari na umuhimu wa kila mtu kupata habari na kuwa na maoni tofauti katika masuala mbalimabli katika jamii, ulitambuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 1948 katika Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu, kuwa uhuru wa habari na maoni ni moja ya haki za msingi za Binadamu, pale Azimio hilo lilipotamka kwenye Ibara ya 19 kwamba kila mtu atakuwa na haki ya kupata habari bila kubughudhiwa, atakuwa na haki ya kujieleza, kutafuta na kupokea habari, kutoa taarifa na habari, bila mipaka, kupitia matamshi, maandishi, machapisho, au kupitia sanaa, au njia yoyote ile ya mawasiliano kwa masharti ya mujibu wa sheria, ili kulinda hadhi na haki ya watu wengine, kulinda usalama wa taifa, amani na afya ya jamii na maadili, kwa ufupi huu ndiyo msingi wa haki ya uhuru wa kujieleza na maoni (Freedom of Expression and Opinion).
Maudhui hayo pia yaliingizwa kwenye Ibara ya 19 ya Mkataba wa Umoja wa
Mataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966. Tanzania ililikubali Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu mara tu tulipopata uhuru, na pia imeridhia mkataba huu wa haki za kiraia na kisiasa, na inawajibika kuutekeleza. Ili kufafanua maudhui ya Ibara ya 19 ya Mkataba wa Haki za Kiraia na Kisiasa kwa undani zaidi, Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (yaani Human Rights Committee) imefafanua mambo kadhaa ambayo ni muhimu kuzingatiwa na kila nchi mwanachama. Katika tamko lake la mwongozo namba 34 kuhusu haki ya uhuru wa kujieleza na maoni, lililotolewa katika kikao chake cha 102 kilichokutana Geneva tarehe 11 hadi 29 Julai 2011, Kamati ilisema kuwa haki hii ni haki ya msingi katika maendeleo ya mwanadamu, na ni msingi muhimu wa jamii iliyo huru na ya kidemokrasia.
Kamati ilisema pia kwamba Uhuru wa kujieleza na maoni ni msingi
muhimu sana katika uwepo wa uwazi na uwajibikaji, ambazo ni nguzo muhimu katika ulinzi na utetezi wa haki za binadamu.
Kamati ilitamka pia kwamba maudhui ya haki hii yanatakiwa kuheshimiwa na
mihimili yote ya nchi mwanachama, na kwamba sheria yoyote itakayoweka kuhusu jinsi ya kutekeleza haki hii lazima iheshimu miongozo inayotolewa na Kamati hii, ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kutafsiri maana ya haki ya uhuru wa kujieleza na maoni.
Tunafahamu pia kwamba haki hii ya kujieleza na maoni imetamkwa pia
katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika Ibara ya 18 kama haki ya msingi inayolindwa kikatiba hapa nchini. Ndugu wajumbe wa Bodi ya Baraza, na wageni waalikwa, napenda niombe kila mwenye nafasi apitie Tamko la mwongozo namba 34 uliyotolewa na Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, kwani muda hauruhusu kupitia kila lililomo. Kamati inachambua mambo mengi yakiwemo nafasi ya vyombo vya habari mbalimbali. Kamati inasema kuwa tasnia ya habari iliyo huru ni nguzo kuu katika demokrasia. (It constitutes one of the cornerstones in a democratic society.) Kamati inatambua wajibu wa vyombo vya habari kupokea taarifa na kuzifikisha kwa wananchi na inasema; ..The free communication of information and ideas about public and political issues between citizens, candidates and elected representatives is essential. This implies a free press and other media able to comment on public issues without censorship or restraint and to inform public opinion. The public also has a corresponding right to receive media output. (msistizo umeongezwa) Kwa ufupi Kamati inasema kuwa vyombo vya habari vinapopata taarifa au habari zinazohusu jamii au masuala ya kisiasa, vina wajibu wa kuzifikisha kwa jamii, na wawakilishi wao. Hii ina maana kwamba vyombo vya habari vilivyo huru vina wajibu wa kutoa maoni yao juu ya masuala yanayohusu umma bila vikwazo vyovyote, na Jamii pia wanahaki ya kuarifiwa taarifa au habari hizo kupitia vyombo vya habari.
Kuhusu masharti yanayoweza kuwekwa na sheria kuhusu uhuru wa kujieleza
na maoni, Kamati inasema kwamba, masharti hayo lazima yatimize vigezo vya ulazima na uuwiano (necessity and proportionality) wa uwepo wa masharti hayo. Kamati inasema, nanukuu; Paragraph 3 may never be invoked as a justification for the muzzling of any advocacy of multi-party democracy, democratic tenets and human rights. Nor, under any circumstances, can an attack on a person, because of the exercise of his or her freedom of opinion or expression, including such forms of attack as arbitrary arrest, torture, threats to life and killing, be compatible with article 19. Journalists are frequently subjected to such threats, intimidation and attacks because of their activities. So too are persons who engage in the gathering and analysis of information on the human rights situation and who publish human rights-related reports, including judges and lawyers. All such attacks should be vigorously investigated in a timely fashion, and the perpetrators prosecuted, and the victims, or, in the case of killings, their representatives, be in receipt of appropriate forms of redress. Kamati inasema kwamba, Ibara ya 19(3) ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, inayotamka uwepo wa masharti kuhusu kulinda hadhi na haki za wengine, maslahi ya usalama wa taifa na jamii, isitumike kwa nia ya kudumaza demokrasia na haki za binadamu, ama kutishia uhuru wa mtu kujieleza, au hata kwa namna yoyote ile, kusababisha mwandishi au mtu mwingine yeyote anapohusika na ukusanyaji au uchambuzi wa habari kupigwa, kuteswa, au hata kuuwawa, mambo ambayo hayaendani na haki inayolindwa chini ya Ibara ya 19. Na ikitokea hivyo basi matukio hayo ya kijinai yapelelezwe na wahusika kuadhibiwa.
Nimeona niliweke jambo hilo bayana kwa kuwa nimeshitushwa niliposoma
kwenye Taarifa ya Uchunguzi inaposema katika ukurasa wa 10, nanukuu: However, there was an aura of disappointment as it was noted that while television is squarely affected by the government ban, it was the print media that was making a lot of noise in protesting against the move. The position of media owners is said to be cautious if anything. Senior editors who also form the leadership of TEF cite reigning fear due to the unpredictability of the regime for the stance of the owners. (Msisitizo umeongezwa.)
Taarifa ya Kuzuiwa kwa Matangazo ya Moja kwa Moja ya Shughuli za Bunge
ni taarifa iliyosheheni uchunguzi unaonyesha faida na hasara za uamuzi huo. Ukiondoa suala la gharama ambalo nalo pia limechambuliwa, na kuonekana kwamba matangazo yangeweza kuendelea kwa kugharamiwa na vyanzo visivyo vya serikali, kimsingi taarifa inaonyesha uzoefu wa nchi mbali mbali, kuwa matangazo hayo ni kitu bora kwa jamii. Taarifa hii inaweza kusaidia viongozi wanaohusika na maamuzi hayo kuona ni jinsi gani uhuru wa maoni ni muhimu kuliko gharama. Kuna usemi usemao kwamba demokrasia siyo kitu rahisi, na ili kuijenga ni budi kuigharamia. Kwa maoni yangu, na ukiangalia haki ya wananchi waliyonayo ndani ya mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu, na ndani ya Katiba ya nchi, haki ya kupata taarifa mbalimbali na kuwa na maoni ni haki ya msingi, kwani inawawezesha wananchi kufikia maamuzi katika masuala muhimu yanayogusa maisha yao ya kila siku. Kwa hiyo napenda niwapongeze Baraza la Habari Tanzania kwa utafiti na uchunguzi mlioufanya mpaka kutengeneza ripoti hii ya Nchi yetu, Bunge Letu. Lakini pia napenda nitoe tahadhari kwamba iwapo tayari kuna taharuki ya uoga katika uandishi wa habari kama ambavyo taarifa ya uchunguzi inavyosema, siamini kama jamii itakuwa inapata taarifa na habari sahihi za matukio mbali mbali yanayotokea nchini. Kwani iwapo waandishi wa habari wataaanza kuandika habari ama kwa woga, ama kwa kutumia self censorship, ni lazima kwamba weledi utapungua, habari zitaandikwa za kumpendeza msomaji na habari za uchunguzi zenye kuibua maovu zitapotea, na hatutakuwa na habari za uchambuzi. Kwa maana hiyo mchakato wa kutafuta wandishi mahiri ili wawanie Tuzo hautafanikiwa, kwani ubora wa taarifa na habari utapotea, na kwa kiwango kikubwa ubora wa tasnia ya habari ambao umekuwa kwa kiwango kikubwa tangu baada ya mfumo wa vyama vingi kuanza utapotea.
Naamini hatutafika huko iwapo tutazingatia misingi ya haki ya uhuru wa
kujieleza na maoni, na pia misingi ya utawala bora. Kwa hiyo basi nichukue fursa hii kuwashukuru tena Baraza la Habari Tanzania kwa kunialika. Niwapongeze kwa kutoa taarifa nzuri ya Uchunguzi wa Uamuzi wa Kusitisha matangazo ya Shughuli za Bunge, Nchi yetu, Bunge Letu, na niwatakie
Mchakato wenye mafanikio katika kuwania Tuzo za Uandishi mahiri,
Excellence in Journalism Award Tanzania (EJAT 2016). Baada ya kusema hayo, napenda kutamka kwamba taarifa ya Uchunguzi, Nchi yetu, Bunge Letu imezinduliwa, na Mchakato wa EJAT 2016 umeanza rasmi.