You are on page 1of 2

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu: 255-22-2114512, 2116898 OFISI YA RAIS,
E-mail: press@ikulu.go.tz IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
Tovuti : www.ikulu.go.tz
11400 DAR ES SALAAM.
Faksi: 255-22-2113425
Tanzania.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli


leo tarehe 15 Mei, 2018 amefanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es
Salaam, na kuagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoza kodi zote
zinazostahili na kuruhusu mafuta ya kula yaliyohifadhiwa katika matanki ya
Kurasini kusambazwa ili kuepusha upungufu wa mafuta ya kula unaoweza
kujitokeza.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo baada ya kupokea ripoti ya timu ya
uchunguzi juu ya uhalisia na ubora wa mafuta ya kula iliyoongozwa na Prof.
Joseph Buchweishaija ambayo imefanya uchunguzi katika matanki 43 yenye tani
105,630 za mafuta ya kula na kubaini kuwa kati ya matanki hayo, 7 yana na
mafuta yaliyoboreshwa (refined oil), 14 yana na mafuta yaliyoboreshwa kiasi
(semi refined oil), 4 yana ni mafuta ya kutengenezea sabuni (Refined Stearin)
na 18 ni mafuta ghafi (crude oil).

Matokeo ya ripoti hiyo yameonesha kuwa, tofauti na taarifa zilizowasilishwa TRA


na kampuni za uagizaji wa mafuta za Vegetable Oil Terminal (VOT), Tanzania
Liquid Storage (TLS) na East Coast Oils and Fats Limited (EC) ambazo
zilionesha sehemu kubwa ya mafuta hayo ni ghafi ambayo hutozwa kodi asilimia
10, imebainika kuwa kuna kiasi kikubwa cha mafuta yasiyo ghafi na ambayo
yanapaswa kutozwa kodi asilimia 25.

Kufuatia matokeo hayo Mhe. Rais Magufuli ameagiza mafuta yote yanayostahili
kutozwa kodi ya asilimia 10 yatozwe hivyo, yanayostahili kutozwa kodi asilimia 25
yatozwe kwa kiwango hicho na wafanyabiashara wote waliofanya udanganyifu
katika nyaraka kwa kuonesha kuwa mafuta yao ni ghafi wakati sio ghafi wapigwe
faini kwa mujibu wa sheria na mafuta yaanze kusambazwa haraka iwezekanavyo.

Mhe. Rais Magufuli amempongeza Prof. Buchweishaija na timu yake kwa


kufanya uchunguzi wa kisayansi katika mafuta hayo, na pia amemtaka Mkemia
Mkuu wa Serikali na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kufanya kazi kwa
1
kuzingatia maadili ili kuondoa mianya ya wafanyabiashara wanaofanya hujuma
dhidi ya uchumi na afya za Watanzania.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara


ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupeleka bungeni mabadiliko ya sheria za
kodi za mafuta ili kuondoa mianya ya ukwepaji wa kodi kwa waagizaji wa mafuta
wanaodai mafuta ni ghafi wakati sio ghafi kwa lengo la kukwepa kulipa kodi halali
za Serikali.

“Nataka niwahakikishie Watanzania wote na ndugu zangu Waislamu


mnaoanza Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, hakutakuwa na upungufu wa
mafuta, na wanaofanya mchezo wa kutishia kuadimika kwa mafuta ili
waachiwe kuingiza mafuta kwa kukwepa kodi hawataweza, nataka
niwahakikishie Serikali ipo makini” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa


hatua ilizochukua kuwadhibiti waliotaka kukwepa kodi ya mafuta hayo na
amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James
kumthibitisha Bw. Ben Usaje Asubisye kuwa Kamishna wa Forodha na Ushuru
wa Bidhaa.

Kabla ya kuondoka bandarini hapo Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Waziri


wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage na Katibu Mkuu
wake Prof. Elisante Ole Gabriel amekutana na wananchi wanaofanya shughuli
mbalimbali nje ya bandari ya Dar es Salaam na kuwaeleza kuwa Serikali
inachukua hatua za kudhibiti na kukabiliana na udanganyifu katika uagizaji wa
mafuta ili kuhakikisha wananchi wanakula mafuta salama, inakusanya kodi stahili
na viwanda vya ndani ambavyo huzalisha ajira na kukuza uchumi wa nchi
vinalindwa.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Mei, 2018

You might also like