You are on page 1of 21

SEMINA YA NENO LA MUNGU ~ UWANJA WA TANGANYIKA PACKERS KAWE - DAR ES SALAAM: Na

MWL. CHRISTOPHER MWAKASEGE.


SOMO: UDHIHIRISHO WA NGUVU ZA MUNGU UNAPOMSHUKURU MUNGU
SIKU YA KWANZA: 3 DISEMBA, 2020

MALENGO YA SOMO
Malengo 3 makubwa ya somo hili ni haya yafuatayo:-
➖Ujue aina mbalimbali za kumshukuru Mungu.
➖Uimarishe imani yako ili unapo mshukuru Mungu udhihirisho wa Nguvu za Mungu uonekane na
uongezeke.
➖Ukue katika imani ya kumjua Mungu zaidi katika Yesu Kristo. (Mungu ni Neno na Yesu ni Neno kwa
hiyo kila Neno limebeba sura ya Mungu na sura ya Yesu. Hivyo kadri unavyolisoma zaidi linakusaidia
kumjua Mungu zaidi katika Yesu Kristo na kwa sababu hiyo imani yako inaongezeka)

Na kwa kujifunza somo hili tutakwenda kujifunza kwa mifano ili iwe rahisi zaidi kulielewa.

MFANO WA KWANZA
KUMSHUKURU MUNGU WAKATI AHADI ALIYOKUPA YA KUKUSAIDIA BADO HUJAIONA IKITOKEA

Soma: 2 Mambo ya Nyakati 20:1-25


Katika mfano huu wa kwanza tutaangalia mambo machache ambayo Mungu anataka tuone.

JAMBO LA KWANZA
1. TATIZO LINAPOKUSUKUMA KUOMBA KWA JUHUDI NA KWA BIDII

Biblia inazungumza juu ya kuomba kwa juhudi,bidii na bila kukoma pia inazungumza misingi tofauti
tofauti ya kuomba.

Ukisoma mstari wa 1-4 katika 2 Mambo ya Nyakati 20, utaona kabisa maombi ya namna hii unayapata tu
pale ukifika mahali hakuna plan B. Ni Mungu kukusaidia na bila hivyo umekwama. Huwezi kuomba kwa
bidii kama hujafika mahali hapo maana kama una Plan B basi huwezi kuwa na msukumo wa kuomba
kwa bidii.

Lazima ujue ya kwamba ukitaka kutoka hapo ulipo ni lazima awe ni Mungu peke yake kakusaidia. Na
kama kuna mtu anaweza kukusaidia basi atatoa upepo kwenye maombi yako. Sio vibaya kupata msaada
kutoka kwa watu maana Mungu anaweza kukunyanyulia watu wengi sana. Lakini hapa tunazungumzia
masuala ambayo watu wengi sana wanaofuatilia somo hili wanapitia.

Yehoshafati kwa jinsi ya kibinadamu angeweza kuitisha jeshi lake na angeweza kuita Wafalme marafiki ili
wamsaidie katika ile vita. Lakini unaona Yehoshafati katikati ya kuzungukwa na majeshi ya maadui
hakuogopa kutafuta nafasi ya kuomba msaada kwa Mungu wake.

Watu wengi sana wanapokumbwa na matatizo makubwa sana huwa wanapoteza utulivu ndani yao na
hawawezi hata kuomba wala kumtafuta Mungu kwanza.
Katika mazingira hayo unakuta mtu anatafuta watu wa kumsaidia na msaada kila mahali anapoweza ili
asaidie. Kutafuta misaada kwa watu si vibaya lakini angalia wenzetu walichofanya cha kumtafuta Mungu
na kutafuta msaada wake kwanza.

Maandiko yanatuonyesha kabisa Yehoshafati pamoja na kuogopa na ile hofu aliyoipata ndani yake
ilimsukuma kwenda kwa Mungu.

Yehoshafati alipoanza kuomba (ukisoma mpaka ule mstari wa 12) unaona kabisa ni mtu ambaye alikuwa
na utulivu. Kwa sababu alipangilia maombi yake vizuri akimkumbusha Mungu safari zote walizofanya na
jinsi ambavyo wale Mungu alisema ni ndugu zao hivyo wasiondolewe.

Ndipo akamwambia Mungu waondolewe kwa sababu ya wanachowafanyia na akamweleza Mungu


mahali walipo na hata akiwaambia wapigane nao hawawezi kwa sababu ya wingi wa jeshi lile la maadui
zao.

Na akasema Mungu akiwauliza kitu watajibu hawajui bali macho yao yanamwangalia Yeye peke yake. Hii
ni sawa na mtu aliyeamua kupambana yeye mwenyewe kwa kila mbinu halafu akikwama anarudi kwa
Bwana na kujieleza namna hiyo.

Yehoshafati alikuwa kiongozi wa kabila la Yuda sasa walipofika Yerusalemu watu wake walifikiri
watapata suluhisho kutoka kwake, ila yeye akawaambia watafute uso wa Bwana. Sasa unapofika mahali
kama hapa unapaswa uombe kwa Bwana na hautakiwi uombe huku umechanganyikiwa au una hofu
(panic). Omba ukiwa na utulivu kutoka kwa Mungu, hata kama utakuwa unalia huku ukiomba haina
shida, bali usiwe umemkasirikia Bwana.

JAMBO LA PILI
2. MAOMBI YALIWAPA JIBU LA AHADI ISIYO NA UDHIHIRISHO WAKATI WANAJIBIWA.

Ukisoma pale mstari wa 13 utaona kuna maelezo ya muhimu pale, sasa tatizo langu linakuja hapa kuwa
kwa nini Mungu asiwajibu pale pale badala ya kusubiri hadi hiyo kesho?
Watu wengi wanapoomba Mungu anawajibu kwa kuwapa maandiko lakini huoni udhihirisho wa hilo
andiko la ahadi. Wengine wameshapokea neno linalosema Mungu atawatetea bila wao kupigana lakini
anawaambia kesho huku majeshi ya maadui yamewazunguka.

Unaweza ukakutana na mstari kwenye Biblia ambao umebeba ahadi na ukatambua kabisa Mungu
anasema nawe lakini unakuta haujadhihirishwa .

Na neno linakuja kuwa “simameni muone wokovu wa BWANA” wakati huo jeshi la adui limewazunguka.
Mstari kama huo unaweza ukausoma na kuuhubiri lakini ni kazi sana kuuweka kwenye matendo.

Haijalishi Mungu anakupa ahadi ya namna gani, kama unajua hujafikia nafasi (kiwango cha imani) kama
ya wenzetu lazima hofu itakuwepo. Kwa wengine ni rahisi sana kutafuta mpango mbadala na wengine
watazimia wakiwa huko ndani kabla adui hajafika.

JAMBO LA TATU
3. SI KILA MTU ANAWEZA KUSEMA MANENO YA KUINUA IMANI YAKO UNAPOTAZAMANA NA TATIZO
AMBALO ULITEGEMEA MUNGU AWE AMELIMALIZA, LAKINI BADO LIPO.
Kwenye mstari wa 20 - 21 utaona maneno ya muhimu hapa kuwa akina Yehoshafati walipopewa ule
ujumbe wa ahadi, ndani ya mioyo yao walipokea lile jibu lao kwa imani kabla hawajaiona.

Marko 11:24
Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni
awasamehe na ninyi makosa yenu.

Biblia inasema ili mpokee lazima muamini kwanza mnapokea. Maana yake tunapokea kwanza ndani ya
mioyo yetu ndipo yanadhihirishwa kwa nje. Kwa hiyo inatakiwa tuyapokee kwanza ndani yetu kwa imani
ndipo yanakuwa yetu.

Kwa maana hiyo tunapokea kwanza ahadi kwa imani ndani ya mioyo yetu kabla Mungu hajayadhirisha
kuwa halisi. Sasa ukirudi kwenye hii habari inaonyesha hawa Watu walipokea kwa imani. Maana
walipokea kabisa na katika habari hiyo utaona vitu vitatu pale kuanzia mstari wa 17-18.

Katika mstari wa "18 Yehoshafati akainama kichwa, kifulifuli; wakaanguka mbele za Bwana Yuda wote na
wakaao Yerusalemu, wakimsujudia Bwana". Maana yake ni kitu ambacho kilitoka moyoni kwao maana
waliamua kumuabudu Mungu wakati wamezungukwa na maadui.

Unapokuwa umezungukwa na tatizo na Mungu anakusemesha na ndani ya moyo wako unajua uaminifu
wa Mungu jinsi ulivyo. Unasema hata kama sijaona uaminifu wa Mungu ulivyo lakini najua ambacho
Mungu umesema ni halisi na hakika. Ndani yako imani ikipokea kuna kitu kinakuwa halisi kwako
ambacho wakati mwingine unakuwa unajiuliza je nina akili yangu sawa sawa maana kwa mazingira
niliyonayo sitakiwi kufanya kitu cha jinsi hii.

Hapa tunaona namna ambavyo Yehoshafati alipopokea ule ujumbe alianguka kufulifuli na kumsujudu
Mungu. Japo alikuwa kazungukwa na maadui .

2 Mambo ya Nyakati 20:19


Na Walawi, wa wana wa Wakohathi na wa wana wa Wakorahi, wakasimama ili wamsifu Bwana, Mungu
wa Israeli, kwa sauti kuu sana.

Sasa fikiria wanafanya hivyo wakati wamezungukwa na maadui. Ni rahisi kusema maadui watasikia na
kuja kutuvamia maana watajua tulipokaa kwa sababu watajua tupo katika ibada na hatujajiandaa kwa
ajili ya vita.

Moyo wako unapopokea kwa imani na kumwangalia Mungu kuwa yeye ni mkuu kuliko kuangalia
matatizo ambayo yamekuzunguka. Moyo ukiisha kubali ndani yako inatoka hali kuu ya kumsifu Mungu
mpaka watu wengine watakushangaa.

Moyo wako ukipokea kwa imani

1.Utaabudu
2.Utasifu

Kusifu hutahitaji kwaya kukusaidia pia hata waimbaji hawatasukumwa kusifu. Maana kutakuwa na
namna fulani ndani yako nzuri ya kumsifu Mungu kwa sababu kajibu maombi yao.
Mstari wa 20 kilitokea kitu cha ajabu kidogo maana unasema "Wakaamka asubuhi na mapema". Huwezi
kuamka kama hukulala hili ina maana walipata amani ya kwenda kulala. Je unawezaje ukalala katika
mazingira ya namna hiyo. Lazima awe ni Mungu peke yake ambaye atakuwa kakupa usingizi katika
mazingira ya namna hiyo.

Katika mazingira hayo kama si Mungu kukusaidia huwezi kulala. Maana inaweza ikafika mpaka asubuhi
hujaweza kupata hata usingizi yaani unageuka huku na huku bila kulala.

Kama ukiona namna hiyo na hauna namna nyingine ya kufanya, unamwambia Mungu kuwa Mungu
mimi sina uwezo wa kutatua hili tatizo maana ni kubwa sana macho yangu yanakutazama wewe tu.

Sasa kwanini unaanza tena kupanga namna ya kutoka wakati umesema unamtegemea Mungu?

Ukiwa katika hali ya namna hiyo endelea kutafakari ahadi ya Bwana ndani yako. Ukiona katika nafsi yako
maswali yanakuja kutoka katika kona moja achilia ahadi kutokea kona nyingine sema nafsi yangu
usisahau kuwa tumeahidiwa na Bwana kuwa vita si vyetu ni vya Bwana na tutaona wokovu wa Bwana.

Upande mwingine wa nafsi yako unaweza ukawa unasema Bwana kaahidi na kusema ni kesho. Lakini
upande mwingine utakuwa unasema nani kasema acha kesho ijisumbukie yenyewe na tunataka leo.
Japo mtabishana sana huko lakini ukiwa na maandiko ya kutosha ndani yako ya kunyamazisha hiyo kona
ya nafsi ambayo inapiga kelele mwishoni itanyamaza tu.

Wafilipi 4:6-7
Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja
zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia
zenu katika Kristo Yesu.

Matokeo ya kwamba umekabidhi jambo mikononi mwa Bwana amani itakuja ndani yako. Amani
inayopita akili na fahamu inakuja kwako.

Japo mwili utapiga kelele lakini moyo utatulia ndani yako na kuambia mwili kuwa nyamaza maana
tumeshapokea. Mawazo yanaweza yakaja kwako lakini endelea kuisemesha nafsi yako na kuikiri ahadi
ya Bwana. Maana utauambia mwili kuwa nisingeweza kupata utulivu wa jinsi hii katika changamoto hizi.

Ukirudi kwenye hiyo habari utaona kuwa walipoamka asubuhi walifikiri hawatayakuta majeshi ila
walishangaa baada ya kuona majeshi yako pale pale.

2 Mambo ya Nyakati 20:20


Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka,
Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini Bwana,
Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.

Baada ya kutiwa moyo, waliabudu, walisujudu na kumsifu Mungu kwa sauti kubwa sana. Maana
walipata amani mpaka shetani aliwashangaa sana maana waliweza kulala katikati ya maadui kwa sababu
Mungu aliwaambia kesho wataona wokovu wake.
Kulipokucha asubuhi waliona wale askari yaani maadui zao wanawatazama kwa hiyo uwe na uhakika
kuwa mioyo yao iliinama tena. Ndio maana Yehoshafati alisema mwaminini Mungu ina maana imani yao
iliyumba. Waaminini manabii wake ina maana walipuuzia ile ahadi ambayo walipewa jana.

Si rahisi kupata watu ambao wanaweza wakakutia moyo katika mazingira ya namna hiyo. Pia ukisoma
habari za Ayubu utaona kuwa mambo yalipokuwa mazito kuna watu waliacha imani zao ziyumbe.

Mke wa Ayubu alipoona uvumilivu umemshinda alimwambia Ayubu amtukane Mungu. Maana sasa
kama yeye ndio anataka kufanya hivyo si angemtukana yeye mwenyewe tu!. Kwanini anataka na mume
wake naye amtukane Mungu? Yeye alifikiri imani ya Ayubu imeloa kama yake.

Walipokuja marafiki wa Ayubu wakamtazama na walimsemesha maneno magumu sana kiasi ambacho
Ayubu akawaita ni marafiki wataabishaji. Walimsemesha maneno magumu sana ya kumrudisha nyuma
ili asiendelee na Mungu wake na Ayubu alikuwa na kila sababu ya kumuacha na kumdharau Mungu
wake.

Ayubu alijisemea "Bwana alitoa na Bwana ametwaa" ni maneno mazuri sana, Ayubu anatuambia yeye
hajui kilichotokea lakini anachojua yuko mikononi mwa Mungu na ameruhusu kama hajaruhusu basi
kuna mahali kakosea lakini kwa vyovyote vile hamuoni Shetani kama msababishaji.

Shetani anakasirika sana usipompa utukufu, na Mungu hakumuonyesha sababu ya yeye kuwa katika hali
ile. Na ndio maana kuna vitu vingine Mungu hawezi kukuruhusu uone maana vitamaliza imani yako
kabisa.

Unaweza ukawa unapita kwenye kipindi kigumu sana unamwambia Mungu uombeje alafu unasikia
moyoni "shukuru kwa kila jambo" kinaweza kuwa kigumu sana kukitekeleza. Unaweza kujifanya wa
kiroho sana ukaanza kushukuru na Mungu anajua tu unaiga unashukuru mdomoni lakini moyoni hamna
shukrani.

USHUHUDA
Katika uzazi tulionao nyumbani mwetu, tulipoteza mimba moja. Wakati ule nilikuwa naenda Canada
kihuduma na nilijua kilichokuwa kinatokea nikaomba sana lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote.

Lakini nikiwaombea wengine wenye shida ya namna hiyo na Mungu anawavusha ila mimi sikuvuka.

Baadae nikampigia simu mke wangu kumuuliza anaendeleaje, akaniambia mimba imeharibika. Sasa
fikiria kesho yake nilikuwa naanza semina ya kuhubiri kuwa Mungu anajibu maombi. Nilimuuliza mke
wangu kama yeye ana amani akaniambia anayo, akaniuliza kama nina amani nikamwambia wazi "sina".
Akaniuliza sasa ndio nafanyaje, nikamjibu kweli sijui.

Yule mwenyeji wangu aliponitazama akajua kuna habari mbaya nikamueleza, akaniuliza sasa ndio
nafanyaje? Nikamjibu pia sijui. Nikaingia chumbani, nikamuuliza Mungu sasa ndio naombaje?
Akaniambia nishukuru kwa kila jambo, nikamjibu Mungu siwezi. Sikuwa na sababu ya kuficha kwa
sababu Mungu ananijua vizuri labda anisaidie tu nashukuruje.

Na ndipo aliponisemesha maneno magumu sana, la kwanza akasema 1. Yeye ni Mungu na atabaki kuwa
Mungu hata kama hajajibu ninavyotaka. La pili akasema 2. Mimi na yeye tumetoka mbali sana kwa hiyo
hili lisitugombanishe. Nikamwambia Mungu kama anataka nimshukuru anisaidie. Nikapiga magoti na
nguvu za Mungu zikanishukia na moyo wangu ukaanza kububujikwa kwa shukrani.

Lakini ukijuliza unashukuruje maana kwa jinsi ya kawaida ulichokuwa unaomba huna. Hawa watu
wamemsifu Mungu na wakalala waliweka imani yao kwenye matendo wanaamka asubuhi Tatizo bado
lipo. Ndio maana walipewa neno la kuwatia moyo.

JAMBO LA NNE
5.KUMSHUKURU MUNGU UNAPOSIKIA MOYONI KUMSHUKURU ILI AGEUZE JIBU LA AHADI LIWE JIBU
HALISI

2 Mambo ya Nyakati. 20:21-22


"Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia BWANA, na kumsifu
katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni BWANA; kwa maana fadhili
zake ni za milele. Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni,
na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa."

Walipokuwa wanaendelea kusogea wakiimba na kusifu na ili kuonyesha kwamba imani yao imerudi
wakatanguliza waimbaji mbele ya askari wakawekwa nyuma kwa sababu walikuwa wanajiandaa
kupigana Mungu akawaambia vita si yao na wataangalia tu wokovu wa Bwana.

Sasa kitu kinachonifikirisha zaidi ni huu msitari wa 22 unaosema "Nao walipoanza kuimba na kusifu,.."
ndipo udhihirisho wa Bwana ukaja. Kwanini Mungu alisubiri waimbe na kusifu ndio adhirishe nguvu
zake? Kwa sababu walipoamka asubuhi imani yao ilifika mahali ambapo haiwezi kusukuma upako wa
Mungu uingie kazini kwa ajili ya kudhihirisha neno ambalo Mungu kaweka.

Ukisoma Biblia utajua kuwa kinachovutia muujiza wako ni imani yako. Ukisoma miujiza mingi ambayo
aliifanya Yesu alipokuwa akitembea hapa Duniani alikuwa anasema imani yako imekuponya, imekuokoa.
Nguvu zilikuwa zinatoka ndani yake lakini alikuwa anasema imani ndio imevuta upako mahali ulipo.

Imani huja kwa kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo. Neno lile ambalo umepewa yaani ahadi na
ukianza kuliweka katika matendo kama mtu yule aliyepokea ndipo unaona matokeo.

Hawa watu katika mistari tuliyosoma tunaona kuwa jana yake waliimba na kumsifu Mungu sana. Lakini
ule muda wa udhihirisho ulikuwa bado ambao Mungu aliwaambia maana alisema kesho.

Lakini imani yao ilikuwa imelala tena. Sasa kama Mungu anakuambia unasafiri kesho na unajaza gari
yako mafuta tayari kwa ajili ya safari. Lakini kuna kitu ambacho kinatokea asubuhi unaona matairi ya gari
yako hayana upepo na oil iko chini. Katika mazingira hayo Mungu akisema anza safari huwezi kuanza
safari kwasababu imani uliyokuwa nayo jana ya safari leo hauna tena na huwezi chukua safari. Mpaka
hapo utengeneze gari lako ndipo imani yako iweze kukaa sawa sawa.

Katika habari hii tunaona tena Yehoshafati akisema mwaminini Mungu na mtathibitika. Hii ni kwa
sababu waliacha tena kumwamini Mungu. Pia alisema waaminini manabii wake nanyi mtafanikiwa. Lile
neno la ahadi lilotoka pale lilikuwa la kwao lakini asubuhi walipoamka waliacha kumwamini Mungu na
lile neno ambalo walipewa.
Mungu alikuwa anawasubiri na Yehoshafati alianza kuwashauri wenzie kuwa tusiharibu hapa Mungu
alisema kesho na ndio imefika sasa.

Katika mazingira haya tuliyonayo basi tuanze tena kuamsha ile imani tuliyokuwa nayo jana.

Ukisoma unaona jana yake walimsifu Mungu na wakalala. Lakini asubuhi imani ilipata shida. Lakini
walipoanza kuimba tena waliimba kutoka moyoni na imani yao ikajengeka kwa upya maana ilikuwa
imetoka moyoni mwao kabisa. Kwa hiyo waakachilia imani ndani yao ambapo walipoanza kuimba
Mungu akaweza waviziao. Maana tunaona walipokuwa wanaendelea kuomba walishangaa kuona Watu
wameuana wao kwa wao bila wao kurusha mkuki hata mmoja. Pia Biblia inasema walikaa pale siku tatu
wakichukua nyara ambazo zilikuwa pale.

Kuna kushukuru kwa imani ambako kunaachilia nguvu za Mungu zidhihirishe ahadi ambayo umepewa
lakini bado hujaiona katika maisha yako. Mungu anasubiri hatua yako ya kutoka moyoni ili umshukuru ili
aweze kuachilia nguvu zake.

JAMBO LA TANO
5.TATHIMINI MAOMBI YOTE AMBAYO UMEKUWA UKIYAOMBA TANGU MWAKA UANZE

Jitathimini wewe mwenyewe ndani yako kama Mungu alishakujibu. Wengine wanaandika mistari hiyo
na wengine wanakumbuka kabisa kuwa Mungu alinisemesha mstari huu. Mungu alipokusemesha mistari
hiyo kuna mambo mawili yalitokea. Kama Mungu alikusemesha na anataka moyo wako upokee maana
yake unakuta mzigo wa kuomba ulikatika na ukaingia mzigo wa kumuabudu na kumsifu Mungu. Kwa
hiyo ukapata amani ipitayo fahamu zote japo mazingira hayajabadilika lakini ndani yako una amani
ambayo unashindwa hata kuieleza.

Japo unataka kuliombea hilo jambo lakini ndani yako kunaingia kushukuru. Ukifika mahali pa namna hiyo
basi ujue kabisa kuwa Mungu kajibu katika ulimwengu wa roho. Kwa hiyo endelea kushukuru kwa imani
na Mungu ataachilia udhihirisho ndani yako.

Ukiona ndani yako umeacha kuomba na umepoteza kumuabudu Mungu na kumsifu Mungu ulikokuwa
nako na amani imeanza kupotea ndani yako. Sasa kama lile jambo likija tena unashindwa kuomba na
kumshukuru Mungu ndani yako basi ujue kuwa umezira na umeumia ndani yako. Rudi kwa Bwana
akusaidie ili atengeneze tairi ambalo limepata pancha. Maana huwezi endelea na safari wakati upepo
unatoka.

Leo nataka tuombe hapa ungana nasi katika kusikiliza Somo la Leo YouTube na sogeza mbele ile sehemu
ya maombi. Sikiliza hapo na Mungu akubariki sana.

Tuonane tena katika siku ya pili ya somo hili zuri.

SEMINA YA NENO LA MUNGU ~ UWANJA WA TANGANYIKA PACKERS KAWE - DAR ES SALAAM: MWL.
CHRISTOPHER MWAKASEGE.
SOMO: UDHIHIRISHO WA NGUVU ZA MUNGU UNAPOMSHUKURU MUNGU
SIKU YA PILI: 4 DISEMBA, 2020

MALENGO YA SOMO
Malengo 3 makubwa ya somo hili ni haya yafuatayo:-
➖ Ujue aina mbalimbali za kumshukuru Mungu.
➖ Uimarishe imani yako ili unapomshukuru Mungu udhihirisho wa Nguvu za Mungu uonekane na
uongezeke
➖ Ukue katika imani ya kumjua Mungu zaidi katika Yesu Kristo.
Leo nataka tujifunze kwa kuangalia mfano wa pili

MFANO WA PILI
2. KUMSHUKURU MUNGU KWA ALIYOKUTENDEA MSIMU ULIOPITA KUNAKOMFANYA AKUSAIDIE
KWENYE MSIMU MPYA

Neno la kusimamia ni kutoka katika kitabu kile cha Kutoka 18:8-12


Kwa kuangalia mfano huu wa pili nataka tuangalie mambo kadhaa pia ili uweze kuelewa na kupata kile
Mungu alichokusudia.

JAMBO LA KWANZA
1. ULIMWENGU MZIMA (MATAIFA YOTE) UPO MWANZONI MWA MSIMU MPYA
2.
Mataifa yote ulimwenguni tupo kwenye msimu mpya lakini mwanzoni. Na katika msimu mpya kuna
mabadiliko makubwa sana ambayo yapo na yanakuja. Na kati ya eneo mojawapo ambalo litaguswa kwa
ajili ya mabadiliko ni mifumo (systems).
Na ninachosikia kukueleza leo ni kwamba mojawapo ya Mifumo ambayo itabadilika ni pamoja na:-
1. **Upimaji wa utendaji kazi**.
2. **Mifumo ya kimaamuzi inayodai mgawanyo wa kimaamuzi (nani aamue nini)**
3. **Mifumo ya ajira hasa kwenye vigezo vya kuajiri**
Na haya mabadiliko pamoja na mengine mengi yatagusa mioyo ya watu, akili zao, miili yao, muda wao
na mazingira wanayoishi wakubwa kwa wadogo, viongozi pamoja na wale wanaoogozwa Na kila Taifa
litaguzwa kivyake kivyake

JAMBO LA PILI
2. UMEINGIA MSIMU MPYA UKIWA NA HALI GANI UKILINGANISHA NA HALI ULIYOKUWA NAYO MSIMU
ULIOPITA

Tumesoma yale mazungumzo katika kitabu cha Kutoka 18 kati ya Musa na Mkwewe kuhani mkuu wa
Midiani, mzee Yethro.

Tuangalie kwanza Kutoka 19:1 pia linganisha na ile Kutoka 12:1-2 Katika Kutoka 19 Biblia inasema ni
mwezi wa tatu. Hapa Kutoka 12 unaona kuwa Mungu alisema mtaanza kuhesabu miezi upya maana
yake ulikuwa ni msimu mpya kwao.

Sasa angalia Kutoka 12:41-42 Mungu aliwatangazia pia kuwa sasa wanaingia katika msimu mpya na
mfumo wa kalenda zao nao unaenda kubadilika. Mungu alifuta ile miaka ya ile kalenda iliyokuwepo
ambayo walikuwa wanaitumia.

Kutoka 19 unaona kuwa ilikuwa imepita miezi mitatu. Sasa wana wa Israel sijajua kama walijua maana
yake nini hayo mabadiliko mpaka pale ambapo waliona wanaanza kujikusanya kwa ajili ya kuondoka.
Walitamani sana kuona mazingira yao yanabadilika wakiwa Misri maana hawakua na mpango wa
kwenda Kanaani.
Katika ile sura ya 15 ghafla walianza kuona mabadiliko makubwa sana. Kitu cha kwanza walikutana na
kukosa maji maana walisafiri siku 3 bila maji kwa hiyo walikuwa na kiu. Lakini walipokuta maji yalikuwa
machungu. Katika hali hiyo walianza kumnung'unikia Musa na Mungu.

Katika sura ya 17 walifika Refudimu. Napo hapo hawakukuta maji, wakapata msaada na wakapata maji.
Katika hali hiyo napo waliendelea kulalamika na kunung'unika. Baada ya hapo walikutana na Waamaleki
wakapigania vita na wakashinda.

Katika sura ya 18 tunaona mzee Yethro akienda kumsalimia Musa na akiwapeleka binti yake na wanawe
wawili. Musa alimsimulia Baba mkwe wake matendo makuu ambayo Mungu aliyafanya kwa Farao na
namna ambavyo aliwatoa Misri. Pia alimwambia namna ambavyo Mungu aliwasaidia katika safari
walipokuwa njiani.

Mzee Yethro alisema na ahimidiwe Bwana Mungu wa Israel. Mungu alimsukuma kusindikiza Shukrani
zake na sadaka. Ilikuwa ni busara sana wamshukuru Mungu kwa sababu ya alichowafanyia jana, mioyo
yao ingefunguka na kujua kama aliwasaidia na pale, angewasaidia na hapo pia. Lakini kwa sababu ndani
yao walikuwa wanalinganisha na hali ya sasa kiasi ambacho wanaona kama vile hakukuwa na sababu ya
kuja pale.

Angalia ndani ya moyo wako je unamuona nani zaidi? Unaona mazingira unayopitia au unamuona
Mungu alie pamoja nawe katika hayo mazingira? Kipi unakisikia zaidi kati ya sauti inayotoka kwenye
hayo mazingira magumu au unasikia sauti ya neno ulilopewa kupita nalo kwenye hayo mazingira
magumu, kipi kina sauti ndani yako kwa sababu ndicho kitakachoamua hatua zako mbele yako.

JAMBO LA TATU
3. MUNGU ALITUMIA MAZINGIRA YA MWANZO YA MSIMU MPYA KUJIJULISHA ZAIDI KWA WANA
WA ISRAELI

Mungu alijitambulisha kwa Musa kama Mungu wa baba zake, Wa Ibrahim, Isaka na Yakobo, Musa
akauliza atakapoenda kule na wakamuuliza ametumwa na nani asemeje, Mungu akamwambia yeye ni
Mungu Niko ambae niko.

Kwa hiyo Musa alikuwa sahihi kabisa kumuuliza Mungu yeye anaitwa nani?. Na tangu wakati ule Mungu
alikuwa anatumia mazingira yote na kupita jangwani kujijulisha kwao yeye ni nani waendelee kumjua
zaidi kabla hawajafika Kanaani, kwa sababu Mbele yako kuna mafanikio lakini usipomjua Mungu katika
shida hautamjua kwenye mafanikio.

Walipovuka tu bahari ya Shamu, walipoanza tu kutembea hakukuwa na maji na waliyoyapata yalikuwa


machungu, lakini Mungu akajifunua kwao kama Mungu mponyaji akayatibu yale maji, yaani Jehova
Raphar, wao walikuwa wanafurahia muujiza wa maji lakini Mungu alifurahia kwa sababu amepata fursa
ya kujitambulisha kwao lakini hawakumtambua walitambua maji kama vile watu wengi wanafurahia
muujiza hawataki kumtambua Mungu aliyewaletea muujiza.

Kwenye msimu mpya watu wanajawa na kiu ya kutoka kwenye shida bila kujali nani anawatoa kwenye
shida, wana wa Israeli kwenye sura ya 15 walikuwa na shida na maji bila kujali nani anawaletea maji, na
Mungu alitaka kutumia hiyo shida ili wajue yupo Mungu ni Mungu mponyaji, ili watakapokuwa
wanaenda huko watakapopata shida yoyote wajue yupo Mungu Jehovah Rapha katikati yao, imani
isitindike, lakini wao walifurahia maji. Ndio maana walipopata tena hiyo shida ya maji kwenye sura ya 17
walilalamika kwa sababu wameshasahau.

Kwenye sura ya 16 katika mazingira ya kukosa chakula Mungu alijifunua kwao kama Adonai yaani Mungu
Mkuu, alijifunua kama Elohim, Yehova-yire (God is my provider) ili wapate kujua kuwa yule Mungu
aliyemsaidia Ibrahimu kwa ajili ya kupata sadaka, Mungu alimpatia kondoo, ndiye atakayewapatia
chakula.

Sasa kwa sababu walichelewa kumjua Mungu, walichelewa kufika Kanaani na kuna wengine hawakufika
kabisa. Hii si kwa sababu Mungu aliacha kufanya miujiza, ni kwamba hawakudaka kile Mungu alikuwa
anawafundisha mwanzoni.

Mazingira magumu ni fursa kwa Mungu kujijulisha kuwa Yeye ni nani. Hata kama hayo mazingira ni
magumu kiasi gani, Mungu hujijulisha hapo. Kwenye mazingira unayopitia usijaribu kumtafuta shetani
au mtu kwa sababu utamwona kwa haraka, bali umtafute Mungu.

JAMBO LA NNE
4. SHUKRANI YA YETHRO ILIYOAMBATANA NA SADAKA ILIFUNGULIA HEKIMA YA MUNGU KWA AJILI YA
MSIMU UJAO

Ukisoma kuanzia Kutoka 18:13 utaona baada ya sadaka kutolewa, asubuhi iliyofuatia Musa aliendelea
kutoa huduma (atoe hukumu, ajibu maswali ya watu, asome sheria, n.k kwa watu wanaomzunguka)
akiwa peke yake na ilikaa foleni ndefu.

Mzee Yethro akapita pale akamwuliza Musa, unafanya nini hapa, na Musa akamweleza anachokifanya.
Na majibu ya Mzee Yethro yapo kwenye Kutoka 18:17

Kitu kilichotokea ni kwamba mabadiliko yaliingia kwenye mfumo wa kutathmini kazi. Jambo hilo hilo
Musa alipolifanya huko nyuma lilikuwa bora, zuri na watu walikuwa wanalifuata ila muda hakujua kuwa
msimu mpya umeanza na umekuja na mabadiliko. Mabadiliko yaliyokuja ni namna ya kutathmini
mabadiliko ya utendaji wa kazi.

Kutoka 18:21-22 Ukisoma hapa utaona kuwa kuna ajira mpya ambazo zitakuja maana msimu mpya
unadai mgawanyo wa majukumu kimaamuzi. Kilichosukuma huo mgao ni kupunguza uwezo wa Musa
kuamua kila kitu na likapelekwa kwa wengine katika makundi tofauti tofauti na yakapewa uwezo wa
kuamua. Lakini walibakiza mambo machache ambayo yataamuliwa na Musa.

Katika msimu mpya pia kutawepo na msisitizo wa vigezo vya namna ya kuwapata watu ambao
watakuwa katika hizo nafasi ambavyo hukuvizoea kuviona.

Kutatokea kupanuka kwa huduma na kazi na ndio maana Mungu anakuinulia watu mapema ambao
watakusaidia maana mbele yako kunapanuka.

Mungu aliwaambia wana wa Israel kuwa huu ni msimu mpya kwa hiyo wanatakiwa waondoke kule
Misri. Japo wangeweza kufunga na kuomba kuwa Mungu tunaomba tubadilishie mazingira ya hapa,
wangeweza kukaa pale na wasione baraka za Mungu maana Mungu anataka waende mahali pengine.
Kwa hiyo katika msimu mpya unahitaji kutega sikio kitu ambacho Mungu anakuambia. Kuna watu
watadhoofika akili kwa sababu watakuwa wanafurahia sana kitu ambacho mtumishi anafanya kuliko
kujiendeleza kielimu au kusoma. Haijalishi kuwa ni wahubiri wazuri kiasi gani lakini hawapati wao muda
wa kusoma Biblia na wa kutafuta nguvu za Mungu ili awajaze tena kwa sababu nguvu zimepungua.
Lakini watakuwa wako busy sana kwenye huduma kiasi ambacho hawatajua ni wakati gani nguvu za
Mungu zimeisha ndani, au neno la Mungu walilokuwa nalo limetumika tayari na hawajaona kitu kipya
ambacho Mungu anataka waone.

Kuna watu wanajivunia kufanya kazi bila kupumzika na hiyo sio kwamba uko kiroho. Kupumzika ni kiroho
maana maandiko yanatuambia kuwa Yesu aliwaita wanafunzi wake pembeni ili waweze kupumzika
kidogo maana hata chakula walikuwa hawajala. Maana walipoenda mahali pengine walikuta makutano
wanawasubiri.

Mstari wa 23 Kutoka 18 anasema Kwamba utafanya jambo hili, na Mungu akikuagiza hivyo, basi utaweza
kusimama wewe, na watu hawa wote nao watakwenda mahali pao kwa amani. Maana yake kutatokea
kukosa amani kwa sababu ya uzito wa ile kazi kiasi cha kuona hajui tena kitu cha kufanya. Hii ni kwa
sababu hajui kilichotokea katika msimu mpya au Mungu kamsemesha kitu cha kufanya na yeye hayupo
tayari kwenda mbele za Mungu kutafuta msaada. Lakini hataweza kusimama na kuendelea na hilo
jukumu wenyewe.

Kuna watu ambao wataacha huduma au kazi wenyewe maana mzigo utakuwa mzito na ndani yao
watakuwa hawana amani, maana Biblia inasema amani ya Kristo na iamue ndani yenu. Itafuteni amani
na muifuate. Mtatoka kwa furaha na mtaongozwa kwa amani. Amani ipitayo fahamu zote itakusaidia.
Kukosa amani ni ishara ya kwamba huendi sawa sawa na Mungu anavyotaka.

Kukosa amani kukizidi nyumbani kwako kutaambukiza mtaani. Hii ni Dunia jaribu kutafuta watu ambao
wamekosa amani nyumbani, ofisini utawakuta wako mtaani. Kwa hiyo lazima liwepo neno la Bwana
maana Yesu ni Mfalme wa amani ambalo litawasaidia watu katika mazingira ya kukosa amani na Yesu
ataleta amani, furaha na tumaini ndani yako.

Kwa sababu tunaona tofauti hulazimiki kuona jangwa ukiwa jangwani. Unaweza ukaona Kaanani ukiwa
jangwani maana Jangwani ni mahali pa kuangalia Kaanani. Musa alionyeshwa Kaanani akiwa mwishoni
mwa jangwani katika mlima Nebo.

Kuna kitu Mungu kapanga kwa ajili yako kizuri lakini kitaamuliwa hapo unapitaje mwanzoni mwa msimu
mpya. Je moyo uko tayari kushukuru?. Kama huwezi kushukuru hapo mahali ulipo basi shukuru kwa kile
ambacho kilifanyika jana na juzi. Kama leo umekosa maji lakini juzi Mungu alikupa maji. Jifunze
kushukuru kwa hilo na mshukuru Mungu kwa ajili ya msimu uliopita.

Tuombe, ungana nasi kuomba katika maombi haya kwa kutazama YouTube. Sogeza kule mwishoni na
utasikiliza maombi haya. Pia endelea kusikiliza na kusikiliza semina hii katika link pale juu.

Mungu akubariki sana

SEMINA YA NENO LA MUNGU ~ UWANJA WA TANGANYIKA PACKERS KAWE - DAR ES SALAAM: MWL.
CHRISTOPHER MWAKASEGE.
SOMO: UDHIHIRISHO WA NGUVU ZA MUNGU UNAPOMSHUKURU MUNGU
SIKU YA TATU: 5 DISEMBA, 2020
MALENGO YA SOMO
Malengo 3 makubwa ya somo hili ni haya yafuatayo:-
➖ Ujue aina mbalimbali za kumshukuru Mungu.
➖ Uimarishe imani yako ili unapomshukuru Mungu udhihirisho wa Nguvu za Mungu uonekane na
uongezeke
➖ Ukue katika imani ya kumjua Mungu zaidi katika Yesu Kristo.

Jana tuliangalia mfano wa pili na leo nataka tuendelee.

MFANO WA PILI
2. KUMSHUKURU MUNGU KWA ALIYOKUTENDEA MSIMU ULIOPITA KUNAKOMFANYA AKUSAIDIE
KWENYE MSIMU MPYA

Tulisoma Kitabu cha Kutoka 18:8-12 Kutoka 18 imeanza kuelezea habari za Mzee Yethro baba mkwe wa
Musa ambaye ni Kuhani wa wa Midian. Alipokuwa anarudi nyumbani kwa Musa baada ya kukaa nao
mbali kidogo.

Baada ya hapo unaona yule mzee akisindikiza shukrani yake kwa kutoa sadaka.

Pia tulitazama jambo la nne

JAMBO LA NNE
4. SHUKRANI YA YETHRO ILIYOAMBATANA NA SADAKA ILIFUNGULIA HEKIMA YA MUNGU KWA AJILI YA
MSIMU UJAO

Ile hekima ambayo Mungu alimpa Yethro iligawanyika kwenye vipengele kadhaa.

Ukirudi sasa katika ile habari ya kutoka 18 unaona asubuhi yake Musa aliwapanga watu foleni kama
kawaida yake. Maana huoni akipiga mbiu ya kuwa watu waanze kwenda. Lakini tunaona tu asubuhi
yake watu wakijipanga foleni.

Biblia inatuambia kubwa Mzee Yethro alimwambia Musa kwa kufanya vile atadhoofika, atashindwa
kusimama, atakosa amani, hatakuwa na nafasi ya kutosha.

Kwa hiyo akipata watu wa kumsaidia wataenda ule mzigo ambao msimu uliopita ulikuwa mwepesi
kwake ghafla msimu mpya umekuwa mzito. Na Mungu ameweka kwa maksudi kabisa ili kupata nafasi ya
watu wengine kuja.

Kwa lugha nyingine hili jambo lilikuwa linalazimisha kupanua wigo wa imani ya Musa iongezeke.

KUNA MAENEO MATATU AMBAYO IMANI YA MUSA ILITAKIWA IONGEZEKE

Eneo la kwanza
➖Kumwamini Mungu anaweza kumpa watu sahihi.
Eneo la pili
➖Kuweza kuwaamini watu wengine kuwa wanaweza kutumiwa na Mungu kama wewe

Hiyo ni changamoto ngumu sana kwa watu wengi. lazima ujue namna ya kwenda mbele za Mungu kwa
maombi ili aweze kukupa watu.

Luka 6:12
Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu.

Tunaona Yesu alikesha usiku kucha akiomba Mungu apate wanafunzi. Na baada ya kutoka mlimani Yesu
aliwaita wanafunzi wake wengi na akachagua kumi na mbili ambao aliwaita mitume.

Kwa hiyo pia ni lazima ujifunze kuwaamini watu wengine kuwa Mungu anaweza kuwatumia. Kama vile
Musa alivyoambiwa achague watu wa kumsaidia maana Mungu anaweza kuwatumia na wao.

JAMBO LA TANO
5. ANAYEMSHUKURU MUNGU KWA AJILI YA ALICHOFANYA KWA MSIMU ULIOPITA, NDIYE ANAYEPEWA
HEKIMA YA KUKABILIANA NA KUFANIKIWA KATIKA MSIMU MPYA

Swali linakuja:
Kama Mungu alijua Musa anahitaji hekima hiyo kwa nini alimpa Yethro? Wakati Musa ndio kaitwa na
amepewa upako wa kazi hiyo.

Sasa kwa nini Mungu hakumwambia Musa hilo jambo moja kwa moja?

Yethro alipewa kwa sababu NDIYE ALIYEONA UMUHIMU WA KUMSHUKURU MUNGU KWA IMANI KWA
AJILI YA KITU KILICHOFANYIKA MSIMU ULIOPITA.

SWALI: Kwanini Yethro alisukumwa kuambatanisha ile shukrani na sadaka?,

JIBU, Kilichomsukuma Yethro kuunganisha shukrani yake na sadaka ni ile imani iliyokuwa ndani yake

Biblia inasema Imani ni kuwa na hakika ya mambo uyatarajiayo na imani isipokuwa na matendo imekufa,
Imani ndio inayokusukuma kuchukua hatua.

VITU VILIVYO TENGENEZA IMANI NDANI YA YETHRO AU VILINIFANYA NIONE IMANI NDANI YA YETHRO
AMBAVYO WATU WENGI HUWA HAWANA WANAPOTOA SADAKA.

1. YETHRO ALIMPA MUNGU WA MUSA NAFASI YA KWANZA MOYONI MWAKE KULIKO MIUNGU
MINGINE

Kutoka. 18:11
"Sasa najua ya kuwa BWANA ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa
unyeti.".

Anasema, "Sasa najua ya kuwa BWANA ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo
walilowatenda kwa unyeti." Huyu mzee aliichukua nafasi ya mungu wake ndani ya moyo wake akampa
Mungu wa Musa.
Kujua maana yake kuwa na uhakika, uhakika maana yake kuwa na imani.

Na kwa imani twafahamu.

Ukisoma Zaburi 50:23 Atoaye dhabihu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye
mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.. Maana yake anayetoa sadaka za Shukrani kwa
Mungu ndiye anayefanya Mungu ajulikane.

Kwa hiyo kule kutoa kwake sadaka ina maana kuna imani ambayo ilitumika ndani yake.

JAMBO LA PILI.
2.MUDA WA KWENDA KUTAFUTA SADAKA YA KUILETA ILIYO SAHIHI.

Hili utalijua kuwa kati ya mstari wa 11 na 12 Biblia ilinyamaza.

Kutoka. 18:11-12
Sasa najua ya kuwa BWANA ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa
unyeti.Yethro mkwewe Musa akamletea Mungu sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; na Haruni akaja, na
wazee wote wa Israeli, wale chakula pamoja na mkwewe Musa mbele za Mungu

Swali linakuja, hii sadaka mzee Yethro alimletea Bwana kutoka wapi? Maana alikuwa amekuja kwa
mkwe wake kumsalimia na alisimuliwa ule ushuhuda akiwa pale kwa Musa. Kwa hiyo hakujiandaa kuwa
na sadaka muda ule.

Aliposikia ule ushuhuda, ulitengeneza imani ndani yake. Baada ya pale alitoa shukrani ya maneno
ambayo ilianza kumsukuma kupeleka sadaka.

MFANO:
Fikiria Mkristo ambaye anasali kanisani na huwa anatoa sadaka zake vizuri tu. Ghafla anaugua au
anataka kupata cheo. Sasa anaamua kuchanganya mambo yaani aende kwa Mchungaji au anataka
kwenda mganga. Na anaenda kwa mganga usiku na wanamwambia aina ya sadaka ambayo wanataka
kwa mfano Beberu mwenyewe kidevu mweupe. Mtu huyo atazunguka katika minada kutafuta huyo
beberu na akipata anampeleka kwa mganga.

Akimpata anampeleka kwa mganga huenda naye yuko mbali kwa hiyo anasafiri masaa manne au
matano. Na watamchinja ili apate kukabiliwa lakini wakati kanisani kachukua tu noti moja tu na
anatumia dakika tano au kumi kufika hapo. Alafu atagemee kupata majibu kwa Mungu? Hapana kule
alikotoa sadaka ya beberu ndipo katoa kwa imani na ndipo atakapoona udhihirisho wa nguvu za mapepo
kumsaidia.

Musa hakujua kama ni msimu mpya kwake.Baada ya kuvuka bahari ya shamu watu wake walikuwa
wanamng'unikia tu juu yake na mpaka aliweza kupoteza kibali kwa watu kabisa.

Hata Ndugu zake yaani Haruni na Miriam waliuliza kama alisikia vizuri katika habari za kuoa kwake.
Kwani mwanzo alipooa hawakuona mpaka walipovuka bahari ya shamu ndipo wanaanza kupata walakini
katika kuoa kwake?.
Mungu akubariki sana na endelea kumshukuru Mungu kwa ajili ya somo hili

SEMINA YA NENO LA MUNGU ~ UWANJA WA TANGANYIKA PACKERS KAWE - DAR ES SALAAM: MWL.
CHRISTOPHER MWAKASEGE.
SOMO: UDHIHIRISHO WA NGUVU ZA MUNGU UNAPOMSHUKURU MUNGU
SIKU YA NNE: 6 DISEMBA, 2020

MALENGO YA SOMO
Bwana Yesu asifiwe, Katika kumalizia somo hili, tathmini kama malengo haya matatu yamefikiwa.
Endelea kuliweka katika matendo somo hili ili uendelee kupata kitu cha kukusaidia.

Malengo 3 makubwa ya somo hili ni haya yafuatayo:-


➖ Ujue aina mbalimbali za kumshukuru Mungu.
➖ Uimarishe imani yako ili unapomshukuru Mungu udhihirisho wa Nguvu za Mungu uonekane na
uongezeke
➖ Ukue katika imani ya kumjua Mungu zaidi katika Yesu Kristo

MFANO WA TATU.
3.KUMSHUKURU MUNGU KWA VICHACHE ALIVYOKUPA INGAWA HAJAKUPA KWA KIWANGO
ULICHOOMBA AU ULICHOTARAJIA

Soma Luka 17:11-19


Katika mfano huu wa tatu nataka tutazame mambo matatu katika eneo la kumshukuru Mungu kwa
vichache ambavyo amekupa..

JAMBO LA KWANZA
1. SI KILA WAKATI MUNGU ATAKUPA CHOTE ULICHOMUOMBA KWA WAKATI MMOJA ULE ULE.

Inawezekana kabisa saa ambayo Mungu anakutembelea akakuponya kwa asilimia 10% na 90% zikabaki.
Na wakati mwingine uponyaji ukaongezeka na kufika asilimia 50%. Lakini wewe ulitaka upate yote 100%
wakati huo huo. Hivyo ndivyo mtu yeyote anayeomba anataka apewe majibu yake.

Kuna kipofu Yesu alimgusa mara moja akaona miti kama inatembea na akamgusa tena mara ya pili na
akaona wazi wazi. Lakini kuna Kipofu mwingine Yesu alimgusa mara moja tu na akapata kuona.

Kwa hiyo ni rahisi sana Yesu akatatua shida ya mtu kwa mara ya kwanza, mtu mmoja akipewa 50% na
mwingine akapata 100% siku ile ile. Huyu aliyepata 50% ni rahisi kuuliza hali ya kiroho ya Yesu kuwa siku
ile ilikuwaje yeye aombe na ampe 50% wakati mwingine alipewa zote 100%.

Je umewahi kufikiria ukiomba Mungu laki 1 lakini akakupa 10,000. Alafu mwingine anasimama
kushuhudia kuwa nilimuomba Mungu Laki moja na akanipa laki mbili. Sasa utajaribu kufikiria kuwa je
ni Mungu yule yule ambaye mimi nilimuomba au?.

Kwa mfano fikiria mtu anaomba kwa Mungu apate kazi ambayo atakuwa anapata mshahara mkubwa.
Lakini anapata kazi ambayo inamlipa mshahara mdogo. Ndani yake anaendelea na mawindo ya kazi
nyingine.
Katika mazingira hayo ni watu wachache sana ambao watakuwa na hali ya kumshukuru Mungu kwa
hicho kidogo walichonacho. Lakini wengine wataendelea kuomba ili wapate kazi nyingine na kusema
Mungu umesema tuombe bila kuchoka. Na wachache sana ambao watakuwa na moyo wa kushukuru
kwa hicho kidogo waliochopata.

Kuna watoto wengine ambao tunawalea wanaweza wasijue umuhimu wa kumshukuru Mungu kwa hali
ambazo wanazo na neema ya Mungu ambayo ametupa.

Usipowafundisha wanaweza wakashindwa kumshukuru Mungu hata kwa ngazi ambayo wamekutana
nayo ya maisha wanapokuja Duniani.

USHUHUDA.
Wakati fulani tulipita katika mkoa mmoja hapa nchini na wakati huo mjukuu wetu alikuwa ni mdogo.
Aliona wanafunzi wakienda shule asubuhi wakiwa wamevaa kandambili (Ndala).

Akachungulia nje ya kioo cha gari akawaona akatuuliza. Ivi wale watoto hawana baba zao? Tukamuuliza
kwa ajili ya nini akasema wanaendaje shule kwa mguu. Yeye alikuwa anapelekwa shule na gari. Kwa hiyo
haelewi kuwa kuna wengine wanaenda shule kwa miguu.

Wakati tunafikiria tunamjibuje akatuuliza swali lingine akasema kwanini hawana viatu. Wanaendaje
shule wakiwa wamevaa Ndala za kwendea bafuni. Yeye alikuwa haelewi kwanini wale watoto wanaenda
shule wakiwa wamevaa Ndala. Maana mazoea kuona Ndala tunaendea bafuni ila wengine wanaenda
shule.

Ilibidi tuseme nae katika ule.umri mdogo aweze kuelewa neema ya Mungu ili ajue namna ya
kumshukuru Mungu. Wakati mwingine tunakuwa na mafundisho ndani ya kanisa kubwa ukiisha okoka
unatakiwa utoke hapa chini na uende hapa juu.

Mungu hakutuumba ili tupande lift, tukipanda lifti hatutengenezi msuli! Lazima tupande ngazi. Tunatoka
imani kwenda imani, utukufu kwenda utukufu, nguvu juu ya nguvu, neno juu ya neno, amri juu ya amri,
kanuni juu ya kanuni ili njiani tuwe tunatengeneza msuli.

Saa Mungu amekusogeza hatua utamshukuru kwa hiyo hatua moja.

Biblia inasema hatua za mwenye haki zinaongozwa na Bwana inamaanisha anategemea ukanyage hatua.

Wakolosai 3:15
Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa
shukrani.

Ukiona amani ya kristo ipitayo akili zote, amani ya Mungu iko ndani ya moyo wako basi jua kubwa
Mungu anategemea uwe na moyo wa shukurani. Inawezekana huna chakula cha kutosha lakini kama
una amani moyoni mwako wewe ni mtu ambaye unatakiwa kwenda mbele za Mungu kwa shukrani.
Haijalishi chakula ni kidogo kiasi gani kuna wengine wanalala hawajala.

Mara kwa mara tunapokuwa mezani na watoto wangu wakija kutusalimia maana sasa kila mtu anaishi
kwake. Mara nyingi tunajaribu kuzungumza nao maisha tuliyoishi huko nyuma ili wasije wakafikiri
tuliteremka kama uyoga.
Siku moja tulikuwa tunakula mikate mezani tunaweka na siagi juu halafu ikaja picha tulipokuwa wadogo
kwa sababu tulikuwa tunapenda mikate mno na saa nyingine baba au mama alikuwa anakosa hela ya
mkate. Kwa hiyo kama wazazi walikuwa wanafikiria watoto wake wakikosa mkate itakuwaje?. Kwa hiyo
mama alikuwa akata ugali wa jana kwa slices , halafu zinapangwa kama mikate sasa tulikuwa tunapaka
blueband juu yake. Na tunakula kama mkate kabisa ila ni ugali.

Haijalishi maisha uliyonayo kama unakula kiasi kidogo sana ila jua kuwa kuna watu wanalala bila kupata
chakula. Ukiona Mungu amekusudia umepata chakula kidogo na bado una amani, hulalamiki Biblia
inasema uwe mtu wa shukurani.

Kama huna pesa za kutosha lakini unayo amani una kitu kikubwa kwa sababu kuna watu hawana pesa na
hawana amani inakuwa ngumu sana kwa sababu maamuzi yao hayatakuwa sahihi kwa kuwa Biblia
inasema amani ya kristo iamue mioyoni mwenu. Ukikosa pesa na ukakosa amani utakosa utulivu na
unaweza kufanya kitu chochote kile kwa sababu umekosa amani.

Mungu alikusaidia ukafika mahali huna pesa za kutosha lakini ukafika mahali Mungu anakupa amani
yake ujue katikati ya kukosa pesa Bwana yuko pamoja na wewe. Huwezi kufanya maamuzi ambayo
hajakaa sawa. Kama biashara yako haiko sawa. Kama huna pesa ya kutosha na una amani moyoni,
umshukuru Bwana hicho ndio kitu kikubwa.

Kuna watu hawana pesa, hawana amani; wana hali ngumu sana kwa sababu maamuzi yao hayatakuwa
sahihi.

USHUHUDA
Nikiwa mkoa mmoja tulikuwa tunajiandaa kwa ajili ya semina, nikapata nafasi ya kuongea na baadhi ya
watu pale mjini wakiwemo wafanyabiashara ili wapate kuokoka kwa sababu wengi walikuwa
hawajaokoka.

Roho Mtakatifu akaniambia nisihubiri hicho, nikamwuliza nihubiri nini akaniambia kichwa somo
"UMUHIMU WA KUNIPOKEA KWENYE BIASHARA ZAO". Nikamwuliza hiyo imeandikwa wapi, akanieleza
jinsi alivyoingia kwenye boti ya Petro. Akasema waambie wamkaribishe kwenye boti zao na sio kwenye
mioyo yao halafu atawapatia samaki na wakishapata samaki watamjua yeye ni nani.

Nikafurahi kwa kupata mahubiri mazuri kabisa na nikachapa injili hiyo na mwishoni nikauliza wanaohitaji
kumkaribisha Yesu kwenye biashara zao wakatoka wengi na nikawaongoza sala ya toba. Na nikawaalika
kuja kwenye semina tuliyoenda kuifanya pale halafu nikaondoka.

Baada ya siku mbili tatu za semina hiyo, wakaja baadhi yao na nilipoita watu kuokoka nikaona na wao
wanatoka. Baadaye mmoja aliniomba kuonana naye kuwa kuna kitu anataka kuniambia.

Huyo mtu akasema hanifahamu na hajawahi kuja kwenye semina zetu. Lakini kilichomsukuma kuja ni
kile kitu alichosikia kutoka kwangu. Aliniambia kuwa kesho yake asubuhi alikuwa amejipanga kwenda
kwa mganga. Nikamwuliza kwa shida gani, akasema ana wiki ya pili hajauza kitu watu wanafika dukani
kwake na wanaondoka bila kununua.
Nikamwuliza kama yeye ni Mkristo akanijibu ndiyo. Nikamwuliza sasa ni kitu gani kinamfanya aende kwa
mganga akajibu kuwa kuna watu walimshauri kuwa ili afanikiwe kwenye biashara lazima aende kwa
mganga wa kienyeji.

Nikamwuliza sasa nini kimetokea? Akasema baada ya kufanya ile sala ya kumkaribisha Yesu kwenye boti
(dukani) sasa kesho yake asubuhi akaona watu wanaingia na kununua bidhaa.

Pia alikuwa haongei na mke wake sasa watu walipoanza kununua ikawafanya waanze kuongea na
wakaanza kujiuliza kulikoni?

Ukiona unapita kwenye hali ya namna hiyo huku una amani moyoni mwako, unatakiwa uwe na moyo wa
shukrani kwa sababu si kila mtu anayepitia hali kama hiyo anakuwa na amani moyoni mwake.

Ndoa yako inaweza isiwe na amani lakini hakikisha moyo wako uwe na amani. Kuna wengine ndoa
zikikosa amani na wao wanakosa amani halafu wanafanya vitu ambayo havijakaa sawa.

Ukienda mbele za Mungu na ukamkabidhi hilo jambo na akakupa amani ipitayo fahamu zote, Biblia
inasema umshukuru Mungu.

Inawezekana una vita kubwa na Mungu hakupi ushindi wa vita hivyo ndani ya muda huo na akakupa
ushindi kwa sehemu ndogo tu na ukawa na uhakika kuwa amekupa ushindi, halafu vita vingine vikiinuka
Mungu anakufungulia ushindi.

Mungu akikushindia vita kwenye sehemu ya kwanza umshukuru kwa kusema “Wewe ni Mungu ambaye
umenisaidia kwenye vita hii na uko pamoja nami, haijalishi vita nyingine itaibuka huko mbele kwa
sababu najua wewe ni Jehova - nisi UTANIPIGANIA TENA.”

JAMBO LA PILI
2. UNAPOPATA KITU KIDOGO KUTOKA KWA MUNGU KULIKO ULICHOOMBA MOYO WAKO UNAKUWA
NA HALI GANI

Luka 17:16 - 17
“akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria. Yesu akajibu, akanena,
Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi?”

Ikimaanisha ndani ya wale 10 kuna Wayahudi .Nilimuuliza Yesu kuhusu hili swali kuwa alijuaje kuwa
wametakaswa 10? Kwa sababu maandiko yanasema walipokuwa wanampigia kelele wakiwa
wamesimama mbali na wala wasingemwona kwa ukaribu kutokana na sheria ya wakati ule. Kila
wakiwaona watu lazima wawatamkie mapema kuwa wao wana ukoma, ni najisi kwa hiyo watu wanakaa
nao mbali.

Sasa ile Yesu kusema “hawakutakaswa 10?” Sasa unaweza ukamuuliza kama aliwaona wapi kwa sababu
walikuwa mbali. Pia walipokuwa wakienda walitakasika ikimaanisha walitakasika baada ya kuondoka
mbele ya Yesu. Walitoka na ukoma sasa alijuaje kama wametakasika wote 10? Na pale hakukuwa na
mtu wa kujibu swali hilo. Sasa kwa nini aliuliza?

Uwe na uhakika alikuwa haulizi swali ambalo mimi nilifikiri kuna swali hapo. Jibu: Alichokuwa anauliza
hali za mioyo yao kwa sababu walipotakaswa ndani ya mioyo yao walitakiwa kuwa na moyo wa shukrani.
Haijalishi ile mioyo ilikuwa inaenda kwa makuhani kwa shukrani (kwenda kupata certificate of clearance)
kwamba wanaruhusiwa kuingia na kukaa na jamii lakini hawakuwa na moyo wa shukrani.

Unapoenda kumshukuru Mungu si kitu kidogo ingawa anaweza kukufanyia kidogo lakini yeye anaangalia
hali ya moyo wako ikoje pale anapokupa kitu; una shukrani kwa kiwango kipi.

Hesabu 11:4-6
"Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia
tena, wakasema, N’nani atakayetupa nyama tule? Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na
yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu; lakini sasa roho zetu zimekauka;
hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu."

Unaelewa maana yake nini mbele za Mungu? Ukisoma ule mstari wa 10 unasema hivi "Basi Musa
akawasikia watu wakilia katika jamaa zao zote, kila mtu mlangoni pa hema yake; na hasira za BWANA
zikawaka sana; Musa naye akakasirika."

Mungu alikasirika sana akawapa pigo, aliwakasirikia kwa sababu Ile sura ya 16 ni msimu mpya uliingia na
Mungu alikuwa anazungumza nao walipokuwa wamekumbuka masufuria ya Misri. Mungu akawaletea
MANA na kware wale. Mungu alisema anawalatea Mana ili awajaribu kama watatii sheria yake au la, na
hapo ndipo alipoanza kuwatengenezae nidhamu ya kuiheshimu siku ya sabato.

Walianza kulalamika kuwa Mana inawakausha kiroho chao na Mungu alikasirika, kwa sababu Mungu
alikuwa anatumia ile mana kufanya kitu kingine bora zaidi na hawakukiona.

Kama Mungu anaweza kumsaidia mtu 100% wewe akakusaidia 20% usikasirike, inawezekana yule kuna
kitu hataona kama utakachoona wewe, hatajua kumvumilia na kutembea na Bwana, kushikwa mkono
hatua kwa hatua yeye anaweza asijue hicho kitu. Wewe unakuwa na ushuhuda wa kutembea na Mungu
hatua kwa hatua.

Wana wa Israeli waliwezaje kuona duni kitu alichowapa Mungu, kwa sababu kama unakiona duni basi
na Mungu unamuona duni na yeye. Haijalishi ni kitu kidogo kiasi gani kama umepewa na Mungu
inamaanisha na Mungu yupo ndani yake, ukikidharau umemdharau Mungu pia, na kwa sababu Mungu
amekupa Mshukuru yeye.

JAMBO LA TATU
3. YESU ALIKUWA NA KITU GANI CHA ZAIDI ATAKE WARUDI KUSHUKURU KWA MZIGO NAMNA ILE

Ukisoma ile Luka 17:18 na wa 19 inasema


"Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu? Akamwambia, Inuka, enenda
zako, imani yako imekuokoa." ukisoma msitari wa 17 kuna anauliza kwa mzigo sana anasema "je
hawakutakaswa wote 10, je 9 wameenda wapi?"

Ukiangalia ule msitari wa 19 unatupa kitu kingine, inasema "Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani
yako imekuokoa.". Nilipokuwa nasoma haya maneno "imani yako imekuokoa" nikaenda kuyatafuta
kwenye miujiza mingine ya Yesu nikakuta yamejrudiarudia nikajua hazungumzii wokovu tulio nao sasa
kwa sababu usingeweza kutokea bila msalaba.
Nikaanza kutafuta kwenye Biblia za kiingereza, niliipenda sana Tafsiri ya Amplified Bible wao yale
maneno "Imani yako imekuokoa" wameandika wanasema "Your Faith has restored you to health"
maana yake Imani yako imekurudishia tena afya yako.

Biblia inasema alirudishiwa maana yake kuna kitu kiliondolewa katika katika maisha yake na ule
ugonjwa lakini sasa kimerudi tena. Kwa hiyo waliokuwa wakienda ule ukoma uliisha lakini walibaki
hawana vidole. Lakini yule mmoja aliporudi kushukuru Yesu aliona imani yake imeongezeka ndani ya
yule mtu.

Hii ni sababu ambayo Daudi anasema anatafakari shuhuda za Bwana kitandani kwake. Ili akiamka
asubuhi awe na kitu ndani yake. Shuhuda ni neno lililowekwa kwenye matendo. Na kwasababu hiyo lina
kazi ya kukuwekea imani ndani yako

Kwa hiyo ile imani iliyotoka ndani yako kuna kitu cha zaidi imekuongezea na kukurudishia vile vitu
ulivyopoteza. Kwa hiyo vikatokea tena vidole ambavyo vilipotea.

Pia akamwambia unarudishiwa afya yako. Maana yake wale walipona tu lakini huyu alirudishiwa na afya
yake. Kuna tofauti kati ya uponyaji na afya. Uponyaji Mungu anashughulika na ugonjwa tu lakini afya
Mungu anashughulika na mfumo wako wa kuishi.

Afya ni mfumo wa maisha. Yaani Yesu alimfanya yule aliyeugua ukoma asirudi tena kwenye maisha
yaliyomfanya augue ukoma. Wale wengine wakifurahia uponyaji lakini wataenda kuishi maisha yale yale
ambayo yaliwaletea ugonjwa. Kwa hiyo yanaweza wakatae tena ugonjwa.

Lakini yule alirudishiwa mfumo wa kuishi ambao unatunza afya yake. Yote haya aliyapata alipoenda
kushukuru kwa ajili ya uponyaji kidogo aliopata akapata cha zaidi ambacho hakutegemea.

Fikiria kesho yake wanakutana na wale ambao walikuwa wakoma.Maana waliachana bila kuagana. Alafu
wale 9 wanamtazama mwenzao sura yake iko tofauti maana sasa ana afya.Ukiwa na afya unakuwa
tofauti hata sura yako inaonesha.

Sasa baada ya kukutana wote pamoja na yule mwenzao aliyeenda kumshukuru Yesu. Wanaona
mwenzao ana afya nzuri na ana vidole vyake tena. Lakini wao hawana vidole, wanaweza wakakimbia, ila
baada ya kupata ujasiri wanaweza kuuliza mwenzao kuwa sasa wewe hivi vidole umepata wapi?.

Yule mtu aliyeshukuru atasema nilirudi tena kwa Yesu na nilianguka miguuni pake kumshukuru.
Akaniambia enenda zako amani yako imani imekuokoa. Basi nikaona vidole vyangu vimerudi. Wale
wengine watasema mbona tulikuwa tunapiga kelele wote pale kusema wewe mwana wa Daudi
uturehemu. Yaani wewe katika kushukuru tu ndio umepata hivi?

Walisahau kuwa baada ya kumwomba Yesu pale aliwajibu kwa asilimia 50%. 50% ya ule uponyaji wao
ulibaki kwenye shukrani.

Ghafla wale 9 waliobaki ndipo wanaona umuhimu wa kushukuru. Sijajua kama wale watu walikuwa na
uhuru kama tulionao sasa wa kama unataka kwenda kwa Mungu unaenda katika roho na kweli. Sio
kama wakati ule ulikuwa lazima uende Yerusalemu au katika mlima ule. Maana unaweza ukamshukuru
Mungu mahali popote ulipo na ukapata kitu kutoka kwa Yesu.
Yule mmoja aliyekwenda kushukuru alipata cha zaidi cha kurudishiwa afya yake baada ya kwenda
kushukuru.

Na mimi niliona hilo, kwa hiyo huwa nawaambia Watanzania tusiache kushukuru kwa mwaka huu 2020.
Kama ulimwomba Mungu vitu 10 na kakupa viwili mshukuru kwa kupata hivyo hivyo viwili. Hata kama
hajakupa kitu mshukuru kwa kuwa kakutegea sikio.

Fanya zoezi la kumshukuru Mungu ili imani yako inyanyuke ndani yako. Ukijifunza utashangaa vitu
ambavyo Mungu atakuongezea. Kama kuna uponyaji wa 100% na Mungu kakupa asilimia 10%.
Mshukuru kwa hizo asilimia 10%. Na uwe na uhakika Mungu atakupa cha asilimia 20%.

Hapa ndio mwisho wa semina yetu na endelea kumshukuru Mungu toka moyoni mwako.

Mungu akubariki sana

You might also like