You are on page 1of 2

UJUMBE WA MKUTANO MKUU WA MWAKA WA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI

TANZANIA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2010

UTANGULIZI
Sisi Maaskofu Wakatoliki Tanzania, tumekuwa katika Mkutano wetu Mkuu wa 63 wa kawaida wa mwaka,
ili kutathmini shughuli zinazofanywa na Idara na Vitengo vyetu mbalimbali, na vile vile kuainisha mipango
ya kutekeleza kazi na shughuli hizo kwa kipindi cha mwaka 2010/2011.

Tulianza mkutano wetu kwa kutafakari juu ya mtazamo ambao tunaamini utaongoza shughuli na kazi zetu
zote kwa kipindi cha mwaka ujao. Wazo hilo ni “Kanisa katika Tanzania na huduma ya upatanisho, Haki na
Amani.” Lengo la tafakari hiyo, ni kubaini ni namna gani Kanisa la Tanzania, katika maana yake ya jumla,
linaweza kutoa mchango katika kuleta Upatanisho, Haki na Amani katika Jamii yetu na kwingineko.

Tumefanya kikao hiki, ikiwa ni takriban miezi mitatu imebaki kufikia uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na
Madiwani utakaofanyika mwezi Oktoba 2010. Tunatambua ukweli kwamba, uchaguzi huru wa Viongozi ni
mojawapo ya vielelezo vya demokrasia, kwa sababu, ndiyo fursa inayowapa wananchi uhuru wa kuonyesha
chaguo lao la kisiasa. Hata hivyo, tunatambua vile vile kwamba, uchaguzi, katika nchi nyingi Barani Afrika,
kimekuwa ndicho chanzo cha vurugu mbalimbali ambazo, mara nyingine huishia katika umwagaji wa damu.
Kwa hiyo basi, sisi, kadiri ya nafasi yetu kama Viongozi wa dini na raia wa nchi yetu ya Tanzania
tunatambua kuwa tuna wajibu na haki ya kusema yafuatayo juu ya uchaguzi ujao:

WAPIGA KURA
Kwanza kabisa, tunawahimiza wale wote waliojiandikisha kupiga kura wajitokeze kwa zoezi la kupiga kura.
Kwa kufanya hivyo watatimiza wajibu na haki yao kama raia wa nchi hii. Katika kupiga kura, tunawaalika
wawe makini. Wawachague viongozi wanaoweza kuwajibika. Wakati wa kampeni, raia wajitahidi kuwahoji
wagombea na wapime udhati wa nia yao kwa kufuata vigezo vya hadhi ya utu wa mwanadamu na tunu za
kimaadili. Kamwe wasimchague mtu kwa sababu ya shinikizo, kwa misingi ya ukabila, dini, rangi, jinsia
wala kwa sababu ya takrima au rushwa. Kwa bahati mbaya, suala la rushwa limekuwa likijitokeza karibu
katika kila uchaguzi. Pengine mbaya zaidi, baadhi ya wananchi wamejenga tabia ya kuendesha maisha yao
kwa kutegemea rushwa wanazopewa na Wanasiasa wakati uchaguzi unapofika na hata baada ya uchaguzi.
Jambo hilo limesababisha baadhi ya Wanasiasa kuendelea kubaki madarakani pamoja na kwamba
walikwisha kupoteza mvuto na ushawishi wa kisiasa na hata uwezo na sifa za uongozi.

Sambamba na hilo, tunalaani hali iliyojitokeza katika chaguzi zilizopita ya baadhi ya wapiga kura kudaiwa
kuuza vitambulisho vyao vya kupigia kura. Juu ya hili, tunawakumbusha kwamba, kuchagua viongozi
wanaowajibika ni wajibu wa wapiga kura wote. Huwezi kuchagua viongozi wanaowajibika endapo utauza
kitambulisho chako cha kupigia kura. Tunawakumbusha kwamba, kuuza kura yako maana yake ni sawa na
kuwachagua viongozi wasiofaa na hivyo kusababisha utawala mbaya, hali kadhalika, kufanya hivyo na ni
usaliti wa uraia mwema. Tena ni kuuza uhuru wako na haki yako ya msingi kama raia.

VYAMA NA WAGOMBEA
Aidha, tunawaalika wagombea wote katika nafasi mbalimbali, waheshimu kanuni za uchaguzi katika hatua
zake mbalimbali. Mara kadhaa imetokea kwamba, kipindi cha kampeni za uchaguzi kutumika na baadhi ya
wagombea kuwachafua wenzao kwa njia mbalimbali. Uzoefu unatuonesha kwamba, katika chaguzi ndogo
zilizofanyika, kulikuwa na vurugu kutokana na maneno ya kashfa na migongano kati ya vyama. Katika hili,
tunaviomba vyama na wagombea wawe na heshima kwa wapinzani wao, washindane katika kunadi sera zao
ambazo zinaweza kuwashawishi wapiga kura na siyo kushindana kwa maneno ya kashfa na matusi ambayo
husababisha uvunjifu wa amani.
Pamoja na hilo, kuna wimbi ambalo limejitokeza mara kadhaa katika chaguzi mbalimbali; baadhi ya vyama
na wagombea kukosa ukomavu wa kisiasa, unyofu na unyenyekevu wa kukubali matokeo hasa ya kushindwa
katika uchaguzi, hata pale ambapo inaonekana kwamba taratibu na kanuni zote za uchaguzi zilifuatwa. Juu
ya hilo, tunahimiza vyama na wagombea watakaokuwa wameshindwa kihalali kukubali matokeo ya
uchaguzi na kuungana na raia wengine katika kuijenga nchi.

Hata hivyo, tunawaalika Wagombea ambao wanadhani kwamba hawakushindwa katika uchaguzi kwa njia ya
haki, watafute haki zao kwa namna inayokubalika kisheria kuliko kuhamasisha vurugu na ghasia ambazo
matokeo yake ni kusababisha uharibifu wa mali na pengine hata kupoteza maisha ya watu bila sababu za
msingi.

Tunapenda pia kuvihimiza vyama kuwa wazi kwa kubainisha sera na itikadi zao mapema. Vyama vyote
vijali na vilenge kujenga demokrasia ya kweli. Pia vilenge kusitawisha uwajibikaji kwa kutonadi sera mbovu
au zisizotekelezeka.

SERIKALI NA VYOMBO VYAKE


Mara nyingi vurugu zinazofanywa na vyama na wagombea mbalimbali ama kukataa matokeo husababishwa
na hisia kwamba kanuni mbalimbali za uchaguzi hazikuheshimiwa, ama kwamba hakukuwa na uwazi katika
uchaguzi. Juu ya hili, tunahimiza Tume ya Uchaguzi ya Taifa ( NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar ( ZEC)
zijijengee imani na heshima kwa wananchi kwa kusimamia uchaguzi kwa kuheshimu Katiba na kanuni za
uchaguzi ili uchaguzi uwe na uonekane kweli kuwa huru, wa haki, wazi na wenye usalama.

Sambamba na hilo, pamoja na ukweli kwamba vyombo vya Dola ni muhimu katika kulinda usalama hasa
wakati wa kipindi cha uchaguzi, mara kadhaa imetokea kwamba, nguvu kupita kiasi zimetumika na vyombo
hivyo kuliko ilivyohitajika. Tunaviomba vyombo vya Dola vitumie nguvu zake kwa mujibu wa taratibu na
sheria za nchi, kwa kuzingatia maadili ya kazi yao pasipo kuegemea upande wowote, ili uchaguzi uwe kweli
huru.

VYOMBO VYA HABARI


Tunatambua kwamba vyombo vya habari ni sehemu muhimu kabisa katika Jamii. Mara nyingi, hasa nyakati
za uchaguzi, vyombo hivi vimekuwa vikitumika kuandika habari ambazo zimekuwa zikiwachanganya watu
na pengine zinazoleta uchochezi na chuki. Tunawaalika wanahabari wote kuwajibika katika kazi yao,
waandike habari za ukweli wakiheshimu kanuni za demokrasia na hivyo kusaidia ili uchaguzi uwe wa amani
na kuwasaidia watu wawachague viongozi bora.

VIONGOZI WA DINI MBALIMBALI


Tukiwa viongozi wa dini, tunawaalika viongozi wenzetu wa dini mbalimbali kutoegemea upande wowote
wala kushika uelekeo wa kikundi fulani. Tuwe sauti ya wasio na sauti, wenye kupima mambo kwa ukomavu,
upeo, haki na kweli, pasipo kuathiri uadilifu wetu.

HITIMISHO
Tunamalizia kwa kuwahakikishia sala zetu kwa ajili ya Nchi yetu hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi ili
uchaguzi uwe kweli huru, wa haki, wazi na wenye usalama kwetu sote, ili tuwapate viongozi ambao
wataliongoza Taifa hili kwa kujali maslahi ya wote na ambao watatusaidia kujenga jamii yenye upendo,
umoja, haki, Amani, na maendeleo ya kweli.

AMANI IWE NANYI NYOTE!

Kurasini, Dar Es Salaam


2 Julai 2010.

You might also like