You are on page 1of 11

HOTUBA YA MHESHIMIWA NOEL AMOS MTAFYA, RAIS WA

SERIKALI YA WANAFUNZI CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM


WAKATI WA KUAGANA NA KULIVUNJA BUNGE LA SERIKALI YA
WANAFUNZI CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM, UKUMBI WA
BUNGE ATB TAREHE 8 MEI 2021

Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa Makamu wa Rais;
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Mheshimiwa Waziri Mkuu;
Mheshimiwa Naibu Spika;
Mheshimiwa Naibu Jaji Mkuu;
Waheshimiwa Mawaziri, Wabunge na Majaji wote,
Wanafunzi, wageni waalikwa, na wafuatiliaji wa siasa za DARUSO

Tunayo kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutujalia
uzima na kutuwezesha kuishuhudia siku hii adhimu katika historia ya Bunge letu na
serikali yetu. Hatimaye siku ya kuvunja Bunge imewadia ili kuwezesha hatua husika
za mchakato wa Uchaguzi ziweze kuteendelea.
Naamini haikuwa rahisi au kwa akili za kibinadamu kumaliza uongozi salama, kwani
wengi walishindwa na hata kuishia njiani, lakini kwa neem ana uweza wa Mungu leo
hii tunahitimisha kwa ushindi na furaha. Sifa na utukufu ni kwa Mungu Muumba
Mbingu na Nchi.

Mheshimiwa Spika;
Nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kulihutubia Bunge lako tukufu ili niweze
kutimiza wajibu wangu wa msingi na wa Kikatiba. Lakini, shukrani zangu kubwa ni
kwa uongozi wako mahiri na shupavu. Umeliongoza Bunge vizuri. Najua haikuwa kazi
rahisi maana penye wengi pana mengi. Lakini kwa uhodari mkubwa umeweza
kulifikisha jahazi bandarini salama salmini. Hakika wewe ni nahodha makini na
jemedari hodari, uliyethibitisha uhodari na umakini wako katika uwanja wa medani.

Mheshimiwa Spika;
Niruhusu pia nitoe shukrani na pongezi zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge
kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya. Mmetimiza ipasavyo wajibu wenu wa Kikatiba
wa kusimamia Serikali. Nawashukuru kwa ushirikiano wenu na msaada wenu. Ni
ukweli ulio wazi kuwa bila ya ninyi Wabunge wetu na Bunge hili, tusingeweza kupata
mafaniko na maendeleo tuliyo yapata. Mmejijengea nyinyi wenyewe na Bunge letu
heshima kubwa ndani na nje ya viunga vya chuo. Mmeitendea haki demokrasia ya
serikali na kuliletea heshima kubwa Bunge letu. Kwani ili serikali yoyote iweze kufanya
vyema inahitaji Bunge imara litakaloweza kuisimamia, kwa maana rahisi ubora wa
Bunge unapimwa kwa kuangalia ubora wa serikali. Hongereni sana Waheshimiwa
Wabunge.
Mheshimiwa Spika;
Tarehe 25 Julai 2020 nilipozindua Bunge hili nilielezea mtazamo wangu kuhusu serikali
yetu na kutaja majukumu ya msingi na vipaumbele vya Serikali hii ya Mwaka
2020/2021. Nilisema tutatekeleza wajibu wetu na vipaumbele hivyo kwa kuitengeneza
DARUSO kuwa na hadhi na heshima Zaidi ya hapo awali yaani “MAKE DARUSO
GREAT AGAIN”. Leo tarehe 08 Mei 2021 wakati wa kuvunja Bunge hili nitaeleza
mafanikio tuliyopata na changamoto zilizotukabili katika kipindi hicho. Kama ilivyo ada,
leo tunafikia mwisho wa uhai wa Bunge letu naomba kutumia fursa hii kutoa mrejesho
wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali na yale mambo ambayo tuliahidi na kupanga
kufanya.
UMOJA, AMANI NA USALAMA
Mheshimiwa Spika;
Niliahidi kuwa katika kipindi cha uongozi wangu nitafanya kila niwezalo kuhakikisha
kuwa DARUSO inaendelea kuwa moja na watu wake wanaendelea kuwa wamoja,
wanaopendana na kushirikiana licha ya tofauti zao za, dini, hali ya kuwa mlemavu,
jinsia, tahasusi au program, makabila, mahali watokako, na ufuasi wa vyama vya
siasa. Pia, kwamba serikali yetu itaendelea kuwa yenye amani, usalama na utulivu na
ushirkiano mzuri baina ya Rais na Makamu wa Rais, Serikali na mihimili mingine ya
serikali..
Leo tunapoagana, ninyi na mimi, ni mashuhuda kuwa licha ya tofauti zetu mbalimbali
tumebakia kuwa wamoja, wenye upendo na ushirikiano wa aina kuwahi kutokea.

Mheshimiwa Spika;
Niruhusuni, nitumie nafasi hii kuwashukuru viongozi wakuu wenzangu, Makamu wa
Rais, Mhe. Happy Itros Sanga, Waziri Mkuu Mhe. Abdlrahman Makere, Jaji Mkuu Mhe.
Asajile Mwakyusa, Spika wa Bunge hili tukufu Mhe. Christopher Titus, Baraza la
Mwazairi, Waheshimiwa Majaji na Washimiwa wabunge wote, viongozi wa taasisi
mbalimbali, viongozi wa vikundi vya dini na wanadaruso wote kwa ushindi tulioupata
katika kudumisha umoja, amani, ushirkiano na upendo baina yetu.

UTAWALA BORA
Mheshimiwa Spika;
Tarehe 25 Julai 2020 nilipozindua na kulifungua rasmi Bunge hili, niliahidi juu ya
dhamira ya serikali yangu katika kuheshimu utawala bora na kuheshimu na kuthamini
mchango wa mihimili mingine ya serikali katika utekelezaji wa majukumu ya serikali.
Katika kipindi cha uongozi wangu tumetekeleza dhamira yetu ya kujenga na
kuimarisha utawala bora kwa kufuata sera, sheria, na mifumo iliyopo. Tumefanya
hivyo katika maeneo yote muhimu yakiwemo yale yahusuyo uendeshaji wa shughuli
mbalimbali za serikali ya wanafunzi, mapambano dhidi ya rushwa, maadili ya viongozi,
ukusanyaji wa mapato, nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na mgawano wa
madaraka kati ya mihimili ya serikali. Na katika hili nipende kutoa pongezi za dhati
kwa wakuu wa mihili yaani Mhe. Spika na Mhe. Jaji Mkuu kwa ushirikiano mkubwa
walioutoa kwa niaba ya mihimili wanayoiongoza kwani bila mchango wao tusingelifika
leo kwa mafanikio haya makubwa. Hakika hongereni sana.

USAWA WA KIJINSIA
Mheshimiwa Spika;
Niliahidi wakati wa kampeni na wakati wa kuzindua Bunge hili, kuwa tutaongeza
ushiriki wa wanawake katika shughuli na nyanja mbalimbali za maisha ya wanafunzi
ikiwemo nafasi za maamuzi. Ninyi na mimi ni mashahidi kwamba tumetimiza ahadi
hiyo kwa mafanikio makubwa. Idadi ya Wabunge wanawake imeongezeka kutoka 32
mwaka 2019/2020 hadi 55 mwaka huu.
Tumeongeza idadi ya wanawake katika ngazi zote kuu za uamuzi. Kwa mfano, tuliteua
wanawake 8 katika Baraza langu Mawaziri,
Lakini pia katika muhimili wa mahakama tulikua na Majaji wanawake 8, na kwa
upekee kabisa nichukue nafasi hii kuipongeza shule kuu ya Biashara UDBS kwa kuwa
na Mwenyekiti na Katibu ambao wote ni wanawake. Aidha nipongeze ndaki, taasisi na
shule kuu nyingine zote ambazo zimeendelea kuzingatia usawa wa kijinsia kama vile
nyumbani kwangu CoSS, na sehemu ningine kama CoET,SOED, UDSOL, CoICT, SJMC.
Ni matamanio yangu kuona siku moja tunapata Rais wa serikali ya Wanafunzi
Mwanamke kama ilivyo sasa katika Taifa letu la Tanzania. Na rasmi nichukue nafasi
kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais katika historia ya Tanzania
tokea uhuru, hii ikiwa ni kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, na kama heshima nawaomba waheshimiwa
wabunge tusimame kwa dakika moja ili kumkumbuka na kuenzi mema aliyoyafanya
kwa nchi yetu hasa katika sekta ya elimu ya juu nchini……….Mungu ailaze roho ya
mpendwa wetu pema peponi.

USHIRIKISHWAJI WA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUMU


Serikali yangu iliamini katika msemo wa kingereza unaosema “Disability is not inability”
hivyo kwa kulitambua hilo serikali yetu iliunda Wizara malumu kwa ajili ya
kushughulikia changamoto za wanafunzi wenye mahitaji maalumu iliyoitwa Wizara ya
Jinsia na Makundi Maalumu, lakini pia serikali ilitenga kiasi cha fedha katika bajeti yake
kwa ajili ya kununua vifaa mbali mbali kwa ajili ya wanafunzi hao.
Lakini pia vikao mbalimbali vilifanyika vilivyo wakutanisha wanafunzi wenye mahitaji
maalumu na Serikali vyenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto za wanafunzi
wenye mahitaji maalumu.
Aidha serikali yetu iliendelea kuwashirikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika
nafasi mbalimbali za uongozi Mfano Niliteua mheshimiwa Baatha Ntoteye ambaye ni
Naibu Ktibu Mkuu wa Umoja wa Wanafunzi wenye mahitaji maalumu kuwa mbunge
na baadae Naibu Waziri wa Jinsia na Makundi maalumu, pia nilimteua mheshimiwa
Rabia Athuman Abdalah ambaye ni Mwenyekiti wa Wanafunzi wenye mahitaji
maalumu kuwa Naibu Waziri wa Michezo na Burudani.
Serikali yetu iliheshimu takwa la katiba kama ibara ya 13 (3) (d) inayotaja na kuwapa
sifa mwenyekiti na katibu wa taasisi ya wanafunzi wenye ulemavu kuwa wabunge,
tofauti kabisa na taasisi nyingine ambapo viongozi wao si wabunge katika Bunge hili
tukufu.
Pia nipende kuwashukuru na kuwapongeza viongozi wa taasisi ya wanafunzi wenye
ulemavu kwa ushirikiano mkubwa waliokua wakiutoa kwa serikali hasa katika
kuwasilisha changamoto za wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa serikali kwa ajili
ya ufumbuzi.

USHIRIKISHWA WA WANAFUNZI WA SHAHADA ZA UZAMILI NA UMAHILI


Mheshimiwa Spika;
Wakati wa kampeni na hata katika hotuba yangu ya kufungua Bunge hili, nilitoa
mwelekeo wa serikali kuwa, serikali hii itatoa nafasi na kuhakikisha ushirikishwaji wa
wanafunzi wa shahada za Umahili na uzamili unaongezeka. Ambapo nilimteua
mwakilishi wa wanafunzi wa shahada za umamili na uzamili katika serikali yangu ili
kuwakilisha wanafunzi hao katika vikao mbalimbali vya maamuzi, lakini pia nilimtea
mwanafunzi wa shahada ya umahili kwenye Balaza langu la mawaziri kama Naibu
Waziri Wizara ya Elimu.
Lakini pia, Serikali yetu ilileta muswada hapa Bungeni ambao ulieleza kuwa katika
nafasi tatu za watendaji katika ngazi ya ndaki, taasisi na shule kuu mmoja kati ya
watendaji watatu awe ni mwanafunzi wa shahada za uzamili na umahili. Na nipende
kuchukua nafasi hii kulishukuru Bunge hili tukufu na waheshimiwa Wabunge wote kwa
kupitisha muswada huu. Hakika asanteni sana.
Aidha napenda kutoa rai kwa serikali ijayo iweze kufanya juhudi Zaidi katika kuongeza
ushiriki wa wanafunzi haw ana umuhimu wao.

SANAA NA MICHEZO
Mheshimiwa Spika;
Niliahidi kusaidia kukuza michezo na sanaa katika Chuo chetu. Kupita Wizara ya
Michezo na Burudani serikali yetu iliendesha shughuli mbalimbali zenye lengo la
kukuza na kuinua sekta ya michezo, Sanaa na burudani. Serikali yetu ilifanikiwa
kuipeleka timu yetu katika mashindano ya Michezo ya Vyuo Vikuu yaliyofanyika kitaifa
Dodoma ambapo chuo chetu kiliibuka kidedea katika mashindano.
Serikali yetu pia iliandaa tamasha kubwa la michezo lililokuwa na lengo la
kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza. Bonanza hilo lilihusisha michezo
mbalimabli pamoja na burudani ya muziki kutoka kwa wasanii kama Ben Pol, Kala
Jeremiah, B2 K na wengine wengi.
Serikali yetu iliandaa michezo mbali mbali ya kirafiki ya ndani na nje kama mchezo
dhidi ya Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Ardhi ikiwa ni sehemu ya kuboresha
mahusiano na vyuo vingine.

MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO NA VYUO, TAASISI NYINGINE


Mheshimiwa Spika;
Katika ilani yangu ya uchaguzi na wakati nalihutubia Bunge hili niliahidi kwamba
Serikali yangu itafanya kila iwezalo kuhakikisha DARUSO inakuwa na uhusiano mzuri
na serikali nyingine za wanafunzi katika vyuo vingine kutoka ndani na nje ya nchi. Leo,
mwaka mmoja baadae napenda kuwahakikishia kuwa ahadi yetu tumeitekeleza, tena
vizuri kuliko tulivyotegemea. DARUSO ni rafiki wa kila serikali za wanafunzi katika vyuo
mbalimbali na kila shirika, taasisi za kifedha nakadhalika. Hadhi yetu katika uso wa
jamii imepanda sana. Tunaheshimiwa, tunasikilizwa, tunathaminiwa na kuaminiwa na
watu, serikali, serikali za vyuo vingine na taasisi mbalimbali.
Katika kipindi hiki tumetembelewa na wageni wengi mashuhuri kutoka vyuo
mbalimbali. Tumeweka historia kwa kutembelewa mfululizo na Marais, Mawaziri
Wakuu na Mawaziri kutoka vyuo mbalimbali. Aidha, tulitembelewa na Meneja wa
kanda ya Dar es salaam na Pwani wa CRDB mazungumzo haya ndio yaliyopelekea
kupata ufadhili wa kiasi cha fedha zilizosaidia kuendesha Bonanza la kuwakaribisha
mwaka wa kwanza.
Tumeshirikishwa katika shughuli nyingi na mikutano mingi. Nimepata fursa ya kushiriki
katika mikutano mbalimbali inayohusu wanafunzi wa elimu ya juu ndani nan je ya nchi
hasa kwa njia ya mtandao hii ikiwa ni kutokana na uwepo wa ugonjwa wa COVID 19..
Nimewahi kushiriki katika mafunzo uongozi yenye jina “Youth Program Leadership and
Governance Conference 2021” iliyoandaliwa na shirika la Shina Inc la nchini Marekani
ambapo serikali yetu ilitunukiwa cheti cha pongezi kama sehemu ya kutambua
mchango Madhubuti iliyoutoa katika mkutano huo, cheti hiki kitakabithiwa kama
kumbukumbu kwa serikali yetu.
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki tumeboresha ushirikiano na matawi yetu yalioko nje au mbali kidogo
ya kampasi ya Mwalimu J.K Nyerere yaani tawi letu la afya Mbeya, na sayansi za bahari
Zanzibar. Hii ikiwa ni sehemu ya kufahamu changamoto za wanafunzi walioko katika
matawi hayo
UCHAGUZI MKUU
Mheshimiwa Spika;
Leo rasmi nitalivunja Bunge hili, ili kuelekea katika mchakato wa uchaguzi ambao
utatuwezesha kupata viongozi watakao tuongoza kwa kipindi kijacho cha mwaka
mmoja kwa mwaka wa masomo 2021/2022.
Napenda kuchukua nafasi hii kuwahimiza vijana wenye sifa kwa mujibu wa Katiba yetu
kugombea nafasi mbali mbali za Uongozi katika serikali ya wanafunzi kwa mwaka huu
wa masomo mwaka 2021/2022.
Mwaka huu tunatamani kuona mwamko mkubwa wa wanawake kugombea nafasi
mbali mbali za uongozi, kwani kwa kipindi kirefu tumekua tukishuhudia ushiriki mdogo
wa wanawake katika kugombea nafasi mbali mbali.
Aidha kama nilivyozungumza awali nafasi ya Rais haikuwekwa kwa ajiri ya wanaume
tuu, bali tunaweza kuwa na Rais mwanamke pia. Ni ndoto yangu kuona DARUSO siku
moja inapata Rais mwanamke kwani uongozi si jinsia bali ni nidhamu na hekima aliyo
nayo mtu wa jinsia yoyote.
Aidha serikali ya wanafunzi haifungamani na chama chochote cha kisiasa, na hii ni
kwa mujibu wa katiba ya DARUSO. Hivyo nitoe rai kwa wanafunzi wote bila kujali
tofauti zozote za kiitikadi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Napenda kuwahakikishia kuwa kila mwanafunzi mwenye sifa ya kugombea au kupiga
kura atapata fursa ya kufanya hivyo kwani ni haki ya msingi ya kikatiba. Shime
wanaDARUSO tuhimize watu wajitokeze kupiga kura ili wasikose haki yao hiyo.
Ni Imani yangu kuwa Tume ya Uchaguzi na Kamati ya Rufaa zilizoundwa leo, zitaenda
kusimamia mchakato huu wa uchaguzi kwa kufuata misingi na taratibu ambazo taasisi
yetu imejiwekea kwa kipindi sasa.

MATAMANIO YETU KWENYE SERIKALI IJAYO


Mheshimiwa Spika, naomba nitumie wasaha huu pia kutoa baadhi ya mapendekezo
ambayo kama yatafanyiwa kazi itaendelea kukuza hadhi na heshima ya DARUSO
ndani nan je ya nchi.
1. Kuzingatia usawa wa kijinsia hasa katika nafasi za uteuzi
2. Kuongeza ushiriki wa wanafunzi wa shahada za uzamili na umahili
3. Ushirikishwaji wa wanafunzi wa kimataifa (international students)
4. Kuendendeleza ushirikiano mzuri baina mihili
5. Changamoto yoyote inayoweza kutokea, majadiriano ya mezani iwe ni njia na
chaguo lenu la kwanza kwani hakuna kinachoshindikana kwa mazungumzo na
ukizingatia menejmenti na Serikali ya Tanzania ni Sikivu sana.

SALAMU ZA KUAGA
Mheshimiwa Spika;
Tulipanga kufanya mengi na tumefanikiwa mengi, lakini hatukuweza kuyamaliza yote
kwa sababu ya changamoto mbalimbali na kubwa zaidi ni uhaba wa rasilimali fedha
na wakati mwingine rasilimali watu, vitendea kazi, baadhi ya viongozi kushindwa kutoa
ushirikiano wa kutosha na urasimu. Hata hivyo tumeweza kutekeleza zaidi ya asilimia
80 ya ahadi zetu zilizomo kwenye Ilani za Uchaguzi na mipango ya Serikali.
Siku moja mama yangu aliniuliza, je, utakapomaliza uongozi wako utapenda Wana
DARUSO wakukumbuke kwa lipi? Nikamjibu, nitapenda Wana DARUSO waseme, “Rais
Mtafya alitukuta kuleee! na sasa anatuacha hapa palipo juu”. Mimi na ninyi ni
mashahidi kuwa tulipo leo ni bora zaidi ya kule tulipokuwa jana.
Changamoto katika taasisi kubwa kama hii haziishi kila siku zinaibuka mpya. Kila
ukimaliza moja inazaa changamoto nyingine. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa watangulizi
wangu, wao walifanya walipoweza. Nami namwachia atayekuja, naye afanye yake na
yatakayobakia atamwachia atakayemfuatia. Jambo linalonipa faraja ni kuwa nami
nimetoa mchango wangu kwa maendeleo ya DARUSO na Chuo chetu kwa ujumla
wake.

SHUKRANI
Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa spika katika kuagana na wabunge katika bunge lako hili tukufu ambalo
mimi pia ni sehemu ya bunge ninayo mengi yakushukuru, ninao wengi wa
kuwashukuru wakwanza ni wana DARUSO wenzangu ambao walinipa fursa hii adhimu
ya kuwatumikia katika nafasi kubwa na ya juu kabisa katika serikali ya wanafunzi na
walionesha Imani na kuniheshimu kwa kunichaguwa kuwa Rais wao, nawashukuru
kwa ushirikiano wao mkubwa kwangu, kwa serikali yangu, na kwa bunge letu tukufu
katika kipindi chetu chote cha uongozi .

Nawashukuru pia kwa kutimiza wajibu wao na haki yao ya msingi kama inavyosema
Katiba ya DARUSO inayowapa haki ya kuchagua viongozi wao, kuendelea na shughuli
za kitaaluma, natambua na kuheshimu mchango wao mkubwa na walivyoniuunga
mkono na kuisaidia na kuendelea kuiamini serikali yangu. Nasema asanteni sana

Mheshimiwa spika

Napenda kuwashukuru viongozi wenzangu wakuu, wakuu wa mihimili. Nitakuwa


mchoyo wa fadhila nisipokushukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mhe.Happy Itros
Sanga kwa msaada wako, ushauri wako na ushirikiano wa karibu ulionipatia katika
kipindi hiki cha uongozi wetu. Nakutakia kila la heri katika maisha yako baada ya mimi
na wewe kumaliza kipindi chetu cha uongozi. Namshukuru Waziri Mkuu Mhe.
Abdulrahman Ayatullah Makere ambae ndie aliyekuwa kiongozi wa shughuli za serikali
bungeni, Nakushukuru kwa ushirikiano wako mkubwa, msaada wako na ushauri wako
wa hekima na busara ambao umewezesha mafanikio tuliyoyapata katika kujenga
serikali yetu na katika kuimarisha DARUSO.
Nawashukuru pia Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi, Makatibu Wakuu
wa wizara, kwa mchango wao katika kufanikisha majukumu ya Awamu yangu.
Mmenisaidia sana. Kwa kweli mafanikio haya tunayozungumza leo yameletwa na
juhudi zenu.
Nawashukuru viongozi wa muhimili wa mahakama chini ya Jaji Mkuu Mhe. Asajile
Mwakyusa na Naibu Jaji Mkuu Mhe. Adam Masawe na Waheshimwa Majaji wote hakika
mchango na ushikiano wenu ni mkubwa sana.
Kipekee nilishukuru Bunge hili chini ya Spika wetu Mhe. Titus Christopher na Naibu
wake Sande Sirori na waheshimiwa Wabunge wote kwani Mchango wenu ni mkubwa
mno hasa katika kuisimamia serikali yetu
Napenda pia kuzishukuru taasisi na vikundi mbali mbali vilivyopo hapa chuoni kwa
kuniunga mkono mimi na Serikali yangu na kwa mchango wenu muhimu. Nawaomba
muendelee kuilea amani ya chuo chetu.
Napenda pia kuishukuru Ofisi ya Mshauri wa wanafunzi chini ya mama yetu Paulina
Mabuga, miongozo, malezi na ushauri wake umechangia sisi kuweza kufika hapa.
Napenda pia kuishukuru menejimenti ya Chuo kwa ushirikiano na usikivu wao hasa
pale tulipowapelekea changamoto zetu.
Nitakua si mwenye busara kutowashukuru watangulizi wangu, napenda kuishukuru
serikali iliyopita kwa kazi kubwa waliyoifanya, nawapongeza sana. Hakika mtukaribishe
huko msoga.
Mwisho lakini sio mwisho wa umuhimu, naishukuru sana familia yangu. Mchango wao
umekua mkubwa sana mpaka mimi kufika hapa leo

HITIMISHO
Mheshimiwa Spika;
Ninapoagana na Bunge letu natambua kuwa baadhi ya Wabunge mnarudi kutetea viti
vyenu au nafasi nyingine mbalimbali nawatakia kila la kheri. Naelewa hofu na mashaka
mliyonayo. Mwenyezi Mungu awape utulivu na subira. Nawatakia mapumziko mema
kwa wale ambao mmeamua kustaafu. Wale wanaogombea Urais, Makamu wa Rais au
nafasi yoyote waliomo humu nawatakia kila la kheri, na nawashukuru kwa kuonyesha
nia ya kunipokea mzigo huu mzito. Nawatakiwa heri katika matamanio yenu.
Kwa ndugu zangu Wana DARUSO wenzangu, nawashukuruni kwa kuniamini na
kunichagua nafasi ya juu katiba katika serikali yetu. Nawashukuru kwa kuniunga
mkono wakati wote wa uongozi wangu. Mmenipa heshima kubwa ambayo sitakaa
nisahau maishani mwangu. Ninamaliza kipindi changu cha uongozi nikiwa nawapenda
sana na nitaendelea kuwapenda mpaka siku Mwenyezi Mungu atakaponiita. Nitawa-
miss kama mtumishi na kiongozi wenu mkuu lakini tutakutana kwa urahisi zaidi nikiwa
raia. Baada ya hotuba yangu ndefu, sasa natangaza kuwa nilimevunja Bunge
hili rasmi, lakini serikali itaendelea kutekeleza majukumu yake mpaka siku viongozi
wapya watakapo apa kwa mujibu wa Katiba.
Mungu ibariki DARUSO, Mungu bariki Chuo Kikuu cha DSM, Mungu bariki
Tanzania.
Asanteni kwa kunisikiliza!

Noel Amos Mtafya,


Rais Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es salaam,
0765773652
noelamos21@gmail.com

You might also like