You are on page 1of 6

RASIMU RISALA YA WATANZANIA WAISHIO UINGEREZA KWA MHESHIMIWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO TANZANIA TAREHE: 30 MACHI 2014 SIKU:

JUMAPILI MAHALI: Sattavis Patidar Centre Forty Avenue, Wembley Park Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Salma Kikwete, Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Balozi, Waheshimiwa wageni wote mlioandamana na ujumbe wa Mheshimiwa Rais, Wageni waalikwa, Mabibi na mabwana, itifaki imezingatiwa. Awali ya yote, Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa fursa hii ya kujumuika nanyi katika kusanyiko hili adhimu. Kwa niaba ya Watanzania waishio Uingereza, tuna furaha kubwa ya kuwakaribisheni tena hapa London. Mheshimiwa Rais , Mbele yako ni baadhi tu ya WaTanzania Walioko Uingereza. Nchi hii kwa takwimu za haraka inakadiriwa kuwa na watanzania zaidi ya laki moja na nusu. Na ingawa kuna mtazamo potofu kwamba Watanzania wote walioko hapa ni wabeba mabox. Mheshimiwa hapa kuna Madaktari, Manesi, Walimu, Wanasheria, Wahasibu, Watawala na kadhalika. Vilevile wapo Wafanyabiashara na Wanafunzi pia. Mheshimiwa Rais, tunaomba kuchukua fursa hii kukupa pole kwa kazi nzito ya utekelezaji wa majukumu mazito uliyonayo. Sote tunafahamu kwamba umekwishalitumikia taifa kwa muda mrefu wa maisha yako na muda si mrefu unamaliza muhula wako wa mwisho wa Urais. Katika kipindi chote hicho tumeshuhudia ujasiri wako, kujituma kwako, hekima yako, upendo wako na
1

misimamo thabiti hata katika vipindi vigumu vyenye changamoto kali. Pamoja na pole hizo, hatuna budi kukushukuru kwa dhati na kukupongeza kwa kazi nzuri unayoifanya. Mheshimiwa Rais, tunaomba pia kutumia nafasi hii kukupongeza wewe binafsi na Taifa letu kwa kutimiza miaka 50 ya uhuru (kwa Tanzania Bara na Zanzibar) na Muungano wetu. Watanzania ndani na nje ya nchi hatuna budi kuwaenzi waasisi wa taifa letu Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Karume, pamoja na wazalendo wote waliojitolea maisha yao kuhakikisha tunaishi katika nchi huru, yenye amani na upendo. Aidha tunakupongeza kwa kuanzisha mjadala wa marekebisho ya Katiba na hatimaye kuzindua Bunge rasmi hivi majuzi. Sisi WaTanzania wa Nje tunakuhakikishia tuko pamoja nanyi nyumbani kwa dua, sala, maombezi na kadhalika ili mchakato huu umalizike salama na kwa faida ya Taifa letu na vizazi vijavyo. Tunaunga Mkono Kauli mbiu uliyoitoa ya Tanzania Kwanza. Mheshimiwa Rais, huku nje tumekuwa tukifuatilia kwa karibu na kupata taarifa nyingi zenye kutia moyo kuhusu maendeleo ya nchi yetu, hasa kiuchumi. Tunajisikia kutembea kifua mbele tunaposoma taarifa kwamba uchumi wetu umekuwa ukikua kwa kasi ya wastani wa asilimia 7. Hongera sana Mheshimiwa. Mheshimiwa Rais, kama ule usemi wa Kiswahili unavyosema Elimu ni Ufunguo wa Maisha, nasi tunaelewa umuhimu wa sekta ya elimu katika kukuza uchumi wa nchi. Kwa mantiki hii, tunapenda kukupongeza wewe binafsi na Serikali yako kwa jitihada za kuimarisha sekta ya Elimu ya Nchi yetu. Umeweza kupanua wigo wa elimu ya juu nchini kwa kujenga au kupanua vyuo vikuu kadhaa. Chuo Kikuu cha Dodoma chenye heshima na hadhi ya kimataifa ni kielelezo tosha cha mafanikio hayo. Ni muhimu pia tukatambua mchango mkubwa wa mifuko ya pensheni, kama vile NSSF chini ya Mkurugenzi wake Dr Dau na taasisi mbalimbali katika kusaidia kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo nchini kama wa ujenzi wa chuo Kikuu hicho, au daraja la kigamboni na mingine mingi. Mheshimiwa Rais, tunatambua sana mchango wako katika kuimarisha usawa wa kijinsia. Katika kipindi cha uongozi wako umetoa fursa za kipekee kwa akina Mama kwa kuwapa nafasi za uongozi mkubwa Serikalini na Taasisi
2

za Umma. Hii inadhihirisha jinsi gani unavyothamini usawa wa kijinsia kwa watu wote bila upendeleo. Aidha Mheshimiwa Rais, tukupongeze kwa jitihada na umahiri wako wa kuitangaza nchi yetu kimataifa na kuiweka Tanzania kwenye dira ya dunia. Umeweza kujenga mahusiano mazuri na Viongozi wakuu wa Mataifa mbali mbali na Makubwa duniani. Tanzania imekuwa rafiki mwema wa wengi kwa sababu ya hekma zako na ucheshi wako binafsi. Katika Nyanja za kimataifa, tunapenda pia kukumbuka mchango wako wa hotuba wakati wa mazishi ya Mzee Nelson Mandela. hatutosahau jinsi ulivyotufariji katika hotuba ile kwa kumuenzi Baba wa Taifa letu Marehemu Mwalimu Nyerere. Pamoja na kutotambuliwa na wengi, ilikuwa dhahiri kwamba mchango wa Mwalimu na Taifa letu katika harakati za kuikomboa Afrika Kusini ulitakiwa kupigiwa tarumbeta katika shughuli ile ya maombolezo. Mheshimiwa Rais, kabla ya kumaliza risala hii tunaomba kwa ufupi tuligusie suala la Uraia wa WaTanzania tulioko nje ya Nchi, na ambalo ndio changamoto yetu kubwa na ya Msingi. Kwanza tunaomba kukushukuru kwa dhati ya mioyo yetu tukizingatia ya kwamba binafsi yako Umekuwa ni mtetezi wetu mkubwa, kwa kujaribu kwa kadri ya uwezo wako kutushirikisha ipasavyo katika maendeleo ya Nchi. Ingawa tunajua kwamba suala hili litajadiliwa katika Bunge maalum huko Dodoma, tunaomba tutoa rai ya kwamba kwetu sisi hatma ya uraia ya wale wote wenye asili na nasaba ya Tanzania, waliochukua uraia katika nchi nyingine bado ni kama ndoto ambayo tunajaribu kuikamata. Labda kwa kuwa suala hili liko jikoni Mheshimiwa, tunaomba kusema tu kwamba, ingawa binafsi yako na baadhi ya Viongozi waandamizi mfano Mheshimiwa Benard Membe mnaelewa na kulipigania hili, watanzania wengi walioko nje ya Tanzania na waliochukua uraia wa nchi nyingine wanasikia unyonge sana kana kwamba Nchi yetu ya asili haituthamini ipasanyo na tunakosa haki zetu za msingi ilihali maisha yetu ya nje siku zote ni ya ugenini. Mheshimiwa, Si kweli kabisa kwamba tuliacha Uraia wetu kwa kutoipenda nchi yetu kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu na makundi. Sisi na vizazi vyetu hatuwezi kukubalika huku nje kama kwetu hata siku moja. Kwa kifupi
3

sisi tunaishi nje ya Tanzania lakini mawazo yetu yote na mioyo yetu iko Tanzania. Hali yetu ya maisha imekuwa kama ule msemo kwamba ahera hatupo na duniani wanatutafuta. Tunaomba kuchukua fursa hii adhimu kuungana na watanzania wenzetu wengine wanaoishi nchi zingine ughaibuni kukueleza kilio, wito na nia yetu ya kupatiwa utambulisho wetu wa asili yetu na haki yetu muhimu kama raia wa Tanzania. Mheshimiwa Rais, watanzania kwa asili ni watu wakarimu na wenye moyo wa uzalendo kwa nchi yetu. Hii inadhihirisha pamoja na changamoto nyingi, watanzania wanaoishi ughaibuni tunawakumbuka na kuwasaidia ndugu na jamii yetu nyumbani. Rai yetu kwako Mheshimiwa, tunaomba utusaidie kulipigia debe suala hili ukiwa kama Mlezi wetu, kwa kupitia Wajumbe wa Bunge la katiba, kama sisi wenyewe tunavyofanya ili waweze kuliangalia na kulipitisha katika nadharia inayofaa na kueleweka. Kwa kufahamu hazina kubwa tuliyonayo ya taaluma mbalimbali, Mheshimiwa Rais, tunaomba pia Serikali yetu isisite kututumia muda wowote ili nasi tuweze kuchangia kwa njia mbadala, mawazo yetu katika kujenga nchi. Miongoni mwetu tunaweza kukuhakikishia kuna waliobobea na wenye ubunifu muhimu kwa taaluma mbalimbali za kuweza kusaidia Taifa letu. Kwa kuzingatia ya kwamba dunia ya sasa ipo katika ushindani wa mafanikio na maboresho ya kiuchumi na kijamii, hivyo dhana ya kujifunza mbinu na mikakati ya kimaendeleo haina budi kushirikisha ubadilishanaji wa elimu, maarifa, uzoefu na ubunifu. Mheshimiwa Rais ikumbukwe pia kwamba Kwetu sisi wakazi wa nje ya nchi, kuna mtihani mkubwa wa kumiliki Ardhi, nyumba na kuwekeza kwa ujumla. Hofu yetu wengi ni kwamba sheria inaweza kutufanya kupoteza mali zetu kwa kukosa haki kiuraia. Mheshimiwa Rais, hata hivyo, tunakushukuru kwa kuanzisha Idara ya Dispora katika Wizara ya Mambo ya Nje. Hatua hii imedhihirisha kutambua kwako mchango wetu katika uchumi wa Nchi. Tunaomba pia kushauri
4

kwamba sasa kuwe na dawati la Diaspora katika kila Balozi zetu kubwa duniani ili kufanikisha Zaidi malengo na kuwa karibu na WaTanzania. Mheshimiwa Rais, tunakushukuru sana kwa kuweka utaratibu wa kuonana na kuongea na WaTanzania kila unapoweza katika safari zako za Nje ya Nchi. Kwa fursa hii basi, ujio wako tunaweza kuutumia kwa kuleta kwako maombi yetu mawili. Kwanza, kwa kufahamu kuwa Tanzania sasa iko katika mkakati wa kuandaa sera ya Diaspora, tunaomba Sera hii iweke wazi juu ya umiliki wa Ardhi na vilevile Biashara. Pili, tunaomba serikali yako itupatie viwanja kwa kutenga sehemu maalum kwa ajili ya WaTanzania walioko nje, kama zilivyofanya nchi nyingine za Afrika kwa mfano Ghana na Sierra Leone. Kuwa na uhakika wa kupata kiwanja halali kutoka serikalini utatusaidia katika kufikia malengo ya uwekezaji nyumbani. Na Serikali yako itakapotutengea sehemu hizi kwa mfano, basi tutapata nguvu ya kuwaapproach makampuni kama NSSF na NHC na vilevile mabenki Makubwa ili kuona nao watatusaidia vipi katika kufikia malengo yetu , na hatimae kuchangia zaidi katika Ukuaji wa Uchumi. Mheshimiwa Rais, mwaka huu mwezi wa June 2014, hapa London tunatarajia kuwa na Mkutano Mkubwa wa Diaspora. Lengo la Mkutano huo ni kuwaunganisha WaTanzania wa UK na Tanzania kwa kuleta huduma za makampuni makubwa, pamoja na taasisi za umma nchini Tanzania hapa Uingereza. Tunategemea muda huo ukifika Bunge la Katiba litakuwa limemaliza kazi yake na labda kutakuwa na uhakika wa muelekeo wa suala la Uraia. Hii itasaidia sana katika kuuza bidhaa kama vile za mabenki na nyumba kwa Watanzania wa UK. Mheshimiwa Rais, tuna imani Ubalozi wetu utakupa taarifa rasmi na ingawa wazungu husema its a long shot kwa kuwa ndio umetoka hapa leo, bado tunakukaribisha kwenye Diaspora Conference 2014. Aidha tunaomba kuchukua fursa hii kumshukuru Balozi wetu Peter Kallaghe kwa kutuwezesha kuendelea na shughuli hii ya maandalizi ya Mkutano wa Diaspora 2014. Kazi hii ni nzito, lakini kwa ushirikiano tunaoupata toka kwake binafsi na maafisa wake, naona tutafanikiwa vizuri. Kwa kuhitimisha, Hongera za Mwisho tunatoa kwa Mama yetu kwa kazi Nzuri anazozifanya za kumuendeleza Mwanamke na Mtoto wa Kike
5

Kitanzania. Tumeshuhudia kampeni zake tofauti, kwa mfano katika Nyanja ya Elimu na afya, ikiwemo ile ya Mtoto wa mwenzio ni wako, mkinge na maambukizi ya ukimwi. Hali kadhalika kwenye Elimu juzi ameweza kufanya Mahafali ya kwanza ya Shule ya Taasisi yake WAMA-NAKAYAMA na kwa ufaulu mzuri sana . Kwa hakika tukianza kuongea kuhusu mchango wako katika jamii yetu mama , tutaanza speech nyingine hapa ya kurasa 100. Hivyo naomba kuishia tu kwa kusema Hongera.

MUNGU IBARIKI TANZANIA. MUNGU WABARIKI VIONGOZI WETU. Mheshimiwa Rais, naomba kwa heshma na Taadhima kuwasilisha Risala ya WaTanzania wa UK. ASANTENI.

You might also like