Kitanzi
Kitanzi
SURA YA KWANZA
Anakwenda Baura nje kidogo ya mji wa Kondoa, nyumbani kwa wazazi wake. Hii
ni baada ya kukaa Dar es Salaam kwa miaka mitatu bila kwenda kwao, lakini sasa
analazimika kwenda kutokana na matatizo makubwa aliyokuwa nayo.
Matatizo mazito!
Pengine watu wazima katika ukoo wao wangeweza kumpa msaada mkubwa na
hatimaye furaha yake kurejea. Anatembea kwa uchovu, anapokwenda bado ni
mbali, lakini hajakata tamaa. Anazidi kutembea akiwa na simanzi tele moyoni.
Huyu ni Davina, msichana mrembo mwenye mvuto wa kutosha, ambaye
mwanaume yeyote aliyekamilika anaweza kushawishika kuwa naye. Matatizo
aliyokuwa nayo yalikuwa makubwa kuliko umri wake, kwa kumwangalia tu,
utagundua hajafikisha miaka 27! Ni binti mdogo sana, lakini yupo kwenye mateso
makali.
Baada ya mwendo mrefu sana, akaanza kuona nyumba kwa mbali katika kijiji
kilichokuwa mbele yake. Kwa bahati nzuri, akapita kijana mmoja aliyekuwa
akiendesha baiskeli. Akamsimamisha.
2
“Habari yako?” Davina akasalimia.
“Salama, vipi hali yako?”
“Njema...samahani kaka...”
“Usijali dada yangu, unasemaje?”
“Unakwenda Baura unipe lifti?”
“Hapana, naishia Kisewi.”
“Hata hapo patanitosha, utakuwa umenisogeza kidogo.”
“Twende.”
Davina akaketi kwenye kiti cha baiskeli kisha akaweka begi lake kichwani,
baiskeli ikaondoka taratibu. Moyoni alitamani sana yule kijana amfikishe
nyumbani kwao lakini kwa sababu alikuwa haelekei huko alishindwa kuelewa
atamshawishi vipi ili amkubalie.
“Mimi naitwa Mathayo, sijui wewe mwenzangu?”
“Davina.”
“Davina? Jina zuri sana.”
“Nashukuru hata wewe pia.”
“Umesema unaishia Kisewi, huwezi kunisaidia kuniwahisha nyumbani jamani,
maana nimechoka sana!”
“Hapana...kama nilivyokuambia awali, halafu isitoshe nimeagizwa vitu muhimu na
wazee.”
“Basi nitakupa soda!”
“Shilingi ngapi?”
“We’ unataka ngapi?”
“Elfu mbili!”
“Nitakupa tano!”
“Sawa.”
Kilikuwa kiasi kikubwa sana cha pesa kwa Mathayo, kwa Davina halikuwa jambo
la kufikiria mara mbili, alichohitaji ilikuwa ni kufikishwa nyumbani kwao haraka.
Kwanza alikuwa amechoka, lakini mbaya zaidi alikuwa katika matatizo makubwa
sana ambayo ufumbuzi wake ulikuwa nyumbani kwao.
Baada ya mwendo kidogo, baiskeli ilifunga breki nje ya boma la akina Davina.
Akashuka na kumlipa yule kijana pesa yake, akamshukuru na kuagana naye.
Akaingia ndani akianza kulia. Sauti ya kilio chake ndiyo iliyowachanganya watu
waliokuwa ndani. Wa kwanza kutoka alikuwa ni mama yake.
3
Akampokea, naye bila kuuliza sababu za kilio cha mwanaye, akaanza kulia. Baba
yake Davina akatoka haraka na kuwapokea, akawakaribisha kwenye jamvi chini ya
mnyaa.
“Vilio havitasaidia kitu, kama hamtasema kwanza kinachowaliza!” akasema.
Hakuna aliyejibu.
“Mama Davina, kuna nini?”
“Sijui...nimempokea mtoto akilia, nashindwa kuelewa amepatwa na tatizo gani?”
“Sasa kama hujui tatizo, kwa nini unalia?”
“Ningefanyaje kama mwanangu mwenyewe analia? Namjua vizuri sana Davina,
asingemwaga machozi yake kama hana matatizo!”
“Hata hivyo siyo suluhisho, vipi mwanangu? Hebu tuliza kwanza moyo, unieleze
vizuri ni nini tatizo?” mzee Ngamseni akasema kwa sauti ya kusihi.
“Nateseka baba, kila siku nimekuwa wa kulia, nitaishi hivi hadi lini?”
“Lakini kuteseka kuna chanzo mwanangu, hebu niambie kwanza, tatizo ni nini?”
Kwako Davina.
Nilikupenda sana na bado ninakupenda. Wewe na ulimwengu wote unatakiwa
kuendelea kufahamu kwamba, bado nakupenda. Nimekufa na penzi lako na
ninatesekea penzi lako. Naumia kukupoteza mpenzi wangu, lakini nasikitika
kwamba, kifo changu hakikuwa cha kawaida.
Kilipangwa! Tena kimepangwa na binadamu ambaye siku moja atakufa kama
mimi, ameamua kufanya hivyo kwa masilahi yake, lakini nakuhakikishia, hawezi
kufahanikiwa kamwe. Nafikiri unakumbuka kuwa mimi siyo wa kukubali
kushindwa kirahisi!
4
Unakumbuka jinsi nilivyokupata kwa shida, halafu leo hii anakuja mtu kujaribu
kuniingilia. Jambo hili haliwezekani na wala sitaliruhusu liwezekane. Naomba
kukuahidi jambo moja; kuliko huyo mpuuzi awe na wewe, ni bora nikuchukue uje
kuishi na mimi huku kuzimu.
Hili nitalitekeleza, muda mfupi ujao.
Kumbuka kwamba mimi ni mtu wa kusimamia mambo yangu vizuri. Hili pia
nitalisimamia! Nakutakia maisha mema, yenye maandalizi mema ya kuja huku
kuzimu nilipo. Nakupenda na sitakuacha.
Wako akupendaye,
Jeff.
Mzee Ngamseni akavuta pumzi ndefu sana, kisha akazishusha taratibu sana.
Akawatizama Davina na mkewe kwa zamu, kisha akaangalia chini. Kimya cha
dakika kadhaa kikapita, hakuna aliyezungumza, ingawa mzee Ngamseni
alionekana dhahiri kuwa na kitu anataka kuzungumza, lakini hakufanya hivyo.
Wakabaki wanatizamana kwa muda mrefu sana. Mama anamtazama mwana, mtoto
anatizama baba na baba anamtizama mkewe!
Wanatizamana.
Mpaka wakati huo, mama yake na Davina alikuwa hafahamu chochote juu ya
kilichokuwa kikiendelea.
Ni Davina na baba yake tu, ambaye aliisoma barua ile ndiyo waliokuwa
wakifahamu. Woga tele ukatanda. Baada ya kufikiria kwa muda mrefu sana, mzee
Ngamseni akamgeukia mwanaye na kumwambia...
“Mbona sielewi-elewi?”
“Ndiyo hivyo baba!”
“Inaonekana aliyeandika hii barua ni marehemu siyo?”
“Ndiyo!”
“Enhee ni nani?”
“Jeff!”
“Jeff...!!!”
“...ndiyo baba ni Jeff, yule kijana niliyewapa taarifa kwamba anataka kunioa.”
“Si alikufa?”
“Ndiyo baba, lakini nashangaa pamoja na kwamba amekufa, ameniandikia barua!”
5
“Haiwezekani...kuwa na akili mwanangu, tangu lini mtu aliyekufa akaandika
barua? Aliyekufa, amekufa...hana uwezo wa kufanya lolote, hana nguvu ya uhai,
sasa amekuandikia vipi? Usijichanganye kwa mambo madogo yasiyo na maana.”
“Yana maana baba, naujua vizuri sana mwandiko wa marehemu Jeff, ndiyo huu.
Haya mambo siyo ya mzaha baba, mwenyewe naogopa sana.”
“Huna haja ya kuogopa mwanangu, mtu ambaye anataka kukutisha, hashindwi
kukuandikia barua na kujifanya ndiye Jeff... lazima kuna mtu anajaribu
kukuchezea.”
“Basi na awepo, lakini hata saini yake ni ile ni ile! Nani anaweza kuandika barua
kwa kuiga mwandiko wa mtu pamoja na saini yake? Mimi sina imani na hilo
kabisa wazazi wangu.”
“Lakini bado anaweza kughushi tu mwanangu, watu wanaghushi vitu vingapi, ije
kuwa sahihi? Kumbuka kuwa unaishi Dar es Salaam mama, sehemu ambayo ina
kila kitu na kila aina ya watu, watu wa mjini wajanja sana mama.
“Mh! Baba...mbona naona kama huchukulii uzito hili suala? Sikiliza baba, hebu
ona hii barua, ona muhuri wa mahali ipotokea, angalia na anwani zake.
Zimeandikwaje?” Davina akasema kwa ukali akiwa anatetemeka.
Mzee Ngamseni akaikunjua ile barua kwa mara nyingine, taratibu akasoma anwani
za mwandishi wa barua ile. Ilisomeka hivi;
JEFF SEBASTIAN,
PRIVATE BAG,
KUZIMU MJINI.
Mzee Ngamseni akashtuka sana!
Davina hakuzungumza neno, akatoa bahasha aliyokuwa ameirudisha kwenye begi.
Akampatia baba yake, mzee Ngamseni alielewa kabisa alichokuwa akimaamisha
mwanaye. Alitakiwa kusoma muhuri wa Kituo cha Posta ilipotokea barua hiyo.
Yaliandikwa maneno kwa herufi kubwa yenye rangi nyeusi, yaliyosomeka;
MAKAO MAKUU YA POSTA,
PRIVATE BAG,
KUZIMU.
6
“Ndiyo baba!”
“Unajua maana ya kufa?”
“Ndiyo...nafahamu...!!!”
“Ni nini?”
“Ni ile hali ya kupoteza pumzi ya uhai, roho kuachana na mwili!”
“Kwa hiyo roho ya Jeff imeachana na mwili wake siyo?”
“Ndiyo baba!”
“Amekufa si ndiyo?”
“Hata kwenye mazishi yake nilikuwepo, nilishuhudia akifukiwa mbele ya macho
yangu. Kifupi naamini Jeff amekufa!”
“Kama hayo yote uliyoyasema ni sawa, basi tambua kwamba hakuna marehemu
anayeweza kuandika barua, acha ujinga,” Mzee Ngamseni akasema akisimama na
kuondoka zake.
“Lakini baba...”
“Lakini nini? Usiwe na akili pungufu kiasi hicho binti yangu, rudi zako mjini,
ukaendelee na kazi, acha kupoteza muda wako. Wajanja wanataka kucheza na akili
yako!” mzee Ngamseni hakuzungumza kitu, mguu wa kwanza, mguu wa pili
anaondoka zake.
Alikuwa anakwenda kilabuni.
Huku nyuma akaacha kilio cha mama na mwana!
***
Siku hiyo ilikuwa ngumu sana kwa Gerald, ofisi haikukalika! Kila alichokifanya
alihisi kama anakosea. Alikuwa mchovu kuliko kawaida. Siku nzima hakuna
alichokifanya zaidi ya kuchukua faili na kupekua-peua kisha kulirudisha mahali
pake.
Alikuwa amechoka kupindukia! Saa 9:30 mchana aliamua kuondoka zake, kwanza
hakuwa na cha maana cha kufanya. Akatoka na kwenda kwenye gari lake,
akaingia. Mara akajishangaa anakosa mahali pa kwenda!
“Nakwenda wapi?” akajiuliza mwenyewe bila kupata majibu.
Akabaki anapiga-piga usukani wa gari lake bila kupata muelekeo.
“Yeah! Nimekumbuka, acha nipitie kwanza Posta nikacheki barua,” akajisemea
mwenyewe moyoni mwake.
Ni wiki ya tatu sasa alikuwa hajapita Posta kuangalia barua. Akawasha gari na
kuondoka kwa mwendo wa kasi sana. Muda mfupi baadaye alikuwa Posta,
7
akafungua sanduku lake na kutoa barua, hakuwa na haraka ya kuziangalia,
akaingia kwenye gari na kwenda zake nyumbani.
Alipofika tu, alifikia sebuleni ambapo alianza kutizama barua moja baada ya
nyingine. Alipofikia bahasha hii ya khaki, iliyoandikwa kwa kalamu ya rangi
nyekundu, akashtuka sana.
Hakushtushwa na bahasha wala rangi ya wino uliotumika. Alishtushwa na muhuri
wa mahali ilipotoka. Barua ile ilikuwa na muhuri wa kuzimu! Akaifungua haraka,
anwani ya mwandishi nayo ikamchanganya!
Ile barua ilitoka kwa Jeff, rafiki yake wa siku nyingi, ambaye alifariki miezi
kadhaa iliyopita. Jeff yule yule anayemsumbua Davina kwa barua yake yenye
maneno makali ya kutisha.
Gerald akaanza kuisoma barua ile kimya kimya. Kila neno alilolisoma, alihisi
kuchanganyikiwa. Akajikuta anapiga kelele...
“MZIMUUUUUU....”
Gerald alizidi kutetemeka. Woga ukamtanda. Ghafla akaamua kunyamaza.
Akawaza inakuwaje Jeff rafiki yake ambaye alifariki, tena alishuka mpaka kaburini
na kupokea jeneza lake, aandike barua?
Lilikuwa swali zito sana, ambalo kwa akili zake mwenyewe asingeweza kujijibu.
Moyo wake ukazidi kwenda mbio, akapoteza furaha yake kabisa.
“Lakini haiwezekani bwana, siwezi kuchanganyikiwa na kitu kidogo kama hiki,
yaani mtu aliyekufa anaandika barua? Haya yatakuwa maajabu ya mwaka...acha
ninywe zangu pombe, nipumzike...” Gerald akawaza akienda kwenye jokofu na
kutoa chupa mbili za bia.
Akaanza kunywa kwa fujo!
Alikunywa sana siku hiyo akiamini alikuwa anapoteza mawazo. Alipofika bia ya
kumi alijikuta akipitiwa na usingizi pale pale sebuleni. Aliposhtuka ilikuwa ni saa
kumi na moja alfajiri! Amevimba mwili mzima kwa kung’atwa na mbu!
Hakuwa na kumbukumbu yoyote ile, lakini alipotupa macho yake mezani, akaona
ile barua. Akakumbuka kila kitu. Akaivuta na kuanza kurudia kuisoma. Machozi
kama maji yakaanza kutiririka machoni mwake.
Ile barua ilimuumiza sana, kama ni kweli ilikuwa imetokea kwa Jeff, ilikuwa na
hatari sana kwake, lakini hata kama siyo kweli, kwa nini atishiwe kiasi kile? Kwa
8
mara ya tatu sasa, anarudia kusoma ile barua. safari hii akaisoma kwa sauti ya
chini.
Ilikuwa barua yenye maneno makali sana. Maneno ya kuumiza na kuchoma moyo.
Maneno ya kukatisha tamaa ya maisha. Barua yenyewe ilisomeka hivi;
Kwako mpendwa Gerald.
Salaam!
Nilikupenda sana rafiki yangu Gerald, lakini sasa nakuchukia sana! Naomba
ufahamu kuwa, kuanzia unaposoma barua hii, ujue kwamba wewe ni adui yangu
namba moja! Nakuchukia kwa sababu mbili; Mosi, kusababisha kifo changu na
pili, kwa sababu unanichukia.
Labda nikukumbushe kidogo, unajua vizuri sana jinsi ninavyompenda Davina,
unajua sana! Tuachane na hilo, najua unafahamu kwamba Davina ni mwanamke
mzuri mno, lakini mwanzoni hakuwa hivyo, nilimkuta akiwa hana matunzo, na ni
mimi ndiye niliyehakikisha Davina anakuwa kama alivyo leo!
Mimi ndiyo nimempendezesha hadi ukajikuta umeshawishika kunisaliti. Usivyo na
roho ya kibinadamu, ukaona unitoe duniani kabisa, umefanikiwa rafiki, lakini
damu yangu haitapotea bure brother. Nitafanya kitu kama kisasi kwa uliyonifanyia.
Fahamu kuwa umeniua nikiwa na malengo mengi sana na Davina wangu, nilikuwa
nakaribia kumuoa, lakini wewe umekatisha ndoa yetu. Ukaniua.
Kwa barua hii, nakutaka uachane kabisa na mpango wako wa kumuoa Davina.
Nina ushahidi wa asilimia mia moja, kuwa wewe ndiye uliyepanga kifo changu,
umefanikiwa! Kufanikisha kwako unyama huo, hakumaanishi kwamba nia yako ya
kumuoa Davina imetimia...
Hujafanikiwa!
Na hutafanikiwa!
Davina ni mwanamke ambaye nampenda kwa moyo wangu wote. Hawezi kufunga
ndoa na mtu mwingine yeyote zaidi yangu! Kwa taarifa yako, ahadi hiyo lazima
itimie.
Hivi karibuni, nitamchukua Davina na kumleta huku kuzimu ambapo nitafunga
naye ndoa na kuishi naye milele huku, kama tulivyoahidiana mwanzoni. Kwa
9
kifupi, acha kumfuatilia, ukikaidi na wewe pia nitakuchukua uje huku kuzimu ili
tupambane vizuri.
Kaka, ni bora nilipize kisasi ukiwa huko huko duniani ambapo sikuoni, kuliko
nikuchukue uje huku ambako nitakuwa nakuona! Lakini adhabu yako inaweza
kupungua kama utaacha kumfuatilia Davina.
Najua bado hujamwambia kama unampenda, na sasa hivi amesafiri, amekwenda
Kondoa. Nakushauri usifanye hivyo. Mwache mpenzi wangu tafadhali. Kumbuka
kwamba, naandika barua hii, kwa baraka zote za mizimu ya babu zangu ambao
nimekutana nao huku. Hawa wameahidi kunisaidia, iwapo wataona nashindwa
kukudhibiti. Unaweza kuona ni jinsi gani vita ilivyo kubwa na hatari.
Gerald wewe si mgeni kwangu, unanijua vizuri sana hasa ninapokuwa nimeamua
kusimamia mambo! Hili pia nitalisimamia mpaka mwisho. Usije ukajidanganya
kwamba huu ni mzimu wangu!
Hapana rafiki.
It’s me,
Jeff.
Gerald alirudia kusoma ile barua zaidi ya mara tano, maneno hayakubadilika.
Yalikuwa yale yale. Akatizama na anwani ya mwandishi kwa mara nyingine.
Ilikuwa ile ile!
Akageuza bahasha na kuangalia muhuri wa ilipotokea, ulikuwa ule ule!
Akahisi kuchanganyikiwa!
Kilichomchanganya zaidi ni jinsi anavyoandika, mwandiko na sahihi. Kila kitu
ilikuwa ni Jeff. Kwa vyovyote vile, barua ilikuwa imetoka kwa Jeff, lakini swali la
msingi ambalo lilizidi kuutibua ubongo wake lilikuwa ni; Marehemu anaweza
kuandika barua?
“Shiiiiiit...nitajua la kufanya...mtu mzima hatishiwi nyau bwana. Iwe ni kweli Jeff
kaandika, isiwe kweli, nitajua la kufanya. Kubwa zaidi, siwezi kuacha kumfuatilia
Davina, mwanamke anayeutesa moyo wangu.
10
“Mimi ni Gerald, mwanaume wa shoka, najiamini na nasema wazi kwamba,
Davina ndiye mke wangu. Aliyekufa amekufa, lake halipo tena,” maneno haya
yalizunguka kichwani mwa Gerald akijipa-piga kifua.
Akaingia chumbani kulala.
11
SURA YA PILI
12
“Hivi Halima ulikuwa unakumbuka kwenda Posta kweli mdogo wangu, tangu
nimekwenda Kondoa?” hili lilikuwa swali la kwanza kabisa, Davina kumuuliza
housegirl wake mara baada ya kufika nyumbani kwake Tandika anapoishi.
“Ndiyo dada, tena kila siku...”
“Umepata barua?”
“Ndiyo!” Halima akajibu huku akifungua droo moja katika kabati maalum la
vitabu na kutoa barua tisa na kumkabidhi.
Haraka, Davina akaanza kufungua moja baada ya nyingine akiangalia majina ya
watumaji. Kati ya barua zile tisa, tatu zilikuwa za Jeff. Akaanza kuisoma barua ya
kwanza...
Iliandikwa hivi; Mpenzi wangu wa moyo Davina.
Nilikupenda, nakupenda na bado nitaendelea kukupenda daima.
Pole na safari mpenzi. Najua kwa nini ulifunga safari kwenda Kondoa. Usiendelee
kusumbuka mpenzi, huu siyo mzimu wangu, ni mimi mwenyewe Jeff.
Kama nilivyokuambia awali, ahadi yangu ya ndoa iko pale pale! Ila kutakuwa na
mabadiliko kidogo, ndoa yetu ifafungwa huku kuzimu badala ya duniani kama
tulivyopanga.
Mimi pia sikupenda hili litokee, lakini mtu mmoja mwenye roho ya kinyama
amesababisha haya. Sitakutajia leo wala kesho, siku ukija huku ndiyo nitakuambia
ni nani mtu huyo.
Endelea kujiandaa mpenzi, siku si nyingi nitakuja kukuchukua.
Nikupendaye kwa dhati,
Jeff Sebastian.
Davina akabaki ameduwaa! Akaanza kutetemeka. Akajikuta anapiga kelele...
“JEFF MPENZI WANGU, KWA NINI UNANITESA?”
Machozi ndicho kitu pekee ambacho kingeweza kumpunguzia machungu Davina.
Alilia sana. Akili yake haikukaa sawa. Barua za vitisho kutoka kwa marehemu Jeff
zilizidi kumchanganya!
13
Marehemu kuandika barua siyo jambo jepesi, ambalo linaweza kuchukuliwa ki-
wepesi kiasi kile! Lilikuwa jambo zito ambalo ufumbuzi wake pengine ungehitaji
wanajimu!
Kwa binti mdogo kama Davina, hakika asingeweza kujua mambo hayo,
asingeweza kufanya chochote kile bila ya uangalizi ulio sahihi na makini.
Uangalizi huo usingeweza kupatikana mahali popote zaidi ya kwa wazazi wake!
Baba yake!
Ni baba, kwa sababu mwanaume wa Kiafrika ndiye kichwa cha nyumba. Maamuzi
yake huwa ya mwisho na hakuna ambaye anaweza kuyayumbisha!
Alipofika hapo, akazidisha kilio zaidi, alifanya hivyo kwa sababu baba yake,
ambaye ndiye agetakiwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha jambo lile linaisha,
ndiye ambaye anapingana naye kwa asilimia mia moja!
Haamini mizimu!
Haamini uchawi!
Davina anazidi kuchanganyikiwa!
“Nikimbilie wapi mimi jamani? Kama baba yangu mwenyewe ambaye ndiye
mwenye uwezo wa kunisaidia anakataa na anasema wazi kuwa haamini mizimu?
Lakini siyo haamini, bali haamini kabisa juu ya hili jambo...
“Anaweza kuwa sahihi kidogo, lakini kwa nini hataki kuishughulisha akili yake
zaidi ya hapo? Kweli kuna marehemu ambaye anaweza kuandika barua kweli?
Kwa nini hawezi kuona hili tatizo?!!” Davina anajisemea maneno haya akizidisha
kilio.
Halima, msichana wake wa kazi, baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu
akisikiliza kilio cha bosi wake, sasa ameshindwa kuvumilia. Anajisogeza kichovu
hadi kwenye mlango wa chumba cha Davina.
Hakuwa na haja ya kugonga, akaingia moja kwa moja hadi chumbani. Akamkuta
Davina akizidi kulia, akiwa amekumbatia bahasha ya khaki. Kwa haraka, Halima
akajua ilikuwa ni taarifa za msiba.
14
“Kuna nini dada?” Halima akamwuliza dada yake, akiwa ameketi chini
akimtizama kwa huruma.
“Niache tu, Halima mdogo wangu, niache...”
“Kwa nini nikuache? Kuna nini kwani dada’ngu?”
“Jeff!”
“Jeff kafanyaje tena?”
“Kaandika barua zingine, tena tatu...nimeshasoma moja, anaendelea kusisitiza
atakuja kunichukua hivi karibuni!”
“...sikiliza dada, hebu kwanza nyamaza kulia. Tuliza moyo kwanza...unajua sasa
naanza kuingiwa na wasiwasi juu ya hili jambo. Nadhani tunatakiwa kufanya kitu
fulani kwanza.
“Nahisi kuna kamchezo kanachezwa, utakuwa unalia na kujiumiza kumbe kuna
watu wanafanya mambo yao...lakini naona kabisa njia ya kupata ukweli,” Halima
akasema kwa utulivu sana.
“...anaonekana anajua jambo fulani huyu, acha nimsikilize...” akawaza Davina na
kusema: “Kwani mdogo wangu, we’ ulikuwa unafikiri kuna nini?”
“Siyo rahisi kusema moja kwa moja nafikiri nini, lakini naweza kushauri kitu kwa
ajili ya kuutafuta ukweli. Nenda Posta, uonane na uongozi, waeleze juu ya jambo
hili, halafu waombe barua zote zitakazotumwa, zisiingizwe kwenye sanduku letu
moja kwa moja, zihifadhiwe mahali maalum, ambapo tutakuwa tunazifuata
hapo...” Halima akashauri.”
“Halafu?”
“Wakati huo tutakuwa tunaendelea kufungua sanduku letu kama kawaida, ikiwa
zile barua ni za miujiza, zitaendelea kuingia lakini kama ni mchezo, basi hapo
mchezaji atakuwa amenasa, maana hakutakuwa na barua kwenye sanduku letu,
isitoshe hata Uongozi wa Posta utakuwa na taarifa kuwa barua zote zinafikia
sehemu maalum na siyo kwenye sanduku. Naona huu unaweza kuwa mwanzo wa
kuelekea kwenye kuupata ukweli,” alisema Halima kwa utulivu sana akionekana
kupangilia vyema hoja yake.
15
Davina alimwangalia yule binti akiwa haamini kabisa kuwa maneno yale yalikuwa
yanatokea kwenye kinywa chake. Hakuamini kama Halima angeweza kuwa na
maneno yenye akili kama yake. Akasimama kisha akamkumbatia kwa furaha.
“Ushauri wako umenipa nguvu, unaweza kusaidia kuujua ukweli. Nitafanya hili
zoezi kesho asubuhi, halafu kesho hiyo hiyo narudi Kondoa, lakini nikirudi
nitafaya kitu kwa ajili yako...” Davina alimwambia Halima.
“Nitashukuru sana dada...nitafurahi sana.”
“Anza kufurahi mapema, amini kwamba umenifungua. Ahsante sana Halima,
nashukuru sana.”
“Usijali dada, ni wajibu wangu, sehemu ya kazi yangu. Wewe ni dada yangu,
inanipasa kukusaidia ushauri pale inapobidi, hasa katika mambo mazito kama
haya,” Halima akamwambia Davina.
Davina akaingia bafuni, baadaye akarudi chumbani kubadili nguo, kisha akajongea
sebuleni na kuanza kuangalia filamu. Aliisubiria kesho kwa hamu kubwa sana.
***
Gerald aliamka asubuhi akiwa na nguvu mpya, hata akili yake ilikuwa mpya.
Hakuwa amelewa kama jana yake, Gerald huyu ni mpya na mzima wa afya njema.
Barua ya Jeff ikarudia upya kichwani mwake.
Ikafunguka ubongoni mwake na kuanza kuisoma. Alipofikia sehemu iliyoandikwa
kuwa Davina alikwenda Kondoa, akachanganyikiwa kidogo. Kwake ilikuwa nafasi
ya kuweza kuanza kutafuta ukweli wa ile barua.
“Yap! Hapa hapa nitaujua ukweli, nampigia Davina sasa hivi,” akawaza Gerald
huku akibonyeza namba za Davina na kupeleka simu sikioni.
Muda mfupi tu, baadaye Davina akapokea...
“Vipi shem Gerald, za siku mwanya?” sauti laini ya Davina ikasikika.
“Salama, enhee hebu niambie, uko wapi?”
“Town, naelekea Posta!”
16
“Posta? Kufanya nini jamani wakati una msichana wako wa kazi?”
“Ni special case Gerald, lazima niende mimi!”
“Special case? Sipaswi kujua?”
“Ni habari ndefu shemeji yangu, lakini fahamu kwamba Jeff ananisumbua
sana...nafikiri tukionana nitakueleza vizuri zaidi!”
“Jeff anakusumbua kivipi? Shemeji yangu unaanza kuzeeka vibaya! Jeff si
tumemzika?” Gerald alitamka maneno hayo kwa ujasiri, lakini moyoni mwake
akiwa na wasiwasi mwingi sana na hamu ya kutaka kujua kitakachofuata.
Alianza kuhisi kuwa Davina naye aliandikiwa barua. Alihitaji sana kuujua ukweli
zaidi.
“Ndiyo maana nimekuambia tukikutana tutaonana.”
“Lini sasa, maana umenishtua sana!”
“Wiki ijayo.”
“Kwa nini isiwe leo?”
“Nina safari asubuhi hii baada ya kutoka Posta, nakwenda Kondoa...nimetoka huko
jana tu, lakini nalazimika kurudi tena leo, sababu ni hiyo ya Jeff kuniandikia barua,
nachanganyikiwa sana shemeji yangu,” Davina alisema kwa sauti iliyojaa majonzi.
Gerald alihisi kuchanganyikiwa. Hapo akajua kwamba ni marehemu Jeff alikuwa
akiandika barua. Akakata simu.
Kitendo cha Davina kumthibitishia kwamba ni kweli alikwenda Kondoa siku za
karibuni na siku hiyo pia alikuwa njiani kwenda huko baada ya kutoka Posta
alipokwenda kwa mambo yake binafsi, kilimchanganya sana Gerald!
Alibaki ameishikilia ile simu asijue la kufanya. Moyo wake ukaingiwa na ubaridi
mkali, akahisi kama kizungu-zungu kikali. Akajitupa kitandani. Barua ya Jeff
ilimchanganya sana, lakini kubwa zaidi ambalo lilimtisha ni kwamba, kifo cha
Jeff kilikuwa cha siri kubwa sana. Ni kweli yeye ndiye chanzo.
Muuaji!
17
Ni yeye ndiye aliyepanga njama zote za kifo cha Jeff na ni kweli kwamba alifanya
hivyo ili aweze kumpata Davina kirahisi! Alishawishika kufanya hivyo kutokana
na penzi lao kuwa motomoto na lisilo na dalili za kuvunjika kirahisi.
Njia pekee ambayo ingemsaidia kumpata Davina ilikuwa ni kumuondoa Jeff
duniani! Jambo lilo likapangwa katika vikao vya siri na wakafanikisha kwa
asilimia mia moja!
Hakuna mtu aliyegundua jambo hilo, lakini kuandikiwa barua na Jeff, tena kwa
mwandiko wake mwenyewe na kuelezea tukio zima lilivyokuwa, kulimpa mashaka
sana.
Akili ikachemka...
“Natakiwa kufanya jambo lingine zaidi. Sitakiwa kuwa mjinga wa kiwango
kikubwa kiasi hiki, kuna mtu aidha ananisaliti au alinisaliti...yes I think so! I have
to do something to prove it. I’m Gerald...” Gerald akajikuta akitamka kwa sauti ya
juu akipiga-piga kifua chake.
Akachukua simu yake, akitaka kupiga namba fulani, lakini kabla hajafanya hivyo,
simu yake ikaita. Macho yakaganda kwenye kioo baada ya kuona jina la Davina.
Akajishauri sana, lakini mwisho wake akaamua kupokea.
“Yes shem...” Gerald akasema.
“Vipi ulikata simu au ilikatika?”
“Bwana wangu! Mitandao yenyewe hii ya mjini...ilikatika. enhee niambie!”
“Ndiyo kama nilivyokuambia shemeji yangu, yaani nimechanganyikiwa sana,
nafikiri nitakuwa na mambo mengi ya kuzungumza na wewe nikirudi Kondoa,”
Davina akasema kwa sauti ya upole sana.
Gerald akashtuka.
Mambo mengi?
Moja kwa moja Gerald akafikiri inawezekana katika barua alizotumiwa na Jeff,
amemtaja!
“Ni juu ya hii issue ya barua za Jeff?”
“Ndiyo!”
18
“Mbona maajabu lakini? Enhee, hivi ameandika nini hasa kwenye hizo barua
zake?” Gerald akauliza kimitego, akihitaji kujua kitu zaidi.
“Vitisho tu...sijui eti anataka kuja kunichukua...ah, nimechoka sasa, lakini nikirudi
Kondoa nitakutafuta. Sitegemei kukaa muda mrefu sana.”
“Sawa, safari njema.”
“Ok! Ahsante sana.”
Wakakata simu zao.
Jeff alibaki ameishikilia ile simu kwa muda mrefu sana, baadaye akakumbuka
kufanya mambo mawili muhimu. Kwanza kabisa alitakiwa kukaa kikao na wale
jamaa wote waliokuwa wanashughulikia mauaji ya Jeff, pili, alitakiwa kumtaarifu
meneja wake kwamba hatafika ofisini siku hiyo, ili akaimu nafasi yake. Kwanza,
akampigia meneja.
“Nina dharura, sitafika ofisini leo, pengine na hata kesho. Endelea na majukumu
yako kama kawaida na viporo vyangu vilivyopo ofisini kwangu, lakini kumbuka
usiruhusu malipo yoyote wiki hii, kazi njema Edward,” Gerald aliongea kwa sauti
tulivu, iliyoonyesha kuwa ana jambo zito lakini lisilohitaji ushauri wa mtu yeyote.
“Nimekuelewa bosi.”
Gerald akavuta pumzi ndefu sana, kisha akazishusha kwa mkupuo huku
akitembeza macho yake kila kona ya chumba chake nadhifu. Akabonyeza namba
za Fikiri, Mkuu wa Kikundi cha Kigaidi cha Nyamangumu, lakini alizoeleka zaidi
kwa jina la Master. Huyu ndiye aliyeongoza zoezi zima la mauaji ya Jeff.
“Master unanifahamu vizuri nilivyo makini na mambo yangu, lakini kama kuna
mambo ambayo nayachukia zaidi duniani, basi ni USALITI!” Hivi ndivyo Gerald
alivyoanza kuzungumza, baada ya Master kupokea simu.
“Unamaanisha nini mkubwa?”
“Saa 2:00 usiku wa leo, nahitaji kukutana na wewe pamoja na jopo zima
lililoshughulikia kifo cha Jeff. Ni muhimu sana, zingatia tafadhali!”
“Wapi?”
“Pale pa siku zote!”
19
“Shwari!”
***
“Kwa nini umeamua kufanya hivi?” Meneja Mkuu wa Posta akamwuliza Davina,
baada ya kumweleza nia yake ya kuzuia barua zisiende moja kwa moja kwenye
sanduku lake.
“...ni habari ndefu sana bosi, unaweza kustaajabu kidogo. Iko hivi....” Davina
akamsimulia kila kitu.
Meneja akachanganyikiwa!
“Unahisi kuna mtu wetu labda anatumiwa kukuchezea?”
“I’m not sure, lakini nafikiri tujaribu kufanya hivi kwanza, tunaweza kugundua
kitu fulani. Nina safari asubuhi hii, baada ya wiki moja nitakuwa nimerudi, hapo
ndipo tutakapojua kitu fulani,” Davina akasema.
“Ok! Hakuna tabu katika hili, ukirudi tuwasiliane.”
“Ahsante sana.”
Davina akatoka nje ya Posta, akachukua taxi iliyompeleka Kariakoo, mtaa wa
Kamata, zilizopo ofisi za basi la Scandinavia.
***
Saa 12:00 za jioni, basi la Scandnavia liliingia mjini Dodoma, ikiwa ni safari ya
saa sita kutokea Dar es Salaam. Davina alishuka akiwa mchovu sana. Kwa muda
huo haikuwa rahisi kupata usafiri wa Kondoa, hata kama angepata isingekuwa
rahisi kufika Baura kwa miguu, akipita kwenye mapori peke yake, tena
mwanamke!
Akaamua kulala pale Dodoma.
Akatafuta hoteli nzuri, akapumzika kwa maandalizi ya kwenda Baura, Kondoa,
asubuhi inayofuata.
20
Saa 7 na dakika zake za usiku, akiwa katika usingizi mzito, akasikia simu yake
ikiita, akapuuza akidhani huenda alikuwa ndotoni. Simu ikaita hadi ikakatika.
Baada ya muda ikaanza kuita tena, akaamka na kutizama kwenye kioo cha simu.
Hapakuwa na namba!
Ilikuwa ni private!
Akapokea...
“Haloo...” Davina akaongea kwa uchovu sana.
“Yes mpenzi wangu Davina...pole kwa uchovu wa safari, lakini nakushangaa sana
ni kwa nini hutaki kusikiliza maagizo yangu?” ilikuwa sauti ya taratibu sana,
ambayo hakuifahamu mapema, lakini kila muda ulivyozidi kusogea, ndivyo
alivyozidi kuikumbuka vizuri ile sauti.
Ilikuwa sauti ya Jeff.
“Nani mwenzangu?” Davina aliuliza kwa sauti ya juu, iliyojaa woga na kavu,
macho akiwa ameyatoa kuliko kawaida.
“Usiniambie umeshaisahau hii sauti mpenzi, Jeff hapa nazungumza kutoka
kuzimu...”
“What?”
“Jeff...narudia tena kukuonya, fuata maagizo yangu tafadhali, acha ubishi usio na
maana. Kwa nini unakuwa mgumu kuelewa? Sasa Kondoa unakwenda kufanya
nini? Unapaswa kusubiri hadi nitakapokuja kukuchukua na siyo vinginevyo.
Nitafurahi kama asubuhi utapanda gari la kurudi Dar na siyo kujisumbua kwenda
Kondoa. Usiku mwema.”
Davina alihisi kuzimia!
21
SURA YA TATU
22
“Hujuma, kuna kaujanja fulani hivi kanachezwa...kuna mchezo tu...yupo mtu
ametusaliti,” Gerald akasisitiza.
“Hivi Gerald una kichaa? Jeff alikufa hakufa?” Master akamwuliza kwa hasira.
“Alikufa!”
“Alizikwa, hajazikwa?”
“Alizikwa?”
“Sasa huu ujanja unaosema ni upi? Inamaana hauna imani na sisi? Mbona kazi
yako ilifanyika kwa uaminifu mkubwa na wewe umeshuhudia mpaka maziko yake
au unataka kutuchoma?”
“Siyo hivyo Master!”
“Bali?”
“Lakini mbona anaandika barua sasa?” Gerald akasema akifungua bahasha yake ya
khaki na kutoa barua na kuwapa ili waisome.
Wote walipigwa na butwaa.
“Lakini mimi siamini kama ni Jeff mwenyewe ndiye aliyeandika hii barua!”
“Kwa kwanini?”
“Mtu aliyekufa hawezi kuandika barua, kwanza hana uhusiano wala mawasiliano
yoyote na dunia, si ameshakufa jamani?”
“Lakini huo ni mwandiko wake niliouzoea na hata sahihi ni yake pia!”
“Hata kama...kuna mtu anaghushi, amini usiamini. Sasa ukiendekeza hisia hizo,
tunaweza kuharibu uhusiano wetu mzuri kikazi kwa sababu ya mtu anayekuchezea
akili, siamini kama kuna kijana wangu anaweza kunisaliti, siamini hata kidogo!”
Master akasema kwa kujiamini.
“Kweli Master?” Gerald akauliza.
“Bila shaka unaniamini.”
“Poa...”
23
Kikao kikaahirishwa, Gerald akiwa hana matumani kabisa. Akaondoka akiendelea
kuwaza njia za kuutafuta ukweli zaidi, lakini kwa sasa alikuwa na hamu sana ya
kuzungumza na Davina, ambaye alionekana kuwa na siri nzito moyoni mwake.
***
Anaamka kitandani, anajisogeza kwenye swich ya taa, anawasha. Anahema kwa
kasi na kuzidi kuchanganyikiwa! Anafungua simu yake kwenye ‘Call register’
kisha anabonyeza ‘Received calls’ halafu anaangalia namba ya mwisho kupigwa.
Haionekani!
Ilikuwa private number!
Lakini kila alipojaribu kuvuta kumbukumbu vizuri juu ya ile sauti aliyoongea nayo
kwenye simu, anagundua kwamba ni kweli alikuwa anaongea na Jeff. Mpenzi
wake wa zamani ambaye kwa sasa ni marehemu.
Sasa anazidi kuchanganyikiwa, maana amepiga simu kabisa. Tena ametoa onyo
kwamba, hatakiwi kwenda Kondoa na badala yake anatakiwa kugeuza asubuhi
inayofuata kurudi Dar es Salaam.
“No...haiwezekani...” Davina akawaza huku akifungua begi lake na kutoa suruali
nyepesi na blauzi fupi ya kubana, akavaa.
Mara moja akapiga simu Mapokezi. Muda si mrefu sana, simu yake ikapokelewa.
“Mapokezi hapa, naomba nikusaidie tafadhali!” sauti ya msichana wa Mapokezi
ambayo ilijaa uchovu ilisikika.
“Room no. 104, ghorofa ya tatu!”
“Ndiyo!”
“Kuna Klabu gani nzuri ya usiku hapa Dodoma?” Davina akauliza.
“Club 84!”
“Taxi?”
“Zipo. Nimpigie dereva?”
“Tena afanye haraka sana, baada ya dakika 10 nitakuwa hapo!”
24
“Ok!”
Davina aliogopa kuendelea kulala pale hotelini, aliona ni bora aende disko
akapoteze muda hadi asubuhi ili aanze safari ya kwenda Kondoa, bado hakuwa na
wazo la kurejea tena Dar es Salaam.
Muda mfupi baadaye alikuwa kwenye taxi akipelekwa Klabu, alipofika akamlipa
dereva kisha akaingia. Ilikuwa Klabu nzuri kuliko kawaida, hakutegemea kama
Dodoma kungekuwa na ukumbi mzuri kama ule. Kilichoendelea ilikuwa ni
kunywa sana pombe mpaka akalewa chakari!
Uzuri wake, ulikuwa tatizo kubwa kwa wanaume waliomuona akiwa amekaa peke
yake tena mwenye mawazo mengi. Wengi walimfuata na kujaribu kutupa ndoano
zao, lakini Davina hakuwa na muda huo, hakuwaza wala hakuwa na hamu na
wanaume! Alikuwa akiwaza matatizo yake tu!
“Siogopi kitu chochote, najua Jeff umeshakufa, ila kuna mtu anajaribu kucheza na
akili yangu,” Davina akawaza akiendelea kunywa pombe kwa hasira.
Davina aliendelea kunywa hadi saa 10:40 za usiku ambapo wimbo wa mwisho
ulipigwa, akaenda kuchukua taxi na kwenda zake hotelini. Hakulala tena,
akaendelea kutizama runinga hadi kulipokucha. Saa 12:00 alikuwa kwenye basi,
tayari kwa safari ya kwenda Kondoa, nusu saa baadaye.
***
Sauti ya kilio cha Davina ndiyo iliwashtua wazazi wake waliokuwa ndani
wanapata chakula cha mchana! Ilikuwa ni saa tisa na dakika zake za mchana.
Mama yake ndiyo alikuwa wa kwanza kutoka nje na kwenda kumpokea.
Alishajua tatizo ni nini, hakuwa na haja ya kumwuliza. Akamwingiza ndani,
ambapo alipokutanisha macho na baba yake, akazidi kuangua kilio.
“Tulia kwanza mama, mbona unakuwa na hasira hivyo? Umeshakuja nyumbani,
sisi ni wazazi wako, tunakupenda na hatutakuwa tayari kuona unapata matatizo!”
baba yake Davina akasema akimtizama mwanaye usoni.
“Lakini baba, hutaki kuamini kama ni mzimu wa Jeff ndiyo unaonitesa...sasa ona
anavyonitesa, jana nikiwa Dodoma, kanipigia simu na amesisitiza nisije Kondoa,
25
sasa amejuaje kama mimi nakuja huku?!” Davina akamwambia baba yake ambaye
alionekana kushtushwa na kauli ile.
“Amekupigia simu? Una uhakika? Namba zilikuwa zake?” Baba yake akauliza
maswali mfululizo.
“Ndiyo baba nina uhakika na sauti yake, lakini namba hazikutokea, zilikuwa ni
private!”
“Nilikuambia ni uongo, yupo mtu anayekuchezea, maana kama angekuwa yeye,
kwa nini asingekupigia kwa namba zinazoonekana ili baadaye umpigie kama
ukiwa na shida naye?” Mzee Ngamseni akauliza akianza kuonyesha ukali kidogo.
Kabla Davina hajajibu kitu, simu yake ikaanza kuita, akaitoa kwenye mkoba na
kutizama kwenye kioo cha simu!
Ilikuwa private number!
Akapokea...
Alikuwa ni Jeff.
Moyo wa Davina ulizidisha kasi, haikuwa jambo jepesi kuamini kwamba sauti
aliyoisikia kwenye simu yake ilikuwa ya Jeff. Lakini kwake yeye, mwanaume
ambaye alikuwa naye katika mapenzi kwa miaka mitatu, tena siku za mwisho wa
uhai wake alikuwa akilala naye karibu kila siku!
Jeff huyu huyu ambaye alikuwa anampigia simu karibu mara ishirini kwa siku,
wanayecheka naye pamoja. Wanayekula naye pamoja. Wanayetoka pamoja. Kweli
anaweza kusahau sauti yake? Yatakuwa maajabu ya kwanza ya dunia.
Sauti haikuwa ngeni hata kidogo!
Ilikuwa sauti ya Jeff, tena siyo kwa hisia tu, bali alikuwa na uhakika kabisa kuwa
ni yake. Jeff ndiye alikuwa anaongea kwenye simu...
“Umesema Jeff?!” Davina akasema kwa woga akiyatoa macho yake.
“Ndiyo na sioni sababu ya kujitambulisha kwako kila wakati. Sikiliza
Davina...wewe ni mpenzi wangu, nakupenda sana na sipendi kabisa kutumia kauli
za ukali au kuamrisha, lakini wewe ndiyo unasababisha. Nitaendelea hivi hadi
utakapobadilika...
26
“Kwa nini hutaki kuamini ninachokuambia? Kwa nini unakuwa kichwa ngumu?
Nimeshakuambia kwamba mimi nimeuawa na mtu wangu wa karibu ili yeye
akupate wewe, ili kuepusha hilo nataka kuja kukuchukua, sasa kwa nini unakuza
hili jambo hadi inaonekana kama mimi ni mzimu? Mimi si mzimu...ni Jeff halisi.
Jeff, mwanaume wa maisha yako!” sauti ya Jeff ilipenya sawa sawia katika ngoma
za masikio ya Davina.
Davina hakuzungumza kitu zaidi ya kuanza kulia. Wazazi wake wakawa kama
wamepigwa na butwaa, hakuna aliyezungumza chochote zaidi ya kubaki
wanamshangaa.
“Davina...” Jeff akaita simuni.
Davina hakuitika.
“Sikiliza kwa kuwa nimeshakuonya mara nyingi na hutaki kusikia,
nakuhakikishia, sitakusumbua tena. Hutaona ujumbe wangu wa barua, meseji wala
simu. Hutaona yote hayo, lakini nakusisitiza, kamwe usiolewe na mtu yoyote kwa
sababu kwa kufanya hivyo utakuwa unajisumbua. Mwanaume ambaye anatakiwa
kukuoa wewe ni mimi tu na si vinginevyo. Nitahakikisha hili linatimia. Kwaheri ya
kuonana.”
“Usikate simu kwanza, sikiliza wewe ni Jeff kweli?” Davina aliuliza baada ya
kupata ujasiri wa ghafla.
“Ndiyo!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Ulikufa lakini?”
“Ndiyo!”
“Ila bado una nia ya kunioa?”
“Ndiyo!”
“Kivipi sasa wakati tupo sehemu mbili tofauti?”
“Lakini nimeshakuambia kwamba nitakuja kukuchukua na kukuketa huku nilipo?”
27
“Unadhani hilo linawezekana?”
“Sana.”
“Naomba nikuulize swali la mwisho mpenzi wangu Jeff wa maajabu.”
“Uliza.”
“Unafahamu kwamba sasa nipo wapi?”
“Kondoa.”
“Kwa nani?”
“Wazee wako.”
“Safi kabisa, umepatia....nataka ufanye jambo moja jepesi sana kama ni kweli bado
unataka kunioa Jeff!”
Ujasiri wa Davina uliwashangaza sana baba na mama yake, hata yeye mwenyewe
pia alijishangaa sana. Kuzungumza na mzimu wa Jeff bila woga, moyoni mwake
aliona hakuna sababu ya kuwa mwoga tena, wakati kila wakati Jeff alikuwa
anapiga simu.
Hata hivyo kuuliza kwake maswali mengi kulikuwa na makusudi, alikuwa anataka
kuhakikisha kama ni kweli aliyekuwa akizungumza naye alikuwa ni Jeff,
marehemu mpenzi wake. Anavyozungumza, anavyojibu maswali, anavyojieleza,
anavyojiamini na kila kitu kilikuwa ni Jeff mtupu!
Davina alijihakikishia wazi kwamba aliyekuwa anazungumza naye ni Jeff wake!
“Sema Davina, unataka nifanye nini?” Jeff akamwuliza.
“Baba yupo hapa, naomba uzungumze naye na umweleze nia yako ya kunioa na
kunipeleka huko kuzimu ulipo wewe.”
“Sawa...mpe mkwe wangu nizungumze naye!” Jeff alisema kwa sauti tulivu sana.
Davina akampa baba yake simu.
“Haloo haaaalooooo....” baba yake Davina aliita kwenye simu, lakini hakuna
aliyeitika.
Davina alipochukua ile simu, akagundua kwamba simu ilikatika.
28
“Vipi?” mama yake akauliza.
“Imekatika.”
Wote wakabaki kimya wakitizamana kwa zamu, lillikuwa jambo la kushangaza
sana ambalo walishindwa kabisa kuelewa linavyotokea. Kila mmoja alikuwa na
uhakika kwamba Jeff alikuwa marehemu, sasa iweje anapiga simu? Kwa mara ya
kwanza mzee Ngamseni alianza kuamini tukio lile!
“Mwanangu una uhakika kwamba, sauti ilikuwa yake?”
“Ndiyo baba.”
“Kweli kabisa?”
“Nakuhakikishia baba.”
“Basi ni mzimu huu,” mzee huyo alisema kwa sauti ya upole.
“Mi’ nilisema tangu mwanzoni hamkuniamini, sasa mmeshuhudia wenyewe!”
Davina akasema.
“Huu siyo wakati wa kulaumiana mwanangu, kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni
mtambiko haraka sana!”
“Sawa baba. Nashukuru kwa kukubali kunisaidia.”
“Usijali.”
Jioni hiyo hiyo, Kikao cha Ukoo kilikaa na kujadili suala hilo. Kwa sababu Davina
alikuwa na fedha za kutosha, siku iliyofuata asubuhi na mapema shughuli nzima ya
mtambiko ilifanyika. Asubuhi na mapema, Davina alipelekwa mtoni na akina
mama, akaogeshwa mwili mzima kwa maji ya kibuyu ambayo yalichanganywa na
unga wa nafaka za uwele, mtama na mahindi ya njano!
Baada ya zoezi hilo kumalizika, walikwenda kwenye mbuyu mrefu wa maajabu,
ambao siku zote hutumika kwa ajili ya ibada za mizimu. Ng’ombe akachinjwa na
Davina kupakwa damu mwili mzima kisha akavalishwa ngozi kwenye kidole
chake cha mwisho na kiunoni! Wakarudi nyumbani ambapo sherehe ziliendelea
huku ngoma za Kirangi zikipamba shughuli nzima. Watu walicheza, kula na
kunywa kwa furaha hadi asubuhi! Mzee wa Ukoo akamhakikishia tatizo lake
limefika mwisho.
29
“Sasa unaweza kurudi mjini, kuendelea na shughuli zako, hakuna tatizo
litakalokupata tena,” baba yake alimwambia Davina wakati wakimsindiza kwenda
kupanda baiskeli ambayo ingemfikisha Kondoa Mjini ambapo angepanda basi la
kwenda Dodoma na baadaye Dar es Salaam.
“Sawa baba nashukuru sana, sasa nina amani.”
“Mimi nawaacha, mama yako atakupa maagizo mengine!”
“Sawa baba!”
Mzee Ngamseni akaondoka zake, mama yake akaendelea kumsindikiza.
Walipokaribia kufika kwenye kituo cha baiskeli, mama yake akamwambia: “Kuwa
makini mwanangu, lakini kuna masharti mawili makubwa unayotakiwa
kuyazingatia.”
“Yapo hayo mama?”
“Hutakiwi kuvua hiyo pete ya ngozi kidoleni mwako kwa miezi sita. Pili,
huruhusiwi kukutana na mwanaume yeyote kimwili katika kipindi cha miezi
mitatu. Baada ya muda huo kuisha, unaweza kukutana na mwanaume, lakini bila
kuvua ile kamba ya ngozi kiunoni mwako, mpaka miezi mitatu tena baadaye!
Baada ya muda huo kupita, utavua na kuvifunga kwenye kitambaa chekundu na
kwenda kutupa mtoni! Kumbuka siyo baharini wala ziwani, lazima iwe mtoni...”
mama yake akamwambia akiwa amemtulizia macho mwanaye.
“Kifupi natakiwa kuvua pete baada ya miezi mitatu na kamba kiunoni baada ya
miezi sita, pia sitakiwi kukutana na mwanaume mpaka miezi mitatu ipite.
Ukimaanisha kwamba, wakati nakutana na mwanaume huyo lazima niwe na
kamba yangu kiunoni siyo mama?”
“Ndiyo!”
“Unadhani itawezekana?”
“Kwa nini isiwezekane? Nini kinashindikina? Tena unatakiwa kufahamu kwamba
huu ni mkataba wetu na mizimu ambao unatakiwa kuheshimiwa na kulindwa kwa
kila hali, tafadhali sana usitengue sharti hili, kwani kwa kufanya hivyo
utasababisha matatizo makubwa sana, siyo kwako tu, bali kwa ukoo mzima,”
mama yake alitamka maneno hayo kwa kumaanisha alichokisema.
30
“HAIWEZEKANI MAMA, SITAWEZA...”
“Unasemaje?”
“SITAWEZA MAMA!”
Neno ‘haiwezekani mama’ lilikataa kabisa kuingia kichwani mwa mama yake
Davina. Kwa nini isiwezekane? Si ana matatizo? Anasumbuliwa na mzimu wa
mpenzi wake ambaye alikufa muda mrefu uliopita? Tiba ndiyo ameshapatiwa na
alitakiwa kuhakikisha anafuata masharti aliyopewa ili aweze kupona, sasa kwa nini
anasema haiwezekani?
Ni Davina huyu huyu ambaye alikuwa anatofautiana na baba yake kuhusu tatizo
lake, baba yake akiwa haamini mambo ya mizimu na yeye akiamini kwa asilimia
kubwa kwamba mzimu wa Jeff ndiyo ulikuwa unamsumbua. Leo anakataa vipi?
Maswali haya yalizunguka kichwani mwa mwanamke huyu aliyekuwa akimtizama
mwanaye kwa macho ya mshangao wa wazi kabisa.
“Hivi naongea na Davina mwenyewe au na wewe ushakuwa mzimu?” mama yake
akauliza kwa hasira.
“Swali gani hilo mama? Mimi ni Davina...” Davina akasema kwa woga kidogo.
“Haiwezekani Davina mwanangu ninayemjua mimi, aliyekuwa akija akilia
akisema kwamba anatakiwa kufanyiwa mtambiko akatae kufuata taratibu za mila,
hilo haliwezekani kabisa...” mama Davina akasema.
“Mama.”
“Mama nini? Mama kitu gani?”
“Nisikilize kwanza!”
“Kipi cha kukusikiliza, najua ni huo umapepe wako ndiyo unakusumbua, yaani
huwezi kuvumilia kwa miezi mitatu baadaye ukaendelea na mambo yako.
Yatakushinda mtoto wa kike,” mama Davina akazidi kuwa mbogo.
Davina akaa kimya kwa muda, akamtizama mama yake kwa macho ya kuomba
msamaha au kuhitaji huruma ya mama yake.
“Nini?”
31
“Unajua mama sina maana hiyo unayoifikiria wewe, hebu fikiria ni muda gani
tangu Jeff amekufa? Kipindi chote hicho sijawahi kukutana na mwanaume, sina na
wala sina matarajio ya kufanya hivyo, sasa kwa nini niwe na wasiwasi na jambo
hilo?”
“Sasa kumbe nini?”
“Na wala sioni tabu kukaa na hiyo kamba kiunoni hata kwa mwaka mzima, bora
huo mzimu usinisumbue!”
“Sasa kumbe nini?”
“Hii pete mama...nilifikiri ni ya muda mfupi, labda siku mbili au wiki...nitakaa vipi
na hii pete wazi namna hii?”
“Inakuzuia nini?”
“Watu mama. Wengine wanaweza kuhisi mimi mchawi, mshirikina au mwanga!”
“Acha ujinga mwanangu, mkataa asili si jasiri mama. Hizi ni mila zetu na wewe
una matatizo, lazima uvae hiyo pete kwa miezi mitatu mwanangu!”
“Lakini siwezi kutengenezea pete nyingine ya kawaida halafu nikaiweka ndani ya
kidani?”
“Haiwezekani mwanangu, lazima uivae ikiwa halisi, hivyo hivyo bila kubadilisha
kitu chochote.”
Davina alikaa kimya kwa muda.
Hakuutaka mzimu wa Jeff hakika, lakini pia hakupenda kuonekana mchawi wala
mwanga. Afanye nini sasa? Kipi bora? Aonekane mshirikina apone au aonekane si
mshirikina mzimu wa Jeff uendeee kumsumbua? Alitakiwa kuwa na jibu.
“Sawa mama, nitafuata maagizo yote,” Davina alisema akitabasamu.
Mama yake akashangaa sana. Kwa bahati nzuri, baiskeli ikapita.
Wakamsimamisha kijana aliyekuwa akiendesha.
“Wapi dada?”
“Kituoni.”
“Mia tano tu!”
“Usijali nitakupa elfu mbili, unachotakiwa kufanya ni kuniwahisha!”
“Ahsante sana dada yangu, utafurahi mwenyewe.”
“...mama kwaheri,” Davina akamwambia mama yake, baiskeli ikianza kuondoka
taratibu.
“Fika salama mama, nakutakia mafanikio mema mwanangu.”
“Ahsante mama.”
32
Baiskeli ikaondoka, tayari Davina alikuwa na kitu cha kufanya, hakuogopa tena ile
pete, alijua ataifunika na kitambaa muda wote, hapo itakuwa si rahisi watu
kugundua kilichokuwa kikiendelea.
33
SURA YA NNE
34
Kitu pekee ambacho angeweza kufanya kwa wakati huo ilikuwa ni kukutana na
Davina ili amwulize vizuri kuhusu ishu nzima ilivyokuwa!
Mara moja akachukua simu yake na kuanza kutafuta jina la Davina haraka,
alipolipata, akaampigia mara moja. Ni yeye peke yake kwa muda huo ndiyo
angeweza kuwa msaada zaidi.
“Haloo Davina, mambo vipi?”
“Poa.”
“Shwari?”
“Haswaa, vipi mbona kama unahema sana, kuna tatizo?”
“Nahema sana?”
“Ndiyo!”
“Hapana!”
“Lakini mimi ndiyo nakusikia na nahisi kabisa kwamba kuna kitu kinakutatiza, ni
nini?”
“Ondoa hofu Davina, nipo sawa tu, ila nilikuwa nataka kujua kama umesharudi
Dar au bado upo Kondoa.”
“Kwa nini?”
“Nataka kujua.”
“Nimesharudi shemeji yangu, tangu jana nipo hapa mjini!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Mbona hukunijulisha?”
“Kuchanganyikiwa Gerald!”
“Umeshasahau kwamba tulitakiwa kuonana baada ya wewe kurudi Kondoa?”
“Nakumbuka sana!”
“Sasa?”
“Tupange tu...”
“Enheee, unadhani lini inaweza kuwa siku yetu nzuri kuonana?”
“We’ unapenda lini?”
“Hata leo!”
“Leo haiwezekani Gerald, bado nina uchovu mwingi, nahitaji muda wa kupumzika
zaidi.”
“Huwezi kujitahidi jamani?”
“Hapana, huwezi kuamini lakini kwetu ni mbali sana na shughuli yenyewe
iliyofanyika huko si ndogo, nipo hoi Gerald!”
35
“Lakini ingekuwa vizuri zaidi kama tungeonana leo.”
Ilikuwa lazima Gerald azungumze na Davina, alitaka sana kujua nini alichoambiwa
na Jeff kwenye barua. Kwa muda wote huo alikuwa hajapata nafasi ya
kuzungumza naye na kujua ukweli wa tatizo zima, kutokana na barua za Jeff
mwenyewe.
Tayari Gerald alikuwa kama aliyechanganyikiwa, maneno ya Jeff kwenye simu
yalizidi kumfanya ajihisi mkosaji, hilo lisingekuwa tatizo kubwa sana maana
lilikuwa lake na moyo wake, lakini lingeweza kuwa tatizo kubwa kama mtu
mwingine yeyote angejua!
Hakutaka kabisa kuhusishwa na mauaji ya Jeff. Kitu kingine ambacho alikuwa
anakiota kila siku ilikuwa ni kuishi na Davina, alitakiwa kutumia mbinu zote
amuoe.
Kilichomchanganya ni kwamba, ile njia kubwa zaidi na ya mwisho ambayo
aliitumia, ndiyo ambayo ilitaka kuharibika. Kutoa uhai wa mtu kwa sababu ya
penzi halikuwa jambo dogo!
Malipo ambayo yangeweza kutosha kulipia damu ya marehemu Jeff ilikuwa ni
penzi la Davina pekee, hapakuwa na kitu kingine tena.
Kikapita kimya cha muda mrefu kwenye simu bila mtu yeyote kuzungumza kitu.
Baadaye sauti ya Davina ikasikika.
“Gerald...”
“Yes Davina!”
“Naweza kukuuliza swali moja?”
“Hata kumi nipo tayari!”
“Ok! Lakini mi’ nina moja tu!”
“Uliza.”
“Mbona una haraka sana ya kuonana na mimi?”
“Lakini ulisema Jeff anakusumbua na mimi ni rafiki yake...shemeji yako...ni
vyema tuonane leo.”
“Ni hilo tu?”
“Lingine lipi sasa?”
“Ok! Wapi?”
“Rose Garden!”
“Saa ngapi?”
“Saa 3:00 usiku.”
“Poa.”
36
“Haya usikose tafadhali.”
“Lakini kwa nini unakazania sana Gerald? Unanifanya niogope sasa.”
“Nini kinakuogopesha? Nafikiri tukutane tuzungumze.”
“Poa, saa 3:00.”
“Haya shem,” Davina akajibu kwa upole sana, akionekana kuwa na mawazo tele
juu ya kukutana kwao jioni hiyo.
Hakujua Gerald alikuwa na nini hasa cha kukazania kiasi kile, maana kama ni
matatizo yalikuwa yake, kwa nini yeye anakuwa ndiyo anakazania zaidi?
Davina hakuwa na jibu, akabaki na mawazo tele kichwani.
Namna ambavyo Davina alikuwa anauliza maswali ilimfanya Gerald aingiwe na
wasiwasi tele moyoni mwake. Taa nyekundu ikaanza kuwaka ubongoni mwa
Gerald, alishaanza kuhisi kuwa Davina alishagudua kila kitu.
Alishajua kwamba yeye ndiye muuaji. Hii ilikuwa siri kubwa sana, siri ambayo
hakutaka ijulikane, hasa na Davina.
Ni kweli aliua!
Ni kweli alitaka kumuoa Davina!
Ni kweli Jeff alikuwa anamsumbua kwa kumwandikia barua na siku hiyo alimpigia
simu jioni akitokea kazini.
Kila kitu kilikuwa cha ukweli, lakini bado alitakiwa kufanya siri kubwa. Kwake
yeye kukutana na Davina, kulikuwa mwanzo wa mwanga mpya katika utatuzi wa
tatizo hilo.
Hata hivyo, mwisho wa yote alipanga kumuoa Davina, hakuwa na kitu kingine
zaidi. Hiyo ndiyo siri ya mauaji ya Jeff. Marehemu ambaye haeleweki. Marehemu
anayeadika barua!
Maajabu!
***
Saa 2:30 usiku, Gerald alikuwa ameshafika Rose Garden, alikuwa akimsubiri
Davina kwa hamu kubwa! Muda ukazidi kwenda, saa tatu na nusu akaamua
kumpigia, akamjulisha kuwa yupo njiani anaelekea hapo.
Akavuta subira, lakini hadi saa nne na robo, bado alikuwa hajafika. Akaamua
kumpigia tena simu.
Hakupatikana!
Gerald akachanganyikiwa!
Mawazo tele kichwani!
37
Kama kungekuwa na neno lingine ambalo lingeweza kutumika kuonesha kwamba
Gerald alikuwa amechanganyikiwa, hapa lingefaa hakika! Alikuwa
amechanganyikiwa hadi kufikia kiwango cha mwisho na sasa alitakiwa kupata jina
lingine jipya kabisa ambalo lingesherehesha maana ya yeye kuchanganyikiwa.
Kuna wakati alianza kuhisi kwamba, labda mtandao ulikuwa unasumbua, hivyo
akaamua kupiga kwa mara nyingine...jibu lilikuwa lile lile!
Simu haikupatikana!
Kichwa kikazidi kumuuma, alama za hatari zikaanza kusoma mbele yake, moja
kwa moja alihisi kutokea tatizo kubwa sana mbele yake. Kwa nini amwambie yupo
njiani halafu asipatikane? Kuna nini? Gerald aliwaza sana bila kupata jibu
yakinifu!
Maswali magumu!
“Nini kinaendelea hapa? Kwa nini anaonekana kusita kuonana na mimi? Au tayari
ameshajua kinachoendelea? Hapa natakiwa kuwa makini sana vinginevyo naweza
kuingia kwenye matatizo makubwa ambayo yataniumiza baadaye...natakiwa kuwa
na akili za kutosha katika hili.
“Yapo mambo ambayo naweza kuyachukulia kwa wepesi lakini si hili...naona
kabisa tatizo kubwa lililopo mbele yangu na kwa hakika sitaruhusu matatizo mbele
yangu, lazima nifanye jambo fulani hapa,” ubongo wa Gerald ulipata kazi mpya ya
kuhifadhi maneno hayo makali.
Kuna kitu kilizunguka akilini mwake, kwamba yawezekana kabisa, Davina
alivyokuwa kijijini kwako Kondoa, aliambiwa kila kitu na wazee baada ya
kufanyiwa mtambiko na yawezekana kabisa kulikuwa na mpango wa kummaliza.
Hilo lilichukua nafasi kubwa sana kichwani mwake.
“Kipo kitu kipo...lakini mimi ndiyo Gerald bwana, najiamini siku zote. Isitoshe
hata mara moja sijawahi kushindwa na hata hili haliwezi kunishinda,” Gerald
akawaza akiinuka kwa ajili ya kuondoka.
Akapiga hatua za haraka na kwenda kwenye gari lake, akiwa ndiyo kwanza
anaingiza funguo kwa ajili ya kufungua mlango, akashtuliwa na mtu aliyemgusa
begani. Akashtuka sana na kugeuka kwa shauku akiamini labda alikuwa ni Davina.
Akageuka kwa hadhari!
Hakuwa Davina!
Alikuwa mhudumu!
“We’ sister vipi? Hujui wengine tunakuwa na mawazo yetu kichwani...haya sema
kwa nini umenigusa?”
38
“Samahani kaka!”
“Sema shida yako!”
“Ulisahau kulipa,” yule dada akamwambia kwa sauti ya upole akimkabidhi
karatasi iliyokuwa na bili yake.
Gerald akapokea!
“Samahani dada’ngu, nilipitiwa...samahani pia kwa kukufokea, kuna mtu
ananichanganya sana akili yangu,” Gerald akasema akitoa pesa kwenye pochi yake
na kumkabidhi yule dada.
“Ahsante usijali.”
Yule dada akaondoka, Gerald akafunga mlango na kuwasha gari, ile anaanza
kuondoka tu, akaona gari la Davina likiingia getini. Akazima na kushuka. Akaenda
kumpokea.
“Kumbe na wewe ndiyo unafika shem?” Davina akamwambia Gerald akitabasamu.
“Siyo nafika, ndio nilikuwa naondoka zangu.”
“Samahani kwa kuchelewa, lakini pia nilifanya jambo moja la kijinga sana, sikujua
kama naondoka na simu isiyo na chaji, kwahiyo ikazimika ghalfa nikiwa Ilala kwa
Salama, najua ulihisi nimekuzimia, lakini siyo...naomba msamaha shem,” Davina
alisema akiwa ameganda kwenye mlango wa gari lake.
“Umeshasamehewa, usijali Davina.”
Pamoja na kwamba, Gerald alikuwa na mawazo mengi sana juu ya Davina, lakini
alijishangaa akitumia muda mwingi kuutafakari uzuri wa Davina. Alivutiwa mno
na mpangilio wa nguo zake jioni hiyo.
“Umependeza sana Davina, hongera...”
“Ahsante sana, hata wewe pia.”
“Nashukuru.”
Wakaingia ndani na kuketi sehemu tulivu sana.
“Pole na safari, wazee wazima?”
“Wa afya.”
“Enhee, hebu niambie vizuri, ishu iko vipi?”
“Ah! Shemeji yangu, ni maajabu sana na nakosa pa kuanzia, lakini kama
nilivyokuambia awali, marehemu Jeff ananiandikia barua,” Davina alizungumza
kwa sauti ya taratibu sana akiwa ameyatuliza macho yake usoni mwa Gerald.
Gerald alikuwa kimya akiendelea kumsikiliza kwa makini sana, masikio yake
yalikuwa tayari kumeza chochote kutoka kinywani mwa Davina.
39
“Mbaya zaidi, sasa ameanza kunipigia simu, lakini cha ajabu sasa, anatumia
private number!” Davina akazidi kusimulia.
“Huwa anasemaje zaidi?”
“Analalamika kuna mtu amemuua ili anioe!”
Gerald akayatoa macho.
“Amekutajia?” akauliza akionesha woga wa wazi kabisa.
“Vipi mbona umeshtuka hivyo?”
“Hapana, hizi ni habari za kutisha shemeji yangu, wewe mwenyewe unajua wazi
kwamba Jeff alikufa na tulimzika, unadhani siwezi kushangazwa na habari kama
hizi jamani?”
“Nashindwa kuelewa kabisa, halafu anajua mambo yangu mengi sana, hata nikiwa
nasafiri yeye anajua na hunipigia simu. Ni mambo yanayonichanganya sana,”
Davina akasema kwa utulivu sana.
Bado moyo wa Gerald haukuwa umetulia, hakutaka kumuamini Davina moja kwa
moja, kichwani mwake alikuwa akiamini kuwa, Davina aliambiwa kila kitu na Jeff
na alikuwa anamficha tu! Hakutaka kumweleza ukweli wa kinachoendelea,
hakumwambia kama naye aliandikiwa barua pamoja na kupigiwa simu na Jeff,
hiyo ilikuwa siri yake ya moyoni mwake. Alijitahidi sana kuuficha uoga wake kwa
mafanikio makubwa.
“Lakini shem, katika hali ya kawaida, umewahi kusikia mtu aliyekufa akafanya
mawasiliano na aliye hai?”
“Hapana.”
“Sasa mbona unakuwa na imani haba? Kwa nini unaamini kuwa ni yeye?”
“Hata kama ni wewe lazima ungeshtuka. Hivi unadhani ni rahisi kukubali kwamba
marehemu anaweza kuandika barua? Apige na simu? Tena akitoa maneno ya
ukali?
“Anasema atakuja kunichukua anipeleke kuzimu nikaishi naye huko hilo
linawezekana kweli? Fikiria Gerald...hili ni tatizo kubwa?”
“Nini kimefanyika kijijini?”
“Zaidi ya mtambiko ni nini tena?”
“Baada ya huo mtambiko amewasiliana na wewe tena?”
“Hapana...naona hali imetulia, wazee wamenihakikishia, ingawa wamenipa
masharti ya kufuata.”
“Duh! Pole sana Shem, lakini naamini haya mambo yataisha usijali...” Gerald
akasema.
40
Hakuthubutu kufungua mdomo wake kueleza kwamba na yeye alikuwa akitumiwa
ujumbe pamoja na kupigiwa simu na Jeff, hiyo ilibaki kuwa siri ya moyo wake.
Walizungumza mpaka saa sita za usiku, wakaondoka na kwenda majumbani
mwao.
41
SURA YA TANO
Davina aliyatoa macho yake akiwa haamini kabisa anachosoma katika barua ile,
ilikuwa barua yenye maneno mazito kuliko kawada! Kwanza alichanganyikiwa na
jinsi barua yenyewe ilivyoingia, maana mwanzoni alikuwa akifikiria labda kuna
mtu aliyekuwa akihusika na kupokea zile barua kisha kuziweka kwenye sanduku
lake, lakini sasa ni tofauti kabisa!
Barua zilikuwa zinapitia ofisini kwa Meneja Mkuu mwenyewe, sasa iweje mtu
huyo aingie mpaka ofisini kwa bosi wake? Jambo hilo lilimchanganya sana kichwa
chake. Akarudia kuisoma tena ile barua kwa mara ya tatu mfululizo. Alikuwa
akisoma maneno yale yale!
42
‘Hii ni barua yangu ya mwisho kwako, najua upo Kondoa, ukirudi utaikuta! Sijui
ni kwa nini unajisumbua kiasi hiki? Unadhani ukikataza barua zako kupitia
kwenye sanduku lako nitashindwa kukutumia? Utaratibu ninaotumia ni ule ule wa
kawaida, kwahiyo utaikuta barua yako ofisini kwa Meneja Mkuu.
Nimeshazungumza na wewe mpaka nimechoka, napenda kukuambia kwamba,
sitarudia tena maneno haya, kamwe sitajisumbua tena kukupa angalizo. Endelea na
maisha yako, lakini fahamu kwamba nilikupenda sana, nakupenda na bado
hujaondoka moyoni mwangu, utaendelea kuwa wangu siku zote.
Kila unachokifanya, tambua kwamba nakupenda sana, fahamu yupo ambaye moyo
wake unatetemeka kwa ajili yako, yupo anayejua thamani ya pendo lako. Yupo
ambaye alia kwa ajili ya penzi lako. Huyo ni mimi, mwanaume ambaye
niliukabidhi moyo wangu kwako.
Jeff Sebastian.
Kilio cha Davina kilikuwa na sababu mbili, hakulia kwa sababu ya maajabu ya
barua yenyewe tu, sasa machozi yake yalisababishwa na ukali wa maneno
yaliyokuwemo kwenye barua ile, yalikuwa maneno makali yanayochoma kuliko
kawaida. Hata yeye alikiri wazi kwamba alikuwa anampenda sana Jeff, tena kwa
moyo wake wote, lakini hakuwa na haja ya kuumia sana kwa sababu tayari
alikuwa marehemu!
Alishalia mpaka machozi yakakauka, hakuwa na haja ya kujiongezea simanzi ya
moyo wake sana, alichotakiwa kufanya kwa wakati huo ni kutulia na kukubaliana
na hali halisi ilivyokuwa. Kwamba Jeff mwanaume wa maisha yake, hakuwepo
tena duniani!
Akayatoa macho yake akimuelekezea Meneja Mkuu.
“Vipi dada’ngu?”
“Acha tu!”
“Kuna nini?”
“Niache tafadhali!”
“Lakini ni vizuri kama utanijulisha chochote ili nijue jinsi ya kusaidiana na wewe.”
“Niachie mimi...acha tu...ahsante sana...” Davina alitamka maneno hayo huku
akiinuka kitini.
“Sasa barua ziendelee kupitia kwenye sanduku lako la kawaida?”
“Vyovyote mtakavyoona!” Davina alijibu kwa hasira huku akibamiza kwa nguvu
mlango wa ofisi ya Meneja Mkuu.
43
***
“Nimekuta tena barua ya Jeff!”
“Umekuta?”
“Ndiyo!”
“Inasemaje?”
“Kama alivyoniambia kwenye simu, anasema hatanifuatilia tena.”
“Mh! Hii hatari sasa!”
“Mbaya zaidi, barua zenyewe sasa hivi zinapitia ofisini kwa Meneja Mkuu, yaani
nimechanganyikiwa si kidogo, akili yangu haifanyi kazi kabisa, najihisi kama
nikitue hivi, maana naona kimezidi uzito!”
“Usiseme hivyo shem, haya mambo yataisha tu!”
“Yataisha vipi wakati ndiyo kwanza yanaanza?”
“Lakini hakuna lenye mwanzo linalokosa mwisho.”
“Ila hili langu, naona kama halina mwisho.”
“Upo wapi?”
“Mjini, natokea Posta.”
“Jioni naweza kukutana na wewe?”
“Tena?”
“Kwani kuna ubaya?”
“Hapana, lakini unanitisha, nahisi kama una kitu kipya!”
“Sina kitu kipya kwa kweli, lakini nafikiri huu ni wakati wa kuwa karibu zaidi na
wewe shemeji yangu!”
“Ok! Kama umeona hivyo sawa.”
Haya yalikuwa mazungumzo kati ya Davina na Gerald, muda mfupi baada ya
Davina kutoka ofisini kwa Meneja Mkuu wa Posta.
“Wapi sasa?”
“Maeneo ya Sinza!”
“Ipi?”
“Tukutane Mori, muda ukifika nitakujulisha!”
“Sawa, utanijulisha, lakini natakiwa kujua ni muda gani?”
“Kuanzia saa tatu....”
“Mh! Unaposema kuanzia saa tatu, maana yake ni hadi usiku sana, au nimeelewa
vibaya?”
“Umeelewa vibaya, siyo usiku sana, ni mazungumzo ya saa moja tu, nataka tupate
chakula cha usiku pamoja!”
44
“Sawa shemeji yangu!”
“Ok!”
***
Tofauti na matarajio yake, saa 3:00 Davina alikuwa ameshafika Sinza, Mori
kituoni na alikuwa akimsubiria Gerald, alipoona kimya cha muda mrefu baada ya
kusubiri robo saa nzima, akaamua kumpigia.
“Uko wapi?” Davina akauliza.
“Kwani we’ uko wapi?”
“Nimeshafika.”
“Oh! Samahani sana, mimi ndiyo nakatisha hapa kwenye mataa ya Bamaga, dakika
tatu tu nitakuwa hapo.”
“Poa.”
Kweli baada ya muda huo, Gerald alikuwa ameshafika Mori, akampigia Davina na
kumwambia amfuate kwa nyuma, wakaongozana hadi Kwa-Remmy, Gerald
akaegesha kushoto, Davina naye akafanya hivyo, wakaingia ndani ya Mgahawa wa
City Garden. Muda mfupi baada ya kukaa kwenye viti, mhudumu akafika na
kuwasikiliza.
Vyakula vikaletwa, wakaanza kula huku wakizungumza mambo mbalimbali ya
kimaisha. Hawakukaa sana, wakaagana.
Mazoea ya Gerald wa Davina yakazidi, kila wakati alipenda kumpa ofa, alimtumia
meseji mbalimbali zenye tungo nzuri, akimsogeza zaidi karibu yake. Baada ya
miezi mitatu wakawa marafiki wakubwa. Sasa walikuwa zaidi ya mtu na shemeji
yake, walifanya kila kitu isipokuwa ngono, mpaka wao ulikuwa ni ngono tu!
Waliamua kuwa marafiki wa kawaida, huku Gerald akisisitiza kwamba
analazimika kufanya hivyo kwa sababu hana mchumba na pia kwa ajili ya
kumuondolea upweke moyoni mwake baada ya kuondokewa na rafiki yake
mpenzi, Jeff. Davina alilipokea hilo kwa mikono miwili. Kila wikiendi wakawa
wanakwenda disko au kwenye maonesho ya bendi mbalimbali, wakati mwingine
walikwenda ufukweni na kuogelea pamoja!
Mzigo mzito ukazidi kumuelemea Gerald moyoni mwake, wikiendi moja wakiwa
ufukweni akaamua kuutua! Hakuona sababu ya kuendelea kuumia wakati mtu wa
kumweleza hisia zake alikuwa naye. Akapanga maneno ya kumwambia
yakapangika.
45
“Davina, naomba unisikilize, nina mambo ya muhimu sana nataka kuzungumza na
wewe leo...” Gerald akamwambia Davina huku akimpapasa tumbo lake, ufukweni
mwa Bahari ya Hindi eneo la Coco.
“Nakusikiliza Gerald, niambie tu!”
“Hivi umeshawahi kuona mtu mzima akilia?”
“Ndiyo kwenye msiba!”
“Bila msiba, hujamuona mtu mzima akilia?”
“Kwa kweli sijaona!”
“Utajisikiaje kama utamuona mtu mzima akilia kwa sababu yako?”
“Nitajisikia vibaya sana....kwanza sitamani kumliza mtu mzima hata siku moja!”
“Lakini yupo ambaye analia kwa ajili yako!”
“Nani?” Davina akauliza akiyatoa macho yake.
“Mimi Davina...nimekuwa nikilia kwa muda mrefu sana kwa ajili yako, naomba
sasa uyafute machozi yangu! Nibembeleze sasa Davina...sikiliza Davina,
nakupenda sana, nahitaji uwe mpenzi wangu, mke wangu wa baadaye, mama wa
watoto wangu!” Gerald alikuwa akizungumza kwa sauti ya kusihi sana huku
macho yake yakidondosha machozi.
Davina alikuwa ameyatoa macho yake kwa mshangao, hakuamini kama maneno
yale yalikuwa yanatoka kinywani mwa Gerald. Ghafla akajiondoa mikononi
mwake na kumsukuma Gerald pembeni...
“Noooooooo Gerald, noooooooo....” Davina akapiga kelele huku akikimbia.
Gerald akasimama na kumkimbiza!
Davina alikuwa kama aliyechanganyikiwa, kwa Gerald ilikuwa ni pigo na hakuwa
tayari kumpoteza Davina. Akaanza kumkimbiza kwa kasi ufukweni, watu
waliowaona walibaki wanacheka.
Hakufika mbali sana, Gerald alikuwa ameshamshika, akamwangusha chini na
kumlalia! Akambana kwenye mchanga asifurukute.
“Davina kwa nini unafanya hivi?”
“Nimefanya nini?”
“Huoni ulichofanya? Unadhani watu watatufikiriaje?”
“Sikutegemea kama ungeniambia maneno hayo, hivi kumbe ukaribu wetu maana
yake ilikuwa ndiyo hiyo?”
“Siyo hivyo Davina, lakini unatakiwa kukumbuka kwamba mapenzi ni hisia na si
mimi mwenye matakwa ya kukupenda bali hisia kali zilizopo katikati ya moyo
wangu. Tafadhali zipokee mpenzi wangu, nakupenda sana Davina.”
46
“Kwahiyo ulifurahia kifo cha Jeff siyo?”
“Hapana.”
“Sasa kwa nini unanitaka?”
“Ndiyo maana nimekuambia mapenzi!”
“Sasa unawezaje kutembea na mpenzi wa rafiki yako?”
“Nisingeweza kufanya hivyo akiwa hai, lakini amekufa, tena nahisi nitakuwa
namuenzi vizuri rafiki yangu Jeff!”
“Hayo ni mawazo potofu!”
“Si potofu, nakupenda kweli Davina tafadhali naomba uruhusu moyo wangu uingie
kwako, usiniache niteseke...” Gerald alizidi kumshawishi Davina ambaye hakuwa
na dalili hata moja ya kukubali ombi lake.
“Ok! Nipe muda kwanza,” Davina akajibu kwa kifupi baada ya kuona Gerald
anazidi kumsumbua.
Alifanya hivyo kwa nia ya kujinasua kwake kwa muda ule. Gerald akakubaliana na
Davina, akamwachia! Hawakuchukua muda mrefu sana wakaamua kuondoka.
Siku hiyo Davina hakutumia gari lake, hivyo Gerald alilazimika kumpeleka
kwanza Davina nyumbani kwake kisha naye akarudi nyumbani kwake. Kichwani
mwake alikuwa na wazo moja tu, alitakiwa kumpata Davina.
***
Kitanda hakikuwa na raha kwa Gerald, akili yake ilikuwa kwa mrembo Davina,
alitakiwa kutumia akili yake yote kuhakikisha anamweka mikononi mwake, kosa
ambalo hakutakiwa kulifanya ni kuhakikisha kwamba Davina hafahamu na wala
asihisi kama Gerald alikuwa anahusika na kifo cha Jeff kwa namna yoyote ile.
Picha nzima ya Davina ilimtokea akiwa pale kitandani. Akahisi moyo wake
ukienda kasi kuliko kawaida. Usingizi ukamruka kabisa, kitu pekee ambacho
kingeweza kumsaidia akapata usingizi ilikuwa ni kusikia sauti ya Davina. Haraka
akachukua simu yake na kubonyeza namba za Davina.
Punde, simu ikaanza kuita na kitambo kidogo Davina akapokea...
“Vipi mama?”
“Shwari, mbona usiku sana?”
“Nimeshindwa kulala kabisa!”
“Kwa nini?”
“Baby, picha yako inanisumbua kichwani mwangu!”
47
“Unaanisha nini kusema hivyo?”
“Nakupenda sana mpenzi, tafadhali nipe nafasi katika moyo wako!”
“Tena umenikumbusha, mchana nilikuahidi kwamba nitakujibu baada ya kufikiria,
haikuwa hivyo!”
“Khaaa! Kwahiyo ulikuwa na maana gani?”
“Sitaki kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wewe, kama unaona huwezi kuwa
rafiki yangu wa kawaida basi!” Davina alisema maneno hayo kwa hasira kisha
akazima simu.
Gerald akabaki ameduwaa.
Uhusiano wao ukazidi kupamba moto, lakini wakati huo walikuwa kama marafiki
na siyo wapenzi na wala Gerald hakumsumbua tena. Hiyo ndiyo hali halisi
ilivyoonekana kwa nje, lakini ndani ya moyo wa Gerald bado kulikuwa na makovu
makali sana ya mapenzi juu yake.
Wakawa wanatoka kama ilivyokuwa zamani, kila mwisho wa wiki wakawa
wanapunga upepo ufukweni pamoja. Baada ya miezi miwili, tayari Davina alikuwa
ameshaamini kwamba Gerald hawezi kumtongoza tena.
Wikiendi moja, Gerald aliamua kwenda na Davina Morogoro, wakaponda raha
kuanzia Ijumaa jioni hadi Jumapili jioni walipoamua kurudi Dar. Kila kitu
walifanya pamoja kama marafiki, lakini hapakuwa na suala la mapenzi, hata
chumba kila mtu alikuwa na chake!
48
Wakiwa njiani wanarudi, mbele kidogo ya Chalinze, Gerald alikuwa anakimbiza
gari kuliko kawaida, mara nyingi Davina alikuwa anamzuia kukimbiza gari, lakini
hakuelewa.
Kwa mbali kidogo kulikuwa na gari kubwa la mizigo lililokuwa linakimbia kwa
kasi kuliko kawaida. Gerald naye akazidi kukimbiza gari.
“Lakini kwa nini leo unaendesha gari kwa fujo hivi?”
“Nina maana yangu!”
“Maana gani?”
“Nataka tufe!”
“Tufe? Hivi una kichaa Gerald?”
“Bora nife na kichaa changu, kuliko kuendelea kuishi nikiwa mzima huku penzi
langu likiwa halithamiwi!”
“Una maana gani?”
“Wewe si hunipendi? Sasa wote tunakufa, kwa taarifa yako, nalipeleka gari usawa
wa lile lori linalokuja, bora tufe pamoja kuliko kuendelea kunitesa!”
“Usifanye hivyo Gerald!”
“Kwahiyo unanipenda?”
“Unasema...”
“Jibu haraka, napeleka gari!”
Gari lilikuwa katika mwendo mkali sana na Gerald alikuwa akimaanisha kabisa
alichokisema, ghafla Gerald akahama njia, akapeleka gari upande wa kulia kwa nia
ya kugongana na lile gari, taa za gari lake zikiwa zimewashwa mwanga mkali!
“Gerald achaaaaaaaa.....”
“Bora tufe...” Gerald alisema huku akikanyaga mafuta sawasawa.
Wakati huo lile lori nalo likaanza kuyumba na kupoteza mwelekeo. Davina akazidi
kupiga kelele kwa hofu ya kifo kilichokuwa mbele yake!
Dereva wa lori akaanza kuyumba akishindwa kuelewa nia ya dereva aliyehamia
upande wake akiendesha kwa kasi ile. Taratibu akaanza kupuguza mwendo, lakini
Gerald aliendelea kukanyaga mafuta. Alipojaribu kurudi upande wa Gerald akaona
gari kubwa likija upande wake!
Akili yake ikafanya kazi haraka sana, asingeweza kugongana uso kwa uso na gari
kubwa kiasi kile, lakini pia hakuwa tayari kuingiza gari mtaroni, akaona bora
avaane na gari ndogo ambalo kwanza asingeumia sana, lakini pia asingekuwa na
kosa!
Akawa tayari kuvaana!
49
Hatua kama nne tu kabla ya magari kukutana uso kwa uso, Davina akashika
usukanu na kukata kushoto akitetemeka, kisha akaliweka gari sawa. Gerald
akachukia sana!
“Unataka kufanya nini?”
“Unanipenda hunipendi?”
“Acha ujinga Gerald, bado nauhitaji sana uhai wangu, tafadhali acha kufanya
hivyo!”
“Achia usukanu!”
“Na wewe endesha gari vizuri!”
“Sema kwanza kama unanipenda!”
“Sikiliza Gerald, kwa sasa tupo kwenye matatizo, yule jamaa anaweza akageuza na
kutufuata kwahiyo kimbiza gari, tuepukane na hili tatizo kwanza...” Davina
akamwambia Gerald ambaye alitii.
Gari likaondolewa kwa kasi ya ajabu, Gerald alipoanglia kupitia vioo vya pembeni,
akaona lile lori limeegeshwa pembeni, akahisi kwa vyovyote vile, inawezekana
akawa anamfukuza na gari lingine.
Akaamua kukanyaga mafuta zaidi. Kasi aliyokuwa nayo ni kama alikuwa ameiba
gari, mara kadhaa alikosakosa ajali barabarani, lakini alifanikiwa kufika hadi
Kimara salama, hapo akagundua kitu fulani, barabara kubwa ilikuwa hatari sana
kwake, hivyo akakata kulia na kuingia kwenye barabara ya vumbi iliyoelekea
Bonyokwa!
Alikuwa mtalaamu sana wa njia za panya, kwahiyo aliweza kupenyeza hadi
akatokea Makoka na baadaye Tabata kisha akapita Buguruni akanyoosha moja
kwa moja kama anakwenda Kariakoo, alipofika Boma, karibu na Ofisi za Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwenye mataa akakata kushoto kuifuata Barabara ya
Kawawa.
Hapo kidogo roho yake ikawa imetulia, mpaka muda huo hakuna hata mmoja kati
yao, aliyemzungumzisha mwenzake, wote walikuwa kimya. Dakika chache
baadaye, Gerald alikuwa anaegesha gari nje ya Hoteli ya Mamba, Kinondoni,
Studio.
“Shuka,” akamuamuru Davina.
“Tunaenda wapi?”
“Nimesema shuka!”
“Mh! Haya, isiwe tabu...” Davina akasema akishuka kwa unyonge.
50
Gerald akamwonyesha ishara kwamba amfuate nyuma, Davina akafanya hivyo.
Wakaingia ndani na kuketi kwenye meza moja iliyokuwa kwenye kona.
Hakuna aliyeongea!
Wakabaki wanaangaliana.
Mhudumu akawafikia, kila mmoja akaagiza anachokitaka. Macho ya Gerald
yalionesha wazi jinsi alivyokuwa amedhamiria kufa kama angemkosa Davina.
Mara moja Davina akagundua jambo fulani, alijua kwa vyovyote vile, kama
angekataa kuwa naye, kungetokea tatizo kubwa, hasa kifo!
Yeye aue?
Hapana...hakuwa tayari kabisa kwa hilo. Davina akawa wa kwanza kuzungumza.
“Gerald kwanini ulitaka kuniua?”
“Nilitaka kukua au wewe ndiyo unataka kuniua?”
“Kukua? Kivipi?”
“Hivi unashindwa kujua thamani ya maisha yangu kweli? Huoni umuhimu wa
mimi kukupenda siyo? Kwanini unanitesa kiasi hiki, kwanini? Ni kitu gani sina ili
niwe nacho unipende?”
“Siwezi Gerald, sitaweza!”
“Huwezi kunipenda siyo, basi sioni kama kuna haja ya kuendelea kuishi, lazima
nife, tena usiku wa leo,” Gerald hakuwa na masihara kabisa katika hilo.
Alama ya machozi machoni mwake, ilitosha kabisa kuonesha kilichokuwa moyoni
mwake, Davina akatulia kwa muda, akamwangalia Gerald kwa huruma, kisha
akamwambia...
“Basi mpenzi, huna haja ya kufa...acha nikupe moyo wangu, lakini nahitaji penzi la
kweli na siyo la kitapeli.”
“Unasema kweli?” Gerald akapiga kelele.
“Kweli kabisa, acha nikupe maisha yangu!”
“Ahsante mpenzi wangu!”
Hadithi zilizofuata baada ya hapo zilikuwa juu ya ndoto ya maisha yao yajayo, kila
mmoja akiwa na shauku ya kuwa na familia bora, maisha mazuri na kila kilicho
bora. Gerald ndiyo alionekana kuwa na furaha zaidi ya mwenzake, aliwaza ndoa
tu!
“Tena inabidi tufunge ndoa mapema sana.”
“Haraka ya nini mpenzi wangu?”
“Sasa kumbe tunasubiri nini?”
“Sawa!”
51
Baadaye, Gerald akamrudisha Davina nyumbani kwake, mvua ya mabusu
akammiminia, wakaagana kwa ahadi ya kukutana tena kesho yake.
“Nakupenda sana Davina, sasa moyo wangu utatulia.”
“Karibu moyoni mwangu, uwe mwenyeji wa kudumu sasa.”
“Nimefurahi sana, ahsante.”
Gerald akaondoka zake.
52
SURA YA SITA
USIKU ulikuwa mzito sana kwa Davina, alitumia muda mwingi sana kufikiria
uamuzi wake wa kuwa na Gerald, aliona kama anamsaliti Jeff wake waziwazi.
Lakini pia, barua ya Jeff ikimwambia kwamba yupo mtu wake wa karibu ambaye
alimuua ili aweze kuwa naye, ikarudi akilini mwake upya kabisa.
“Au yawezekana Gerald ndiyo alimuua nini?” likaja wazo hilo na kuondoka haraka
sana.
Pamoja na hayo, wazo la kuolewa na Gerald lilikuwa linakataa kabisa kukubali
kutulia akilini mwake. Baadaye akakata shauri...hakuwa tayari kuolewa na Gerald.
Akachukua simu yake na kuandika ujumbe mfupi haraka, kisha akautuma kwenda
kwa Gerald.
Ulikuwa ujumbe mbaya sana. Ulisomeka hivi: “Nimefikiria kwa makini sana juu
ya uamuzi wangu, lakini nimegundua nitakuwa nakosea sana. Samahani kwa hili
Gerald, lakini ukweli ni kwamba, siwezi kuolewa na wewe tena.”
Dakika moja haikupita, tayari simu yake ilikuwa imeshaingiza ujumbe mfupi.
Alipofungua, akagundua kuwa, ulitoka kwa Gerald. Huku akitetemeka, akaanza
kuusoma....
“Pengine hujui thamani ya mapenzi, hujui jinsi ninavyoumia kwa ajili yako,
hufahamu ninavyotesekea penzi lako. Nashukuru kwa uamuzi wako wa kuniua,
endelea kuishi kwa amani, kesho ufurahie kifo changu.
“Ninajiua, lakini kabla sijafanya hivyo, nitaacha ujumbe utakaoeleza sababu za
mimi kujiua. Nashukuru sana Davina, NAKUFA NIKIWA NA MZIGO WA
MAPENZI YAKO MOYONI MWANGU, nitakupenda milele. Buriani.”
Davina alirudia kusoma ule ujumbe kwa zaidi ya mara tatu, lakini maneno
yalikuwa yale yale!
Alihisi kuchanganyikiwa!
Alihisi macho yake yalikuwa hayaoni vizuri, lakini hata alipoyapekecha, bado
meseji ile ilibaki kuwa na maneno yale yale. Davina alihisi tatizo, tena tatizo
kubwa sana na papo hapo, mapigo ya moyo wake yakabadilisha kasi na kwenda
mbio sana.
Akayafumba macho yake kwa muda, akauacha ubongo wake upate nafasi ya
kuchambua mambo peke yake, baadaye akagundua jambo jipya akilini mwake;
53
Alianza kuhisi kumpenda Gerald na kwa hakika hakuwa tayari kabisa kumpoteza
mwanaume ambaye alionesha wazi kuwa na penzi la dhati kwake.
“Hata kama alikuwa rafiki wa marehemu Jeff, tayari Jeff mwenyewe ameshakufa,
sidhani kama kutakuwa na tatizo na hata huyo Jeff mwenyewe huko alipo atakuwa
anafahamu wazi kwamba mimi sijamsaliti kwa makusudi, maana hayupo tena
katika ulimwengu unaoonekana!
“Sina ujanja, inabidi nikubali kuwa na Gerald, inabidi iwe hivyo maana kwakweli
mapenzi yamenielemea sana. Sina jinsi...” aliwaza Davina aliyekuwa ameketi
kwenye sofa kubwa macho yake yakiwa yametulia juu ya kioo cha simu.
Wazo lililokuja kwa haraka ilikuwa ni kumpigia simu Gerald na kumwambia
kwamba, hana haja ya kufa tena, maana alikuwa tayari kuolewa naye. Lilikuwa
zoezi la haraka kuliko kawaida. Akapiga namba za Gerald haraka sana, majibu
aliyopewa yalimtibua!
“...hakikisha namba unayopiga na upige tena...” ndiyo sauti iliyosikika kupitia
kwenye spika ya simu yake.
Haikuwa rahisi kuamini, namba alizopiga zilikuwa ni zile zile, sasa kwa nini
apewe jibu lile? Akarudia tena kupiga zile namba. Majibu yakawa tofauti...
“...namba unayopiga kwa sasa inatumika, jaribu tena baadaye...” hapa kidogo
akapata faraja.
Akasubiri baada ya muda kisha akapiga tena, majibu yalikuwa yale yale. Zikapita
dakika kumi nzima akijaribu kupiga na majibu yakabaki kuwa yale yale.
Akachanganyikiwa. Baadaye kidogo alipopiga, alijibiwa jibu lililomkosesha amani
ya moyo wake kabisa...
“...namba unayopiga kwa sasa haipatikani, jaribu tena baadaye!”
Alirudia zaidi ya mara kumi, lakini simu haikupatikana! Akili yake ikafanya kazi
kama umeme, ilikuwa lazima afanye jambo fulani ili kuhakikisha Gerald hapatwi
na jambo baya.
Kichwani alikuwa na vitu viwili kwa wakati mmoja; Kwanza alikuwa na mzigo
mkubwa sana wa mapenzi kwa Gerald, mapenzi ambayo yalifumuka ghafla sana,
lakini pia alikuwa anaogopa sana kesi ya kusababisha kifo, maana tayari Gerald
alishamweleza wazi kwamba angeandika barua ya kueleza sababu za kifo chake
kabla hajajiua!
“Lazima niende kwake, lazima...tena haraka sana...” wakati Davina anasema
maneno hayo kwa sauti alikuwa anapiga hatua za haraka sana kwenda nje, sehemu
alipoegesha gari lake.
54
Mara moja akaingia na kulipiga moto. Hakuwa na muda wa kupoteza, akaondoka
kwa kasi.
***
Kutoka Tandika hadi Mbezi Beach, kulikuwa na umbali sana, lakini kwa sababu
ilikuwa usiku na hapakuwa na magari mengi barabarani, Davina alipata mwanya
wa kuendesha gari atakavyo.
Baada ya dakika kumi tu, alikuwa ameshafika Mwenge, kwenye makutano ya
Barabara ya Sam Nujoma na Bagamoyo, akashika barabara inayoenda Bagamoyo
kasi yake ikiwa ile ile! Alikuwa tayari kupata ajali mbaya na kupoteza maisha yake
akiwa anamfuatilia Gerald.
Akili zake zilikuwa kama zimeruka, aliwaza kumpata Gerald tu, hakuwa na kitu
kingine chochote tena akilini mwake. Baada ya muda alikuwa anaegesha gari nje
ya nyumba ya Gerald na kugonga mlango kwa nguvu. Mara moja mlinzi akatokea.
Alipokutanisha macho yake na Davina, akafungua mlango haraka kwa kuwa
alikuwa anamfahamu.
“Shikamoo mzee,” Davina akamsalimia na kumpita.
“Marhaba binti yangu, vipi mbona kasi hivyo?”
“Fanya kazi yako...” Davina akamjibu kwa dharau na kuingia ndani.
Vyumba vyote Gerald hakuwepo na simu yake bado ilikuwa haipatikani.
Alipokagua vizuri chumbani kwa Gerald akaona simu yake ikiwa imezimwa
pamoja na ujumbe alioandika kwa mkono. Akachukua haraka na kuanza kusoma...
‘Natambua kujitoa uhai ni kosa, tena kosa la jinai. Pia najua vyema kuwa kujiua ni
dhambi mbele za Mungu, lakini mimi nalazimika kutokana na kupoteza umuhimu
wa kuishi duniani.
Natamani sana kuendelea kuishi, lakini nashindwa kwa sababu yule mwenye
amani ya moyo wangu amenikataa. Nataka jamii nzima itambue kwamba, moyo
wangu unampenda sana Davina, lakini yeye ameonesha wazi kwamba hanitaki.
Nimeshafanya mambo mengi sana ili nimpate, lakini wapi? Imeshindikana.
Sasa naona ni wakati wangu wa kupumzika kuliko kuendelea kunyanyaswa na mtu
ambaye nampenda na siwezi kuishi naye.
Nawaombeni mnisamehe wote. Najua taarifa hizi zitamuumiza sana mama yangu,
lakini sina budi kufanya hivi mama, naomba sana msamaha wako mama’ngu!
KWAKO DAVINA:
55
Nilikupenda sana, huu ukawa wimbo wangu siku zote, lakini hukuupenda na wala
haukukuvutia, nimeona ni bora nife nikuache ufurahi na roho yako. Ahsante sana
Davina. Kwa heri ya kuonana. Acha nimfuate rafiki yangu Jeff.
Kuhusu mwili wangu msihangaike sana, nendeni kwenye pori la Makongo, mbele
kidogo ya Mlimani City, mtauhifadhi.
Nisameheni wote niliowakosea na napenda kuwatangazia kwamba, moyo wangu ni
mweupe kwa wote mlionikosea. Buriani nyote.
Gerald.
Aliikunja ile barua na kuiweka kwenye mfuko wake wa suruali ya jeans kisha
akatoka nje haraka sana.
“Gerald ameondoka muda mrefu sana mzee?”
“Hata robo saa hajamaliza, nilijua labda amekufuata na nilivyoona umerudi,
nikajua alikuwa nyuma yako.”
“No! Amekuaga?”
“Hapana.”
Davina hakuwa na maswali zaidi ya kuondoka kwa kasi ile ile aliyoenda nayo.
Baada ya mwendo wa dakika kadhaa, alikuwa akikatisha eneo la Mlimani City,
akiifuata barabara ya vumbi inayoelekea Makongo. Alinyoosha moja kwa moja
akiendesha kwa kasi kuliko kawaida kwenye barabara ile ya vumbi.
Alipoyatupa macho yake kwenye saa iliyokuwa mbele ya gari, aligundua kwamba
ilishafika saa 7:36 za usiku. Woga ukazidi kumshika, lakini aliendelea kuendesha
gari, akitizama kwa makini kando ya barabara.
Mbele kidogo, akaona gari limeegeshwa pembeni mwa barabara, akapunguza
mwendo na kulisogelea. Hapo akagundua lilikuwa gari la Gerald. Akashuka haraka
na kuangalia kila upande kwa hadhari. Akaingia kwenye eneo lenye giza mbele
yake, kukiwa na mti mingi sana. Woga alioukuwa nao ulikuwa hauelezeki.
“Gerald...Gerald...” aliita kwa sauti ya chini huku woga ukiongezeka moyoni
mwake.
Hata hivyo hakuna aliyeitikia. Aliendelea kwa muda mrefu mpaka aliposikia kama
mti uliokuwa mbele yake ukitingishika, akatulia na kuyatupa macho yake juu ya
mti. Akausogelea ule mti aliokuwa na wasiwasi nao, akaona viatu chini. Hakupata
shida sana kujua kwamba vile vilikuwa viatu vya Gerald.
“Gerald please, naomba usijiue, nipo hapa kwa ajili yako, usife tafadhali, bado
nakuhitaji sana, shuka chini mpenzi wangu, nipo tayari kuwa na wewe kwa hali
56
yoyote,” Davina aliongea kwa sauti ya kusihi ingawa hakumuona Gerald lakini
alijua wazi lazima angekuwa katika ule mti baada ya kuona viatu pale chini.
Aliamini alikuwa bado hajakamilisha zoezi la kujinyonga maana kama ingekuwa
hivyo, angeuona mwili wake ukiwa unaning’inia.
“Hapana Davina, UMECHELEWA....lazima nife...” baada ya sauti ile, kishindo
kikuu kikasikika ikafuatiwa na sauti ya Gerald akilia!
Davina alihisi kuzimia!
Woga tele ukamjaa Davina, alijua kwa vyovyote vile kama Gerald angeanguka
chini, angekuwa na hali mbaya sana kama siyo kufa kabisa.
Kupiga kelel kusingesaidia chochote, kwanza alikuwa mwenyewe, pili ilikuwa ni
porini, lakini kubwa zaidi, kama ingegundulika Gerald alikuwa anataka kujiua,
angekuwa kwenye hatari ya kukabiliana na mkono wa sheria, jambo ambalo
Davina hakutaka litokee kabisa.
Kitu cha ajabu ni kwamba, Gerald hakutua chini, achilia mbali kutua chini, lakini
hata sauti yake ya kilio, ilikuwa ni ya mara moja tu!
Davina akaogopa sana!
Mara moja, akili yake ikafanya kazi kama umeme. Akatoa simu yake ya tochi
akawasha kisha akamwulika juu ya mti. Kwa macho yake mawili akashuhudia
Gerald akiwa amening’inia mikono na miguu kwa pamoja.
Ilionekana kama wakati anajiachia, alitua katikati ya tawi, hivyo tumbo lake kulala
katikati na mikono na miguu kukutana katikati! Davina akazidi kutetemeka kwa
woga...
“Kutetemeka kwangu hakusaidia lolote, lazima nitafute kitu cha kufanya...”
akawaza Davina.
“Geraldiiiiiii....” Davina aliita kwa sauti, lakini Gerald hakuitika.
Akapata wazo la ghafla; “Acha niende Mwenge mara moja nikachukue vijana waje
wamshushe...” akajisemea moyoni mwake huku akipiga hatua za haraka kuelekea
barabarani alipoegesha gari lake.
Alipofika akaingia haraka na kuwasha, kabla ya kuingiza gia, akapata wazo lingine
jipta kabisa...
“Naweza kumpoteza Gerald wangu kama sitakuwa makini hapa...kwani kupanda
mti nimeshasahau mara hii? Inabidi nirudi nipande mwenyewe na nimshushe.
Mwenge ni mbali sana, naweza kukuta ameshakufa.”
Wazo lake liliungwa mkono na yeye mwenyewe, akazima gari na kurudi porini.
Akavua viatu kisha akaanza kupanda juu ya mti taratibu.
57
Kupanda mtini halikuwa jambo geni sana kwa Davina, kwani alipokuwa Kijijini
kwao Baura, alikuwa mtaalamu sana wa kupanda miti ya matunda. Alipanda kwa
shida kidogo, kutokana na kuwa hajapanda miti kwa miaka mingi sana.
Kwa taabu alifika juu, akaketi kwenye tawi moja jirani na alipokuwa ameangukia
Gerald. Alikuwa anahema kwa kasi sana. Kitu cha kwanza alichokichunguza ni
kama Gerald alikuwa anapumua.
Naam...Gerald alikuwa anapumua...
“Gerald...” Davina akaita.
“Niache Davina, niache nataka kufa!”
“Sikia Gerald, najua unataka kufa kwasababu yangu!”
“Ndiyo hivyo, niache ondoka zako,” Gerald akazungumza kwa taabu sana.
“Nimeshaamua kuwa na wewe mpenzi wangu, huna sababu ya kufa tena Gerald,
naomba uniamini!”
“Nimesema nataka kufa, mbona hunielewi? Acha nimfuate rafiki yangu Jeff!”
“Hapana baby, nipo kwa ajili yako baba. Unadhani kama ningekuwa sikupendi
ningekufuata mpaka huku?”
“Hata kama, wewe ni mwongo, naomba ondoka uniache nife peke yangu.”
“Huwezi kufa nikiona, huwezi Gerald.”
“Ondoka tafadhali.”
“Nakupenda Gerald, naomba uniamini mpenzi wangu, nipe nafasi...sasa nimekuja
mzima-mzima, nipe nafasi mpenzi wangu.”
“Hapana nataka kufa!”
“Naona kama hatuelewani Gerald, umesema unataka kufa?”
“Ndiyo!”
“Sababu ni mimi?”
“Ndiyo!”
“Ok! Sasa acha kwanza nikutoe hapo, tuzungumze halafu utaamua kama bado
utataka kufa au kuendelea kuishi.”
Gerald hakujibu.
Davina hakuwa na haja ya kusubiri kauli yake, akasogea taratibu, kisha akamshika
mkono, huku mkono wake mwingine ukiwa umekamata tawi lingine bara-bara.
Akamvuta taratibu na Gerald akajitahidi kujisogeza hadi kwenye tawi lingine.
Akaketi.
“Pole.”
“Ahsante.”
58
“Usife Gerald, nimeshajua kwamba unanipenda kwa dhati, naahidi nitakuwa na
wewe!”
“Kweli?”
“Nakuahidi mpenzi wangu!”
“Haya tushuke tuondoke, hapa si mahali salama kwetu, isitoshe ni usiku mwingi
sana saa hizi!”
“Sawa, lakini unatakiwa kupumzika kwanza, subiri kwanza mpenzi wangu.”
“Sawa.”
Baada ya kama robo saa kupita, Davina na Gerald wakaanza kushuka kwa mtindo
wa Davina kutangulia chini na Gerald kumfuata nyuma yake. Wakafanikiwa
kushuka hadi chini salama.
Davina akamshika mkono na kumwongoza kwenye gari. Akamfungulia mlango na
kuingia.
“Utaweza kuendesha?”
“Ndiyo, usijali.”
“Nikupeleke hospitalini?”
“Hapana labda tupitie Phamramcy tukuchukue Diclopar kwa ajili ya kupunguza
maumivu.”
“Sawa, twende. Wapi sasa?”
“Sinza ya Palestina, huwa hawafungi wale.”
“Ok!”
Wakaondoka kwa mwendo wa taratibu sana hadi Sinza, wakachukua dawa na
kwenda zao Mbezi Beach. Davina hakwenda nyumbani kwake siku hiyo. Alilala
kwa Gerald. Kwa mara ya kwanza wakapeana mapenzi motomoto.
*****
Taarifa za uhusiano wa Gerald na Davina zilipokelewa kwa furaha sana na wazazi
wa pande zote mbili. Hakuna sehemu waliyoweka kipingamizi.
Kwanza kabisa, Gerald alimpeleka Davina nyumbani kwao Marangu, Kilimanjaro
kumtambulisha kabla ya kwenda kijijini kwa akina Davina, Baura, Kondoa mkoani
Dodoma.
Taratibu zote zikafanyika haraka, mahari ikatolewa na hatimaye ndoa ikatangazwa
kanisani. Kama kawaida, baada ya kutangazwa mara tatu mfululizo bila kuwepo
kwa kipingamizi, wiki iliyofuata ilikuwa ya ndoa.
Maandalizi yote yakakamilika!
59
****
Kanisa lilikuwa limejaa watu wengi sana, ndugu, jamaa na marafiki wa karibu wa
pande zote mbili walikuwa wamefurika kanisani. Nyuso zilizojaa tabasamu ndizo
zilizoonekana kila upande wa kanisa hilo.
Mbele ya madhabahu, walikuwa wamesimama Davina akiwa amevalia shela,
Gerald ambaye alikuwa amevaa suti ya rangi ya kijivu na wapambe wao.
Tayari Mchungaji alikuwa ameshawauliza Davina na Gerald kama wapo tayari
kufunga ndoa. Wote walikubali. Kabla ya tendo muhimu la kuunganishwa katika
ndoa takatifu, Mchungaji aliwageukia waumini na kuwauliza kama kuna yeyote
mwenye pingamizi.
“Kabla ya kuwaunganishwa wapendwa hawa, ambao kwa hiyari yao wamekubali
kuwa mwili mmoja katika ndoa takatifu. Je, kuna yeyote mwenye pingamizi?”
Mchungaji aliuliza.
Hakuna aliyejitokeza.
Alirudia kuuliza swali hilo kwa mara ua pili mfululizo, kabla ya kuuliza kwa mara
ya tatu na mwisho...
“Noooo....nooo Pastor...nina pingamizi...” ilikuwa sauti ya kijana kutoka lango kuu
akiingia kanisani pale akikimbia.
Waumini wote wakageuka na kumwangalia. Davina na Gerald wakashtuka sana.
Alikuwa ni Jeff aliyevalia suti nyeupe na viatu vyeupe!
Marehemu Jeff!
KANISA zima lilipigwa na butwaa, wote wakageuka kumuangalia kijana huyo
mtanashati wa kuvutia, akiingia kanisani akitembea kwa mwendo wa haraka.
Mchungaji hakuamini macho yake.
Akavua miwani ili aweze kuona kama alichokuwa anakiona na kusikia kilikuwa
sahihi. Gerald aliishiwa nguvu, lakini alijipa faraja kwamba inawezekana kabisa
ulikuwa mzimu wa Jeff na si Jeff mwenyewe.
Jeff alipokaribia madhabahuni kabisa, kabla hajapanda akazuiwa na Wazee wa
Kanisa.
“Tulia kwanza kijana, tulia,” Mzee mmoja akamwambia.
“Acheni nikazungumze na Mchungaji.”
“Hujazuiwa, lakini zipo taratibu za kufuata.”
“Mwache aje,” Mchungaji akadakia haraka.
Akaongeza: “Njoo kijana.”
Jeff akapanda madhabahuni.
60
“Unaitwa nani?”
“Jeff!”
“Nani?”
“Sebastian.”
Hapo si Davina wala Gerald, walihisi kuchanganyikiwa, maana sauti ilikuwa ya
Jeff kabisa na hata umbo lake lilikuwa ni Jeff mwenyewe, lakini hofu tele
iliyokuwa mioyoni mwao ni kwamba; Jeff ametokea wapi wakati alikufa?
Alizikwa?
“Kwanini unaweka pingamizi?”
“Davina ni mchumba wangu na tulikuwa katika hatua za mwisho kabisa kabla ya
kuoana, lakini yakatokea matatizo.”
“Matatizo gani?”
“Ni habari ndefu Mchungaji, lakini nitaisimulia baadaye kidogo, watu wote
wasikie.”
Mchungaji alipigwa na butwaa, tangu ameanza kazi ya utumishi, hakuwahi
kukutana na tukio kama hilo, siku zote alikuwa akisikia mambo hayo kwa
Wachungaji wenzake, lakini siku hiyo ilitokea kwake mwenyewe.
Akaduwaa.
Akamwangalia Gerald na kumwuliza: “Unamfahamu huyu kijana?”
“Huyo?” Gerald akauliza akitetemeka kwa hofu.
“Ndiyo.”
“Anafanana na marehemu Jeff.”
“Sikiliza Gerald, mimi si marehemu na sijawahi kuwa marehemu hata siku moja.
Siku yangu ya kufa ikifika nitakufa...kifo ni ahadi Gerald, ahadi ambayo kwangu
bado. Sema ukweli unanifahamu au hunifahamu?” Jeff alizungumza kwa ukali
sana, hali ambayo iliwashangaza waumini waliokuwa pale kanisani.
Gerald akaogopa sana, ni Jeff huyu huyu ambaye siku zote amekuwa mkarimu kwa
mambo mema, lakini hakusita kuwa mkali kwenye mambo ya kipuuzi. Kwa sauti
ile, alijirudhisha kabisa kwamba aliyekuwa mbele yake alikuwa ni Jeff mwenyewe.
Hilo alikubaliana nalo kwa asilimia mia moja.
“Unamfahamu au humfahamu?” Mchungaji akarudia swali lile.
“Alikufa!”
“Lakini unamjua?”
“Ndiyo!”
“Anaitwa nani na una uhusiano gani naye?”
61
“Ni Jeff kama alivyosema, kabla ya kifo chake alikuwa rafiki yangu,” Gerald
akasema akitetemeka kwa hofu.
Ombi lake kubwa lilikuwa ni ule uwe mzimu wa Jeff na si Jeff mwenyewe, maana
kama atakuwa ni Jeff basi kitanzi kilikuwa kinamsubiri.
“Davina, unamfahamu huyu kijana?”
“Ndiyo Mchungaji.”
“Ni nani?”
“Anaitwa Jeff, alikuwa mchumba wangu!” Kanisa zima likashtuka.
“Sasa?”
“Alikufa!”
Watu wakazidi kuchanganyikiwa. Inawezekana vipi mtu aliyekufa, aonekane tena
mara ya pili? Lilikuwa jambo la kushangaza sana ambalo liliwaacha watu wote
hoi. Haikuwa rahisi kuamini kuwa aliyekuwa mbele yao alikuwa ni marehemu
Jeff.
Mchungaji akamgeukia tena Jeff: “Enheee...hebu tupe habari kijana. Kwanini
hutaki hawa wafunge ndoa?”
“Hawawezi kufunga ndoa, Gerald ni muuaji mkubwa, yeye ndiye alipanga kifo
changu ili amuoe mpenzi wangu, lakini hilo halitawezekana, nilishamuahidi mara
nyingi katika barua ninazomuandikia yeye na Davina,” Jeff akasema
akilengwalengwa na machozi machoni.
“Kwahiyo ukweli ni upi, uliwahi kufa?”
“Hapana, sijawahi kufa Mchungaji.”
“Mwongo huyu naona anafanana tu na Jeff, anataka kutuharibia ndoa yetu...Jeff
alikufa, sijui huyu ametokea wapi? Lakini nahisi anaweza kuwa pepo, kwanini
asiombewe kwanza baba Mchungaji?”
“Tulia kijana, penye ukweli uongo hujitenga. Kumbuka hii ni nyumba ya Bwana,
mahala Patakatifu, hakuna lolote baya litakalofanyika chini ya dari la Bwana.
Kuwa na amani...yaache haya mambo yaende taratibu, bila shaka yataisha kwa
utaratibu pia.”
62
Mchungaji alipomaliza kusema maneno hayo, akamgeukia tena Jeff na
kumwambia: “Ulikuwa wapi muda wote?”
“Ni habari ndefu Mchungaji, lakini nataka kukuambia kwamba dunia yote
inafahamu mimi nimekufa, hata ndugu na wazazi wangu wote wanafahamu hivyo.
Hawana habari kama nipo hapa leo muda huu.
“Jeff aliyezikwa miaka miwili iliyopita hakuwa mimi. Siku zote hizo nilikuwa
naishi Mwanza. Nikifanya mambo yangu kimya kimya na hakuna aliyekuwa
anajua, lakini nilipanga kumfundisha adabu Gerald.
“Huyu ni binadamu hatari sana, hafai kabisa katika hii jamii, ni yeye ndiye
aliyepanga kifo changu, nikagundua na kukwepa, nataka kuanika ukweli huu leo.”
“Enheee....”
“Yaani inaniuma sana, tulikuwa marafiki wakubwa, lakini kumbe mwenzangu
alikuwa anamtamani mchumba wangu, ndiyo chanzo cha kuamua kupanga njama
za kuniua...
“Kabla sijaanza kusimulia, nainua mikono yangu juu, nikimuomba Mungu wangu
anisaidie kumaliza salama habari hii ya kusikitisha. Lakini naapa mbele ya Mungu
wangu na Kanisa, kwamba haya nitakayoyaongea ni ya kweli na hakuna lolote
ambalo nitaongea la uongo. Eee Mungu wangu naomba unisaidie...” Jeff
alivyomaliza kusema maneno hayo, akaanza kusimulia huku akizidi kulia...
“Gerald ana tamaa sana, hakuona thamani yangu...thamani ya damu yangu ya uhai
ambao nimepewa na Mungu bure, yeye akaona aimwage tena bila hatia yoyote.....”
Ndivyo Jeff alivyoanza kusimulia.
Watu wote walikuwa makini kumsikiliza.
63
SURA YA SABA
64
Dakika tano baadaye, Jeff akarudi sebuleni akiwa ameongozana na mwanamke
mrembo sana. Mzuri. Mwenye kila aina ya sifa anazotakiwa kuwa nazo
mwanamke!
Gerald akatabasamu!
Akatetemeka kwa kiwewe!
“Sijawahi kukutana na mwanamke mrembo kama huyu. Sijawahi. Jeff ni rafiki
yangu kipenzi, lakini kwa mwanamke huyu, urafiki na uishe tu. Nitafanya kila
ninachoweza huyu mwanamke awe wangu...kila ninachoweza...” Gerald akawaza
huku akimtiza mwanamke huyo kwa jicho la mahaba.
Alionekana kukolea kwelikweli.
Mwanamke huyo hakuwa mwingine, ni mtoto mrembo wa Kirangi. Mtoto kutoka
Baura, Kondoa. DAVINA!!!
Kwa dakika tatu nzima Gerald alishindwa kuzungumza kitu chochote, uzuri wa
Davina ukamchanganya sana, alitumia muda huo kumwangalia Davina kuanzia
chini hadi juu na kwa hakika alihisi mapigo yake ya moyo kubadilika.
“Kaka, upo hapa kweli?” Jeff akamwuliza Gerald.
“Yeah, I’m here brother!”
“Kimwili tu, lakini kimawazo, hata kidogo haupo hapa.”
“Unakaribia kupata tuzo ya utabiri sasa Jeff...ni kweli nilikuwa nawaza kuhusu
wale jamaa wa Canada walionipigia mchana!” Gerald akasema akicheka.
Uongo mtupu!!!
“Ah! Achana nao, lazima watakubali tu kaka, halafu kumbuka wameshasoma kila
kitu kwenye mtandao; sehemu ambayo huwa hatufanyi makosa...tunayo lugha ya
ushawishi kaka.”
“Ni kweli kabisa.”
“Sasa Gerald, kutana na Davina....my wife to be, my angel, my love, lahazizi na
kila jina zuri unalolifahamu. Huyu mwanamke nampenda sana, yeye ndiye
ameushikilia moyo wangu!” Jeff akasema akitabasamu.
65
“Nakubali kaka...nashukuru sana,” Gerald akasema, mate ya tamaa ya mahaba
yakimjaa.
“Davina, huyu ni Gerald, rafiki yangu kipenzi, lakini kama nilivyokuambia, ni bosi
wangu pia.”
“Nimefurahi kukufahamu Gerald. Karibu sana.”
“Ahsante shem wangu, ahsante sana.”
Stori mbili tatu zikaendelea, lakini kichwani mwa Gerald alijihisi amebeba mzigo
mzito sana, mzigo wa mapenzi. Mapenzi ya usaliti.
“Sijui lakini...ninachoweza kusema, nitatumia kila aina ya njia, hata kama ni pesa,
lakini huyu mwanamke atakuwa wangu. Potelea mbali kama nitagombana na Jeff,
lakini huyu mwanamke nimpate,” Gerald akawaza akiendelea kupata kinywaji.
Usiku Jeff akampeleka Gerald nyumbani kwake Mbezi Beach.
“Kaka kile kifaa ni noma, umebahatika kupata mwanamke mzuri sana,” Gerald
akasifia.
“Hakuna kaka, wa kawaida tu yule, najua unababaika na umbo lake. Nakujua
vizuri sana wewe ni mtoto wa mawowowo!”
Wote wakacheka.
Jeff akageuza gari na kurudi Sinza.
******
Pamoja na umrimdogo wa miaka 29 aliokuwa nao Gerald, alikuwa na mafanikio
makubwa sana; alikuwa na pesa, cheo kikubwa na vitu vingi vya thamani. Gerald
ndiye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya KSQ ambayo Jeff alikuwa
akifanya kazi.
Jeff na Gerald walitokea kuwa marafiki wakubwa kutokana na umri wao kuwa
sawa, kupenda mambo ya aina moja wote, lakini kubwa zaidi utendaji kazi wao
ulikuwa mzuri na wa kushirikiana.
Kabla ya kifo cha baba yake Gerald, yeye alikuwa ndiye Afisa Uhusiano wa
Kampuni, wakati Jeff akiwa Afisa Masoko. Baada ya kifo cha baba yake,
66
kwakuwa alikuwa ndiye mtoto wa kwanza wa kiume, alirithishwa kampuni hiyo na
kuanzia hapo akawa ndiye Mkiurugenzi.
Alipohamia katika cheo hicho kipya, akamteua swahiba wake Jeff kuwa Afisa
Uhusiano, nafasi ambayo alikuwa nayo awali. Uhamishwaji huo wa nafasi,
ulikwenda sambambamba na uboreshwaji wa masilahi yake!
Urafiki wao ukaongezeka maradufu!
*****
“Huyu ndiye Mkurugenzi wenu?” Lilikuwa swali la kwanza Davina kumuuliza
Jeff aliporudi Mbezi Beach.
“Ndiyo...”
“Samahani kwa hili mpenzi wangu, lakini naona ni bora nikueleze mapema.”
“Nini?”
“Kwa muda mfupi niliomuona rafiki yako, anaonekana hajatulia!”
“Kwanini?”
“Angalia yake ilikuwa inanipa mashaka sana, kwanza alikuwa akiniangalia kwa
kuibia, lakini pia kwa macho fulani hivi ya kimapenzi!”
“Hawezi kufanya hivyo bwana, yule ni rafiki yangu wa damu...labda umemuhisi
vibaya, ile ndiyo angalia yake.”
“Nimekuambia kama tahadhari, sasa kama unataka kufuga matatizo, endelea lakini
kuwa naye makini.”
Davina hakuongea kitu kingine chochote tena baada ya pale. Kwa mbali maneno
ya Davina yalianza kumingia Jeff, lakini hakutaka kufanya haraka, aliamua kujipa
muda zaidi wa kufanya uchunguzi wa madai ya mpenzi wake. Hakuwa hayawahi
wa kukurupuka hovyo...ilikuwa lazima atafute ukweli kwanza!
“Nimekuelewa mpenzi wangu, twende chumbani tukalale.”
“Sawa mpenzi wangu.”
“Enhee, utakaa hadi lini?”
67
“Wewe unataka hadi lini?”
“Miezi sita.”
Davina akacheka sana.
“Ndiyo unioe sasa ukae na mimi moja kwa moja, nikupikie na kukupakulia hadi
uchoke mwenyewe!” Davina akazungumza kwa sauti laini sana.
“Hayo tutapanga mpenzi wangu, usiwe na wasiwasi. Kuna mambo fulani
nayahangaikia, yakikaa sawa tu, tunamaliza.”
“Haya baba miahadi, tukalale bwana, nimechoka.”
Wakaingia chumbani kulala.
******
Usiku ulikuwa mrefu sana kwa Gerald, alihangaika akiwaza njia za kumnasa
Davina. Hakupata. Lakini baada ya kutulia kwa muda mrefu, akaona njia pekee ni
kukutana na Kundi la Kimafia la Nyamangumu Camp, kwa ajili ya kupanga
mipango ya kuwaachanisha Jeff na Davina.
Hapo angemchukua kiulaaniiii!
“Umepanga kutumia njia gani?” Gerald akamwuliza Master Fikiri ambaye
alikuwa ndiye Mkuu wa Kundi lile.
“Tukutane kwanza.”
“Sawa.”
Siku iliyofuata, saa mbili kamili za usiku walikutana katika kikao cha dharula,
katika Hoteli moja katikati ya jiji. Kilikuwa kikao cha watu wawili tu; cha kupanga
mikakati ya kuwaachanisha Jeff na Davina.
“Anatakiwa apatikane mtu wa kumlaghai Davina, kisha wapange kukutana hotelini
ambapo kamera zitakuwa zimetegeshwa, baada ya hapo Jeff anapelekewa video na
picha, hawezi kuvumilia, ataachana naye.
“Baada ya hapo namuandalia zengwe kisha namfukuza kazi, kila kitu kitakuwa
kimeishia hapo...kumbuka kwanza atakuwa na stress za kusalitiwa na mpenzi
wake, halafu namwekea mitego, anaharibu kazi na kumtimua...halafu namchukua
68
Davina bila matatizo yoyote. Unaonaje hapo?” Gerald akamwambia Master
aliyekuwa kimya muda wote.
“Umejaribu kuwaza, lakini fikra zako ni za kizamani sana, rahisi kugundulika.”
“Sasa tufanyeje?”
“Kipo kitu, lakini nina maswali machache kwanza.”
“Uliza.”
“Unampenda Davina?”
“Ndiyo!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Kitu kimoja tu, kinatakiwa kufanyika; JEFF ANATAKIWA KUFA!”
“ Haitajulikana?”
“Mimi ndiye Master...kama upo tayari sema nikupe maelekezo...” Master Fikiri
akasema akichukua sigara moja na kuitupia kinywani, kisha akawasha na kuanza
kuvuta kwa mbwembwe!
“Nipo tayari.”
“Good. Haya ndiyo maamuzi ya kiume. Kitu cha kwanza, utatakiwa kumuajiri mtu
wetu mmoja kwenye kampuni yako, halafu huyo mtu atamaliza kitu mwenyewe.
Kifupi utapanga safari ya kikazi na huyo mtu ambaye ataongozana naye mkoani,
njiani kutakuwa na vijana wangu wa kazi, watawateka na kumuua Jeff, stori
inabaki walitekwa na huyo kijana wangu atajulikana kwamba alinusurika. We
unaonaje?”
“Wazo zuri, lakini kwanini tusipange ajali?”
“Vyovyote iwavyo, lakini kikubwa kinachohitajika hapa ni Jeff afe, wewe ubaki na
Davina.”
Gerald akatabasamu, wakasimama na kukumbatiana, kisha wakaketi.
“Mwagize huyo mtu kesho ofisini kwangu, vipi kuhusu bei?”
69
“Wewe ni ndugu yangu, utanipa milioni hamsini tu kwa kazi nzima!”
"Fanya thelathini kaka!”
“Tufupishe maneno, utanipa arobaini!”
“Poa.”
*****
Jeff alivyofika tu ofisini asubuhi hiyo, alikuta ujumbe kwa Katibu Muhtasi
ukimwambia kuwa anahitajika ofisini kwa bosi mara tu baada ya kufika kazini.
Akatii.
Alimkuta Gerald akiwa ameketi kwenye kiti chake kikubwa, mbele yake kukiwa
na kijana mmoja mtanashati ambaye alionekana mgeni. Jeff alisimama kwa muda,
akimwangalia yule mtu kisha akamwangalia na Gerald, ambaye alimwonesha
ishara ya kumtaka akae.
“Morning!” Jeff akasalimia.
“Morning to you Jeff...nimekuita hapa kwa kitu kimoja, kutana na Roy Maketo,
huyu ni staff wetu mpya, ambaye atashikilia nafasi ya Afisa Masoko uliyokuwa
nayo awali, Lugendo nimemsimamsha kazi leo kutokana na utendaji wake usio na
tija.
“Huyu atakuwa chini yako, tafadhali mpe kila aina ya ushirikiano na umwoneshe
jinsi anavyotakiwa kufanya kazi yake vizuri. Kwa kifupi msimamie,“ Gerald
alisema bila kupepesa macho.
Akatulia kidogo kama anafikiria kitu, kisha akamgeukia Roy na kumwambia:
“Roy, huyu ndiye Jeff Sebastian, ndiye mkuu wako wa kazi, utakuwa chini yake.
Nawatakieni kazi njema,” Gerald akasema kisha akageukia kompyuta yake,
akaendelea na kazi.
Wote wakatawanyika!
“Kwisha habari yake...” Gerald akasema kwa sauti kubwa, muda mfupi baada ya
Roy na Jeff kuondoka.
*****
Gerald akazidi kufurahi, aliona kabisa jinsi kazi iliyobaki itakavyokuwa ndogo.
Mara moja akayanya simu yake na kumpigia Master.
“Vipi kuna tatizo?” Master akauliza mara baada ya kupokea simu.
70
“Tatizo? Tatizo la nini? Hapa shwari tu na hakushtukia mchezo!”
“Najua hawezi kushtuka.”
“Halafu nikaamua kumuweka chini yake kabisa, hapo hawezi kujua hata kama
atatumia mizimu ya kwao!”
Wote wakacheka.
“Tukutane jioni kwa ajili ya mipango zaidi,” Master akasema.
“Sawa, saa ngapi?”
“Saa mbili ndiyo muda mzuri zaidi, kitakuwa kikao cha watu watatu tu; mimi,
wewe na Roy!”
“Sawa kaka.”
******
Kikao kilikuwa tulivu sana, wote walikuwa kimya. Kilikuwa kikao cha watu
watatu tu, ambao walikuwa wameizunguka meza ya duara iliyotengenezwa kwa
vioo tupu.
Gerald akawatizama kwa zamu, alianzia kwa Roy kisha akamalizia kumwangalia
Fikiri-Master. Midomo yake ikatingishika, akionekana kuwa na jambo la kutaka
kuzungumza...
“Ndiyo kaka, naamini huu ni mwanzo mzuri, sasa sijui kazi itafanyika vipi?”
Gerald akaanza kumwambia Master.
“Mipango yote ipo tayari, hata Roy mwenyewe anajua cha kufanya, ni wewe na
muda wako. Sijui unataka hii kazi ikamilike lini?”
“Nataka ikamilike haraka sana.”
“Muda gani?”
“Ndani ya wiki mbili tu, nataka Jeff awe kashahama katika ulimwengu huu.”
“Niachie hiyo kazi, lakini wewe cha kufanya, simamia ukaribu wao hawa vijana,
halafu utawapangia safari siku nitakayokutaarifu, ndani ya wiki hizo mbili, halafu
kiulaiiini kazi inamalizika huku ulimwengu wote ukijua ni ajali.”
“Utafanyaje?”
“Niachie mimi. Unachotakiwa kufahamu ni kwamba, Jeff na Roy watasafiri
pamoja, halafu Jeff atakufa kwenye ajali feki.”
“Sawa.”
Kikao kikafungwa!
Wakatawanyika.
71
Siku zote Roy amekuwa akifanya kazi katika kundi hilo la Kimafia, ameua watu
wengi sana, tena kwa mikono yake mwenyewe. Alishawahi kunyonga mama na
watoto wake wawili wadogo, kwa mikono yake mweyewe na hajawahi kujisikia
huruma.
Kifo cha Jeff hakikumfurahisha hata kidogo, yeye ndiye mwenye mamlaka ya
kumuua Jeff, lakini moyo wake ulikataa kabisa kufanya hilo. Hata yeye
mwenyewe alijishangaa, maana ilikuwa kazi yake ya kila siku. Sehemu ya maisha
yake.
Usiku mzima alikuwa akiweweseka, Jeff alikuwa rafiki mzuri sana kwake, kwa
siku moja aliyofanya naye kazi, aligundua alikuwa kijana muungwana sana na
hakutakiwa kufa hasa kutokana na upole na ukarimu aliouonesha.
“Hapana, siwezi kumuacha Jeff afe,” akawaza.
“Lakini sijui nitatumia njia gani, maana mimi ndiye ninayetakiwa kuhakikisha
anakufa, asipokufa ni wazi kwamba nitakuwa nimejisababishia matatizo! Sasa
nitafanyaje? Maana moyo wangu hautaki kabisa kushuhudia Jeff akifa, ingawa
najua kabisa kwamba kama nisipomuua na ikajulikana ni mimi ndiye
niliyemtorosha, nitapata matatizo makubwa sana. Acha nilale, kesho nitajua la
kufanya,” aliwaza hayo kisha akajifunika shuka na kulala.
*****
Siku iliyofuata, Roy alilazimisha uchangamfu na kumaliza siku salama akiwa hana
jibu ya namna gani angemsaidia Jeff. Ndani ya nafsi yake, hakutaka kabisa kuona
Jeff anakufa, lakini tatizo lilikuwa ni kwa jinsi gani angeweza kumsaidia. Hapo
ndipo palipokuwa na maswali yasiyo na majibu.
Kwa wiki nzima alikuwa bado anafikiria, huku safari yao ikiwa imebaki wiki moja
tu huku Jeff akiwa hafahamu chochote juu ya safari hiyo. Akiwa amejiinamia
ofisini kwake, akapata wazo, lakini ilikuwa lazima apate muda wa kuzungumza na
Jeff kwanza ili amweleze hali halisi ilivyokuwa. Akanyanyua simu iliyokuwa
mezani kwake na kumpigia Jeff.
“Sema Roy, kuna tatizo?” Ilikuwa sauti ya Jeff kwenye simu.
“Hapana boss, nina mazungumzo kidogo na wewe.”
“Njoo ofisini kwangu.”
“Hapana, hayahitaji mimi kuja ofisini kwako, tunaweza kuongea tu, kwenye
simu.”
“Sawa.”
72
“Nataka kukutoa jioni, baada ya kazi.”
“Kunitoa?” Jeff akahamaki.
Alikuwa na kila sababu ya kuhamaki, maana alikuwa hana mazoea kabisa na Roy,
isitoshe alikuwa mgeni na yeye alikuwa bosi wake. Mazoea yametokea wapi?
“Ndiyo...kwanini unashtuka? Nataka kukupa ofa.”
“Ofa?” Jeff akazidi kushtuka, ilikuwa maajabu sana kwa Roy kutaka kumpa yeye
ofa.
“Ndiyo, kwani vipi?”
“Ahsante sana Roy, tufanye siku nyingine, leo nina ratiba nyingine.”
“Hizo ratiba zako hazina umuhimu mkubwa kama mwaliko wangu, naomba
ukubali maana nina habari muhimu kwa ajili yako, tena unatakiwa kuzipata leo.”
“Mbona unanitisha?”
“Sikutishi, nakuambia ukweli, tafadhali sana, naomba tukutane jioni.”
“Wapi na muda gani?”
“Kuhusu muda ni saa tatu kamili usiku, sehemu nitakujulisha muda huo
ukikaribia.”
“Poa.”
“Kazi njema bosi wangu.”
“Nawe pia, ingawa lazima niseme ukweli kuwa umeniacha na maswali mengi
sana.”
“Ni lazima ujiulize maswali, lakini ni bora ujiulize maswali ambayo muda mfupi
ujao utapata majibu yake, kuliko kujiuliza maswali ambayo hujui sehemu
utakayopata majibu. Nakuhakikishia, jioni nitakuwa majibu ya maswali yako.”
“Sawa.”
Wakakata simu zao.
*****
Bado Jeff hajayabandua macho yake usoni mwa Roy ambaye hazungumzi kitu.
Zimeshakatika dakika kumi tangu Jeff amefika katika hoteli hiyo, Sinza jijini Dar
es Salaam. Wamebaki wanaangaliana.
“Nakusikiliza kaka...” Jeff akasema.
“Acha presha mkubwa, lakini nataka kukuambia kwamba, haya mazungumzo yetu
ni siri kubwa sana. Gerald hatakiwi kujua kama niikutana na wewe.”
“Mbona sikuelewi?”
“Utanielewa tu, kaka tulia kwanza.”
73
“Ok! Nakusikiliza.”
“Kwanza nakuomba sana, usipaniki kwa haya nitakayokuambia, wewe ni
mwanaume na ni vyema kuyachukua kama yalivyo. Kikubwa unachotakiwa
kufahamu ni kwamba, nimeamua kwa moyo mmoja kukusaidia.
“Sikiliza Jeff, najua unaamini kwamba nimekuja pale kwa ajili ya kufanya kazi ya
Afisa Masoko, sivyo?”
“Ndiyo!”
“Sasa ukweli sio huo, nimekuja kwa kazi nyingine kabisa, ambayo sitaki
kuifanya.”
“Ni nini?”
“Una mchumba anaitwa Davina?”
“We’ umemjuaje?”
“Unaye au huna?”
“Ninaye.”
“Gerald anamfahamu?”
“Ndiyo!”
“Ok! Sidhani kama nina haja ya kuzunguka kiasi hicho, lakini ukweli ni kwamba,
Gerald anamtaka mchumba’ko!”
“Unasema?”
“Acha papara, hilo ni dogo sana, tulia kwanza, kuna kubwa zaidi.”
“Lipi?”
“Ili aweze kumpata, amepanga kukua!”
“What?”
“Ndiyo...na mimi nipo pale kazini kwa ajili ya kukuua wewe!”
Jeff akayatoa macho yake kwa mshangao mkubwa, hakuamini kama maneno yale
yalitokea kinywani mwa Roy.
Afisa Masoko!
74
SURA YA NANE
KWA muda mrefu sasa, Jeff alikuwa ameyatuliza macho yake usoni kwa Roy
kwa mshangao mkubwa! Haikuwa rahisi kuamini kwamba Roy alikuwa
akizungumza maneno yale kwa kumaanisha. Akayatembeza macho yake katika
mwili mzima wa Roy!
Bado hakutaka kuamini!
Alihisi kama anaota, tena ndoto ndani ya ndoto hiyo anayoiota. Yaani Gerald
anataka kumuua ili aweze kuwa na Davina? Mbona ni jambo jipya na la ajabu
sana?!
“Sikiliza Roy, tunafanya kazi pamoja siyo?” Hatimaye Jeff akasema kwa sauti ya
unyonge sana.
“Ndiyo!”
“Wewe unafanya kazi chini yangu siyo?”
“Ndiyo!”
“Mimi ni bosi wako...nadanganya?!”
“Uko sahihi kabisa.”
“Sasa ni vizuri ukatambua na kuheshimu mamlaka yangu, siamini kama tunapaswa
kutaniana kiasi hiki, tena utani mkubwa kama huu, ambao unahusu maisha yangu.
Hata kama unatania, lakini nadhani ni bora kama utabadilisha utani wako!”
“Sikiliza Jeff, kwanza nazidi kukusisitiza kwamba jambo hili ni siri, hutakiwi
kuvujisha hii siri. Halafu kaa ukijua mimi ni Mafia, sitakuwa tayari kukuacha hai
kama nikijua hii siri imevuja.
“Hii ni kwa faida yako, kazi yangu ilikuwa ni kukuua, lakini kwa moyo wangu wa
upendo, umeamua kukusaidia, lakini sasa naona huamini mpaka haya mambo
yatakapokukuta,” alisema Roy akiwa amemkazia macho Jeff.
Jeff alikuwa kimya kama anayefikiria jambo zito sana kichwani mwake, jambo
linalomchanganya na kumkosesha kabisa furaha. Kwa muda akauacha ubongo
wake uchanganue mambo wenyewe. Akajiuliza maswali mengi sana. Kwamba
inawezekana vipi Roy amfahamu Davina wakati alikuwa mgeni ofisini kwao, tena
hawakuwa na mazoea kabisa?
Hapo sasa akaanza kuhisi kwamba yawezekana kuna ukweli fulani katika jambo
lile.
“Umesema unamfahamu Davina.”
75
“Namsikia.”
“Kutoka kwa?”
“Gerald.”
“Gerald?”
“Sikiza, acha maswali yasiyo na maana, tunatakiwa kupanga jinsi ya kukuokoa,
wewe unatakiwa kufa, tenda imekuja ofisini kwetu, cha msingi ni kuangalia kilicho
mbele yetu siyo mambo yaliyopita.”
“Kwahiyo tutafanyaje?”
“Hilo ndiyo swali sasa...kila kitu nimeshapanga, wiki mbili baadaye tutapangiwa
safari ya kikazi kwenda Dodoma, katika safari hiyo wewe unatakiwa kufa njiani
katika ajali ya kutengeneza...” Roy akasema, Jeff akimsikiliza kwa makini.
“Mungu wangu!”
“Ndiyo hivyo, sasa wewe unatakiwa kutulia. Fuata maagizo yangu.”
“Sawa.”
“Kwanza lazima ujue mimi nafanya hii kazi kwa malipo makubwa, lakini
nimeamua kusaliti kwa ajili yako. Unatakiwa kunipa kifuta machozi kidogo.”
“Kiasi gani?”
“Sitaki pesa nyingi sana, niandalie milioni tano tu!”
“Nitakupa usijali, kwahiyo tutafanyaje?”
“Usiwe na shaka na hilo. Kipo kitu cha kufanya, wewe utaonekana umekufa na
jamii nzima itaamini hivyo.”
“Kivipi?”
“Tutakwenda pamoja katika hiyo safari, lakini wewe fanya maandalizi yako ya
jumla, tukiondoka tutafika mahali tutaachana, utavua nguo ulizovaa na kunipatia,
pamoja na kitambulisho chako, halafu wewe utaondoka zako, uende katika mkoa
mwingine kabisa.
“Huko utaishi maisha mapya, ukiwa tofauti na ulivyo hapa Dar. Lazima ubadilishe
staili yako ya maisha. Kwa kifupi uwe mwingine!”
“Hapo nimekuelewa, lakini sasa nitajulikana vipi nimekufa wakati nitakuwa
nimeondoka?”
“Ndiyo maana nikakuambia utaacha nguo zako pamoja na kitambulisho!”
“Ni kwa ajili ya nini?”
“Nitatafuta maiti ambayo nitaivisha nguo zako na kuweka kitambulisho chako, kila
mtu atajua ni maiti yako!”
“Sasa huoni kwamba sura zitakuwa tofauti?”
76
“Ataharibiwa sura, haitatambulika kabisa, alama itakuwa ni nguo na kitambulisho
chako.”
“Mh! Kweli kazi ipo.”
“Ndiyo hivyo...enhee sema unapenda kwenda mkoa gani?”
“Nitaenda Mwanza, kule ni pazuri zaidi kwa kujificha, nitaanza maisha yangu
kule.”
“Sawa, nadhani tumemaliza, lakini naendelea kukusisitiza kwamba haya ni
mazungumzo ya siri. Usijaribu kumwambia mtu yeyote yule. Fanya maandalizi
yako taratibu na kimya kimya. Chukua fedha zako kwenye akaunti mapema, safari
ni muda wowote kutoka sasa.”
“Poa kaka, nimekuelewa vizuri sana.”
Kilichoendelea hapo ilikuwa ni kunywa pombe kwa kasi ya ajabu.
*****
77
“Yes! Wakubwa. Nimewaita hapa kwa agizo moja muhimu,” Gerald akasema
kisha akameza fundo moja la mate.
Jeff akakaa sawasawa kwenye kiti chake, alishajua kitakachosemwa na Gerald.
“Kifupi mnatakiwa kwenda Dodoma keshokutwa jioni, mnatakiwa mkafanye
ukaguzi wa Tawi letu la huko, pia mtatoa Semina Elekezi kwa watumishi wetu.
Kwa muda mrefu sasa, siridhishwi na ripoti za Dodoma, nahisi kuna kitu. Sasa
mnatakiwa muende kule, mtakuwa huko kwa wiki moja.
“Taratibu nyingine zinaendelea vizuri, gari lipo lakini kwasababu tuna uhaba wa
madereva, mtaendesha wenyewe mkipokezana. Naamini wote ni madereva wazuri
kwahiyo mtabadilishana kwenda na kurudi.”
Wote wakatingisha vichwa, kuashiria kukubaliana na alichokiongea.
Wakatawanyika!
Jeff alihisi moyo kutaka kutoka, hapo aliamini kweli Gerald alikuwa na roho ya
kinyama sana. Hakuamini kabisa alichokisikia, lakini pia ilikuwa vigumu sana
kwake kuamini kuwa Roy alikuwa muuaji! Hapo aliamini.
Jeff alipofika ofisini kwake, mara moja akamwandikia Roy meseji: “Kaka
nimeamini, inabidi nifanye maandalizi mazuri na kwa siri sana.”
“Ni kweli, hata Davina hatakiwi kujua kabisa kuhusu hili. Tuachane na mambo ya
simu, tukutane jioni pale pa siku ile, tujadiliane vizuri. Uje na mzigo wangu
kabisa.”
“Sawa.”
*****
Kitu cha kwanza Jeff kufanya baada ya kukutana na Roy jioni hiyo ilikuwa ni
kutoa fedha kiasi cha milioni tano na kumpatia. Mipango ikaanza...
“Nadhani sasa umeniamini, hatuna muda wa kukaa sana hapa, kama
tulivyozungumza, wewe andaa mambo yako na mimi naandaa mambo yangu,
lakini itabidi uniongeze milioni moja!”
“Za nini tena?”
“Tunatakiwa kupata maiti, suala la maiti si tatizo, ninao vijana wa kazi ambao
watahangaikia hili ndani ya siku tatu, lakini natakiwa kuwalipa.”
“Kesho asubuhi nitakuja nazo ofisini.”
“Sawa.”
Kikao kikafungwa.
78
*****
Usiku mzima Jeff alikuwa na Davina wake wakipeana mahaba mazito, alijitahidi
sana kuhakikisha anamuacha mpenzi wake akiwa ameridhika vya kutosha. Pamoja
na yote, hakuonesha dalili hata moja, kwamba safari yake ya siku inayofuata
ilikuwa ya moja kwa moja!
Hiyo ilibaki kuwa siri yake mwenyewe ndani ya moyo wake, hakuruhusu kabisa
jambo hilo lijulikane na mpenzi wake Davina. Asubuhi Jeff alimuaga mpenzi
wake, lakini Davina alionekana kukosa furaha.
“Vipi mbona unakuwa hivyo?” Jeff akamwuliza Davina.
“Unaniacha peke yangu!”
“Kwani nakwenda kufa, ni safari ya wiki moja tu mpenzi wangu.”
“Haya bwana, lakini sijui kwanini moyo wangu hauna amani na safari yako....sijui
kuna nini?!!” Davina alisema kwa sauti ya taratibu sana akimaanisha
alichokiongea.
Jeff alishtushwa sana na kauli ile, kichwani mwake kukagonga kengele ya hatari.
*****
Jeff alihisi kupoteza furaha ghafla, hakuweza kuelewa ni kwanini Davina alisema
hana imani na safari yake. Ndani ya moyo wake alijua kila kitu kinachoendelea,
lakini hakutakiwa kueleza chochote kwanza, ilikuwa mapema sana kwake kufanya
hivyo!
Mapema sana...
“Kwani unahisi nini?”
“Hata mimi sijui.”
“Hujui?”
“Ndiyo sifahamu kabisa.”
“Sijakuelewa bado.”
“Baby sifahamu kwanini sina amani na safari yako, lakini kikubwa moyo wangu
una mashaka sana. Umeingiwa na baridi ya ghafla, nahisi kutakuwa na tatizo.”
“Hapana usiwaze hivyo mpenzi wangu, amini kwamba nakwenda Dodoma kikazi
na nitarudi salama, kikubwa unatakiwa kuniombea kwa Mungu niende na kurudi
salama.”
“Sawa mpenzi wangu, nitafanya hivyo.”
“Hilo ndiyo la msingi.”
“Tulale basi mpenzi wangu.”
“Haya...sogea basi huku...”
79
Jeff akamsogelea mpenzi wake, wakakumbatiana kimahaba. Taa ikazimwa,
wakalala.
*****
Bado Davina anaendelea kumng’ang’ania Jeff huku akilia kwa uchungu, katika
maisha yao ya kimapenzi, hakuwahi kuwa na uchungu na safari yoyote ya Jeff ya
kikazi kama siku hiyo. Moyo wake ulikuwa mzito kuliko kawaida, hata yeye
mwenyewe alishindwa kuelewa ni kwanini alijihisi mzito kiasi kile.
Amejilaza kifuani mwa Jeff, akilia kwa uchungu bila kukoma, hana dalili za
kunyamaza kabisa.
“Davina nachelewa...” Jeff akamwambia.
“Kwani ni lazima uende?”
“Ingekuwa nakwenda kutembea, isingekuwa lazima sana kwenda, lakini
kwasababu nakwenda kikazi ni lazima...”
“Baby....”
“Unasemaje?”
“Bado nakuhitaji sana Jeff wangu.”
“Hata mimi pia nakupenda na ninakuhitaji sana mpenzi wangu, wewe mwenyewe
ni shahidi wa hilo.”
“Sawa bwana, safiri salama mpenzi wangu, fahamu kwamba nakupenda sana,
moyoni mwangu kuna mzigo mzito wa mapenzi juu yako, siwezi kuishi bila wewe
mpenzi wangu.”
“Siku zote nimekuwa nikilitambua na kuliheshimu sana hilo, itaendelea kuwa
hivyo siku zote za maisha yangu.”
“Ahsante sana,” Davina akajibu akitabasamu.
“Sasa unaniruhusu, siyo mpenzi wangu?”
“Moyo wangu mweupe.”
“Ahsante sana.”
“Lakini bado sijafanya kitu kimoja.”
“Nini?”
“Sijakubusu mpenzi wangu.”
“Hilo tu, mbona rahisi sana, midomo hiyo hapo...mashavu hayo hapo....paji la uso
hilo hapo....nibusu popote upendapo...” Jeff akasema akiachia tabasamu mwanana
sana usoni mwake.
Davina naye akatabasamu.
80
Akamsogelea Jeff kisha akaanza kumwangushia mvua ya mabusu motomoto.
Wakaagana kwa furaha.
*******
Ndani ya ofisi ya Gerald mchana huo, walikuwa wamekaa Gerald, Jeff na Roy
wakijadiliana juu ya mipango ya safari. Kila kitu kilikuwa tayari, kilichokuwa
kinasubiriwa ni muda wa safari tu.
“Nadhani mpo tayari kwa safari sasa,” Gerald akawauliza.
“Ndiyo boss,” Roy akajibu haraka-haraka.
“Gari linamaliziwa kufanyiwa service ya mwisho, endeleeni na kazi kwanza,
mpaka saa kumi, gari litakuwa limeshaletwa. Si vibaya kama mtaanza safari yenu
saa kumi na moja jioni!”
“Tena ni muda mzuri sana, barabara inakuwa imetulia na lami imepoa!” Roy
akasema.
“Sawa, endeleeni na majukumu mengine, baadaye.”
“Ok!”
Wakatawanyika.
Saa kumi na moja kamili, kama walivyokubaliana walikuwa wanaanza safari yao
ya kwenda Dodoma. Wakaagana na Gerald ambaye alikuwa ana furaha sana,
alifurahia safari hiyo maana alijua ilikuwa safari ya mwisho ya Jeff. Safari ambayo
ingempa uhuru wa kuwa na Davina, mwanamke ambaye aliufanya mateka moyo
wake.
Safari ya Dodoma ikaanza. Waliingia Chalinze saa 12:15 za jioni, Roy akaegesha
gari nje ya baa moja maarufu iliyochangamka pale Chalinze. Waliamua kupumzika
kwa muda kwa ajili ya kulanisha makoo yao kwanza.
“Sasa kaka, kitu cha kwanza kabisa unachotakiwa kufanya ni kubadilisha nguo
zako.”
“Ok!”
“Halafu unipatie kitambulisho chako pamoja na vitu vingine muhimu, ifupi uache
pochi yako, pesa ondoa ila acha vitu vya muhimu ambavyo vitaweza kutumika
kama alama yako.”
“Nimekuelewa kaka.”
“Hata simu yako, inabidi uiache.”
“Hapo tutakuwa tumecheza, kila mtu atajua nimekufa.”
“Sasa hili zoezi litafanyika wapi?”
81
“Hapa hapa!”
“Wapi sasa?”
“Chooni, hakuna pengine. Acha niende mara moja na begi langu.”
“Poa kaka, fasta.”
“Usijali.”
Dakika tano baadaye, Roy alirudi akiwa amevaa nguo zingine, kofia ya pama na
miwani ya jua. Akaketi kitini na kumalizia bia yake haraka.
“Kaka hapatufai tena hapa, tuondoke...” Roy akamwambia Jeff.
“Poa, twende.”
Wakasimama na kurudi zao kwenye gari, wakaondoka kwa kasi. Njia nzima
walikuwa wakizungumza na kuweka mipango yao sawa. Mara simu ya Roy ikaita,
alipotizama kwenye kioo cha simu yake, akakutana na jina la Kijasho.
Akatabasamu na kupokea mara moja.
“Niambie kaka...” Roy akatamka maneno hayo, mara baada ya kupokea simu.
“Poa, mambo shwari kabisa.”
“Uko wapi?”
“Nimeshapita Chalinze nakuja, mzigo umepatikana?”
“Ndiyo, ninao hapa!”
“Tayari mmeshauharibu sura?”
“Kaka mwenyewe utapenda, hajulikani kabisa.”
“Poa, tutakutana mbele kidogo ya Mikese.”
“Haya, utanijulisha ukikaribia.”
“Poa.”
Roy alipokata simu, akasimamisha gari pembeni.
“Kaka mambo yanataka kuanza, naona hapa panakutosha, shukia hapa subiri basi
la Morogoro, nenda ukalale hapo, asubuhi na mapema fanya mipango ya safari ya
kwenda Mwanza.”
“Poa.”
“Hakikisha huonekani sura hovyo, sawa?”
“Poa mkubwa, nimekuelewa vizuri sana.”
Roy hakuondoa gari haraka, akasubiri mpaka Jeff alipopanda basi ndipo naye
akaondoka polepole. Aliendelea kuendesha polepole, akitaka giza liingie. Kuna
wakati aliamua kuegesha kabisa njiani kwa muda, akijifanya anakagua gari, lakini
nia yake ilikuwa ni giza.
82
Mwanga haukuwa na kazi na yeye kabisa, ilipotimu saa 1:16 za usiku, akaingia
garini na kuanza tena safari. Akiwa kilometa tano kabla ya kufika Mikese,
akaegesha gari pembeni kwenye pori dogo kando ya barabara kisha akampigia
simu Kijasho.
“Uko wapi Kijasho?”
“Mikese, hapa kwenye mizani.”
“Njoo mbele kama unakuja Chalinze, soma kilometa tano, utaona gari langu.”
“Poa.” Baada ya muda Kijasho alikuwa ameshafika sehemu aliyoagizwa.
“Kaka hapa noma, tuingize magari ndani kidogo.”
“Haina shida.”
Zoezi hilo likafanyika haraka, halafu kilichofuata hapo ikawa ni kuivalisha ile
maiti nguo za Jeff, ikawekewa pochi yenye kila kitu muhimu pamoja na simu.
Baada ya hapo, wakaibeba na kuiingiza kwenye gari la Roy. Malipo yakafanyika
chapchap na kuagana.
“Kaka ahsante sana, waweza kwenda.”
“Poa, kazi njema, ni dili gani lakini?”
“Najua mwenyewe.”
“Poa kaka.”
“Lakini nikutahadharishe kwamba, ikiliki tu mimi na wewe!”
“Hatuaminiani kiasi hicho?”
“Tunawekana sawa tu.”
“Usijali.”
Kila mmoja akaondoka na njia yake, Kijasho akaenda na barabara inayoelekea
Chalinze, Roy akashika barabara inayoenda Morogoro. Akili yake ikiwa sehemu
ya kuliingiza gari. Akakanyaga mafuta kisawasawa, alipofika eneo lenye
mteremko mkali, pembeni kukiwa na mti mingi, akalipeleka gari usawa wa ile
maiti na kuligongesha upande mmoja!
Kilichosikika baadaye ilikuwa ni mshindo mkuu!
Ilikuwa ajali mbaya sana.
****
KWANZA ulisikika mlio mkali wa kupasuka matairi halafu kukawa kimya.
Hakuna sauti ya binadamu iliyosikika baada ya mlio ule. Roy alikuwa katika hali
mbaya sana na hakujitambua! Alipoteza fahamu pale pale!
83
Muda mfupi baadaye, magari mengine yaliyokuwa yakipita eneo lile yalisimama
na kushudia ajali ile mbaya. Haraka simu ikapigwa Polisi na muda mfupi baadaye,
gari lenye maasakari kutoka Kituo cha Polisi Mikese likafika. Roy akatolewa na
kupakiwa kwenye gari pamoja na ile maiti.
Kilichofuata hapo ilikuwa ni kuwapeleka katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro
kwa matibabu, hawakugundua kwamba moja ilikuwa maiti tayari. Baada ya kufika
hospitalini na uchunguzi kufanyika, ile maiti ikagundulika tayari ilikufa! Lakini
kwa bahati mbaya sana, iliharibika sana sehemu ya usoni. Kama walivyofikiria
ndivyo ilivyokuwa, wakaikagua mifukoni na kuona kitambulisho pamoja na pochi
yake ambayo ilikuwa na vitu vyake mbalimbali.
Kitambulisho kile kiliandikwa jina la Jeff Sebastian. Taarifa zikapelekwa Makao
Makuu na usiku huo huo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro akatoa taarifa
kupitia redio Abood na Ukweli za mjini humo.
84
SURA YA TISA
HADI saa 7:30 za usiku, Master alikuwa na Gerald ofisini kwake, wakinywa
sana pombe usiku huo. Hamu yao kubwa ilikuwa ni kusikia Jeff ameshafariki. Hilo
halikutokea. Mbaya zaidi, simu ya Roy ilikuwa haipatikani mpaka muda huo.
Master akaona njia pekee pale ni kuwapigia vijana wake ambao walikuwa njiani
wakimsubiri Roy. Akaweka glasi ya wine mezani, akanyanyua simu na kubonyeza
namba za mmoja wao, akapeleka dole gumba katika kitufe cha kupiga.
Akapeleka simu sikioni.
“Hallow!”
“Ndiyo boss!”
“Mbona kimya?”
“Tumepoteza mawasiliano mkubwa.”
“Mmepoteza mawasiliano, kivipi?”
“Roy hapatikani!”
“Hata sisi pia hatumpati, tukajua kwamba yawezekana kazi yenu
mmeshaimaliza....”
“Hapana mkuu...”
“Kwahiyo hamjakutana mpaka muda huu?”
“Ndiyo, lakini sisi tupo kamili tunasubiri kazi tu.”
“Anyway, endeleeni na kazi, nitawapigia baadaye.”
“Sawa mkuu.”
Simu zikakatwa.
Gerald na Master wakaangaliana.
“Sasa...” wakati Gerald akitaka kuzungumza jambo, mara simu yake ikaita.
Alipotizama kwenye kioo akakutana na jina la Jerome; huyu ni mfanyabishara
mkubwa mjini Morogoro ambaye ni rafiki yake mkubwa.
“Samahani kaka niongee na huyu mtu, sijui ana nini hadi ananipigia simu usiku
huu, inawezekana ana ishu muhimu.”
“Poa ongea naye kaka.”
“Hallow...”
“Kaka!”
“Nipe ripoti mkubwa.”
“Aisee pole sana....” Jerome akasema kwenye simu kwa sauti ya taratibu sana.
85
“Ya nini tena, mbona unanitisha? Au ile zabuni niliyoomba nimezidiwa na wajanja
wa mji kasoro bahari nini kaka?”
“Hapana.”
“Ni nini hasa? Niambie, roho yangu ipo juu juu!”
“Gari yako imepata ajali huku Morogoro na vijana wako wawili walikuwa ndani
ya hilo gari. Mmoja amefariki, mwingine ana hali mbaya, hajazinduka mpaka sasa
hivi.”
“Ni kweli nina vijana wangu wawili walikuwa safarini usiku huu kuelekea
Dodoma, wamepata ajali?’
“Tena mbaya sana, mi nimesikia redioni kwenye gari, nikiwa natokea zangu
Kilakala nilipokuwa nakunywa na rafiki zangu, nikaamua kuja moja kwa moja
mpaka hapa hospitalini.”
“Mungu wangu, ni nani huyo aliyekufa?” Gerald akauliza akiwa na shauku sana ya
kutaka kujua aliyekufa ni nani.
“Ameharibika vibaya sura, siyo rahisi kumtambua, lakini kwa kupitia simu,
kitambulisho na vitu vingine alivyokuwa nayo, imegundulika kwamba anaitwa Jeff
Sebastian na huyu mgonjwa ni Roy Maketo!”
“Ndiyo hao hao...sasa mi nakuja usiku huu huu, nikifika nitakujulisha ndugu
yangu.”
“Sawa kaka, pole sana ndiyo maisha.”
“Ahsante.”
Alipokata simu akamgeukia Master akiwa anatabasamu.
“Vipi kaka?”
“Tayari!!!”
“Niambie....”
“Kashakufa nyang’au yule, lakini inaonekana ni kwa ajali ya bahati mbaya, maana
taarifa zinasema hata Roy hana hali nzuri.”
“Hana hali nzuri?”
“Ndiyo!”
“Duh! Hapo sasa lazima tuwe makini....nimesikia ukiambiwa kitu kama hajarejewa
na fahamu siyo?”
“Ndiyo!”
“Ni hatari, anaweza kuzinduka na kujikuta akianza kutoa siri yetu, lazima tuwe
wajanja hapa kaka.”
“Tufanyeje sasa?”
86
“Anatakiwa kuhamishwa hospitali usiku huu huu.”
“Wataturuhusu kweli?”
“Pesa itaongea....”
Gari mbili aina ya Land Cruiser usiku huo huo zilitoka kuelekea Morogoro. Moja
ikiwa imewabeba Gerald na Master wakiwa wanaendeshwa na dereva wao na
lingine likiwa limebeba vijana wa Master. Kwa mwendo wao mkali, saa mbili tu
baadaye walikuwa wameshafika mjini Morogoro.
Wakafikia katika Hoteli ya Mount Uluguru, wakafanya malipo kisha wakarudi
kwenye magari. Safari yao ikaishia Kahumba Night Club, wakatafuta kona nzuri
wakakaa na kuanza kutunga sheria.
“Mzee mzima tunafanyaje hapa?” Gerald akamwuliza Master.
“Hili zoezi ni jepesi, anayehusika zaidi hapa ni wewe, mpigie rafiki yako kisha
muende hospitalini, muone daktari wa zamu, halafu mweleze shida
yako...uzungumze vizuri, naamini atakusaidia...hakikisha Roy anatoka hospitalini
usiku huu.”
“Poa poa, baadaye...” Gerald akaamka na kuacha bia yake mezani, akaliendea gari
na kuingia.
Dakika mbili badaye, alikuwa kwenye kona ya kuelekea kwenye geti la hospitali
ya mkoa, eneo la Posta. Hapo akachukua simu yake na kumpigia Jerome...
“Nimeshaingia mjini kaka.”
“Kweli unaendesha, upo wapi?”
“Nakaribia getini.”
“Getini kwangu au hospitalini?”
“Hospitalini!”
“Ok! Nakuja, sipo mbali sana na hapo... nipo Bwalo, baada ya dakika mbili tu
nitakuwa hapo!”
“Sawa mkuu wangu!”
Muda huo haukupita Jerome alikuwa ameshafika, wakaongozana hadi ndani ya
hospitali. Wakashuka na kwenda hadi wodini. Wakaomba kuonana na daktari wa
zamu. Huko kazi kubwa iliyofanyika ilikuwa kumuomba awaandikie charge ya
kuwaruhusu waondoke na mgonjwa wao.
“Kwanini mnataka kufanya hivyo lakini?”
“Tunataka kumwamishia kwenye hospitali kubwa zaidi.”
“Lakini hali yake siyo nzuri, hajazinduka bado, kwanini msisubiri kwanza?”
87
“Yote hayo tunayafahamu dokta, lakini tunaomba sana msaada wako....” Gerald
akasema.
“Hapana…siyo taratibu za hospitali yetu, mgonjwa bado anahitajika kuwa na
uangalizi mkubwa.”
“Najua, lakini lengo ni kuhakikisha anapata huduma bora zaidi.”
Baada ya mazungumzo marefu, huku Jerome akitumia umaarufu wake mjini,
walikubaliwa kuondoka na mgonjwa wao usiku ule ule, akiwa hajarejewa na
fahamu. Jerome hakufahamu kitu chochote kilichokuwa kikiendelea, baada ya
kupewa mgonjwa wao, Jerome akaenda zake nyumbani na kumwacha Gerald
akiendelea na safari yake.
“Nimefanikiwa mkubwa,” alikuwa ni Gerald akimwambia Master.
“Safi sana, sasa atakuwa chini ya uangalizi wetu.”
“Kweli kabisa.”
Wakamhamishia katika hospitali moja ya binafsi mjini humo. Gerald na Master
wakarudi Dar usiku huo huo, vijana wa Master wakalala Mount Uluguru.
******
Davina akiwa kwenye foleni akielekea kazini asubuhi hiyo, muuza magazeti alipita
na kumwita. Kama kawaida yake, alinunua magazeti yote ya siku hiyo. Magazeti
karibu yote yalikuwa na habari ya ajali iliyotokea usiku wa kuamkia siku hiyo,
jirani na Mikese nje kidogo ya Morogoro.
Alipokazia macho gazeti moja, alishtushwa kuona picha ya maiti ambayo ilikuwa
imevaa nguo kama alizokuwa amevaa Jeff mara ya mwisho wakati wakiagana kwa
safari ya kwenda Dodoma. Alipoamua kuisoma vizuri habari ile, alishindwa
kuamini, kwani aligundua kwamba mpenzi wake Jeff, alifariki dunia!
“Noooooooooo.....” alitoa sauti hiyo kali, kisha akaangukia usukanu.
Akapoteza fahamu!
Kilichofuata baada ya taa kuruhusu, ilikuwa ni honi mfululizo! Hakuna aliyejua
kwamba Davina alikuwa amezimia!
Jeff alishuka kwenye basi akiwa mchovu sana usiku huo, si wa mwili bali wa
mawazo yanayomtatiza na kumnyima raha kabisa. Alikuwa akiumizwa na jinsi
alivyotakiwa kuanza kuishi maisha mapya yenye kifungo cha kila aina.
Baada ya kushuka kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani, Msamvu mjini
Morogoro, alivuka barabara hadi ng’ambo ya pili kwenye keep-left cha Msamvu.
88
Hapo akaingia kwenye taxi iliyokuwa imeegesha barabarani, ikionekana kuelekea
mjini.
“Mia tano bro ingia, wakifika abiria watatu tunaondoka,” alisema dereva wa taxi
akimkaribisha Jeff.
“Nataka kukodisha mwenyewe, itawezekana?” Jeff akasema kwa sauti tulivu sana.
“Pochi lako tu kaka, sema unakwenda wapi?”
“Nahitaji Gesti yoyote ya bei poa, lakini isiwe nje ya hapa Msamvu na Mji Mpya!”
“Sawa, ipo ninayoifahamu Mji Mpya...bei poa na imetulia, inaitwa Marangu Guest
House, naamini patakufaa sana.”
“Kiasi gani hadi hapo?”
“Elfu na mia tano!”
“Twende.”
Dereva akawasha gari na kuliondoa kwa kasi, dakika moja na sekunde chache
baadaye, alikuwa anakatisha kushoto kwake, jirani na Kituo cha Polisi Mji Mpya,
akiifuata barabara ya vumbi. Dakika moja mbele, alikuwa anaegesha mbele ya baa
hiyo yenye Gesti. Akashuka haraka na kumpatia yule dereva kiasi cha shilingi elfu
mbili, alipotaka kumrudishia chenji yake, Jeff akakataa.
“Utakunywa soda kaka.”
“Ahsante.”
Mguu wa kwanza, mguu wa pili hadi Mapokezi alipochukua chumba na kuingia
ndani kisha kufunga mlango. Bado alikuwa na mawazo lukuki kichwani mwake,
alitakiwa kuwaza jinsi atakavyoanza kuishi maisha mapya ambayo hakuyazoea
kabisa. Alijifungia ndani hadi saa nne na nusu alipotoka nje na kuagiza chips na
nyama choma, akala.
Akaomba kupewa pombe kali na kuingia nayo chumbani. Hiyo ndiyo ikawa dawa
yake ya usingizi!
*****
89
Pamoja na pombe aliyokunywa, aliweza kudamka alfariji sana siku iliyofuata.
Akakimbia bafuni kujimwagia maji, kisha akarudi chumbani kuvaa. Hapo sasa
alitakiwa kuvaa nguo zake za kazi! Alivaa suruali nyeusi ya jeans, kisha akavaa
t.shirt nyeupe na juu yake akavaa jaketi kubwa, kichwani akiwa na kofia aina ya
pama!
Baada ya kukamilisha zoezi hilo, akakusanya nguo zake na vitu vingine vyote
kisha akatoka tayari kwa safari ya kwenda kituoni kutafuta usafiri. Ikiwa ni saa
12:00 za asubuhi, alitembea mwenyewe hadi barabara kubwa, ndipo kulipoanza
kupambazuka kidogo na kupishana na magari ya abiria.
Akaamua kutembea taratibu kwa miguu hadi kituoni, akakata tiketi ya kwenda
Mwanza. Tiketi yake ilionesha wazi kwamba gari lingeingia Morogoro saa 2:30,
hivyo muda huo akautumia kupata kifungua kinywa kisha kusubiri gari. Kama
alivyopata maelekezo, muda huo ulipofika, basi liliingia kituoni, mara moja Jeff
akapanda na kuketi kwenye siti yake.
Dakika chache sana kabla basi halijaondoka kituoni, Jeff aliamua kununua
magazeti ya siku hiyo, huo ulikuwa utaratibu wake siku zote. Wakati gari linaanza
kuondoka Morogoro, Jeff alikuwa amekazia macho gazeti moja lililoandika
kuhusu ajali iliyotokea hapo Morogoro.
Alipotizama picha ya maiti juu ya gazeti, ilikuwa imevaa nguo zake alizokuwa
amevaa jana. Akaamua kuisoma habari nzima! Akashtuka sana...habari ilikuwa
kwamba yeye amefariki dunia!
Haikuwa habari mpya sana, maana aliitarajia, lakini kidogo ilimshtua. Ilimpa
mshtuko kwa sababu kubwa mbili; kwanza ajali iliyotokea inaonekana si ile
iliyopangwa awali na habari iliandikwa wazi kwamba Roy alikuwa na hali mbaya
Hospitali ya Mkoa. Pili, alishindwa kuelewa jinsi mpenzi wake Davina
atakavyopokea habari za kifo chake.
Anamjua vizuri sana Davina...
Akarudisha kumbukumbu zake, jinsi Davina wake anavyompenda,
anavyomthamini, asivyoweza kuishi bila yeye, akakumbuka jinsi ilivyokuwa
imebaki muda mfupi kabla ya ndoa yao. Bila hiyari yake, machozi yakaanza
kumiminika machoni mwake!
90
Ghafla akachanachana magazeti yote na kuyatupa nje kupitia dirishani. Kila mtu
alimshangaa sana, wapo waliomuuliza, lakini hakuwa tayari kuwajibu. Faraja yake
ilikuwa machozi. Njia nzima alilia...
Hakuna aliyejua sababu!
91
SURA YA KUMI
92
waliofikisha taarifa kwa wazazi wake. Mtu wa mwisho kumtafuta alikuwa ni
Davina, lakini kitu cha ajabu, simu yake ilipokelewa na mtu mwingine, tena
mwanaume!
Gerald akashtuka sana!
Asubuhi yote hii?!
“Nani mwenzangu? Siwezi kuongea na mweye simu?” Gerald aliongea maneno
hayo haraka-haraka.
“Samahani ndugu, ni Hospitali ya Taifa Muhimbili hapa...mimi ni Daktari.”
“Muhimbili Hospital?”
“Yeah!”
“Kuna nini tena?”
“Huyu binti ni mgonjwa, ameletwa hapa asubuhi hii baada ya kupoteza fahamu
akiwa anaendesha gari. Hali yake kwasasa si mbaya sana, unaweza kuja
kumwona.”
“Ok!”
Gerald akakata simu akiwa amechanganyikiwa sana.
Bila kumweleza mtu yeyote taarifa za Davina, Gerald aliingia garini haraka na
kuondoka kwa kasi kwenda Muhimbili, akamkuta Davina akiendelea kupatiwa
matibabu. Kilichofanyika ilikuwa ni kuacha fedha za kutosha na kuomba Davina
aendelee kuhudumiwa vyema.
Taarifa zikaenea kwa kasi sana, mchana wa siku hiyo Gerald alikuwa njiani
akielekea Morogoro, akaenda Polisi na kukamilisha taratibu zote, gari lake
lilikuwa limeharibika vibaya, lakini kwake yeye halikuwa tatizo kubwa, alichotaka
kwa wakati huo ilikuwa ni Davina tu.
Baada ya hapo akaenda Hospitalini kushughulikia taratibu nyingine, saa kumi
alasiri, ndugu wa Jeff wakaingia hospitalini, kwakuwa walikuwa
wameshawasiliana, zikafanyika taratibu zote kisha mwili wa Jeff ukachukuliwa na
kupelekwa Dar es Salaam katika chumba cha kuhifadhia maiti ya Hospitali ya
Taifa Muhimbili.
93
Msiba ukawekwa nyumbani kwa wazazi wake na Jeff Kimara. Kutokana na hali
mbaya aliyokuwa nayo, ilipangwa azikwe alasiri ya siku inayofuata. Gerald
hakutulia kabisa, akarudi hospitalini usiku, kwa bahati nzuri alimkuta Davina
akiwa amerejewa na fahamu!
Davina alilia sana!
“Shem, mpenzi wangu amekufa shem...sitamuona tena Jeff wangu
jamani....kwanini lakini? Kwanini imekuwa hivi?” Davina alilia sana akiwa
amemkumbatia Gerald.
“Tuliza moyo shem, jikaze ili uruhusiwe asubuhi angalau ushiriki maziko yake,
maana anazikwa kesho, jipe moyo....haya ni marajibu ambayo lazima ukubaliane
nayo. Tulia shemeji yangu,” Gerald akasema akiwa amezidi kumkumbatia Davina.
Kila mmoja alikuwa akihisi tofauti moyoni mwake, Davina alikuwa akilia kwa
hisia na alimkumbatia Gerald kwa hisia za majonzi, lakini kwa Gerald ilikuwa
tofauti, joto la Davina lilimburudisha kimahaba, alikuwa anasubiria mambo yaishe
ili aweze kutimiza ahadi yake, kumnasa Davina!
Siri iliyokuwa nyuma ya kifo cha Jeff hakuijua! Yeye aliamini amemuua Jeff kwa
siri, lakini Jeff mwenyewe alikuwa na siri ya kifo chake.
Siri ndani ya siri!
Siri sirini!
Kama Davina angeweza kujua kilichokuwa ndani ya Gerald, bila shaka angepata
nguvu za ajabu na kumsukuma pembeni. Gerald hakuwa mtu mzuri kabisa kwake,
alikuwa muuaji wa mchumba wake. Siri hii hakuijua kabisa.
Gerald aliendelea kumng’ang’ania Davina ambaye hakuweza kujua kama
mwenzake alikuwa akijisikia faraja kukumbatiwa na mwanamke mrembo kama
yeye. Akilini mwake alijua alikuwa anapewa pole kutokana na matatizo
yaliyomkuta, lakini ukweli haukuwa huo, Gerald alikuwa na kitu tofauti kabisa
moyoni mwake.
“Jikaze shem, ndiyo maisha.”
“Lakini Gerald imekuwa mapema sana, mapema sana kwa Jeff wangu kufa!”
94
“Usiseme hivyo, kazi ya Mungu haina makosa.”
“Najua, lakini angeniachia basi angalau nifunge naye kwanza ndoa halafu ndiyo
amchukue, imekuwa haraka sana.”
“Ukisema hivyo Davina utakuwa unakufuru, kazi ya Mungu haina makosa Davina.
Kumbuka kwamba, sote tunaelekea huko huko, kinachoonekana hapa ni nani
anatangulia na nani anafuata, lakini wote njia yetu ni moja.”
“Usijali, nashukuru kwa kunipa moyo, ingawa lazima ufahamu kwamba kifo cha
mpenzi wangu kinaninyima raha sana, yaani nakosa amani ya moyoni kabisa...”
Davina alisema huku akionesha simanzi tele.
“Haya ni majaribu ya maisha Davina. Kila chenye uhai lazima kionje mauti,
isitoshe, kila kinachozaliwa lazima kitakufa. Jipe moyo, ujitulize katika kipindi
hiki kigumu, maana hata kama utahangaika na kulia wakati wote, haitasaidia kitu,
maana utakuwa unajiumiza mwenyewe.”
“Nashukuru sana kwa kunipa moyo...ahsante sana.”
“Jitahidi ili kesho nawe, upate nafasi ya kutupia udongo kwenye mwili wa mpenzi
wako!”
“Nitajitahidi.”
Waliendelea kuzungumza mengi ya kupeana moyo, hadi muda wa kuwasabahi
wagonjwa ulipoisha, Gerald akaondoka zake.
******
Saa 5:30 za usiku, basi liliingia jijini Mwanza, wasafiri wakiwa wachovu sana
baada ya mwendo wa saa takribani kumi na sita wakitokea Dar es Salaam hadi
Mwanza. Jeff alishuka akiwa mchovu sana, mwenye koti lake kama kawaida na
kofia yake ya pama.
Hakuwa mgeni sana Mwanza, aliwahi kuishi miaka ya nyuma wakati akisoma
elimu yake ya Seekondari, hivyo hakuwa mgeni sana katika mitaa ya Mwanza.
Alichokifanya baada ya kushuka kwenye basi ni kuingia kwenye taxi moja kwa
moja.
95
“Mwanza Hotel!” Akasema mara moja kisha akatulia akiwa mwenye mawazo tele.
“Sawa brother...karibu Mwanza,” dereva yule akasema.
Jeff hakuitika!
“Bro!” Akaita tena.
“Unasema?” Jeff akajibu kwa kugutuka kidogo.
“Karibu jijini Mwanza.”
“Mimi si mgeni hapa.”
“Samahani kama sikukufurahisha na swali langu!”
“Usijali.”
“Lakini maana yangu ilikuwa kwamba, hata kama wewe ni mwenyeji wa hapa,
sasa umerudi safari una haki ya kukaribishwa!”
“Oyaa wewe ni dereva au dalali, mbona unaongea sana? Nipeleke Mwaza Hotel
baasi, sina kitu kingine ninachohitaji kutoka kwako.”
“Ok! Samahani, sikujua kama hupendi kuzungumza.”
“Fahamu hivyo na kuanzia sasa usinisemeshe kwa chochote mpaka nifike
hotelini!”
Dereva hajibu!
Inaonekana alielewa alichoambiwa. Siku zote Jeff amekuwa mtu mwema na
mwenye kuzungumza sana na watu, lakini kwa muda huu ambao ana matatizo na
mawazo tele kichwani, alikuwa hana hamu ya kuzungumza na mtu yeyote.
Alipenda kupata muda wake peke yake.
Muda wa kuwaza mambo yake akiwa mwenyewe.
Baasi!
Walikuwa kimya mpaka walivyofika hotelini, Jeff akashuka na kutoa noti ya elfu
tano, hakutaka kujua kama pesa aliyotoa inatosha au alitakiwa kurudishiwa chenji.
Akaondoka zake na kwenda Mapokezi. Hapo akapokelewa na tabasamu mwanana
96
lililoshiba. Msichana mrembo mwenye macho ya mviringo, alimpokea kwa
shangwe!
“Habari za kazi.”
“Nzuri tu anko, za kwako!”
“Salama.”
“Karibu sana.”
“Ahsante. Nahitaji malazi.”
“Umepata, lakini tunavyo vya bei tofauti,” akasema msichana huyo akifafanua aina
ya vyumba walivyonavyo.
“Ok! Nipatie hicho cha elfu ishirini na tano!”
“Sawa!” Msichana yule akajibu kisha akachukua maelezo ya Jeff na kuyaandika
kwenye kitabu cha wageni.
Jeff alitoa maelezo ya uongo kwa kila kitu. Kwanza alijitambulisha kwa jina la
Christopher Mkumbo, akasema ametokea Singida, akadanganya kabila kwamba
yeye ni Mnyiramba na kila kitu! Hakutaka kueleza ukweli kabisa. Baada ya
kukamilisha usajili katika kitabu cha wageni, binti yule ambaye baadaye
alijitambulisha kwa jina la Queen alimpeleka chumbani kwake, ghorofa ya 4 katika
hoteli hiyo.
“Karibu sana Chris, lala unono...” Queen akamwambia akitabasamu.
“Nawe pia ulale salama.”
“Chris, silali mimi, bado nipo kazini.”
“Poa, kazi njema.”
“Ahsante.”
Queen akaondoka na kumwacha Jeff peke yake chumbani. Kwanza alivua nguo
zote, akachukua taulo na kujifunga kiunoni, akaingia bafuni kuoga. Aliporudi
akaiendea simu na kubonyeza namba za Restaurant, akaomba kupelekewa mbuzi
na ndizi choma, alipokata simu hiyo, akapiga tena baa, alipoomba mzinga mzima
wa konyagi!
97
Akajilaza kitandani mawazo tele kichwani. Pombe ndiyo ilikuwa ya kwanza
kuletwa chumbani, akaanza kunywa taratibu, imani yake ilikuwa anapunguza
mawazo. Muda mfupi baadaye, chakula kikapelekwa. Akala na kushiba kisha
akaendelea na pombe yake.
Akalewa sana!
Akalala!
Asubuhi alipoamka, aliondoka hotelini pale, lengo lake likiwa ni kutafuta Gesti ya
bei nafuu mitaani. Alitakiwa kutumia akili, kwani kama angeendelea na matumizi
mabaya ya fedha, basi angeishiwa fedha na maisha yake yangekuwa magumu jijini
Mwanza.
Akiwa mitaani, alienda kwenye meza moja ya magazeti na kuanza kupitia vichwa
vya habari katika magazeti ya siku hiyo. Gazeti moja likauchoma moyo wake,
likamwumiza na kumnyong’onyesha.
*****
Umati wa watu ulikuwa umejaa nyumbani kwa wazazi wa Jeff Kimara, katikati
kukiwa na jeneza lenye mwili wa marehemu Jeff. Ibada ya mazishi ilikuwa
ikiendelea. Ndugu wa Jeff walikuwa wanalia sana, baba yake mzazi, mama yake,
wadogo zake na ndugu wengine walikuwa na sura iliyojaa majonzi tele.
Davina muda wote alikuwa amekaa sehemu moja na Gerald, ambaye alionekana
kumfariji sana. Wafanyakazi wa KSQ walikuwa wanalia muda wote, kifo cha Jeff
kiliwahuzunisha wengi sana. Kiliwachoma wengi na kuwaachia simanzi nzito.
Watu wote wakiwa kimya kabisa, mshereheshaji wa maziko hayo, akasogea mbele
akionekana kuwa na tangazo muhimu sana. Akasogeza kipaza sauti karibu yake,
kisha akaanza kuzungumza...
“Ndugu zangu wafiwa, majirani na wote ambao mnahusika kwa namna moja ama
nyingine na msiba huu wa mpedwa wetu Jeff Sebastian. Tunasikitika kwamba,
wakati tukitoa heshima zetu za mwisho, hatutaweza kumuona, kwasababu
ameharibika vibaya sana usoni na kichwa kizima kwa ujumla. Utaratibu
utaotumika ni kufika mbele ya jeneza lenye mwili wa mpendwa wetu, kisha
kuligusa na kupita kabla ya safari ya kwenda makaburini,” Mshereheshaji huyo
alisema kwa sauti ya taratibu sana.
98
Kilio kikaibuka upya!
Watu wakapita mbele ya jeneza kama utaratibu ulivyotangazwa kisha baadaye
jeneza linabebwa na kupelekwa makabuni. Jeneza lenye mwili wa marehemu Jeff
likashushwa kaburini, waombolezaji wakapita mbele ya kaburi na kutupia
mchanga!
Simanzi tele!
Davina naye akapita akiwa ameshikwa na Gerald, wakatupia mchanga na
kuondoka! Watu wakalia sana. Jeff alikuwa bado kijana mdogo, kifo kilimchukua
akiwa na ndoto nyingi sana maishani mwake. Watu walilia sana!
Kila mtu akaamini huo ulikuwa mwisho wa maisha ya Jeff!
Siri iliyokuwa nyuma ya pazia, hakuna aliyeijua. Si Nyamangumu Camp wala
Gerald. Walijua watu watatu tu; Roy, Kijasho na Jeff mwenyewe.
Jeff si marehemu!
Yupo Mwanza!
*****
Jeff aliyatuliza macho yake juu ya gazeti hilo huku akihisi machozi kuanza
kudondoka! Alitakiwa kutulia sana na kujikaza ili machozi yasidondoke maana
kwa hali aliyokuwa nayo ilikuwa vigumu sana kuyazuia machozi yake. Habari ile
ilimchoma moyo!
Ilikuwa imeandikwa gazeti la Uwazi, ikiwa na maandishi makubwa kwa wino
uliokolezwa MSHTUKO! Chini ya maneno hayo, kulikuwa na mandishi mengine
madogo yaliyosomeka; Mchumba wa marehemu Jeff wa KSQ azimia kwenye
foleni, nusura asababishe ajali nyingine, Marehemu Jeff kuzikwa leo Kimara!
Ilikuwa habari mbaya sana kwake, haikuwa mbaya kwa maana ya mpya, lakini
alijaribu kuchukua taswira nzima ya wazazi wake, wadogo zake, ndugu zake
wengine na Davina wake, akachanganyikiwa!
Alishindwa kuelewa ni kiasi gani wangekuwa na huzuni muda wote. Hakuweza
kuitafsiri kwa haraka jinsi nyumbani kwao kutakavyokuwa! Akatoa pesa mfukoni
na kununua gazeti hilo kisha akaondoka zake.
Akatafuta sehemu iliyotulia na kuanza kusoma habari ile kwa makini, kila
aliposoma mstari mmoja ndivyo alivyozidi kulia. Jeff akagundua kitu kingine
tofauti kabisa, aligundua kwamba Davina wake alikuwa akimpenda sana. Moyo
wake ukazidi kuumia na kuugua kwa maumvu makali yasiyopona kwa urahisi.
99
“Kwahiyo mama yangu, atakuwa analia akijua nimekufa kumbe nipo hai...baba
naye atakuwa analia...Davina wangu hadi amezimia akijua nimekufa kumbe nipo.
Kwanini inakuwa hivi lakini? Kwanini jambo hili linatokea kwangu?” Jeff
alijisemea moyoni mwake akizidi kulia.
Hapo sasa akajua kwamba Gerald alikuwa mtu mbaya tena asiyefaa kabisa katika
jamii ya watu wastaarabu. Gerald ni muuaji tena asiye na huruma. Alimchukia
sana na hakuwa na hamu naye kwa namna yoyote ile.
“Lakini lazima siku moja nitafanya kitu...siwezi kumuacha Gerald. Mawili,
nimuue kwa mkono wangu mwenyewe au aozee jela! Yote haya yanawezekana,
lakini nitatulia na kuangalia lipi ni bora zaidi ili nianze nalo. Geraaaaaldiiiiiiiiiii....”
akajikuta amepayuka na kujipiga-piga kifuani.
Ghafla mvua ya machozi ikaanza kumiminika machoni mwake. Machozi kwake,
sasa ikawa ndiyo faraja yake!
*****
“Nakufaaaaaaa...” ndiyo neno la kwanza Roy kutamka siku nne baada ya ajali ile
kutokea.
Ilikuwa ni siku mbili baada ya Jeff kuzikwa. Kwa bahati nzuri, alizunduka mbele
ya vijana wa Nyamangumu Camp, kwa hiyo haraka wakajitahidi kumpa taarifa za
kila kitu kilichotokea na kumbukumbu zake kurejea vyema.
“Kwahiyo tulia, Jeff alikufa!” Alex, mmoja wa vijana wa Nyamangumu
akamwambia.
“Alikufa?”
“Ndiyo, shaka ondoa.”
“Kama ndivyo basi poa.”
Ilikuwa kazi kubwa kidogo kwa Roy kurejewa na kumbukumbu zake haraka,
lakini alijitahidi kuzirudisha polepole, akakumbuka picha nzima. Kabla hajarejewa
na kumbukumbu zake vyema, alikuwa hataki kuzungumza kitu chochote,
alipokumbuka kila kitu, akaelewa mchezo mzima!
Kubwa alililoshukuru ni kwamba hakuna mtu yeyote aliyetilia mashaka ajali ile,
walijua ilikuwa ajali ya kawaida, ya bahati mbaya, maana walipanga kumuua Jeff
njiani wakiwa wanakaribia kabisa kufika Dodoma, lakini hakuna aliyelaumu,
kwasababu kama ni suala la Jeff kufa, tayari alikuwa marehemu tena amelala
kaburini!
*****
100
Siku kumi baadaye Roy alikuwa ameshapona kabisa, akarudishwa Dar es Salaam,
kwenye Makao Makuu ya Nyamangumu Camp. Kiongozi wao Master alikuwa
aamekaa mezani akimwangalia Roy huku akitabasamu.
“Hongera Kamanda, kazi yako nimeikubali, lakini pole kwa matatizo yaliyokupata,
naamini ile ajali haikuwa ile tiliyopanga, lakini tushukuru kwamba wewe ni
mzima.
“Unatakiwa kuendelea kufanya kazi kwa Gerald mpaka hali ya hewa itulie.
Endelea kuwa mchapakazi na usioneshe dalili zozote za kujua ukweli wa kifo
chake, kwanza hakuna boya yeyote aliyeshtukia mchezo. Sawa?!”
“Sawa Mkuu!”
“Kuhusu pesa usijali, mchana nikitoa benki utafurahi, ila kesho nenda karipoti
kazini.”
“Nimekuelewa Mkuu.”
Wakatawanyika.
******
Vilio vikaibuka upya ofisini kwa Gerald, asubuhi hiyo Roy alipowasili kazini,
alisababisha watu walie sana. Kila walipomwangalia walimkumbuka marehemu
Jeff. Kila mtu alimpa pole. Baadaye wafanyakazi wakatulia na kutawanyika.
Siku zikazidi kwenda, Gerald akizidi kumpongeza Roy kila siku kwa kazi
aliyoifanya, lakini moyoni mwa Roy alikuwa hana amani kabisa. Alihisi kufanya
makosa makubwa sana. Ile haikuwa siri tena, tayari alishaanza kumhisi Kijasho
tofauti!
“Kijasho akinisaliti tu, hapa NAUAWA! Na mimi sipo tayari kufa....so what to do
now?! I have to kill him....stooop!” Roy akasema akionekana kuwa na mawazo
sana.
“Ndiyo lazima Kijasho afe, ataniharibia....” Roy akawaza huku kichwa chake
kikianza kupanga mauaji yake.
****
Roy anaendelea kuwaza jinsi atakavyoweza kuondoka kikwazo kilichopo mbele
yake, Kijasho! Ni kweli Kijasho naye alikuwa muuaji mzoefu, mwenye kutunza
siri, lakini si hii ya Nyamangumu ambayo hata mkuu wake wa kazi Master alikuwa
haifahamu.
101
Ilikuwa lazima ahakikishe uhai wake unakatishwa. Lazima. Kama angeacha
kufanya hivyo, basi kulikuwa na hatari ya siri hiyo kuvuja, jambo ambalo kwa
hakika hakutaka kabisa kuliruhusu litokee. Ilikuwa ni hatari kubwa sana kwake.
“Kijasho anatakiwa kufa, lazima afe!” Akawaza akiwa bado hajapata mbinu za
kufanya mauaji yake.
“Lakini mimi najiamini, lazima niwe mjanja, mbinu za mauaji nazifaha vizuri
sana. Kijasho anatakiwa kufa kama wengine wanavyokufa, tofauti hapa ni moja tu;
Kijasho atakufa kwa siri, wakati vifo vingine Camp ilikuwa inajua baaasi...”
aliendelea kuwaza huku ubongo wake ukigoma kabisa kufungua njia ya kumaliza
tatizo lile.
“Njia itapatikana tu, acha niende zangu nyumbani, najua itapatikana tu. Mimi
ndiyo Roy Maketo!” Akawaza akisimama na kwenda ofisini kwa Mkurugenzi
Gerald.
“Sema Maketo,” Gerald akasema baada ya Roy kuingia ofisini kwake bila hodi!
Roy hakujibu!
Akaketi!
“Kamanda wangu...niambie kaka, shwari?”
Bado Roy alikuwa kimya.
“Najua unataka kuchomoka, sasa acha tugawane hivi visenti kwanza, halafu
mambo mengine tutajua mambo mengine baadaye,” Gerald akasema akiatoa
bahasha ya khaki kwenye mfuko wa ndani wa koti.
Akaanza kuchambua noti za elfu kumi-kumi!
Akachomoa noti thelathini na kuziweka mezani.
Roy akatengeneza tabasamu!
“Mimi naondoka, tutaonana kesho,” Roy akasema akichukua zile fedha pale
mezani.
Akasimama.
Akaondoka zake!
Gerald akabaki kumsindikiza kwa macho hadi alipofunga mlango na kuubamiza
tena. Ukjalia puuuuu! Gerald akatingisha kichwa, kwa mbali alihisi Roy alikuwa
na matatizo yanayomchanganya.
Kuwa na matatizo si jambo geni katika maisha, lakini alipata wakati mgumu sana
kuwaza kwamba alikuwa na tatizo gani. Wazo la kwamba kifo cha Jeff kilikuwa
kikimchanganya hakuwa nalo, maana kama ni suala la kuua, kazi iliyomuweka
mjini ilikuwa hiyo! Kuondoa uhai wa watu ili yeye atajirike.
102
Anasumbuliwa na nini sasa? Likabaki kuwa swali lisilo na majibu. Mwenye
majibu alikuwa mmoja tu, Roy! Akabonyeza jina la Roy kwenye simu yake. Sauti
ya upande wa pili ikasikika...
“Kaka vipi?”
“Shwari!”
“Nahisi kama haupo sawa, una tatizo lolote?”
“Nipo poa.”
“Sisi wamoja kaka, if there’s something wrong, just tell me nikusaidie, usibaki
kimya na tatizo ndugu yangu!”
“Worry out men, I’m okay!”
“Basi sawa, tutaonana kesho ofisini.”
“Sawa boss!”
Simu ikakatika.
103
SURA YA KUMI NA MOJA
JIONI hii, Baa ya Penny Pub ilikuwa imetulia sana, ilikuwa na watu wachache
kuliko kawaida ya siku nyingine. Hili halikuwa jambo la kushangaza sana hasa
kutokana na ukweli kwamba ilikuwa Jumatatu.
Kwenye meza ya pembeni kabisa, Roy alikuwa amekaa kwa utulivu sana, mezani
kukiwa na chupa kubwa ya pombe kali, mkononi akiwa na sigara yake ambayo
aliivuta kwa mapozi huku akitolea moshi puani na masikioni.
Ilikuwa siku yake ya burudani, pamoja na kwamba aliamua kustarehe, lakini suala
la atataumia mbinu gani ili aweze kumuua Kijasho, bado liliisumbua sana akili
yake.
Mara akapeleka mkono wake mezani, akachukua glasi yake yenye pombe kisha
akaipeleka kinywani, akaukunja uso kidogo akisikilizia uchungu wa kinywaji kile.
Alipoishusha ile glasi chini, alikuwa akitabasamu!
Tabasamu mwanana!
Tabasamu la ushindi!
“Yes, nimeshapata njia, tayari! Sasa nitamuua Kijasho kirahisi sana...” akasema
kwa sauti kidogo akitabasamu.
Akachukua simu yake, kisha akatafuta namba za Kijasho, alipozipata akabonyeza
kitufe cha kupiga haraka, halafu akaikimbiza sikioni kwa pupa. Kitambo kidogo,
sauti ya Kijasho ikasikika.
“Sema mkubwa, upo?”
“Niende wapi ndugu yangu, vipi Moro shwari?”
“Tunapambana tu, kaka sema dili huku ziii, nyie wa town huko najua ni bata kwa
kwenda mbele!”
“Siyo kiivyo kaka!”
“Nipe mchongo!”
“Ni kweli nina mchongo, ndiyo maana nimekupigia usiku huu. Kifupi nina milioni
mbili zako hapa, ambazo kama unazitaka hata sasa hivi naweza kukupa.”
“Usitake nifunge hiki kibaa hapa Kihonda, niwaambie watu wanywe pesa nalipa
kesho, enheee lete mwanga sumu hiyo!”
“Kuna dili, kesho jioni nakuja, tena na pesa yako kabisa, mchongo mzima hiyo
kesho!”
“Poa, ahsante sana kwa kunipa dili.”
104
“Usijali.”
*****
Siku iliyofuata saa 1:20 za usiku gari ndogo aina ya Mark II Baloon ilikuwa
inaegesha eneo la Masika, pembeni kwa keep left cha Masika, mvua za rasharasha
zikiendelea kunyesha. Ndani ya gari hilo alikuwemo Roy Maketo ambaye alifika
mjini hapo kwa kazi moja tu; mauaji!
Mauaji ya Kijasho.
Tayari giza lilishaanza kuchukua nafasi na mwanga kwenda zake kusubiri siku
mpya! Muda mfupi tu baada ya kuegesha eneo hilo ambalo ni jirani kabisa na
Kituo cha Taxi, simu ya Roy ikaita, macho yake kwenye kioo, jina la Kijasho
likaonekana.
Akapokea haraka; “Nimeshafika kaka, uko wapi?”
“Fungua mlango, nimeshakuona.”
“Ok! Njoo.”
Muda mfupi baadaye mlango ukafunguliwa, Kijasho akaingia na kuketi. Si Kijasho
wala Roy aliyeongea neno lolote, Roy akanyoosha mkono wake siti ya nyuma,
akatoa bia mbili za kopo, akazifungua zote na kumkabidhi moja Kijasho.
“Karibu kaka.”
“Ahsante,” Kijasho akasema akiipeleka kinywani ile bia.
Roy naye akaanza kunywa yake. Bia ikiwa mkononi mwake, akaliondoa gari
lililokuwa silence, akashika barabara inayoelekea kwenye keep left cha kuelekea
Barabara ya Boma na ile ya Sabasaba, alipofika keep left akakata kushoto kuifuata
barabara inayoelekea Posta, akaendesha gari kwa mwendo wa taratibu mpaka
alipofika darajani na kukata kulia akielekea Uwanja wa Jamuhuri. Akaegesha gari
jirani kabisa na uwanja.
“Kaka hapa noma, huoni majangu wapo pale?” Kijasho akamwambia Roy
akimuonesha kwa kidole Kituo Kikuu cha Polisi.
“Acha uoga kaka, siku zote huwezi kudhamiwa mbaya ukiwa sehemu iliyo chini
ya usalama,” Roy akasema akitabasamu.
Muda huo huo akatoa bahasha yenye fedha na kumkabidhi Kijasho. Akaanza
kuhesabu akitabasamu.
“Zipo sawa kaka, ni milioni mbili taslimu!”
“Ok!, sasa twende tukafanye kazi.”
“Wapi?”
105
“Utapajua tukifika.”
Roy akaondoa gari taratibu hadi barabara kubwa, akakata kulia akielekea Kilakala.
Baada ya mwendo wa dakika tano tu, Kijasho alikuwa ameshalala kwenye siti.
Roy akaegesha gari pembeni kidogo. Akaanza kumtingisha kwa nguvu, lakini
hakujigusa!
“Tayari huyu...” Roy akasema akitabasamu.
Ilikuwa kazi ya sumu, bia aliyokunywa Kijasho ilikuwa na sumu, jambo ambalo
Kijasho hakulitambua. Roy akawasha gari na kuliondoka kwa kasi. Aliendesha
kwa kasi ile ile hadi alipofika eneo la Mvua, akapanda milimani na kutafuta
sehemu ya pori dogo. Hakutaka kuiamini sana ile simu. Akakishika kichwa cha
Kijasho vizuri, akakizushusha mara moja kwa nguvu. Ukasikika mlio mdogo wa
kwichwaaa!
Kikawa kinaning’inia!
Alikuwa marehemu.
Akachukua zile fedha mfukoni mwake na kumtupa porini!
“Nisamehe rafiki yangu Kijasho, sikuwa na njia nyingine ya kukufunga mdomo,
lazima ungeniharibia. Pumzika salama rafiki...” Roy akasema akipiga hatua
kulifuata gari lake.
Morogoro haikuwa sehemu salama tena kwake. Akaliondoa gari kwa kasi.
Alikuwa akirudi Dar es Salaam.
“Kazi imeisha!” Roy alisema akipiga usukani
***
Roy aliingia Dar usiku sana, akaenda moja kwa moja nyumbani kwake. Asubuhi
na mapema, kama kawaida akaenda zake kazini. Akaendelea kama kawaida na
majukumu yake. Moyoni mwake akiwa na siri nzito, hakutaka kupoteza hata siku
moja nyumbani, ili kuepusha ushahidi au kumuhusisha kwa namna yoyote na
mauaji ya Kijasho.
Wakati wa chakula cha mchana, hakujisikia kabisa kwenda kula, alichokifanya ni
kuomba ruhusa na kwenda nyumbani kulala, akisema kwamba anajisikia kuumwa,
ingawa ukweli ulikuwa ni kwamba, alizidiwa sana na usingizi.
Siku ya pili yake, magazeti mengi yaliandika habari za kuokokotwa kwa maiti
iliyoonekana kunyongwa! Roy alisoma karibu magazeti yote, eneo la mauaji
106
lilikuwa lile lile, Mvua! Lakini kilichomfurahisha ni kwamba, hapakuwa na dalili
zozote za kumuhusisha na mauaji yale.
“Na wala hawataweza, mimi ni kiboko!” Akawaza akijipiga-piga kifua chake
akitabasamu.
Baada ya habari hiyo kuandikwa na magazeti, siku hiyo wakazi wa Mji wa
Morogoro na Vitongoji vyake, wakafurika katika Hospitali ya Mkoa huo kutambua
mwili wa marehemu.
Hatimaye ukweli ukabainika!
Kwamba aliyekufa ni Kijasho!
Fumbo likaendelea kubaki vile vile, nani aliyemuua? Hakuna aliyejua. Mazishi ya
Kijasho yakafanyika, huku marafiki wengi wakihudhuria. Hata Roy alikuwepo.
Katika hali ya kustaajabisha zaidi, kati ya marafiki walionekana wana simanzi
zaidi ni Roy!
Alilia sana!
Lakini siri alikuwa nayo moyoni!
Kwamba yeye ndiye muuaji!
*****
Jeff alipanga katika gesti ya uchochoroni Mtaa wa Ghana ambapo alilipia shilingi
3000 kila siku. Siku zikazidi kwenda akiwa hana kazi, hapo akapata wazo la
kuhamia katika chumba chake, ndipo aliposaka chumba na kufanikiwa kupata
pango la chumba kimoja, katika nyumba ya Mzee Maige, iliyopo Nyakato.
Moyo wa Jeff ulikuwa mzito sana, lakini alikuwa tayari kuteseka kwa muda mrefu
lakini baadaye amrudishe mpenzi wake Davina mikononi mwake. Akiwa katika
chumba hicho kimoja, alichopanga katika nyumba ya mzee Maige, alilipa jumla ya
shilingi 15000 ikiwa ni fedha ya miezi mitatu, yaani kwa mwezi alilipa elfu tano!
Ukiwa ndani ya chumba hicho, unaweza kuona matundu madogo yaliyotobolewa
na misumari iliyoshikilia bati, hilo lilitosha kabisa kudhibitisha kwamba chumba
hicho kilikuwa kinavuja kipindi cha mvua.
107
Ndani ya chumba chake kulikuwa na kapeti alilotandaza chumba kizima, juu yake
akaweka godoro dogo na ndoo ya maji pembeni! Zaidi ya hapo ni begi lake dogo la
kuhifadhia nguo.
Kilikuwa chumba kwa ajili ya kulala tu, mchana anakwenda kuhangaika kutafuta
riziki Mwaloni (forodhani), jioni anarudi chumbani kwake na kujifungia. Huo
ukawa ndiyo utaratibu mpya wa maisha yake.
Siku zote alikuwa na nywele ndefu, kofia haitoki kichwani na alipenda sana kuvaa
koti wakati wote. Ilikuwa ndiyo utaratibu wake mpya, hakutaka kabisa kujulikana.
Hata jina alikuwa anatumia jipya; Sasa alikuwa anatumia jina la Christopher
Mkumbo au Chris, huku akidai yeye ni Mnyiramba wa Singida.
Wakati akiendelea kufanya kazi ndogondogo Mwaloni, pia alikuwa akihangaikia
ajira ya taaluma yake katika ofisi mbalimbali, alikuwa na sifa zote, lakini tatizo
hakuwa na vyeti. Hakutaka kuonesha vyeti vyake kwasababu hakutaka kabisa
kujulikana jina lake halisi!
Kwa bahati nzuri, akafanikiwa kupata kazi katika Kiwanda kimoja cha Samaki
jijini Mwanza, akaajiriwa kama Afisa Masoko, nafasi ambayo aliitendea haki!
Kwa miezi mitatu tu, alikuwa ameshapandishwa mishahara mara mbili.
Utendaji wake ukawafurahisha sana viongozi wake. Aliendelea kuyafurahia sana
maisha, lakini kichwani mwake aliendelea kuteswa na fikra juu ya mpenzi wake
Davina, wazazi wake na Gerald ambaye alipanga kifo chake ili aweze kumuoa
mpenzi wake.
“Lazima nifanye jambo la kuwatisha kwanza, ili Davina achanganyikiwe,
ashindwe kukubali kuolewa na Gerald, hapo nitakuwa nimecheza. Nitafanyaje?”
Akawaza Jeff akiwa bado hajapata wazo juu ya nini cha kufanya ili kutimiza azma
yake.
“Acha niombe likizo, niende Dar mara moja nikutane na Frank, anaweza kuwa
msaada mkubwa sana kwangu,” akawaza.
Kama alivyopanga, aliandika barua ya kuomba likizo kwa Meneja Mkuu wa
Kampuni na aliporudishiwa majibu, alikuwa amekubaliwa. Hakuwa na muda wa
kupoteza, akapanda basi na kwenda Dar, lakini aliingia kama alivyoondoka! Kofia
108
kubwa ya pama kichwani, ndevu alikuwa ameziachia sana na koti kubwa la kufika
miguuni!
Hata angekutana na nani, isingekuwa rahisi kugundua kwamba aliyekuwa mbele
yake alikuwa ni Jeff. Aliposhuka kwenye basi, akachukua taxi na kumwambia
dereva ampeleke Tandika, akashuka na kufika hadi kwenye nyumba anayoishi
mpenzi wake Davina.
Akasimama nje ya geti akiikodolea macho! Vitu viwili vikimsukuma kufanya
mambo tofauti, msukumo wa kwanza ulimwambia asiondoke mpaka ahakikishe
ameonana na Davina wake, lakini upande mwingine ukimwambia katu asijaribu
kukutana na Davina.
Moyo ukamuenda mbio.
Hisia kali zikamvaa.
Hisia za mapenzi!
Akabaki amesimama akiugulia moyoni. Hakutakiwa kuingia ndani, kwani kufanya
hivyo angekuwa ameshaharibu kila kitu. Alitakiwa kuwa mvumilivu sana.
Avumilie ili baadaye ale mbivu!
Zilizoiva!
Machozi ndiyo ikawa dawa yake ya muda huo, aliamini kwa kulia kungeweza
kumpunguzia machungu makali aliyokuwayo moyoni mwake.
“Lakini kwanini nateseka kiasi hiki? Kwanini? Nitaishi maisha haya mpaka lini?
Kwanini tatizo hili linakuwa kwangu tu, kwanini?” Jeff akawaza akiwa
amesimama karibu kabisa na geti la kuingia chumbani kwa Davina.
Alitamani sana kumuona Davina wake, angalau basi asikie hata sauti yake, aone
tabasamu lake. Alitamani sana kukumbatiwa na Davina, ambusu na kumpiga-piga
mgongoni, alitamani sana mambo hayo, lakini hayakuwezekana tena. Isingekuwa
rahisi kwake kupata nafasi hiyo.
Akaamua kuondoka zake, akiwa ndiyo kwanza anaanza kupiga hatua ya kwanza,
akasikia sauti ya mlango wa geti likifunguka, akasita na kusimama. Akageuza
kichwa chake nyuma kwa tahadhari, macho yakakutana na mwanamke mrembo
sana!
109
Davina!
Akasimama.
Akamwangalia mwanamke huyo akitembea kwa mwendo wa taratibu ambao,
uliweza kabisa kuonesha huzuni aliyokuwa nayo ndani mwake. Davina alionekana
dhahiri kuwa na kitu kinachomtatiza, tena kitu kizito cha kumuumiza moyo wake,
akatembea kwa madaha akionekana kuelekea dukani.
“Masikini mpenzi wangu, yawezekana hapo anawaza kwamba mimi nimeshakufa,
sipo tena duniani...kumbe nipo, tena ninateseka kwa ajili yake...” Jeff akawaza
akiendelea kumwangalia Davina aliyekuwa akizidisha kasi ya kutembea polepole.
Haikuwa rahisi kuendelea kusikilizia maumivu yale makali ya moyo. Akageuka na
kumwacha Davina andelee na mambo yake, akapiga hatua za taratibu hadi kwenye
kituo cha taxi.
Akaingia.
“Wapi?” Dereva akauliza.
“Nipeleke Sinza tafadhali.”
“Ipi?”
“Mori.”
“Mori?”
“Ndiyo, Sinza Mori, halafu nisingependa maswali zaidi, twende Mori, kama
hupafahamu sema nishuke nichukue gari lingine.”
“Napafahamu bro, hakuna tabu, nilikuwa nataka kujua sehemu unayokwenda ili
niweze kufahamu, sikuwa na maana nyingine.”
“Twende.”
Dereva akawasha gari na kuliondoa kwa kasi. Usiku huo hapakuwa na foleni
kubwa sana, hivyo dakika tano tu baadaye walikuwa kwenye mataa ya Tazara
katika Makutano ya Barabara ya Nyerere na Mandela. Akanyoosha na Barabara ya
Mandela moja kwa moja hadi kwenye mataa ya Ubungo, kwenye makutano ya
Barabara ya Morogoro na Sam Nujoma, akashika Barabara ya Sam Nujoma,
110
akaenda moja kwa moja hadi kwenye mataa ya Super Star alipokata kulia kuifuata
barabara inayoelekea Sinza Makaburini.
Hadi muda huo walikuwa hawajaongea chochote, Jeff akiwa na mawazo yake
kichwani na dereva akiwa amefuata msimamo wa mteja wake ambaye
alimtahadharisha kwamba hapendi kuzungumza sana. Mwisho wa makaburi ya
Sinza, dereva akakata kushoto kuishika Barabara ya Shekilango, akanyoosha moja
kwa moja na kupita Sinza ya Kwaremmy kabla ya kushika breki Sinza ya Mori na
kumgeukia abiria wake.
“Tunaingia ndani kidogo au utashukia hapa brother?”
“Kata kulia!”
“Tunafika hadi wapi?”
“Johannesburg Hotel.”
“Ok!”
Dereva akaondoa gari na kuifuata barabara kubwa ya vumbi, dakika moja baadaye
aliegesha gari nje ya Johannesburg Hotel. Jeff hakuzungumza neno lolote, zaidi ya
kufungua pochi yake na kutoa noti mbili; moja ya elfu kumi na nyigine ya elfu
tano, akamkabidhi jumla ya shilingi elfu kumi na tano.
“Ahsante sana brother, ahsante.”
“Usijali,” akasema akishuka.
“Sasa naweza kuchukua simu yako, ili ukihitaji usafiri siku nyingine uniite?”
Jeff hakujibu.
Tayari alikuwa anapanda ngazi fupi za hoteli ile ya kisasa na ya kuvutia! Macho
yake yakafuata kibao kidogo chenye mshale, kilichoandikwa Reception, akafuata
mshale huo mpaka alipopokelewa na tabasamu mwanana na msichana mrembo
aliyekuwa Mapokezi.
“Habari yako sister?” Jeff akasalimia kwa sauti ya upole.
“Salama tu kaka’ngu, karibu.”
“Ahsante sana, naweza kupata malazi?”
111
“Karibu sana, umeshapata.”
“Ok! Nipatie self-contained room please!”
“Umepata kaka, vyumba vyetu vyote ni self-contained, tofauti yake ni kwamba
vingine vinatumia Ac na vingine feni, halafu kuna single room na double room,
sijui ungependa kipi?”
“Nipe single self-contained room, chenye Ac!”
“Ok! Karibu sana, andikisha hapa...” yule dada wa Mapokezi akamwambia
akimkabidhi kitabu cha kuandikisha wageni.
Jeff akaanza kujaza, kama kawaida akadanganya jina lake na taarifa zake zote.
Akalipa na kupandishwa ghorofa ya tatu sehemu kilipo chumba chake, akajitupa
kitandani.
“Ooh! Thanks God....” akasema akijinyoosha.
Alikuwa amechoka sana, mara moja akaingia bafuni kuoga kisha akabonyeza
namba za Restaurant na kuomba apelekewe chakula. Akala na kulala fofofo.
112
SURA YA KUMI NA MBILI
****
Bado mawazo yake yalikuwa ni jinsi gani atakavyoweza kumpata Frank.
Aliyagandisha macho yake juu ya dari akiwa hana amani kabisa. Hakuwa na
namba zake, wala za mtu wake wa karibu, lakini pia ilikuwa vigumu kidogo
kuulizia.
Akili yake ikafanya kazi kwa kasi ya ajabu sana. Alipoyatuliza macho yake juu ya
meza mle chumbani, akaona kitabu kikubwa cha Orodha ya Wateja wa Kampuni
ya Simu na Posta. Akaanza kukagua namba za Frank, ikawa kazi kubwa sana
kuzipata.
Alipoendelea kuangalia vizuri, akafanikiwa kuona namba za Makao Makuu ya
Posta. Akaziandika haraka kwenye simu yake ya mkononi kisha akabonyeza.
Upande wa pili ukaita.
“Hallow!”
“Hallow, habari za kazi?”
“Nzuri tu!”
“Makao Makuu ya Posta, naomba nikusaidie tafadhali!”
113
“Ndipo nilipopiga, tafadhali naomba uniunganishe na Frank Maganga.”
“Frank Maganga?”
“Ndiyo!”
“Nimwambie ni nani?”
“Mwambie Moses!”
“Unapiga simu kutoka wapi”
“Mwanza!” Akadanganya.
“Ok! Subiri kidogo....” sauti ya pili ikamwambia.
Kikapita kimya kifupi, kabla ya sauti ile tena kusikika; “Hallow, yupo kwenye line,
ongea.”
“Hello Frank, vipi rafiki yangu?”
“Salama, nani mwenzangu?”
“Moses kutoka Mwanza.”
“Moses? Nadhani nimekusahau kidogo, ni Moses yupi?”
“Hapana rafiki yangu mimi siyo Moses, lakini naomba nikuambie kwanza kitu
kimoja!”
“Nini? Ni vyema kwanza uniambie wewe ni nani ili nijue nazungumza na nani?”
“Nitakuambia, lakini kabla sijafanya hivyo nataka kukueleza jambo la msingi
kwanza.”
“Ok, niambie.”
“Usiogope rafiki yangu Frank na wala usipige kelele nikikutajia mimi ni nani?”
“Mbona unanitisha? Niambie basi?!”
“Sikiliza Frank, najua unajua nimekufa, sikufa Frank, bado nipo hai na kuna
mambo ya msingi sana nataka unisaidie.”
“Lakini mbona unanichanganya? Nieleze kwanza wewe ni nani?”
“Haya, acha nikuambie, kama unavyotaka. Mimi ni rafiki yako Jeff, ambaye watu
wengi, ukiwemo wewe, wanaamini nimekufa.”
“Nani Jeff? You must be joking!” (Jeff? Lazima unatania!)
“I’m not jocking, ni mimi Jeff naongea, sikiliza nikuambie...Frank! Frank!
Frank...” Jeff aliita kwenye simu, lakini Frank hakuitika.
Hakuchukua muda mrefu sana kugundua kwamba alikuwa akiongea kwenye simu
iliyokatwa!
“Shiiiit!” Jeff akasema na kutupa simu yake kitandani.
*****
114
Frank Maganga alikuwa rafiki wa karibu sana na Jeff, lakini pamoja na ukaribu
wao, alikuwa hajawahi kumkutanisha na mpenzi wake Davina, ingawa alishawahi
kumsikia. Ni siku ya msiba wake pekee ndiyo Frank aliweza kumfahamu Davina
kwa kumwangalia kwa macho!
Hata hivyo hakuwafahamiana na wala hapakuwa na mtu wa kuwatambulisha,
maana wa kufanya hivyo alikuwa ni Jeff mwenyewe ambaye tayari alikuwa ndani
ya jeneza.
Frank alikuwa mfanyakazi wa Posta kwa miaka mingi sana, ni kijana mtaratibu
sana ambaye alisoma na Jeff kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, waliachana
wakati wakienda vyuoni kwasababu kila mtu alikuwa anasomea fani tofauti na
mwenzake. Baada ya kumaliza masomo ya chuo, wakakutana tena Dar, kila mmoja
akiwa na kazi yake!
Kazi kubwa aliyokuwa nayo Frank, ilikuwa ni kukusanya barua zote zilizotumwa
kutoka sehemu mbalimbali na kuziingiza kwenye masanduku! Hiyo ndiyo ilikuwa
kazi yake.
Asubuhi hii inakuwa chungu kwa Jeff kutokana na kukosa ushauri wa rafiki yake
huyu ambaye anaamini anaweza kuwa msada mkubwa sana wa nini afanye. Jeff
anapiga zile namba za Mapokezi kwa mara nyingine, simu ikaita na baada ya
muda, sauti ya msichana ikapokea.
Akatoa ombi lile lile; kuongea na Frank.
“Lakini ni muda mfupi uliopita nimekuunganisha naye.”
“Ni kweli dada’ngu, lakini hakukuwa na maelewano mazuri, kwa bahati mbaya
simu ikakatika.”
“Ok! Subiri kidogo, nakuunganisha moja kwa moja, sawa?”
“Nitashukuru sana,” akajibu Jeff akijitahidi sana kuficha pumzi zake zilizokuwa
zikishuka kwa kasi sana.
“Ongea, yupo kwenye line,” akasikia tena sauti ya yule dada.
Kwanza akavuta pumzi ndefu sana kabla ya kuzishusha taratibu akijiandaa
kuzungumza kwa ushawishi ili asikatiwe simu!
Moyo wa Jeff ulilipuka kwa woga, akitamani sana asikatiwe simu. Alijua ni
kwanini Frank alifanya hivyo. Ilikuwa ni vigumu sana kumuaminisha kwamba
alikuwa mzima wakati alishuhudia maziko yake. Ugumu huo hata Jeff mwenyewe
aliuona, lakini alilaumu kitendo chake cha kukataa hata kumsikiliza.
Alitamani sana apewe nafasi, hata ya dakika tatu tu ili aweze kueleza ukweli, ni
yeye pekee ndiye angeweza kuwa msaada kwake, lakini Frank haamini, haelewi!
115
Akavuta pumzi ndefu sana, kisha akazishusha taratibu sana. Akafungua kinywa
chake na kuanza na kuanza kuzungumza kwa sauti ya kusihi sana...
“Hallow, please usinikatie simu, naomba unisikilize.”
“Unajua wewe ni tapeli ambaye unataka kunihadaa kwa kutumia jina la Jeff, halafu
usivyokuwa na haya, umeiga mpaka na sauti yake ili uweze kuniibia vizuri, sasa
nataka kukuambia umekosea sana, hii ni namba nyingine kaka.”
“Unaweza ukahisi hivyo, lakini ukweli siyo huo, Frank rafiki yangu nikuambie
nini ili uamini kuwa ni mimi rafiki yake mpenzi Jeff?”
“Sema wewe!”
“Wewe ndiyo unataka nikuaminishe, sema nini ambacho uliwahi kufanya na Jeff
na unaamini kabisa mnajua wewe na yeye, nikuambie ili uamini?”
“Jeff rafiki yangu nilisoma naye kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita, sasa
kama kweli ni wewe, niambie tulisoma wapi na wapi?”
“O Level tulisoma Old Moshi Sekondari Moshi, halafu A Level tulisoma Usagara
Sekondari Tanga, wakati huo mimi nilikuwa School President!”
Frank akashtuka sana!
“Kidogo naanza kuamini, unajuaje mambo yote haya?”
“Kwasababu ni mimi mwenyewe Jeff naongea, najua una maswali mengi, lakini
mimi ndiye mwenye majibu na ndiyo sababu hasa iliyonifanya nikupigie simu.”
“Ni wewe Jeff kweli?”
“Ni mimi brother!”
“Lakini si ulikufa kaka?”
“Hapana, zile ni njama tu kaka, mimi ni mzima wa afya njema. Nina mambo
mengi sana ya kuzungumza na wewe, lakini cha msingi unatakiwa kufahamu
kwamba, kwasasa jambo hili lazima liwe siri, tukutane. Tuzungumze na kupanga
jinsi ya kunisaidia.”
“Nini hasa kilitokea?”
“Mapenzi ndugu yangu.”
“Love? What do you mean by that?” (Mapenzi? Unaamaanisha nini kusema
hivyo?)
“It’s a long story brother, nadhani tu-meet, halafu nikupe mkanda mzima
ulivyokuwa, ni ngumu sana kuamini, lakini lazima utaamini ninachokuambia.”
“Ulikuwa wapi kwa kipindi chote hicho?”
116
“Kwasasa naishi Mwanza kaka, nilihangaika sana, lakini kwa bahati nzuri
nikabahatika kupata kazi. Nina likizo ya mwezi mmoja, nimefikia Johannesburg
Hotel, Sinza, Mori. Tafadhali sana tuonane leo.”
“Sawa, nikitoka tu, kazini nitakuwa hapo.”
“Kabla hujakata simu, naomba unipatie namba zako za mkononi tafadhali.”
“Ok! Unayo kalamu hapo?”
“Ndiyo, nitajie!”
Akatajiwa namba za simu na kuzinakili kwenye note book yake. Mwishowe
wakaagana. Jeff akazihifadhi zile namba haraka kwenye simu yake, halafu
akajaribu kama zinapatikana, akapokea Frank.
“Ndiyo namba yangu kaka,” Jeff akasema.
“Poa, baadaye basi!”
“Ahsante sana.”
Wakakata simu.
Tayari mbele ya Jeff kulikuwa na mwanga, hata kama ni mdogo, lakini angalau
alikuwa na mahali pa kuanzia. Angenda kubwa kichwani mwake ni kuhakikisha
Davina haolewi na Gerald na badala yake, yeye ndiye aje kumuoa. Haijalishi hata
kama itakuwa baada ya miaka kumi!
Alitaka ndoa!
Yeye na Davina!
******
Saa 2:18 za usiku, Jeff akiwa sehemu ya vinywaji ya hoteli ile, alimuona Frank
akiingia. Kwanza alikaa kimya akimwangalia jinsi alivyokuwa akibabaika
kumtafuta. Baada ya muda akaona si sahihi kumuhangaisha. Akatoa simu yake na
kupiga.
Frank akapokea haraka; “Uko wai kaka, nimeshaingia hapa!”
“Angalia mbele yako, kama unaelekea toilet!”
“Ni wewe mwenye kofia ya pama?”
“Ndiyo!”
Wakakata simu zao.
Frank akapiga hatua za kivivu hadi alipokaa Jeff. Akaonekana kusita kukaa, macho
yake yalionesha woga wa wazi kabisa. Jeff akamwonesha ishara akae. Kwa woga
Frank akakaa.
117
“Usiwe na wasiwasi ndugu, ni mimi ndugu yako Jeff, usishangae na unatakiwa
utulie sana. Najua unajua nimekufa, lakini nipo sijafa.”
Frank akazidi kuyatoa macho yake kwa mshangao. Muda mfupi mhudumu akafika.
Wote wakaagiza glass za mvinyo mweupe. Wakaanza kunywa. Macho ya Frank
hayakuficha woga uliomo ndani mwake.
“Najua unashangaa nina ndevu nyingi, sizipendi lakini ndiyo maisha yangu mapya
ya kujiepusha na matatizo.”
Jeff akavua kofia yake na kuachwa sura yake halisi ionekane. Alikuwa na tofauti
mbili tu, nywele ndefu na ndevu nyingi.
“Ilikuwaje hasa?” Hatimaye Frank akauliza.
“Acha tu ndugu yangu, aliyezikwa si mimi ni mtu mwingine kabisa, sababu kubwa
ni Davina.”
“Unamaanisha nini?”
“Mimi sikuwa nafahamu chochote, lakini kumbe bosi wangu Gerald alikuwa
amempenda Davina, akafikiria jinsi ya kumpata akakosa, akaona bora afanye
njama za kuniua ili aweze kumpa.”
“Enheee...”
“Kwahiyo akaletwa mtu kazini, anaitwa Roy, ambaye ndiyo alitakiwa kunipeleka
kwenye mauaji. Kama unakumbuka siku ya kifo changu nilikuwa safarini kwenda
Dodoma, sasa nilitakiwa kufa njiani kwa ajali ya kupangwa, lakini kwa bahai nzuri
yule jamaa akaingiwa na huruma na kuamua kunisaidia...” Jeff akamwambia
Frank.
Hakuna kitu alichomficha, akamweleza jinsi mipango ilivyofanyika mpaka maii
nyingine ikapatikana na yeye kwenda Mwanza. Frank akaelewa kila kitu na hapo
sasa woga ukaanza kupungua.
“Aisee pole sana ndugu yangu, ndiyo maana hawakutaka marehemu aonekane?”
“Hiyo ilikuwa ni kwasababu ile maiti iliharibiwa usoni, hii ni dili ambayo
tunafahamu wau watatu tu, mimi, Roy na jamaa mwingine anaitwa Kijasho yupo
Morogoro. Nakuomba sana, jambo hili liwe siri ndugu yangu, usimwambie mtu
yeyote.
“Najua ni vigumu kuwa na siri kubwa kama hii lakini vumilia, tukamilishe
uchunguzi wetu, halafu siku moja mambo yatakuwa hadharani.”
“Ok! Nimekuelewa, sasa unadhani mimi nitakusaidiaje?”
“Nataka siku moja, jamii ielewe ukweli wa tukio zima, lakini kumbuka sitaki
kabisa kumpoteza Davina. Tayari nina wazo kichwani.”
118
“Nini?”
“Kitu cha kwanza kabisa ambacho tunatakiwa kufanya ni kuwatisha Gerald na
Davina, ili wote waogope kuwa pamoja, wakati mipango mingine ikiendelea.”
“Tutatumia njia gani?” Frank akauliza akipeleka glass ya mvinyo kichwani
mwake.
“Barua.”
“Barua kivipi?”
“Natakiwa niwe naandika barua na kuzituma Posta, ndani naandika jina langu kila
kiu, lakini anuwani zinakuwa na kuzimu, nje pia tunagonga muhuri wa kuzimu,
halafu inakuwa na maudhui ya kutisha tu!
“Kazi yako wewe ni kupokea barua zote kupitia sanduku lako, halafu
unazisambaza kwenye masanduku yao.”
“Nimeshakupata, lakini lazima jambo hili liwe siri maana unaweza kunipotezea
kazi.”
“Usijali kaka, nitakuwa makini katika kila hatua ya kila jambo ndugu yangu,
siwezi kukuangusha kaka.”
“Poa, nitafurahi kama ikiwa hivyo.”
“Halafu kitu kingine nahitaji sasa uanze kuwafuatilia kwa karibu, nitakuwezesha
kidogo, kuwa karibu kwa kipindi hiki, ujue nyendo zao, halafu utakuwa ukinitumia
taarifa zote sawa mkubwa?”
“Nimekuelewa vizuri sana, ondoa shaka.”
“Kumbuka kila kitu tulichozungumza hapa ni siri, halafu nimekuja Dar kwa ajili ya
kuzungumza na wewe, kwahiyo sina muda kesho narudi Mwanza. Nahitaji sana
msaada wako ndugu yangu.”
“Usijali kaka, pole kwa yote ndugu yangu. Dunia ina mitihani mingi kaka.”
“Kawaida,” Jeff akasema akimpatia kiasi cha laki tatu mkononi mwake.
“Huu ni mwanzo tu kaka, fanya hii kazi vizuri na kwa uaminifu mkubwa
utafurahi.”
“Ahsante sana kaka, nami pia nitakufurahisha. Poa basi, acha mimi nikuache.”
“Nakutakia utekelezaji mwema.”
“Tegemea ushindi,” Frank akasema akitabasamu wakati akiinuka.
Akaondoka zake.
Mwanga wa mafanikio ukaanza kuonekana, Jeff akamwangalia Frank akiishilia
huku akijihesabu ameshakuwa mshindi. Njia ya mafanikio ilianza kuonekana,
mafanikio ya kumnasa tena Davina. Mwanamke wa ndoto yake.
119
“Safi sana...” akasema kwa sauti akipiga meza kwa nguvu kisha akapandisha ngazi
kuelekea chumbani kwake.
Jeff alifurahi sana kuona ombi lake limekubaliwa na Frank, moja kwa moja.
Akamwangalia kwa jicho la kuibia na kuachia tabasamu mwanana usoni mwake,
kisha akatamka kivivu: “Ahsante sana rafiki yangu, mipango yangu sasa itakuwa
sawa.”
“Tupo pamoja Jeff ndugu yangu, wala usiwe na wasiwasi katika hili.”
“Ok, poa! Chukua hizi fedha zikusaidie japo kwa mafuta,” Jeff akasema akimpatia
kiasi cha laki tatu mkononi mwake.
“Nashukuru sana rafiki yangu!”
“Huu ni mwanzo tu kaka, fanya hii kazi vizuri na kwa uaminifu mkubwa
utafurahi.”
“Ahsante sana, nami pia nitakufurahisha. Poa basi, acha mimi nikuache.”
“Nakutakia utekelezaji mwema.”
“Tegemea ushindi,” Frank akasema akitabasamu wakati akiinuka.
Akaondoka zake.
Mwanga wa mafanikio ukaanza kuonekana, Jeff akamwangalia Frank akiishilia
huku akijihesabu ameshakuwa mshindi. Njia ya mafanikio ilianza kuonekana,
mafanikio ya kumnasa tena Davina wake. Mwanamke wa ndoto yake.
“Safi sana...” akasema kwa sauti akipiga meza kwa nguvu kisha akapandisha ngazi
kuelekea chumbani kwake.
Hakuwa na kazi nyingi sana chumbani, aliishia kuoga kisha kupanga-panga baadhi
ya bidhaa zake, tayari kwa safari ya siku inayofuata kisha akashuka chini,
alipokula na kuanza kufakamia mvinyo kwa fujo!
*****
Kitu cha kwanza Jeff kufanya alipofika Mwanza, ilikuwa ni kwenda kwa fundi wa
kutengeneza mihuri kisha akamwomba amtengenezee muhuri aliouhitaji. Fundi
alishangazwa sana na maandishi aliyokuwa akihitaji kuandikiwa katika muhuri
huo.
“Kwanini unaandika hivi?”
“Vipi?”
“Kuzimu Mjini!”
“Wewe shida yako nini? Unahitaji kujua sababu ya kuandika maneno hayo au
unataka kazi?”
120
“Kazi, ingawa pia ni vyema kujua matumizi ya muhuri wako.”
“Sasa mimi nasema si kazi yako, amua kutengeneza nikulipe bila kukuambia
sababu za kuutengeneza au nimpelekee fundi mwingine.”
“Nitatengeneza kaka.”
“Fanya kazi yako.”
Zoezi hilo lilipokamilika, Jeff alichukua muhuri wake na kwenda nyumbani.
Akakaa mezani kwa utulivu na kuanza kuandika barua za Davina na Gerald.
Alizisoma mara mbilimbili na kuridhika. Alipomaliza akaziweka kwenye bahasha,
kisha akaziingiza tena kwenye bahasha nyingine na kuandika anuwani ya Frank.
Kazi ikawa imeisha!
Huo ukawa mwanzo wa barua za vitisho kwa Gerald na Davina. Utaratibu ukawa
ule ule, anaandika kisha anaweka kwenye bahasha aliyogonga muhuri wa kuzimu,
kisha akaweka tena ndani ya bahasha nyingine ambazo aliandika anwani ya Frank
na kumfikia.
121
SURA YA KUMI NA TATU
FRANK alitimiza kazi yake ipasavyo, hakuwa na mchezo na kazi, kila barua
zilipofika alichana bahasha ya juu na kuziweka kwenye masanduku ya Davina na
Gerald! Frank aliamua kumsaidia rafiki yake ipasavyo. Hata pale Davina alipofika
ofisini kwao na kuzungumza na Meneja, alimpa taarifa zote.
“Amekuja kuonana na Meneja, uamuzi waliouchukua ni kupitisha barua zote
ofisini kwake kwa kipindi ambacho uchunguzi unaendelea.”
“Uchunguzi? Unamaanisha nini?”
“Anahisi kuna mtu anamchezea mchezo hapa ofisini kwetu.”
“Duh! Sasa mambo si ndiyo yameshaharibika kaka?”
“Hapana, hayawezi kuharibika, kwasababu hata hiyo kazi ya kupeleka barua
ofisini kwa Meneja nimepewa mimi.”
“Kwahiyo?”
“Endelea kutuma barua kaka.”
Frank akaendelea na kazi yake kama kawaida, aliwafuatilia kwa karibu sana, hata
pale Davina alipotaka kwenda Kondoa, alijua na kumpa taarifa Jeff.
Jeff akampigia simu Davina usiku ule ule na kumtishia kama kawaida yake,
mwisho wa siku akaamua kusitisha vitisho vyote. Wakati huo alikuwa na taarifa
zenye uthibitisho wa kutosha kwamba Davina na Gerald walikuwa mbioni kufunga
ndoa.
Hilo hakutaka kulipa nafasi kabisa.
“Hawawezi kuoana, labda mimi siyo Jeff, Davina atarudi tena mikononi mwangu,”
Jeff alimwambia Frank kwenye simu wakati alipompigia kumpa taarifa za ndoa ya
Davina na Gerald iliyokuwa mbioni kufungwa.
“Kivipi?”
“Subiri.”
****
Ni usiku wa sita sasa, katika chumba hiki kizuri, chenye hewa safi, lakini
kukikosekana kitu kimoja muhimu kwa Jeff. Usingizi. Ni siku ya sita leo, Jeff
hajalala! Mawazo yake yote ni juu ya mpenzi wake Davina ambaye dalili
zilionekana wazi kabisa kwamba anampoteza!
122
Ilikuwa ni siku nane kabla ya ndoa ya Davina na Gerald kufungwa! Ndoa ya
mpenzi wake. Ndoa haramu, ambayo kwa hakika asingeweza kuiruhusu. Bado ana
mawazo akijaribu kufikiria jinsi atakavyoitengua ndoa hiyo kabla ya kufungwa.
“Nitafanyaje jamani? Mbona akili yangu ipo kama imefikia mwisho? Lakini
siamini kabisa kama hapa ndiyo mwisho wangu wa kufikiri? Kweli ndiyo mwisho
wangu wa kufikiri? Siamini kabisa. Lazima kuna kitu natakiwa kufanya.
“Kuna mahali sijafika kimawazo. Siamini kama kweli mawazo yangu yanaweza
kuwa mwisho wake hapa. Mimi? Mwisho wa kuwaza unaweza kuwa hapa kweli?
Kuna kitu nimesahau....ni nini?” Anawaza Jeff bila kupata majibu yakinifu.
Akiwa katikati ya lindi la mawazo, simu yake ikaita, mara moja akaichukua.
Akakutana na jina la Frank likizunguka kwenye kioo cha simu yake. Hakupokea
haraka. Akatulia kwanza na kuwaza: “Ana nini kipya?”
“Ngoja nipokee....” akasema kwa sauti akibonyeza kitufe cha kupokea na kupeleka
simu sikioni.
“Sema kaka...mbona usiku, kuna jipya?” Jeff akauliza kwa sauti ya taratibu sana.
“Siyo jipya sana kaka, ila nataka kukukumbusha kwamba kesho ni Jumapili!”
“Najua, kwani vipi?”
“Ndoa ya Davina na Gerald inatangazwa kwa mara ya mwisho Kanisani.”
“Pia najua.”
“Kujua pekee hakusaidii kitu, umepanga kufanya nini?”
“Nipe muda hadi kesho asubuhi nitakuwa na la kufanya. Nitakupigia kukujulisha,
usijali.”
“Usiku mwema.”
“Nawe pia.”
Wakakata simu zao.
Jeff alikuwa na mawazo sana, simu ya Frank ilimchanganya sana. Akaendelea
kuusumbua ubongo wake. Mwisho akapata jibu.
“Nimeshajua cha kufanya, acha nilale sasa.”
******
Jumatatu, saa 4:15 za usiku, Jeff alikuwa akishuka kweye basi, katika Kituo Kikuu
cha Mabasi ya Mikoani, Ubungo jijini Dar es Salaam, akitokea Mwanza. Hiyo
ikiwa ni siku mbili baada ya kuzungumza na Jeff kwenye simu. Ilikuwa safari ya
ghafla na ya siri kubwa.
123
Kama kawaida, alikuwa amevalia kofia kubwa kichwani, koti refu na ndevu za
bandia. Akachukua taxi iliyompeleka moja kwa moja Johannesburg Hotel iliyopo
Sinza ya Mori. Hapo akajifungia chumbani kwa siku tatu, bila kutoka nje ya hoteli
hiyo. Safari zake ziliishia Restaurant na chumbani tu!
“Kwahiyo afande ndiyo hivyo, bado nampenda sana mpenzi wangu, najua
hafahamu kinachoendelea, lakini pia nataka Gerald na kundi lake wakamatwe, iwe
fundisho, hawa watu hatari sana,” Jeff alimwambia askari aliyekuwa akichukua
maelezo yake.
“Umeingia lini hapa jijini?”
“Jumatatu.”
“Umefikia wapi?”
“Johannesburg Hotel, Sinza Mori.”
“Taarifa ulizonazo, ndoa ni saa ngapi?”
“Ibada ya ndoa inaanza saa nane kamili za mchana afande.”
“Ok, acha namba zako za simu, sisi tunajipanga vyema, kesho kuanzia saa tano
kamili uwe hapa.”
“Sawa afande.”
Jeff akaondoka zake.
*****
“Siamini kama unaweza kukubali Gerald amuoe Davina,” Frank alimwambia Jeff
kwenye simu, alipompigia mchana huo.
“Nitakuwa mwanaume mpumbavu kuliko wote.”
“Sasa una mipango gani?”
“Njoo hotelini tuongee.”
124
“Hotelini wapi?”
“Pale pa siku ile.”
“Johannesburg?”
“Ndiyo.”
“Upo Dar?”
“Ndiyo maana yake.”
“Tangu lini?”
“Njoo tutaongea huku.”
“Poa.”
Nusu saa baadaye Frank alikuwa chumbani kwa Jeff. Alishangaa sana jinsi
alivyoingia Dar kwa siri! Jeff akafungua begi lake na kutoa suti yake ya kisasa,
nzuri ya kuvutia.
“Ya nini tena?”
“Ya ndoa yangu.”
“Ndoa yako?”
“Ndiyo.”
“Na nani?”
“Davina.”
“Kivipi?”
“Kaa kwanza nikupe michapo kaka...” Jeff akamwambia Frank akitabasamu.
Akamweleza kila kitu jinsi alivyopanga mpango mzima na maaskari. Frank
hakuamini macho yake, akampongeza rafiki yake kwa ujasiri wake mkubwa!
“Lakini lazima unyoe hayo mandevu na manywele yako.”
“Ni kweli, lakini sasa nitawezaje kuingia salon?”
“Kazi nyepesi sana, hapo barabarani kuna salon nyingi sana, kitu cha kufanya,
tutatoka muda wa saa tano hivi, muda ambao wanakaribia kufunga, kwahiyo
hakutakuwa na wateja wengi. Tutatumia muda huo kunyoa na hakuna mtu
atayekuona.”
“Kweli kabisa.”
Ndivyo ilivyokuwa, saa tano walitoka na kwenda barabarani, ambapo Jeff
alinyolewa bila kuonekana na mtu yeyote hatari kwake. Zoezi hilo lilipokamilika,
wakarudi hotelini. Jeff akavaa ile suti yake na viatu, kisha akamgeukia Frank
akitabasamu.
“Haya niambie kaka!” Jeff akamwambia Frank akicheka.
125
“Sina la kuongeza kaka, yaani ni bwana harusi kamili....yaani wagejua kuwa wewe
ndiye muoaji, siyo Gerald, waalikwa wasingejisumbua!”
“Watajiju!!!”
Frank akaondoka na kumwacha Jeff mwenyewe chumbani kwake, akili yake
ikiwaza mambo yatakavyokuwa Kanisani siku inayofuata. Aliwaza sana juu ya
ndoa yake. Alimpenda sana Davina, lakini bado ndani yake kulikuwa na wasiwasi,
aliwaza kama Davina bado alikuwa akimpenda!
Hilo hakulijua!
Alitakiwa kusubiri!
Kesho tu!
*****
Saa 5:00 za asubuhi, Jeff alikuwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay kama
alivyoagizwa na maaskari. Alikuwa amevalia suti yake ya rangi nyeupe, viatu vya
kisasa na alinyoa nywele zake katika mpangilio wa kuvutia kabisa.
Alionekana kama bwana harusi kamili!
Tena halali!
“Kaka naona umepania sana, eeh!” Askari mmoja akamwuliza Jeff kwa mtindo wa
kumtania.
“Si unajua tena kaka, isitoshe ni haki yangu.”
“Ok! Endelea kusubiri kidogo, tutakujulisha kinachoendelea, lakini cha msingi
unachotakiwa kufahamu, tayari kuna gari zima la maaskari lipo maeneo ya
Kanisani linafanya doria, Ibada ikianza, wapo askari kanzu watakaokuwa Kanisani
wakitujulisha kila kitu, kwahiyo shaka ondoa.”
“Sawa afande, nitafurahi sana mkinisaidia.”
“Hiki ni chombo cha usalama ndugu yangu, ni wajibu wetu kuhakikisha unakuwa
salama katika kila kitu. Ondoa hofu uliyonayo, kila kitu kitakuwa sawa.”
“Nashukuru sana. Sijui nitatoa zawadi gani kwenu nikifanikiwa!”
“Huna haja, serikali imetuweka hapa kwa kazi hii, nayo imekuwa ikitulipa
masilahi mazuri na yanayotosha kabisa, kwahiyo huna sababu ya kutoa chochote
ndugu yangu!”
“Ahsante sana, nimefarijika mno kusikia hivyo.”
*****
126
Kanisa lilikuwa limefurika watu wengi sana mchana huo, walikuwa wakishuhudia
tukio muhimu sana la ndoa ya Gerald na Davina. Kwa Gerald ilikuwa siku ya
kihistoria sana kwake, maana alikuwa anatimiza ndoto yake ya siku nyingi.
Ndoto ya kumuoa Davina wake!
Ndani ya kuta za jengo la Kanisa lile, kulikuwa na makachero wa Polisi zaidi ya
watano, wakiangalia kila hatua ya kilichokuwa kikiendelea! Hatimaye muda wa
tukio muhimu kabisa, ukafika. Muda wa kufungisha ndoa.
Kama kawaida Mchungaji aliuliza, kama kuna mtu ana pingamizi ili aweze
kufunga ndoa ile. Akauliza kwa mara ya kwanza, ya pili na alipofika ya tatu,
akasikia sauti kuu kutoka lango kubwa la kuingilia ikitoa pingamizi...
“Noooo....nooo Pastor...nina pingamizi...” ilikuwa sauti ya Jeff, akiingia mbio
kuelekea madhabahuni ambapo Gerald na Davina walikuwa wamesimama tayari
kwa kufunga.
Macho yaliwatoka kwa mshangao, vipi Jeff atokee Kanisani wakati alikuwa
ameshakufa? Jeff alikuwa marehemu! Ukumbi mzima ukapigwa na butwaa!
*****
“Mchungaji hivyo ndivyo ilivyokuwa, huyu Gerald ni mtu mbaya sana, alitaka
kuniua mimi ili yeye atimize lengo lake la kumuoa mpenzi wangu, nilifanya yote
hayo kwa ajili ya mpenzi wangu.
“Bado nampenda sana Davina wangu na sipo tayari kabisa kumpoteza. Nampenda,
nataka kufunga naye ndoa...” Jeff akasema kwa sauti kuu, huku akilia machozi ya
uchungu.
Ghafla alipogeuza macho yake upande wa waumini, akakutanisha uso wake na
Roy! Mafia ambaye aliamua kumsaidia katika mauaji yake, akamkonyeza na
kumuonesha kwa ishara kwamba kulikuwa na hatari na aondoke haraka.
Hakuna aliyegundua tofauti hiyo, taratibu Roy akasimama na kutoka nje ya
Kanisa. Ilikuwa kitedo cha haraka na siri kubwa. Hakika Jeff asingefurahi kuona
Roy anaingizwa hatiani, hasa kutokana na ukweli kwamba ndiye alimyemsaidia
kuwa hai mpaka muda ule.
“Je,Davina unamfahamu Jeff?” Mchungaji akamwuliza Davina kwa sauti ya
taratibu sana.
Jeff akayatupa macho yake kwa Davina, akionekana kuhitaji huruma yake,
hakutaka kukataliwa, alimpenda sana mwanamke huyo.
“Ndiyo Mchungaji, namfahamu, nampenda bado. Kama itawezekana naomba
kufunga naye ndoa.”
127
Moyo wa Jeff ukalipuka kwa furaha!
“Gerald ni ya kweli hayo yaliyosemwa na Jeff?” Mchungaji akamgeukia Gerald na
kumwuliza.
Gerald hakujibu kitu.
Akabaki akilia!
“Tulia hivyo hivyo, upo chini ya ulinzi. Nyoosha mikono yako juu haraka,”
ilikuwa ni sauti ya mmoja wa maaskari waliongia Kanisani ghafla wakiwa na
bastola mikononi.
Gerald hakuwa na la kufanya, akanyoosha mikono yake yake juu, kabla ya
kuamriwa baadaye aishushe na pingu zikafungwa mikononi mwake, akatolewa
katika lango kuu la Kanisa, tayari kwa kufikishwa katika Kituo cha Polisi
Oysterbay. Kelele zikatawala Kanisani, kila mtu akiwa haamini kabisa
kilichotokea.
Jeff akashindwa kujizuia, akajikuta akimkimbilia Davina na kumkumbatia huku
akilia!
Davina akampokea!
Wakakumbatiana!
“Kuna mtu mwenye pingamizi kabla sijafungisha ndoa hii?” Sauti ya Mchungaji
ikasikika, ndiyo iliyowanasua Davina na Jeff waliokuwa wamekumbatiana.
Hakuna aliyejitokeza.
Mara moja ndoa ikafungwa na mambo kubadilika, ikawa huzuni kubwa sana kwa
upande wa akina Gerald, lakini ilikuwa furaha kwa upande wa akina Davina,
kwani walifahamu ni kiasi gani ndugu yao alivyokuwa akimpenda sana Jeff.
Muda mfupi tu baada ya ndoa kufungwa, wazazi wa Jeff pamoja na ndugu
wengine, wakaingia Kanisani. Furaha ikageuka kilio. Walikuwa wakilia kwa
furaha baada ya kumuona mwanao akiwa hai tena. Walipata taarifa hizo muda
mfupi uliopita, baada ya kupigiwa simu na jamaa mmoja aliyekuwa kwenye
sherehe ya harusi hiyo.
Bila kujali utaratibu wa Ibada, Jeff alitoka mbio na kuwafuata wazazi wake.
Akawakumbatia!
“Nipo hai wazazi wangu!”
“Ilikuwaje?” Baba yake Jeff akauliza.
“Ni habari ndefu sana, nitawasimulia nyumbani.”
“Pole sana baba, pole mwanangu. Mungu apewe sifa,” mama Jeff akasema
akimpiga-piga mgongoni.
128
“Aika-mai...” (Ahsante mama) Jeff akaitikia kwa lugha yao ya Kichagga.
Wakaachiana.
Wakatizamana wakitabasamu.
Mara Davina naye akaja mbio, akajitupa kifuani mwa Jeff, akalala akiwaangalia
wazazi wake ambao tayari walikuwa wameshaungana na wazazi wa Jeff.
Wakaachia tabasamu!
Muda mfupi baadaye Vyombo mbalimbali vya Habari vilikuwa Kanisani.
Wakichukua picha na kutaka kufanya mahojiano na Jeff.
“Kaandikeni nipo hai, maelezo mengine nitatoa nikiwaita kwenye press Jumatatu,”
ndivyo Jeff alivyowajibu Waandishi wa Habari.
Kama ndoto ya kupendeza, hatimaye Davina na Jeff wamerudi kuwa pamoja tena.
Ndoto zao zikiwa zimerejea kwa upya. Kila kitu kikabaki kuwa sehemu ya historia
ya maisha yao, sasa walikuwa katika penzi jipya.
Penzi la milele!
MWISHO
129