You are on page 1of 2

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

IDARA YA HABARI - MAELEZO



PRESS RELEASE

P.O. Box 8031, Dar es Salaam, Tel: 2110585, 2122771/3, Fax: 2113814, e-mail: maelezo@habari.go.tz


Serikali inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa potofu zinazoendelea
kuchapishwa na kutangazwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuhusu Watumishi
Waandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Alexander Songorwa ambaye ni
Mkurugenzi, Idara ya Wanyamapori na Prof. Jafari Kideghesho, Mkurugenzi Msaidizi,
Idara ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori.

Kumekuwa na taarifa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kwamba
Wakurugenzi hao walikuwa wamefukuzwa kazi na Waziri wa Maliasili na Utalii, na kisha
kurejeshwa kwa maelekezo ya Ikulu. Taarifa hizo si sahihi.

Ukweli ni kwamba Prof. Alexander Songorwa na Prof. Jafari Kideghesho
hawajawahi kufukuzwa kazi ama kuadhibiwa. Hatua za kinidhamu katika Utumishi wa
Umma zina taratibu na miongozo yake, inayotawaliwa na nyaraka kuu nne, miongoni
mwa nyingine, kama ifuatavyo:

Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 1999;
Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya Mwaka 2002 (kama ilivyorekebishwa
mwaka 2008);
Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003;
Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo, na kwa mujibu wa sheria, kila mtumishi wa umma
anayo mamlaka yake ya ajira na mamlaka yake ya nidhamu.

Mamlaka ya nidhamu ya Prof. Alexander Songorwa na Prof. Jafari Kideghesho
haijawahi kuwachukulia hatua zozote za kinidhamu. Lakini, baada ya Waziri wa
Maliasili na Utalii kuonyesha kutoridhika na utendaji wao, Mamlaka yao ya nidhamu
iliwaruhusu kuchukua likizo zao za mwaka za kawaida. Likizo zao zilipoisha walirejea
kazini kama kawaida.





Hata hivyo, kutokana na yaliyokwisha kutokea, wanataaluma hawa, Prof.
Alexander Songorwa na Prof. Jafari Kideghesho, kwa hiari yao wenyewe, wamekubali
kuchukua majukumu mengine katika Utumishi wa Umma kama watakavyopangiwa.

Serikali inapenda kukumbusha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ameunda Tume ya Uchunguzi kuhusu utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Miongoni
mwa hadidu za rejea za Tume ni kubainisha kila aliyefanya kosa wakati wa kutekeleza
Operesheni Tokomeza na kupendekeza hatua stahiki dhidi ya wahusika. Serikali
inashauri Tume ipewe nafasi ya kukamilisha kazi yake ndipo tutajua mkosaji ni nani na
anastahili kuchukuliwa hatua gani. Serikali inaomba pia kila mwenye taarifa na ushahidi
utakaoisaidia Tume aifikishe kwao.



IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO

Dar es Salaam, 10 Mei, 2014

You might also like