You are on page 1of 21

NANI KABADILI SABATO KWENDA JUMAPILI?

- MUNGU MWENYEWE

Je, nani kabadili siku ya ibada kutoka Sabato kwenda Dominika (Jumapili)?

Mashtaka: Wakatoliki wote na viongozi wao hasa Papa wameibadili Sabato


kwenda Dominika (Jumapili). Mfalme Konstantino pia ndiye hasa aliyeyafanya
mabadiliko hayo na hivyo, kwa vyo vyote, ni binadamu na siyo Mungu aliyefanya
mabadiliko hayo.

Jibu fupi

Mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili) yalifanywa na Mungu


mwenyewe na mwisho wenyewe umetangazwa mara nne katika Biblia. Zisome
sehemu hizo kama zinavyofuatana hapa: Hos 2:11, Ebr 4:4-10, Rum 14:4-10 na
Kol 2:16. Kwa kifupi kabisa, Biblia inasema Mungu mwenyewe ndiye aliyebadili.

Jibu refu: Mabadiliko Yalitabiriwa, Yalitangazwa, Yalifanywa na


Yalitekelezwa

Biblia ipo wazi kabisa kuhusu mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili).
Mosi, mabadiliko hayo yalitabiriwa na Hosea (rej. Hos 2:11). Yeye alitabiri
akisema, “Tena nitaikomesha furaha yake yote na sikukuu zake, na siku zake za
mwandamo wa mwezi na sabato zake na makusanyiko yake yote yaliyoamriwa.”
Pili mabadiliko hayo yalifafanuliwa kwa maneno na matendo ya Yesu Kristo (rej.
vifungu mbalimbali vya Injili, hususan, Mt 12:1-12, Mk 3:2-4, Lk 13:14-16, 14:1-
5, Yn 9:16).

Tatu, mabadiliko yametangazwa katika Ebr 4:4-10. Hapa tunasoma hivi, “Basi,
ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuiogope, mmoja wenu asije
akaonekana ameikosa. Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile
vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu
halikuchanyikana na imani ndani yao waliosikia. Maana sisi tulioamini tunaingia
katika raha ile: Kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu,

1
Hawataingia rahani mwangu: ijapokuwa zile kazi zilimalizika tangu kuwekwa
misingi ya ulimwengu. Kwa maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi,
Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote; na hapa napo,
Hawataingia rahani mwangu.

Basi, kwa kuwa neno hili limebaki kwamba wako watu watakaoingia humo, na
wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi
kwao, AWEKA TENA SIKU FULANI, akisema katika Daudi baada ya muda
mwingi namna hii, Leo kama ilivyonenwa tangu zamani, Leo, kama mtaisikia sauti
yake, Msifanye migumu mioyo yenu. Maana kama Yoshua angaliwapa raha,
asingalinena siku nyingine baadaye. Basi, imesalia raha ya Sabato kwa watu wa
Mungu. Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe
katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi yake. Basi, na tufanye
bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu yeyote asije akaanguka kwa mfano
huo huo wa kuasi.”

Nne, Sabato imebainishwa kuwa ilikuwa kivuli tu Kol 2:16. Hapa tunasoma hivi,
“Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya
sikukuu au mwandamo wa mwezi, au Sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo
yajayo; bali mwili ni wa Kristo”. Na hatimaye siku zote zimetangazwa katika Rum
14: 4-10 kuwa sawa mbele ya Mungu mwenyewe. Hapo tunasoma ifuatavyo:
“Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake
mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana
aweza kumsimamisha. Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku; mwingine
aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe.
Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana,
kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia
amshukuru Mungu. Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi
yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa
Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu
mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki
waliokufa na walio hai pia. Lakini wewe, je! mbona wamhukumu ndugu yako? Au
wewe je! mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele
ya kiti cha hukumu cha Mungu.”

2
Hicho ndicho kitabu cha Ufunuo, kitabu ambacho kinatangaza vifo vya vitu vingi.
Mambo yalipinduliwa hivyo na Mungu mwenyewe. Hebu nikuorodheshea kidogo
mambo yanayosimuliwa na kitabu cha Ufunuo kwamba yalikufa kwa kusudi ya
kuyapisha mambo mapya muhimu. Kinasimulia kwamba hekalu la Yerusalemu
lilikufa kulipisha hekalu la kweli yaani makazi ya Mungu mwenyewe mbinguni.
Ukuhani wa Kiyahudi ulikufa kuupisha ukuhani mkamilifu na wa milele wa Yesu
Kristo pamoja na watu wote wanaobatizwa katika jina lake. Sadaka za Kiyahudi
zilikufa kuipisha sadaka timilifu ya Yesu Kristo msalabani. Kumbe ni katika
tangazo hili la kifo, kitabu cha Ufunuo kinapotangaza kwamba Sabato iliuawa
kuipisha Siku ya Bwana, yaani Jumapili.

Bila shaka Maandiko Matakatifu haya yanakukonga roho na kukubainishia


kwamba mabadiliko yalifanywa na Mungu mwenyewe. Tazama, tumesoma
kwamba Mungu mwenyewe alimtabirisha Nabii Hosea mabadiliko aliyoyakusudia
kutoka Sabato kwenda Jumapili yaani Dominika. Halafu, tumezitaja nukuu nyingi
za Injili zinazomwonesha Yesu akiyaeleza mabadiliko hayo, ijapokuwa Wayahudi
hawakumwelewa vilivyo. Kumbe baada ya kifo cha Yesu, mabadiliko hayo
yalifanyika pale mitume wa Yesu walipopambazukiwa akilini mwao.

Hata hivyo, haikuwa wote walioelewa suala hilo, wengine wakawa bado
wanaililia Sabato hiyo. Kufuatia kituko hicho, mwandishi wa Barua kwa
Waebrania akawaandikia wazi wazi wazi habari hiyo (Ebr 4:1-10) naye Paulo
akakizima kilio cha wasiokubali mabadiliko katika Rum 14:4-10 na
kuwatawanyisha wapigakelele waliokuwa wakiwahangaisha wenzao juu ya Sabato
na sikukuu zingine za kiyahudi kwa maneno murua yaliyomo katika Kol 2:16-17.

Mabadiliko Yalitabiriwa

Sasa hebu tujipatie muda wa kuliweka jibu hili kirefu. Tufuatane kwa utulivu sasa.
Awali ya yote, Biblia inaonesha kwamba Mungu alishamfanya Hosea ayatabiri
mabadiliko hayo. Hosea 2:11 inasomeka wazi wazi kabisa: “Nitazikomesha starehe
zake zote, sikukuu zake za mwezi mwandamo na za Sabato na sikukuu zote
zilizoamriwa”. Neno Sabato katika Kiebrania “shabat” linamaanisha “kupumzika”.
Kwa wayahudi siku hiyo ilikuwa siku ya Bwana wa huruma na walipaswa kuiweka
wakfu kwake (rej. Law 23:3). Siku hiyo walimheshimu Mungu (rej. Mt 12:5, Yn

3
7:23) kwa kumtolea sadaka, kusali na kupumzika kazi kabisa (rej. Isa 56:2, 58:13-
14).

Kama kivuli cha mapumziko halisi yatakayopatikana mbinguni kwa njia ya kifo na
ufufuko wa Yesu Krsto, Mungu aliwawekea wayahudi Sabato kusudi wajipatie
picha ya mambo halisi yajayo mbele yao. Ndipo alipowapa sababu za kujifunza
kupumzika kama mazoezi ya maonjo ya mapumziko halisi. Sababu alizowapa
zilikuwa tatu: kwanza kwamba wamwige Yeye mwenyewe aliyepumzika baada ya
kukamilisha kazi ya kuumba ulimwengu pamoja na vitu na watu waliomo ndani
yake (rej. Kut 20:8-11), pili kwamba Sabato ni ishara ya Mungu kwa wayahudi
kwamba ndiye aliyewatakasa na kuwafanya taifa lake teule (rej. Kut 31:13-18, Eze
20:20) na tatu waishike kama kumbukumbu ya kukombolewa kwao kutoka Misri
(rej. Kum 5:11-15).

Kumbe kadiri Wayahudi walivyojaribu kuishika Sabato, kusudi kukwepa adhabu


zilizotangazwa dhidi ya kuifuja Sabato, walizidisha ugumu. Walimu wa dini na
waandishi waliifafanua amri ya Sabato na kuunga vipengele vingi sana hata ikawa
ni mzigo mzito kwa watu. Aina thelathini na tisa zilikatazwa kufanywa katika siku
ya Sabato, kati yake zikiwamo kazi za kuvuna, kuwinda, kuchuna ngozi, kufuta
herufi mbili, kuandika herufi mbili, kuchoma mkaa, kupika, kutembea zaidi ya
mwendo wa Sabato, kuponya magonjwa yasiyo ya dharura na kadhalika. Mambo
yaliyokatazwa yalikuwa mengi sana na vipengele vidogo vidogo vikaongezeka
hata amri yenyewe ikatisha kama miiba ya nungunungu. Zaidi ya hayo, zikawekwa
Sabato chungu mzima, Sabato za ardhi, Sabato za miaka ndiyo jubilei mbali mbali
na kadhalika (rej. Law 25:1 – 26:46).

Kwa mtindo huu wa mambo, ikadhihirika wazi kwamba mtu alikuwa anawajibika
kwa Sabato kana kwamba aliumbwa kwa ajili hiyo, wakati Sabato iliwekwa kwa
ajili ya binadamu apate kustarehe na hivyo kujionjesha Sabato ya kweli
itakayokuja mwishoni mwa historia. Kifupi, kiutendaji, mtu aligeuzwa mtumwa
kwa Sabato, starehe ikakosekana kukabaki mashaka na wasiwasi mwingi sana.
Wayahudi waliiogopa sana Sabato, si hasa kwa sababu ya kumpenda na kumtii
Mungu isipokuwa kwa sababu ya adhabu zake, hasa kuangamizwa kwa
Yerusalemu na kupelekwa utumwani (rej. Yer 17:19-27, Eze 20:20-24).

Mabadiliko Yalitangazwa na Yesu Kristo

4
Mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili) yalifafanuliwa kirefu kwa
maneno na matendo ya Yesu Kristo (rej. sehemu mbalimbali za Injili). Mungu
alipowaona wayahudi wakihangaika na Sabato akazidi kuchanua katika nia yake
ya kuifuta. Ndipo, Bwana wetu Yesu Kristo, alipokuja akawaelimisha watu
kwamba binadamu hakuumbwa mtumwa wa Sabato hata kidogo. Badala yake,
Yesu Kristo, aliwaelimisha wote, kwa maneno na matendo yake kwamba Yeye
alikuwa ni Bwana wa Sabato na hivyo, kwa mamlaka hayo na kwa utume wake
aliopewa na Baba, anawaalika watu kutenda mema badala ya kujiumiza kwa wasi
wasi wa kuivunja Sabato na hivyo labda kuadhibiwa na Mungu (rej. Mk 2:27f).

Yesu alijitangaza kuwa Mungu mwenye mamlaka ya kuibadili hiyo Sabato kwa
sababu aliiweka yeye mwenyewe. Na hiyo ni kawaida na mantiki, aliyeitunga
sheria ndiye anayeweza kuitangua. Yesu aliwaambia Wayahudi, “Sabato ilifanyika
kwa ajili ya mwanadamu, si mwandamu kwa ajili ya Sabato, Basi Mwana wa
Adamu ndiye Bwana wa Sabato pia” (Mk 2:27f). Japokuwa Yesu alitangaza jambo
hili, Wayahudi hawakumwelewa hata kidogo na kwa namna hiyo walimlalamkia
yeye na wafuasi wake ambao kutokana na kumwelewa mwalimu wao walishaanza
kuonesha dalili za kutoitilia maanani Sabato kwa mtindo wa kiyahudi (rej. Mt
12:1-12, 3:2-4, Lk 13:14-16, 14:1-5, Yn 9:16).

Hatimaye, Yesu alihitimisha mabadiliko yenyewe kwa kukamilisha matendo ya


ukombozi katika siku ya kwanza ya juma (kwa hesabu za kiyahudi), ndio Jumapili
au siku ya Bwana. Siku hiyo alifufuka katika wafu kwa utukufu mkuu. Kumbe
hapo hapo, ukiangalia nyuma, utaona kumbe ilikuwa siku kama hiyo Mungu
alipoumba ulimwengu kwa Neno, hii maana yake kwa ufufuko wake, Yesu aliye
Neno, Mungu anaumba upya ulimwengu. Na tena siku ya namna hiyo hiyo, ndiyo
atakayoitumia huko mbele kuwatokea wafuasi wake na hatimaye kuwaletea Roho
Mtakatifu atakayelizindua Taifa jipya la Mungu, Kanisa. Basi Pentekoste ikawa
pia Jumapili. Kwa haya yote, Jumapili ikatekwa yote na Bwana na ndipo kifupi
ikawa SIKU YA BWANA, kwa vile jinsi kila jambo kuu la Bwana, alivyokuwa
akilifanya siku hiyo. Basi kwa Kilatini SIKU YA BWANA ndiyo DOMINIKA.
Kwa hali hii basi akadhihirisha kwamba Yeye, aliyekuwa akisubiriwa ameshafika
na yote yaliyokuwa yakifanyika na wayahudi, sikukuu za mwezi na hata Sabato
yalikuwa ni vivuli tu (rej. Kol 2:16-17).

5
Juhudi hizi za Yesu hazikuzaa matunda mara moja. Kumbe, elimu aliyotoa Yesu
Kristo kuhusu Sabato, kwa maneno na matendo tunayoyaorodhesha hapa,
haikuingia kabisa vichwani mwa wayahudi na hata wafuasi wake walisitasita
kuipokea. Kwa kisa hicho, baada ya Yesu kupaa mbinguni, wayahudi waliendelea
kuishika Sabato na kukusanyika kwa ibada katika siku hiyo. Basi Mtume Paulo
alipotaka kuwakuta Wayahudi wamekusanyika kwa wingi pamoja aliwatafuta
katika siku ya Sabato (rej. Mdo 13:14, 42, 44, 16:13, 17:2, 18:4), kwa Wakristo
alijua ilikuwa siku ya Dominika (rej. Mdo 20:7). Hata hivyo, kiujumla, kwa
sababu ya uzito na woga wa kubandukana na siku waliyoizoea kusudi kuifuata siku
mpya, wafuasi wa Yesu walikuwa njia panda na hivyo wakawa wanahudhuria
Sabato pamoja na wayahudi wote na SIKU YA BWANA ilipofika wakawa
wanajikusanya peke yao ili kusali, kusoma maandishi yao (ndiyo yaliyogeuka
baadaye Agano Jipya) na kuumega mkate (rej. Mdo 20:7).

Mabadiliko Yalitekelezwa na Wafuasi wa Yesu

Kitendo cha wafuasi wa Yesu kusali huku na huku, Sabato na Wayahudi na


Dominika peke yao, hakikuchukua muda mrefu kubainika. Wakuu wa wayahudi
waling’amua kwamba kuna wayahudi wenye tabia za pande mbili. Wanajiunga na
ibada za wayahudi na kishapo siku ya pili yake wanasali peke yao, wakisoma
maandishi yao na kumega mkate huku wakimkiri Yesu Kristo kama Mwana wa
Mungu na mkombozi wa wanadamu. Ndipo walipotunga ombi la kumi na mbili na
kulitia kati ya sala yao ya maombi kumi na nane (tefillah), sala iliyokuwa ikisaliwa
kila Sabato na wayahudi wote katika mwendo wao wa ibada.

Ombi la kumi na mbili halikuwa ombi, bali sala ya kulaani waasi wa dini na hivyo
wakiwamo ndani yake Wakristo. Ombi hilo lilisema: “Kusiwe na tumaini kwa
waasi wa dini na uung’oe kwa haraka utawala wenye kiburi (dola ya kirumi)
katika siku zetu. Wanazareni (wayahudi Wakristo) na ‘minim’ (wayahudi wazushi)
wafe mara moja; wafutwe kwenye kitabu cha uzima na wasiorodheshwe pamoja na
wenye haki”. Mwisho mwa ombi hili, kama ilivyotakiwa kwa kila ombi, watu
waliokusanyika kwa ibada iliwapasa kuitikia, “Utukuzwe wewe, Bwana
unayenyenyekesha kiburi”.

Kwa kweli, kwa ombi hili au laana hii, Roho Mtakatifu, mfariji na mkumbushaji
wa mafundisho ya Yesu, aliwakumbusha wafuasi wa Yesu kwamba Bwana wao

6
alishawawekea siku mpya, yaani ile SIKU YAKE, ndiyo siku ya kwanza ya juma.
Siku hiyo ilikuwa njema na bora kwa kila hali kwani ilikuwa ni siku ya ufufuko wa
Bwana mwenyewe, siku ya kuimarishwa kwao na Roho Mtakatifu na kuzaliwa
Kanisa la Kristo (Pentekoste), siku aliyoitumia Yesu kuwatokea wafuasi wake
baada ya ufufuko wake na hata, kihistoria, siku Mungu alipoanza kuumba
ulimwengu. Na mathali, Pasaka au ufufuko wa Bwana ni uumbaji mpya wa
ulimwengu, siku ya kwanza ya juma ilikuwa kama siku mambo yalipoumbwa
upya. Kwa sifa hizo zote, Wakristo wa mwanzo waligundua haja na uhalali wa
kuhamia siku mpya na kuiadhimishwa kwa Bwana.

Basi Wakristo, mara wakaacha kabisa kuhudhuria ibada za Sabato, wakawa tangu
wakati huo wanakusanyika Dominika tu. Hivyo akitafutwa mtu aliyeanza kuiacha
Sabato turudi hadi kwa mitume katika karne ile ile ya kwanza. Kwa nini walifanya
hivyo? Walifanya hivyo kwa sababu walimwelewa vizuri Kristo kwamba busara
inadai usishonee kiraka kipya kwenye nguo ya zamani na wala usitie divai mpya
kwenye viriba vya zamani. Hayo aliyasema Yesu alipokuwa akiwaeleza Wayahudi
kwamba mafundisho yake mapya hayaoani na desturi zao za kale. Alisema,
“Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile
kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi. Wala watu
hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka,
divai ikamwagika na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya,
vikahifadhika vyote” (rej. Mt 9:16-17).

Kifupi, wanafunzi wa kwanza wa Yesu, ndio mitume na wafuasi wengine,


walioanza, kimatendo, kuachana na Sabato. Tena hayo yanashuhudiwa hata na
maandishi ya kale pia. Mtakatifu Ignasio wa Antiokia, mtu ambaye alimfuatia
Mtume Petro kama kiongozi wa jumuiya hiyo ya mahali maarufu sana, mahali
ambapo jina “Wakristo” lilianza pia kutumika (rej. Mdo 11:26), alipokuwa
akienda kuuawa huko Roma aliandika barua saba za mafundisho na mawaidha
muruwa kwa Wakristo. Kati ya barua hizo, ile iliyoelekezwa kwa wamagnesia,
inasema wazi juu ya mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika. Ameandika hivi,
“Watu (yaani Wakristo) ambao hapo awali walifuata mfumo wa kale wamefika
kwenye tumaini jipya. Hawaifuati tena Sabato kwa sababu wanaweka kitovu cha
maisha yao katika Siku ya Bwana, ambapo Yeye na kifo chake kilitupatia uhai”
(rej. namba 6-9). Na kisha kuhusiana na Wakristo kung’ang’ania mambo ya

7
kiyahudi anaendelea kusema, “Ni upumbavu kuwa na Yesu midomoni na wakati
huo huo kufuata mila za kiyahudi” (rej. namba 10-15).

Wengine Walibaki Kuililia Sabato ya Kale

Hata hivyo, kuachana na Sabato hakukupokeleka na Wakristo wote. Ndiyo kisa


basi Mtume Paulo na watu wengine waliomwelewa na kumwamini Yesu pasipo
mashaka, hawakuacha kuwaelewesha Wakristo kuhusu mabadiliko hayo, asili yake
na sababu zake na kwamba kama Wakristo hawakupasika kubabaishwa tena
kuhusu sikukuu za kiyahudi na Sabato (rej. Mdo 20:7, Kol 2:16, Rum 14: 4-10).

Mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili) yametangazwa katika Ebr 4:1-


10. Mwandishi wa Barua kwa Waebrania, alijihusisha na kuwaelewesha Wakristo
juu ya mabadiliko ya siku kutoka Sabato kwenda Dominika au Jumapili. Ndipo
alipowafafanulia kwamba Mungu alishaifuta Sabato na kuitangaza siku nyingine,
ndiyo Dominika. Na sababu ya Mungu kuifuta Sabato ilikuwa moja tu, ilishindwa
kuwaelekeza watu kwenye kusudio la kuwekwa kwake. Badala ya kuwaelekeza
watu kwenye raha ya milele, iliwatia watu hofu na usumbufu mwingi tu.
Kuhakikisha haya soma vizuri Ebr 4:1-10.

Mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili) yalisubiriwa hata kimantiki


kwa sababu Sabato yenyewe iliwekwa kama kivuli tu (rej. Kol 2:16). Mtume Paulo
au mwandishi wa Barua kwa Wakolosai, awaye ye yote yule, aliingia naye katika
shauri hilo hilo la mahangaiko ya watu na mambo ya kiyahudi. Barua kwa
Wakolosai inasema na kusisitiza kusudi kila mkristo afahamu wazi wazi kwamba
sikukuu za kiyahudi pamoja na sabato vyote vilikuwa vivuli. Yesu alipofika,
ukawa mwisho wa vitu hivyo na hivyo mtu asijaribu kuwababaisha Wakristo kwa
kuwadai warejee huku kwenye mambo ya kiyahudi (rej. Kol 2:16-17).

Sabato Isivyo Chochote Kijiografia

Mabadiliko ya Sabato kwenda Dominika (Jumapili) ni pia mapinduzi ya uelewa


mpevu kwa vile, mbele ya Mungu, siku zote ni sawa. Mungu ni mmoja na siku si
jambo la kwake. Hivyo, ni wanadamu katika ufupi wao wa uhai wanaohangaika na
siku, majuma, miezi, miaka, miongo, karne na milenia. Kwa Bwana miaka mingi
ni kama siku moja tu na siku moja ni kama miaka mingi (rej. 2Pet 3: 8).

8
Basi kwa ukweli huu, siku ye yote inaweza kuadhimishwa kwani anaadhimishwa
kwa Bwana na wala si kwa siku kama siku (rej. Rum 14: 4-10). Biblia, ni kitabu
kilichoandikwa kwa uvuvio na si utunzi wa akili za waandishi tu. Hilo
linadhihirika pia kwenye suala hili hili la Sabato. Kumbe Mtume Paulo
alisemeshwa kinabii na Roho Mtakatifu atufunulie jambo lingelilojulikana vyema
baadaye kwa kukua kwa elimu ya jiografia na kosmolojia. Mtume Paulo katika
Rum 14:4-10 alisemeshwa atuambie tuache mabishano juu ya Sabato, kwa sababu,
mbele ya Bwana, siku zote ni sawa. Jambo hilo kumbe ni kweli kama mtu
atajielimisha katika jiografia.

Kwa kweli, ukijuia vizuri Jiografia huwezi kujisumbua na kuing’ang’ania siku


inayoitwa Sabato au Jumamosi maana siku hiyo hiyo wakati huo huo mahali
pengine ni Jumapili au Jumamosi. Unanibisha? Basi, hujui Jiografia au labda
ulikariri tu huko darasani kwako. Ikiwa hivyo, kaa jamvini pako nikujuvye. Ni
hivi, Jiografia inaweka wazi kwamba, kutokana na kusigana kwa dunia kuliona
jua, kuna siku mbili duniani. Wanakoliona jua kwanza ndiyo huingia asubuhi na
mchana kabla ya kule kuliko na giza bado. Basi, mstari wa kufikirika unaoitwa
“mstari wa tarehe wa kimataifa” (international date line) umechorwa sehemu
fulani huko pande za New Zealand kuitenga dunia katika siku mbili zake. Ndipo
basi, huko mashariki zaidi huwa siku nyingine tofauti na magharibi zaidi. Hivi,
mathalani, upande mashariki ukiwa ni Jumamosi, upande wa magharibi ni Ijumaa
ama mashariki kukiwa ni Jumapili, magharibi ni Jumamosi. Kumbe kwa Mungu
ni siku moja tu, Yeye hana siku za kusigana. Hivyo, kwa ukweli wa kijiografia,
hakuna Jumamosi au Sabato iliyo Sabato. Inategemea ulipo, Sabato ile ile inaweza
kuwa ni Jumapili au Ijumaa. Hivi, ubishi wa Sabato kama siku kuabudu duniani ni
upuuzi mtupu.

Kama hujanielewa hebu nikulete, mara moja, kwenye kitendawili cha kitoto. Ikiwa
watu, huku magharibi, watang’ang’ania kwenda kusali Jumamosi, watakuwa
wamekwenda kusali siku gani kwani masaa yale yale kwa upande wa magharibi ni
bado Ijumaa? Au siku moja baadaye, wengine watakapokwenda kusali
waking’ang’ania kuwa Jumapili, wanakuwa wanakwenda kusali siku gani wakati
huko magharibi ndiyo Jumamosi? Kumbe siku ni mbili kwa binadamu
tunaotegemea kuzipima siku zetu kwa jua. Mbele ya Mungu, asiye na siku, siku
yake ni moja ile ile. Kwa hali hiyo, ukweli unakuwa mmoja kwamba, mbele ya

9
Mungu, siku zote ni sawa na hivyo ye yote anayekusudia kuadhimisha siku,
aiadhimishe kwa Bwana tu asijisumbue na jina la siku (rej. tena Rum 14:4-10).

Wakristo Walikutana Jumapili

Kwa vile Wakristo waligundua kwamba Jumapili, ndiyo iliyokuwa siku yao,
walijizoeza kukutana Jumapili kusali, kumsifu Mungu, kutoa sadaka na michango
kwa ajili ya wenye dhiki. Kwamba mambo yalikwenda hivyo tunasoma katika
Biblia hususan katika 1 Kor 16:1-2. Hapa tunasoma, “Kwa habari ya ile michango
kwa ajili ya watakatifu, kama vile nilivyoamuru makanisa ya Galatia, nanyi
fanyeni vivyo. Siku ya kwanza ya juma (ndiyo siku ya Bwana, Jumapili) kila mtu
kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikwa kwake; ili kwamba
michango isifanyike hapo nitakapokuja.”

Kwa maneno haya, hakuna ubishi kwamba Wakristo wakijipatia desturi ya


kukutana Jumapili kwa sala na shughuli za pamoja. Na hivi walioing’ang’ania
Sabato walikuwa watu wagumu wa kuyapokea mambo mapya, watu ambao
hawakosekani katika shughuli na mahali popote duniani.

Kaisari Konstantino Aliipa Nguvu Kawaida Iliyokuwapo

Baada ya Biblia kuweka sawa habari za Sabato namna hiyo, na Wakristo kujasiri
kuishika siku ya Bwana badala ya siku muflisi, Sabato, katika miaka ya karne ya
nne, alitokea katika historia Kaisari aliyeupenda ukristo. Yeye alikuwa ni matokeo
ya sala za Wakristo kuwaombea viongozi wa dunia wausaidie ukristo ukue
duniani. Kaisari huyo aliitwa Konstantino, aliyetawala tangu 306-337 B.K.,
aliupatia ukristo amani kutoka kwenye madhulumu ambayo makaisari wengi
walikuwa wakilifanyia Kanisa. Yeye akatangaza rasmi kwamba ile siku
inayoshikwa na Wakristo kwa masuala ya sala kwa Mungu wao iwe siku rasmi ya
mapumziko kwa watu wote katika dola yake, yaani dola ya kirumi. Ndipo
mapumziko ya Dominika yakawa rasmi tangu wakati ule. Hii maana yake ni
kwamba Konstantino siye aliyeiunda Dominika na wala siye aliyeanzisha mambo
ya ibada yawe katika siku hiyo. Yeye anakuja kuipatia Jumapili nguvu ya kidola
tu.

Hapa huanzishwa hoja zisizo na miguu wala mikono. Wengine humtaja


Konstantino au Papa fulani, kama mwanzilishi wa Dominika. Historia fupi

10
iliyotolewa hapo juu, yaani mintarafu nyakati za Yesu na baadaye wanafunzi wake,
ndiyo inayotuonesha kwamba Dominika ilianza kuwa siku ya ibada kwa Wakristo
zamani za karne ya kwanza tayari na wala siyo katika karne ya nne. Basi,
kichekesho cha kumtaja Konstantino au Papa fulani kama mwanzilishi wa
Dominika kinaweza kulingana na kichekesho cha mtu atakayemtaja kiongozi
fulani wa leo kama mwanzilishi wa taratibu ya kula au kuvaa kwa binadamu.
Itakuwa ni kichekesho cha mwaka kwa sababu watu wamekuwa wakila na kuvaa
hata kabla kiongozi huo hajaliona jua la ulimwengu huu. Ndivyo ilivyo kwa
Konstantino, hawezi kuanzisha kitu katika karne, kitu kilichoanza kabla hajazaliwa
mwenyewe katika karne ya kwanza.

Kiroja cha Bi Hellen Kufufua Sabato

Kama umenifuatilia vyema, natumaini umeshaelewa kwamba Sabato ilishakufa


katika karne ya kwanza. Kumbe baada ya karne kumi na saba kupita, Wakristo
wakiishika Dominika, akatokea bibi wa kiroja. Bibi Hellen White, ambaye
Wasabato humwita nabii, katika miaka ya 1800 akaja na hadithi kwamba
ameoneshwa maono. Alichukuliwa na Mungu akaingizwa katika hekalu la
mbinguni na humu akaona mbao mbili za amri za Mungu. Katika kuzitazama mbao
hizo akaona zile amri zinang’aa lakini katika kung’aa ile ya Sabato ikawa inang’aa
zaidi kuliko zingine zote. Hapo akawa amejulishwa kwamba amri ile ilikuwa ya
muhimu zaidi. Basi kwa kufuata “maono”, akawasisitizia wanadamu warejee
kwenye Sabato na hapo ndipo likaanza kanisa la Wasabato.

Tuyapime Maono ya Bi Hellen

Tumeagizwa Wakristo tusiipokee kila kinachodaiwa kuwa roho maana mambo


mengine wala si roho ya kweli. Ndiyo kisa, tumeagizwa tuzipime roho. Tunasoma,
“Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho kwamba zimetokana na
Mungu, kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili
mwajua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika
mwili yatokana na Mungu. Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na
hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja. Na sasa
imekwisha kuwako duniani” (1Yoh 4:1-3). Kama sasa tunataka tuyapime maono
ya Bi Hellen White, unaweza kuniuliza mizani au darubini ya kupimia roho ni

11
nini? Jibu kwa swali lako hilo ni rahisi kabisa. Ni kwamba hakuna mizani wala
darubini nyingine tofauti na Maandiko Matakatifu hayo hayo.

Maono ya Bi Hellen ni Uongo Kibiblia

Sasa hebu tuyapime maono ya Bi Hellen White kwa maneno ya Maandiko


Matakatifu. Nikisema kwa mkato maono hayo ni ya uongo na hivyo ujumbe wake
ni wa uongo na sisi Wakristo tusithubutu kuufuata kwa sababu sisi tunapaswa
kufuata kilichopo kwenye Biblia au kile kilichosemwa na Bwana mwenyewe na
kutufikia sisi kwa Biblia au kwa njia ya maelezo ya wale waliokula na kunywa
pamoja naye. Ukichuanisha na maneno ya Biblia, uongo wa Nabii Bibi Hellen
White, unaanzia kwenye mazingira ya maono yenyewe. Mazingira ni ya uongo
kabisa kwa sababu Biblia, kwa kupitia mwandishi wake aliyevuviwa na Roho
Mtakatifu, ukipenda jina Yohana Mtakatifu katika kitabu chake cha Ufunuo,
inasema mbinguni hakuna hekalu na wala hakutakuwa na hekalu (rej. Ufu 21:22-
23). Imeandikwa, Nami sikuona hekalu ndani yake, kwa maana Bwana Mungu
Mwenyezi na Mwanakondoo, ndio hekalu lake. Na mji ule hauhitaji jua wala
mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni
Mwanakondoo. Na mataifa watatembea katika nuru yake. Na wafalme wa nchi
huleta utukufu wao ndani yake”. Kama Maandiko yanasema hivi, iweje basi Hellen
White alione hekalu wakati halipo? Mkweli nani? Yeye au Biblia?

Mwito wa Bi Hellen ni Kinyume na Mafundisho ya Yesu

Zaidi ya hapo, ukipima tena maono hayo kwa mujibu wa Maandiko Matakatifu,
uongo wenyewe umejipandikiza katika kupingana na kauli ya Mwana wa Mungu,
mwalimu wa kwanza na wa kweli kupita wanadamu wote wenye nyama na mwili.
Yesu alipoulizwa amri ipi ni kuu kuliko zingine, alijibu mara moja kwamba ni ile
ya kumpenda Mungu na jirani aliye sawa nasi (rej. Mt 22:34-40, Mk 12:28-34, Lk
10:25-28). Hata Yesu Kristo ametuachia upendo kama amri na alama
itakayotutambulisha Wakristo po pote duniani wala siyo Sabato (rej. Yn 13:31-35).
Sasa wakati Yesu Kristo anasema hayo yote iweje Nabii Bibi Hellen White awe na
jibu la Sabato? Tazama, mbona anachosema Bi Hellen ni tofauti na kile alichosema
Kristo hata kabla ya yeye hajazaliwa?

Kama huo si upinga Kristo, ni nini tena? Hapo ndipo anapoingia Bi Hellen na siku
hizi msimamo wake kuendelezwa na wafuasi wake. Na Maandiko yanasema mtu

12
akianza tu na hatua ya kupingana na Kristo anakuwa sababu ya mabishano,
magomvi na fujo zingine hatari na mwishowe kuishia katika shughuli za biashara
ndani ya dini. Ndugu yangu, jambo hili ni la kweli asilimia mia moja na ni bayana
kwa kila anayeweza kumtathimini vizuri Bi Hellen na sasa wafuasi wake
wanaomfuata baada ya kuasiana na Kanisa Katoliki.

Fungua macho utaona na kushuhudia mwendo huo wa mambo. Hakika Biblia


haisemi uongo. Sikiliza alivyoonywa Timotheo na mzee wa mang’amuzi yaani
Mtume Paulo. Kijana aliambiwa, “Unapaswa kufundisha na kuhubiri mambo haya.
Mtu yeyote anayefundisha kinyume cha mambo haya, na ambaye hakubaliani na
maneno ya kweli ya Bwana wetu Yesu Kristo na mafundisho ya uchaji wa Mungu,
huyo amejaa majivuno na wala hajui chochote. Ni mtu wa kupenda ubishi na
magombano juu ya maneno matupu na huyo husababisha wivu, ugomvi, matusi,
shuku mbaya, na ubishi usio na kikomo kutoka kwa watu ambao akili zao
zimeharibika, na ambao hawana ukweli. Wanadhani dini ni njia ya kupatia utajiri”
(1Tim 6:1-6). Kama kweli wewe unamwogopa Mungu, utatambua kwamba haya
hizi zilikuwa zinawatabiri Wasabato. Kama huniungi mkono sasa hivi, nakuomba
ukae chini uwachunguze na kuwatathmini Wasabato ukianzia asili yao, mambo
yao wanayosema na kufanya na jinsi wanaitumia dini sasa hivi. Ikitokea kwamba
mimi nimekosea, nipigie simu nikuombe radhi.

Wewe Unamfuata Nani Kiimani?

Hapa mimi natoa uhuru kwa kila msomaji wa kijitabu hiki. Ni kwamba hapa kila
Mkristo aamue mwenyewe kumfuata Yesu Kristo Bwana wake au kusikiliza vioja
vya Bibi Hellen White na pia kujiunga na Wasabato wanaojaribu kututiriza
Wakristo wenzao kana kwamba tumewakosea. Mimi na roho yangu naisikiliza
Biblia na kumfuata Yesu Kristo, Bwana wangu. Mimi siwezi kumfuasa
mwanadamu ambaye kwa vipimo dhahiri vya Maandiko Matakatifu anapingana na
Kristo Bwana wangu. Siwezi kumfuata mpinga Kristo, labda niwe nimelewa au
nimechanganyikiwa! Wewe, ndugu yangu, amua mwenyewe leo baada ya maelezo
haya.

Turudie, Mungu Mwenyewe Ndiye Aliyebadili Sabato

Hatimaye, ndugu yangu, Wakristo lazima tukubaliane kwamba ni Mungu


mwenyewe aliyeibadili Sabato kwenda Jumapili. Basi, mabadiliko hayo

13
hayakuletwa na Wakatoliki wala na viongozi wao, wala si na Papa fulani wala
mfalme Kostantino. Hilo tumeoneshwa wazi wazi katika Maandiko Matakatifu
ambayo yanatuwekea wazi ukweli kwamba Bwana Mungu wetu ametuwekea siku
nyingine badala ya Sabato ya kale. Tuasindikie mate wino ungalipo. Ushuhuda wa
kwamba Sabato ilifutwa na kuwekwa siku nyingine uko wazi kabisa kwani katika
Maandiko Matakatifu tunasoma hivi:

“Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuiogope, mmoja wenu
asije akaonekana ameikosa. Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema
vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu
halikuchanyikana na imani ndani yao waliosikia. Maana sisi tulioamini tunaingia
katika raha ile: Kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu,
Hawataingia rahani mwangu: ijapokuwa zile kazi zilimalizika tangu kuwekwa
misingi ya ulimwengu. Kwa maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi,
Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote; na hapa napo,
Hawataingia rahani mwangu.

Basi, kwa kuwa neno hili limebaki kwamba wako watu watakaoingia humo, na
wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi
kwao, AWEKA TENA SIKU FULANI, akisema katika Daudi baada ya muda
mwingi namna hii, Leo kama ilivyonenwa tangu zamani, Leo, kama mtaisikia sauti
yake, Msifanye migumu mioyo yenu. Maana kama Yoshua angaliwapa raha,
asingalinena siku nyingine baadaye. Basi, imesalia raha ya Sabato kwa watu wa
Mungu. Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe
katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi yake. Basi, na tufanye
bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu yeyote asije akaanguka kwa mfano
huo huo wa kuasi “(Ebr 4:1-10).

Mwandishi ananeneshwa na Roho Mtakatifu hapa. Sababu ya kufutwa Sabato


inatolewa hapa. Ni kwa sababu Sabato ya kale ilishaharibiwa kabisa na haikuweza
kumpa yeyote manufaa yoyote. Ndipo basi ilifutiliwa mbali na Mungu mwenyewe.
Ukilinganisha Sabato na mkeka uliopasuka, basi mwenye nyumba ameukataa na
kuutupilia mbali. Sasa kama muasisi wa Sabato mwenyewe ameitupilia mbali,
wewe na mimi ni nani hata tuikote na kuing’ang’ania upya?

14
Kurudia Sabato ni Kuukarabati Mkeka Uliotupwa

Kwa kuwa ukweli ndio huo nilikueleza hadi sasa, si busara kuukarabati wala
kuuokota mkeka wa zamani kama mwenye nyumba ameamua kuleta mkeka mpya.
Mungu alishaitupilia mbali Sabato iweje tuirudie tena? “Tumerogwa”?

Mungu alishaona Sabato haitufai sisi tunaochukua mahali pa taifa la Israeli ya


zamani. Kwa kifupi, ni kusema kwamba zile sababu za kushika Sabato walizopewa
Wayahudi, zimepinduliwa na kubwagwa na Mungu mwenyewe. Ziliwafaa
wenyewe na Agano lao la Kale. Zilikuwa sababu za taifa la Kiyahudi, kumbe sisi
ni Wakristo, taifa jipya llilokombolewa na Yesu kutoka dhambini na kwenye mauti
kwa damu yake azizi. Sisis si Wayahudi waliokombolewa na Mungu kwa mkono
wa Musa toka utumwani Misri na baadaye wakatakiwa kuishika Sababo ya kale
vinginevyo wengeadhibiwa kwa mateso mbalimbali pamoja na kupelekwa
utumwani.

Hayo yote yalikuwa maamrisho ya mfano wa ukombozi wetu halisi. Si hilo tu, bali
maelezo na taarifa hii kwamba Sabato ya kiyahudi imesitishwa imetoka kinywani
mwa Mwana wake wa pekee, ndiye Yesu Kristo ambaye wote tumeamriwa
tumsikilize kwani ndiye ufunuo wa kweli wa Mungu (rej. Ebr 1:1-4). Narudia
kusema, yale yote yalikuwa ni mfano tu. Mahali pa Musa palikuwa pa Yesu
mwenyewe na mahali pa kivuli cha Sabato palikuwa pa Siku ya Bwana ndiyo
Dominikla au Jumapili. Lakini husikika pia hoja ya kuchekesha kwamba eti
ukishika Jumapili ambayo inaitwa “Sun-day” unamwabudu mungu jua ambaye
alikuwa akiabudiwa siku hiyo.

Ndugu zanguni hii ni hoja kweli? Mbona hii ni hewa tu? Ikiwa ni hivyo nani
anasalimika na uabudu miungu? Mbona kila siku kulikuwa na mungu fulani
anayeabudiwa? Tuache utoto. Hiyo ingekuwa na maana Waislamu wanaoabudu
siku ya Ijumaa, wanamwabudu mungu aliyekuwa anaabudiwa Ijumaa. Na hapo
hapo ingemaanisha kuishika Sabato ambayo inaitwa Saturday kwa Kiingereza
maana yake ni hiyo hiyo yaani kumwambuidu “mungu satur” ambaye alikuwa
akiabudiwa siku hiyo, yaani Sabato ya Wayahudi. Basi, tuache hoja isiyo na
mashiko kama hii. Majina ni mbali na ibada kwa mungu fulani ni mbali. Ibada
haikai kwenye jina la siku au mwezi isipokuwa katika nia kamili ya mtu, imani na
matendo halisi ya kumsujudia huyo anathaminiwa kama mungu.

15
Ubora na Utukufu wa Siku Mpya, Jumapili

Tukirudia mada yetu, ni kwamba wala haina utata siku iliyowekwa pahala pa
Sabato, ni siku ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambapo hata uzima wetu
unafufuliwa na ni siku hiyo pia Roho Mtakatifu alipowashukia mitume na
kuanzisha Kanisa takatifu na kazi ya uinjilishaji duniani (ndiyo siku ya Pentekoste)
kama tunavyosoma bila shida katika Mdo 2:1-13. Kwa sababu hiyo, Dominika ni
siku tukufu kuliko siku zingine zote kwa vile ndiyo utimilifu wa lengo la Sabato na
kupita Sabato. Basi, kwa mujibu wa amri ya kwanza na ya tatu ya Mungu, Kanisa
huadhimisha SIKU YA BWANA. Ndipo binadamu tumeamriwa kufanya kazi kwa
siku sita, yaani kutenda mambo yetu yote, lakini tuiweke siku ya Sabato ya Bwana
(Dominika) kama siku takatifu kwa Bwana na kustarehe kabisa.

Kuitunza Sabato ni Kusherekea Mkesha wa Siku ya Uhuru

Kuitunza Sabato mbele ya Dominika ingelingana na kusherekea mkesha wa siku


ya uhuru badala ya siku ya uhuru yenyewe. Taifa litakalofanya hivyo litachekesha
na labda litakuwa la watu punguani. Aidha mtu kupita huko na huko kuwahimiza
watu washerehekee mkesha wa uhuru badala ya siku ya uhuru wenyewe
ingelikuwa sawa na kucheza Ze Comedy.

Nani amegeuka mkondo wa mambo hata kugeukia tena Sabato wakati Wakristo wa
kwanza kwa kumwelewa vyema Yesu Kristo walishaitupilia mbali? Jibu ni wazi.
Ni mmoja wa waanzilishi wa dhehebu la Wasabato, yule mama anayejulikana
kama nabii. Kwa taarifa yako waanzilishi wa dhehebu la Wasabato ni akina Hiram
Edson, Joseph Bates, E.G. Harmon na Hellen White. Katika hawa aliyekuja na
moto wa kurudisha Sabato ni huyo mama ambaye alikuwa mke wa E.G. Harmon.
Mwanamke huyo anaheshimiwa na Wasabato kama nabii na vitabu vyake, kama
vile Vita Kuu, Afya na Raha na Ushindaji, vinasomwa na Wasabato karibu kama
misahafu.

Wasabato Wasimnyanyase Yeyote

Maono ya uwongo ya Bi Hellen yasiwe sababu ya kuwanyanyasia Wakristo wasio


Wasabato. Wala si siri, makanisa yanayofuata mabadiliko yaliyoletwa na Mungu
mwenyewe kutoka Sabato kwenda Dominika yananyanyaswa kweli kweli na kauli
za Wasabato wanaomfuasa Bi Hellen White. Lakini, hivi unabii wa mama huyo ni

16
wa kweli hata tutishike nao? Hapana, wala si wa kweli. Unabii wa mama huyu
lazima tuukatae. Kwa nini tuukatae?

Tuhimizane Tumkatae Bi Hellen na Maono Yake

Ni kwa sababu kuna sababu tatu zinazotuhalalisha tumkatae kama nabii. Mosi,
kitabu cha Ufunuo kinaonesha kufungwa kwa unabii, yaani kwamba baada ya
mambo yaliyoandikwa humo kusingekuwa na ufunuo wowote wa pekee.
Ukamilifu wa ufunuo ulitokea katika ujio wa Yesu Kristo. Alichosema yeye
ndicho kitu cha kilele. Sasa Bi Hellen anakujaje na mapya kumpikua Yesu Kristo?
Tunasoma, “Mungu ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa
sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi, amesema na sisi katika
Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.
Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wa wake na chapa ya nafsi yake,
akavichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi,
aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu, amefanyika bora kupita malaika kwa
kadiri jina alilorithi liliyo tukufu kuliko lao” (Ebr 4:1-4).

Si hivyo tu hata mintarafu ufunuo wa zamani mihuri yake imevunjwa na Yesu


Kristo mwenyewe, sasa yeye unabii wa Hellen White unaanzia wapi? Tunasoma,
“Kisha nikaona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha
enzi kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba. Nikaona
malaika mwenye nguvu akihubiri kwa sauti kuu, Ni nani astahiliye kukifungua
kitabu na kuzivunja muhuri zake. Wala hapakuwa na mtu mbinguni, wala juu ya
nchi, wala chini ya nchi, aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama.
Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kikifungua hicho
kitabu, wala kukitazama. Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie;
tazama Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate
kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba.

Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale
wazee, Mwanakondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye
pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika
dunia yote. Akaja , akakitwaa kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye
aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi. Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai
wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya Mwanakondoo, kila

17
mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni
maombi ya wakatakatifu, nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe
kukitwaaa hicho kitabu na kizifungua muhuri zake, kwa kuwa ulichinjwa,
ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na
taifa, ukawafanya kuwa ufalme wa makuhani, kwa Mungu wetu, nao wanamiliki
juu ya nchi” (Ufu 5:1-10).

Mintarafu kusasambua ovyo ufunuo wa Mungu, mwandishi wa kitabu cha Ufunuo


alishakatazwa, sasa Bi Hellen White anapata wapi nguvu ya kuja na ufunuo mpya?
Kuhusu marufuku hiyo tunasoma, “Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao,
nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie
muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike” (Ufu 10:4).
Hatimaye, maneno ya ufunuo yaliachwa wazi bila muhuri kwa vile yalivyokuwa
njiani kutimia. Juu ya jambo hili, tunasoma hivi: “Akaniambia, Usiyatie muhuri
maneno ya unabii wa kitabu hiki kwa maana wakati huo umekaribia” (Ufu 22:10).
Sasa Bi Hellen White anaongezaje maneno ya ufunuo mpya?

Pili, tuukatae unabii wake kwa vile zile anazoziita njozi, kama elfu mbili hivi, ni
batili kwani zinaonesha jinsi alivyojaa chuki kwa Baba Mtakatifu na Kanisa
Katoliki nasi tunajua kwamba si kazi ya Mungu Roho Mtakatifu kumjaza mtu
chuki kali hivyo dhidi ya mwanadamu mwingine. Kazi hiyo hufanywa na Shetani
nayo huonesha kwamba moyo wa mtu umejaa uovu kwani kilichomjaa mtu
moyoni ndicho kimtokacho. Tunasoma, “Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao
matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti
hutambulikana kwa matunda yake; maana katika miiba hawachumi tini, wala
katika michongoma hawachui zabibu. Mtu mwema katika hazina njema ya moyo
wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa
yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake”
(rej. Lk 6:43-45). Hakika chuki dhidi ya Baba Mtakatifu na Kanisa Katoliki
inatoka katika moyo uliofurika uovu. Na kwa jinsi hii maono yake hayawezi
kutoka kwa Roho Mtakatifu.

Tatu, tuukatae unabii wake kwa sababu mafundisho yake yanaonesha kwamba
haijui Biblia. Hoja hii ya tatu nimeshaishuhudia tayari. Nimesema ameota ndoto
akaona huko mbinguni kuna hekalu wakati Maandiko yanatakaa jambo kama hilo
(rej. tena Ufu 22:22-24). Kisha nimeshashuhudia kwamba kule kusisitiza kwamba

18
Sabato ndiyo amri kuu kunapinga na kile alichotuambia Bwana wetu Yesu Kristo
aliyesisitiza kwamba amri kuu ni upendo (rej. tena Mt 22: 34-40). Naomba itoshe
nilivyokuambia nawe uyapuuze maono ya Mrs. Harmon tunayemchambua hapa.

Majibu kwa Mashtaka ya Ziada

Nikiendelea kidogo, naomba ruksa nijibu mashtaka mawili sambamba wanayotoa


Wasabato dhidi ya Wakatoliki: mosi kwamba ndio mnyama yule Shetani aliyejipa
jukumu la kubadili majira na pili kwamba Kanisa lenyewe linakiri kufanya hivyo
katika Katekisimu zake na katika vitabu vya waandishi fulani fulani wa Kanisa
Katoliki.

Mintarafu hoja ya kwanza ni hivi mnyama ni Bi Hellen White aliyethubutu


kumpinga Mungu. Mungu aliibadili siku ya Sabato yeye akijipa jukumu la
kuirudisha kwa maelezo ya maono yake batili kabisa. Tumeshaonesha jinsi yalivyo
batili kwa kadiri ya mizani na darubini ya Maandiko Matakatifu.

Halafu mintarafu hoja ya pili ni hivi Kanisa linajihusisha na mabadiliko hayo si


kama ‘mtendaji’ kwani hakuna mkutano mkuu (mtaguso) wowote wa Kanisa
Katoliki uliojadili hoja ya Sabato na kuamua kuibadili kwenda Dominika ila
kwamba Mungu aliibadilisha Sabato pale alipoanzisha enzi ya Israeli mpya yaani
Kanisa. Natumaini wasomaji wangu hoja hii si ya kitaalamu mno kiasi cha
kutonielewa ninachosema. Ninasema hivi Kanisa linajisikia kuhusika na
ubadilishaji wa Sabato kwenda Dominika kwa vile Mungu aliufanya kuanzia pale
lilipoanza kuwako nalo kwa mamlaka yaliyopata kutoka kwa Mungu ikayasimamia
na kuyaendeleza mabadiliko hayo.

Malumbano Sasa Yakome

Naomba hadi hapa shtaka la kwamba Kanisa Katoliki limebadili majira, yaani
kutoka Sabato kwenda Dominika (Jumapili), lififie kabisa. Si unajua kwamba hoja
yenyewe hukokotolewa kutoka Dan 7:25 mahali palipoandikwa, “Naye atanena
maneno kinyume chake Aliye Juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye
Juu, naye ataazimu kubadili majira na sheria”.

Kama unavyoisoma sasa, hoja hii haitaji Kanisa Katoliki bali kwa kinyume chake
inawataja Wasabato wenyewe. Ndugu zangu Wasabato hawalifahamu jambo hili
kwa sababu ndivyo ilivyo, “Jambo usilolifahamu ni sawa na usiku wa giza.” Kwa

19
vipi? Ni hivi, kama Yesu kwa maneno na matendo yake alisema Sabato si lolote na
wala si chochote “maana mtu hakuuumbwa kwa ajili ya Sabato”, mtu anayesema
Sabato ndiyo yote katika yote ndiye anayeazimu kubadili majira na sheria. Na
moja kwa moja mtu huyo anakuwa ndiye mpinga Kristo kwa sababu anapingana
na kauli ya Kristo mwenyewe. Hilo ndilo alilofanya Nabii Hellen na
kuwasadikisha maelfu ya watu kauli yake kengeufu.

Aidha, kama Yesu alisema kwamba amri kuu ni upendo (rej. Mt 22:37) na akataka
iwatambulishe wafuasi wake popote watakapokuwapo (rej. Yn 13:35), anapokuja
Nabii Hellen na kusema eti amri kuu ni Sabato ni upinga Kristo wa wazi wazi na
kumfuasa mpinga Kristo kama huyo ni kuwa wapinga Kristo wadogo wadogo
nyuma ya huyo mkubwa. Ona ushuhuda wa Maandiko Matakatifu. Bila shaka, hata
wewe unakumbuka Yesu aliulizwa swali juu ya amri ya kwanza na kuu naye
akatoa jibu mwafaka hata wasomi na walimu wa enzi zake wakamvulia kofia.

Tunasoma, “Na Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale


Masadukayo, walifanya shauri pamoja. Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza,
akimjaribu: Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende
Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili
zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo,
nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea
torati yote na manabii” na wakati akiwaaga wanafunzi wake jioni iliyotangulia kifo
chake alisema na kuagiza, “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi
mmekuwa wanafunzi wangu mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yn 13:35). Sasa
Nabii Hellen anathubutuje kusema kinyume cha maneno hayo ya Kristo ambaye
tumepewa tumsikilize? Kama huo si upinga Kristo wenyewe ni nini tena?
Hatukumbiki maneno ya Maandiko Matakatifu, “Huyu ni mwanangu, mpendwa
wangu, msikieni yeye” (Mk 9:7)? Na kwa upande wetu, kwa nini, tunamsikiliza
binadamu tena? “Tumechanganyikiwa” au “tumerogwa”?

Hatima: Tusihangaishane Juu ya Sabato Ilikuwa Kivuli tu

Kwa sasa hitimisha fikra zako kwa nukuu hii: “Basi, mtu asiwahukumu ninyi
katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi ,
au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo. Mtu
asiwanyang’anye thawabu yenu, kwa kunyenyekea kwa mapenzi yake mwenyewe

20
na kuabudu malaika, akijitia katika maono yake na kujivuna bure, kwa akili zake
za kimwili; wala hakishiki Kichwa, ambacho kwa yeye mwili wote ukiruzukiwa na
kuungamanishwa na viungo na mishipa, hukua kwa maongeo yatokayo kwa
Mungu” (Kol 2:16-19).

Basi, kifupi, tumeamriwa tuikumbuke Dominika, tuitakase na tusifanye kazi yotote


nzito. Kwa kisa hicho, ndugu yangu sisi tuhudhurie misa takatifu na kama haipo
misa basi tuhudhurie ibada bila padre na kwa ujumla tuitakaase vyema siku hiyo.
Matendo hayo yote ndiyo mwonjo halisi wa raha itakayoisikia siku ile ya mwisho
Sabato (Dominika) ya mbinguni.

21

You might also like