You are on page 1of 14

Mwalimu Mwingisi

Utangulizi
Kazi za fasihi huchunguzwa kwa kina ili kupata uhakika wa maudhui na kufafanua vipengele
muhimu kama lugha ilivyotumika. Nadharia nyingi zimewekwa ili kuhakiki kazi hizi za fasihi.
Kwanza, dhana hii ya nadharia imetolewa maelezo na wasomi mbalimbali; kama vile
(J. S Mdee na wenzake, 2011) wanaeleza kwamba nadharia ni mpango wa mawazo uliotungwa
ili kuelekeza jinsi ya kufanya au kutekeleza jambo fulani. Kwa msingi huo nadharia hubeba
mawazo, dhana au maelezo yatolewayo kwa nia au kwa lengo la kueleza hali fulani, chanzo,
muundo, utendaji na mwingiliano wa ndani na nje. Sengo naye (2009) anafasili nadharia kuwa
ni wazo kuu, fikra kuu, mwongozo mkuu wa mtu, watu au jamii ya pahala fulani, wakati fulani
na kwa sababu fulani. Tukirejelea mawazo yake, tunaweza kufasiri dhana hii kuwa dira na
mwongozo wa kulikabili jambo kifalsafa, kidini, kimantiki, kijamii na kiutamaduni. Pia inaweza
elezwa kuwa ni mawazo au mwongozo unaomwongoza mtafiti au mchambuzi wa jambo fulani
ili kuweza kulikabili jambo hilo ambalo halijapata kupatiwa ufumbuzi au ukweli wake.

TUKI (2004) wanafasiri nadharia kuwa ni mawazo, maelezo au mwongozo uliopangwa ili
kusaidia kueleza, kutatua au kutekeleza jambo fulani. Kulingana na maelezo ya Wafula R. M
(2004) nadharia husheheni mwongozo wa mikakati ya usomaji wa kazi ya fasihi na hucheza
nafasi ya dira katika kuhakiki na kufanya unamuzi fulani. Kwa upande mwingine wasomi
Wafula na Njogu (2007) wanafafanua na kupambanua nadharia kuwa jumla ya maelekezo
yanayomsaidia msomaji au mhakiki kuifahamu kazi ya fasihi kwa kufuata utaratibu maalumu.
Wanadokeza zaidi kuwa dhana hii hurejelea istilahi ya kijumla inayomaanisha mwongozo
unaomwelekeza msomaji wa kazi ya fasihi kuifahamu kazi hiyo vizuri katika vipengele
mbalimbali vya kazi ya fasihi na namna vinaunganika kuleta umoja katika kazi husika. Kwa
mfano jinsi maudhui hulingana na manthari au jinsi mandhari yanavyolingana na wahusika
katika kazi ya fasihi.

Mwalimu Wamitila (2003) anaeleza kuwa nadharia hutumiwa kumaanisha kauli za kijumla au
kaida zinazomwongoza msomaji katika ufasiri wa maana uliopo katika fasihi. Kwa mfano
katika kuelewa maudhui katika kazi ile ya fasihi. Fauka ya hayo, anasema kuwa ni njia ya
kisayanzi inayohusika na kanuni za kijumla na zinazohusika katika utatuzi wa swala fulani
katika kazi ya kifasihi na pia ni nyenzo ya kufikia malengo fulani ya kiusomi.
Nadharia za kuhakiki hata hivyo ni nyenzo tu ya kutusaidia kulifikia lengo fulani na kila nyenzo
huwa na ubora na udhaifu. Vilevile nadharia huzuka katika mazingira maalum ambayo yana

1
Mwalimumwingisi@gmail.com,
Chuo Kikuu Cha NAIROBI
Mwalimu Mwingisi

wasifu na utamaduni mahususi. Hii ni kumaanisha kuwa, hatupaswi kupofushwa na nadharia


kiasi cha kutotambua kuwa zina udhaifu wa kuvimulika vipengele fulani vinavyohusiana na
lugha na fasihi zetu.
Nadharia za kuhakiki vilevile huathiriana sana. Huwa vigumu kuongea kuhusu swala la ubunifu
katika nadharia yoyote ya kuhakiki. Madai haya yenye mashiko yametambuliwa na wasomi
maarufu kama vile Wellek.

Zaidi ya hayo, nadharia hizi zimegawika katika makundi mengi kutegemea malengo na mbinu
zake. Kunazo zinazomulika maswala bia ya kiulimwengu yanayotokeza katika fasihi,
zinazohusiana na saikolojia kama vile saikolojia changanuzi, zinazohusiana na visasili,
zinazojihusisha na maswala ya jamii, za umuundo wa fasihi miongoni mwa zingine nyingi.
Baadhi ya nadharia hizi ni kama vile, nadharia za kisosholojia, za kifeministi, semiotiki,
naratolojia n.k

Nadharia ya Ufeministi
Ufeministi ni dhana itokanayo na neno la kilatini 'femina' linalomaanisha mwanamke. Dhana
hii inarejelea uwakilishaji wa haki za wanawake kufuatana na imani ya usawa wa kijinsia.
Imejikita sana katika mwamko wa wanawake unaolenga kupigania na kukomesha udhalimu
dhidi yao na kufichua matatizo wanayoyapitia katika jamii.

Mbatiah (2001) anaeleza kuwa Ufeministi ni nadharia ya fasihi ambayo inajishughulisha na


utetezi wa haki za wanawake dhidi ya ugandamizwaji katika jamii yenye mfumo uliodhibitiwa
na wanaume. Kulingana na mawazo yake, nadharia imedhamiria kuupigania ukombozi wa
mwanamke kutokana na pingu za kitamaduni, kiuchumi, kidini, kijamii na kisiasa. Pingu
anazozirejelea ni misimamo ya itikadi ya kiume ya ubabedume.

Mawimbi ya kifeministi yalianza kuvuma ulimwenguni katika karne ya kumi na tisa na


yakashika nguvu miaka ya sitini na sabini ya karne ya ishirini. Kulingana na Ntarangwi (2004)
nadharia ya Ufeministi iliibuka katika muungano wa ukombozi wa wanawake uliopamba moto
katika miaka ya sitini huko Marekani. Wakati huo, wanawake hasa wa Kimagharibi walianza
kuzungumzia matatizo yao kwa kuyaandika.
Kwa uwazi na ubayana maswala ya kifeministi yalishika mizizi miaka ya sitini. Kulikuwa na
jitihada mbalimbali za kupigania usawa baina ya wanaume na wanawake ingawa

2
Mwalimumwingisi@gmail.com,
Chuo Kikuu Cha NAIROBI
Mwalimu Mwingisi

hazikuchapishwa kama anavyodai Bonny Onyoni (2002). Kwa mfano, katika nchi ya Ufaransa
kuanzia mwaka 1789 hadi mwaka 1795, inadaiwa kulikuwa na maandamano ya wanawake
kutetea kudunishwa walichokiita 'Msimbo wa Napoleon'. Katika tetesi zao, walidai kuwa
kiongozi Napoleon alikuwa amesema kuwa, akili za wanawake ni dhaifu zikilinganishwa na za
wanaume. Kwa hivyo, wanawake walifaa kupewa elimu ya kiwango cha chini kama ya
ushonaji. Hili lilipelekea wanawake hao kuandamana wakitaka madai hayo kutupiliwa mbali.

Marekani Kaskazini mwaka wa 1848 pia kulikuwa na kundi la wanawake lililoungana katika
juhudi za kuleta ukombozi wa wanawake. Kulifanyika mkutano jijini New York ambapo
wanawake walitangazwa kuwa huru katika misingi ya kukubaliwa kupiga kura, kupewa elimu
ya kutosha, kupewa nafasi sawa za kufanya biashara, usawa wa kupata fidia, usawa wa kisheria
na kupata ajira. Ithibati za kimaandishi za kifeministi zenye utaratibu na zilizowekea msingi
nadharia ya ufeministi ni ‘A vindication of the Rights of Women’ ya Mary Wollstonecraft
(1792) na ‘A Room of One's Own ya Virginia’ Woolf (1929). Mary Woollstonecraft ni
mwandishi aliyeasisi mazungumzo kuhusu maswala ya wanawake na kulalama kuhusu hali
wanawake walikuwa wanapitia katika jamii. Simone de Beauvoir katika kazi yake ya ‘The
Second Sex’ mwaka wa 1952 alichangia pakubwa maendeleo ya uhakiki wa kifeministi. Katika
kazi yake alibainisha, kukosoa na kupiga vita asasi zilizomdhalilisha au kumdunisha
mwanamke. Alizifafanua asasi zinazowadunisha wanawake kama vile dini, ndoa na utamaduni.
Beauvoir anasema kuwa dini humkandamiza mwanamke kwa kumfundisha kunyenyekea. Ndoa
nayo imejengwa kwenye misingi na imani ya uwezo mkubwa alionao mwanamume
akilinganishwa na mwanamke. Kulingana naye ndoa, humsawiri mwanamke katika tamathali
hasi na duni.

Mwandishi mwingine ni Kate Millett katika kazi ya ‘Sexual Politics’ anaonyesha athari kubwa
katika historia ya Ufeministi. Millett aliwashambulia sana waandishi wanaume kama vile Henry
Miller, Norman Miller, Jean Gennet na D.H.Lawrence kutokana na jinsi walivyowasawiri
wahusika wa kike. Kutokana na aliyoyagundua katika kazi hizo, Millett anabainisha kuwa
miundo ya kijamii pamoja na asasi zake zinashirikiana kumkandamiza mwanamke. Millett
vilevile anaikosoa mikabala ya saikolojia changanuzi ya Sigmund Freud kwani ina mapendeleo
makubwa kwa mfumo wa ki-ubabedume. Mwanasaikolojia huyu alidai kuwa mtoto wa kike
huanza kujichukia mara tu anapogundua kuwa hana kiungo cha kiume. Hali hii husababisha
alichokiita `wivu’ wa zubu'. Kutokana na wazo la 'wivu wa zubu' la Freud, Millet anaeleza kuwa

3
Mwalimumwingisi@gmail.com,
Chuo Kikuu Cha NAIROBI
Mwalimu Mwingisi

wivu uliopo ni wa uwezo alio nao mwanamume kutokana na muundo wa kijamii. Mwanamke
anakuwa na wivu wa kinachoashiriwa na hilo zubu wala sio zubu kama kiungo cha mwili.

Hali kadhalika, msomi wa Kinigeria Bi. AbiodunOgundipe-Leslie (1994) anasema kuwa


wanawake wamepewa majukumu duni na yanayosawiriwa kwa ubaya kama vile kuwa wachawi
na wanaume nao husawiriwa kuwa werevu, wenye nguvu na kuaminika na wenye uwezo wa
uongozi kwa kuzaliwa. Ogundipe-Leslie anaeleza hali kama hii huchangia kumdunisha na
kumtesa mwanamke katika jamii.

Nadharia ya Ufeministi, imegawika katika matapo mbalimbali kutegemea vigezo mbalimbali.


Wafula na Njogu wanaeleza kuwa matapo haya hubainishwa kupitia njia za kiitikadi na
kimaeneo. Mkabala wa kiitikadi unahusu mitazamo mitatu ambayo ni, Ufeministi Huru,
Ufeministi wa Kijamaa na Ufeministi wa Kimapinduzi. Ufeministi Huru hutetea usawa kati ya
wanawake na wanaume katika ngazi zote za maisha. Ufeministi wa Kijamaa hujishughulisha na
ukosoaji wa jamii na kuwahimiza wanaume kushiriki katika malezi ya watoto na kadhia
nyingine ambazo kimapokeo zimechukuliwa kuwa kazi za wanawake. Ufeministi Kimapinduzi
humchukulia mwanamume kama adui mkubwa zaidi wa mwanamke. Huhusisha ukandamizwaji
wa mwanamke na tofauti za kimaumbile. Pia hushikilia kuwa wanawake wanapaswa waitawale
miili yao na hata wasiolewe.

Njia ya kuainisha matapo ya Ufeministi kimaeneo huhusisha Ufeministi na maeneo ya


kijiografia. Waainishaji wa kimaeneo ni Mary Eagleton (1991) na Ross Murfin (1991).
Wanaugawa ufeministi katika matapo manne. Kwanza, Ufeministi wa Kifaransa, Ufeministi wa
Kingereza, Ufeministi wa Kimarekani na Ufeministi wa Kiafrika. Kwanza katika tapo la
Ufeministi wa Kifaransa unalenga kufafanua jinsi lugha hutoa maana ya mtumiaji wake.
Wanadai kuwa lugha kama inavyotumiwa ni zao la taasubi za kiume. Wanasema kuwa lugha
inampendelea mwanamume kuliko mwanamke. Jazanda za kuelezea uwezo, nguvu na mamlaka
ni za kiume na ilhali zile zenye kusawiria ulegevu na kutoweza ni za kike.
Ufeministi wa Kimarekani unahusishwa na kazi ya Mary Ellman Thinking about Women
(1968). Mary aliangalia jinsi wanawake wanasawiriwa kwa namna mbalimbali katika kazi
zilizoandikwa na wanaume na jinsi wanaume walivyoendeleza usawiri huo hasi wa wanawake
katika kazi zao. Betty Friedan katika The Feminine Mystique (1963) anachunguza maisha ya
mwanamke ambayo anasema ni jambo lisiloeleweka na wanaume na pia wanawake wenyewe.

4
Mwalimumwingisi@gmail.com,
Chuo Kikuu Cha NAIROBI
Mwalimu Mwingisi

Tapo hili linashikilia kwamba, wanawake wana namna yao ya kipekee ya kuandika na kujieleza.
Aidha, wanasema kuwa kuna dhamira zinazorudiwarudiwa katika tungo za wanawake.
Wanashugulikia kazi za fasihi zilizotungwa na wanawake na pia wanaume maadamu zinaongea
juu ya wanawake.

Ufeministi wa Kiingereza huchukulia kuwa, mambo ya kihistoria na siasa ndiyo huathiri


matendo ya wanawake. Tapo hili lilidhamiria kuwashirikisha wanafunzi katika maswala ya
kufanya uamuzi na kuondoa dhuluma dhidi ya jinsia ya kike.
Ufeministi wa Kiafrika ulihusishwa na bara la Afrika. Wanawake wa Kiafrika walisisitiza zaidi
upinzani dhidi ya utamaduni unaomnyima mwanamke nafasi ya kutekeleza malengo yake.
Miongoni mwa vitengo vya utamaduni huu ni ; desturi na mila zinazomdhalilisha kama vile
kuonewa kwa mwanamke asiyezaa, kukosa uwezo wa kuchagua kuwa mke au mzazi wa
mwanajamii, tohara na ukeketwaji wa wanawake pamoja na kimya cha kulazimishwa. Millett
(1977) anasema kwamba Ufeministi wa Kiafrika umetokana na utamaduni katika jamii
iliyojikita katika kilimo na ushiriakiano wa kijamii. Umejengeka katika misingi thabiti ya
kumhusisha mwanamke katika shughuli tofauti za jamii bila kuangalia asasi zinazotawaliwa na
mwanamume. Kulingana na Millett, Ufeministi wa Kiafrika husisitiza usawa katika shughuli za
jamii na utoaji uamuzi kwa wanawake na wanaume. Strobel (1980) anauona ufeministi wa
Kiafrika kama uliokumbana na changamoto nyingi kutokana na asasi tofauti kwa sababu huwa
unataka kujua chanzo cha ubaguzi katika maswala ya kiutawala. Mwelekeo pinzani unasisitiza
uongozi wa jinsia ya kiume ambao umeupa changamoto nyingi sana mwelekeo wa Ufeministi
wa Kiafrika. Steady (1981) anasema kuwa Ufeministi wa Kiafrika unajikita katika misingi
inayoangalia majukumu tofauti ya kijinsia kama yanayotegemeana na kukamilishana, yenye
usambamba na usawa katika kuiendeleza jamii. Anaeleza kuwa Ufeministi wa Kiafrika huweka
pamoja maswala ya jinsia, ubaguzi, utabaka na mielekeo tofauti ya kiutamaduni ili kuibua
Ufeministi unaomwangalia mwanamke kama kiumbe lakini sio kama kiumbe kijinsia.
Anaongezea kuwa Ufeministi wa Kiafrika huchunguza maswala ya kitamaduni yanayomlemaza
mwanamke. Aidha hushughulikia maswala ya kijinsia kwa kujikita katika muktadha wa
Kiafrika.

Mihimili ya kimsingi ya nadharia ya Ufeministi


Nadharia hii inanuia kuwasawazisha wanadamu kwa upande wa jinsia na utamaduni na
kupigania jamii mpya yenye msingi katika amali za kibinadamu na wala si za kimaumbile na za

5
Mwalimumwingisi@gmail.com,
Chuo Kikuu Cha NAIROBI
Mwalimu Mwingisi

kijadi. Vilevile ni mtazamo unaokuza na kuendeleza hisia za umoja wa wanawake kama kundi
linalodhulumiwa. Aidha, lengo muhimu la nadharia hii ni kuvumbua na kuziweka wazi kazi za
sanaa zilizotungwa na wanawake ambazo zimepuuzwa kwa sababu ya utamaduni
unaompendelea mwanamume.

Pia inanuia kuchunguza historia ya fasihi ya jadi ya kike na kuwamulika waandishi wa kike
waliotambua hali za wanawake na ambao wanaweza kuchukuliwa kama vielelezo kwa
wasomaji wao. Mbatiah anaeleza kuwa lengo kuu la uhakiki wa kifeministi na hasa Ufeministi
wa Kiafrika ni kuzua mikakati ambayo itaangazia kutathmini jinsia ya kike, mitazamo, thamani
na matakwa ya wanawake sio tu katika fasihi, bali nyanja zote za maisha ya binadamu.

Nadharia hii hunuia kuzindua mwamko kwa wanawake na jinsi wanavyojiona na uhusiano wao
na watu wengine.

Nadharia ya Semiotiki
Neno semiotiki limetokana na mnyambuliko wa neno la Kigiriki ‘semeion’ lenye maana ya
ishara linalowakilisha vikundi vya wafuasi wa mielekeo fulani kulingana na maelezo ya John
Selden. Kwa upande mwingine Wamitila anapambanua kwamba ‘ semiotiki’ ni neno la lugha ya
Kiyunani lenye maana ya ishara na ambalo linatumiwa kuelezea mielekeo ya makundi fulani ya
kihakiki. Wamitila anakubaliana na Selden kuhusu asili ya neno semiotiki kwa kuwarejelea
wasomi Bailey, Matejk na Steiner walioeleza kuwa‘ semiotiki ni mchakato ambapo vitu na
matukio huja kutambuliwa kama ishara na kiumbe hai ambacho kinahisi. Kulingana na Selden
semiotiki ni taaluma ambayo hufanya kazi kwenye desturi pana za kiutamaduni zinazohusisha
ishara violwa na ishara tajwa. Anapozungumzia semiotiki ya kisasa anasema kuwa inatumiwa
kurejelea uwanja unaoendelea kubadilika wa elimu ya masomo ambayo huangaza fenomena ya
maana katika jamii.

Mwanafalsafa wa kiitalia Umberto Eco anaeleza kuwa semiotiki inahusishwa na kila kitu
kinachoweza kuchukuliwa kuwa ishara. Dhana hii ya semioiki vile vile imefasiriwa na kutolewa
mawazo na wataalamu na waandishi mbalimbali kama vile; Massamba anasema kuwa semiotiki
ni taaluma ya kisayansi inayojishughulisha na uchunguzi na uchanganuzi wa mifumo ya ishara
mbalimbali ikiwa inazingatia zaidi uhusiano baina ya kiwakilishi na kiwakilishwa.

6
Mwalimumwingisi@gmail.com,
Chuo Kikuu Cha NAIROBI
Mwalimu Mwingisi

Vilevile, Wafula na Njogu wameeleza semiotiki kuwa taaluma ya mipangilio ya ishara


zinazomwezesha binadamu kuona vitu au hali kama ishara zenye maana. Kulingana na maelezo
ya wataalamu hawa, semiotiki hujishughulikia maswala ya ishara, matumizi ya ishara na
matumizi ya lugha kwa jumla katika kazi za kifasihi. Wachunguzi hawa wanaeleza kuwa
semiotiki huzungumzia uashiriaji wa vipashio vya lugha au tamathali ilhali nadharia ya
umuundo inahusu namna ishara zinavyowekwa katika utaratibu unaoziwezesha kufahamika.
Mwalimu Wamitila naye amedai kuwa semiotiki ni aina ya nadharia ya kimuundo
inayojishughulisha na ishara na maana za ishara hizo katika kazi za kifasihi. Semiotiki
huangazia uashiriaji na jinsi kazi za kifasihi zinavyowasiliana na wasomaji. Nadharia hii aidha
huchunguza kwa nini kazi za kifasihi zina maana zilizo nazo kwa wasomaji wa kazi hizo. Kwa
ujumla semiotiki ni mfumo wa ishara ambazo zinawakilisha kitu au maana fulani.

Nadharia ya semiotiki imegawika katika matawi tofauti tofauti. Msomi Nauta anadai kuwa
kuna matawi matatu makuu ya semiotiki ambayo ni semiotiki fafanuzi, semiotiki tekelezi na
semiotiki halisi. Umberto Eco anatafiti na kuongezea kundi la semiotiki ya wanyama (zuolojia)
ambalo ni kiwango cha chini kabisa,kundi hili linahusu tabia za kimawasiliano za viumbe
visivyo binadamu.
Makundi haya manne makuu ya semiotiki yamegawanywa katika vipera vya semioti kisintaksia
ambalo linahusiana na uhusiano wa ishara katika miundo rasmi ya vipengele vya kifasihi. Pili ni
la semiotiki pragmatiki inayohusiana na ishara na athari zake kwa wanaozitumi. Semiotiki
semantiki linahusiana na ishara na maana ya vitu inavyorejelea na semiotiki wasilishi.Pia kuna
migao mingine kama vile, semiotiki ya kiakili, semiotiki ya
kiutamaduni, semiotiki viumbe hai, semiotiki ya kifasihi, semiotiki ya kimuziki, semiotiki ya
kijamii, semiotiki ya violwa n.k

Fauka ya hayo, semiotiki inamulika jinsi kazi ya fasihi inavyowasiliana na wasomaji. Nadaharia
hii inaeleza zaidi jinsi matini yanavyofasiriw na namna inavyooana na wasomaji wake.
Mihimili ya Nadharia ya Semiotiki
Nadharia hii imejikita katika maelezo ya mwanaisimu mashuhuri Ferdinard de Saussure
aliyeeleza kuwa lugha ni mfumo wa ishara ambazo huangaza na kuunda mkufu wa ishara.
Alidai kuwa kila ishara huwa na sehemu mbili ambazo ni ishara yambwa/kiashirii husimamia
sauti au wasilisho la kimaandishi/matini na kifasiri/kiashiriwa ambayo ni maana ya kiashirii.
Maelezo haya yanadhihirisha kuwa kiashirii ni neno lenyewe na kiashiriwa ni maana yenyewe

7
Mwalimumwingisi@gmail.com,
Chuo Kikuu Cha NAIROBI
Mwalimu Mwingisi

ya kiashirii. Madai haya yanamaanisha kuwa kiashirii ni picha-sauti ilhali kiashiriwa ni dhana
na ishara ni jumla ya matokeo ya uhusiano baina ya kiashirii na kiashiriwa Kwa mujibu wa
Ferdinard semiotiki huangalia matini yoyote ile kama iliyosheheni ishara mbalimbali
zinazofungamanishwa na maana ya kifasihi. Kwa mfano, kiashirii cha neno ‘chui’ ni sauti ya
kiutamkaji au herufi za kiuandikaji lakini kiashiriwa ni mnyama anayefugwa wa porini. Kwa
hivo uhusiano uliopo ni wa kinasibu.

Wanasemiotiki hata hivyo wanashikilia kuwa, kiashirii huweza kuwa kile kile bali
kinachoashiriwa kinaweza kuwa tofauti. Kwa mfano, huko Ulaya, neno ‘pombe’ huweza kuwa
ishara ya urafiki, pongezi, wema, ukarimu au mapenzi lakini kiashirii kinabaki kuwa neno
‘mvinyo’. Kwa hivyo, tunaweza kusema kuwa kiashirii kimoja kinakuwa na viashiriwa vingi
katika lugha ya kawaida. Mwanaisimu mwingine Peirce anaendeleza uchunguzi wa Saussure
wa ishara kuwa na sehemu mbili kiashirii na kiashiriwa na anaongezea kipengele cha tatu
ambacho ni sehemu ya kifasiri. Anaeleza kuwa ishara ina misingi inayoibua aina tatu za ishara
ambazo ni kielekezi, ishara-tanakali na taashira. Kielekezi kulingana naye hueleza na kufafanua
uhusiano uliopo baina ya ishara na kinachoashiriwa. Kwa mfano katika kazi ya fasihi,
kunaweza tokea kilio katika giza na kuashiria kuwepo kwa mtu fulani. Kwa upande mwingine,
ishara-tanakali huonyesha mahali au hali ambapo pana uhusiano kati ya ishara na kiashiriwa.
Katika kipengele hiki,michoro au picha ni ishara- tanakali zinazoeleweka. Kwa mfano milio,
‘miaoo’ ni ishara- tanakali wa paka. Hatimaye Peirce aligusia dhana ya taashira ambayo
aliitumia kuelezea aina ya ishara inayoashiria kutegemea matumizi ya kinasibu na kikawaida au
ya kidhahania.

Peirce anamedai kuwa ishara hutegemezwa kwenye msingi fulani ili kufasiriwa, na hili linaoana
na dai la Mswisi Saussure kuwa ishara hazina upekee wa maana ila zinapofasiriwa. Kupitia
juhudi zake, nadharia ya semiotiki haikuishia kuzisambaza sifa za kitaaluma sana kama
ulivyofanya umuundo.
Hata hivyo, Wafula na Njogu wamedhihirisha kwamba Mswizi katika uchanganuzi wake wa
kisemiotiki, alijikita sana katika dhima ya ishara katika jamii naye Peirce akatafiti namna ishara
zilivyotumiwa kufafanua vitendo maalum na maana ya ishara hiyo ikitokana na sheria fulani za
kiutamaduni, kitanzu na lugha.

Nadharia ya Simulizi/Naratolojia

8
Mwalimumwingisi@gmail.com,
Chuo Kikuu Cha NAIROBI
Mwalimu Mwingisi

Nadharia hii inahusiana na usimulizi wa hadithi. Hadidhi ni fabula inayoelezewa kwa mtiririko
wa kimantiki unaosimulia kuhusu tukio fulani. Prince anafafanua dhana ya simulizi kama
uelezaji wa tukio moja au mengi ya kihalisia au kibunilizi.

Kulingana na maelezo ya Gérard Genette, simulizi ni mfuatano halisi au ya kibunulizi ambayo


ni kiini au yanayolengwa na usemi fualni. kulingana naye, simulizi huhusisha utambwaji wa
matukio. Nadharia hii huchunguza sifa zinazohusisha simulizi na kuzitenganisha nyingine.
Msingi wake umewekwa na Mwanafalsafa Plato ambaye anadai kuwa usimuliaji hulingana na
udhihirishaji. Plato anazua vipengele viwili ambavyo ni mimesia na digesia. Katika mimesia
mtunzi hajitokeza waziwazi kama msemaji ilhali katika digesia msemaji anaweza kutambulika
na hadhira yake. pia Mtaalamu Lord Raglan katika kazi yake ya The Hero iliyosheheni maiasha
ya mashujaa wa kitamaaduni kama vile Oedipus, Robi Hood amechangia sana katika kukua kwa
nadharia hii. Anaeleza kuwa lazima kuwe na mfuatano maalum wa matukio katika uandishi
kama vilekutabiriwa kwa kuzaliwa kwa shujaa, kuzaliwa kwake, maajabu yake, ukombozi wake
na hatimaye kifo chakekutokana na usaliti.

Wahakiki wa kinaratolojia wamebainisha dhana mbili katika usimulizi; wakati hadithi na wakati
matini. wakati hadithi ni wakati inaochukua hadithi husika kuanzia mwazo hadi mwisho. Wakati
unaweza kueleweka kwa urahisi kwa kuwa unaweza kuwa baina ya siku moja, miezi mitatu au
miaka mingi inayohusisha vizazi.
Dhana ya wakati matini ni wakati inayochukua wakati fulani kusomwa. Wakati huu ni vigumu
kutathminiwa ila itategemea muda atakaouchukua msomaji na kasi yake. Hali kadhalika, kuna
wakati ambapo wakati matiniunakuwa mrefu ukilinganishwa na wakati hadithi. Hili
limejitokeza katika hadithi ya S. A Mohammed ya Kiza katika Nuru, ambapo Mvita amefika
ofisini na hajatenda lolote bado kwa muda mrefu ilhali msomaji anaendelea kusoma.

Mihimili ya Nadharia ya Naratolojia


Nadharia ya naratolojia hujikita katika kipengele cha wakati ambacho huangaliwa kwa
kuvichunguza vigezo kama vile mpangilio, muda na idadimarudio. Katika kigezo cha
mpangilio, matukio huweza kusimuliwa katika mfuatano wa kiwakati ama kwa kutofungamana.
yasimuliwapo kiwakati, msuko na hadithi huwa huwa na mapangilio sawa. Kwa upande wa
muda, hujiita katika uhusiano katika hadithi na kipindi ambacho kimechukuliwa, kipindi kirefu
au kifupi? Muda katika nadharia ya naratolojia hujitokeza katika jinsi tano;-

9
Mwalimumwingisi@gmail.com,
Chuo Kikuu Cha NAIROBI
Mwalimu Mwingisi

Kwanza, muhtasari ambapo muda wa usemi/matini(usomaji) unachukuliwa kuwa mfupi kuliko


ule wa hadithi. Kulingana na Rimmon-Kenan kasi ya hadithi huharakishwa katika muhstasari
itokanayo na ufupishwaji wa muda fulani kwa kauli chache.
udondoshaji ni dhana nyingine ambayo hurejelea pale mabapo maelezo fulani yameachwa
katika matini fulani, (mwanda nunge wa kimatini) ilhali hadithi yenyewe ina wakati fulani.
Katika hali hii wakati hadithi na wakati matini huwa tofauti. Vilevile onyesho ni dhana
nyingine ambayo huleta sifa ya uigizaji katika matini yoyoyte ile.
Katika dhana ya idadimarudio au umara wahakiki wa naratolojia hurejelea mara ambazo
matukio hutokea katika hadithi au mara ngapi matukio hayo yanasimuliwa. Wananaratolojia
wamebainisha aina tatu za urudiaji kama vile, tukio lililotokea mara moja linaweza kusimuliwa
mara moja, pia tukio lenyewe laweza kusimuliwa mara kadhaa na panakuwa na urudiaji wa
kisimulizi na hatimaye tukio likitokea mara kadhaa linasimuliwa mara moja.
Uhakiki wa kinaratolojia huwaangalia wahusika kama kipengele muhimu cha matini ya kifasihi.
Katika kuwabainisha wahusika, kuna uelezaji wa moja kwa moja ambapo maelezo ya wazi wazi
kumhusu mhusika yanatolewa na mwandishi. Kwa mfano katika Rosa Mistika maelezo kuhusu
yanatolewa waziwazi na mwandishi.
Katika uwasilishaji usio wa moja kwa moja unahusisha matendo ya wahusika, maneno yao, sue
zao, mandhari au hali zao. Msomaji huangalia jinsi wahusika wamewasilishwa na mandishi na
kuwatambua.
Kipengele kingine cha uhakiki huu ni mtazamo wa mhakiki/mtambaji. Mwandishi huwa na
mtazamo fulani kuhusu maswala kadhaa na ambao labda angetaka amshirikishe msomaji.
Nadaria ya naratolojia inahusiana na mwelemeo wake mkuu kwenye muundo wa kazi bila
kuhusisha na muktadha wa kihistoria, kijamii, kisiasa au kitamaduni wa kazi zenyewe.

Nadharia ya Udhanaishi

Nadharia ya udhanaishi huangalia maisha ya mwanadamu. Hujikita katika kuhakiki fujo na


udhaifu wa maisha ya mwanadamu, upweke na usiri unaomkumba, kihoro na hofu kubwa
anazozipitia, utupu na ubwege wa maisha, swala la uhuru, kifo na hatimaye uhusiano uliopo
baina ya binadamu na Mwenyezi Mungu. Nadharia hii imetafasiriwa na kupambanuliwa na
wataalamu mbalimbali. kama vile;-

Kimani Njogu na Rocha Chimerah (1999) wanafasiri Udhanaishi kuwa nadharia ambayo
inajibidisha na dhana ya Maisha. Wasomi hawa wanajaribu kuuliza swali la kifalsafa kuwa

10
Mwalimumwingisi@gmail.com,
Chuo Kikuu Cha NAIROBI
Mwalimu Mwingisi

Maisha ni nini?. Kwa undani wanajikita kutafiti nafasi ya mwanadamu ulimwenguni. Kwa
upande mwingine.

Wamitila, K. W. (2003) Katika Kamusi ya fasihi Istilahi na nadharia anaeleza kuwa


“Udhanaishi ni dhana inayotumiwa kuelezea falsafa ya kuwako na Maisha. Dhana hii inatumiwa
kueleza Maono au Mitazamo unaohusiana na hali ya Maisha ya binadamu, nafasi na jukumu
lake ulimwenguni na uhusiano wake na Mungu. Wanjala Simiyu (2012) kwa upande mwingine
katika Kitovu cha fasihi simulizi anasema kuwa Udhanaishi ni falsafa au Mtazamo wa Maisha
ulio na kitovu chake katika swali kuwa, anaeleza kuwa maisha ni nini na yana maana gani kwa
binadamu?, ni kwa njia gani mwanadamu anaweza kuyabadilisha maisha yake yaliyojaa dhiki,
mashaka na huzuni.

Nadharia ya udhanaishi ni falsafa inayoshugulikia maswala kuhusu maisha; ni mtazamo


unaokagua hali ya nafasi ya mtu katika ulimwengu anamoishi na pia ni falsafa inayozungumzia
uhusianao uliomo kati ya mtu na mungu na iwapo mtu anapaswa kuamini kuwepo kwa
mungu.Vilevile, inatusaidia kuhakiki maisha ya mwanadamu anayeishi katika ulimwengu
uliojaa shida na matatizo mengi ambayo yanayosababishwa na binadamu mwenyewe. Shida
zinayoyapitia ni kama vita, njaa na uchumi kuzorota, kukosa kazi, ajali barabarani. Matatizo
haya yanafanya mwanadamu kukata tamaa na kushuku iwapo kweli mungu yuko.

Waasisi wa nadharia hii ni wanafalsafa Soren KierKegaard wa Ki-Den, Mjeruani Friedrich


Nietzsche, Martin Heidegger na Gabriel Marcel.Kulingana na Kieregaard mtu haishi kwa nguvu
zake mwenyewe kwa kuwa kuna nguvu zinazomtawala ambozo ni za mungu. Anaendelea kuwa
binadamu anapoishi hutenda dhambi na ili apate utulivu wa kiroho inambidi atubu dhambi hizo.
Wanaamini kuwepo kwa mungu kwa binadamu wote.

Mwanafalsafa huyu anaeleza kuwa binadamu ni kikaragosi cha nguvu zilizomuumba ni katika
kuzicha mtu huyu hupata utulivu wa kiroho .Kulingana naye, udhanaishi ni dhana ya hofu pale
ambapo binadamu huogopa adhabu kutoka kwa mungu kwa hivyo amefunikwa na wasiwasi
hataki na kumkosea mungu na kuhimiza ubinafsi wa binadamu. Friedrich Nietzche (1927)
katika kazi yake ya joyful wisdom” asema kuwa mungu amekufa. Tamko hili lake pamoja na
misimamo ya wenzake vinakuwa misingi muhimu ya kuzuka kwa udhanaishi wa ukanaji
mungu.

Nadharia hii ilishika sana baada ya vita vikuu vya dunia ambapo watu walikata tamaa maishani.
Kulingana na wanafalsafa walioshikilia dhana hii walidai kuwa mtu anapozaliwa, hujipata
ametumbukia katika ombwe la aina fulani.Vilevile mtu yuko huru kuishi tu na kukabiliana

11
Mwalimumwingisi@gmail.com,
Chuo Kikuu Cha NAIROBI
Mwalimu Mwingisi

vilivyo na ulimwengu unaomzunguka. Mwandishi Kezilahabi ni muasisi wa nadharia hii katika


Kiswahili kwa kuwa kazi zake nyingi zimejikita katika maisha ya binadamu, kama vile Dunia
uwanja wa fujo, Rosa Mistika miongoni mwa zingine.

Mihimili ya Udhanaishi

Nadharia hii imejengeka katika nguzo kadhaa kama ilivyoasiriwa na wanafalsafa mbalimbali.

Kwa kuwa ilizalishwa baada ya Vita Kuu ya Kwanza vya Dunia, wakati binadamu alikaa kukata
tamaa, imejikita katika mihimili ifyatayo

Kwanza baadhi ya wanaudhanaishi wanatilia mkazo matatizo halisi yanayomsibu mwanadamu


na wanakwepa imani ya kinjozi juu ya imani ya kuishi. Kulingana wasomi wa Kijerumani
Heidegger na Jaspers, watu walikata tamaa kwa kuwepo kwa wasiwasi na hofu kwa sababu ya
giza la fujo na mapambano ya silaha.

Wanafalsafa hawa pia hawaamini uwepo wa Mungu na uumbaji wake wa ulimwengu. Kwa
kuzingatia maafa yaliyokuwa yakiwasibu wanadamu wakati wa vita vya dunia. Madai haya
yalipata mashiko miongoni mwa wanafalsafa waliodai kuwa iwapo mungu angalikuwepo basi
hangeruhusu watu kuendelea kutenda uovu na kuwanyanyasa watu waso hatia.

Udhanaishi inatambua uhuru wa watu wa uchaguzi na hatua ya wazi katika mambo mawili. Tu
kwa njia ya uchaguzi wao wa kuchukua hatua, watu wanaweza kutambua kwamba bure, kwa
sababu asili ya binadamu ni waliochaguliwa na matendo yao wenyewe kuamua.

Vilevile, nadharia hii huamini katika juhudi za mtu binafsi kujisaka au kupambana na maisha
huishia katika umauti. Inashikilia kuwa binadamu imejaa mateso na pindi tu binadamu
anapozaliwa hivyo basi huwa amejipata katika ulimweng wa mateso na shida hivyo basi kifo tu
ndiyo huwa hatima ya kila kitu. Hali kadhalika, hujadili hali kama vile mashaka na uchovu wa
mambo mbalimbali yanayotutatiza maishani na jinsi yanavyoathili maisha ya yetu.

Maudhui yanayotajwa na wadhanaishi ni kama vile uhuru wa mtu binafsi, uwezo wake wa
kujifikilia na kujiamlia. Udhanaishi unafafanua jinsi uhuru wa binadamu umeshikwa na pingu
za utamaduni wa jadi na mila. Kulingana na washikilizi, ni bora kutambua umuhimu wa
kuchagua na kutenda kulingana na uchaguzi na kujitolea majukumu ya maisha

Pia hujadili na kugusia maudhui ya ukengeushi ambapo binadamu huwa amekata tamaa au
amekosa uhakika maishani. Huwa imembidi kubadilika na kuanza maisha ambayo ni kinyume.

12
Mwalimumwingisi@gmail.com,
Chuo Kikuu Cha NAIROBI
Mwalimu Mwingisi

Nadharia hii kwa ufupi inayarejelea maisha ya binadamu, uhusiano wa binadamu katika
ulimwengu na masaibu...

HITIMISHO

Nadharia kama dira ya kuhakiki kazi ya fasihi, pia huwa na dhima ya kuchunguza, kuainisha na
kutafiti kazi hizi. Kwa ufupi nadharia hufanya kazi ya fasihi kueleweka vyema. Kwa kuwa
fasihi ina dhima kubwa sana katika jamii.

13
Mwalimumwingisi@gmail.com,
Chuo Kikuu Cha NAIROBI
Mwalimu Mwingisi

MAREJELEO

Wafula Richard na Kimani Njogu (2007) Nadharia na Uhakiki wa Fasihi, Jomo Kenyatta

Foundation.

Kyallo W. Wamitila (2002) Uhakiki wa Fasihi ,Misingi na vipengele vyake, Phoenix publishers

Kyallo W. Wamitila (2003) Kamusi ya fasihi,Istilahi na Nadharia, Focus Publications Ltd.

Author Ameir Issa Haji (1982) Misingi ya nadharia ya fasihi, Taasisi

Kimani Njogu na Chimera R.(1999) Ufundishaji wa fasihi,Nadharia na Mbinu, Jomo Kenyatta

foundation.

TUKI, Kamusi ya Kiswahili Sanifu, (2004), Nairobi, Oxford University Press.

‘HESHIMA NA UTUKUFU KWA MWENYEZI MUUMBA’

14
Mwalimumwingisi@gmail.com,
Chuo Kikuu Cha NAIROBI

You might also like