You are on page 1of 7

Nadharia ya isimumuundo. Mbinu za kimuundo katika uchanganuzi wa vipengele vya fonolojia.

Katika makala hii tutajadili maana ya fonolojia na maana ya isimumuundo kasha usuli wa nadharia ya
isimumuundo. Katika kiini cha makala hiii ni Ubainishaji wa vipengele vya kifonojia na Ubainishaji wa
mbinu za kimuundo pamoja na ufafanuzi wa mbinu hizo katika vipengele vya kifonolojia. Kisha
tutahitimisha mjadala wetu.
Kwa mujibu wa Mugulu (1999) akimrejelea Fudge (1973) anasema kwamba fonolojia ni kiwango
kimojawapo cha lugha fulani kilicho na vipashio vidogo zaidi kuliko vipashio vingine vyote vya lugha.
Vipashio vya kifonolojiani fonimu na alofoni zake.
Dosari ya fasili hii ni kwamba haijafafanua kiwango kipi cha lugha ambacho kinahusika na fonolojia
kwani lugha inaviwango mbalimbali.
Massamba (2010) anasema kuwa fonolojia ni tawi la isimu linalojishughulisha na mfumo wa sauti
(asilia) za lugha. Hii inamaana kwamba, kila lugha mahususi inamfumo wake wa sauti ambamo
maneno hujengwa. Ki ukweli fonolojia hujihusisha na namna sauti zinavyotumika katika maneno ya
lugha mahususi katika kuleta maana.
Massamba na wenzake (2004) wanafafanua kuwa, fonolojia ni tawi la isimu ambalo hujishughusha
na uchunguzi, uchambuzi na uainishaji wa sauti pambanuzi ambazo hutumika katika mifumo
mbalimbali ya sauti za lugha za binadamu.
Massamba (2010), pamoja naMassamba na wenzake (2004), wanaonekana kufanana katika fasili
zao juu ya fonolojia isipokuwa, Massamba na wenzake (2004), wameonesha kuwa fonolojia si tawi
linalojihusisha na mfumo wa sauti tu, bali huzichunguza, huzichambua pamoja na kuziainisha sauti
hizo.
TUKI (1990) wanasema kuwa, fonolojia ni tawi la isimu ambalo hushughulikia uchambuzi wa mfumo
wa sauti zinazotumiwa katika lugha fulani.
Vilevile dosari ya fasili hii ni kwamba, imeegemea upande mmoja tu yaani uchambuzi wa mfumo wa
sauti za lugha fulani na kusahau kuwa taaluma hii ya fonolojia haijikiti tu katika uchambuzi bali
huzingatia uchambuzi, uchunguzi pamoja na uainishaji wa sauti hizo kama asemavyo Massamba na
wenzake (2004). “fonolojia ni tawi la isimu ambalo hujishughusha na uchunguzi, uchambuzi na
uainishaji wa sauti pambanuzi ambazo hutumika katika mifumo mbalimbali ya sauti za lugha za
binadamu.”
Kwa mujibu waMatthews (2001)anafafanua kwamba, Isimumuundo ni tawi la isimu ambalo hutumika
kama kihuzi cha kinadharia kinachochunguza au kuchambua na kuelezea muundo wa lugha kwa
kuzingatia vipengele vya lugha pamoja na uhusiano wake katika kuunda kitu kikubwa zaidi.
Pia isimumuundo ni mkabala unaochambua na kufafanua mfumo wa lugha kama unavyojibainisha
ukilinganisha na kipindi maalum katika historia.
Baada ya kuangalia fasili hizo ufuatao ni usuli wa nadharia ya isimumuundo kwa mujibu waMatthews
(kishatajwa). Nadharia ya umuundo ilianzia Ufaransa miaka ya 1900 na mwanzilishi wake ni
Ferdinand de Saussure katika dhana yake ya langue (umilisi) na parole (utendi).
Nadharia ya isimumuundo imejadiliwa na matapo makuu mawili yaani tapo la Ulaya na tapo la
Marekani
Awali ya yote wanasimu wa awali walijaribu kuchunguza lugha kwa kulinganisha zaidi na historia.
Ferdinand hakuridhika na ulinganishaji huo kwani aliona kwamba ulikuwa unajibu swali kuwa asili ya
lugha hiyo ni wapi, lakini haikujibu swali kuwa hiyo lugha inamfumo gani.
Tapo la Ulaya lilitoa hoja kuu zifuatazo katika nadharia hii:
Lugha inamfumo, yaani lugha ni mfumo ambao una elemeti zinazotagusana.
Lugha ni mfumo wa alama: kwa mfano kelele ni lugha endapo tu zitawasilisha au kuelezea mawazo
fulani, mfano dhana (dhahania), kiashiria na kiashiriwa.
Lugha hushughulika katika viwango viwili ambavyo ni langue (umilisi) na parole (utendi)
Baada ya tapo la Ulaya lilifuata tapo la Marekani ambalo nalo lilifafanua dhana ya umuundo au
nadharia hii ya isimu muundo kama ifuatavyo: Hapo awali watu walijishughulisha na uchunguzi wa
lugha za Marekani yenye asili ya kihindi, walikuwa wanaanthropolojia, lakini ilionekana kuwa
hawakuwa na mbinu mahususi ambazo wangezifuata ili kuweza kufafanua lugha hizo.
Kutokana na mapungufu hayo wakatokea wanaumuundo wa kimarekani walioongozwa na Bloomfield
ambaye yeye aliona kuwa uchunguzi wa lugha unapaswa kujikita katika kile watu wanachokisema.
Hivyo basi walipendekeza hoja kuu zifuatazo.
Isimu ni sayansi fafanuzi; yaani inafafanua kile watu wanachokisema na sio kile wanachotakiwa
kusema.
Kila lugha ni mfumo ulio na taratibu zake: lugha haipaswi kuchambuliwa kwa kutumia lugha nyingine,
bali inapaswa kuchambuliwa kwa kutumia mfumo wake wenyewe.
Lugha ni mfumo ambao vipashio vidogovidogo zaidi huunganika kimpangilio ili kuunda vipashio
vikubwa zaidi. Wanamuundo hawa walipendekeza taratibu ambazo walianza kuzitumia kwa
kuchambua vipashio vidogo kabisa na kuviainisha na kuvipambanua katika ruwaza ambazo
zilitumika kuunganisha ilikuunda vipashio vikubwa zaidi.
Maana haipaswi kuwa sehemu ya ufafanuzi wa kiisimu. Bloomfield na wafuasi wengine wa tapo hili
waliona kuwa maana ni dhana ya kinasibu ambayo haiwezi kuchunguzika, kwa hiyo si ya kisayansi.
Taratibu za kutambua vipashio katika lugha ni lazima ziwe halisi na zenye kufuata taratibu maalum.
Baada ya usuli wa nadharia ya isimumuundo, vifuatavyo ni vipengele vya kifonolojia pamoja na
mbinu za kimuundo katikaufafanuzi wa vipengele hivyo(kifonolojia) kwa mifano. Vipengele hivyo ni
sauti (foni), alofoni, fonimu na silabi. Pia mbinu zitumikazo na wanaisimumuundo katika ufafanuzi wa
vipengele hivyo ni mbinu ya uainishaji, sintagmatiki, paradigmatiki, moza, jozi pekee, mpishano huru,
mgawanyo kamilishani, mgawanyo wa kiutoano, na ubadala.
Kwa kuanza na mbinu ya uainishaji. Kwa mujibu wa Kamusi ya Karne ya 21(2011), uainishaji ni
“upangaji wa vitu au viumbe katika makundi kwa mujibu wa jinsi vinavyohusiana.”
Hivyo basi, katika muktadha wa kifolonojia tunaweza kusema kuwa, uanishaji ni upangaji wa vipashio
katika makundi kulingana na nduni zake bainifu au uhusiano wake. Kwa mfano: kosonanti za
Kiswahili ziliainishwa kulingana na namna zinavyotamkwa, mahali pa matamshi na hali ya nyuzi
sauti.
Kwa mfano: konsonanti “m”, “n”, “g” waliziainisha kama nazali pamoja na kuzipa sifa zake kama
vile; [m] [n]
+kons +kons
+nazali +nazali
+midomo +ufizi
+ghuna +ghuna

Hivyo kila sauti waliipa nduni za ziada na nduni bainifu, zilizotofautisha fonimu moja na nyingine. Kwa
mfano fonimu; “s” na “l”
[s]=kikwamizi [l]= kitambaza
+kons +kons
+kikwa +kitambaza
+ufizi +ufizi
-unazali -unazali
-ghuna +ughuna

Mbinu ya pili sintagmatiki; sintagmatiki ni ubadilishanaji wa nafasi ya vipashio vya kifonolojia (fonimu)
kwa njia ya mlalo. Hivyo katika lugha ya Kiswahili vipashio kwa kawaida hupangwa katika mfuatano
maalum wenye mahusiano, ambao ni;
K+I – b+a = ba mfano katika neno “baba”
K+K+I – c+h+a = cha mfano katika neno “chama”
K+K+K+I – m+b+w+a = mbwa mfano katika neno “mbwa”
Hivyo basi mbinu hii ya sintagmatiki imejikita zaidi katika kuangalia mpangilio sahihi wa sauti katika
lugha husika kiulalo. Na kamwe huwezi kukuta neno “ngoma”limeandikwa ngmoa, au kata – ktaa.
Vilevile hata muundo wa silabi za Kiswahili hubainishwa idadi yake kwa kufuata mbinu ya
kisintagmatiki, yaani kuhesabu kwa ulalo kuanzia kushoto kuelekea kulia. Mfano neno
“Anajichekelesha” neno hili lina silabi 7 ambazo ni $$ A$$ na $$ ji $$ che $$ ke $$ le $$ sha $
$ 1 2 3 4 5 6
7
Mbinu ya tatu ni mbini ya paradigmatiki, neno paradigmatiki limetokana na neno paradigm likiwa na
maana ya kundi la vitu vinavyoweza kukaa pamoja kutokana na mahusiano yao.
Hivyo paradigmatiki kwa mujibu wa The New American Dictionary paradigmatiki ni mahusiano wima
baina ya vipengele vya kiisimu vinavyounda muundo mkubwa zaidi kama vile sentensi. Kwa hiyo,
nadharia hii hubainisha vipashio kiuwima zaidi. Kwa mfano;
m
mw nafasi iliyokaliwa na /m/ inaweza kukaliwa na mu pia mw
w
Pia katika muundo wa lugha ya Kiswahili sauti huweza kubadilishana nafasi kiparadigmatiki (wima)
na kuunda neno jingine lenye maana tofauti na lile la awali. Kwa mfano katika neno “pata” tunaweza
kupata maneno yafuatayo kwa kubadilisha fonimu (konsonanti) kiuwima;
/p/+/a/+/t/+/a/ = (pata)
/b/+/a/+/t/+/a/ = (bata)
/k/+/a/+/t/+/a/ = (kata)
/n/+/a/+/t/+/a/ = (nata)

Vilevile tunaona kwamba katika maneno hayo kama tutatoa kosonanti au sauti /p/ na kuweka irabu
au sauti /e/ ni dhahiri kwamba maneno hayo hayatakuwa na maana yoyote katika lugha ya Kiswahili
kwa sababu lugha ya Kiswahili haina mfuatano wa I+I+K+I katika kuunda silabi badala yake
inamfuatano wa K+K+I
Mbinu ya nne ni mbinu ya moza, kwa mujibu wa McCarthy (1989), moza ni mapangilio wa vipashio
ulio katika mkururo. Mbinu hii huangalia mpangilio wa kimfuatano katika fonimu. Kwa mfano; foni
“abc” zitafuatana na fonimu “xyz” inategemewa kwamba mpangilio wa “abc” unaweza tu kufanana na
“xyz” na sio “yxz” nk.

Mfano.1mama, baba, kaka lala


walewale, kulekule, vilevile,
imba, cheza, kula, oga
Maneno haya katika mfano.1 yapo katika mfuatano na mpangilio wa sauti unaokubalika katika lugha
ya Kiswahili.
Mfano.2 mmaa, bbaa, kkaa, aall
wlwlaeae, klkluuee, vvlliiee
iamb, chzea, uakl, oag
Maneno katika mfano.2 hayapo katika mfuatano na mpangilio wa sauti unaokubalika katika lugha ya
Kiswahili.

Mbinu nyingine ya kimuundo inayotumika katika utambuzi wa vipengele vya kifonolojia kama vile
fonimu ni mbinu ya jozi sahili au jozi pekee.
Hapa wanamuundo huchukua maneno mawili yanayofanana kwa idadi mfano, bata [bata] = sauti nne
na bati [bati] = sauti nne. Katika maneno haya sauti zinazotofautiana ni /a/ na /i/ kwa sababu hizi ni
fonimu mbili tofauti.
Pia maneno haya yana maana mbili tofauti kutokana na sauti tofauti yaani /a/ na /i/. Vilevile maneno
kata na bata tunapata maana mbili tofauti kutokana na sauti mbili tofauti yaani /k/ na /b/
Mbinu nyingine ni ile ya mgawanyo kamilishani; mbinu hii inadai kwamba kuna mazingira ambapo
kuna sauti mbili zinazofanana ambapo sauti hizo mbili zinagawana mazingira ya kutokea. Kwa
mfano: kama “A” ikitaokea katika mazingira ya kwanza basi haiwezi kutokea katika mzaingira ya pili.
Kamwe haziingiliani. Lakini katika lugha ya Kiswahili hakuna sifa kama hii. Sifa hii tunaipata katika
lugha ya Ciruri/chiruri.
Kwa mfano neno “Imbusi” – mbuzi = “Ogubusi” – mbuzi mkubwa.

Mbinu nyingine ni mbinu ya mpishano huru, katika mbinu hii kuna kuwa na sauti mbili ambazo
zinaweza kutokea sehemu yoyote au mazingira yoyote bila ya kikwazo. kwa mfano; Gari – ghari
Zambi – dhambi
Agenda – ajenda

Mbinu hii hutumika katika kubainisha alofoni za fonimu moja.


Mgullu (1999) akimrejelea Hyman (1975) anaeleza kuwa mbinu nyingine ambayo hutumiwa wakati
wa kuchambua sauti ambazo ni fonimu au alofoni za lugha fulani ni ile ya mgawanyo wa kiutoano.
Utoano ni dhana ambayo imeelezwa vizuri na Hyman kuwa, katika fonolojia ni dhana ambayo
hutumiwa kuelezea uhusiano uliopo baina ya sauti mbili au zaidi ambazo haziwezi kutokea katika
mazingira sawa.
Mfano, katika lugha ya Kiingereza kuna sauti /P / yenye mpumuo na sauti /P/ isiyo na mpumuo
ambazo tunaelewa wazi kuwa [P ] hutokea mwanzoni mwa neno tu, kwa mfano, katika /pin/, /pen/,
/put/, nk. Kwa upande mwingine /p/ isiyo na mpumuo hutokea sehemu yoyote ya neno isipokuwa
mwanzoni. Hapa tunapata kigezo muhimu sana cha kutofautisha fonimu na alofoni.

Hivyo basi, mbinu walizotumia wanamuundo katika uchambuzina ufafanuzi wa vipengele vya
kifonolojia zimekuwa msingi mkubwa sana katika uchambuzi wa data mbalimbali za lugha duniani na
ndizo zimekuwa chanzo cha kuwafanya wanaisimu yaliofuatia kupata mahali pa kuanzia katika
kufanya uchunguzi wa lugha mbalimbali duniania.

MAREJEO:
Jewell, E. J and A. Frank. (2005). The New Oxford American Dictionary. (2nd
Edit).Oxford University Press. New York.
Mdee, J. S. na wenzake (2011). Kamusi ya Karne ya 21.Longhorn Publishers (K)
Ltd. Nairobi.
Massamba, D.P.B na wenzake. (2009).Fonolojia ya Kiswahili Sanifu (Fokisa): Sekondari na
Vyuo.Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Massamba, D.P.B. (2010). Phonological Theory: History and Development. Institute of
Kiswahili Studies (IKS). Dar es Salaam.
Metthews, P. (2001). A short History of Structural Linguistics. Cambridge University Press.
British.
McCarthy, J.J. (1989). “Linear Order in Phonological Representation.”Linguistics Department
Faculty Publication Series Paper 45.http:// scholarworks.umass.ed/linguist_faculty_pubs/45
Mgullu, R.S. (1999).Mtalaa wa isimu: Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili.
Longhornpublishers.Ltd. Nairobi.
TUKI, (1990).Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam.

You might also like