You are on page 1of 5

CHIMBUKO LA KISWAHILI

Chimbuko ni asili au fasili.Wataalamu wanahitilafiana kuhusu suala la mahali hasa ambapo


ndipo chimbuko la lugha ya Kiswahili.Wapo wanaodai kuwa lugha ya Kiswahili inatokana na
kingozi, lugha ya Kaskazini Mashariki mwa Kenya. Wengine wanasema kuwa, chimbuko la
Kiswahili ni Kishovi kilichozungumzwa na watu wa Bagamoyo Mzizima eneo linalojulikana
kwa jina la Dar es Salaam hadi Kilwa.Ama kwa hakika utafiti uliofanywa hivi karibuni na watu
kama Chami(1994) na Massamba(1992, 1996) umeonyesha wazi kuwa madai hayo hayana
ukweli na yanahitaji kutazamwa upya.

Mtaalamu mmojawapo aliyewahi kutoa hisia kwamba pengine lugha ya Kiswahili iliinukia
katika sehemu mbalimbali za upwa wa Afrika Mashariki ni yule Freeman- Grenville (1959).
Katika makala yake ya Medieval for Swahili alidai kuwa lugha ya Kiswahili ilianza na
kuinukia katika upwa wote wa Afrika Mashariki kama ambavyo baadhi ya maneno, majina ya
watawala na maofisa wa serikali yanavyojitokeza katika fasihi ya Historia ya Pate
yanavyoonyesha.

Maelezo hayo ya Freeman yanaashiria kwamba, lugha ya Kiswahili haikuanzia sehemu moja
maalumu. Massamba na wenzake (1999) wanasema, watu walioishi katika maeneo mbalimbali
katika upwa wa Afrika Mashariki walikuwa wakizungumza lugha zao mbalimbali. Lakini kwa
kuwa lugha hizo zote zilikuwa za Kibantu, zilikuwa hazitofautiani sana.

Ushahidi wa kiisimu unathibitishwa kwa misingi inayohusu sayansi ya lugha. Unadhihirisha


kuwa, Kiswahili ni lugha ya Kibantu. Isimu ni taaluma inayoangalia na kuichambua lugha kwa
undani kutumia njia ya kisayansi kuzungukia tanzu kama vile; isimu historia, isimu linganishi,
isimu jamii, isimu matumizi, isimu nafsia na isimu fafanuzi.

Lugha ya Kiswahili ilifanyiwa utafiti na uchambuzi na wanataaluma kadhaa kwa madhumuni ya


kuiainisha kama ilikuwa yenye misingi ya Kibantu au la. Mwanataaluma Malcom Guthrie
kutoka Chuo Kikuu cha London, Uingereza alifanya uchunguzi wa mashina/mizizi(viini) ya
maneno 22,000 kutoka lugha 200 za Kibantu. Katika uchunguzi wake, alikuta mizizi (mashina)
2,300 imezagaa katika lugha mbalimbali za Kibantu na Kiswahili kikiwemo. Mashina/mizizi 500
yalilingana katika lugha zote 200. Mashina haya yalipatikana katika lugha zote za Kibantu.
Mashina haya yalikuwa ya asili moja. Baadhi ya lugha hizo 200 zilizofanyiwa uchunguzi,
Kiswahili kilionyesha kuitikia ulinganifu sawa na kikongo (44%).

Katika kuchunguza ni asilimia ngapi za mashina hayo 500 yamo katika kila lugha, ilionekana
mgawo ufuatao:
Kiwemba kizungumzwacho Zambia - 54%
Kiluba kizungumzwacho Katanga - 51%
Kikongo kizungumzwacho Kongo - 44%
Kiswahili kizungumzwacho Afrika Mashariki - 44%
Kisukuma kizungumzwacho Tanzania - 41%
Kiyao kizungumzwacho Tanzania/ Msumbiji - 35%
Sotho kizungumzwacho Botswana - 20%
Rundi kizungumzwacho Burundi - 43%
Kinyoro kizungumzwacho Uganda - 37%
Zulu kizungumzwacho Afrika Kusini - 29%

Matokeo ya utafiti huo yaweza kutufanya tutoe kauli kadhaa za msingi kuhusiana na asili ya
Kiswahili.
i. Ni wazi mashina mengi ya lugha za Kibantu yapo Afrika ya kati hasa sehemu
zinazozungukia mkoa wa Katanga huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na
kupungua kadri unavyoelekea mbali na sehemu hiyo. Kwa msingi huo, ni wazi pia
kwamba Wabantu walienea kutoka sehemu hizo na kuja sehemu mbalimbali zikiwemo
zile za Afrika Mashariki.
ii. Kutokana na matokeo ya utafiti huo ni wazi kuwa, lugha ya Kiswahili ni ya Kibantu.
Kama madai yale ya kusema Kiswahili asili yake ni Kiarabu yangekuwa sahihi, basi
lugha hiyo ingehusiana mno na Kiarabu.

Vipengele vinavyothibitisha kwamba Kiswahili ni lugha ya Kibantu ni:

1. Msamiati
Msamiati wa msingi wa lugha ya Kiswahili na lugha za Kibantu unafanana kabisa. Msamiati wa
msingi ni ule unaohusu mambo ambayo hayabadilikibadiliki kutokana na mabadiliko ya
utamaduni. Tofauti zinaweza kujitokeza katika matamshi au mabadiliko kidogo ya viambishi
vyake, lakini si katika mzizi.

Mfano
Kiswahili Kindali Kikisii Kizigua
Mtu Umundu Omonto Mntu
Maji Amishi Amache Manzi

2. Sentensi za Kiswahili
Miundo ya tungo (sentensi) za maneno ya Kiswahili zinafanana sana na miundo ya tungo za
maneno ya Kibantu. Sentensi za Kiswahili na lugha za Kibantu zina kiima na kiarifu.

Mfano
K A
Kiswahili - Juma/anakula ugali
Kizigua - Juma/ adya ugali
Kisukuma - Juma/ alelya bugali

3. Ngeli za majina
Hapa kuna makubaliano kufuatana na ngeli katika maumbo ya nomino(Umoja na wingi wa
majina) pamoja na upatanisho wa kisarufi.
a. Kigezo cha maumbo ya majina
Kigezo hiki hufuata maumbo ya umoja na wingi katika kuyaainisha majina. Majina yaliyo mengi
katika lugha ya Kiswahili na lugha za Kibantu hufuata mkondo wa umoja na wingi. Majina ya
lugha ya Kiswahili na lugha za Kibantu yaliyo mengi yana maumbo dhahiri ya umoja na wingi.
Mfano

Umoja Wingi
Kiswahili Mtu Watu
Mtoto Watoto

Kikisii Omonto Abanto


Omwana Abana

Kindali Mundu Bhandu


Mwana Bhana

b. Kigezo cha upatanisho wa kisarufi


Katika kigezo hiki tunaangalia uhusiano ulipo kati ya nomino/vivumishi na viambishi awali vya
nafsi katika vitenzi vya Kiswahili na Kibantu. Vivumishi, majina pamoja na vitenzi hivyo
hubadilika kutokana na maumbo ya umoja na wingi.

Mfano
Umoja Wingi
Kiswahili Baba analima Baba wanalima
Kijita Tata kalima Batata abalima
Kindali Utata akulima Abhatata bhakulima

4. Vitenzi vya Kiswahili na Kibantu


Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya vitenzi vya Kiswahili na vile vya Kibantu. Vipengele
vinavyothibitisha uhusiano huu ni: Viambishi, mnyambuliko pamoja na mwanzo/mwisho wa
vitenzi.

a) Viambishi
Lugha ya Kiswahili na lugha za Kibantu vitenzi vyake hujengwa na mzizi(kiini) pamoja na
viambishi vyake(awali na tamati).

Mfano
Kiswahili - analima - A-na-lima
Kikuyu - arerema A-re-rema
Kindali - akulima - A-ku-lim-a
1 2 3 4

1 - Kiambishi awali kipatanishi cha nafsi.


2 Kiambishi awali cha njeo (wakati uliopo).
3 Mzizi/Kiini.
4 - Kiambishi tamati

b) Mnyambuliko wa vitenzi
Mnyambuliko wa vitenzi vya Kiswahili hufanana na ule wa vitenzi vya lugha za Kibantu.
Mfano
Kiswahili - Kucheka - Kuchekesha - Kuchekelea
Kindali - Kuseka - Kusekasha - Kusekelela

c) Mwishilizo wa vitenzi
Vitenzi vya lugha za Kibantu na Kiswahili huishia na irabu a

Mfano

Kiswahili - Kukimbia -Kushuka


Kisukuma - Kupila - Kutenda
Kikisii - Kominyoka - Goika

5. Miishilizo ya maneno ya Kiswahili na Kibantu


Maneno yoteya Kiswahili na lugha zote za Kibantu huishia na irabu. Maneno ambayo hayaishii
na irabu ni yale ambayo tumeyachukua kutoka lugha za kigeni.

Mfano

Nomino: Baba Kiswahili.


Tata Kindali
Kitenzi: Lima Kiswahili
Kulima Kindali
Kielezi: Polepole Kiswahili
Kanandikanandi Kindali

6. Idadi ya irabu
Kiswahili na lugha za Kibantu zote zina irabu tano ambazo ni:

a e i o u

Katika sehemu za Mombasa, Kivumba, Kimtangata katika sehemu za Pwani ya Kaskazini mwa
Tanzania, Kimakunduchi, Kihadimu, Kitumbatu katika sehemu za Unguja naPemba n.k. Hilo
ndilo lilikuwa chimbuko la lugha ya Kiswahili kama tuijuavyo leo.Ukizichunguza kwa makini
lahaja hizo za Kiswahili ni dhahiri kuwa ni lugha kamili zinazojitegemea. Vile vile lahaja hizo
zinafanana zaidi na lugha nyingine za Kibantu kuliko zinavyofanana na lahaja ya Kiswahili
sanifu ambayo ina maneno mengi ya kigeni.
MAREJELEO

Maganga (1997), OSW 102: Historia ya Kiswahili. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Masebo, J.A Nyengiwine, N. (2002), Na ya Lugha ya Kiswahili, Kidato cha 5&6; Aroplus
Industries Ltd: Dar es Salaam.

Nkwera, Fr. F. V. (2003), Sarufi, Fasihina Uandishi wa Vitabu, Sekondari na Chuo Kikuu;
Creative Prints Ltd: Dar es Salaam.

You might also like