You are on page 1of 9

AKS303 GROUP2.

SWALI; NI VIGUMU KUBAINISHA ALOFONI YA KISWAHILI. JADILI.


30MKS

UTANGULIZI.
Mbalu.

MWILI.
Ken$derrik.
Nicholus $ peter.
Meshak $ Frank.
Mariam $ kwamboka

HITIMISHO NA MAREJELEO.
Celestine.

1
UTANGULIZI.
Mgullu (1999) akimnukuu Hartman (1972) anasema kuwa alofoni ni sauti mojawapo
miongoni mwa sauti kadhaa zinazowakilisha fonimu moja. Alofoni hutokea katika mazingira
mahsusi (mazingira ya kiutoano).
Aidha, Mgullu (keshatajwa) akimnukuu Ladefoged (1962) anasema kuwa alofoni ni
matamshi tofauti tofauti ya fonimu moja. Pia anasema alofoni za fonimu moja huunda kundi
moja la sauti ambazo;
1. Hazibadili maana ya neno,
2. Hutokea katika mazingira tofauti ya kifonetiki, na
3. Alofoni zote hufanana sana kifonetiki.
Kutokana na fasili hizo, naweza kusema alofoni ni maumbo tofauti tofauti ya fonimu moja,
ingawa maumbo hayo huwa na tofauti ndogo ndogo za kifonetiki lakini hayaleti tofauti
yoyote katika maana za maneno. Tuchukue mifano ya maneno kutoka katika lugha ya Kiingereza;
tea; eat; writer; /thi:/ /i:t/ /raita/
Katika maneno yetu hapo juu sauti [th] inayotokea mwanzoni mwa neno, na sauti [t]
inayotokea popote ni alofoni za fonimu /t/. Sauti hizi hazibadili maana ya maneno, zinatokea
katika mazingira tofauti na zinafanana sana kifonetiki.
Katamba (1996) anasema alofoni zinaweza kujitokeza pia katika maneno:
tea; two; eighth; /ti:/ /twu/ /eitɵ/
[t] katika /ti:/ utamkwa wakati midomo ikiwa imesambaa, [tw] katika /twu/ hutamkwa wakati
midomo ikiwa mviringo na [t] katika /eitɵ/ ni sauti ya meno. Hivyo [t], [tw]na [t] ni alofoni za
fonimu /t/

Katamba (keshatajwa) anasema si kila sauti zenye kubadilishana mazingira basi zaweza
kuwa alofoni katika lugha ya Kiingereza. Kwa mfano sauti /h/ na /ŋ/ hubadilishana mazingira
ya utokeaji (sauti /h/ hutokea mwanzoni mwa silabi ikifuatiwa na irabu mfano; hat, head, n.k
wakati sauti /ŋ/ hutokea mwishoni mwa silabi katika konsonanti zilizoungana, mfano; longer,
long, bung n.k), lakini hazifanani kifonetiki hivyo haziwezi kuwa alofoni za sauti moja.
Aghalabu alofoni hutumiwa katika muktadha au mazingira ya kifonetiki yaliyo tofauti,
ambapo alofoni moja ikitumika katika mazingira fulani basi nyingine haiwezi kutumika
katika mazingira hayo hayo

Alofoni katika lugha ya Kiswahili ni dhana ambayo haijashughulikiwa vizuri. Hii ni


kutokana na wataalamu mbalimbali kutofautiana juu ya dhana hii. Tofauti hizi za
wataalam zinajitokeza juu sauti za lugha wanazozitoa kama mifano ya alofoni za
Kiswahili. Wengine huenda mbali na kusema kuwa lugha ya Kiswahili haina Alofoni.
Madhumuni ya makala hii ni kujaribu kuchunguza alofoni katika lugha ya Kiswahili.
Na kufikia hitimisho iwapo lugha ya Kiswahili ina Alofoni au la. Na iwapo lugha ya
Kiswahili ina alofoni basi alofoni hizo ni zipi? Tutachunguza dhana ya alofoni kama
inavyofasiliwa na wataalam mbalimbali, mbinu mbalimbali za kuzitambua alofoni na
fonimu za lugha.

2
MWILI/HOJA.
Alofoni katika lugha ya Kiswahili.
Sasa tuchunguze dhana ya alofoni kama inavyojadiliwa na wataalamu mbalimbali wa
Isimu ya Kiswahili. Hapa tutaonesha fasili pamoja na mifano ya alofoni katika lugha ya
Kiswahili kwa mujibu wa wataalamu hao.
Massamba na wenzake (2013) wanasema alofoni ni sura au maumbo mbalimbali ya
fonimu moja. Fonimu za lugha huweza kupata sura tofauti tofauti kulingana na
mazingira katika neno ambamo hutokea. Hii ina maana kwamba fonimu inaweza
kubadilika ikachukua umbo moja kutokana na kutokea kwake katika mazingira fulani
na ikaweza pia kubadilika ikachukua umbo jingine kutokana na kutokea kwake katika
mazingira mengine tofauti katika neno. Wanatoa mifano ya alofoni kutoka katika lugha
ya Kiswahili kama ifuatavyo:
Mofimu za neno Matamshi yake
(a) ki+ti ki+refu [kiti kirɛfu]
(b) ki+ti ki+eusi [kiti ʦeusi]
(c) u+limi m+refu [ulimi mrɛfu]
(d) n+limi n+refu [ndimi ndɛfu]
(e) n+buzi [mbuzi]
(f) n+dama [ndama]
(g) n+gombe [ᵑᵓᵐᵇᵋ]
Katika mifano ya Kiswahili hapo juu, tunaona mabadiliko ya kifonimu yakijitokeza.
Katika mfano wa (b) fonimu /k/ inapofuatiwa na irabu /i/ halafu kukawa na mpaka wa
mofimu, kisha ikafuatiwa na irabu /e/ hubadilika na kuwa /ch/ ki+eusi = [tseusi] na
katika (d) tunaona wazi kuwa fonimu /l/ inapotanguliwa na nazali /n/ hubadilika na
kuwa /d/ [n+limi = ndimi]. Halikadhalika katika mifano ya (e) na (g) tunaona kwamba
nazali /n/ inapofuatiwa na kitamkwa /b/ hubadilika na kuwa /m/, inapofuatiwa na
kitamkwa /d/ hubakia /n/, na inapoafuatiwa na kitamkwa /g/ hubadilika na kuwa /ᵑ/.
Hii ina maana kwamba katika mazingira haya sauti [ts] ni alofani ya fonimu /k/, [d]
ni alofoni ya fonimu /l/ na [m], [n] na [ᵑ] ni alofani za fonimu /N/ (katika fonolijia
herufi hii kubwa hutumika kuwakilisha dhana ya nazali) na alama /N/ ikiwa kama
kiwakilishi cha fonimu kuu

Alofoni hizo hapo juu zimetokana na michakato ya mofofonolojia(taaluma ya isimu


inayoshughulikia uchunguzi na uainishaji wa vipengere vya kifonolojia vinavyoathiri
maumbo ya mofimu au vipegere vya kisarufi vinavyoathiri maumbo ya fonimu).
Pamoja na

3
kwamba mabadiliko haya yameitwa mabadiliko ya kifonimu lakini tukichunguza vizuri
tutaona kwamba kwa kiasi kikubwa ni maumbo yaliyobadilika na kwa kiasi Fulani
fonimu.
Kwa mfano, mofimu ya ngeli ya tisa {n-} katika majina kama vile nyumba, mbuzi,
ng’ombe,
n.k (inabadilika katika mazingira tabirifu) kuwa mofimi {m},{ŋ} na wakati mwingine
hubaki vilevile {n}. Mchakato huu huitwa mchakato wa au kanuni ya konsonanti
kuathiri nazali.
Hivi kwamba mofimu {n} hubadilika na kuwa mofimu {m} pale inapokuwa imeitangulia
sauti ya midomo. Halikadhalika mofimu {n} hubadilika na kuwa mofimu {ŋ} pale
inapokuwa imeitangulia sauti ya kakaa laini.
Kwa mantiki hii basi maumbo haya yote yatakuwa yanaiwakilisha mofimu moja yaani
ngeli ya tisa {n-}. Kama hivi ndivyo basi maumbo hayo yatakuwa ni alomofu na si
alofoni.
Alomofu ni mojawapo ya viwakilishi viwili au zaidi vya mofimu moja ambavyo
hujitokeza katika mazingira tofauti ya mtoano. Massamba na wenzake(2012)
Katika data ambayo imetolewa na Massamba na wenzake (wameshatanjwa) kuna
baadhi ya sauti ambazo zinatokana na michakato ya kifonolojia au badiliko la
kifonolojia ambapo nazali huiathiri konsonanti inayoambatana nayo ili kurahisisha
matamshi. Sauti zinazoathirika hapa ni sauti za likwidi (kimadende /r/ na kitambaza
/l/).
(a) u+limi m+refu [ulimi mrɛfu]
(b) n+limi n+refu [ndimi ndɛfu]

Sauti /l/ hubadilika na kuwa kipasuo /d/ katika mazingira ya kutanguliwawa na


nazali /n/,
vilevile sauti /r/ hubadilika na kuwa kipasuo /d/ katika mazingira ya kutanguliwa na
nazali /n/.
Sauti hizi zinatokea katika mazingira ya kiutoano na zinafanana sana kifonetiki hivyo
twaweza kuziita alofoni.
Tuchunguze sifa za kifonetiki za sauti /r/ na /d/, na /l/ na /d/
/r/ /d/ /l/ /d/
+kons +kons +kons +kons
+ufizi +ufizi +ufizi +ufizi
+kimadende +kipasuo +ktambaza +kipasuo
10
Mdee (1986), anadai kuwa sauti [x] na [h] ni alofani za fonimu /h/ kama inavyodhihirika

4
katika maneno /kheri/ na /heri/.
Tukichunguza sauti hizi, ni kweli kwamba hazileti tofauti za maana katika lugha ya
Kiswahili isipokuwa sauti hizi ni tofauti mno kifonetiki. Wakati sauti /x/ ni ya kakaa
laini, sauti /h/ ni ya glota.
Je, sauti moja inaweza kutamkiwa katika sehemu mbili tofauti?
Matinde (2012) anasema alofoni ni maumbo mawili au zaidi ambayo huwakilisha
fonimu moja. Anaendelea kwa kusema kuwa alofoni ni matamshi tofauti tofauti ya
fonimu moja ambayo hujitokeza kutegemea mazingira ya utokeaji wa sauti hiyo.
Matinde(keshatajwa) yeye anatofautiana na wanaisimu kama Mdee (ameshatajwa)
ambao wanasema lugha ya Kiswahili ina alofoni kwa kutumia jozi za maneno/kheri/
na /heri/ wakisema /x/ na /h/ ni alofani za fonimu /h/. Anasema tukizingatia vigezo vya
kutambulisha alofoni, hizi ni sauti ambazo ni tofauti kabisa kwa misingi ya sifa bainifu
za kifonetiki, hususan jinsi ya kutamkwa na mahali pa kutamkiwa.

Matinde (ameshatajwa) anasema alofoni katika lugha ya Kiswahili sawa na lugha ya


Kiingereza, hudhihirika na vipasuo hafifu, hivi kwamba kipasuo hafifu kinapokuwa
mwanzoni mwa neno kutamkwa kikiwa na mpumuo, ilhali kipasuo hicho
kinapotanguliwa na fonimu tofauti hutamkwa bila mpumuo. Kwa mfano neno /pale/
kipasuo (p) hutamkwa kikiwa na mpumuo (ph) lakini kipasuo hicho kinapotanguliwa
na fonimu tofauti kwa mfano katika neno /alipo/ kipasuo /p/ hutamkwa bila mpumuo.
Anaendelea kueleza kuwa hali hii
hudhihirishwa pia katika maneno;
Neno Utamkaji
Katika /khatika/
Palipo /phalipo/
Panda /phanda/
Kaa /khaa/
Kwa hivyo, maumbo yote mawili yaani [p] na [ph] ni alofani za fonimu /p/. Aidha,
maumbo
[k] na [kh] ni alofani za fonimu /k/.
11
Sauti alizozionesha Matinde (keshatajwa) ambazo ni kama alofoni ni vibadala tu katika
lugha
ambavyo hutokana na tofauti za kilahaja. Lakini pia mtindo wa uzungumzaji waweza
kusababisha vibadala hivi. Ndio maana si hajabu kukutana na binti wa kimjini
akitamka kwa
madaa “palipo uzia penyeza mapenzi”.

5
Matamshi yake ni kama; /phalipho uzia phenyeza maphenzi/
Mpumuo sio sifa bainifu ya sauti za Kiswahili sanifu. Sina bainifu za sauti za Kiswahili
ni
kama vile; sifa ya ukonsonanti, namna ya kutamka, mahali pa kutamkia, mkao wa glota
na
unazali.

6
HITIMISHO.

Kwa maoni yangu, lugha ya Kiswahili inazo alofoni, ila ni vizuri zaidi kuwa makini
katika kuzibaini alofoni hizo. Kwa mfano; sauti /u/ hutamkwa tofauti tofauti ikitokea
katika mazingira fulani. Katika maneno; kisu, kinu. Elimu na mtaalamu. Hivyo basi
vigezo vinavyotupatia alofoni vitumike kwa uangalifu sana. Kwa mfano, katika kigezo
cha kufanana sana kifonetiki sauti huchukuliwa kwamba ni tofauti sana iwapo
zitatofautiana mahala pa kutamkia. Pia dhana ya alofoni isichanganywe na alomofu
kwa sababu afoloni hurejelea sauti wakati alomofu urejelea umbo.

Tumeona kuanzia mwanzo wa mjadala kwamba ni vigumu kubainisha alofoni katika


lugha ya Kiswahili. Ugumu huu unatokana na ukweli kwamba wataalam wametoa
mifano ambayo inakinzana labda kutokana na vigezo vya uainishaji kutofautiana.
Baadhi ya mifano haikidhi sifa za alofoni.
Nihitimishe kwa kutoa rai kwa wanazuoni na wanazuoni watarajiwa kuendelea kufanya
tafiti zaidi zitakazolenga kuchunguza alofoni katika lugha ya Kiswahili. Pia Niseme wazi
hapa kuwa alofoni hizo zikidhi sifa au vigezo vya kuitwa alofoni.

7
MAREJELEO:
Jones, D. (1950) An Outline of English Phonetics. New Delhi, Kalyani Publishers.
Habwe, J na Peter K.(2004). Msingi ya sarufi ya Kiswahili.Phoenix Publishers. Nairobi.
Katamba, F.(1996). An Introduction to Phonology. New York: Longman
Ladefoged, P.(1962) Element of Acoustic Phonetics. London: University of Chicago
Press.
Massamba,D.P.B, Kihore,Y.M na Msanjila,Y.P(2013) Fonolojia ya Kiswahili
Sanifu. Sekondari naVyuo. Dar es salaam: TUKI.
Massamba,D.P.B, Kihore,Y.M na Msanjila,Y.P(2012) Sarufi Maumbo ya Kiswahili.
Sekondari na Vyuo. Dar es salaam: TUKI.
Matinde, S.R.(2012) DAFINA YA LUGHA. Isimu na Nadharia. Mwanza: Serengeti
Educational Publishers (T) Ltd.
Mdee, J.(1986). Kiswahili: Muundo na Matumizi Yake. Nairobi: Intercontinental
Publishers
Ltd.
Mgullu, R. S.(1999) Mtalaa wa Isimu, Fonetiki na Fonolojia ya Lugha ya Kiswahili.
Nairobi. Longhorn Publishers.
TUKI (2013) Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Oxford University Press.

8
9

You might also like