You are on page 1of 118

KENYATTA UNIVERSITY

INSTITUTE OF OPEN LEARNING

AKS 201: INTRODUCTION TO THE STUDY


OF LITERATURE

GERALD NJAGI MATTI

DEPARTMENT OF KISWAHILI AND


AFRICAN LANGUAGES
2

UTANGULIZI
Fasihi ni somo ambalo linahusika na maswala mengi ya kijamii. Uelewaji wa
fasihi ni sawa na uelewaji wa mifumo mbalimbali ambayo hutawala jamii.
Mifumo hiyo inahusika na historia na maendeleo ya jamii za kilimwengu kwa
upande wa uchumi, siasa, utamaduni, dini, n.k.

Mtalaa huu unalenga kuwapa wanafunzi na wasomi wengine nafasi ya kuielewa


fika taaluma ya fasihi. Mambo ya kimsingi yanayohusiana na somo la fasihi
yamezingatiwa katika mtalaa. Nyanja za fasihi zikiwemo fasihi simulizi, riwaya,
hadithi fupi, tamthilia na ushairi zimejadiliwa. Hayo ni pamoja na maswali ya
kufanyia mazoezi, vitabu na makala mbalimbali za kurejelea katika kila utanzu
ulioshughulikiwa.

Kufikia mwisho wa mtalaa huu, msomi atakuwa amefafanukiwa na mawazo ya


kifasihi yatakayomuwezesha kujihami katika kukabiliana na kuelewa kwa urahisi
mambo yanayohusiana na taaluma ya fasihi.
3

VIFUPISHO

K.y.m - Kabla ya Masihi

B.y.m. - Baada ya Masihi

Kmf - Kwa mfano

K.v. - Kama vile

n.k. - na kadhalika

E.A.E.P. - East African Educational Publishers

O.U.P. - Oxford University Press

J.K.F. - Jomo Kenyatta Foundation

D.P.H. - Dar es Salaam Publishing House

T.U.K.I - Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili

D.U.P - Dar es Salaam University Press

T.K.L.K. - Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni

K.L.B - Kenya Literature Bureau

E.A.L.B. - East African Literature Bureau

T.P.H - Tanzania Publishing House


4

YALIYOMO

Utangulizi…………………………………………………………………… 2

Vifupisho …………………………………………………………………… 3

Somo la Kwanza: Dhana ya Fasihi

1.0 Utangulizi…………………………………………………………… 8

1.1.O Malengo…………………………………………………………… . 8

1.2.0 Maana ya Sanaa………………………………………………….. 8

1.2.1 Aina ya Sanaa…………………………………………………….. 10

1.3.0 Maana ya Fasihi………………………………………………….. 14

1.3.1 Aina za Fasihi…………………………………………………….. 14

1.4.0 Fani na Maudhui katika Fasihi…………………………………. 15

1.4.1 Fani katika Fasihi…………………………………………………. 16

1.4.2 Maudhui katika Fasihi……………………………………………. 27

1.5.0 Fasihi na Maisha…………………………………………………. 27

1.6.0 Jukumu la Fasihi…………………………………………………. 29

1.7.0 Muhtasari…………………………………………………………. 30

1.8.0 Zoezi………………………………………………………………. 30

1.9.0 Marejeleo Teule………………………………………………….. 30

Somo la Pili: Fasihi Simulizi

2.0 Utangulizi……………………………………………………………… 32

2.1.0 Malengo………………………………………………………………. 32

2.2.0 Maana ya Fasihi Simulizi……………………………………………. 32


5

2.3.0 Majukumu ya Fasihi Simulizi……………………………………….. 35

2.4.0 Fasihi Simulizi na Fasihi Andishi…………………………………… 37

2.5.0 Tanzu za Fasihi Simulizi…………………………………………… 40

2.5.1 Hadithi ……………………………………………………………… 41

2.5.2 Nyimbo……………………………………………………………… 50

2.5.3 Semi………………………………………………………………… 53

2.5.4 Sanaa za Maigizo………………………………………………… . 56

2.6.0 Utafiti Katika Fasihi Simulizi……………………………………… 57

2.7.0 Fasihi Simulizi Sasa………………………………………………. 60

2.8.0 Muhtasari…………………………………………………………… 61

2.9.0 Zoezi………………………………………………………………… 61

2.10.0 Marejeleo Teule…………………………………………………… 61

Somo la Tatu: Riwaya

3.0 Utangulizi………………………………………………………….. 63

3.1.0 Malengo…………………………………………………………… 63

3.2.0 Maana ya Riwaya………………………………………………… 63

3.3.0 Chimbuko la Riwaya……………………………………………… 68

3.4.0 Aina za Riwaya…………………………………………………… 69

3.5.0 Uchambuzi wa Riwaya…………………………………………. 72

3.6.0 Muhtasari…………………………………………………………… 75

3.7.0 Zoezi ………………………………………………………………. 75

3.8.0 Marejeleo Teule……………………………………………………. 76


6

Somo la Nne: Hadithi Fupi

4.0 Utangulizi…………………………………………………………… 77

4.1.0 Malengo……………………………………………………………. 77

4.2.0 Maana ya Hadithi Fupi……………………………………………. 77

4.3.0 Sifa za Hadithi Fupi………………………………………………. . 78

4.4.0 Uchambuzi wa Hadithi Fupi……………………………………… 82

4.5 .0 Muhtasari…………………………………………………………… 84

4.6 .0 Zoezi……………………………………………………………….. 85

4.7 .0 Marejeleo Teule…………………………………………………… 85

Somo la Tano: Tamthilia

5.0 Utangulizi…………………………………………………………… 86

5.1.0 Malengo…………………………………………………………… . 86

5.2.0 Dhana na Maana ya Tamthilia…………………………………… 86

5.3.0 Chimbuko la Tamthilia…………………………………………… . 88

5.4.0 Aina za Tamthilia…………………………………………………. 91

5.5.0 Vijenzi vya Tamthilia……………………………………………… 95

5.6.0 Uchambuzi wa Tamthilia………………………………………… 100

5.7.0 Muhtasari………………………………………………………….. 102

5.8.0 Zoezi………………………………………………………………. 102

5.9.0 Marejeleo Teule…………………………………………………… 102


7

Somo la Sita: Ushairi

5.0 Utangulizi…………………………………………………………… 103

6.1.0 Malengo…………………………………………………………… 103

6.2.0 Dhana ya Ushairi…………………………………………………. 103

6.2.1. Asili ya Ushairi……………………………………………………. 104

6.3.0 Vijenzi vya Ushairi………………………………………………… 105

6.4.0 Sifa za Mashairi……………………………………………………. 108

6.5.0 Uchambuzi wa Mashairi………………………………………….. 113

6.6.0 Muhtasari…………………………………………………………… 115

6.7.0 Zoezi………………………………………………………………… 115

6.8.0 Marejeleo Teule……………………………………………………. 115

7.0 Marejeleo ya Jumla……………………………………………….. 116


8

SOMO LA KWANZA

DHANA YA FASIHI

1.0 UTANGULIZI

Somo hili linaeleza dhana ya fasihi. Fasihi ni sanaa. Kwa hivyo, kabla ya

kuingilia dhana ya fasihi, maana ya sanaa na historia yake vimeelezwa. Kisha,

tumeonyesha fasihi ni nini. Mambo mengine ambayo somo hili limeshughulikia

ni pamoja na fani na maudhui katika fasihi; fasihi na maisha; na uchambuzi na

uhakiki wa fasihi.

1.1.0 MALENGO

Kufikia mwisho wa somo hili utaweza:


1. Kuelezea maana ya sanaa
2. Kutoa maana ya fasihi.
3. Kutambua fani na maudhui katika fasihi
4. Kuonyesha uhusiano uliopo baina ya fasihi na maisha

1.2.0 MAANA YA SANAA

Kamusi ya Oxford Advanced Learners’ Dictionary inatoa maana nne za neno

sanaa:

1) Kuumba au kupendezwa na kitu chenye urembo, hasa sanaa tumizi

k.v.uchongaji, rangi, ususi, nguo, ujenzi, n.k.

2) Ujuzi katika kuibuka na vitu vyenye urembo k.v. utunzi, uchezaji,

uimbaji,n.k.

3) Masomo ya sanaa k.v. lugha, fasihi, historia, n.k. ambapo ujuzi wa

kiumbuji hutawala kinyume na umakini unaohitajika katika sayansi.


9

4) Uwezo au ujuzi unaoweza kupatikana kutokana na mazoezi k.v. Uwezo

wa kuwa mkakamavu wakati wa kuhojiwa; kutia uzi katika tundu la

sindano, kuandika barua nzuri, n.k.

Kutokana na maelezo hayo, sanaa inaweza kuelezewa kama chochote

kinachotokana na ubunifu na umbuji wa binadamu. Sanaa ni nguvu, weledi na

kipawa alichonacho binadamu cha kuunda kitu cha kupendeza. Sanaa ni kila

kitu kinachotokana na ule umahiri wa binadamu wa kuremba mazingira yake.

Sanaa ni chochote katika dunia chenye haiba, kinachopendeza rohoni, machoni

na katika hisia. Katika mazingira yetu, tumezungukwa na sanaa ya vitu vyenye

maumbile, rangi, sura, kimo na mielekeo tofauti tofauti. Huu ni ujumi ambao

kama dunia ingeukosa, haingependeza na ingetusinya.

? Je, hebu fikiria; ulimwengu ungekuwaje bila sanaa?

Ujumi, ambao ni taaluma inayohusika na urembo, na kwa kiwango kidogo

kinyume chake, ubaya (kitu cha kuchukiza machoni), inazingatia pia mambo ya

sanaa na taaluma zingine kama vile falsafa ya sanaa, uhakiki wa sanaa na

saikolojia na sosholojia ya sanaa. Kupitia sanaa tunapata uzuri unaojitokeza

katika umbo linalotumiwa na mtu kuelezea hisia zinazomgusa kupitia vielelezo

vyenye dhana maalum.


10

1.2.1 AINA ZA SANAA

Kulingana na Muhando na Balisidya (1976) sanaa imegawika katika mafungu

matatu:

(a) Sanaa za uonyesho

Hizi ni sanaa ambazo uzuri wake unajitokeza katika umbo la kudumu linaloweza

kuhifadhiwa na uzuri wake kuonyeshwa wakati wowote. Sanaa hizi ni kama

uchoraji, uchongaji, kutarizi, ufinyanzi, n.k Matokeo ya sanaa hizi ni vitu kama

vile picha, vinyago, nguo zilizotariziwa, vyungu, n.k.

(b) Sanaa za ghibu

Uzuri wa sanaa hizi haupo kwenye umbo linaloonekana kwa macho au

kushikika, bali ni katika umbo linalogusa hisia. Sanaa hizi ni kama vile ushairi,

nyimbo, muziki, n.k. ambapo uzuri wake unatokana na kuzisikia kwa masikio.

(c) Sanaa za vitendo

Sanaa hizi hujitokeza kupitia umbo la vitendo, na ili kupata uzuri wake,

inampasa mtu kutazama vitendo vikifanyika. Umbo la sanaa hizi linalazimisha

kuwepo kwa mwanasanaa na mtazamaji wa sanaa mahali pamoja kwa wakati

mmoja. Sanaa hizi pia huitwa sanaa za maonyesho kwa sababu lazima wakati

zinapotendeka awepo mtu wa kuonyeshwa, kwani uzuri wake umo katika vitendo

vyenyewe.

Uhusiano wa msanii na sanaa yake huelezwa kupitia uhusiano wake na chombo


11

chake cha kusanii. Mchoraji ana rangi na vifaa vyake; mpiga zeze ana zeze;

mfinyanzi ana udongo na vifaa vingine; muigizaji ala yake ni yeye mwenyewe,

n.k. Uumbaji wa sanaa hubadilika kadri jamii inavyobadilika na jinsi maisha na

misingi ya maendeleo inavyobadilika katika jamii.

1.2.3 ASILI YA SANAA

Kuna mitazamo miwili kuhusiana na asili ya sanaa:

i) Mtazamo wa kidhanifu

ii) Mtazamo wa kiyakinifu

1) Mtazamo wa kidhanifu

Mtazamo huu ni wa kudhania tu. Kulingana na mtazamo huu, inaaminika kuwa

sanaa (ikiwemo fasihi), hutokana na Mungu. Mwanasanaa huipokea sanaa hiyo

kutoka kwa Mungu ikiwa umekwishakupikwa na kuivishwa. Huu ni mtazamo wa

wanafalsafa wa Kigiriki na Kirumi kama vile Socrates, Plato na Aristotle ambao

waliuchunguza ulimwengu wa sanaa na asili yake.

Kulingana na wanafalsafa hawa, matengenezo ya sanaa huonekana kuwa ni

shughuli ya kiungu inayomwiga Mungu ambaye ndiye msanii wa kwanza. Sanaa

hutoka kwa Mungu na kumfikia msanii ambaye huipitisha kwa jamii:

Mungu - Sanaa - Msanii - jamii

Mtazamo huu unapinga wazo kwamba sanaa hutokana na jitihada za akili na


12

mikono ya binadamu. Sanaa hupokelewa kutoka kwa mikono ambayo binadamu

hana uwezo wa kuiona. Mtazamo huu unamtenga msanii na jamii yake na

wakati huo huo kumwinua na kumfanya kuonekana kuwa wa ajabu na aliye

karibu na Mungu kuliko watu wengine wa kawaida. Mtazamo huu umetumika

sana kufafanua ushairi, hasa ule wa zamani.

ZINGATIA:

Katika utamaduni wa Kiswahili mtazamo huu umetumiwa na


wataalamu kama vile F.V. Nkwera (1985) anayesema: “Fasihi ni
sanaa ambayo huanzia kwa Muumba, humfikia mtu katika
vipengele mbalimbali … ni hekima ambayo mtu ameshirikishwa
apate kumtambua muumba weke.”

ii) Mtazamo wa kiyakinifu

Kulingana na mtazamo huu, chimbuko la sanaa ni mazingira halisi ya jamii hapa

hapa duniani. Sanaa yoyote ni zao la mazingira, nayo hususan ya mwanzo,

ilifungamana na kazi na uzalishaji mali.

Wanamtazamo huu wanasema kuwa tangu dunia iumbwe wanadamu

wamekuwa wakitafuta njia na nyenzo za kuendeshea vyema na kuendeleza

mbele maisha yao. Kupitia utafiti na majaribio mzomzo ya kisayansi ya kutafuta

ukweli kuhusu mazingira, sayansi imefaulu kuelezea chanzo cha binadamu, jinsi

alivyoanza kufanya kazi, na historia yake yote tangu mwanzo wake hadi sasa.
13

Sanaa ni kazi ya mikono na akili ya binadamu, nayo aghalabu ina umbo dhahiri

lenye maana na dhana maalum. Sanaa ni kazi za binadamu zenye mwigo wa

uyakini uliofungamana na wakati, mazingira na mifumo ya jamii zinazohusika.

Baada ya kuzuka kwa lugha, sanaa ya mwanzo ilifuatia. Sanaa hii haikutokana

na Mungu, bali ilitokana na kazi alizofanya binadamu katika kupambana na

mazingira yake. Binadamu wa kwanza alianza kwa kutunga maneno na sauti

zilizofuata mapigo ya zana za kazi. Alitumia zana hizo za kazi kuziimba nyimbo

wakati alipokuwa akifanya kazi. Wimbo wa kazi ukawa ndio sanaa ya mwanzo.

Wimbo huo wa kazi ulimpa binadamu nguvu mpya na ari zaidi ya kuendelea

kufanya kazi. Wimbo ulitoa nguvu za kimiujiza zilizomfanya mtu kusahau uchovu

na kutojali jasho jingi mwilini au jua kali angani. Sanaa hii ilihusika na manufaa

na maslahi ya wanajamii wote. Kwa kufungamana na mahitaji ya kukidhi haja za

lazima za binadamu, sanaa ilikuwa kifaa muhimu katika kutenda kazi.

Jamii zilipoanza kugawanyika katika matabaka, sanaa ilianza kuchukua sura

mpya. Kazi zilianza kugawiwa makundi ya watu mbalimbali; kama vile wahunzi,

wawindaji, wakulima, waimbaji, askari, n.k. Sanaa ikawa inaendeleza majukumu

haya mapya ya kijamii. Mifumo iliyofuata ilizaa sanaa mbalimbali zenye

malengo yaliyolingana na mazingira na hali hizo mbalimbali.


14

Kadri urazini wa binadamu ulivyozidi kupanuka, ndivyo umbuji ulivyozidi

kuibusha sura mpya za sanaa. Baada ya nyimbo, kukaanza utambaji wa hadithi

na ughani wa ushairi. Pole pole, fasihi ikaanza kuzaliwa kama sehemu ya jamii.

1.3.0 MAANA YA FASIHI

Fasihi ni sanaa. Kama sanaa nyingine yoyote, fasihi ni chombo chenye misingi

yake katika ubunifu. Katika ubunifu huu, binadamu hutumia lugha. Kwa hivyo,

fasihi ni sanaa ya lugha. Mwanafasihi huifinyanga lugha kisanii ili kuelezea

tajriba za binadamu. Ufinyanzi huu wa lugha huifanya fasihi ipendeze na kuvutia

kwa msikilizaji au msomaji. Ili lugha hiyo ipendeze, inabidi wakati mwingine

kukiuka baadhi ya kaida za lugha ya kawaida na hivyo kuwa na lugha teule.

1.3.1 AINA ZA FASIHI

Kuna aina mbili za fasihi:

(i) Fasihi simulizi

(ii) Fasihi andishi

(i) Fasihi simulizi hupitishwa kupitia mdomo. Haya ni masimulizi ambapo

maneno hutumiwa kisanaa kupitia masimulizi ya mdomo na sauti

ambayo huambatanishwa na ishara ili kuyapa masimulizi nguvu.

Katika fasihi hii, hadhira hushiriki katika kuuliza maswali, kushangilia,

n.k. Fasihi hii huhifadhiwa nyoyoni ingawa siku hizi huwekwa kwenye

kanda au kuandikwa vitabuni. Uhakiki wa fasihi simulizi huwa na

mguso wa papo kwa hapo.


15

(ii) Fasihi andishi ilizuka baada ya mapinduzi ya viwanda ya karne ya 18

na 19 kule Ulaya ambayo yaliambatana na uvumbuzi wa hati za

maandishi. Maandishi yakaanza kutumika kama namna mojawapo ya

kuwasiliana (baina ya binadamu). Sanaa ya lugha (fasihi) ikaanza

kuhifadhiwa na kupitishwa kutoka kizazi hadi kizazi kupitia kwa

maandishi. Maandishi pia yalipanua tanzu za fasihi; tukawa na riwaya,

tamthilia, hadithi fupi na ushairi ulioandikwa.

Katika kubuni, kuandika, kuhakiki, na kupembua kazi za fasihi andishi,

maneno hutumiwa kama chombo cha kuendelezea, kuelezea,

kuwakilishia na kufafanulia mawazo na fikira.

1.4.0 FANI NA MAUDHUI KATIKA FASIHI

Kazi yoyote ya fasihi ina yaliyomo au maudhui. Lengo kuu la fasihi ni

kuwasilisha ujumbe kwa wapokezi wa fasihi hiyo. Ujumbe au yaliyomo katika

fasihi huwasilishwa kupitia ufundi. Mbinu anazotumia mwandishi au msimulizi

wa fasihi huitwa fani. Sehemu hii itaangalia swala la fani na maudhui katika

fasihi.

ZINGATIA:

Fani na maudhui ni kama chai katika kikombe; ambapo fani ni kikombe


chenyewe na maudhui ni ile chai inayobebwa na kikombe hicho.
16

1.4.1 FANI KATIKA FASIHI

Katika fani, msomaji anapaswa kuzingatia mambo yafuatayo:

• Muundo au mtiririko wa kazi yenyewe.

• Mtindo aliotumia mwandishi.

• Lugha ya mwandishi.

• Mandhari yaliyochorwa na mtunzi.

• Wahusika walioumbwa na mwandishi.

Tuangalie kila kipengele na namna kinavyosaidia katika kufanikisha kazi ya

mwandishi.

1.4.1.1 Muundo

Muundo ni mpango au mtiririko wa kazi ya fasihi kwa upande wa visa na

matukio. Katika muundo, tunaangalia jinsi msanii alivyofuma, kuunda na

kuunganisha tukio moja na lingine, kitendo kimoja na kingine, wazo na wazo,

sura na sura, ubeti na ubeti, n.k.

Katika kuzingatia maswala hayo, msanii huipatia kazi yake umbo la namna

fulani. Ili kupata umbo hilo, matukio hupangwa kupitia hali ya kuwa na mwanzo,

katikati na mwisho. Kutegemea matakwa na azma ya mwandishi, muundo

unaweza kuwa wa moja kwa moja au wa kiuchangamano. Muundo wa riwaya ya

Kiu (M.S. Mohamed) na tamthilia ya Kitumbua Kimeingia Mchanga (S.A.

Mohamed) ni mifano mizuri ya maandishi yaliyofuata muundo wa moja kwa moja.


17

? Kwa kuzingatia fasihi ya Kiswahili, toa mifano sita ya kazi na miundo


ambayo kazi hizo imefuata.

1.4.1.2 Lugha

Kama tulivyosema, fasihi ni sanaa ya lugha. Lugha ndiyo nyenzo kuu katika

uandishi wa kazi za fasihi. Mwandishi wa fasihi hutumia lugha kuwasilisha

maudhui au ujumbe wake. Jinsi mwandishi alivyotumia lugha yake huathiri kwa

kiasi kikubwa jinsi msomaji atakavyoathiriwa na kazi hiyo. Matumizi ya lugha

huzingatia mambo yafuatayo:

(i) Tamathali za usemi

Tamathali za usemi ni maneno au sentensi ambazo hutumiwa na wasanii wa

fasihi ili kutia nguvu katika maana, mtindo na hata sauti katika maandishi ama

usemi. Tamathali hutumiwa kuipamba na kuongezea utamu katika lugha ya

fasihi. Kuna aina nyingi za tamathali za usemi. Baadhi yake ni:

(a) Tashbihi (mshabaha)

Katika tamathali hii, watu au vitu viwili au zaidi hulinganishwa na watu au vitu

vingine kwa kutumia maneno k.mf: kama, mithili ya, kana kwamba, mfano wa,

n.k. Mfano ni kusema: Juma alikuwa mwembamba mithili ya sindano.

(b) Sitiari

Sitiari hulinganisha watu au vitu bila kutumia viunganishi - linganishi. Watu au

vituu hivyo hulinganishwa kana kwamba viko sawa kabisa. Kwa nfano: Kadenge

ni simba. – Maanake Kadenge ni shupavu kama simba.


18

(c) Tashihisi / uhuishaji

Hapa, vitu visivyokuwa na sifa walizo nazo watu au viumbe vyenye uhai, hupewa

sifa hizo. Kwa nfano: Kalamu yangu ilitema wino jana asubuhi.

(d) Taniaba

Katika tamathali hii, jina la mtu binafsi hutumiwa kwa watu wengine wenye tabia,

mienendo, hali au kazi sawa na mtu huyo. Kwa mfano: Kuna malaika wengi

katika hii dunia.

(e) Taashira

Jina au sehemu ya kitu kimoja au kitu kidogo kinachohusiana na kingine kikubwa

hutumika katika kuwakilisha kitu kamili. Mfano ni: Bakari alikuwa na moyo wa

kusaidia.

(f) Majazi

Hii ni aina ya sitiari ambapo jina la mtu, kitu au mahali hufanana na tabia ya mtu

huyo, hali au kazi ya kitu au mahali hapo. Mfano ni mwandishi kumwita mhusika

mwenye tabia ya udaku Ndumakuwili.

(g) Lakabu

Lakabu huweka uhusiano wa kawaida wa maneno mawili kisarufi katika hali ya

kinyume. Kwa mfano: Mwangi ni hodari darasani –maanake hawezi chochote.


19

(h) Tabaini

Maneno au mawazo yanayokinzana sana hutumiwa katika sentensi ili kuleta

msisitizo wa mawazo yatolewayo. Kwa mfano: Mtu huyo ailkuwa si wa mbele si

wa nyuma.

(i) Tashtiti

Tashtiti hutumika pale ambapo swali linaulizwa huku jibu lake linafahamika wazi

wazi. Swali hilo huulizwa ama kwa ajili ya msisitizo tu au kwa nia ya kutoa

mshangao. Mfano ni: Lo! Asee, ni wewe? - Na anajua wazi ni wewe.

(j) Tanakali sauti

Haya ni maneno au nomino zinazoundwa katika sentensi kutokana na sauti au

milio inayofanana. Mfano huo huweza kutokana na kurudiwa kwa neno au

maneno yafananayo au miigo ya milio inayohusika. Kwa mfano: Alitumbukia

mtoni chubwi!

(k) Chuku / Udamisi

Tamathali hii inahusu utiliaji chumvi kuhusu uwezo wa viumbe, tabia zao na sifa

zao kwa madhumuni ya kuchekesha au kusisitiza. Mfano ni: Tulililia marehemu

Mzee Kenyatta hadi kukawa na bahari ya machozi.

(l) Kinaya / Kejeli

Maneno hutumika kinyume kabisa na maana yanayotakikana kutoa. Kejeli

huweza kuchanganya tamathali zinginezo kama vile ubeuzi uliofichika, kinyume,


20

tabaini na msisitizo bayana. Kwa mfano: Ama kwa kweli, mzee huyo ni tajiri – na

kumbe hana chochote.

(m) Dhihaka

Hii ni kejeli ambayo ina ubeuzi mkali, jahili unaopenya kweli kweli. Dhihaka

hutoa maneno ambayo kijuujuu ni mazuri lakini yana maana iliyo kinyume ndani

yake. Kwa mfano: Ulipoanza mchezo wa kulala mapema, nilijua utafaulu mtihani

wako.

? Kupitia kazi za fasihi ya Kiswahili ulizosoma, toa mifano ya tamathali za


semi zilizoelezewa hapa juu.

(ii) Methali, Misemo na Nahau

Hizi ni kauli fupi ambazo hutia vikolezo muhimu katika lugha ya fasihi na

kuufanya ujumbe kuwa mzito. Vipengele hivi huipatia lugha uhai kwa kuifanya

ikaribiane na jinsi inavyotumiwa katika hali halisi. Maana za kauli hizi za lugha

zimetolewa katika sehemu ya semi ya Somo la Pili (Angalia ukurasa wa 52-4).

(iii) Msamiati

Uchunguzi wa lugha hauna budi kuangalia jinsi mwandishi alivyotumia msamiati

wake. Msamiati hufungamana na matukio, muktadha na mandhari ya kazi ya

fasihi.
21

(iv) Taswira

Taswira ni mkusanyiko wa picha mbalimbali ziundwazo kupitia maelezo ya

waandishi katika kazi za fasihi. Picha hizi hujengwa kwa matumizi ya lugha au

maelezo fulani ili kuufanya ujumbe kujitokeza kwa msisitizo mkubwa. Tamathali

za semi husaidia katika kujenga taswira ya maandishi ya kifasihi.

(v) Taharuki

Taharuki ni mbinu ambapo mwandishi hutoa hali ya kusisimua hadhira kutokana

na shauku ya kutaka kujua jinsi mambo yatakavyojiri katika sura au sehemu

zinazofuata za kazi ya fasihi. Taharuki hujengwa makusudi kimfanya msomaji

aendelee kusubiri jambo litakalotokea.

(vi) Mvutano

Mbinu hii hushirikiana na taharuki ili kutoa hali ya mvutano au mkinzano baina ya

wahusika au hata katika nafsi ya mhusika mmoja wa kazi ya fasihi. Mvutano

huo hutokea baina ya taswira mbili au zaidi, hasa katika ushairi.

1.4.1.3 Mandhari

Mandhari yana nafasi na umuhimu mkubwa sana katika kazi ya fasihi . Mandhari

ni usawiri wa mazingira ambapo mahusiano na matukio baina ya wahusika

huendelea. Mandhari kwa hivyo, yana uhusiano mkubwa na vipengele vingine

vya utunzi kama vile wahusika, dhamira, maudhui, n.k.


22

1.4.1.4 Mtindo

Mtindo ni namna ambavyo mwandishi wa fasihi huitunga kazi yake na kuipatia

sura ambayo kifani na kimaudhui, huainisha kazi hiyo. Mtindo kwa hivyo ni

upangaji wa fani na maudhui kwa njia ambayo inadhihirisha upekee wa

mwandishi wa kazi hiyo. Mtindo humfanya msomaji wa kazi ya fasihi amtambue

mwandishi wa kazi fulani hata bila kuelezwa au kusoma jina la mwandishi huyo.

Kwa hivyo mtindo ni mazoea ya mwandishi au msanii fulani ya kuandika na kwa

jumla yanahusisha:

i) Usimulizi wake

ii) Uteuzi wa msamiati

iii) Tamathali za usemi alizotumia

iv) Uteuzi wa lugha yake

v) Jinsi alivyoanza, kuendeleza na kumaliza kazi yake

vi) Mpangilio wa matukio

vii) Taswira, taharuki na mvutano

viii) Usawiri wake wa wahusika kwa majina, tabia na hulka zao

Mtindo huweza pia kuwa wa kipindi fulani au wa eneo fulani. Kinachozingatiwa

hapa ni jinsi waandishi fulani wanavyoonyesha sifa fulani zinazofanana katika

kipindi fulani cha kihistoria au eneo fulani la kijiografia.

1.4.1.5 Wahusika

Matukio yanayopatikana katika kazi ya fasihi huwa na watu au viumbe

wanaoyatenda. Hawa huitwa wahusika. Kwa hivyo, wahusika ni viumbe wa


23

mawazoni wanaoumbwa na mwandishi na kuibuka katika kazi yake ya fasihi.

Wahusika wa fasihi hukusudiwa kuwakilisha tabia za watu katika maisha au

mazingira halisi.

Wahusika wanaweza kuwa wanyama, wadudu, mimea, mashetani, miungu,

majitu, mazimwi, n.k. Wahusika wanaweza pia kuwa vivuli vya mawazoni

ambavyo havina mshabaha sana na maisha halisi ya duniani. Kwa mfano

wanaweza kuwa viumbe ambavyo ni nusu-watu nusu-malaika, nusu-majini;

viumbe visivyoonekana lakini vinasimuliwa tu. Karibuni kumezuka wahusika

ambao ni maroboti na vibonzo ambao wametokana na ubunifu wa kisayansi.

Mwandishi au msanii huwazua wahusika ambao wanaambatana na uhalisia wa

maisha alioupata katika uzoefu wake wa kuishi. Hii ni kutokana na kuwa fasihi

imeshikana sana na maisha ya watu na inahusu watu hao na maisha yao.

Mhusika huanza katika ugunduzi wa mwandishi na hatimaye kumea akilini na

kuwa sehemu ya fikra zake na kisha kuchujwa na itikadi yake na kumalizikia

katika mfuatano wa lugha yake.

1.4.1.6 Ujenzi wa Wahusika

Wahusika hujengwa kutokana na mojawapo ya mambo yafuatayo:

(i) Tabia ya mtu fulani ambaye mwandishi amempeleleza kwa

kuongozwa na tafakuri yake. Mwandishi huongeza au kupunguza hiki

na kile katika tabia hiyo kwa mujibu wa jinsi anavyotaka kumwasilisha


24

au kumsisitiza mhusika wake.

(ii) Tabia ya mtu ambaye mwandishi amemsikia akihadithiwa au kumsoma

mahali na kuibadilisha tabia hiyo katika ubunifu wake huku

akimpunguza au kumzidisha.

(iii) Dhana fulani ya kimaisha k.v. wema, utu, ujahili, ulaghai, uadilifu,

ukaidi,utiifu, n.k.

(iv) Ndoto, ruya au nishai ya mwandishi inayomfanya mhusika wake kuwa

jini, shetani, dudu, nyama nyama au dude dude bila kuwa na mashiko

na watu halisi ingawa katiwa chumvi.

(v) Mwandishi kuchangiachangia wasifu wa tabia za watu anaowajua au

aliowapeleleza au kuwasoma katika pitia pitia zake.

(vi) Mwandishi kuchangiachangia wasifu wa tabia bila kigezo cha mtu

yeyote bali kutokana na ndoto na ubunifu wa mwandishi mwenyewe.

(vii) Mhusika katika kazi ya fasihi anaweza kumwakilisha mwandishi

mwenywe.

1.4.1.7 Aina za Wahusika

Hakuna njia maalum ya kuainisha wahusika wa kifasihi. Hata hivyo, tunaweza

kuzingatia aina za wahusika katika vitengo vikuu vifuatavyo ambavyo

vinahusiana na kuingiliana.

(i) Wahusika Wakuu

Wahusika wakuu hujitokeza kila mara katika kazi ya fasihi tangu mwanzo hadi

mwisho. Maudhui makuu huendelezwa kupitia mhusika mkuu wa kazi ya fasihi


25

kuliko wahusika wengine. Wahusika hawa mara nyingi huitwa midomo au vipaza

sauti vya waandishi.

Mhusika mkuu huchorwa kwa mapana na marefu ya maisha na tabia zake ili

kukamilisha ubinafsi wake. Hata hivyo, si lazima kuwe na mhusika mkuu mmoja

katika kazi ya fasihi. Wahusika wakuu wanaweza kuwa wawili na zaidi

kutegemea matakwa na azma ya mwandishi.

(ii) Wahusika Wadogo

Wahusika wa aina hii hujitokeza hapa na pale katika kazi ya fasihi ili

kuukamilisha ulimwengu wa kazi hiyo. Wahusika hawa husaidia katika kujenga

maudhui madogo madogo katika kazi za fasihi hivyo kusaidia kukuza dhamira

na maudhui makuu ya kazi hiyo.

Mhusika huamuliwa kuwa mdogo kwa kulinganishwa nafasi yake na ile ya

wahusika wengine katika kazi ya fasihi hasa kwa upande wa kujenga na kukuza

dhamira kuu ya kazi husika.

(iii) Wahusika Mviringo

Mhusika mviringo humkaribia sana mwanadamu halisi kwa ulinganifu wa wasifu

na tabia. Kwa hivyo, mhusika huyo huaminika na kukubalika katika kipimo cha

ukweli na uhalisia wa maisha. Mhusika mviringo hukua na kubadilika katika hali

zake za kitabia na kihisia. Mhusika huyo huwa na sehemu ya uzuri na ubaya,

hivyo huwa na tabia za kupendeza na tabia za kuchukiza.


26

(iv) Wahusika Bapa

Hawa ni wahusika ambao hawageuziki kwa sababu hawakuviringwa. Wahusika

bapa hufuata mstari mmoja ule ule wa matendo na tabia zilizokusudiwa

kuwasilishwa na kusisitizwa na mwandishi. Wahusika hao hawabadiliki wala

kulingana na maisha halisi. Kwa hivyo hawaaminiki katika kigezo cha uhalisia

wa maisha. Mhusika bapa huwa ametiwa chumvi mno na kuambatana na

mambo ya kiajabuajabu.

Mhusika bapa hukusudiwa kuwa hivyo na mwandishi. Mhusika huyo hutumiwa

katika kukidhi haja ya kusisitiza wazo kuu fulani au tabia fulani, hasa juu ya

wema au ubaya. Mhusika bapa husawiriwa kama mbaya au mwema tangu

mwanzo hadi mwisho wa kazi husika ya fasihi.

(v) Wahusika Vinyago

Wahusika vinyago huchorwa na mwandishi kwa kutaka kukejeli tabia fulani ya

kuchekesha. Wahusika hao wanafanana na wahusika bapa. Tofauti ni kwamba

vinyago ni lazima wakejeliwe, wafanyiwe ishtizai na tashtiti, wakati bapa si lazima

wafanyiwe hivyo. Wahusika vinyago huchorwa dude dude, nyama nyama, jinga

jinga, n.k.

? Kwa kutumia kazi zozote mbili za fasihi ulizozisoma, eleza aina na


umuhimu wa wahusika wanaopatikana katika kazi hizo.
27

1.4.2 MAUDHUI KATIKA FASIHI

Dhana ya maudhui inashughulikiwa pamoja na dhana ya dhamira. Mwandishi

anapoanza kuandika kazi yake, huongozwa na lengo fulani. Msomaji huenda

asiwe na bahati ya kukutana na mwandishi na kumwuliza lengo au alichokusudia

kusema katika kazi yake. Msomaji atalazimika kusoma kazi hiyo kwa makini na

kutambua wazo kuu ambalo limekuzwa na kuendelezwa na mwandishi kuanzia

mwanzo hadi mwisho. Hiyo ndiyo dhamira ya kazi hiyo ya fasihi. Aghalabu

lengo au wazo hilo kuu huweza kutolewa kupitia kichwa au anwani ya kazi

inayohusika.

Katika kuendeleza lengo kuu, kunazuka mambo mengine mengi. Msomaji

atapata ujumbe, msimamo na falsafa ya mwandishi kuhusiana na lengo au wazo

kuu. Mwelekeo huo wa mawazo ya mwandishi hutolewa kupitia maudhui. Kwa

hivyo, maudhui ni yaliyomo au jumla ya masuala yanayozungumziwa katika kazi

ya fasihi. Maudhui huibuka katika uendelezaji na ukuzaji wa dhamira au wazo

kuu la kazi ya kifasihi. Kwa kifupi, dhamira hujitokeza kama sehemu ya

maudhui.

1.5.0 FASIHI NA MAISHA

Fasihi hujishughulisha na binadamu na maisha yake. Fasihi huathiri, kugusa na

kuonyesha hali ya maisha ya binadamu kupitia usanii wa lugha. Kuna mawanda

matatu ambapo fasihi inaonekana ikisaidia binadamu. Tuangalie mawanda

hayo matatu na namna yanavyohusiana na fasihi.


28

1.5.1 Fasihi katika Dini na Maadili

Fasihi imetumika kama maombi ili binadamu apendeze machoni mwa Mungu au

miungu yake. Lengo la fasihi ya aina hii ni kumfanya binadamu kuwa mwema

zaidi na kumkaribia muumba wake kitabia na kimaadili.

Fasihi hutumika kufundisha binadamu kuhusu maisha mema na maana ya

uadilifu. Kwa kufanya hivyo, fasihi humtengeneza binadamu kitabia na kimaadili.

Katika Kiswahili, kazi za fasihi ambazo zinaweza kuingia katika kiwango hiki ni

pamoja na Siku ya Watenzi Wote (Shaaban Robert), Al Inkishafi (A. Nassir) and

Utenzi wa Mwanakupona (Mwanakupona). Kazi hizi zote zimeshughulikia

maswala mema katika maisha ya binadamu.

1.5.2 Fashi na Jamii

Fasihi imetumika kama chombo cha kukuza na kudumisha uhusiano mwema

baina ya binadamu na jamii yake. Fasihi kwa hali hiyo hutoa mafunzo na maadili

yanayojenga mshikamano wa jamii. Kazi za fasihi hutoa mafunzo kuhusiana na

ukarimu, uaminifu, uhusiano wa ndoa, mapenzi, n.k.

Katika fasihi ya Kiswahili waandishi wengi wameshughulika na nafasi ya fasihi

katika jamii. Kwa mfano, Kezilahabi katika kazi zake kama vile Kichwa Maji,

Rosa Mistika na Dunia Uwanja wa Fujo anasaili maisha na maana yake.

Mwandishi huyu anaonyesha binadamu kama kiumbe anayeanza kufa pindi

azaliwapo. Naye Rocha Chimerah katika riwaya yake ya Nyongo Mkalia Ini

amesawiri mivutano na migogoro ya kitabaka katika jamii nyingi za Kiafrika.


29

1.5.3 Fashi na Mtu Binafsi

Kuna maandishi mengi ya kifasihi ambayo yanasimulia maisha katika kiwango

cha mtu binafsi. Maandishi ya aina hiyo husaidia katika kumwinua binadamu ili

awakaribie au kuwafikia mashujaa wa kijamii kwa upande wa tabia na matendo.

Fasihi hufurahisha na vile vile kuwafundisha binadamu binafsi kuwa wazuri zaidi.

Fasihi hukuza hisia za binadamu hivyo kuwa muhimu katika kiwango cha mtu

binafsi. Katika Kiswahili, kuna Maandishi kama vile Maisha Yangu Baada ya

Miaka Hamsini na Wasifu Wa Siti Binti Saad (Shaaban Robert), Mzalendo

Kimathi (N. Thiong’o na N. Mirii) na Siku Njema (K. Walibora) ambayo

yameshughulikia maisha ya watu binafsi.

1.6.0 JUKUMU LA FASIHI

Kwa muda mrefu imechukuliwa kwamba jukumu la fasihi ni kuelimisha na

kustarehesha. Fasihi huwasilisha hali, maingiliano, mivutano na mikinzano

miongoni mwa binadamu na mazingira yako. Mafunzo ya fasihi hupatikana

kupitia ule usawiri wa wahusika, kauli zinazotolewa na mwandishi, na falsafa na

misimamo mbalimbali ya watunzi. Waandishi wengi hujaribu kusimulia maisha

katika mapana na marefu yake kupitia lugha teule ili kugusa hisia za wasomaji.

Kutosheka tunakokupata katika kazi za fasihi hakupatikani kutokana na habari

tunazozipata katika kazi hizo bali hutokana na ufinyanzi wa lugha teule,

uhodari wa masimulizi na undani wa maisha tunaokumbana nao. Maudhui ya

kazi za fasihi ni lazima yawe na mguso ndipo yaweze kunasa na kuteka hisia za

wasomaji. Kwa hivyo, kuna uhusiano mkubwa baina ya fasihi na matukio ya


30

jamii na hili ndilo jukumu la sanaa hiyo.

1.7.0 MUHTASARI:

Katika somo hili, tumetanguliza kozi hii kwa kushughulikia dhana ya fasihi.
Tumeona namna fasihi kama sanaa ya lugha ilivyo na maswala mbalimbali
yanayoijenga. Katika somo hili, maana na asili ya sanaa, ikiwemo fasihi
imetolewa. Hiyo ni pamoja na vigezo na vipengele vinavyojitokeza katika
ufahamu wa fani na maudhui kama matapo makuu ya fasihi. Mwisho, somo hili
limezingatia uhusiano uliopo baina ya fasihi na maisha. Somo linalofuata
linahusu fasihi simulizi kama mojawapo ya aina kuu mbili za fasihi.

1.8.0 ZOEZI:

1. Huku ukitoa mifano, fafanua kauli kwamba ‘fasihi ni sanaa ya lugha’.


2. Jadili maana na asili ya sanaa kama inavyozungumziwa na wanazuoni.
3. Fani ni kiumbiumbi cha nje na maudhui ni kiumbiumbi cha ndani cha kazi
ya fasihi. Tathmini.
4. Onyesha jinsi fasihi inavyohusiana na kuathiri maisha ya binadamu.
5. Eleza vipengele vifuatavyo vya fasihi
(i) Maudhui
(ii) Wahusika
(iii) Mtindo
(iv) Taswira
(v) Tamathali za usemi
31

1.9 MAREJELEO TEULE

Njogu, K. & Chimerah, R (1999): Ufundihsaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu.

Nairobi: Jomo Kenyatta foundation

Matti, G.N. (2003): Mwongozo wa Kitumbua Kimeingia Mchanga.Nairobi:

Africawide Network.

Mohamed,S.A. (1995): Kunga za Nathari ya Kiswahili. Nairobi: Oxford

University Press.

Senkoro, F.E.M.K. ( 1982) : Fasihi Dar es Salaam: Press and Publicity Centre.

Wamitila,K.W. (2002): Uhakiki wa Fasihi: Misingi na Vipengele Vyake. Nairobi:

Phoenix Publishers Ltd.

____________(2003): Kichocheo cha Fasihi: Simulizi na Andishi. Nairobi:

Focus Books
32

SOMO LA PILI

FASIHI SIMULIZI

2.0 UTANGULIZI

Fasihi simulizi hupitishwa kupitia maneno ya mdomoni na kuhifadhiwa katika

nyoyo ili iweze kupitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Katika somo hili,

tutaangalia fasihi simulizi kama aina mojawapo ya fasihi. Somo hili litaanza kwa

kuelezea maana ya fasihi simulizi. Kisha, tutaangalia majukumu ya fasihi

simulizi na tofauti baina ya fasihi hii na fasihi andishi. Somo hili vile vile

linashughulika na tanzu mbalimbali za fasihi simulizi pamoja na utafiti na

mwelekeo wa sasa katika fasihi hiyo.

2.1.0 MALENGO

Kufikia mwisho wa somo hili, utaweza kufahamu:


1. Maana ya fasihi simulizi
2. Majukumu ya fasihi simulizi
3. Fasihi simulizi na fasihi andishi
4. Tanzu za fasihi simulizi
5. Fasihi simulizi sasa

2.2.0 MAANA YA FASIHI SIMULIZI

? Fasihi simulizi ni nini?

Fasihi simulizi imechukuliwa kama sanaa ambayo si ya maana hasa na watafiti

wa kimagharibi. Fasihi hii imechukuliwa kama sanaa ya mijitu isiyofahamu kitu,


33

mijinga isiyojua kusoma na kuandika na ambayo haikuweza kufarajika kwa kazi

yoyote ‘njema’ ya kutumia akili ila mikono na maguvu yao. Watafiti hawa

walioathiriwa na kasumba za kikoloni wanasema ‘ustaarabu’ na ‘maendeleo’

vilifutilia mbali alama au mabaki yoyote ya fasihi hiyo ya ‘kishenzi’. Mawazo

kama haya yametokana na hali kwamba fasihi simulizi imekuwa na tabia ya

kukashifu mabepari na kutukuza wiano wa kijamii.

Fasihi simulizi ni kitovu cha maendeleo ya mwanadamu kinyume na mawazo

hasi yaliyoletwa na wataalamu wa kimagharibi. Fasihi hii ni chombo cha

wanyonge na walio wengi. Fasihi simulizi ni fasihi kwa hali yake na wala sio

kijakazi au mtumwa wa taaluma nyingine. Watu wengi wasiojua kusoma na

kuandika wanatoa hisia zao na mawazo yao ya ndani kwa kutumia chombo hiki

cha kisanaa. Hata kwa waliosoma, fasihi simulizi inaishia katika shughuli za

utamaduni na uzalishaji mali. Fasihi simulizi inatoa mchango mkubwa sana kwa

fasihi andishi usioweza kuepukika.

Fasihi simulizi inadai ukale zaidi ya fasihi andishi pamoja na haki ya kujiri na

kuendelea kujiri katika jamii zote. Fasihi hiyo huibuka na kuoana na utamaduni

wa jamii fulani, na utamaduni huo kukua kwa misingi ya uzalishaji mali

ukiambatana na uhusiano wa watu kijamii pamoja na jumlisho la amali zao. Kale

kulikuwa na uendelezaji wa sehemu kadha za utamaduni kama vile mambo ya

ndoa, arusi, uzazi, malezi, marika, mafunzo mbalimbali ya mazingira na shughuli

kama za jando, sherehe maalum na amali zilizohusu imani juu ya

miungu,mashetani na mizimu. Fasihi simulizi kimekuwa chombo cha kuhifadhi,


34

kulinda na kuendeleza amali hizo, na ilizuka katika tanzu zake k.v. ngoma,

ushairi , nyimbo, ngano, hadithi, majigambo, itikadi, methali, vitendawili, n.k.

Fasihi simulizi ni kitu kinachoendelea wala hakijatuwama pahala pamoja;

imekuwa ikibadilika kwa madhumuni ya mifumo ya jamii pamoja na amali zake.

Fasihi simulizi inaambatana na matatizo ya kijamii kama yalivyo leo na ni laizima

iwakilishe mawazo ya walio wengi.

Fasihi hiyo imedumu kwa sababu isingaliweza kufa ikiwa ni sehemu ya maisha

ya wanadamu vijijini. Kwa hivyo, imeachwa kuendelea, kuundwa na kuishi bila

bughudha katika jamii.

Katika historia ya jamii za ulimwengu, fasihi simulizi ilitangulia fasihi andishi. Hii

ni fasihi iliyopokezanwa kwa njia ya mdomo. Nyenzo kuu hapa ilikuwa usemi au

neno lililosemwa, ngoma inayochezwa au sauti inayoimbwa. Hiyo kwa kweli

ndiyo fasihi simulizi; fasihi ambayo ilikuwa njia ya kujieleza, kujielewa na

kujifahamu kwa binadamu. Katika kulitekeleza hili, fasihi hiyo ilimtumbuiza na

kumpa binadamu burudani ya kujiliwaza, n.k.

Baada ya mabadiliko na maendeleo ya kiteknolojia, fasihi simulizi sasa imeweza

kuhifadhiwa kwa njia mbalimbali k.v. vinasa sauti, kanda za video na kompyuta.

Vile vile ni katika vitabu vingi vilivyokusanya methali, vitendawili, nahau, semi,

mashairi, tendi au nyimbo na ngano ambazo hapo kabla zilihusishwa na

masimulizi ya midomo tu.


35

2.3.0 MAJUKUMU YA FASIHI SIMULIZI

Kwa jumla tunaweza kugawa wajibu wa fasihi simulizi katika majukumu

yanayohusiana na burudani, elimu, ujitambulishaji, ujamiishaji na ukuzaji wa

stadi za lugha. Baadhi ya majukumu maalum ya fasihi simulizi ni kama

yafuatayo:

2.3.1 Kuburudisha

Fasihi simulizi huweza kutumiwa kama burudani. Tanzu kama hadithi, ushairi,

semi na nyimbo huweza kutumiwa kuwaburudisha wanaohusika. Watoto katika

jamii nyingi, kwa mfano, hutegeana vitendawili kama njia ya kujiburudisha.

Aidha, hadithi, ngano, hekaya na hurafa hutambwa kama njia ya burudani.

2.3.2 Kuelimisha

Fasihi simulizi ni njia kuu ya kuelimisha hasa katika jamii ambapo mfumo wa

kimaandishi haujashika sana. Wanajamii wanaweza kuzipitisha thamani za

kijamii, historia yao, utamaduni na matamanio yao kutoka kizazi kimoja hadi

kingine kwa kutumia fasihi simulizi.

2.3.3 Kuhifadhi Historia na Utamaduni

Fasihi simulizi ni nyenzo kuu na muhimu ya kuzihifadhi amali muhimu za kijamii.

Aidha, wanajamii wanaweza kujua historia zao kupitia fasihi simulizi. Maarifa

haya husaidia mwanajamii kujielewa na kujitambua.


36

2.3.4 Kufundisha

Katika tanzu mbalimbali za fasihi simulizi, kuna maadili na mafundisho ya

kuwaelekeza, kuwaadibu, kuwaonya na kuwaongoza watu kwenye matarajio ya

jamii yao. Kwa mfano, jamii nyingi zilitumia fasihi hii kama njia ya kuwaelekeza

na kuwafundisha vijana mienendo mizuri, maadili yafaayo na falsafa zifaazo

katika maisha yao.

2.3.5: Kuunganisha Watu

Kuwepo kwa fasihi simulizi kunakuwa msingi muhimu wa wanajamii waliopo

kuunganishwa na wale waliotangulia. Watu wakitambiwa hadithi zao, vitendawili

vyao, methali zao na nyimbo zao, umbali wa kiwakati kati ya vizazi

vilivyotangulia, vilivyopo na vijavyo unafupishwa.

2.3.6 Kutoa Mwelekeo

Kwa kuelimishana na kuyapitisha mawazo yanayohusiana na jamii, fasihi simulizi

inawahakikishia wanajamii mwelekeo na matumaini katika maisha ya baadaye.

2.3.7 Kukuza na Kustawisha Lugha

Fasihi simulizi hutegemea usemi na matamko. Mambo haya huwezekana kupitia

maongezi, matamshi na uimbaji. Kwa njia hii, fasihi simulizi huchangia katika

kuboresha uwezo wetu wa kuzimiliki na kuzimudu stadi za lugha. Tanzu kama

vile vitanza ulimi husaidia kuhakikisha kuwa utamkaji wa maneno ni mzuri, na

vitendawili hukuza uwezo wa kuwaza haraka haraka na vyema. Nazo hadithi


37

hukuza uwezo wa kukumbuka.

2.3.7 Kukuza Ushirikiano na Uelewano

Fasihi simulizi si mali ya mtu mmoja bali ni ya jamii nzima. Hadithi husimuliwa

kwa hadhira kubwa na pana. Shughuli hii huhusisha jamii nzima na hukuza

ushirikiano na uelewano wa wanajamii wote.

2.4.0 FASIHI SIMULIZI NA FASIHI ANDISHI

? Kuna uhusiano gani kati ya fasihi simulizi na fasihi andishi?

Fasihi simulizi na fasihi andishi zina uhusiano mkubwa sana. Kwa mfano, baadhi

ya tungo zinazopatikana katika jamii mbalimbali zilikuwako kabla ya kuvumbuliwa

kwa maandishi. Tunapochunguza baadhi ya tungo za fasihi andishi, tunaona

taathira fulani za fasihi simulizi. Na tunapochunguza kazi nyingine zilizoandikwa

katika tanzu nyinginezo, tunaona jinsi zinavyoakisi mbinu za usimulizi za fasihi

andishi.

2.4.1 Uwasilishaji

Fasihi simulizi huwasilishwa kwa njia ya mdomo kwa kusimuliwa, kuimbwa,

kutongolewa au kughaniwa. Fasihi andishi huwasilishwa kwa njia ya maandishi.

2.4.2 Utendaji

Hadhira ya fasihi simulizi inaweza kuwa tendaji ambayo inashiriki na kuchangia

katika uwasilishaji wa kazi inayohusika. Hadhira ya fasihi andishi hupokea

ujumbe wake kwa hali ya kutulia tuli.


38

2.4.3 Ubunifu

Fasihi simulizi hubuniwa papo kwa hapo na kutolewa hapo hapo. Mtambaji

huweza kuingiza ubunifu wake wakati wa kutamba na kusimulia hadithi. Ubunifu

wa fasihi andishi hutokea tu wakati wa kuandika. Baada ya kuandikwa, kazi hiyo

hubakia vile vile na msomaji hana nafasi ya kuingiza ubunifu wake bila hatari ya

kubadilisha kazi asilia.

2.4.4 Wakati

Uwasilishaji au upokezanaji wa fasihi simulizi hufanyika katika wakati maalum.

Kuna vipindi maalum kwa mfano vya kutegeana vitendawili na vya kusimuliana

hadithi, hasa wakati wa jioni, katika jamii nyingi. Uwasilishaji huu pia hufanyika

kwenye vikao maalum. Fasihi andishi haifungwi na kipengele cha wakati au

sehemu fulani maalum. Msomaji anaweza kuisoma kazi iliyoandikwa wakati

wowote ule na mahali popote pale.

2.4.5 Historia na Utamaduni

Fasihi simulizi inatumiwa na jamii nyingi kama njia ya kupashana maarifa

yanayohusiana na historia au tamaduni fulani za wanajamii, matamanio yao,

mitazamo yao, n.k. Fasihi andishi inaweza kujihusisha na maswala haya au

kuyapuuza.
39

2.4.6 Vichocheo

Uwasilishaji wa fasihi simulizi hutegemea vitu kama vile mavazi, mabadiliko ya

kihisia ya mtambaji, miondoko yake, maigizo, ishara, n.k. kama vichocheo vya

ujumbe. Fasihi andishi (isipokuwa sanaa za maigizo) hujihusisha na matumizi ya

lugha kama nyenzo ya pekee ya kuwasilisha hisia, vionjo na maudhui yake na

mtunzi wake hana nafasi aliyo nayo mtambaji wa fasihi simulizi.

2.4.7 Uhuru wa Msanii

Katika fasihi simulizi, mwasilishaji ana uhuru mpana wa kubadilisha mbinu na

hata mwendo wa kazi anayoiwasilisha papo kwa hapo. Katika fasihi hiyo, swala

la ufaraguzi lina nafasi kubwa na ubora wa uwasilishaji hutegemea ufundi wa

mtambaji. Kinyume na uhuru huu, kazi za fasihi andishi hazibadiliki kwani

msomaji hana uhuru wa kuibadilisha kazi iliyokwisha kuandikwa.

2.4.7 Hadhira

Hadhira ya fasihi simulizi huathiri uwasilishaji kwa namna fulani. Hadhira

hushiriki katika kutoa maoni, kuuliza maswali, kucheka, kuimba, n.k. hivyo

kuathiri uwasilishaji. Hadhira ya fasihi andishi haina athari ya moja kwa moja kwa

msanii ambaye huandika kazi yake peke yake.

2.4.8. Umilikaji

Fasihi simulizi ni mali au milki ya jamii kutokana na kupokezanwa kutoka kizazi

kimoja hadi kingine. Kazi za fasihi andishi humilikiwa na wasanii wanaohusika

wenyewe.
40

2.4.9 Ukale

Fasihi simulizi ina vitanzu vingi vyenye historia ndefu. Fasihi hii imekuwako

kabla ya kuvumbuliwa kwa maandishi na inahusishwa kwa kiasi kikubwa na

tamaduni simulizi zisizotegemea maandishi. Kwa upande wake, fasihi andishi

ina vitanzu vichache na imeanza tu baada ya maandishi kuanza au kuzuka kwa

tamaduni andishi.

2.4.10 Kuhifadhiwa

Kuhifadhiwa kwa fasihi simulizi kuna ugumu mkubwa ikilinganishwa na fasihi

andishi. Fasihi simulizi hupokezanwa kwa mdomo na sehemu fulani huweza

kupotea au kusahaulika kutokana na mtu kushindwa kwa urahisi kutokana na

kuwa katika hali ambayo si thabiti.

2.4.11 Ugiligili

Tanzu za fasihi simulizi zina ugiligili au kuingiliana vikubwa sana. Kwa mfano,

methali huweza kuwa kitendawili na kitendawili kuwa methali. Fasihi andishi

huwa na tanzu ambazo zimejitambulisha na kujisimamia.

2.5.0 TANZU ZA FASIHI SIMULIZI

Utanzu ni mgawanyo au tawi la kitu au taaluma fulani. Tanzu za fasihi simulizi ni

matawi mbalimbali yanayoitambulisha fasihi hiyo. Uainishaji wa tanzu hizo

hutegemea sifa fulani fulani zinazohusiana na kila utanzu.


41

Misingi ya kuainishia tanzu za fasihi simulizi ni kupitia mswali kama:

Ni lugha gani iliyotumiwa katika uwasilishaji?

Ni lugha ya mjazo au nathari?

Ni lugha ya kishairi?

Pana matumizi ya mazungumzo?

Kuna uimbaji?

Ni utanzu mfupi wenye muundo tata na wa kimafumbo?

Pana uigizaji au maonyesho?

Maudhui yaliyopewa uzito ni yepi?

Pana ubunifu wa kiasi gani?

Pana mitindo gani ya mianzo na miisho?

Wahusika ni wa aina gani?

Kwa kutumia vipengele na majibu ya maswali hayo tunaibuka na tanzu

mbalimbali za fasihi simulizi. Kila utanzu una vijitawi au vipera kadha.

2.5.1 HADITHI

Hadithi ni masimulizi ambayo yanatumia lugha ya mjazo au lugha ya nathari na

mtiririko wake huwa mwepesi au sahihi. Urefu wa hadithi hutofautiana kutoka

kitanzu au kipera kimoja hadi kingine. Kuna hadithi za kubuni na hadithi za

kihistoria.
42

2.5.1.1 Uwasilishaji wa Hadithi

Hadithi huwasilishwa kwa hadhira kwa utendaji ambao unaweza kuhusishwa na

sifa kadha. Sifa hizo huitwa mbinu au mikakati ya usimulizi au utambaji.

i) Mianzo

Katika jamii nyingi, hadithi za mapokeo huwa na vitangulizi au mianzo

maalum. Kwa mfano, Waswahili hutanguliza hadithi kwa jinsi tofauti tofauti

k.v.

Paukwa --- pakawa

Hadithi hadithi --- Hadithi njoo ---

Atokeani! --- Naam Twaibu! --- n.k

KUMBUKA:

Mianzo maalum ya hadithi huwa na majukumu kadha:


• Huwa njia ya kuwavutia wasikilizaji pamoja na kuivuta makini ya hadhira
• Hutumiwa kumtambulisha mtambaji wa hadithi
• Huashiria na kuonyesha mwanzo wa hadithi
• Huweka mpaka wazi kati ya ulimwengu halisi na ulimwengu wa hadithi.

(ii) Kimalizio

Katika jamii nyingi, kuna mtindo maalum wa kumalizia hadithi. Hii ni fomula ya

mwisho au kimalizio.

Jamii nyingi huwa na kimalizio “hadithi yangu imemalizikia

hapo”.
43

KUMBUKA:

Kimalizio:
• Huashiria mwisho au kumalizika kwa hadithi.
• Huwa kitangulizi cha shughuli inayofuatia utambaji au mwanzo wa utambaji
mwingine.
• Huashiria mtambaji mwingine kuanza hadithi yake.
• Huwapumzisha wasikilizaji au kuituliza hadhira ambayo ilikuwa makini wakati
wa usimulizi.

3.5.1.2 Umuhimu wa Hadithi

Hadithi huwa na umuhimu mkubwa katika jamii. Baadhi ya kazi ambazo

hutekelezwa na hadithi ni kama zifuatazo:

(i) Kutoa Mwelekeo

Hadithi hutoa mwelekeo katika jamii. Hadithi hufumbata mtazamo wa jamii

pamoja na falsafa yake katika kuelekeza jamii husika.

(ii) Kutoa Maadili

Hadithi huwa na mafunzo maalum. Mafunzo hayo hutokana na mambo

yanayopatikana katika hadithi hiyo.

(iii) Kuelekeza

Hadithi huonya, huadibu na huelimisha pamoja na kushauri na kunasihi jamii.

Wahusika wa hadithi hupewa sifa za kuelekeza au zinazopaswa kupuuzwa.

Wahusika wenye sifa nzuri huangaliwa kama vielelezo bora vya jamii ifaayo.
44

(iv) Kuelimisha

Hadithi hurithisha jamii elimu, thamani na amali muhimu kutoka kizazi kimoja

hadi kingine. Hivyo, hadithi huwa nyenzo muhimu ya kurithishana elimu ya jadi

katika jamii inayohusika.

(v) Kuburudisha

Hadithi nyingi hutambwa majira ya jioni hasa baada ya kazi za kutwa. Usimulizi

huu huwa njia nzuri ya kuwaburudisha wasikilizaji.

(vi) Kukuza Ushirikiano

Hadithi husaidia kuendeleza uhusiano baina ya wanajamii hivyo kukuza

ushirikiano. Hadithi husimuliwa mbele ya hadhira ya watu waliojumuika pamoja

hivyo kujenga misingi imara ya ushirikiano wa kijamii.

2.5.1.3 Sifa za Hadithi

Ufanifu wa hadithi hutegemea mambo mengi. Tunapoichunguza hadithi ya

fashihi simulizi, tunachambua sifa kadha. Uchunguzi wa sifa hizo ni muhimu

kama msingi wa kuielewa miundo ya hadithi hizo na viini vyake.

(i) Hadithi na Maudhui

Hadithi huwa na lengo au wazo kuu (dhamira) na yaliyomo (maudhui) yaliyoibuka

katika kusimuliwa kwake.


45

(ii) Msuko

Msuko ni namna matumikio ya hadithi yanavyopangwa kuanzia mwanzo hadi

mwisho. Hadithi huwa na kitangulizi, mvutano unaoendeleza mgogoro, kilele au

upeo na hatimaye mwisho au masuluhisho.

(iii) Urudiaji

Hadithi huwa na urudiaji wa vipengele mbalimbali vya muundo k.v. virai, maneno,

sentensi, vifungu, nyimbo, n.k. Kuna pia urudiaji wa mawazo, fikra, maono, n.k.

Urudiaji huyafanya mambo yaliyorudiwa kukumbukika na pia kusisitizwa.

(iv) Nyimbo

Nyimbo hutumiwa sana katika masimulizi ya hadithi. Nyimbo husisitiza wazo kuu

na kuishirikisha hadhira katika hadithi. Nyimbo pia huongezea uhai katika hadithi

na kuwapambanua wahusika wanaopatikana katika hadithi.

(v) Wahusika

Wahusika wa hadithi huwa binadamu au wanyama ambao wamepewa sifa za

binadamu. Jamii mbalimbali huwa na wahusika wenye sifa tofauti tofauti.

Wahusika husaidia katika kuendeleza maudhui ya hadithi kupitia tabia na hulka

zao.

(vi) Uigizaji

Msimuliaji au mtambaji wa hadithi huiga sauti mbalimbali za wahusika na

mwendo wa wanyama k.v. wa kuchechemea, kujipindapinda, kuchapa, n.k.


46

Wasimulizi wakati mwingine hutumia maleba ili kutia uhai katika kisa

wanachotamba na kusimulia ili kuhakikisha hadhira imepata mguso wa kutosha.

2.5.1.4 AINA ZA HADITHI

Hadithi zinaweza kuwekwa katika makundi makuu mawili yenye vitanzu vidogo

vidogo. Kuna hadithi za kubuni ambazo hujengwa katika misingi ya ubunifu au

kubuni au kuwaza na kufikiria kisa fulani. Mifano ya hadithi hizi ni hekaya,

hurafa, istiara na mbazi.

Aina ya pili ya hadithi ni zile za historia. Hadithi hizi huwa na misingi yake katika

matukio ya kihistoria yaliyotokea. Hadithi kama vile visasili, mighani/ visakale,

shajara, tarihi na kumbukumbu huingia katika tapo hili.

(i) Hadithi za Kubuni au Ngano

Ngano ni hadithi za kubuni ambazo huwatumia wahusika mbalimbali kusimulia

kisa fulani chenye mafunzo. Ngano huwa na vipera mbalimbali.

(a) Ngano za mazimwi /majitu

Hizi ni ngano ambazo huwa na mazimwi au majitu kama wahusika wake

wakuu. Wahusika hupewa wasifu uliowatenga na binadamu wa kawaida k.v.

kuwa na jicho moja, mguu mmoja, mikono mingi, n.k. Wahusika hawa

huwakilisha tabia mbaya katika jamii ili kutahadharisha wanajamii dhidi ya

tabia hizo. Mfano ni hadithi ya Zimwi na Msichana Mtundu katika utamaduni

wa Waswahili.
47

(b) Ngano za kishujaa

Hadithi hizi husimulia maisha, matendo na matukio yanayohusiana na shujaa

wa jamii fulani ambaye anaweza kuwa aliishi au ni wa kudhania tu. Hadithi ya

Fumo Lyongo ni mfano mzuri.

(c) Ngano za usuli

Hizi ni ngano ambazo hutoa ya asili au chanzo cha jambo au hali fulani kwa

kujaribu kujibu swali: Kwa nini hali fulani ikawa kama ilivyo?

(d) Hekaya

Hekaya ni hadithi za kijanja. Zinahusu mhusika mmoja ambaye hujifanya

rafiki kwa wengine kwa nia ya kujinufaisha mwenyewe kupitia hila na ujanja.

Hekaya za Abunuwasi ni mifano mizuri ya hadithi za hekaya.

KUMBUKA:

• Hekaya huchunguza udanganyifu na mgogoro kati ya uhalisi na


hali isiyokuwa na uhalisia.
• Hekaya huwaonya watu dhidi ya kudanganyika haraka.
• Hekaya huonyesha yanayoweza kuwapata wadanganyifu au
waongo katika jamii

(e) Hurafa

Wahusika wa hadithi hizi ni wanyama wanaowakilsha binadamu wenye sifa

za wanyama hao. Sifa hizo huhimizwa au kushutumiwa katika jamii. Hurafa

zote kwa hivyo huwa na lengo la kufundisha au kutoa maadili. Waswahili


48

wana hadithi ya Simba, Punda na Sungura ambayo ni mfano mzuri wa

hurafa.

(f) Ngano za mtanziko

Ngano hizi hutoa mtanziko au ugumu wa kuamua jambo la kuchagua. Ngano

za aina hii huishia kwa swali ambalo mtambaji huiachia hadhira kulijibu au

kulitafutia ufumbuzi.

(g) Ngano za kimafumbo

Hizi ni ngano zinazokuwa na mafumbo kwa kubeba maana nyingine ya ndani

au iliyofichika katika utambaji wake. Ngano za kimafumbo hujumlisha:

Istiara - Hadithi zenye maana fiche

Vigano - Hadithi ambazo huwa na wadhifa wa methali

Kidaizo - Kisa kifupi chenye mtu au tukio fulani lenye maana ya ziada

inayotoa maadili fulani.

(h) Ngano za kichimbakazi

Ngano hizi huwa ni sehemu ya sanaa-jaadiya na hukita kwenye matendo ya

mhusika ambaye hukumbana na masahibu mengi lakini mwishowe huishi

maisha ya raha.

(i) Soga

Hizi ni hadithi ndogo ndogo zinazohusisha utani na ucheshi kwa nia ya

kuchekesha na kukejeli na hujengwa kwenye tukio moja.


49

(j) Hadithi za kihistoria

Hadithi hizi hutumika kama njia kuu za kuwajulisha wanajamii historia yao,

asili yao na ukale wao kama nguzo muhimu ya kujitambulisha. Hadithi za

kihistoria ni za aina mbalimbali: Mifano mizuri ni hadithi za Adamu na Hawaa

katika Biblia, Gikuyu na Mumbi katika utamaduni wa Wakikuyu na Mbodze na

Matsozi katika utamaduni wa Wamijikenda.

(i) Tarihi

Hizi ni hadithi za kihistoria kuhusiana na matukio ambayo ni ya kweli na

yamewahi kutokea katika historia ya jamii husika. Tarihi hugusia matukio

ya kihistoria k.v. utamaduni, utawala, n.k.

(ii) Mighani

Mighani husimulia matendo ya mashujaa wa jamii fulani kwa kuchanganya

historia na chuku ya kifasihi; na husheheni matendo ya kiajabu ajabu,

miujiza, maajabu, uchawi, n.k. Hadithi ya Samsoni na Delaila katika Biblia

ni mfano mzuri.

(iii) Visasili

Kisasili ni hadithi inayoelezea asili au chanzo cha kitu fulani. Hadithi hizi

husimulia asili ya ulimwengu, mwenendo wake, msingi wa mtazamo na

imani za jamii, asili ya matendo au hali k.v. kifo, asili ya matukio fulani,

wasifu fulani wa kimaumbile, tabia na wasifu wa wanyama fulani,n.k.

Hadithi ya Asili ya Kifo ni mfano mwafaka wa kisasili.


50

(iv) Kumbukumbu

Hizi husimulia maelezo au matukio yanayohusishwa na jamii au mtu

fulani. Sifa zinazohusu wasifu au tawasifu huingia katika tapo hili. Hadithi

Rwanda Magere inaingia katika aina hii ya hadithi.

(v) Shajara

Ni hadithi zinazoelezea matukio au matendo ya mtu au watu fulani kwa

mujibu wa kutokea kwake. Mfano wa Kuumbwa kwa Dunia katika Biblia ni

shajara.

2.5.2 NYIMBO

Nyimbo ni tungo zenye mahadhi ya sauti inayopanda na kushuka. Nyimbo

hutumia lugha ya mkato, matumizi ya picha na mapigo ya silabi na hupangwa

kwa utaratibu au muwala wenye mapigo ya kimuziki au wizani. Nyimbo ni utanzu

muhimu sana wa fasihi simulizi. Nyimbo huwa na mawazo mazito na hunuiwa

kuonyesha uhusiano wa kijamii, mgogoro, kukejeli, kuliwaza, kubembeleza,

kutumbuiza, kuongoa na kuburudisha. Takribani shughuli zote za maisha ya

binadamu huambatanishwa na uimbaji wa nyimbo.


51

KUMBUKA:

Sifa kuu za nyimbo :


• Maneno yanayoimbwa kwa mpangilio maalum
• Hadhira inayoimbiwa
• Muktadha k.mf: sherehe, ibada, kilio, ufugaji, kuvuna, n.k.
• Ala au vyombo vya muziki
• Sauti ya mwimbaji.

2.5.2.1 Dhima ya Nyimbo

Nyimbo huwa na majukumu au dhima za jumla zifuatazo katika jamii.

(a) Kuhifadhi

Nyimbo huhifadhi matukio muhimu ya kihistoria katika jamii mbalimbali.

(b) Utamaduni

Nyimbo hutumiwa kama nyenzo muhimu ya kupitisha thamani za kitamaduni

katika jamii.

(c) Burudani

Nyimbo ni njia ya kutumbuiza na kumpatia msikilizaji na mwimbaji burudani.

(d) Ujumi

Nyimbo huonyesha ubunifu na ujumi wa tamaduni za jamii kupitia muundo

maalum, wenye uzito na lugha teule, ishara na picha nzito.


52

(e) Kuhamasisha

Nyimbo huhamasisha watu kutenda kazi au kushirikiana katika kufanya kazi.

(f) Kuelimisha

Nyimbo huelimisha na kupitisha maarifa mbalimbali miongoni mwa jamii.

(g) Fahari

Nyimbo ni kiakisi kizuri cha fahari waliyo nayo wanajamii kuhusiana na mila na

utamaduni wao.

2.5.2.2 AINA ZA NYIMBO

Kuna aina nyingi za nyimbo. Aina kuu ni kama zifuatazo:

(i) Bembezi

Nyimbo ambazo hutumiwa kuwabembeleza watoto walale. Ni nyimbo za

kuwatumbuiza na kuwaongoa watoto na huimbwa kwa sauti au mahadhi ya chini.

Mifano ni Mwana Huyu Ana Nini na Howa Howa Kibibie katika utamaduni wa

Waswahili.

(ii) Mbolezi

Hizi ni nyimbo zinazoimbwa wakati wa maombolezi au maafa na hutufichulia

mtazamo wa jamii husika kuhusiana na dhana ya kifo.

(iii) Wawe

Nyimbo za wakulima huitwa ‘wawe’. Nyimbo hizi huimbwa na wakulima


53

kuonyesha hisia kuhusiana na kazi ya kulima.

(iv) Nyimbo za kisiasa

Nyimbo hizi hutumiwa katika kuwahamasisha na kuwaleta watu pamoja kisiasa.

(v) Nyimbo za mapenzi

Nyimbo zinazoimbwa kutoa hisia za mapenzi kupitia lugha iliyojaa ufundi, umbuji

na yenye kufurahisha.

(vii) Tendi

Hizi ni tungo ndefu ambazo huimbwa na mafundi fulani wa kuimba na huwahusu

mashujaa wa jamii hasa kuzaliwa kwao, kuishi kwao, shida zao, vita na matendo

yao ya kishujaa na kufa kwao.

(viii) Nyiso

Nyiso ni nyimbo zinazohusiana na jando na unyago. Nyimbo hizi za tohara

hutumiwa kumjulisha mwanajamii matarajio ya jamii, mwelekeo na kumwingiza

katika kundi fulani la kijamii.

(ix) Ngonjera

Hizi ni tungo za kishairi zenye muundo wa mapokeo ambapo mhusika mmoja

husema jambo katika ubeti mmoja na mwingine kumjibu katika ubeti mwingine.

(x) Majigambo
54

Hizi ni nyimbo za kujisifu ambazo hutumia ufiche, tamathali na taswira nzito

katika lugha ya mhusika anayejisifu au kujigamba.

2.5.3 SEMI

Semi ni utanzu wa fasihi simulizi unaojumlisha tungo fupifupi zenye kutumia

picha, tamathali, na ishara. Semi hubeba maudhui yenye maana zinazofuatana

na vifungu vya maneno au habari zilizokamilika katika matumizi yake. Katika

utanzu huu tuna methali, vitendawili, misemo, nahau na misimu.

2.5.3.1 Methali

Methali ni misemo inayotumiwa kuelezea kitu kwa njia ya picha na kwa ufupi ili

itoe maadili au maonyo fulani. Methali mara nyingi huwa na sehemu mbili.

Sehemu ya kwanza husemwa na mshauri na ya pili hukamilishwa na mshauriwa.

Methali humwingiza msikilizaji katika hali ya kufikiri, kuchambua na kupatanisha

ukweli na hali ili ajue maana ya ndani iliyokusudiwa.

KUMBUKA:

Methali nyingi huwa:


• Ζimetumia tashbiha.
• Ni sitiari kutokana na mienendo ya binadamu.
• Ζimetumia balagha ikichanganywa na chuku.
• Zimetumia kejeli.
• Zimetumia vidokezo katika matukio halisi.

Methali hutumiwa katika:


55

Kuipamba lugha katika fasihi andishi, nyimbo, mashairi na

mazungumzo ya kawaida

Kueleza shughuli za jamii husika zinazoweza kuwepo, pale

zimefikia au kupotea kutokana na sababu mbalimbali.

Kuelezea hali ya tukio au msimamo na mahusiano baina ya jamii

mbalimbali

Kuonyesha hali halisi ya jamii mbalimbali

Kuonyesha hali halisi za maisha ya watu fulani

Kujenga kejeli na kufumba.

2.5.3.2 Vitendawili

Vitendawili ni mafumbo yanayofumbiwa watu na kuombwa kuyafumbua. Hii ni

fani muhimu sana ya kuchemsha bongo ama kuzoesha akili kutumia mantiki na

kushika kumbukumbu. Vitendawili ni aina ya sitiari ambazo hutumia na kutoa

taswira za vitu, mawazo, dhana, watu na maumbile hayo katika mazingira

maalum na kwa wakati maalum.

Mahali, wakati na namna ya kutega na kutegua kitendawili hutofautiana kutoka

jamii hadi nyingine. Vitendawili huwa na sifa ya ufupi wa maelezo ambayo

wakati mwingine huweza kuwa neno moja tu. Vitendawili hujengwa na miigo na

mifananisho na milinganisho ya maana, sauti, rangi, ukubwa na udogo.

Vitendawil vinaweza kugawanywa kati ya:

Vinavyoshughulikia uhalisia
56

Vinavyoshughulikia mimea

Vinavyoshughulikia wanyama

Vinavyoshughulikia sehemu za mwili

Vinavyoshughulikia maisha ya nyumbani

Vinavyoshughulikia vyombo vya jikoni

Vinavyohusu utamaduni wa mzungu

na kadhalika

2.5.3.3 Misemo

Misemo hutumika kutambulisha mazingira maalum au kuijulisha hadhira wakati

unaohusika katika kazi ya fasihi inayoshughulikiwa. Misemo huzuka na

kutoweka kutokana na hali mbalimbali za kimazingira. Maneno hutumika kama

yalivyo katika mazingira maalum kuleta maana maluum.

2.5.3.4 Misimu

Haya ni maneno au misemo ambayo huzuka ghafla katika misimu au wakati

fulani hasa kutokana na mambo au matukio maalum ya msimu au wakati huo.

Misimu ni semi au maneno ya kitamathali ambayo huzuka na kufa ghafla.

2.5.3.5 Nahau

Nahau ni misemo iliyojengwa kwa kutumia maneno ya kawaida lakini huwa

imesetiri maana tofauti iliyobebwa na maneno hayo katika hali ya kawaida.

Nahau huwa na matumizi sawa na misemo lakini huwa zimeshika mizizi zaidi
57

katika jamii na hadhira yake ni pana zaidi. Nahau hutumiwa na wasanii wa fasihi

kutajirisha maelezo yao na kutoa picha halisi ya hali fulani.

2.5.4 SANAA ZA MAIGIZO

Sanaa za maigizo ni mpangilio wa maneno ambayo huambatana na utendaji au

uigizaji wa wahusika. Fasihi simulizi hutumia sanaa za maigizo katika kukejeli,

kudhihaki, kukosoa au hata kuburudisha. Uigizaji hautegemei sauti tu bali pia

maleba na mapiku pamoja na matendo yasiyoandamana na sauti kama ilivyo na

uigizaji bubu.

Katika fasihi simulizi, uigizaji hujumlisha vitengo kama vile michezo (ya watoto),

majigambo, vichekesho, ngonjera na mazungumzo.

2.6.0 UTAFITI KATIKA FASIHI SIMULIZI

? Je, utafiti wa fasihi simulizi unahusisha nini?

Utafiti hufanywa kwa nia ya kutalii na kufanya uchambuzi fulani. Kuna haja ya

kukusanya data kuhusiana na fasihi simulizi ili kuihifadhi fasihi hiyo.

Utafiti wa fasihi simulizi utasaidia kuelewa mtazamo wa jamii kuhusu


ulimwengu.
Utafiti wa aina hii husaidia mwanafunzi kukuza na kupevusha stadi za
utafiti ili azitumie katika masomo na shughuli nyingine.
Mtafiti wa fasihi simulizi huweza kujihusisha na fasihi hii na kuweza
kuielewa kwa kina kupitia kuisikia, kuihisi na kushiriki katika shughuli
nzima.
Kuna maswala mengi ambayo hayajafanyiwa utafiti katika fasihi
58

simulizi na kuyatafitia kutahakikisha kuwa amali na thamani hizo

muhimu hazipotei.

Pana umuhimu wa kufanya utafiti ili kuhakikisha historia, imani na

itikadi, taaluma, vito na vipengele muhimu vya fasihi zetu

vimehifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.

2.6.1 Hatua za Utafiti

Kila utafiti huwa na hatua ambazo hufuatwa. Hatua hizi humwezesha mtafiti

kufikia malengo yake na kupata data anayohitaji kwa njia ifaayo.

(a) Maandalizi

Maandalizi hufuata utaratibu maalum. Mtafiti abainishe lengo na mipaka ya

utafiti wake. Atambue mahali pa utafiti na kutafuta utafiti mwingine uliowahi

kufanywa kuhusu mada yake. Abainishe muda na wakati wa kufanya utafiti.

Aone kwamba ana watu wa kutegemewa. Abainishe mbinu za utafiti. Afanye

makadirio ya gharama ya utafiti na kuhakikisha amepata vitu vyote

atakavyohitaji katika utafiti mzima.

(b) Uteuzi wa sampuli

Sampuli ni kundi la wahojiwa wanaoteuliwa ili kuwa kiwakilishi cha jamii pana

katika eneo fulani. Inachukuliwa kuwa majibu yanayotokana na wajibu wa hao

yanawakilisha jamii pana husika. Uteuzi wa sampuli unaweza kuwa wa:

Kubahatisha
59

Kimfumo

Mtabakisho

Makundi kihatua

Kimakusudi

Welekeo urari na ukubwa

Makundi

(c) Ukusanyaji wa data

Ukusanyaji wa data hufanyika kwa kutumia njia mbalimbali za uchunguzi, hojaji,

mahojiano pamoja na kushiriki katika utendaji.

(d) Kurekodi maarifa/maelezo

Huku ni kurekodi maarifa, data au maelezo anayotamani kuandika, kunasa kwa

vyombo mbalimbali, n.k.

(e) Uchambuzi wa data

Uchambuzi unahusu kupanga na kuainisha data iliyokusanywa kwenye tanzu na

vipera mbalimbali kutegemea misingi fulani. Aidha, ni kutambua dhamira, motifu,

mbinu kuu na hata majukumu ya tanzu au vipera hivyo. Mwisho, ni kufasiri

maelezo na data iliyokusanywa na kufanya maamuzi ya kuhitimisha utafiti wako.

Mbinu na vifaa vinavyosaidia kukusanya data ni pamoja na:

Hojaji

Mahojiano
60

Uchunguzi

Maandishi

Kinasa sauti
Video, n.k.

2.7.0 FASIHI SIMULIZI SASA

Fasihi simulizi imekumbwa na matatizo mengi katika jamii za kisasa. Matatizo

hayo yanatokana na hali mbalimbali katika maisha ya sasa:

Ukosefu wa utafiti wa kutosha wa baadhi ya tanzu za fasihi simulizi

ambazo baada ya muda huenda zikasahaulika.

Kuadimika kwa wataalam wa kutosha wa fasihi simulizi.

Ukuaji wa fasihi andishi ambayo inatwaa nafasi ya fasihi simulizi

Uwezekano wa waliosoma kuathiriwa na fasihi andishi kiasi cha

kuathiri na hata kubadilisha fasihi simulizi.

Fasihi simulizi kupuuzwa na taasisi na mifumo ya elimu inayotilia

mkazo fasihi andishi.

Kusambaa kwa lugha za kigeni zinazotishia kuua lugha za kienyeji

pamoja na utamaduni wa fasihi simulizi.

Katika kuhakikisha kuwa fasihi simulizi imebakia hai na kuwepo katika siku zijazo

tunahitaji:

Kuona kwamba fasihi simulizi inaanza kufundishwa katika viwango

mbalimbali vya elimu.

Kuhimiza wasomi kujihusisha na utafiti wa fasihi simulizi ili kuyapamba

maarifa kuhusiana na fasihi hiyo.


61

Kuhakikisha fasihi simulizi imepewa nafasi inayostahiki katika

tamaduni na sera za kitaifa.

Kuhimiza utafiti na machapisho yanayohusiana na fasihi simulizi za

jamii mbalimbali.

2.8.0 MUHTASARI:

Katika somo hili, tumeshughulikia fasihi simulizi kama utanzu


mmojawapo wa taaluma ya fasihi. Kupitia somo hili, tumeweza kuelezea
maana ya
fasihi simulizi na tofauti baina ya fasihi hiyo na fasihi andishi. Tumeona
pia nafasi ya fasihi hii katika jamii katika kudhibiti itikadi, historia, falsafa
na utamaduni wa jamii. Fasihi hii inasaidia katika kutoa mafunzo pamoja
na kufurahisha na kuburudisha. Fasihi simulizi vile vile huendeleza na
kukuza lugha. Kwa jumla, fasihi simulizi humsaidia mtu kukua kimawazo,
kitabia na kilugha, hasa kupitia tanzu mbalimbali ambazo tumejadili katika
somo hili. Somo linalofuata linashughulikia utanzu wa riwaya.

2.9.0 ZOEZI:

1. Kwa kutoa mifano, eleza maana na majukumu ya fasihi simulizi katika


jamii.
2. Onyesha namna fasihi simulizi inavyolingana na kutofautiana na fasihi
andishi.
3. Kupitia mifano kutoka katika jamii yako, ainisha tanzu za fasihi simulizi.
4. Utafiti ni nini? Chagua utanzu mmoja wa fasihi simulizi na uufanyie
utafiti katika jamii yako. Kumbuka kufuata hatua zote za utafiti.
5. Ni matatizo gani yanayoikumba fasihi simulizi na tunaweza
kukabilianaje na matatizo hayo?
62

2.11.0 MAREJELEO TEULE

1. Balisidya, M.L. (1987): ‘Tanzu na Fani za Fasihi simulizi’ katika Mulika

Na 16. Dar es Salaam: T.U.K.I.

2. Njogu, K. & Chimerah, R. (1999): Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na

Mbinu Nairobi: J.K.F.

3. Mazrui, A.M. & Syambo, B.K. (1992): Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi:

E.A.E.P.

4. Sengo,T.S.Y. (1987): Fasihi Simulizi: Sekondari na Vyuo Dar-es-

Salaam Nyanza Publications Agency.

5. Wamitila, K.W. (2003): Kichocheo cha Fasihi: Simulizi na Andishi.

Nairobi: Focus Books Ltd.


63

SOMO LA TATU

RIWAYA

3.0 UTANGULIZI

Somo hili linahusu riwaya kama utanzu wa fasihi andishi. Riwaya ni utanzu

uliotokana na masimulizi ya kale ya ngano na hadithi. Baada ya kubuniwa kwa

hati za kimaandishi hadithi zilianza kuandikwa na kuitwa riwaya. Somo hili

linaangalia riwaya ya Kiswahili. Katika somo kuna maelezo ya maana, historia

na maendeleo ya riwaya ya Kiswahili. Aidha, somo hili linatoa aina za riwaya na

namna za kuchambua na kuhakiki maandishi ya kinathari au riwaya.

3.1.0 MALENGO

Kufikia mwisho wa somo hili, utakuwa:

1. Umefahamu maana ya riwaya.

2. Umejua historia na maendeleo ya riwaya ya Kiswahili

3. Umetambua aina mbalimbali za riwaya

5. Umeelewa jinsi mbalimbali za kuhakiki na kuchambua riwaya.

3.2.0 MAANA YA RIWAYA

? Riwaya ni nini.
64

Neno riwaya lina asili ya lugha ya Kiarabu na lina maana ya hadithi au umbo

fulani la hadithi. Katika Kiswahili tumelichukua neno hilo kwa maana ya hadithi

yenye fani na umbo mahususi. Hata hivyo, maana ya riwaya ina utata wake.

Sababu ni kwamba tunahitaji kuwa na vigezo mahsusi vya kutuwezesha kuamua

ni ipi riwaya na ipi si riwaya. Kutokana na hali hiyo, kuna maana mbalimbali

zilizotolewa kuelezea dhana ya riwaya.

Riwaya ni hadithi au kisa kirefu kilichoandikwa kinathari. Ni maandishi ya nathari

yanayosimulia hadithi ya kubuni ambayo kwa kawaida huwa ina uzito, upana na

urefu wa kisa, yenye wahusika wa aina mbalimbali. Riwaya huwa na mtiririko

wenye visehemu vingi au wenye migogoro midogo ndani yake na uchoraji (au

usawiri) wa wahusika kwa undani zaidi kuliko hadithi au hadithi fupi.

Riwaya ni kisa changamano kinachoweza kuchambuliwa au kuhakikiwa kwa

uzito na undani kwa kuzingatia mambo mbalimbali, kama vile maudhui, dhamira,

mtindo, wahusika na mtindo.

Riwaya ni kisa ambacho urefu wake unakiruhusu kutamba na

kutambaa mahali pengi na kuambaa vizingiti vingi kwa utashi wa

mwandishi wake.

Riwaya ni kisa cha kutosha, chenye zaidi ya tukio moja.

Riwaya ni hadithi ndefu ya kubuni, yenye visa vingi, wahusika zaidi ya

mmoja na yenye mazungumzo na maelezo yanayozingatia kwa undani

na mapana, maisha ya jamii.


65

Riwaya ni hadithi inayoweza kuanzia maneno 35,000 kuendelea. Si

urefu tu; riwaya huwa na uchangamano wa matukio, ujenzi wa

wahusika na dhamira, miundo na hata mtindo wake maalum.

Riwaya ni masimulizi ya visa vilivyotiririshwa kufuatana na wakati wake

- chakula cha jioni baada ya chamsha kinywa, Jumanne baada ya

Jumatatu, kuoza baada ya kufa - inahitajika kumfanya msomaji awe na

hamu ya kujua litakalotokea baadaye au linalofuata.

Riwaya ni kisa cha kubuni kilichoandikwa kinathari.

Maelezo hayo ya dhana ya riwaya yanaelekea kutilia maanani vipengele kadha:

• Urefu

• Mchangamano au Uchangamano

• Wingi na mwingiliano wa vitushi

• Wahusika wengi waliosawiriwa kwa undani

• Dhamira na maudhui mengi

• Upana au mawanda

Kupitia maelezo hayo, tunaona kuwa riwaya inatumia nyenzo au mtindo wa

uandishi. Kwa hivyo, mtindo wa riwaya unapatikana katika jamii yenye ujuzi wa

kusoma na kuandika kama njia ya kuihifadhi na kuiwasilisha.

Riwaya ya Kiswahili si kongwe sana wala si ya asili ya Afrika Mashariki. Ni

uwanja mgeni na vitengo na vigezo vyake vingi ni vya kigeni.


66

ZINGATIA:

Kutokana na maelezo yaliyotolewa na wahakiki na waandishi


mbalimbali: • Riwaya ni masimulizi yaliyojengwa katika misingi ya uyakinifu
yenye visa
changamano.
• Riwaya hujijengea usadikifu wa kipekee unaotokana na mfuatano mahususi wa
visa vilivyopangwa kiwakati.
• Riwaya huwa na dhamira, maudhui na mtindo unaobainika na huzingatia
uhalisia.
• Riwaya huwa na masimulizi yaliyoendelezwa kimantiki na yanayofahamika na
kukubalika kibinadamu.

3.2.1 Sifa za Riwaya

Kutokana na ufafanuzi uliotolewa wa dhana ya riwaya tunaweza kusema kuna

sifa zifuatazo za utanzu huu:

• Katika riwaya, kuna nafasi ya kujadili na kuhusisha maswala mengi zaidi

ya kijamii na kihistoria (urefu, uketo na upana)

• Riwaya hutoa nafasi ya kukuza wahusika kwa undani zaidi kwa

mwandishi. Kuna nafasi ya uchaguzi na ya kueleza mandhari au

mazingira ili yadhihirike vyema zaidi na wahusika kufahamika kwa

ukamilifu zaidi.

• Riwaya huwa na maudhui mengi na dhamira pana zaidi. Aghalabu

maudhui hayo hutatiza wakati mwingine lakini yanahusiana.

• Riwaya huwa na aina tofauti tofauti za wahusika. Kuna wahusika nguli na

/ au wakinzani na wahusika wengine kama vile bapa na duara.

• Katika riwaya, kuna uwezekano wa kumfahamu nguli au


67

mhusika/wahusika wakuu vyema zaidi kwa kuzingatia maisha yao kama

yanavyochorwa na mwandishi. Kwa sababu hii, tunaweza kuifahamu kwa

urahisi na kwa undani zaidi jamii ya mwandishi au ya hadithini.

• Riwaya huwa na migogoro na migongano mingi inayofuatana, kuhusiana

na kutokea kwa pamoja.

• Ploti au mtiririko wa vitushi katika riwaya huwa umefumwa au kuundwa

kwa njia ya uchangamano ukielekea upeo mmoja lakini uliojengeka kwa

vipeo vingine vidogo vidogo.

• Katika riwaya , ploti kuu huwa na viploti au vitushi vya aina aina ambavyo

huchangia mkondo na maendeleo ya hadithi. Hii ni kumaanisha riwaya

huwa na visa vingine vingi nje ya kisa kikuu ambavyo husaidia kukuza

kisa au hadithi kuu.

• Maendeleo au mkondo wa riwaya hubainisha mabadiliko mengi

yanayotuwezesha kufahamikiwa au kupata uvumbuzi wa aina mbalimbali

ya maswala na jamii anayosawiri mwandishi.

• Mfuatano wa visa ndio msingi au uti wa mgongo wa riwaya na ndiyo sifa

ya asili ya ngano, riwaya, n.k.

KUMBUKA:

• Μwandishi wa riwaya huweza kujenga, kukuza na kuumba wahusika


wake kwa
ukamilifu wakawa wa kuvuta mapenzi au chuki ya wasomaji
kinafsia, kiakili na kimwili.
• Riwaya inaweza kutumia muundo au mtazamo wowote wenye mchangamano
wa akili ya mwandishi mwenyewe.
• Κukawiza vituko na kujenga ngazi za vipeo mwishoni, kati na mwanzoni
mwa riwaya husaidia kujenga muundo na kuainisha mtindo wa mwandishi.
68

3.3.0 CHIMBUKO LA RIWAYA

Riwaya imetokana na utunzi wa hadithi. Asili ya riwaya imo katika uelemeo wa

uandishi. Riwaya za kwanza ulimwenguni zimejengwa na kubuniwa kwa hati ya

maandishi. Riwaya ilizuka kutokana na maendeleo ya usomaji yaliyofanya

riwaya nyingi ziandikwe.

Uchangamano wa maisha ya jamii kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi ulizusha

haja ya kuwa na utanzu wa kifasihi ulio na uchangamano kifani na kimaudhui.

Katika bara Ulaya, wanasanaa walipata wasomaji hasa wanawake waliobaki

nyumbani wanaume walipoenda kufanya kazi viwandani. Wanawake wakawa na

wakati wa kusoma maandiko marefu. Miongoni mwa riwaya za mwanzo ni

Robinson Crusoe iliyoandikwa na Daniel Defoe. Mwandishi Charles Dickens pia

alitoa riwaya kadhaa.

Kuzuka kwa riwaya kulifungamana na kuzuka kwa ubepari ambao ulizaa miji na

viwanda. Mapinduzi ya viwanda yalikuja na ugunduzi wa mitambo ya kupiga

chapa ambapo maandiko marefu yaliweza kuchapwa na nakala nyingi kutolewa

kwa haraka.

Katika Kiswahli, riwaya ni utanzu mgeni. Umbo hili limekuja pamoja na hati
tulizorithi kutoka kwa mataifa yaliyotutawala. Historia ya fasihi ya Kiswahili
inaelekea kuonyesha kuwa utanzu wa riwaya na ule wa ushairi zilikuwa pamoja
kwa muda mrefu. Mgawanyo umeanza kuonekana baada ya Wajerumani
kufundisha hati za Kirumi. Riwaya za awali za Kiswahili zinaonyesha maendeleo
mazuri katika kukua kwake.
69

Riwaya ya Kiswahili hivi sasa imepiga hatua kubwa kifani na kimaudhui kuliko

hata ile ya watangulizi wake. Mwandishi wa riwaya ya Kiswahili ameiona jamii

ikibadilika katika mila, desturi na mienendo kutokana na hali na nguvu mpya za

kiuchumi na kimaendeleo, na ameandika juu yake.

3.4.0 AINA ZA RIWAYA

Riwaya zipo za aina mbalimbali kutegemea ufundi, lengo na makusudio ya

mwandishi. Ijapokuwa riwaya hudhihirisha tofauti za kimtindo, kimaudhui,

kiitikadi na kidhamira, tunaweza kubainisha kwa jumla aina au mikondo kadha

katika utanzu wa riwaya.

3.4.1 Riwaya za Kijazanda

Wakati mwingine aina hizi za riwaya huitwa riwaya za kimajazi au riwaya za

kimafumbo. Katika aina hii ya riwaya, mwandishi hutumia majazi mara nyingi

anapotaka kufundisha maadili. Majina ya mahali na wahusika hutumiwa

kuwakilisha sifa fulani pamoja na imani ya mwandishi.

Mafumbo hutumika wakati mwandishi anataka kuuficha ujumbe au dhamira yake

hasa iwapo ujumbe huo unaweza kumletea balaa au kumtia hatarini. Mojawapo

ya riwaya zinazoingia katika tapo hili ni Mafuta (K.Mkangi).


70

3.4.2 Riwaya za Upelelezi

Hizi ni riwaya zilizoathiriwa na riwaya za kigeni katika Kiswahili. Riwaya hizi

hazikuzalika katika mazingira ya Kiswahili au Kiafrika. Hata hivyo, aina hii ya

riwaya inaendeleza maadili fulani ya kijamii na kibinadamu. Riwaya ya upelelezi

hutumia sadfa na taharuki. Katika riwaya hizo, usadikifu haupo au ni mdogo

sana. Wahusika wengi wanasawiriwa kama wajinga isipokuwa mhusika mkuu

ambaye ni mpelelezi.

Katika fasihi ya Kiswahili, mwandishi anayesifika sana wa hadithi za upelelezi ni

Mohamed Said Abdulla (au Bw Msa kama anavyojiita katika riwaya zake).

Inadaiwa mwandishi huyu ameathiriwa na mwandishi wa Kingereza Arthur

Canon Doyle ambapo wahusika Bw Msa na Najun wa M.S. Abdulla wanafanana

sana na Sharlock Holmes na Dr. Watson wa Doyle. Baadhi ya riwaya za M.S.

Abdulla ni Kisima cha Giningi, Mzimu wa Watu wa Kale na Duniani Kuna Watu.

3.4.3 Riwaya za Kihalisia

Riwaya za aina hii huzungumzia maisha ya binadamu katika hali na mazingira ya

kuaminika. Riwaya hizi huonyesha jinsi binadamu anavyoathiriwa na

kufinyangwa na mazingira yake. Aina hizi huitwa pia riwaya za kisaikolojia kwani

zinasawiri misukumo inayofanya wahusika watende mambo fulani. Katika riwaya

kama hizi, dhana ya usimulizi, usawiri wa wahusika na uchangamano ni muhimu

sana. Mafunzo yanatokana na maisha ya wahusika wala siyo matamshi ya

mwandishi kama ilivyo na riwaya za kimajazi. Mifano ya riwaya hizi katika fasihi

ya Kiswahili ni Mali ya Maskini (Z.Burhani) na Lwindiko (M.M.Mvungi).


71

3.4.4 Riwaya za Uhalisia wa Kijamaa

Hizi ni riwaya zinazoonyesha matukio na wahusika katika misingi ya uhalisi wa

kijamaa. Katika riwaya hizi waandishi wake wanazingatia itikadi ya ujamaa na

kudhihirisha wahusika kitabaka. Riwaya hizo husawiri mitafaruku na mikinzano

ya kijamii kama inayosababishwa na tofauti za kitabaka zinazoletwa na mfumo

wa kiuchumi wa kibepari au kimwinyi.

Riwaya za uhalisia wa kijamaa zinapendekeza kwa njia ya moja kwa moja au

kwa vidokezo ukombozi wa wachochole dhidi ya dhuluma na uonevu na

zinalenga ujenzi wa jamii mpya ambamo kila mtu atanufaika na juhudi za jasho

lake. Baadhi ya riwaya za aina hii katika Kiswahili ni Dunia Mti Mkavu na Kiza

Katika Nuru (S.A. Mohamed), Mafuta na Walenisi (K. Mkangi) na Kasri ya Mwinyi

Fuad (S.A. Shafi).

3.4.5 Riwaya za Kitamaushi/Kidhanaishi

Riwaya hizi pia huitwa riwaya za kifalsafa kwani zinasaili maisha kwa jicho au

mtazamo wa kifalsafa. Katika riwaya hizi, hakuna chochote kinachopewa nafasi

ya kuchanua. Zinazusha maswala kama maana ya maisha na kuonyesha

kwamba maisha hayana maana.

Katika riwaya hizo, waandishi huonyesha fadhaa, ubinafsi, kutokuwa na imani au


kutamauka na kukengeuka kwa jumla. Mwandishi mashuhuri anayezingatia
mtazamo huu katika Kiswahili ni Euphrase Kezilahabi katika takribani riwaya
zake zote. Riwaya hizo ni kama Kichwa Maji, Dunia Uwanja wa Fujo na Rosa
Mistika.
72

3.4.5 Riwaya za Tawasifu na Wasifu

Wasifu ni maandishi ambapo mwandishi husimulia maisha ya mtu mwingine. Na

tawasifu ni pale ambapo mwandishi anaandika juu ya maisha yake mwenyewe.

Katika riwaya za aina hii, waandishi hutumia masimulizi ya nafsi ya kwanza

mara nyingi. Mfano wa wasifu ni Wasifu wa Siti Binti Saad (S. Robert) na

tawasifu ni Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini na mwandishi huyo huyo.

KUMBUKA:

Ili kubainisha riwaya fulani ni ya aina gani, msomaji huongozwa na:


• Dhamira na maudhui
• Ujumbe
• Falsafa
• Wahusika na usawiri wake
• Mandhari
• Muundo na mtindo
• Ukweli na uhalisia
• Hukumu ya kitathmini
• Nafsi ya usimulizi

ZOEZI:

Jaribu kusoma aina mbalimbali za riwaya za Kiswahili huku ukitoa sifa


za kila aina.

3.5.0 UCHAMBUZI WA RIWAYA

Katika uchambuzi au uhakiki wa riwaya tunaongozwa na vipengele mbalimbali

vinavyojenga hadithi. Vijenzi hivyo humwelekeza mhakiki katika kutathmini na

kuitolea kauli riwaya aliyoisoma. Katika sehemu hii tutaangalia baadhi ya


73

maswala ambayo husaidia katika uchambuzi wa riwaya.

KUMBUKA:

Uchambuzi au uhakiki wa fasihi hutegemea ujuzi na tajriba ya mhakiki.


Kwa hivyo, hatuna kauli ya mwisho kuhusiana na kazi yoyote ya kifasihi na kazi
moja inaweza kuwa na tahakiki tofauti tofauti.

3.5.1 Muundo wa Riwaya

Riwaya inakamatisha vipengele kadha kwa wakati mmoja. Vipengele hivyo ni

kama vile ploti, hadithi, saikolojia, falsafa na mazungumzo. Riwaya huwa na

masimulizi kwa mujibu wa hadithi inayotokea kiwakati na kimasafa. Riwaya pia

huwa na wahusika wanoingiza wasifu wao, mavazi yao, mchukuo wao, tabia zao

katika sifa na ila zao. Mambo haya yote husaidia katika kupata malengo na

maudhui ya mwandihsi katika riwaya.

3.5.2 Hadithi au Ploti

Katika kipengele hiki, tunaangalia muhtasari wa riwaya kwa kuchunguza mtiririko

wa vitushi. Kupitia hadithi, tunapata kile ambacho riwaya inazungumzia.

Ujumbe huo hupatikana na jinsi visa na matukio yalivyojengwa hadithini. Hali hii

huambatana na uchunguzi, mpangilio na ufundi wa kusimulia matukio

yaliyoungwa vyema. Hadithi au ploti huipatia kazi ya fasihi urembo wa kifani na

umoja wake.
74

3.5.3 Usimulizi

Katika usimulizi, riwaya husheheni mambo mbalimbali. Kwanza ni matumizi ya

nafsi. Mwandishi anaweza akatumia ama nafsi ya kwanza, ya pili au hata ya

tatu. Jambo lingine ni maelezo au masimulizi ya mtunzi ambapo anaelezea

mandhari, mazingira na wahusika kwa maneno yake mwenyewe.

Katika kipengele cha usimulizi, tuna mazungumzo ya wahusika ambayo

hufafanua zaidi tabia na hulka za wahusika hao. Kuna vile vile mjadala au

uzungumzi nafsia ambapo mhusika huweza kuzungumza na kuwasiliana na nafsi

yake mwenyewe. Vipengele hivi hujenga riwaya na kuipatia umbo

linalojitosheleza.

3.5.4 Ukweli (Uhalisia) na Fantasia

Riwaya inafungamana na ukweli ingawa pia huhusiana na ndoto na fantasia.

Katika uhalisia, kuna uwiano wa yale yanayotokea katika riwaya na yanayotokea

nje katika maisha ya kila siku - mambo yanayosadikika na kuelezeka - bila

miujiza na mazigazi ndani yake. Wakati mwingine katika riwaya mnakuwa na

mashetani, majini, madudu, na malaika, hata wababe wenye nguvu za kiajabu.

3.5.5 Wakati

Riwaya hutokea baina ya ncha mbili za wakati - mwanzo na mwisho na baina

yake panaweza kuwa na muda unaohusishwa na dakika, saa, siku, miezi, miaka,

mikaka na hata karne. Kigezo cha wakati husaidia kuiweka riwaya katika

mkabala na muktadha fulani wa kiuchambuzi.


75

3.5.6 Mazingira

Mazingira ni mandhari au mahali ambapo hadithi inatokea au matendo au vituko

vinapotokea. Katika upana wake, inaweza ikachukua dunia, nchi, jiji, mji, kijiji,

kitongoji na hata ndani ya nyumba. Katika mazingira, tunaelewa maisha ya

wahusika na athari yake katika mielekeo na falsafa zao.

3.5.6 Saikolojia

Wahusika na matendo yao huhusu mambo ya akili, roho na hisia zao. Mambo

haya yanazingatiwa chini ya kipengele cha saikolojia. Kuna saikolojia za aina

nyingi. Kwa mfano, kuna saikolojia za kidini, ubaguzi wa rangi, wanaotawala,

saikolojia ya kukataa na kupinga unyonge na udhaifu, n.k. Saikolojia husaidia

kufafanua tabia na hulka za wahusika na nafasi yake katika kufanikisha dhamira

kuu ya mwandishi.

3.6.0 MUHTASARI:

Somo hili limeshughulikia utanzu wa riwaya kama mmojawapo wa tanzu


za nathari za fasihi. Viungo vya riwaya kama vile mandhari, maudhui, wahusika,
msuko, n.k. na namna viungo hivi vinavyojengwa, kujitokeza na kutumika katika
uchambuzi na uelewaji wa riwaya vimeonyeshwa. Katika somo linalofuata,
tutaangalia utanzu mwingine wa nathari ambao ni hadithi fupi.
76

3.7.0 ZOEZI:

1. Riwaya ni nini? Eleza kwa tafsili historia na maendeleo ya riwaya


ya
Kiswahili.
2. Utanzu wa riwaya ni mgeni katika utamaduni wa Waafrika. Jadili.
3. Kwa kutoa mifano mwafaka, ainisha riwaya za Kiswahili.
4. Onyesha vipengele muhimu vya kuchambulia riwaya na uelezee ufaafu
wa kila kipengele katika kuelewa riwaya ya Kiswahili.
5. Eleza sifa kuu za riwaya na kuonyesha udhaifu wa kila sifa.

3.8 MAREJELEO TEULE

1. Njogu, K. & Chimerah, R. . (1999): Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia

na Mbinu Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

2. Hawthorn, J. (1997): Studying the Novel London: Edward Arnold.

3. Mohamed, S.A. (1995): Kunga za Nathari ya Kiswahili Nairobi: E.A.E.P.

4. Msokile, M. (1993): Misingi ya Uhakiki wa Fasihi Nairobi: E.A.E.P.

5. Senkoro, F.E.M.K. (1982): Fasihi Dar es Salaam: Press and Publicity

Centre.

6. Wamitila, K.W. (2002): Uhakiki wa fasihi: Misingi na Vipengele Vyake

Nairobi: Phoenix Publishers Ltd.


77

SOMO LA NNE

HADITHI FUPI

4.0 UTANGULIZI

Hadithi fupi ni utanzu ulioanza baada ya ushairi na nyimbo katika wakati maalum

wa historia ya jamii. Somo hili linashughulika na utanzu wa hadithi fupi. Katika

somo hili, maana ya hadithi fupi imetolewa. Kisha, kuna sifa za hadithi fupi na

mwisho, ni uchambuzi wa hadithi fupi.

4.1.0 MALENGO

Kufikia mwisho wa somo hili, utaweza kufahamu:


1. Dhana ya hadithi fupi.
2. Sifa kuu za hadithi fupi.
3. Jinsi za kuchambua hadithi fupi.

4.2.0 MAANA YA HADITHI FUPI

? Toa maana ya hadithi fupi.

Hadithi fupi inaweza kuelezewa kama hadithi inayojifunga kwa idadi ndogo ya

wahusika na tukio fulani maalum, isiyoonyesha mabadiliko ya sehemu na wakati

wa matukio (mandhari) kwa upana na isiyojiingiza kwenye undani wa wahusika.

Hadithi fupi husomeka kwa kipindi kifupi sana.


78

4.2.1 Asili na Maendeleo ya Hadithi Fupi

Ngano zimekuwa na athari kubwa katika ulimwengu wa fasihi andishi. Binadamu

alipopiga hatua za kimaendeleo na kuvumbua hati za uandishi, ngano zilianza

kuhifadhiwa kimaandishi. Pole pole ngano hizo zikaanza kubadilika kimtindo na

kimuundo na kuwa hadithi fupi. Katika Kiswahili, hadithi fupi za mwanzo

hazikuhusiana na Waafrika wala utamaduni wao. Mfano ni hadithi za Hekaya za

Abunuasi na Alfu Lela Ulela ambazo zilikuwa na asili ya Kiarabu.

Baadaye, ilibidi waandishi kuibuka na hadithi ambazo zilikuwa na wahusika,

mazingira na matukio yanayoakisi maisha ya Waafrika. Fasihi ya maana ni

lazima iweze kuelezea maudhui yanayohusisha utamaduni, imani, mazingira na

saikolojia ya jamii husika. Jambo hili halikuzingatiwa wala kuendelezwa na

hadithi fupi za kigeni. Baadhi ya hadithi fupi zilizoandikwa na Waafrika kufuatana

na misingi ya historia na utamaduni wa Mwafrika ni Kicheko cha Ushindi (M.S.

Mohamed), Si Shetani Si Wazimu (S.A. Mohamed) na Pendo La Heba (G.

King’ei & R. Wafula).

4.3.0 SIFA ZA HADITHI FUPI

Hadithi fupi hutofautiana kadri walivyo tofauti waandishi wake. Hata hivyo, kuna

sifa fulani zinazohusishwa na utanzu huu ambazo tunaweza kuzitambulisha.


79

4.3.1 Wakati

Hadithi fupi huhusisha kipindi kifupi kiwakati. Kutokana na ufupi wa muda na

upana wake, mwandishi wa hadithi fupi hana wakati wa kueleza mambo,

matukio, wahusika na migogoro kwa kina.

4.3.2 Ufupi

Ufupi wa utanzu wa hadithi fupi unaathiri uteuzi wa mwandishi wa mbinu za

uandishi, uwasilishaji wake pamoja na athari nzima ya uandishi wenyewe kwa

wasomaji.

4.3.3 Wahusika

Hadithi fupi huwa na idadi ndogo ya wahusika. Hadithi hizo hujifunga katika tukio

moja tu. Ili kulikuza tukio au tendo hilo, wahusika huwa wachache. Kuwepo kwa

wahusika wengi huhitaji muda, kipindi na wakati wa kuwakuza, kuwaendeleza,

n.k.; wakati ambao mwandishi wa hadithi fupi hana. Wahusika hao hupewa sifa

za kijumla na hutokana na jadi ya kimaadili ambapo wahusika hugawanywa

katika makundi mawili: wahusiska wema na wahusika waovu au wabaya.

4.3.4 Mandhari

Mandhari katika hadithi fupi hayapewi nafasi kubwa na wakati mwingine,

hatuelezwi kabisa kuhusu mandhari ya hadithi hiyo. Aghalabu matukio ya hadithi

fupi hutokea mahali pamoja tu. Hayahusishi sehemu nyingi kwa sababu

msisitizo huwa kwenye tendo wala sio mahali.


80

4.3.5 Usimulizi

Hadithi fupi huwa na usimulizi sahili kwa kuwepo kwa msimulizi mmoja au

mhusika mmoja anayetumiwa na mwandishi kama jicho la kuangalia na kupima

yanayotendeka.

4.3.6 Mgogoro

Mgogoro katika hadithi fupi hukuzwa mapema na kwa njia ya wazi. Mvutano

huwa baina ya mhusika mmoja na mwingine hivyo kuzua mgogoro unaotutia

hamu ya kusoma ili tujue ni nani atakayefanikiwa.

4.3.7 Upeo

Hadithi fupi huanza karibu na upeo wa hadithi. Mwandishi hana nafasi wala

uhuru wa kutoa maelezo ya kujenga matukio hadi kufikia kwenye kilele. Mwisho

wa hadithi fupi pia huwa na mkokotezo na msisitizo fulani.

4.3.8 Ufunguzi

Mwandihsi wa hadithi fupi hana wakati wa kutoa maelezo mengi ya ufunguzi

yanayouweka msingi wa matukio, wahusika au mandhari.

4.3.9 Mvuto

Msukumo mkubwa katika hadithi fupi uko kwenye jinsi hadithi itakavyokwisha.

Lazima mwandishi amvute msomaji katika kujua litakalotokea hadi mwisho wa

hadithi. Hadithi nzuri humteka msomaji mpaka mwisho atakapoona ufumbuzi au


81

usuluhishi wa tatizo kuu.

4.3.10 Uelekezaji

Mwandishi wa hadithi fupi husimulia na kutoa maelezo yake kwa njia ya

uelekezaji kuliko uelezaji wa moja kwa moja. Mwandishi huwa na muda mfupi

kwa hivyo inambidi kuacha baadhi ya mambo bila kuyasema wazi wazi.

4.3.11 Usomwaji

Hadithi fupi huweza kusomwa katika kikao kimoja na kwa muda mfupi. Msomaji

hatakiwi kutua kwa muda mrefu ili aweze kutafakari anayoyasoma.

4.3.12 Mawazo

Badala ya kuonyesha wahusika wakiendelea na kukua kimawazo, hadithi fupi

huwaonyesha wahusika katika kipindi fulani tu cha mvutano, uwe wa nje au wa

ndani.

4.3.13 Ukamilifu

Ingawa wahusika wa hadithi fupi hawakuendelezwa, mwandishi huwasilisha

wahusika hao kwa njia ambayo wanaonekana kama wamekuzwa na

kukamilishwa. Hata kama tunawaona kwa kipindi kifupi, tunahisi kuwa wahusika

hao wamekamilika kabisa.

4.3.14 Msuko

Msuko wa hadithi fupi ni sahili, sio changamano. Matukio yake huwa ya

mfululizo wa moja kwa moja kwanzia mwanzo mpaka mwisho bila kutumia mbinu
82

rejeshi.

4.3.15 Athari

Mwandishi wa hadithi fupi hutumia mbinu zinazomfikirisha msomaji na hata

kumshtua. Mwandishi hufanya hivi ili msomaji afikirie na kutafakari kuhusu

matukio ya hadithini. Hadithi hizi huwa na mwisho usiotazamiwa na ugeukaji wa

matukio au msuko.

4.3.16 Uhuru

Mwandishi wa hadithi fupi hana uhuru wa kuyapoteza maneno. Kila neno au

maelezo anayotoa lazima yachangie kwenye athari nzima ya hadithi. Mwandishi

hana uhuru wa kutoka nje ya maelezo au mkondo wa hadithi na kusimulia

mambo ambayo hayahusiani na tendo kuu.

Kwa jumla, tunaweza kusema kuwa sifa muhimu ya hadithi fupi ni ufupi,

mkokotezo, uwazi na uwezo wa kuathiri msomaji au hadhira yake.

4.4.0 UCHAMBUZI WA HADITHI FUPI

Katika uchambuzi wa hadithi fupi, msomaji anapaswa kuzingatia sifa

tulizozungumzia hapo juu. Vipengele vingi vinavyohusika na uchambuzi wa

riwaya, tamthilia na hata ushairi hutumika pia katika kuchambua hadithi fupi.

Kama tulivyoona katika somo la kwanza, uchambuzi wa kazi ya fasihi huzingatia

fani na maudhui. Vipengele hivi vinahusika na hadithi fupi.


83

4.4.1 Maudhui

Kaitka kusoma na kuchambua hadithi fupi, msomaji achunguze lengo kuu na

ujumbe wa mwandishi. Msomaji anaweza kuelekezwa kwenye lengo kuu au

dhamira ya hadithi na kichwa cha hadithi yenyewe. Kisha, msomaji atafute na

kubainisha msimamo wa mwandishi pamoja na mwelekeo wake wa kimawazo na

kifalsafa.

4.4.2 Fani

Fani, kama tulivyoona katika somo la kwanza, ni njia iliyotumiwa na mwandishi

katika kuwasilisha maudhui ya kazi yake. Katika hadithi fupi, msomaji anaweza

kuzingatia vipengele vifuatavyo vya fani katika uchambuzi wake.

(i) Muundo

Msomaji anapaswa kuangalia mpangilio wa matukio katika hadithi. Muundo wa

hadithi hushughulikiwa kwa kuangalia mwanzo, kati na mwisho wa kisa husika.

(ii) Lugha

Mwandishi wa hadithi fupi hutumia lugha kuwasilisha maudhui yake. Jinsi

mwandishi huyo alivyotumia lugha yake, huathiri kwa kiasi kikubwa jinsi msomaji

atakavyoathiriwa na kazi hiyo. Msomaji wa hadithi fupi achunguze namna

mwandishi alivyotumia vipengele vya lugha kama vile tamathali za semi,

misemo, nahau na methali, taswira, msamiati, n.k.


84

(iii) Mandhari

Mandhari yana nafasi muhimu katika hadithi fupi. Msomaji ajitahidi kuangalia

kama kuna uhusiano baina ya mandhari na vipengele vingine vya utunzi k.v.

wahusika, dhamira na maudhui, ujumbe, n.k.

(iv) Wahusika

Katika hadithi fupi, wahusika hawana nafasi ya kukuzwa kwa mapana na marefu

yao. Msomaji achunguze wahusika waliotumika, mhusika mkuu, migogoro na

mivutano baina ya wahusika, na mahusiano ya wahusika hao na dhamira na

maudhui ya hadithi.

(v) Mtindo

Msomaji achunguze jinsi mwandishi wa hadithi fupi alivyotumia mtindo

unaomtambulisha kwa upande wa usimulizi wake, uteuzi wa msamiati, tamathali

za semi, lugha yake, mpangilio wa matukio na usawiri wa wahusika, miongoni

mwa mengine. Kupitia vigezo hivyo, msomaji ataweza kuitolea kauli hadithi fupi

anayoichunguza na kuichambua.

4.5 .0 MUHTASARI

Katika somo hili, tumeangalia vipengele vya kimsingi vya utanzu wa


hadithi fupi ambavyo vinautofautisha na utanzu wa riwaya tulioshughulikia katika
somo lililotangulia. Tumeona sifa mbalimbali zinazohusiana na hadithi fupi
pamoja na vipengele ambavyo vingemshughulisha mhakiki au mchambuzi wa
hadithi fupi. Katika somo linalofuata, tutachunguza utanzu wa tamthilia na
vipengele vyake muhimu.
85

4.6.0 ZOEZI:

1. Hadithi fupi ni nini? Tofautisha kati ya hadithi fupi na riwaya kwa upande
wa fani na maudhui.
2. Tunga hadithi fupi ya kurasa mbili au tatu. Angalia kama hadithi yako
imezingatia sifa zote kuu za hadithi fupi zilizojadiliwa.
3. Ni vipengele vipi vinavyomsaidia mhakiki wa hadithi fupi kurahisisha kazi
yake?
4. Kwa nini mkazo mkubwa katika hadithi fupi ni jinsi hadithi hiyo
ilivyomalizika?
5. Fanya utafiti kuhusu sababu zinazotinga kuendelea na kustawi kwa
utanzu wa hadithi fupi ikilinganishwa na tanzu zingine katika fasihi ya
Kiswahili.

4.7.0 MAREJELEO TEULE

1. Njogu, K. & Chimerah, R. (1999): Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na

Mbinu Nairobi: J.K.F.

2. Mbatia, M. (2000): Mwendawazimu na Hadithi Nyingine Nairobi: N.U.P.

3. Msokile, M. (1992): Misingi ya Hadithi Fupi Dar es Salaam: O.U.P.

4. Wamitila, K.W. (2002): Uhakiki wa Fasihi: Misingi na vipengele Vyake

Nairobi: Phoenix Publishers Ltd.

5. ____________ (2003): Kichocheo cha Fasihi: Simulizi na Andishi

Nairobi: Focus Books Ltd.


86

SOMO LA TANO

TAMTHILIA

5.0 UTANGULIZI

Tamthilia ni utanzu ambao hutegemea mazungumzo na uigizaji ili kuuwasilisha

ujumbe wake. Somo hili linachunguza utanzu huu. Katika somo hili, maana na

chimbuko la tamthilia vimetolewa. Aidha, kuna historia fupi ya tamthilia na aina

za tamthilia. Sifa za tamthilia zimejadiliwa pamoja na uhakiki na uchambuzi wa

tamthilia.

5.1.0 MALENGO

Baada ya kupitia somo hili, utaweza kufahamikiwa na:


1. Dhana na maana ya tamthilia
2. Chimbuko na historia ya tamthilia (ya Kiswahili)
3. Sifa kuu/vijenzi vya tamthilia
4. Namna ya kuhakiki na kuchambua tamthilia.

5.2.0 DHANA NA MAANA YA TAMTHILIA

? Eleza dhana na maana ya tamthilia

Tamthilia ni neno la Kiarabu lenye maana ya kumithilisha au kufananisha. Katika

Kiswahili, tamthilia linatumika kwa maana ya michezo ya kuigiza. Katika

tamthilia huwa kuna ufananishaji ambapo mwigizaji hujifananisha na mhusika wa

mchezo wakati wa kuigiza. Kulingana na Kamusi ya Kiswahili Sanifu, tamthilia ni


87

utungo wa kisanaa ambao huweka wazo fulani katika matendo na mazungumzo.

Kutokana na maelezo hayo, tunaweza kusema kwamba tamthilia ni utungo

ambao unaweza kuwa umeandikwa au haukwandikwa unaoliweka wazo

linalowasilishwa katika umbo la tukio la kuliwezesha kutendeka mbele ya

hadhira. Somo hili linajadili kuhusu tamthilia iliyoandikwa ambapo mtindo wa

mazungumzo ya wahusika umetumika. Kigezo kikuu cha tamthilia ni kuweza

kuwasilishwa jukwaani na kutazamwa na hadhira.

Tamthilia huwa na umbo lenye mpangilio maalum, mtiririko wa vitendo

vitendwavyo, pahala fulani pa kutendea na kugawika katika kitendo cha kwanza,

cha pili, cha tatu, n.k. na kila kitendo kikawa na maonyesho yake k.v. onyesho la

kwanza, la pili, la tatu, n.k. Tamthilia ni fasihi au sanaa tendaji ambayo si ya

kusomwa tu bali pia huigizwa. Tamthilia hutafsiriwa na kufasiliwa katika vitendo

vinavyoonekana, miondoko na sauti jukwaani. Hata hivyo, tamthilia huweza

kusomwa kimya kimya.

Mazungumzo baina ya wahusika sio majibizano tu ya usemi au kauli tupu bali ni

msingi mkuu wa kuendelezwa na kukuzwa kwa tendo kuu la kimaigizo katika

tamthilia fulani. Kama sanaa ya utendaji, kwa hivyo, suala la uigizaji na utendaji

kwenye jukwaa ni muhimu sana na lazima lichunguzwe katika uchambuzi

wowote wa tamthilia.
88

5.3.0 CHIMBUKO LA TAMTHILIA

Chanzo cha sanaa za maigizo ambazo ndizo asili ya drama au tamthilia ni

sherehe za kidini au matambiko. Wagiriki wa zamani walicheza na kuimba

wakizunguka madhabahu au pahala patakatifu na pia kuigiza visasili na visakale

vilivyolingana au kufungamana na maisha ya miungu wao.

Katika sherehe za matambiko, kulikuwa na drama yenye utendaji, uigizaji na

mavazi maalum (maleba na mapiku) yaliyotumika wakati tu wa sherehe hizo.

Uchina pia kulizuka drama iliyoambatana na sherehe za kidini na vile vile Misri

katika miaka ya 2000 k.y.m. Tamthilia za kwanza kuwahi kuandikwa zilitokana

na utamaduni wa Ugiriki katika karne ya 6 k.y.m.

Katika Afrika, hali kama hiyo inajidhihirisha. Dhana ya sanaa za maigizo na hata

tamthilia ikiwa na maana ya utendaji wa dhana, haikuanza tu na majilio ya

wakoloni hapa Afrika. Matambiko katika jamii mbalimbali yalizaa aina ya utendaji

katika baadhi ya ngoma, majigambo ya kiasili na masimulizi mbalimbali ya

Mwafrika. Katika utamaduni wa Waswahili, kabla ya kuja kwa watu wa ulaya ya

magharibi na kuleta drama yao, Waswahili walitunga na kughani tendi ambazo

baadhi yake ziliandikwa kwa hati ya Kiarabu.

Baadhi ya tendi zinaelezea kwa namna ya maigizo, matendo na kutofautisha


maneno ya wahusika mbalimbali na ya wasimulizi, maswala mbalimbali ya
utamaduni wa Waswahili. Maigizo hayo hutoa maelezo ya mandhari, mavazi na
vifaa vingine ambayo yote yanafanana na jukwaa la kisasa tunalosoma na
89

kutumia katika michezo ya kuigiza.

5.3.1 Historia Fupi ya Tamthilia ya Kiswahili

Tamthilia andishi ililetwa katika utamaduni wa Waswahili na lugha ya Kiswahili

wakati wa ukoloni. Mabadiliko ya mifumo ya kiuchumi na maendeleo ya

kiteknolojia yalileta drama iliyojitenga na dini na kujisimamia. Drama hiyo

ikaanza kuelezea fikra na maisha ya kila siku ya jamii. Tamthilia zikaanza

kuandikwa na kuigizwa majukwaani au kwenye kumbi zilizojengwa maalum kwa

shughuli hiyo. Hii ndiyo tamthilia iliyoletwa na wazungu.

Tangu miaka ya awali ya utawala wa wazungu hadi uhuru, kuliigizwa michezo ya

kuigiza ya kiulaya na mingi ilikuwa miongoni mwa sanaa za maigizo za

kibwanyenye. Tamthilia hizi zilidumu baina ya 1920-1960 katika mashule, na

kwa lugha ya Kiingereza. Hii ilikuwa drama ya mambo–leo na ilitokana na

ustaarabu wa Kizungu na yenye madhumuni ya wazungu kujifurahisha na

kujiliwaza.

Michezo hiyo ya mwanzo ilitumia watoto wa shule na waigizaji wengine katika

miji mikubwa k.v. Nairobi, Mombasa, Dar es Salaam na Kampala katika kumbi

zilizoitwa ‘little theatres’ kwa kutoa burudani kwa wakoloni. Michezo ya awali

ilimbeza Mwafrika na tabia zake, hasa hali ya kutojua kusoma na kuandika.

Baadhi ya tamthilia hizo zilitafsiriwa kwa Kiswahili na wamishonari k.v. ‘Bwana

Amekufa’ (The Lord is Dead) na ‘Wanawake Wenye Akili’ (Intelligent Girls). Huu

ukawa mwanzo wa tamthilia zilizoandikwa kwa lugha ya Kiswahili.


90

Katika miaka ya arobaini na hamsini, wazungu ambao awali walikuwa wameona

sanaa za maigizo za Kiafrika kama sanaa za kishenzi, waliamua kuziendeleza

sanaa hizo. Ngoma na maigizo hayo yakaanza mashuleni ili yaonyeshwe kwa

wananchi kama sehemu ya kuburudika kwa Mwafrika. Makundi yakaundwa

mashuleni kwa madhumuni hayo na baadhi ya michezo kutafsiriwa katika lugha

ya Kiswahili.

Baadaye, kwenye miaka ya hamsini na sitini, michezo ya Kiswahili iliandikwa

ambayo ilivuma mashuleni na baadhi yake kuchapishwa. Mifano ya michezo

hiyo ni Afadhali mchawi, Mgeni Karibu, Nakupenda lakini …, Nimelogwa Nasiwe

na Mpenzi, n.k. Mnamo mwaka 1957 kulianzishwa mashindano ya maigizo

mashuleni ambayo yalitoa changamoto kubwa kuhusiana na utoaji wa vitabu.

Michezo hiyo iliendelea mashuleni hadi mwaka wa 1963 ambapo msaada kutoka

shirikia la British Council ulikatizwa.

Katika kipindi cha ukoloni hasa kuanzia miaka ya arobaini na kuendelea, nje na

ndani ya mashule kulizuka vichekesho. Vichekesho hivyo vilikuwa na lengo la

kuburudisha na havikuwa na maudhui mazito kujadili matatizo katika jamii.

Vichekesho hivyo viliwacheka watu wa shamba na kuwadhihaki wasiojua

ustaarabu wa kizungu na lugha ya kimombo. Kulianzishwa pia maigizo ya

redioni ambapo Mwafrika alikuwa mhusika mkuu. Kupitia michezo hiyo,

ilidhaniwa kuwa Mwafrika angesahau harakati za kudai uhuru na badala yake

kuanza kuucheka ujinga wa Mwafrika mwenzake. Hata hivyo, juhudi zote hizo
91

hazikufua dafu na Mwafrika alipigana na kujinyakulia uhuru.

Baada ya uhuru, sanaa za maigizo zilichukua sura mpya. Miaka ya sitini,

kutokana na juhudi za kisiasa, kielimu na kitamaduni, kulianza makundi ya

maigizo ambayo yalidhamiria kuonyesha utamduni wa Mwafrika na maadili

mbalimbali k.v. falsafa, dini, siasa, utamaduni, kasumba, matatizo ya jamii, n.k.

Tamthilia zingine zilitafsiriwa kutoka lugha za kigeni, hasa Kiingereza k.mf Juliasi

Kaizari, Mabepari wa Venisi, Mfalme Edipode, n.k.

Baadaye, kumeibuka watunzi wengi ambao wametunga na kuigiza tamthilia

mbalimbali. Watunzi k.v. E. Hussein, D. Mulwa, A. Mazrui, C.N. Chacha, P.

Muhando, n.k. wametunga tamthilia nyingi ambazo zimeendelea kuzingatia

matatizo ya jamii na namna ya kuishi vyema. Maudhui ya tamthilia hizo

yanahusu maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, kitamaduni, kidini na kifalsafa.

Mwafrika ameacha kumcheka asiyejua kusoma na kuandika na kuanza

kumcheka mwenzake anayemwiga mzungu na kuwa mzungu mweusi.

5.4.0 AINA ZA TAMTHILIA

Ujuzi wa vipengele mbalimbali vya tamthilia tulivyozungumzia unatusaidia

kusoma na kuelewa tamthilia vizuri. Tamthilia ni za aina kadha. Kila aina ina

sifa zake maalum. Aina hizo za tamthilia ni kama zifuatazo:


92

5.4.1 Tanzia

Tamthilia ya tanzia huhusika na mambo yenye uzito kifikira na kihisia katika

maisha ya binadamu. Katika tamthilia za aina hii, mhusika mkuu hupewa sifa

nyingi zinazovutia na kupendeza. Lakini mhusika huyo hukabiliwa na shida au

tatizo ambalo linaweza kumpata mtu yeyote. Namna anavyojaribu kukabiliana

na tatizo hilo na kupigana vita kuishinda shida inayomkabili, hali ya malimwengu

na hali au tabia ya binadamu zinamfanya asiweze kufaulu na mwishowe

anashindwa.

Wahusika wa tanzia husawiriwa vizuri ndipo waweze kuaminika kama binadamu

wa kweli. Msuko wa tamthilia hiyo hukita kwenye wazo moja bila kuingilia viploti

vingine vidogo vidogo. Mbinu hizi huelekeza hadhira katika kukubali kwamba

yaliyomfika mhusika mkuu au nguli hayakuweza kuepukika. Kwa kuelewa

kwamba nguli ni kama aliyeingia katika mtego wa majaaliwa usioepukika

kunatufanya tumwonee huruma; na kule kuelewa kwetu kwamba haya yanaweza

kumpata yeyote kati yetu, kunatutia hofu.

Juhudi na ushujaa wa nguli katika kupambana na shida ile kufa na kupona

hutupa moyo wa kuendelea na mapambano na kutujaza imani inayotofurahisha

kwamba binadamu si kiumbe dhaifu. Katika tamthilia za tanzia, nguli wakati

mwingine hufa au kuuawa, lakini kifo chake si kama cha ajali barabarani. Ni kifo

kinachokuja baada ya mapambano marefu yanayochipuza hisia za ushujaa wa

binadamu. Kwa hivyo, msuko wa mapambano dhidi ya shida fulani huwa

muhimu zaidi katika tamthilia za tanzia kuliko kifo kinachotokana na mapambano


93

hayo.

Katika fashi ya Kiswahili, tamthilia tafsiri ya Mfalme Edipode (Sofokile) ni mfano

mzuri wa tamthilia tanzia. Zingine ni k.v., Mzalendo Kimathi (N. Thiong’o na M.

Mugo), Kinjeketile (E. Hussein), Pungwa (S.A. Mohamed) na Kilio cha Haki (A.

Mazrui).

5.4.2 Futuhi

Futuhi ni tamthilia ambayo hutuchorea picha yakini ya maisha ingawa usawiri

huo hauna undani na uzito kama ule unaojitokeza katika tanzia. Kwa sababu hii,

majaaliwa ya wahusika wa futuhi huiathiri hadhira kihisia kwa kiwango cha chini

zaidi kuliko tanzia inavyoathiri wahusika wake.

Lengo la kimsingi la futuhi ni kuchangamsha na huishia kwa namna ya

kufurahisha. Futuhi kwa hivyo hujikwepesha na maswala ya kuhuzunisha au

kutia hofu. Athari ya futuhi ya kuchekesha hutokana na matendo, mienendo ya

wahusika na hitilafu au ila za kuingiliana kwa kiusemi.

5.4.3 Melodrama

Melodrama inafanana sana na tanzia ingawa mara nyingi nguli wa melodrama

humalizika na ushindi, matokeo yake yanasisimua sana, na mwendo wa msuko

wake huwa ni wa haraka haraka zaidi. Wahusika wake huvutia na kufurahisha

lakini hawana sifa za kishujaa. Dhamira ya melodrama huzungukia mvutano kati

ya wema na uovu au ubaya. Miishio ya tamthilia hizi haina sifa ya mtakasohisia


94

kama ilivyo na tanzia bali huwa ni aina ya ushindi wa mhusika mwema.

5.4.4 Kichekesho

Kichekesho ni aina ya tamthilia ambayo huwa na uwezo wa kusababisha kicheko

kingi kutokana na mbinu za kifutuhi ya chini kama ucheshi, hali zisizokuwa za

kawaida k.v. wahusika wasio wa kike kuvaa mavazi ya kike na wale wa kike

kuvaa ya kiume, visa vya mapenzi ya kuchekesha, mikimbizano jukwaani, n.k.

5.4.5 Tanzia-ramsa

Hii ni aina ya tamthilia ambayo huonyesha mabadiliko ya aina fulani

yanayogeuza mwelekeo wa matukio ya kitanzia na kuufanya kuwa tofauti au wa

kufurahisha. Tanzia-ramsa ni kama tanzia inayoishia kwa furaha.

5.4.6 Tamthilia za Kihistoria

Hizi ni tamthilia zinazojengwa kutokana na mhusika au matukio ya kihistoria.

Mfano ni tamthilia za Kinjeketile (E. Hussein) na Mkwava wa Uhehe (M.M.

Mulokozi).

5.4.7 Tamthilia Tatizo

Tamthilia tatizo huzungumzia swala fulani katika jamii. Tamthilia hizi pia huitwa

tamthilia tasnifu na kuna mifano mingi katika fasihi ya Kiswahili k.v. Mnara

Wawaka Moto (R. Chimerah), Mashetani (E. Hussein), Kitumbua Kimeingia

Mchanga (S.A. Mohamed), Mama Ee (A.K. Mwachofi), Natala (K. Wa Mberia),

n.k.
95

5.5.0 VIJENZI VYA TAMTHILIA

Tamthilia hutegemea zaidi vitendo na mazungumzo ambapo wazo

linalowasilishwa huwekwa katika umbo la tukio la kuliwezesha kutendeka mbele

ya hadhira. Tamthilia hujengwa na vipengele mbalimbali ambayo huitambulisha

na tanzu zingine za fasihi k.v. riwaya, hadithi fupi na ushairi.

5.5.1 Muundo wa Tamthilia

Tamthilia huwa imegawika katika sehemu ambazo zinaitwa matendo (au

sehemu) na maonyesho. Tamthilia inaweza kuwa na maonyesho pekee bila

matendo. Mwandishi hulazimika kuuvunja mfululizo wa tamthilia katika sehemu

za matendo na maonyesho, ili aichukue hadhira yake mbele na nyuma, na hapa

na pale. Tamthilia huchukua muda mfupi lakini inahusu matukio ya muda mrefu

zaidi k.v. siku, majuma, miezi au hata miaka. Tamthilia ni lazima ionyeshe mpito

wa wakati.

5.5.2 Dhamira na Maudhui

Tamthilia, kama zilivyo kazi nyinginezo za fasihi, ina dhamira na maudhui.

Vigezo hivi hukuzwa kupitia mazungumzo na matendo ya wahusika kuanzia

onyesho la kwanza hadi onyesho la mwisho.

5.5.3 Uigizaji

Katika tamthilia, tendo ni muhimu sana. Jinsi sehemu mbalimbali

zinavyohusiana na kuchangia kwenye tendo kuu ni muhimu kwa kuwa zina

matokeo makubwa kwenye athari ya kazi nzima. Katika tamthilia, drama ni


96

tendo na wahusika pia ni tendo.

Tendo katika tamthilia huletwa na ile hamu, msukumo, na tamaa ya kutaka

kukipata kitu fulani. Mhusika anayetaka kitu fulani hukumbana na vikwazo,

vizuizi na upinzani, hivyo kuibusha au kuzusha mgogoro. Jinsi msukumo wa kila

upande unavyokuwa muhimu na mkubwa, ndivyo mgogoro unavyojidhihirisha

wazi. Kwa njia hii, tamaa ya msomaji huwa kubwa sana na hutaka kuendelea

kusoma.

KUMBUKA:

Katika tamthilia:
• Matendo ya wahusika hudhihirika kupitia utendaji wa jukwaani.
• Mgogoro katika tendo huanza pale wahusika wanapata hamu fulani lakini
pana kizuizi.
• Udhati wa tendo hutegemea udhabiti wa wahusika

5.5.4 Msuko wa Matukio

Katika tamthilia, mvutano na mgogoro hukuzwa baina ya mhusika na mhusika

mwingine, mhusika na nafsi yake, au mhusika na tabaka fulani. Msuko na

mgogoro ni msingi mkubwa wa muundo wa tamthilia na uandishi wa tamthilia.

Msuko wa tamthilia huwa na sehemu kadha.

(i) Ufunguzi

Mwandishi huanza kwa kuonyesha mambo yanayoathiri matukio ili kutambulisha


97

msuko ukifunguka mapema.

(ii) Upeo

Upeo ni kilele cha tendo katika tamthilia. Upeo unaofaa huanza kutosheleza

matarajio au kuyageuza kwa mshtukizo au utoshelezi wa tukio la kidrama.

(iii) Mgeuko

Mgeuko hutokea pale tendo fulani kuu huelekea upande mmoja kisha ghafla

likageuka na kuelekea kwingineko.

(iv) Ufumbuzi

Katika sehemu hii, msuko hufumbuliwa na tunapata suluhisho la mgogoro

uliokuwepo katika tamthilia.

KUMBUKA:

• Kiwango cha maarifa ya hadhira huathiri matendo jukwaani na ukuaji wa


mgogoro na msuko wenyewe.
• Tamthilia zingine huwa na misuko sambamba ambapo misuko miwili au
zaidi hutumika ili kulinganisha na kutoa uamuzi.

(v) Mpomoko

Baada ya kupata kilele na masuluhisho ya mvutano na mgogoro, hufika hatua ya

mwisho ya msuko wa tamthilia. Mpomoko ni pale ambapo mwandishi huitolea

tamati au kuhitimisha matukio katika tamthilia.


98

5.5.5. Mazungumzo

Mazungumzo pia huitwa dialojia na hutumiwa kuelezea majibizano kati ya

wahusika waliopo jukwaani au katika tamthilia. Mazungumzo sio maongezi au

majibizano kwa ajili ya kujibizana tu. Mazungumzo hutumika kuendeleza tendo

kuu katika tamthilia. Mazunguzo ndiyo nguzo za kukuza na kupanua dhamira na

maudhui. Mazungumzo nafsi na uzungumzinafsi wa wahusika huchukuliwa

kama sehemu ya mazungumzo ya tamthilia kwani yanaendeleza tendo kuu.

Kwa jumla, mazungumzo ndiyo njia kuu ya kuendeleza hadithi iliyopo katika

tamthilia kwani mwandishi hana uhuru wa kutumia mbinu za usimulizi kama ilivyo

na tanzu za nathari.

5.5.6 Maelezo ya Jukwaa

Haya ni maelezo ambayo huandikwa kwa mabano katika tamthilia kwa hati ya

mlazo. Maelezo au maelekezo hayo huongoza mienendo na miondoko ya

wahusika na kutoa maelezo kuhusu wasifu wa wahusika k.v. mavazi, lugha,

ishara, matendo, n.k. Maelezo hufafanua mandhari au mahali pa mchezo na

matendo mbalimbali yanayotokea jukwaani kati ya mengine.

5.5.7 Mandhari

Mandhari katika tamthilia hutumiwa kuelezea sehemu ambapo tendo fulani

linatendeka. Mandhari hurejelea mazingira ya jukwaani na hata wakati

wenyewe. Baadhi ya mambo yanayohusu mandhari ya tamthilia ni.


99

(i) Maleba

Maleba huweza kuonyesha kipindi fulani cha kihistoria na hali zilizohusiana na

kipindi hicho. Maleba pia hutumika pamoja na mapiku au vinyago kuwapatia

wahusika sifa ambazo si za binadamu wa kawaida.

(ii) Eneo la uigizaji

Eneo la uigizaji huwa ni jukwaani ambapo wahusika huingiliana katika matendo

yao. Ukubwa au upana wa eneo hili ni muhimu katika kutoa athari ya tamthilia

na kuupitisha ujumbe.

(iii) Mwangaza

Mwangaza au taa hutumiwa kuwamulika wahusika na mandhari yao jukwaani.

Mwangaza unaweza kutumiwa kutoa picha fulani ambayo inafungamanishwa na

tendo kuu. Kwa mfano, taa nyekundu huonyesha hatari, giza kuonyesha uovu,

ukosefu wa mwelekeo, n.k. ilhali mwangaza mwangavu hutoa hali ya kawaida

au matumaini.

5.5.8 Wahusika

Wahusika katika tamthilia ndio nguzo kuu ya matendo ya kidrama. Katika

tamthilia, kuna mambo ambayo yanahusiana na wahusika:

• Mazungumzo nafsi hutumiwa kutoa mawazo ya ndani ya wahusika.

• Matumizi ya ‘kando’ hutumika kama mbinu ya kufichua msimamo wa

mhusika mmoja kumhusu mwingine au kuonyesha hali ilivyo tofauti na

alivyosema au kutenda jambo fulani.


100

• Wahusika wazuri si lazima wafanane na watu halisi bora waweze

kukubalika katika muktadha wa tamthilia na ulimwengu wa ubunifu ili

kuendeleza tendo kuu.

• Wahusika wa tamthilia hujengwa kwa ulinganuzi ambapo mhusika

husawiriwa kinyume na mwenzake au wenzake.

• Wahusika hudhihirishwa na kukuzwa vyema kwa matumizi ya

mazungumzo.

• Wahusika hupewa majina ya kuwatambulisha kwa kutegemea matendo

kuliko usimulizi wa mwandishi.

5.6.0 UCHAMBUZI WA TAMTHILIA

Msingi na vipengele vinavyohusika katika uchambuzi wa tanzu kama riwaya au

hadithi fupi huweza kutumiwa katika kuhakiki tamthilia. Hata hivyo, kuna sifa

maalum ambazo zinautenga utanzu wa tamthilia na tanzu za kinathari. Tamthilia

huandikwa kama hadithi ya kuwasilishwa jukwaani. Muundo na mtindo wa

tamthilia hutegemea sana mbinu za uigizaji au uwasilishaji jukwaani. Matendo

na mazungumzo huchukua nafasi kubwa katika kuwasilisha maudhui ya

tamthilia. Uchambuzi wa tamthilia unafaa kuoanisha mbinu zote za uandishi wa

tamthilia.

Mhakiki achunguze namna maonyesho yanavyoendeleza na kukuza

hadithi pamoja na kukuza wahusika na hali ya uigizaji.

Msomaji ajaribu kutambua maswala makuu yanayoibuka kutokana na

tabia za wahusika na vidokezo vingine alivyotoa mwandishi kupitia

mbinu za uandishi.
101

Matendo, maelezo na mazungumzo ya wahusika na mahusiano yao ni

muhimu.

Mchambuzi azingatie namna msuko wa tamthilia unavyosaidia

kuonyesha usuli na kuendeleza ujumbe wa mwandishi.

Msomaji atambue mbinu alizotumia mwandishi na mtindo wake wa

kutiririsha tamthilia.

Mchunguzi aangalie hadhira iliyolengwa na mwandishi na kama lugha

iliyotumiwa inaafikiana na viwango vya hadhira hiyo.

Mwisho, mhakiki azingatie maonyesho na matendo yaliyotumiwa na

mwandishi na umuhimu wake katika kukuza na kuendeleza maudhui.

Kisha, mhakiki atoe kauli yake kama njia ya kuhitimisha uchambuzi

wake.

5.7.0 MUHTASARI:

Somo hili limechunguza vipengele na misingi mbalimbali muhimu katika


uelewaji wa utanzu wa tamthilia. Tumeona kuwa tamthilia hutegemea sana
mazungumzo na vitendo kama mbinu za kuendelezea dhamira, maudhui na
ujumbe wake. Vipengele na vigezo muhimu katika uchambuzi wa tamthilia
vimeangaziwa. Somo linalofuata linachunguza utanzu ambao una historia ndefu
katika fasihi ya Kiswahili; utanzu wa ushairi.
102

5.8.0 ZOEZI

1. Tamthilia ni nini? Eleza chimbuko la utanzu wa tamthilia.


2. Tamthilia ya Kiswahili ina historia ndefu. Kwa kutoa mifano, jadili kauli hii.
3. Mgogoro na msuko una nafasi gani katika muundo wa tamthilia?
4. Jadili kwa kina na kwa kutoa mifano vijenzi vikuu vya utanzu wa tamthilia.
5. Tunga tamthilia fupi kisha uichambue kupitia vigezo vikuu vya kuhakiki
tamthilia.

5.10.0 MAREJELEO TEULE

1. Mazigwa, S.A. (1991): Fasihi ya Kiswahili Peramiho: Benedictine

Publications Ndanda.

2. Msokile, M. (1993): Misingi ya Uhakiki wa Fasihi Nairobi: E.A.E.P.

3. Muhando, P. & Balisidya, N. (1976): Fasihi na Sanaa za Maonyesho.

Dar es Salaam: T.P.H.

4. Wafula, R.M. (1999): Uhakiki wa Tamthilia: Historia na Maendeleo Yake

Nairobi: J.K.F.

5. Wamitila, K.W. (2003): Kichocheo cha Fasihi: Simulizi na Andishi

Nairobi: Focus Books Ltd.


103

SOMO LA SITA

USHAIRI
6.0 UTANGULIZI

Ushairi ni utanzu mwingine wa fasihi. Ushairi ni sanaa ya kipekee ambayo

hufuata ufundi maalum katika utunzi wake. Katika somo hili, tunaangalia ushairi

kwa kutoa maelezo ya dhana ya ushairi na historia yake. Tumetoa pia sifa na

aina za mashairi pamoja na jinsi za kuchambua mashairi.

6.1.0 MALENGO

Somo hili litakuwezesha kuelewa:


1. Maana ya ushairi
2. Historia ya ushairi wa Kiswahili
3. Aina za mashairi
4. Sifa za mashairi
5. Uchambuzi wa ushairi

6.2.0 DHANA YA USHAIRI

Shairi ni neno linalotumiwa kueleza utungo wenye muundo maalum, mpangilio

mahususi wa maneno, unaotumia lugha ya mkato na unaogusia swala fulani la

maisha ya jamii. Utungo huo unaweza ukafuata kanuni fulani za utunzi (arudhi)

au hata usifuate kanuni hizo. Taaluma ya ushairi imeelezewa kama sanaa ya

vina inayopambanuliwa kama nyimbo zenye ufasaha wa maneno machache au

muhtasari. Shairi huwa na mlingano wa sauti za herufi, lugha tamu na fupi, na

hubeba mawazo, maono na fikra nzito inayofanya moyo uathirike pakubwa.


104

Shairi huwa na urari wa mizani kamili yenye lugha isiyokuwa na kashfa au matusi

ndani yake. Shairi pia huwa na vina vinavyopatana na muwala pamoja na

maana iliyo bora yenye ufundisho ndani yake, furahisho, mvuto wa maarifa na

kasida za kusifika. Mfano mzuri wa maana ya shairi umetolewa na Abdilatif

Abdalla (1973) anaposema:

“… Na utungo ufaao kupewa jina la ushairi si utungo wowote tu bali ni

utungo ambao katika kila ubeti wake kuna ulinganifu wa vina vitukufu

vilivyopangwa kimoja baada ya chenziye; wenye vipande vilivyo na

ulinganifu wa mizani zisizopungufu wala zilizozidi; na vipande hivyo viwe

vimetandwa na maneno ya mkato maalum na yenye lugha nyofu, tamu na

laini, lugha ambayo ni tetelezi kwa ulimi na kwa kuitamka, lugha ambayo

ina uzito wa fikra, tamu kwa mdomo wa kuisema, tumbuizi kwa masikio ya

kuisikia na yenye kuathiri moyo uliokusudiwa.”

Kutokana na maelezo hayo, ushairi unaonekana kuwa sanaa ya kipekee. Shairi

hutumia lugha ya mkato lakini tamu ambayo ni ya kitamathali inayotoa maana

fiche kupitia mbinu za ulinganishi na jazanda.

6.2.1 ASILI YA USHAIRI

Chanzo cha ushairi ni nyimbo ambazo ziliimbwa katika magoma ya harusi, katika

pungwa, sherehe za jando na unyago, wakati wa kufanya kazi kwa ushirikiano,

wakati wa kuwabembeleza watoto, wakati wa majonzi, n.k. Manju au malenga

wa nyimbo hizo wakazidi kutopea katika taaluma hiyo na kuanza kutumia

utaratibu maalum wa kuziimba. Baadaye wakawa wanatumia urari na vina

katika kuimba mistari ya nyimbo na huo ukawa ndio mwanzo wa ushairi.


105

6.2.2 AINA ZA MASHAIRI

Ushairi unaweza kugawanywa katika mafungu makuu mawili.

(i) Tenzi

Utenzi ni utungo ambao kimaudhui huwa unaeleza tukio fulani linalotukia katika

jamii au lililowahi kutokea. Tendi huweza kuwa maelezo ya wasifu wa mtu fulani,

jambo fulani la kihistoria au jambo lolote zito linaloelezwa kwa maelezo marefu.

Tenzi huwa na beti nyingi kuliko mashairi na huweza kuwa na beti kama 200,

300, 400 au zaidi kutegemea ufundi wa mwandishi au mtunzi. Tenzi kwa hivyo

huweza kuchukua muda mrefu kutungwa na kughaniwa.

(ii) Mashairi

Shairi ni utungo ambao umenuia kueleza kwa ufupi mambo fulani kuhusu

binadamu na mazingira yake. Mashairi hueleza mambo yanayohusu binadamu

na maisha yake ya kila siku. Tungo hizi huwa za aina nyingi kutegemea dhamira

mbalimbali k.v. mashairi ya simango, kashfa, wasifu, uzindushi, waadhi,

majigambo, n.k.

6.3.0 VIJENZI VYA USHAIRI

Ushairi ni utanzu ambao umejengwa na vipengele kadha ambavyo husaidia

katika kupatia tungo zake sura na sifa maalum.


106

6.3.1 Mitindo ya Mashairi

Mashairi ya Kiswahili yana mitindo mingi katika utungaji wake na hutegemea

sana ufundi wa mtunzi mwenyewe.

(i) Mtindo pindu

Katika mtindo pindu, silabi mbili za mwisho wa msitari (au kina cha kati)

hurudiwarudiwa. Kwa mfano, kama mstari wa kwanza umeishia kwa neno

“fahamu”, mstari wa pili utaanza na silabi mbili za mwisho ambazo ni “hamu”.

Mtindo huu pia huitwa ‘mtindo mkufu’.

(ii) Mtindo wa msisitizo

Mtindo wa msisitizo hujitokeza kwa namna mbili kuu:

(a) Msisitizo wima

Msisitizo wima ni ile hali ya kuwa na neno moja (au mawili) likitokea

mwanzoni na kisha likarudiwarudiwa katika kila mstari wa shairi zima. Mtindo

huu si wa kutafuta urahisi wa kupata maneno ya kutumia au kulipamba shairi

kwa namna fulani bali unatia shadda au mkazo maalum katika shairi husika.

(b) Msisitizo ulalo

Mtindo huu hutumia kibwagizo au kiitikio kama kiini cha habari katika shairi.

Kibwagizo hicho hurudiwarudiwa katika kila ubeti wa shairi kama njia ya

kusisitiza ujumbe maalum unaobebwa na shairi hilo.


107

(iii) Beti kubadilisha vina

Mtindo huu hufuata utaratibu ambapo ubeti wa kwanza huwa na kina cha kati na

cha mwisho ambavyo hubadilishana nafasi katika ubeti unaofuata. Tunaweza

kuwa na hali ya kubadilishana vina vya kati kutoka ubeti hadi ubeti ilhali vina vya

mwisho katika kila ubeti hubakia vile vile. Ama tukawa na mtindo unaoruhusu

kipande kizima cha msitari wa mwisho wa ubeti kuweza kurudirudiwa kama

chanzo cha ubeti unaofuatia. Kwa mfano:

‘Uwanjani nayanena, leo wote wataona’;

kama msitari wa mwisho, msitari wa kwanza wa ubeti wa pili utaanza na:

‘leo wote wataona, …’

6.3.2 Miundo ya Mashairi

Ushairi una miundo mbalimbali kutegemea ufundi na ubunifu wa mshairi

mwenyewe.

(i) Tarbia

Huu ni muundo ambao umekuwa na mashiko kuliko miundo mingine. Katika

tarbia, kila ubeti wa shairi huwa na mistari minne na kila msitari kuwa na mizani

kumi na sita. Kila msitari huwa na vipande viwili yenye mizani nane kila kipande.

(ii) Tathnia

Katika tathnia, ubeti huwa na mistari miwili. Muundo huu hutumika zaidi katika

nyimbo na ni nadra sana katika mashairi ya kawaida, mashairi ya kusomwa

kama mashairi au ya kuimbwa kishairi.


108

(iii) Tathlitha

Muundo wa tathlitha huwa na mashairi ambapo beti huwa na mistari mitatu kila

moja.

(iii) Takhmisa

Takhmisa ni muundo wa shairi ambapo kila ubeti huwa na mistari mitano mitano.

(v) Sabilia

Katika muundo huu, mtunzi au mshairi huwa na uhuru wa kuweka zaidi ya

mistari mitano katika kila ubeti wa shairi lake.

6.4.0 SIFA ZA MASHAIRI

Kuna sifa za mashairi ambazo husaidia katika kuelewa utanzu huu. Kupitia sifa

za mashairi, tunaweza kubainisha mashairi mbalimbali.

6.4.1. Toni

Mshairi hutumia maneno kueleza mawazo fulani kuhusu maisha. Kwa hivyo,

kuna umuhimu wa kuichunguza toni ya shairi. Toni ya shairi inafungamana kwa

kiasi kikubwa na masuala anayozungumzia mshairi. Kwa mfano, shairi

linalogusia unyonyaji litaelekea kuwa na toni ya uchungu. Ni muhimu

kukumbuka kuwa toni huweza kubadilika katika shairi lile moja.


109

6.4.2 Msamiati

Jinsi mshairi anavyoteua msamiati wake ni muhimu katika kuwasilisha ujumbe

wake pamoja na athari za ujumbe huo kwa wasomaji wake. Mshairi anaweza

kutumia lugha ya kawaida au msamiati maalum kutegemea maudhui ya shairi

lake. Hali hii husababisha neno fulani kuwa na maana zaidi ya moja na ndiyo

msingi wa utata katika ushairi wa Kiswahili.

KUMBUKA:

Ili kupata msamiati wa mshairi na maana yake:


• Angalia muktadha wa kila neno katika kuleta maana fulani tofauti na ile ya
kawaida.
• Maneno yanaweza kuwa na maana za kijuujuu au maana za kitamathali.
• Uwezo wa maneno au msamiati hupimwa kutokana na uwezo wake wa
kuuwasilisha ujumbe wa mshairi

6.4.3 Taswira au Jazanda

Mshairi anaweza kutumia taswira au jazanda kwa nia ya kuchochea hisia za

msomaji za kuona, kugusa, kunusa, kuonja, kwenda, kuhisi joto, n.k. Mshairi

hatumii taswira au jazanda za kila siku ambazo zimechakaa bali huunda mpya

zenye mnato.

6.4.4 Vina na Mizani

Vina na mizani ni sehemu ya mbinu za kisauti zinazopatikana katika ushairi.

Vina ni silabi zinazofanana na ambazo hupatikana katika sehemu moja katika

mpangilio wa shairi. Nayo mizani ni silabi zinazotamkika. Vina na mizani ni


110

sehemu muhimu katika kutunga mashairi.

6.4.5. Kibwagizo

Huu ni msitari wa mwisho ambao mara nyingi huwa wa namna moja katika beti

zote za shairi. Mpangilio wa vina katika kibwagizo wakati mwingine huwa tofauti

na ile mistari mingine katika ubeti.

6.4.6 Urari

Urari ni mpangilio wa mistari katika ubeti. Unaweza kusoma ubeti halafu

ukasema msitari huu wa pili ungekuwa wa kwanza na wa kwanza ukawa wa pili,

au wa tatu ungekuwa wa pili, n.k. Habari katika msitari zinatakiwa kuungana na

kuumana kutoka mwanzo mpaka mwisho wa ubeti. Ubeti ukiwa na mistari

mitatu, minne au zaidi, shairi husemekana kuwa na urari mzuri.

6.4.7 Muwala

Muwala ni mfuatanisho wa habari kutoka ubeti hadi ubeti kufuatana na ule

mtiririko wa habari zenyewe. Unaweza kulitazama shairi ukaona ubeti fulani

ungekuwa wa kwanza na wa pili au ubeti fulani ungekuwa mahali fulani au hata

pengine kuondoa ubeti fulani bila kuharibu habari na dhamira kuu ya shairi.

Kufanya hivyo ni kuchunga na kuhakikisha muwala mzuri katika shairi.

6.4.8 Utoshelezo

Katika ushairi, ni muhimu kwa kila ubeti kuweza kujitosheleza kikamilifu kwa

habari au ujumbe unaotolewa na mshairi kwa msomaji ili afahamu anaelezwa


111

nini katika ubeti ule.

6.4.9 Umaana

Shairi zuri ni lile ambalo ukilisoma utafahamu kitu fulani. Shairi bila maana

litakuwa upuuzi mtupu. Shairi la Kiswahili sio tu lifuate kanuni za utunzi bali ni

sharti liwe na maana. Kuna mashairi ambayo ukiyasoma hutaelewa mtunzi

alikusudia kusema nini. Hali kama hiyo hutokana na pengine kuchanganya

habari nyingi katika shairi moja au ubeti mmoja au kuweka maneno katika

muwala usiokuwa wake hivyo kukosa maana.

6.4.10 Kunga

Kunga ni siri ya shairi au kulihifadhi lisiwe wazi sana. Kunga ni kutumia maneno

ambayo si matusi, wala kashfa; fumbo lifumbe, ili wenzio walifumbue, lisiwe

fumbo halafu ukalifumbua humo humo katika shairi hilo hilo.

6.4.11 Urudiaji

Urudiaji katika ushairi ni jambo la kawaida na huweza kupatikana katika viwango

vya sauti, neno, msitari au hata ubeti, hasa katika tungo ndefu. Kuna urudiaji wa

namna tofauti tafauti:

(i) Takriri

Huu ni urudiaji wa kukariri au wa kutokea mara kadha. Urudiaji wa aina hii

huweza kupatikana katika ngazi za vina, mizani, sauti, neno, msitari, kifungu, n.k.

ili kusisitiza jambo fulani au kuremba lugha ya shairi.


112

(ii) Usambamba

Usambamba ni urudiaji wa miundo fulani katika shairi k.v. kipande au msitari wa

ubeti kwa nia ya kutilia mkazo ujumbe fulani.

(iii) Unyambuaji

Hii ni mbinu ya urudiaji ambapo neno fulani linanyambuliwa na kuunda maneno

mengine yanayofanana nalo. Hii ni sifa inayoingiliana na muundo wa Kiswahili

na lugha zingine za Kibantu na husaidia katika kuimarisha wizani au rithimu.

KUMBUKA:

Kurudiarudia maneno katika shairi hupunguza na kuharibu utamu wa


shairi na kupunguza hamasa za msomaji ambaye humwona mtunzi kama
ambaye hana msamiati au lugha yake ni finyu. Isipokuwa katika mashairi ya
msisitizo, kurudiarudia maneno hakufai.

6.4.2 Anwani au Kichwa cha Shairi

Unaweza kuwa na shairi ambalo halina anwani au jina; bora limefuata kanuni

zote za shairi na msomaji atafurahia baada ya kupata ujumbe uliomo. Lakini

shairi kama hilo litakosa au kupungukiwa na utamu litakapokosa jina au anwani.

Shairi kama hilo, huwa ni kama hadithi bila kichwa. Kwa hivyo, ni muhimu kwa

shairi kuwa na jina au anwani.


113

6.4.12 Kutochanganya Dhamira

Shairi huwa na dhamira moja. Kuchanganya dhamira mbili au tatu katika shairi

moja ni kuliharibu shairi kwani ni kama kuchanganya hadithi mbili au tatu na

kuzipatia jina moja. Shairi hubeba dhamira moja mwanzo hadi mwisho ndipo

lipendeze kwa msomaji. Shairi halitakiwi kuwa na beti nyingi. Shairi kama

limejadili dhamira yake kikamilifu, linatakiwa kukoma pale la sivyo, kuna hatari

ya kuingia kwenye dhamira nyingine kama shairi hilo litaendelea.

6.5.0 UCHAMBUZI WA MASHAIRI

Katika uchambuzi wa mashairi, msomaji anapaswa kuangalia dhamira, maudhui,

falsafa na ujumbe mwingine ambao mwandishi ametoa. Namna sifa za mashairi

tulizoona zilivyotumiwa na mshairi husaidia kuelewa na kuhakiki ushairi.

6.5.1. Dhamira na Maudhui

Hili ni lengo la mshairi katika kutunga shairi lake. Dhamira hujitokeza kwa wazo

kuu ambalo hukuzwa katika shairi kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Katika

kuliendeleza wazo hili kuu, masuala mengine mengi huibuka. Haya ndiyo

maudhui ya shairi. Katika kuchambua dhamira na maudhui, msomaji aangalie

hadhira iliyolengwa na mwandishi na kubainisha mtazamo na falsafa ya mshairi

katika shairi lake.

(i) Ujumbe
114

Ujumbe ni taarifa aipatayo msomaji anaposoma shairi fulani. Ujumbe unaweza

kuwa mbaya (wenye mafunzo mabaya) au mzuri.

(ii) Falsafa

Falsafa ni fikra kuu ya mtunzi katika shairi. Fikra hizo hutokana na imani na

misimamo ya mwandishi ambayo huathiri kwa kiasi fulani namna anavyotazama

mazingira yake ya kisiasa, kiuchumi, kidini, kitamaduni na kijamii.

6.5.2. Matumizi ya Lugha

Katika kuchunguza lugha ya shairi, msomaji anaongozwa na:

Msamiati wa mwandishi ambapo atangalia uteuzi wa maneno, maana

ya maneno hayo na ufaafu wa maneno kama yalivyotumika

Sajili za lugha. Hali ya mwandishi kutumia lugha inayoafikiana na

muktadha au uwanja au tabaka fulani.

Tamathali za semi alizotumia mshairi na kama zinaeleweka na kutoa

maana kwa shairi na pia mchango wake katika kuendeleza dhamira

kuu.

KUMBUKA:

Wakati wa kuchunguza lugha zingatia:


• Shairi hupata maana kwa kuwasilishwa kwa mtindo wa kitamathali bali sio
ule wa moja kwa moja.
• Shairi lazima litumie lugha ambayo inatoa maadili muhimu kwa msomaji.
• Shairi huweza kutumia taswira, toni, msamiati na mbinu za sauti katika
kuboresha utunzi wake na kutoa maudhui.
115

6.6.0 MUHTASARI

Somo hili ni la mwisho katika kozi hii. Katika somo hili, tumeona maana
na vipengele mbalimbali vya utanzu wa ushairi. Historia fupi ya ushairi na aina
zake, pamoja na viungo mbalimbali vimehulutiwa kutegemea vipimo vya mizani,
vina na mishororo. Somo hili pia limeangazia jinsi mbalimbali zinazoweza
kutumika katika uchambuzi na uhakiki wa ushairi. Mambo zaidi kuhusiana na
taaluma ya ushairi yatashughulikiwa katika kozi maalum zinazohusiana na
utanzu huu.

6.7.0 ZOEZI

1. Ushairi ni nini? Tofautisha ushairi na nyimbo kwa upande wa mtindo na


muundo.
2. Bainisha historia ya ushairi wa Kiswahili.
3. Tafuta shairi lolote na kupitia sifa za mashairi, kisha utathmini kufaulu au
kutofaulu kwa mtunzi wa shairi hilo.
4. Ni vigezo gani vinavyomwongoza mchambuzi wa mashairi katika kuhakiki
mashairi?
5. Tunga shairi la beti tano kisha umpe mwenzako alihakiki na kutoa maoni
kuhusiana na ubora wake

6.7.0 MAREJELEO TEULE

1. Abdalla, A. (1973): Sauti ya Dhiki. Nairobi OUP

2. Njogu, K. & Chimerah, R. (1999): Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na

Mbinu. Nairobi. JKF

3. T.U.K.I. (1985): Fasihi III. Makala za Semina za Waandishi wa

Kiswahili Dar es Salaam: T.U.K.I.

4. Ombuge, R. & Kisia, A. (1999): Uchambuzi wa Mashairi. Nairobi:


Standard Textbooks
116

7.0 MAREJELEO YA JUMLA

Abdalla, A. (1973): Sauti ya Dhiki Nairobi: O.U.P.

Abedi, A. (1954): Sheria za Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri Abedi Nairobi:


E.A.L.B.

Bertoncini, E.Z. (1989): Outline of Swahili Literature: Prose, Fiction and Drama
Leiden: E.J. Brill

Birch, D. (1989): Language, Literature and Critical Practice London: Routeledge

Coombes, J. (1953): Literature and Criticism Middlesex: Chatto and Windus

Daiches, D. (1981): Critical Approaches to Literature London: Hutchinson &


Company

Forster, E.M. (1927): Aspects of the Novel London: Penguin Books.

Gikandi, C. (1987): Reading the African Novel Nairobi: Heinemann


Publishers Ltd.

Hawthorn, J. (1997): Studying the Novel London: Edward Arnold

Hegel, G.W.F. (1979): Introduction to Aesthetics Oxford: Clarendon

Hochman, B. (1985): Character in Literature Ithaca : Cornell University Press.

Jones, E.D. (Mh) (1975): African Literature Today London: Heinemann

Kabira, W. (NW) Gikuyu Oral Literature Nairobi: Heinemann Publishers

Kamusi ya Kiswahili Sanifu (1981) Dar es Salaam: T.U.K.I

Kiswahili (Jarida): Majuzuu mbalimbali

Matti, G.N. (2003): Mwongozo wa Kitumbua Kimeingia Mchanga Nairobi:


Africawide Network

______ (2003): Mwongozo wa Kiu Nairobi: Africawide Network.

Mazigwa, S.A. (1991): Fasihi ya Kiswahili Peramiho: Benedictine Publications


Ndanda

Mazrui, A.M. & Syambo, B.K. (1992): Uchambuzi wa Fasihi Nairobi: E.A.E.P.
117

Mbatia, M. (Mh) (2000): Mwendawazimu na Hadithi Nyingine Nairobi: J.K.F.

Mbele, M. (1980): Viewpoints: Essays on Literature and Drama Nairobi K.L.B.

Mohamed, S.A. (1995): Kunga za Nathari ya Kiswahili Nairobi: E.A.E.P.

Msokile, M. (1992): Misingi ya Hadithi Fupi Dar es Salaam: D.U.P.

_______ (1993): Misingi ya Uhakiki Nairobi: E.A.E.P.

Muhando, P. & Balisidya, N. (1976): Fasihi na Sanaa za Maonyesho Dar es


Salaam: T.P.H.

Mulika (Jarida): Majuzuu mbalimbali

Nandwa, J. & Bukenya, A. (1983): Oral Literature for Schools Nairobi: Longhorn
Publishers.

Njogu, K. & Chimera, R. (1999): Uhakiki wa Fasihi: Nadharia na Mbinu Nairobi:


J.K.F.

Nkwera, F.M.V. (1985): Sarufi na Fasihi: Sekondari na Vyuo Dar es Salaam:


T.P. H.

Ombuge, R. & Kisia, A. (1999): Uchambuzi wa Mashairi Nairobi: standard Text


Books.

Oxford Advanced Learners Dictionary (1995): london: O.U.P

Sengo, T.S.Y. (1987): Fasihi Simulizi: Sekondari na Vyuo Dar-es-Salaam:


Nyanza Publications Agency.

Senkoro, F.E.M.K. (1982): Fasihi Dar es Salaam: Press and Publicity Centre

______ (1987): Fasihi na Jamii Dar es Salaam: Press and Publicity Centre

T.K.L.K. (1981): Misingi ya Nadharia ya Fasihi Zanzibar: TKLK

Topan, F. (1971): Uchambuzi wa Maandishi ya Kiswahili I Nairobi: O.U.P.

______ (1977): Uchambuzi wa Maandishi ya Kiswahili II Nairobi: O.U.P.

T.U.K.I (1983): Fasihi III: Makala za Semina Dar es Sallam: TUKI

Wafula, R.M. (1999): Uhakiki wa Tamthilia: Historia na Maendeleo Yake


Nairobi: J.K.F.
118

Wamitila, K.W. (2002): Uhakiki wa Fasihi: Misingi na Vipengele Vyake Nairobi:


Phoenix Publishers.

_______ (2003): Kichocheo cha Fasihi: Simulizi na Andishi Nairobi: Focus Books

Wellek & Warren (1949): Theory of Literature Harmondsworth: Penguin Books.

You might also like