You are on page 1of 3

ASILI YA UTUME WA DAMU AZIZI

Tunapoangazia namna gani Utume wa Damu Azizi ulianza hadi kutufikia sisi leo hii,
tunalazimika kuanzia pale kwenye Msalaba wa Kristo: Yohane 34:19 “Askari mmojawapo
alimchoma ubavu kwa mkuki na mara ikatoka Damu na Maji.”

Historia na Mapokeo Matakatifu yanabainisha kwa, yule askari wa Kirumi aliyemchoma


Yesu Kristo ubavu kwa mkuki na mara ikatoka Damu na Maji, aliitwa kwa jina la Longinus,
huyu askari alikuwa na chongo (jicho moja halioni) na mara baada ya kumchoma, ile Damu na
Maji, vilimmwagikia katika uso wake na vazi lake la kiaskari, kwa muujiza akapona saa ile ile
chongo na akawa anaona vizuri huku lile vazi lake likiwa limebeba Damu ya Kristo. Pia
inasemekana ndiye yule aliyesema, “Hakika yake Huyu alikuwa Mwana wa Mungu” Mathayo
27:54. Hapa tunaongelea mwaka 27 mwezi April tarehe 16 saa kenda alasiri siku ya Ijumaa Kuu.

Historia na Mapokeo Matakatifu inaendelea kutusimulia kuwa, huyu Longinus baada ya


kupokea uponyaji na kukiri ungamo la Imani kwa Yes Kristo Msulibiwa, ndiyo ulikuwa mwanzo
wa wongofu wake. Hivyo basi, aliamua kuondoka Yerusalem na kurudi kwao Roma, alipofika
huko kwao, aliwasimulia familia yake, ndugu jamaa na marafiki zake matendo Makuu ya Mungu
na hatua aliyofikia kiroho, yaan wongofu wa kweli. Huyu askari alirudi kwao Roma akiwa na
lile vazi lake la kiaskari lililomwagikiwa Damu na Maji kutoka ubavuni mwa Kristo.

Longinus huyu huko Roma alikuwa anatoka ukoo wa Savelli, na alipofika na


kuwasimulia yote yaliyotukia, akawaonesha na lile vazi jekundu lililolowanishwa kwa Damu na
Maji ya Kristo. Ukoo ukaamua kuliweka vazi hili katika sehemu maalum ya kukutanikia kusali
kwa wanaukoo wote. Vazi likawa kivutio kikubwa kwa wanaukoo wote wa Savelli na kwa watu
wengi sana. Vazi hilo kwa miaka mingi na karne nyingi, likawa sababu na kichocheo cha
kuwaunganisha na kuwakutanisha wanaukoo wote kwa pamoja ili kutolea sala na maombi yao.
Kwa muujiza na nguvu ya Damu Takatifu ya Kristo, maombi ya wanaukoo yakawa yanajibiwa
na watu kadha wa kadha waliokuwa wagonjwa, wakigusa vazi lile wanapona mara moja.

Hali hii ikaendelea hivi kwa muda mrefu na ikavuta watu wengi sana katika Heshima,
Ibada na Uchaji kwa Damu ya Kristo. Watu wakaona na kushuhudia Nguvu na Uweza wa Damu
ya Kristo katika maisha yao. Kwa bahati mbaya ukoo wa Savelli ukaanza kuisha na kutoweka
taratibu, huku tayari wakiwa wanatambua umuhimu wa lile vazi lililobeba Damu na Maji ya
Kristo Yesu, wakaona ni busara na haki kulipeleka vazi hilo kwenye mojawapo ya Makanisa ili
Ibada na Heshima kwa Damu Takatifu sana ya Kristo iendelezwe huko. Ndipo mwaka 1708
wakalikabidhi vazi hilo la thamani kubwa kwenye Kanisa la Mtakatifu Nikolausi huko Roma.

Pale katika Kanisa la Mtakatifu Nikolausi, vazi hilo likawekwa chini ya Msalaba na kwa
sababu watu walishasikia habari za vazi hilo, hivyo watu wakaitikia kwa haraka na kwa hamasa
kubwa sana, kumbe tayari katika Kanisa la Mtakatifu Nikolausi kikundi cha Waamini wachache
wakaanza kusali na kuabudu Damu ya Kristo iliyokuwa katika lile vazi. Watu wakazidi
kuongezeka na kufanya sehemu hiyo kuwa maarufu zaidi na zaidi. Hapa pia watu wakawa
wanasali na maombi yao yanajibiwa mara moja, lakini pia waliokuwa wagonjwa na wenye shida
mbalimbali za kimwili, walipogusa vazi lile tu, wakapona mara. Kanisa la Mtakatifu Nikolausi
likazidi kupata umaarufu lakini zaidi sana, vazi na Damu ya Kristo likakoleza Imani kwa watu.

Ilipotimia miaka 100 tangu vazi hilo kukabidhiwa kwenye Kanisa la Mtakatifu Nikolausi
yaan 8.12.1808, Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, walifanya Jubilei na
sherehe kubwa. Mwaka huu msimamizi wa Kanisa la Mtakatifu Nikolausi na mlezi wa kikundi
cha Waamini wenye Ibada na Heshima kwa Damu Takatifu sana ya Yesu Kristo, ni Padre mzee
na mcha Mungu Fransisko Albertini ambaye tayari ameshafahamiana na Padre kijana kabisa
wa miezi mitano Gaspar del Bufalo (Upadrisho 31.7.1808), ambaye pia ni Baba wa kiroho wa
Gaspar del Bufalo na Padre Fransisko Albertini amebeba maono na utabiri kutoka kwa Sista
Maria Agnes kuhusu Padre Gaspar del Bufalo. Padre huyu kijana tayari ameshapata sifa na jina
la Mhubiri hodari.

Katika maandalizi ya Jubilei hiyo ndipo Fransisko Albertini anawazawaza amualike nani
ili aje awafundishe Waamini wenye hiyo Ibada na Heshima kwa Damu Azizi; ndipo anamualika
mwanae wa kiroho Padre Gaspar del Bufalo kuja kuwahubiria na kuwafundisha kuhusu Damu
Takatifu sana ya Yesu. Padre Gaspar del Bufalo anafika Kanisa la Mtakatifu Nikolausi na
anahubiri na kufundisha kwa kina na mapana kuhusu Damu Takatifu sana ya Yesu na
anawavutia watu wengi sana. Anachochea moto kwa watu kuipenda Damu Takatifu sana ya
Yesu, Waamini wanakuwa na hamasa zaidi na siku hiyo hiyo ya tarehe 8.12.1808 wanaanzisha
rasmi Ushirika wa Damu Azizi (Confraternity of the Most Precious Blood) katika Kanisa la
Mtakatifu Nikolausi wakijikita katika kuabudu Damu Azizi ya kwenye vazi la askari Longinus,
ambaye sasa ni Mtakatifu.

Baada ya hapo Ushirika huu unaenea na kuambukizwa taratibu katika Makanisa na


Parokia zingine za Roma na watu wengi zaidi wanaongezeka katika Ibada hii adhimu kwa Damu
Azizi ya Yesu Kristo, hatimaye ukaitwa Ushirika Mkuu wa Damu Azizi ya Kristo (Arch-
confraternity of the Most Precious Blood) chini ya uongozi na ulezi wa Padre Fransisko Albertini
huku akimtumia Padre Gaspar del Bufalo kama mkufunzi wa Ushirika huu. Ushirika huu Mkuu
umeendelea kuenea hatua baada ya hatua na mwaka hata mwaka, watu Walei na Waklero
wakijiunga na hatimaye ndiyo ukazaa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Kristo hapo
tarehe 15.8.1815. Shirika letu ni tunda halisi la Utume wa Damu Azizi ya Kristo na huo Ushirika
ndiyo sasa unaitwa Chama cha Utume wa Walei wa Damu Azizi ya Yesu Kristo au Unio Sanguis
Christi (USC).

Kadiri Shirika lilivyozidi kuenea na kukua, ndivyo Chama cha Utume wa Damu
kilivyozidi kuenea na kusambaa, kwani Mtakatifu Gaspar del Bufalo anasisistiza hili kwamba,
popote alipo Mmisionari wa Damu Azizi ya Kristo, ni lazima asisitize Ibada kwa Damu Azizi na
awavutie na kuwaalika Walei waanzishe na wajiunge katika Chama cha Utume wa Damu Azizi.
Hii imepelekea kuwa na Chama cha Utume wa Damu Azizi hata sasa katika maeneo yetu
tunayofanya utume. Utume wa Damu umetufikia hata leo hii sisi kwa juhudi kubwa za Mtakatifu
Longinus, Padre Fransisko Albertini, Mtakatifu Gaspar del Bufalo, Mtumishi wa Mungu Yohane
Merlin na wengine wengi ambao wamekuwa wakereketwa wa Ibada kwa Damu Azizi ya Kristo.

Hivi ndivyo asili na chanzo cha Chama cha Utume wa Damu Azizi kilivyoanza na
kilivyoenea duniani kote. Tunaishukuru Damu Takatifu sana kwa kutuunganisha watu kutoka
kila kabila, lugha, jamaa na taifa ili tumtumikie mungu wetu katika kuiabudu na kuitukuza damu
Takatifu sana ya Yesu, Ufunuo wa Yohane 5:9. Shime kwa Mwanautume wa Damu Azizi ya
Kristo, jua asili yako, jua canzo chako na jua thamani yako kuwa umekombolewa si kwa fedha
wala dhahabu vyenye kuharibika, bali kwa Damu ya Mwana wa Mungu, 1 Petro 1:17-19. Hii
ikufanye usikose bidii katika kuiabudu na kuitukuza Damu Takatifu ya Yesu katika maisha yote.

You might also like