You are on page 1of 40

KATIBA INAYOPENDEKEZWA

Maudhui ya Msingi

1.0 UTANGULIZI

chakato wa kutunga Katiba ya Jamhuri


ya Muungano wa Tanzania umefikia
hatua ya wananchi kuipigia kura Katiba
Inayopendekezwa, iliyopitishwa na Bunge Maalum
tarehe 4 Oktoba, 2014. Awali, Tume ya Mabadiliko
ya Katiba ilitoa Rasimu ya Kwanza tarehe 3
Juni, 2013 na Rasimu ya Pili ilitolewa tarehe 30
Desemba, 2014 na kuwasilishwa kwenye Bunge
Maalum tarehe 21 Februari, 2014.
Baada ya Bunge Maalum kukamilisha majukumu
kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
ya mwaka 2011, tunda lililozaliwa ni KATIBA
INAYOPENDEKEZWA. Hatua inayofuata ni ya
wananchi kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa.
Hivyo basi, kwa mujibu wa sheria,
wananchi ndiyo wenye uamuzi na kauli
ya mwisho juu ya upatikanaji wa Katiba
Mpya.
Toleo hili linalenga kujenga na kuimarisha uelewa
wa wananchi kuhusu Katiba Inayopendekezwa ili
kufahamu maudhui mapya na yale yaliyoboreshwa
ikilinganishwa na yaliyomo katika Katiba ya
mwaka 1977, na kuwawezesha Watanzania wote
kuielewa Katiba Inayopendekezwa ili kufanya
uamuzi sahihi wakati wa upigaji kura ya maoni
ifikapo Aprili 30, 2015.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

2.1 Sura ya Kwanza


Sura ya kwanza ina maudhui ya jumla yafuatayo:

a) Alama na Sikukuu za Taifa (Ibara ya 3)



Bendera ya Taifa

b) Lugha ya Taifa na
Mawasiliano Mbadala
(Ibara ya 4)

Katika nchi yetu tumekuwa na alama za


utambulisho kama vile bendera, nembo na wimbo
wa taifa. Hizi hazikuwahi kuwekwa ndani ya Katiba
ingawaje zinatawaliwa na sheria husika. Katiba
Inayopendekezwa imeziweka katika maudhui
ili kuhakikisha zinafahamika vema na zinapewa
ulinzi wa kikatiba. Alama hizo ni sikukuu za taifa,
bendera, wimbo wa taifa. Sikukuu za taifa ni
Siku ya Uhuru wa Tanganyika, Siku ya Mapinduzi
ya Zanzibar na Siku ya Muungano. Kuingizwa
kwa mambo haya katika Katiba siyo tu kutakuza
uelewa wa wananchi kuhusu alama muhimu za
taifa na kuzitaja wazi, bali pia kutajenga na kukuza
uzalendo wa wananchi kwa taifa lao.

Kiswahili ni hazina na tunu kwa taifa letu. Ni lugha inayobainisha


umoja na utaifa wetu. Ni lugha ambayo tunaienzi sana kama nyenzo
ya kukuza mshikamano wa kitaifa na maelewano ndani ya jamii zetu.
Katiba Inayopendekezwa imetambua umuhimu huu na sasa Kiswahili
kinatajwa ndani ya Katiba. Kwa mnasaba huu, pamoja na kuwa lugha
ya taifa, Katiba Inayopendekezwa inaelekeza Kiswahili kutumika katika
mawasiliano rasmi ya kitaifa na kiserikali.

Nembo ya Taifa

Katika jamii yetu tunao watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali unaoathiri
fursa zao za kupata mawasiliano kimaandishi au kwa alama. Kwa kutambua
hili, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, Katiba Inayopendekezwa
inataja lugha ya alama kwa viziwi, na lugha ya alama mguso kwa viziwi
wasioona kuwa lugha rasmi za mawasiliano. Hii ni hatua kubwa katika
kuhakikisha kwamba ndugu zetu wenye ulemavu wanapata haki zao za aina
mbalimbali ikiwamo haki ya kuwekewa mazingira imara ya kupata na kufanya
mawasiliano kwa lugha muafaka kwao.
KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

c) Tunu za Taifa (Ibara ya 5)


Katiba Inayopendekezwa imeainisha


tunu za taifa. Tunu ni kitu adhimu, ni
kitu cha pekee, ni hidaya, ni zawadi. Ni
kitu ambacho kwa muktadha wa ibara
hii ni zawadi pekee kwa taifa letu. Hivyo
Katiba Inayopendekezwa inazitaja tunu za
taifa kwa nia ya kulitanabahisha taifa letu
umuhimu wa kuzienzi na kuzilinda kama
mboni ya jicho. Tunu zinazotajwa ni lugha
ya Kiswahili, Muungano, utu na udugu,
na amani na utulivu. Tunu hizi zitakuwa
muhimili mmojawapo wa kujenga umoja
na utangamano wa kitaifa.

d) Misingi ya Utawala Bora


(Ibara ya 6)

Mara kadhaa tumesikia kilio cha wananchi


wa ngazi zote wakitaka nchi yetu iwe imara
na madhubuti katika kuweka na kuzingatia
utawala bora. Ibara ya 6 inaiweka wazi misingi
ya utawala bora kama masharti ya kufuatwa
na viongozi na watumishi wa umma. Kuiweka
misingi hii katika ibara ya 6 (na siyo ibara ya 5
inayohusu tunu za taifa) ni kuifanya iwe kipimo
cha utendaji na utumishi wa umma. Huu
utakuwa ni wajibu na si hiyari ya mtumishi wa
umma kuamua kama anaienzi misingi hiyo
au la, tofauti na kama ambavyo angeweza
kuzienzi tunu zilizomo kwenye ibara ya 5, lakini
zisingeweza kuchukuliwa kama kigezo cha
kupima uwajibikaji na utendaji wake kwa umma
endapo atashindwa kuizingatia.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

e) Mamlaka ya Wananchi
(Ibara ya 7)

Nchi yoyote inayoamini katika


demokrasia na utawala wa kisheria ni
sharti itambue mamlaka ya wananchi
wake. Katiba Inayopendekezwa
inazingatia ukweli kwamba wananchi
ndiyo msingi na chimbuko la mamlaka
yote ya uendeshaji na utawala wa nchi.
Katiba Inayopendekezwa inatamka wazi
kuwa Serikali zote mbili yaani Serikali ya
Muungano (SMT) na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar (SMZ), zitapata mamlaka na
madaraka yake kutoka kwa wananchi.
Kwa msingi huu Serikali itawajibika
kuhakikisha kwamba kunakuwepo
mifumo thabiti inayolenga kuwashirikisha
wananchi kikamilifu katika shughuli zote
za uendeshaji wa taifa lao.

f) Ukuu na Utii wa Katiba


(Ibara ya 9)

Wakati wote wa maisha


ya taifa letu
tumekuwa na
ufahamu kwamba
Katiba ndiyo Sheria
mama, Katiba ndiyo
chimbuko na dira ya
taifa. Ndiyo msingi
wa sheria zote. Katiba
Inayopendekezwa
inaubainisha ukuu huu
katika ibara ya 9.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

2.2 Sura ya Pili


Sura ya pili inatoa dira ya mambo ambayo yataongoza maudhui ya
Katiba na sheria nyingine zote zitakazotungwa ndani ya Jamhuri ya
Muungano. Sura hii ina maudhui ya jumla yafuatayo:
a) Malengo Makuu
(Ibara ya 11 15)

Lengo la ujumla la Katiba


inayopendekezwa ni kulinda, kuimarisha
na kudumisha haki, usawa, udugu, amani,
umoja na utangamano wa wananchi kwa
kuzingatia ustawi wao na kujenga taifa
huru lenye demokrasia, utawala bora,
maendeleo endelevu na kujitegemea.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

Pamoja na lengo la ujumla, Katiba


Inayopendekezwa imebainisha kwa
kina malengo mengine makuu ya
Serikali katika Nyanja za kisiasa,
kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Umuhimu wa malengo haya ni
kutoa dira katika kupanga na
kutekeleza mikakati mbalimbali ya
maendeleo ya nchi yetu.

b)


Dira ya Maendeleo, Mipango na Utekelezaji


wa Malengo ya Taifa (Ibara ya 16 21)

Katika taifa letu tumekuwa na mipango mingi ya maendeleo.


Mipango hii, pamoja na kuainisha mwelekeo na matarajio ya
nchi yetu, haikuwahi kuwekewa msisitizo wa kikatiba. Katiba
Inayopendekezwa inaainisha Dira ya Maendeleo ya Taifa.
Dira ya Maendeleo ya Taifa ndiyo itakayokuwa msingi mkuu
katika kutekeleza mipango yote ya maendeleo na kukuza
ustawi wa taifa letu na watu wake wote.
Katika kuimarisha mwelekeo mpya wa maendeleo ya nchi
yetu, Katiba Inayopendekezwa inatambua umuhimu wa
shughuli za utafiti wa maendeleo kama msingi wa kukuza
uchumi na kuimarisha sekta nyingine za taifa.
Nchi yetu hivi sasa inayo Tume ya Mipango ya Taifa. Chombo
hiki sasa kimetambuliwa kikatiba kama chombo cha
kupanga na kusimamia utekelezaji wa malengo ya kiuchumi
na ya kijamii.

Katika kuimarisha mchango


wa sayansi na teknolojia, Tume
ya Sayansi na Teknolojia sasa
itakuwa chombo cha kikatiba
cha kusimamia, kuratibu, kutafiti,
na kushauri masuala ya sayansi
na teknolojia nchini. Hatua hizi
zote zinalenga kuweka mazingira
madhubuti ya kikatiba na
kisheria yatakayoongeza kasi ya
maendeleo katika nchi zetu kwa
kutumia sayansi, teknolojia na
utafiti.

c) Sera ya Mambo ya Nje


(Ibara ya 22)

Kwa sasa nchi yetu inayo Sera


ya Mambo ya Nje. Katika
Katiba Inayopendekezwa
Sera hiyo imeboreshwa
zaidi ili kuhakikisha kwamba
inatekelezwa kikamilifu kwa
kulinda maslahi ya taifa,
kukuza maendeleo na kuleta
ushirikiano wenye tija kwa
nchi yetu.
KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

2.3 Sura ya Tatu

ura hii ni mpya kabisa. Ni mara ya kwanza kuwa na


vipengele ndani ya Katiba vinavyogusa rasilimali kuu za
taifa letu na kuziwekea ulinzi wa kikatiba kwa manufaa
ya wananchi. Ibara za mwanzo za Katiba Inayopendekezwa
zimeainisha dira na matarajio ya taifa letu katika Nyanja
mbalimbali za maendeleo. Sura ya tatu inaainisha ile dhana
inayokubalika duniani kote kwamba msingi mkuu wa
maendeleo ya taifa lolote ni kujiletea maendeleo kwa kutumia
rasilimali zake. Sura ya tatu inaainisha baadhi ya rasilimali za
msingi za nchi yetu kama vile ardhi, maliasili na madini.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

Ardhi, Maliasili na Mazingira


(Ibara ya 23 27)

Katiba Inayopendekezwa inataja wazi


kuwa ardhi ndiyo rasilimali kuu kwa ajili
ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na
ustawi wa nchi na watu wake. Hivyo,
Serikali zetu mbili (SMT na SMZ) zitaweka
mipango bora ya matumizi endelevu
ya ardhi kwa faida ya kizazi cha sasa na
vizazi vijavyo.

Vile vile, ili kuhakikisha kwamba ardhi


inawanufaisha wananchi, haki ya kumiliki
ardhi inatajwa kuwa ni kwa raia wa
Tanzania pekee, na mtu ambaye siyo raia
wa Tanzania atakuwa na haki ya kutumia
ardhi kwa uwekezaji na maendeleo
mengine ya kiuchumi na makaazi.

Ifahamike vema kwamba haki ya kumiliki


ardhi na mali nyingine ni ya wananchi wote.
Hata hivyo, wanawake katika baadhi ya jamii
zetu wamekosa kuifaidi haki hii kikamilifu.
Katiba Inayopendekezwa imeona umuhimu
wa kuwawekea wanawake ulinzi wa kikatiba
katika eneo hili. Hivyo kwa mujibu wa ibara
ya 23(2)(d) mwanamke atakuwa na haki
sawa na mwanaume ya kupata, kumiliki,
kutumia, kuendeleza na kusimamia ardhi.
Ni kwa mara ya kwanza haki hii inatajwa
kwa ufasaha wa aina yake.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

Jamii yetu ina utajiri wa kuwa na makundi


mbalimbali yenye mahitaji yanayotofautiana.
Katiba Inayopendekezwa imetambua haki
za makundi haya ya kumiliki, kutumia,
kuendeleza na kuhifadhi ardhi kwa makundi
ya wakulima, wavuvi, wafugaji, wachimbaji
madini na makundi madogo kwa shughuli
zao mbalimbali za kila siku. Haki hii itakuwa
ni kwa Watanzania wote.

Hata hivyo, na kama ilivyo sasa, Serikali


inaweza kulazimika kutumia ardhi au
sehemu ya ardhi kwa ajili ya maendeleo ya
kiuchumi na ya kijamii yenye maslahi mapana
ya nchi. Katika mazingira hayo, Katiba
Inayopendekezwa inaeleza wazi kwamba
Serikali itakuwa na wajibu wa kuweka
utaratibu wa kisheria kwa ajili ya malipo ya
fidia stahiki kwa mmiliki wa ardhi hiyo.

10

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

Kuhusu maliasili za nchi, Katiba


Inayopendekezwa imetamka
kuwa maliasili zote za taifa
ikiwa ni pamoja na madini, gesi
na mafuta ni mali ya umma na
zitatumika kwa manufaa ya kizazi
cha sasa na vizazi vijavyo.

Kwa upande wa mazingira, Katiba Inayopendekezwa


inaielekeza Serikali kuweka mipango na mikakati
ya kuhakikisha matumizi endelevu, uhifadhi na
usimamizi wa mazingira na maliasili kwa manufaa ya
kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Mazingira ni uti wa mgongo wa maendeleo
stahimilivu ya nchi yeyote. Kwa kutambua hilo,
Mazingira ni mojawapo ya maeneo mapya na
muhimu yaliyopewa kipaumbele. Nchi yetu na nchi
nyingine nyingi duniani zimeshuhudia majanga
yanayotokana na mabadiliko ya tabia-nchi. Ibara hii
itatoa fursa kwa wananchi na Serikali yao kuhakikisha
panakuwa na mipango madhubuti ya kulinda
mazingira.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

11

2.4 Sura ya Nne

wa miongo kadhaa nchi yetu imekuwa na maadili ya miiko ya uongozi katika sura zake
mbalimbali. Wengi watakumbuka kwamba tumewahi kuwa na waraka uliojulikana sana
kama Mwongozo wa TANU; tumekuwa na miiko iliyotokana na Azimio la Arusha; tumekuwa
na taratibu za kiutumishi zinazoainisha miiko ya maadili ya uongozi. Yote haya yanadhihirisha
kwamba nchi yetu na watu wake hawana ugeni katika eneo hili. Ni wazi, hata hivyo, kwamba
taifa letu limekua, misingi ya haki na uhuru imepanuka, mahitaji ya leo, si mahitaji ya jana. Yote
haya yamekuwa na taathira katika kusimamia na kutekeleza miiko na maadili ya viongozi. Katiba
Inayopendekezwa imetambua haya. Hivyo katika Sura ya nne misingi thabiti ya miiko na maadili
inawekwa.
Kuwekwa kwa misingi hii ndani ya Katiba ni jambo muhimu na la lazima. Lakini ni wazi kuwa
kuwekwa kwa misingi hii ndani ya Katiba peke yake, hakutuhakikishii utekelezaji na umadhubuti
tunaoukusudia. Hivyo Katiba Inayopendekezwa inaelekeza kutungwa kwa sheria mahsusi
zitakazoweka kwa kina utaratibu wa kutekeleza misingi hiyo mikuu. Kwa mfano, msingi wa
kikatiba umewekwa kuhusu haja ya viongozi wa umma kuwasilisha serikalini zawadi mbalimbali
wanazozipata wakiwa katika utumishi wa umma. Huu ni msingi mzuri na muhimu. Lakini kwa
taratibu za uandishi wa Katiba, haiwezekani kuweka maudhui ya kina ndani ya Katiba yanayohusu
utekelezaji wa msingi huu. Hivyo pamoja na kuuweka mwiko huu wa maadili ndani ya Katiba
itakuwa muhimu kwa sheria kutungwa ili kuelekeza utekelezaji wake kwa undani. Sheria hii itahitaji
kuainisha aina za zawadi ambazo mtumishi wa umma atapaswa kuzikabidhi serikalini;
kueleza namna ya kusajili na kuweka kumbukumbu za maandishi
za zawadi hizo; kueleza zitahifadhiwa wapi,
na mamlaka gani; utunzaji
wake; matumizi yake baada
ya kukabidhiwa kwenye
mamlaka husika; zitauzwa
au zitatumikaje; ndani ya
muda gani; kwa manufaa ya
nani, na kadhalika. Haya yote
hayawezekani kukaa kwenye
Katiba na ndiyo sababu Katiba
Inayopendekezwa
inataka
maeneo yote haya yaainishwe
vizuri zaidi ndani ya sheria, tofauti
na kuwekwa kwenye Katiba pekee,
kwani asili yake Katiba haiwezi
kuweka maelekezo ya aina hii kwa
kina, haiweki katazo, wala adhabu.
Sheria ndiyo yenye uwezo wa
kufanya yote haya.

12

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

Kwa mantiki hii, sura ya nne ya Katiba Inayopendekezwa ina


maudhui ya msingi yafuatayo:

a) Maadili na Miiko ya Uongozi


na Utumishi wa Umma
(Ibara ya 28 31)

Hili ni eneo muhimu sana katika kukuza


na kuendeleza utawala bora. Katiba
Inayopendekezwa inatambua kuwa
madaraka anayopewa kiongozi wa umma
ni dhamana katika kutekeleza wajibu
wake. Hivyo, kiongozi wa umma atatumia
madaraka yake kwa:i. Kuzingatia masharti ya Katiba;
ii. Kuheshimu wananchi;
iii. Kukuza hadhi ya taifa na kulinda
heshima ya ofisi anayoitumikia; na
iv. Kukuza heshima ya ofisi kwa
wananchi

Kiongozi wa umma
atapaswa kuzingatia
yafuatayo:-


i. Kufanya uteuzi bila ubaguzi
kwa kuzingatia uwezo, sifa na
mwenendo unaofaa,
ii. Kutoa uamuzi bila kujali udugu,
ukabila, udini, rushwa, na
ubaguzi wa aina yoyote.
iii. Kutoa huduma pasipo upendeleo
na kwa kufuata maslahi ya
umma.
KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

13

Kiongozi wa umma, akiwa katika


kazi za ofisi au kazi binafsi au
amejumuika na watu wengine
atahakikisha kwamba mwenendo
wake:


i. Hauruhusu kutokea mgongano kati ya
maslahi binafsi na maslahi ya utumishi wa
umma;
ii. Haushushi hadhi ya ofisi anayofanyia kazi;
au hauruhusu matumizi ya ofisi ya umma
kwa maslahi binafsi.

14

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

Kiongozi wa umma ataheshimu na kutii


maadili ya uongozi wa umma na miiko
ya uongozi. Katiba Inayopendekezwa
inaelekeza kutungwa kwa sheria
itakayoinyambua misingi hii muhimu
na kutaja adhabu pale itakapokiukwa.

2.5 Sura ya Tano


Haki za Binadamu

uniani kote Sura ya Haki za Binadamu ina umuhimu wa pekee. Kukaa kwake ndani
ya Katiba ni kuhakikisha zinalindwa kama sehemu mojawapo ya wajibu wa dola kwa
raia. Katiba Inayopendekezwa katika Sura hii imebainisha haki zote kama zilivyo
katika Tangazo la Dunia la Haki za Binadamu la Mwaka 1948. Tofauti na baadhi ya watu
wanavyopotosha, haki hizi zinaweza kutiliwa nguvu mahakamani kwa mujibu wa Ibara ya
65(2) ya Katiba Inayopendekezwa. Sura ya pili ya Katiba Inayopendekezwa inataja malengo
muhimu ya taifa. Malengo yamewekwa kwa nia ya kutoa dira kwa Serikali na vyombo vyake
wanapopanga mikakati mbalimbali ya maendeleo. Utekelezaji wa malengo yale ni endelevu
na hivyo Serikali haipaswi kufikishwa mahakamani endapo utekelezaji wake utachelewa. Hii
ni kwa sababu malengo yale yanabainisha azma ya Serikali ya kuyazingatia katika utekelezaji
wa mpango wa maendeleo. Hakuna Katiba yoyote duniani imeweka utaratibu wa kuifikisha
Serikali mahakamani endapo malengo hayatatimia. Hivyo si sawa kusema kwamba katika
eneo lile kuna haki ambazo haziwezi kudaiwa mahakamani.

Katiba Inayopendekezwa imeingiza kizazi kipya cha haki za


binadamu na kuimarisha haki za makundi maalum kama ifuatavyo:i. Haki za Wanawake

Katiba Inayopendekezwa imewapa wanawake haki sawa na wanaume


ikiwemo haki ya kushiriki katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni
na kijamii. Katiba Inayopendekezwa imepiga marufuku vitendo vya
ukatili, ubaguzi, dhuluma, udhalilishaji, unyanyasaji na mila potofu dhidi
ya wanawake [Ibara za
12; na 57(b)]. Ibara hizi
ni za manufaa sana kwa
wanawake, hasa kwa
kuzingatia kiwango
kikubwa kilichopo cha
matukio ya ukatili na
unyanyasaji wa kijinsia
katika baadhi ya jamii
ndani ya nchi yetu.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

15

Vile vile, Katiba Inayopendekezwa


inawapa wanawake haki nyingine za
msingi zifuatazo:


16

Kushiriki bila ubaguzi katika uchaguzi na ngazi


zote za maamuzi [Ibara za 57 (c) na 129(4)].
Fursa na haki ya ujira sawa na wanaume kwa
kazi zenye sifa zinazofanana [Ibara ya 57 (d)];
Kupata huduma bora za afya ikiwemo afya ya
uzazi salama [Ibara ya 57(f )];
Haki ya kupata kumiliki mali [Ibara za 57(g),
47(1) na 23(2)]. Haki hii ni muhimu sana
katika maendeleo ya wanawake hususan
kwa sehemu ambazo wanawake wamekuwa
wakinyimwa haki ya kumiliki mali.
Ajira ya mwanamke kulindwa wakati wa
ujauzito na anapojifungua [Ibara ya 57(e)];
Haki ya kupata maji safi na salama
[Ibara ya 51];
Haki ya kusaidiana katika matunzo na malezi
ya mtoto [Ibara ya 53(1)(g)]. Hii ni fursa ye
pekee kwa wanawake ambao walikuwa
wametelekezwa na wenza wao.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

Sura hii inazungumzia haki za


binadamu kwa ujumla wake. Zipo vile
vile ibara nyingine ndani ya Katiba
Inayopendekezwa zinazosisitiza haki
za makundi mbalimbali wakiwemo
wanawake, watoto, wachimbaji
wadogo na haki za jamii wanaoishi
kutegemea uoto wa asili na mazingira
yanayowazunguka kwa ajili ya chakula,
malazi na mahitaji mengine ya maisha.
Kwa mfano katika Utangulizi wa Katiba
Inayopendekezwa, miongoni mwa
mambo ya kuzingatia katika misingi
ya utawala bora ni usawa wa jinsia
[Ibara ya 6(2)(g)]. Misingi hii ni ya
muhimu sana katika kulinda, kukuza na
kuendeleza haki za wanawake.

ii. Haki ya uhuru wa habari na


vyombo vya habari (Ibara ya 40)

Katiba Inayopendekezwa inatoa haki na


uhuru wa mtu na vyombo vya habari
kutafuta, kupata, kutumia na kusambaza
habari na taarifa sahihi. Ibara hii inaondoa
malalamiko ya muda mrefu ya wanahabari
na wamiliki na vyombo vya habari ya
kutokuwa huru katika utekelezaji wa kazi na
majukumu yao ya kila siku.

Halikadhalika, Ibara hii inaielekeza


Serikali kujiendesha kwa uwazi (Open
Government) katika utekelezaji wa
shughuli zake. Ibara hii inalenga kuwapa
wananchi haki ya kujua nini kinaendelea
ndani ya Serikali yao, uwajibikaji wake
kwa wananchi na kuimarisha dhana
nzima ya mamlaka ya wananchi
katika kusimamia Serikali. Ibara hii ni
mwendelezo wa misingi ya utawala bora
ambayo inatajwa katika Ibara ya 6.
Aidha, Ibara ya 214 ya Katiba
Inayopendekezwa inatoa fursa kwa sekta
ya habari kuanzisha tume kwa ajili ya
usimamizi, uratibu na utoaji huduma
kwa wananchi.
KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

17

iii. Haki za wafanyakazi na


waajiri (Ibara ya 45)

18

Katiba Inayopendekezwa imebainisha


haki za wafanyakazi mahali pao pa kazi.
Jambo hili litaondoa manunguniko
ya wafanyakazi kuonewa na waajiri,
kupewa ujira usiostahili kulingana na kazi
wanazozifanya na kuachishwa kazi bila
kufuata utaratibu. Hivyo, haki hii sasa
inalindwa na kupewa nguvu ya kikatiba.
Kwa upande mwingine, haki za mwajiri pia
zimeainishwa.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

iv. Haki za wakulima, wafugaji,


wavuvi na wachimba madini
(Ibara ya 46)

Kwa mara ya kwanza katika taifa letu, Katiba


Inayopendekezwa imeyatambua makundi
madogo madogo ya wakulima na wafugaji,
wavuvi na wachimba madini ambayo
mara kwa mara yamekuwa yakiathiriwa
na migogoro ya ardhi. Kimsingi, makundi
yote hayo yana maslahi yanayofanana na
kushabihiana kwa kiasi kikubwa. Kutokana
na hali hii migogoro imekuwa ikizuka mara
kwa mara kwa sababu tu ya kugombania
maslahi hayo. Katiba Inayopendekezwa
kwa kutambua na kuzingatia ukweli huo,
inazitaja na kuzitambua haki za makundi
hayo kwa nia ya kuhakikisha kwamba
maslahi yao yanalindwa.

v. Haki ya mazingira safi, afya, na maji salama


(Ibara ya 50 -51)

Hili ni eneo jipya katika muktadha wa haki mbalimbali


zinazotambuliwa duniani hivi sasa. Katika siku za nyuma
Mahakama iliwahi kutafsiri haki ya kuishi kuwa inajumuisha haki
ya mazingira safi, afya, na maji salama, lakini haikuwahi kuwekwa
ndani ya Katiba au sheria. Haki hii sasa inawekewa misingi thabiti
ya utekelezaji, Katiba Inayopendekezwa inazibainisha haki hizi
waziwazi na kuelekeza mamlaka ya nchi kuhakikisha kwamba
wananchi wanajengewa utaratibu utakaowawezesha kuishi katika
mazingira safi na salama; wanapata maji safi na salama kwa ajili ya
kujenga jamii iliyo na afya bora.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

19

vi. Haki za mtoto


(Ibara ya 53)

20

Haki za mtoto zimekuwa sehemu


ya sheria mbalimbali za nchi yetu.
Pamoja na kuwepo kwa Sheria
ya Mtoto ya mwaka 2009, Katiba
Inayopendekezwa imeimarisha
misingi ya kuzitambua haki
za mtoto kikatiba. Jambo hili
limetokana na hali halisi ya mazingira
wanayokabiliana nayo watoto katika
nchi yetu. Katiba Inayopendekezwa
inalenga kuhakikisha kwamba
zinakuwepo sheria mahsusi za
kuwalinda watoto dhidi ya ubaguzi
na unyanyasaji wa aina zote.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

vii. Haki na wajibu wa vijana


(Ibara ya 54)

Ibara hii ni mpya na ni mara ya kwanza kuwekwa


kikatiba. Katiba Inayopendekezwa inatambua haki
za vijana na wajibu walionao kwa jamii. Katiba
Inayopendekezwa inaielekeza Serikali kuhakikisha
kwamba vijana wanawekewa mazingira mazuri
ya kuwa raia wema na kupatiwa fursa za kushiriki
kikamilifu katika masuala ya kisiasa, kiuchumi,
kijamii na kiutamaduni. Sambamba na hilo, Katiba
Inayopendekezwa inaielekeza Serikali kuanzisha
Baraza la Vijana la Taifa. Baraza hili litakuwa muhimu
sana kwa vijana kutoka katika makundi mbalimbali
ya jamii kupata jukwaa la kupaza sauti zao, kujadili
changamoto mbalimbali zinazowakabili na
kushirikiana na Serikali katika kuzikabili.

viii. Haki za watu wenye ulemavu



(Ibara ya 55)

Kwa kipindi kirefu watu wenye ulemavu wamekuwa


wakikabiliwa na changamoto mbalimbali. Pamoja na
kuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha kupata
haki ya mawasiliano [Ibara ya
4(4)], Katiba Inayopendekezwa
imeainisha haki mahsusi za watu
wenye ulemavu. Baadhi ya haki
hizo ni: haki ya kuheshimiwa,
kutambuliwa na kulindwa dhidi
ya vitendo vinavyoshusha utu wa
mtu mwenye ulemavu. Vitendo
hivyo ni pamoja na ubaguzi,
uonevu, ukatili na mila potofu.


Vile vile, Katiba Inayopendekezwa
inaelekeza kwamba watu wenye ulemavu
wana haki ya kupata elimu kwa kutumia
vifaa maalum na kushiriki katika nafasi
za uwakilishi na shughuli za kijamii,
kuwekewa miundombinu na mazingira
yanayofaa yatakayomwezesha kwenda
anapotaka, kutumia vyombo vya usafiri,
kupata habari, kutumia lugha ya alama,
alama mguso, maandishi ya nukta nundu,
maandishi yaliyokuzwa, kupata ajira,
kufanya kazi na kupata huduma bora
za afya na uzazi salama. Kutambulika
kwa kundi hili kikatiba ni fursa nzuri
ya kuhakikisha kwamba taifa letu
linaondokana na vitendo ambayo vina
sura ya ukatili, ubaguzi na unyanyapaa, na
badala yake kuwapa fursa ya kujiendeleza
kisiasa, kiuchumi na kijamii.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

21

ix.

x.

22

Haki za makundi madogo katika jamii (Ibara ya 56)

Katiba Inayopendekezwa inaweka masharti ya ulinzi wa haki za makundi madogo


ikiwa ni pamoja na baadhi wanajamii wenzetu wanaoishi kwa kuwinda, kukusanya
matunda na mimea mingine ya asili. Katiba Inayopendekezwa inaainisha haja ya
kujenga mazingira yatakayoyawezesha makundi haya kushiriki katika uongozi wa
mamlaka za nchi, kupata fursa maalum za elimu, kujiendeleza kiuchumi, kupata ajira
na kutengewa maeneo ya ardhi ambayo
kwa desturi makundi hayo huyatumia kwa
makaazi na kupata riziki ya chakula.

Haki ya wazee (Ibara ya 58)


Wazee ni hazina ya taifa letu. Katiba
Inayopendekezwa inatambua umuhimu
huu wa wazee katika jamii. Ndani
ya Katiba Inayopendekezwa wazee
wanapewa fursa ya kushiriki katika
shughuli za kimaendeleo na kijamii,
kupata huduma mbalimbali na kulindwa
dhidi ya vitendo vya ukatili. Kupitia
Katiba Inayopendekezwa kutawekwa
miundombinu na mazingira bora
yatakayowawezesha kwenda wanakotaka
na kutumia vyombo vya usafiri wa umma
kwa gharama nafuu.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

xi.

Haki za Wasanii (Ibara ya 59)

Kama zilivyo haki nyingine nyingi, ni mara ya


kwanza Katiba inazianzisha haki za wasanii. Katiba
Inayopendekezwa inaonyesha hivyo katika Ibara
ya 59. Haki hizi zinajumuisha haki-miliki ambazo
zitawasaidia kulinda kazi zao za ubunifu, ufatifi
na hatimaye kukuza Sanaa, taaluma, ubunifu na
ugunduzi kwa manufaa yao binafsi na taifa kwa
jumla. Hili ni kundi muhimu katika kukuza fursa
za ajira kwa vijana na kuiletea sifa na heshima nchi
yetu kwa kutumia Sanaa na ubunifu wao. Ni kundi
ambalo lina uwezo mkubwa wa kuitangaza nchi
yetu katika Nyanja za kiuchumi, kiutamaduni na
kijamii. Hivyo, Katiba Inayopendekezwa inajenga
mazingira mazuri ya kundi hili kuthaminiwa,
kuendelezwa na kulindwa.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

23

2.6 Sura ya Sita


Sura ya sita ina maudhui ya jumla yafuatayo:-

a) Uraia katika Jamhuri ya


Muungano
(Ibara ya 70 71)

24

Suala la uraia limetamkwa kwenye


Katiba Inayopendekezwa. Katiba
Inayopendekezwa imebainisha aina
za uraia katika Jamhuri ya Muungano
ya Tanzania kuwa ni uraia wa kuzaliwa
na uraia wa kuandikishwa.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

b) Hadhi maalum ya watu wenye


asili au nasaba ya Tanzania
(Ibara ya 72)

Katiba Inayopendekezwa inatoa nafasi kwa


mtu yeyote mwenye asili au nasaba ya Tanzania
na ambaye alikoma kuwa raia wa Jamhuri ya
Muungano kwa kupata uraia wa nchi nyingine,
kuwa na hadhi maalum atakapokuwa katika
Jamhuri ya Muungano. Hii itawafanya watu
wenye sifa hizo kupata stahili na fursa ambazo
ni tofauti na zile za wageni wawapo ndani ya
nchi ya asili yao.

2.7 Sura ya Saba


Sura ya saba ina maudhui ya jumla yafuatayo:

a) Mahusiano kati ya
Serikali ya Jamhuri ya
Muungano ya Tanzania
na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar (Ibara ya 77)

b)

Katika kuhakikisha kwamba


changamoto za Muungano
zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu,
Katiba Inayopendekezwa inaweka
utaratibu wa mahusiano baina ya
Tanzania Bara na Zanzibar kwa
lengo la kukuza umoja, na kulinda
maslahi ya Taifa na maendeleo ya
wananchi.

Wajibu wa viongozi kulinda Muungano (Ibara ya 78)


Katiba Inayopendekezwa imetambua wajibu wa pekee wa viongozi
wakuu wa nchi kuulinda na kuutetea Muungano. Viongozi hao ni
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Rais wa Zanzibar,
Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania
na Makamu wa Rais wa
Zanzibar. Katika kutekeleza
majukumu yao, viongozi
hao wanapewa jukumu la
kuhakikisha kuwa wanatetea,
wanalinda, wanaimarisha na
kudumisha umoja wa Jamhuri
ya Muungano ya Tanzania.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

25

2.8 Sura ya Nane


Sura ya nane ina maudhui ya jumla yafuatayo:a) Hadhi ya Rais wa Zanzibar
(Ibara ya 99)

Katiba Inayopendekezwa imerejesha


hadhi ya Rais wa Zanzibar kuwa
Makamu wa Pili wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Suala hili
linajibu na kutatua changamoto ya
muda mrefu kuhusu nafasi na hadhi
ya Rais wa Zanzibar katika Muungano.
Awali katika Hati ya makubaliano ya
Muungano Rais wa Zanzibar alipewa
hadhi na nafasi ya kuwa Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano.

b) Idadi ya Mawaziri
(Ibara ya 115)

26

Kwa mara ya kwanza


inapendekezwa kuwepo
kwa ukomo wa idadi
ya mawaziri kikatiba.
Hivi sasa kuundwa kwa
Wizara na uteuzi wa
mawaziri hakuongozwi
na sheria yoyote. Katiba
Inayopendekezwa
imeweka ukomo wa idadi
ya mawaziri wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano isiyozidi arobaini. Ni dhahiri kwamba jambo
hili litaipunguzia Serikali gharama za uendeshaji na kurahisisha
usimamizi wa shughuli za Serikali.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

c) Wananchi kuihoji Serikali


(Ibara ya 116)
Muundo wa Bunge unaopendekezwa ni ule ambao mawaziri
wanatokana na wabunge. Katiba Inayopendekezwa inaendeleza
utaratibu huu.
Huu ni utaratibu unaohakikisha kwamba
Serikali inawajibika moja kwa moja kwa wananchi. Ni utaratibu
unaowawezesha wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi
kupata fursa ya kuisimamia Serikali kupitia maswali Bungeni na
kuhoji utendaji wake. Utaratibu huu unaakisi vizuri falsafa iliyomo
kwenye Ibara ya 7 ambayo inaeleza kwamba msingi wa mamlaka
yote ya nchi ni wananchi wenyewe.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

27

2.9 Sura ya Tisa


Sura ya tisa ina maudhui ya jumla yafuatayo:a) Uhusiano na Uratibu wa Mambo ya Muungano
(Ibara za 127 128)
Katiba Inayopendekezwa inaimarisha Muungano wetu kwa
kuanzisha Tume ya Usimamizi na Uratibu wa Mambo ya
Muungano. Chombo hiki, pamoja na mambo mengine, kitakuwa
na jukumu la kukuza na kuratibu ushirikiano baina ya Serikali
ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar. Mojawapo ya malengo ya uratibu huu ni kuimarisha
ushirikiano na uhusiano baina ya Serikali hizi mbili na kukuza
kiwango cha utoaji huduma kwa wananchi wote.

Kwa utaratibu wa sasa ipo Kamati


inayoshughulikia masuala ya
Muungano ambayo inaongozwa
na Makamu wa Rais. Kwa Katiba
Inayopendekezwa chombo hiki sasa
kitakuwa na nguvu ya kisheria na
hivyo kuweka mfumo madhubuti
zaidi wa kushughulikia changamoto
za Muungano na pia kuratibu
masuala mengine yanayohusiana
na ushirikiano kati ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
na kati ya Tanzania Bara na Tanzania
Zanzibar kwa ujumla wake.

28

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

2.10 Sura ya Kumi


Sura ya kumi ina maudhui ya jumla yafuatayo:
a)

Muundo wa Bunge Ibara ya 129.


Katiba Inayopendekezwa imeweka ukomo wa idadi
ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano. Idadi ya
wabunge imetajwa kutopungua mia tatu arobaini
(340) na kutozidi mia tatu tisini (390). Hatua hii
itasaidia sana kudhibiti ongezeko la majimbo
ya uchaguzi na hivyo kupunguza gharama za
uendeshaji. Idadi inayotajwa itajumuisha wabunge
wote wanaotoka Tanzania Bara na wale wanaotoka
Zanzibar. Katiba Inayopendekezwa inamtaka Rais
kuteua watu watano kutoka katika kundi la watu
wenye ulemavu kuwa wabunge. Hii ni fursa nzuri
ya kuhakikisha kwamba kundi hili muhimu linapata
uwakilishi wa uhakika Bungeni.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

29

2.11 Sura ya Kumi na Mbili


Sura ya Kumi na Mbili ina maudhui ya jumla yafuatayo:

a) Mahakama ya Juu
(Ibara ya 171 174)

30

Mahakama ya Juu ya Jamhuri ya Muungano


ndiyo itakuwa chombo cha mwisho cha utoaji
haki nchini. Hiki ni chombo kipya ndani ya Katiba
Inayopendekezwa na imeongezwa ili kupanua wigo
wa utoaji haki na kukifanya kuwa chombo chenye
mamlaka ya mwisho katika kutatua mashauri ya
aina mbalimbali nchini. Chombo hiki pia kitakuwa
na mamlaka ya kushughulikia mashauri yanayohusu
matokeo ya uchaguzi wa Rais na kusikiliza mashauri
baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhusu
tafsiri ya Katiba.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

2.12 Sura ya Kumi na Tatu


Sura ya Kumi na tatu ina maudhui ya jumla yafuatayo:

a)

Tume ya Utumishi wa Umma


(Ibara ya 210 212)


Katiba Inayopendekezwa inaanzisha Tume ya
Utumishi wa Umma ambayo itakuwa chombo cha
juu chenye mamlaka ya nidhamu na uratibu wa
mambo yote ya utumishi wa umma katika Jamhuri ya
Muungano. Pamoja na kazi zake nyingine, Chombo
hiki kitahakikisha kwamba kunakuwepo uwakilishi
na uwiano mzuri wa watumishi wa umma kutoka
Tanzania Zanzibar na Bara.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

31

2.13 Sura ya Kumi na Nne


Sura ya Kumi na Nne ina maeneo mapya ambayo hayamo katika
Katiba ya Mwaka 1977 maeneo haya ni:

32

Mgombea huru
(Ibara ya 216)
Katiba Inayopendekezwa inaanzisha
utaratibu wa kuwa na mgombea huru
katika nafasi mbalimbali za uchaguzi
kwa ngazi zote. Hili ni jambo jipya
linaloonesha kukua na kukomaa kwa
demokrasia katika nchi yetu.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

Tume Huru ya Uchaguzi


(Ibara ya 217 223)
Katiba Inayopendekezwa imeanzisha
Tume Huru ya Uchaguzi. Kuanzishwa
kwa chombo hiki kunatoa majawabu
ya changamoto na maswali ya muda
mrefu kuhusu uhuru wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi katika kusimamia na
kuendesha chaguzi hapa nchini.

2.14 Sura ya Kumi na Tano


Sura ya Kumi na Tano ina maudhui ya jumla yafuatayo:

a)


Chombo cha Kuzuia na Kupambana na Rushwa


(Ibara ya 249)
Kwa mara ya kwanza nchini, Katiba Inayopendekezwa inaelekeza
kuanzishwa kwa chombo cha kikatiba cha kuzuia na kupambana na
rushwa. Lengo ni kuhakikisha nchi yetu inakuwa na chombo huru
na chenye nguvu ya kupambana na rushwa ili kujenga taifa lenye
uadilifu na kuimarisha utawala bora.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

33

SEHEMU YA TATU
3.0 UTATUZI WA CHANGAMOTO ZA MUUNGANO
Sehemu hii ya waraka ni mahsusi kwa ajili ya kubainisha
namna ambavyo changamoto za Muungano zimepatiwa
ufumbuzi ndani ya Katiba Inayopendekezwa.

angu kuasisiwa kwa Muungano wetu mwaka 1964, kumekuwepo na


changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa Mambo ya Muungano.
Changamoto hizo zimekuwa zikishughulikiwa na tume na kamati
mbalimbali zilizokuwa zinaundwa katika vipindi tofauti vya uongozi wa
nchi yetu. Miongoni mwa tume na kamati hizo ni Tume ya Jaji Nyalali (1991),
Kamati ya Amina Salum Ali (1992), Kamati ya Shellukindo (1994), Kamati ya
Jaji Mark Bomani (1995), Kamati ya Shamhuna (1977), Kamati ya Jaji Kisanga
(1998), Kamati ya Ramia (2000) na Kamati ya Pamoja na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (2006).

Aidha, hadi mchakato wa kuandika Katiba mpya


unaanza, changamoto kubwa zilizokuwa zinaendelea
kutafutiwa ufumbuzi ni kama ifuatavyo:






34

Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asilia;


Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje;
Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za
Muungano;
Rais wa Zanzibar kuondolewa kuwa Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano;
Orodha ya mambo ya Muungano kuongezeka
kutoka mambo 11 mpaka 22;
Uwezo wa SMZ kukopa ndani na nje ya nchi; na
Maamuzi kuhusu utatuzi wa changamoto za
Muungano kukosa nguvu za kisheria.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

Katiba Inayopendekezwa imejielekeza kutatua


changamoto hizo kama ifuatavyo:
a) Kuanzishwa kwa Tume ya Mambo ya Muungano

Ibara ya 127 ya Katiba Inayopendekezwa inaanzisha Tume ya Usimamizi na Uratibu wa mambo ya


Muungano. Tume hii, pamoja na mambo mengine, itakuwa na jukumu maalum la kuwezesha uratibu
na ushirikiano wa sera, sheria, mipango na mikakati baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Uratibu huu utasaidia sana kubainisha changamoto
zozote zitakazojitokeza katika kutekeleza shughuli za Muungano. Itakumbukwa kwamba hivi sasa
ipo Kamati inayoongozwa na Makamu wa Rais ya kushughulikia changamoto na masuala mengine
ya Muungano. Kamati hii haikuanzishwa kikatiba, hivyo ipo mifano ambayo utekelezaji wa maamuzi
ya Kamati ulitegemea sana uhusiano mzuri kati ya watendaji na taasisi husika za pande zote mbili.
Uhusiano mzuri na utashi wa kisiasa ni mambo muhimu. Hata hivyo, Katiba Inayopendekezwa
imeona hii haitoshi. Hivyo, mojawapo ya malengo ya kuanzishwa kwa Tume hii ni kujenga misingi
imara ya kikatiba ya utekelezaji wa shughuli za Muungano na kuyapa nguvu ya kisheria maamuzi
mbalimbali yatakayotolewa na Tume hii.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

35

b) Nafasi na hadhi ya Rais wa


Zanzibar


Kwa mujibu wa Hati ya Makubaliano ya
Muungano, Rais wa Zanzibar alikuwa
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
ya Tanzania. Hata hivyo, kufuatia mabadiliko
mbalimbali yaliyotokea katika nchi yetu,
hususani kurejeshwa kwa mfumo wa vyama
vingi vya siasa mwaka 1992, nafasi ya Rais wa
Zanzibar kama Makamu wa Rais iliondolewa.
Baada ya mabadiliko mbalimbali ya kisiasa na
kikatiba (hususan kwa upande wa Zanzibar,
na uzoefu uliopatikana wa namna bora zaidi
ya kuimarisha Muungano wetu), Katiba
Inayopendekezwa inarejesha nafasi ya Rais wa
Zanzibar kama Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano kupitia Ibara ya 99(b).

36

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

c) Ushirikiano na uhusiano wa Zanzibar na


Taasisi za Kimataifa

Jambo hili ni miongoni mwa mambo ambayo


yalionekana kuwa moja ya changamoto zilizoukabili
ustawi wa Muungano na maendeleo ya pande zote mbili
za Muungano wetu. Katiba Inayopendekezwa inatambua
umuhimu huu na haja ya kuimarisha mamlaka ya
Zanzibar kwa mambo yasiyo ya Muungano yanayohusu
Zanzibar. Katiba Inayopendekezwa inajibu hoja hii
kupitia Ibara ya 76. Kwa mujibu wa ibara hii, Zanzibar
itakuwa na uwezo na uhuru wa kuanzisha uhusiano au
ushirikiano na jumuiya au taasisi yoyote ya kikanda au
kimataifa kwa mambo yanayoihusu.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

37

d) Uwezo wa Zanzibar kukopa ndani na nje ya nchi



Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977, inaweka mamlaka ya kukopa


nje ya nchi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Katika muktadha wa
kuimarisha uwezo na uhuru wa Zanzibar kwa shughuli za maendeleo yake,
Katiba Inayopendekezwa katika Ibara ya 261 inatoa mamlaka kwa SMZ kukopa
fedha ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano bila ya kulazimika kupitia Serikali
ya Muungano. Kwa minajili hii, endapo mkopo husika utahitaji dhamana, basi
Serikalii ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania itatoa dhamana kwa mkopo
unaoombwa. Ni wazi utaratibu huu utarahisisha sana upatikanaji wa mikopo
kwa maendeleo na ustawi wa Zanzibar.

e) Orodha ya Mambo ya Muungano



38

Muungao wetu ulianza kwa kuainisha mambo 11 ambayo ndiyo yaliyokuwa


msingi wa ushirikiano kati ya iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri
ya Watu wa Zanzibar. Hadi leo ushirikiano umekua na kufikia mambo 22.
Katika kipindi cha miaka takriban hamsini ya Muungano wetu mahitaji na
mazingira yamebadilika. Pande zote mbili za Muungano zimejiimarisha kwa
namna mbalimbali katika maendeleo yao. Kwa kuzingatia ukweli huu, Katiba
Inayopendekezwa inaainisha masuala 16 badala ya 22 ya sasa [Ibara ya 74(3)].
Miongoni mwa mambo yaliyopunguzwa ni suala la utafutaji na uchimbaji wa
mafuta na gesi asilia ambalo kipekee lilionekana kuwa changamoto kubwa
katika ustawi na maendeleo ya taifa letu.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA - Maudhui ya Msingi

f) Ajira katika Taasisi za Muungano



Mojawapo ya changamoto zilizojitokeza katika uhai wa Muungano


wetu ni suala la ajira ya wananchi wa pande zote mbili katika taasisi za
Muungano. Pamoja na Tume ya Utumishi wa Umma kuwa na jukumu la
ujumla katika eneo hili, Katiba Inayopendekezwa katika Ibara ya 128(1)(f )
na 128(3) inataja wazi kwamba Tume ya Usimamizi na Uratibu wa Mambo
ya Muungano itakuwa vile vile na jukumu la kusimamia uwakilishi wa
pande zote mbili za Muungano ndani ya ajira ya utumishi wa Jamhuri ya
Muungano. Aidha, Tume itaweka utaratibu utakaowezesha uteuzi wa
viongozi na watumishi katika taasisi au Wizara za Muungano kufanyika
kwa kuzingatia uwakilishi wa pande zote mbili za Muungano. Hii ni hatua
muhimu ya kuleta uwiano murua, kupata mchango chanya wa wananchi
wote katika ajira na kuuimarisha Muungano wetu.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA -Maudhui ya Msingi

39

Tanzania Women Cross-Party Platform (T-WCP ULINGO)


P.O Box 65454, Dar es Salaam
Email: twcpulingo@gmail.com
Tel: +255 784 600416

You might also like