You are on page 1of 2

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu: 255-262961500/1 OFISI YA RAIS,
Nukushi: 255-262961502 IKULU,
1 BARABARA YA JULIUS NYERERE,
Baruapepe: press@ikulu.go.tz
CHAMWINO,
Tovuti : www.ikulu.go.tz
S.L.P 1102,
40400 DODOMA.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 17 Februari, 2020 amezindua kipindi cha 2 cha awamu ya 3 ya mpango wa
kunusuru kaya masikini wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III), katika ukumbi
wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Sherehe za uzinduzi huo zimehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu


Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Marais
Wastaafu Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi, Mhe. Benjamin William Mkapa na Mhe.
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mabalozi, Viongozi Wakuu
wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini na Viongozi wa vyama vya Siasa.

Akizungumza katika sherehe hizo, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Marais


Wastaafu wa kuasisi na kuiendeleza TASAF ambayo imetoa mchango mkubwa katika
kupunguza umasikini hapa nchini.

Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa juhudi za kukabiliana na umasikini hapa nchini
ikiwemo mpango wa TASAF zimepata mafanikio makubwa ambapo takwimu za Ofisi
ya Taifa ya Takwimu zimeonesha kuwa kati ya mwaka 1990/91 na 2017/18 umasikini
wa mahitaji ya msingi (Basic Needs) umepungua kutoka asilimia 39.0 hadi 26.4,
umasikini wa chakula umepungua kutoka asilimia 19.7 hadi 9.5, na kwamba takwimu za
Benki ya Dunia zinaonesha kuwa Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kasi kubwa ya
kupambana na umasikini kati ya nchi za Afrika zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara.

Amebainisha kuwa utekelezaji wa TASAF ulioanza mwaka 2000 na ambao kwa sasa
upo katika awamu ya 3 na utagharimu shilingi Trilioni 4.109 zikiwemo shilingi Trilioni
2.032 za kipindi cha pili cha awamu ya tatu amepangwa kunufaisha Halmashauri zote
185 za Tanzania Bara na Wilaya 11 za Zanzibar, na kwamba baada ya kufanya
maboresho sasa ruzuku imepunguzwa kutoka asilimia 67 hadi 38 na itaelekezwa kwa
wazee wasiojiweza, watoto wadogo na kwa wenye kiwango kikubwa cha ulemavu.

1 Ikulu Mawasiliano – 17 Februari, 2020


Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa asilimia 60 (sawa na Shilingi Trilioni 1.22) ya
fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo takribani 30,000 iliyopo kwenye
vijiji na mitaa 16,596 ya Tanzania Bara na Shehia 388 za Zanzibar na miradi hiyo
itahusisha afya, elimu, maji, barabara na mazingira. Miradi hii inatarajiwa kuzalisha ajira
Milioni 1.2 kwa watu wenye nguvu walio katika kaya masikini.

Amesisitiza kuwa licha ya kuwa sehemu ya fedha hizo ni ufadhili, sehemu kubwa
ambayo ni kiasi cha shilingi Trilioni 1.035 ni mkopo kutoka Benki ya Dunia na hivyo
amewaagiza viongozi wote wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri kuhakikisha
wanasimamia utekelezaji mzuri wa mpango huo na kwamba kufanikiwa ama
kutofanikiwa kwake itakuwa ni kipimo cha kama wanastahili kuendelea na nyadhifa zao
ama laa.

“Mathalani katika zoezi la uhakiki wa kaya masikini lililofanywa kuanzia Novemba


2015 hadi Juni 2017 tuliweza kubaini kaya masikini hewa 73,561. Hii ni aibu sana
kwa viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladslaus Mwamanga amesema TASAF
imepata mafanikio makubwa katika awamu zake zote ambapo katika awamu ya 1 kaya
1,704 zilinufaika na ufadhili wa shilingi Bilioni 72, Awamu ya 2 kaya 12,347 zilinufaika
na ufadhili wa shilingi Bilioni 430 na kipindi cha 1 cha awamu ya 3 Mamlaka za Serikali
za Mitaa 159 za Tanzania Bara na Zanzibar yote zimenufaika na ufadhili ya shilingi
Trilioni 1.46.

Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa amesema pamoja na


takwimu kuonesha Tanzania inafanya vizuri katika kupunguza umasikini, viashiria vya
huduma za kijamii navyo vinaonesha Tanzania imepiga hatua kubwa ambapo
uandikishaji wanafunzi Shule za Msingi umepanda kutoka asilimia 78 ( 2012) hadi
kufikia asilimia 83 (2018) na huenda imefika zaidi ya asilimia 90 hivi sasa, upatikanaji
wa maji kutoka vyanzo bora umepanda hadi kufikia 83, nyumba za Watanzania
zimeezekwa mabati kwa asilimia 84.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
17 Dar es Salaam.

2 Ikulu Mawasiliano – 17 Februari, 2020

You might also like