Yaliyomo Dibaji Utangulizi ………………………………………………………………………… Sura ya Kwanza: Upendo ……………………………………………………….. Sura ya Pili: Furaha ……………………………………………………………… Sura ya Tatu: Amani …………………………………………………………….. Sura ya Nne: Uvumilivu …………………………………………………………. Sura ya Tano: Utu wema …………………………………………………………… Utangulizi Baada ya vitabu vyangu kuhusu makosa ya binadamu katika Biblia, nisingeliitendea haki Biblia kama nisingeliandika kuhusu wema wa binadamu. Ninasema hivyo kwa sababu si vyema kuiangalia Biblia kwa jicho lililokaa senta. Asikwambie mtu, Biblia ni neno la Mungu lenye lengo maalum na neno la Mungu limekusudiwa kuwaadilisha watu ili waishi maisha ya kikamilifu hapa duniani ili mwishowe wajiunge na Mungu katika uzima wa milele. Kwa ukweli huo, Biblia inarekodi kwa ajili yetu yote mabaya na mema ya mwanadamu kusudi wanadamu waoneshwe katika picha yao kamili. Pande hizo mbili ndizo nilizozichukua kindakindaki. Ndipo katika kitabu BIBLIA NA MAKOSA YA BINADAMU (Sehemu I-III) nilieleza kwa mapana makosa ya binadamu ili binadamu tunaopumua sasa hapa duniani tusirudie upumbavu wa wenzetu anaokataza Mungu wetu. Ndiyo kisa basi nikachambua kwa urefu orodha za maovu zilizomo katika Marko 7:20-23; Rum 1:29-31 na Gal 5:19-21. Lakini Mungu wetu ni mkamilifu na anataka sana tuwe wakamilifu kama yeye (Kum 18:13; 2 Sam 22:31; 1 Nya 28:9; Mt 5:48; Ebr 13:21). Hata hivyo ukamilifu wetu utakuja kwa mazoezi. Ukamilifu wa Mungu hauna mashaka, isipokuwa ni huo wetu unaotiwa majaribuni mara kwa mara hata Waswahili wakasema: “Hujafa, hujaumbika” yaani wakati tunaishi chochote kinaweza kutokea. Kumbe basi ni hapo inapotujuzu binadamu tualikane tupige jaramba tuwe wakamilifu. Kwa hali hiyo ninapaswa nigeukie upande wa pili wa mambo kwa kitabu hiki BIBLIA NA WEMA WA BINADAMU (Sehemu I-III) kusudi binadamu tunaopumua sasa hapa duniani tujifunze kila jema litakalotupatia matunda yenye kudumu nyumbani kwetu kwa Mungu. Basi kwa kukidhi lengo la kitabu hiki, awali ya yote nimeichukua orodha ya Gal 5: 22-23 panapotajwa mema yafuatayo: upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Kishapo nikaioanisha orodha hiyo na orodha ya Flp 4:8 na 2 Pet 1:5-6. Nadhani sikufanya vibaya. Katika Flp 4:8 tumeandikiwa na Paulo hivi, “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yoyote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo ya staha, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa njema, ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yoyote, yatafakarini hayo”. Katika 2 Pet 1:5-6 tunasoma, “Kwa upande wenu katika imani yenu tieni wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu na katika upendano wa ndugu, upendo”. Lakini katika orodha hiyo ya tatu limetokea neno lingine la ajabu ambalo kwalo ninapata nguvu ya kuwahimizeni wote mnaomtafuta Mungu kutoacha tabia ya kujisomea na kujielimisha katika mambo ya imani. Ni kwa neno hilo usomalo, “Katika imani yenu tieni wema, na katika wema maarifa (2 Pet 1:5). Kwa kauli hiyo, kumbe haishauriwi kumfuta Mungu katika umbumbumbu wa imani. Tusome, tusome tukajiongezee maarifa katika imani yetu. Kwa ufupi, Biblia inatuambia imani na maarifa havipingani hata kwa dawa. Karibu basi usome kitabu hiki kusudi uujue vyema upana wa uwanja wa mazoezi ya kuwa mkamilifu kwa kutenda wema pasipo kulegea. Padre Titus Amigu, Septemba 2010
A BOOK OF DIVINE BLESSINGS - Entering into the Best Things God has ordained for you in this life - SWAHILI EDITION: School of the Holy Spirit Series 3 of 12, Stage 1 of 3