You are on page 1of 21

SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.

ME/SOMAVITABUTANZANIA

UCHAMBUZI WA KITABU; The 4-Hour Workweek (JINSI YA KUPUNGUZA


MUDA WA KUFANYA KAZI NA KUPATA MATOKEO MAKUBWA ZAIDI).
Imezoeleka kwamba muda wa kawaida wa kufanya kazi ni masaa 40 (arobaini)
kwa wiki, yaani masaa 8 kwa siku na siku 5 za wiki. Vipi kama akitokea mtu na
kukuambia kwamba unaweza kufanya kazi muda mchache zaidi kwa wiki, yaani
masaa 4 (manne) lakini ukapata matokeo makubwa zaidi kuliko ulivyokuwa
unafanya kwa masaa 40? Nina hakika utasema haiwezekani na mtu huyo
amechanganyikiwa. Lakini utakuwa unakosea sana.
Timothy Ferriss, mwandishi, mjasiriamali na mwekezaji, ametuonesha jinsi
ambavyo hilo linawezekana, kwa jinsi ambavyo alifanya yeye mwenyewe na
hata ambavyo wengine pia wanafanya. Kwa kuweza kufanya kazi kwa muda
mchache zaidi na kupata matokeo makubwa zaidi.
Tim kwenye kitabu chake kinachoitwa The 4-Hour Workweek: Escape 9–5, Live
Anywhere, and Join the New Rich ametupa maarifa sahihi na mbinu za kuweza
kuepuka kufanya kazi kwa muda mrefu na hivyo kuwa na muda mwingi wa
kufurahia maisha yetu kwa kufanya yale ambayo ni muhimu na tunayoyajali
zaidi. Kama tunavyojua, sehemu kubwa ya watu hawapendi zile kazi
wanazozifanya, hivyo kama kuna njia ya kupunguza muda wa kufanya kazi na
kupata matokeo makubwa, itakuwa ukombozi kwa wengi.
Njia anayotufundisha Tim, inawafaa watu wote, walioajiriwa na waliojiajiri,
lakini utekelezaji wake unatofautiana baina ya watu hao, kama ambavyo
tutajifunza. Hivyo usioe kwamba kitu hiki ni kwa watu fulani tu, kinawezekana
kwa yeyote kama tu utajipanga vizuri na kuchukua hatua kupitia yale
unayojifunza.
Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu THE 4-HOUR WORKWEEK uweze kujifunza
jinsi ya kufanya kazi kwa muda mfupi huku ukizalisha matokeo makubwa zaidi.

KWA NINI UNAKIHITAJI KITABU HIKI.


Tim anaanza kitabu chake kwa kutupa sababu kwa nini kila mtu anapaswa
kusoma na kufanyia kazi yale yaliyopo kwenye kitabu chake. Zifuatazo ni
sababu muhimu za wewe kusoma na kufanyia kazi kitabu hiki.
Moja; njia ya zamani haifanyi tena kazi. Kwamba ufanye kazi miaka 30 au 40
kisha ustaafu na ndiyo uweze kupumzika na kufurahia maisha ni njia ambayo
haifanyi kazi kwenye zama hizi. Kwa sababu kwanza huna uhakika wa kuwa na
ajira kwa kipindi chote hicho na hata ukiwa nayo, unapokuja kustaafu unajikuta
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

huna uhuru wa kifedha wa kukuwezesha kuishi kama unavyotaka wewe. Hivyo


Tim anashauri uchukue hatua ndogo ndogo za mapumziko (mini retirement)
kwa wakati ulionao sasa na siyo kusubiri mpaka ufike miaka 60.
Mbili; maisha hayapaswi kuwa magumu kama ambavyo tunayafanya yawe.
Watu wengi wameaminishwa na kuamini kwamba maisha lazima yawe
magumu, lazima ufanye kazi asubuhi mpaka jioni kila siku ndiyo ufanikiwe,
hivyo wengi wamekuwa wanaonekana tu wapo kazini, lakini hakuna matokeo
makubwa wanayozalisha. Kupitia kitabu hiki utajifunza jinsi ya kuzalisha
matokeo makubwa ndani ya muda mfupi na hivyo kuweza kupunguza muda
wako wa kazi.
Tatu; kitabu hiki kinatofautiana na vitabu vingine kwa njia zifuatazo;
1. Hakiegemei kwenye tatizo, bali kwenye suluhisho la tatizo.
2. Hakikuambii kuhusu kujibana ili ufurahie maisha ya baadaye, badala yake
kinakuambia ufurahie maisha ya sasa.
3. Hakikufundishi jinsi ya kupata kazi bora kwako, bali kinakuonesha jinsi ya
kutumia kazi uliyonayo sasa kupata uhuru mkubwa wa muda wako.

MWONGOZO MKUU WA YALE UNAYOKWENDA KUJIFUNZA NA HATUA


NNE ZA KUFIKIA UHURU WA MAISHA YAKO.
Ujumbe mkuu wa kitabu cha THE 4-HOUR WORKWEEK ni mtu kupata uhuru
kutoka kwenye kazi au biashara ambayo anaifanya. Na uhuru ambao Tim
ameuzungumzia ni wa aina tatu, ambazo ni uhuru wa muda (kufanya kazi kwa
muda mfupi), uhuru wa kipato (kuingiza kipato hata kama hufanyi kazi moja
kwa moja) na uhuru wa eneo (kuweza kusafiri popote utakapo bila ya kazi yako
kukuzuia). Ukiweza kuwa na uhuru huo wa aina tatu, basi maisha yako
yatakuwa bora sana.
Ili kufikia uhuru huo, kuna hatua nne muhimu za kuchukua ambazo Tim
ametushirikisha kwenye kitabu chake.
HATUA YA KWANZA NI D (DEFINITION)
Hapa unabadili sheria na kanuni zote za mchezo wa kazi au biashara na
kujiwekea utaratibu wako mpya ambao utautumia kuendesha maisha ya
tofauti kwako kwenye eneo la kazi.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

HATUA YA PILI NI E (ELIMINATION)


Hapa unakwenda kufuta mambo yote yasiyo muhimu na ambayo yanachukua
muda wakoi mwingi, hivyo kubaki na machache muhimu ambayo yanachukua
muda wako mchache. Hapa ndipo unapokwenda kupunguza sana muda wako
wa kazi na kupata uhuru wa kwanza ambao ni MUDA.
HATUA YA TATU NI A (AUTOMATION)
Hapa unatengeneza mpango wa kulipwa hata kama wewe haupo, unajenga
misingi ya kuiwezesha biashara au kazi yako kujiendesha yenyewe hata kama
wewe haupo na wewe kupokea fedha. Kupitia hatua hii, unapata uhuru wa pili
ambao ni FEDHA.
HATUA YA NNE NI L (LIBERATION)
Hapa unapata uhuru kamili wa maisha yako, kwa kuweza kuwa eneo lolote
duniani huku kazi au biashara yako ikiendelea kujiendesha yenyewe na fedha
zikiingia. Hapa unapata uhuru wa tatu ambao ni wa ENEO.
Kwa pamoja, hatua hizi nne zinatupa neno DEAL, ambapo ni kutengeneza
mpango mpya, kufuta yasiyo muhimu, kuiwezesha kazi kwenda bila wewe
kuwepo na kuwa huru kusafiri kwenda popote.
Katika utekelezaji wa hatua hizi nne, Tim anashauri waliojiajiri kutumia
mtiririko huo wa DEAL, lakini walioajiriwa kutumia mtiririko wa DELA, yaani
kwa waajiriwa, kabla hajaweza kutengeneza njia ya kazi yake kwenda bila ya
yeye kuwepo, anapaswa kutengeneza kwanza uhuru wa kutokuwepo kwenye
kazi. Tutajifunza hili kwenye uchambuzi huu unaonendelea.
Karibu sasa tuingie kwenye hatua moja moja na kujifunza mambo muhimu ya
kufanyia kazi.

HATUA YA KWANZA; WEKA MIPANGO MIPYA (DEFINITION)


Kama tulivyojifunza kwenye utangulizi, hatua ya kwanza ya kujenga uhuru wa
maisha yako ni kuanza kuweka mipango mipya kwako. Hapa unajenga misingi
ya maisha ambayo ni sahihi kwako na siyo kuiga yale ambayo kila mtu
anafanya. Hatua hii ni muhimu sana kwa sababu ndiyo inakugusa wewe moja
kwa moja na inakuwezesha kujijua wewe mwenyewe na kujua misingi sahihi
kwako kufuata.
Karibu tujifunze na kuweka mipango mipya itakayotupa uhuru mkubwa
kwenye maisha yetu.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

VITU VINNE VYA KUDHIBITI ILI KUONGEZA KIPATO CHAKO.


Kama unataka kuongeza kipato chako maradufu, basi unapaswa kudhibiti vitu
hivi vinne kwenye maisha yako.
Kwanza unapaswa kudhibiti nini unachofanya (what), lazima uweze kuchagua
wewe mwenyewe kile unachofanya na siyo kulazimika kufanya chochote
kinachopatikana.
Pili unapaswa kudhibiti wakati gani unafanya kitu hicho (when), lazima uwe na
uhuru wa kuchagua muda wako wa kufanya kazi na siyo kulazimika kufanya
kama wengine.
Tatu unapaswa kudhibiti eneo unalofanyia kazi yako (where), lazima uwe huru
kufanya kazi hiyo pale unapochagua wewe kuifanya na siyo kulazimika kuifanye
maeneo ambayo wengine wanaifanyia.
Nne unapaswa kudhibiti watu unaofanya nao kazi hiyo (whom), lazima uwe
huru kuchagua nani upo tayari kufanya naye kazi na siyo kulazimika kufanya
kazi na kila mtu.
Kupitia kitabu hiki, tunakwenda kujifunza jinsi tunavyoweza kudhibiti maeneo
haya manne, kuwa huru na kuongeza kipato chetu.
JINSI YA KUIVUKA HOFU YA KUCHUKUA HATUA.
Kila mtu anajua kabisa ni nini anapaswa kufanya ili kuwa na maisha anayotaka
kuwa nayo. Ukiongea na watu wengi ambao wapo kwenye ajira lakini
hawapendi kazi wanazozifanya, wanajua kabisa kwamba wanapaswa kuanzisha
biashara zao, au kutafuta kazi nyingine ambayo ni bora zaidi kwao.
Lakini pamoja na kujua hayo yote, wengi hawachukui hatua, na hii ni kwa
sababu wengi wanakuwa na hofu.
Wengi wamekuwa wanajipa picha mbaya kabla hata ya kuchukua hatua, mfano
mtu anapofikiria kuacha kazi na kwenda kuanza biashara, anapata picha mbaya
ya biashara kushindwa na kukosa kabisa kipato cha kuendesha maisha yake.
Tim anatuambia hofu hii ni ya kawaida na inampata kila mtu, hata wale
unaowaona kwa nje ni jasiri na wanachukua hatua kubwa.
Zifuatazo ni njia ambazo Tim anashauri tuzitumie ili kuweza kuondokana na
hofu inayotuzuia kupiga hatua;

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Moja; elewa hofu uliyonayo. Kwanza kabisa lazima uielewe hofu uliyonayo,
kwa kuangalia uhalisia wa kile unachohofia, jipe picha ya nini kibaya kabisa
kinaweza kutokea pale utakapochukua hatua. Je utakufa? Je utapata ulemavu
wa kudumu? Na pia jiulize ni kwa uhakika kiasi gani hayo unayofikiria
yatatokea. Unapoelewa kwa kina kile unachohofia, unapunguza nguvu yake,
kwa mfano utagundua kwamba unachohofia siyo kikubwa kama unavyohofia,
kwa mfano kama utaacha kazi na uingie kwenye biashara, hata kama biashara
hiyo itakufa haiwezi kupelekea wewe kufa, bado utakuwa hai na utaweza
kufanyia kazi mambo mengine, ikiwepo hata kurudi kwenye ajira.
Mbili; fanya kile unachohofia kufanya. Njia pekee ya kuishinda hofu ni kufanya
kile unachohofia kufanya, kwa sababu hofu huwa imebeba kile ambacho
unapaswa kukifanya. Unapata hofu kwa sababu kinakuwa ni kitu kipya na
kikubwa kuliko ulivyozoea. Jijengee tabia ya kufanya kitu kidogo unachohofia
kila siku na hilo litakujengea ujasiri wa kukabiliana na hofu nyingine. Tim
anashauri ujijengee tabia ya kuwasiliana na watu maarufu kila siku na
kuhakikisha wanakupa muda wao, ni jambo gumu na ambalo utahofia
kulifanya, lakini ukiweza litakupa ujasiri sana.
Tatu; jua gharama ambayo hofu inakupa. Piga hesabu na ujue ni gharama kiasi
gani hofu zako zinakuingizia, kwa kujua ni vitu gani unakosa kifedha, kimwili na
hata kiakili kwa kutokuchukua hatua. Unahofia kufanya kwa sababu ya kuona
utapoteza, lakini ambacho huoni ni kwamba kwa kutokuchukua hatua,
inakugharimu sana kifedha, kimuda, kiutulivu wa akili na kadhalika. Hebu fikiria
inakugharimu kiasi gani kuendelea kufanya kazi usiyoipenda kwa miaka
mingine kumi badala ya kuchukua hatua sahihi sasa? Ukishaona gharama
ambazo hofu inakuingizia, inakusukuma kuchukua hatua.
KUWA TOFAUTI NI RAHISI KULIKO KUWA KAWAIDA.
Kinachowazuia wengi kuchukua hatua sahihi kwenye maisha yao ni kukubali
kuwa kawaida. Kufanya kile ambacho kila mtu anafanya kwa namna ambayo
wengine nao wanafanya. Hapa unajiweka kwenye ushindani mkali na hivyo
mambo kuwa magumu.
Lakini kama utachagua kuwa tofauti, unaondokana na kundi kubwa la
wanaofanya kawaida na hivyo inakuwa rahisi kwako, kwa sababu ushindani
unakuwa mdogo na nafasi ya wewe kufanya makubwa inakuwa nzuri.
Tim anatushauri tuache kuweka malengo ya kawaida na badala yake tuweke
malengo ambayo siyo ya kawaida. Yaani kama mtu atasikia malengo yako na
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

kukuambia vizuri basi ujue hayo ni ya kawaida. Lakini kama mtu atasikia
malengo yako na kukuambia acha kujidanganya, huwezi kufikia malengo hayo
basi jua una malengo ya tofauti na una nafasi kubwa ya kuyafikia kama
utajituma kweli.
Unapojiwekea malengo makubwa na yasiyo ya kawaida yanakusukuma sana
kuyafikia na hivyo unaweza kuvuka vikwazo na changamoto nyingi. Lakini
unapokuwa na malengo ya kawaida, unaishia kuchukua hatua za kawaida na
changamoto ndogo sana inatosha kukuondoa kabisa kwenye malengo yako.
Manufaa ni makubwa pale palipo na watu wachache, siku zote kileleni kuna
watu wachache kuliko chini, na hewa safi pia kwa sababu hakuna
msongamano. Hivyo hakikisha wewe unakuwa wa tofauti, unalenga kileleni
penye wachache na siyo chini penye kila mtu.
SWALI MUHIMU KUJIULIZA ILI UWE NA MAISHA BORA KWAKO.
Maswali ambayo wengi wamekuwa wanajiuliza ni nini nataka au yapi malengo
yangu. Maswali yote hayo yamekuwa yanawarudisha kwenye mazoea ambayo
wamekuwa wanayaishi maisha yao yote.
Kama unataka kuwa na maisha bora na ya tofauti kwako, basi unapaswa
kuuliza maswali tofauti pia.
Na swali moja ambalo Tim anashauri kila mtu kujiuliza ni kitu gani
kinanisisimua. Hapa unapaswa kujua kile kitu ambacho kinakupa hamasa
kubwa kukifanya, kile ambacho unapenda kweli kukifanya na upo tayari
kukifanya muda wote. Kitu hiki kinakuwa cha tofauti kabisa kwako na ukikijua
na kukifanyia kazi, maisha yako yatakuwa ya tofauti.
Wengi wamezika vile vitu vinavyowasisimua na kuamua kuishi maisha ambayo
wameangiwa na jamii ndiyo maana maisha yao siyo bora. Epuka hilo kwa kujua
kinachokupa hamasa na kukifanya.
SIFA TATU ZA NDOTO UNAYOPASWA KUJIWEKEA.
Badala ya kuweka malengo ya kawaida kama wengine, unapaswa kuwa na
ndoto kubwa ya maisha ambayo unayataka wewe, yenye maana kwako na
yanayokupa nafasi ya kufanya kile unachopenda.
Katika kujiwekea ndoto hiyo, lazima iwe na sifa hizi tatu;
1. Unaweka hatua kwa hatua za kufikia ndoto hiyo. Usiishie tu kujiambia
unataka kufika sehemu fulani, bali jua utafikaje sehemu hiyo.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

2. Isiwe ya kawaida ambayo wengine wanakubaliana nayo, lazima iwe kubwa


na isiyo ya kawaida ili ikusukume zaidi.
3. Iwe kitu unachopenda kufanya na hivyo kuondoa utupu unaojengeka ndani
yako pale unapopunguza muda wa kufanya kazi. Lengo la ndoto hii siyo kuwa
sehemu ya kazi yako, bali kuwa sehemu ya maisha yako, hivyo lazima iwe
inakuridhisha na isijenge utupu ndani yako.
Hii ndiyo hatua ya kwanza ya kutengeneza uhuru wa maisha yako, ambapo
umejiwekea mipango mipya, ikiwepo ndoto kubwa na a tofauti kabisa na
kuweza kuvuka hofu inayokuzuia kuchukua hatua.

HATUA YA PILI; FUTA YASIYO MUHIMU (ELIMINATION)


Hatua ya pili kwenye kutengeneza uhuru kamili wa maisha yako ni
kutengeneza uhuru wa muda. Muda tulionao ni mchache na wenye ukomo,
hakuna mwenye uwezo wa kuongeza hata sekunde moja kwenye siku yake.
Hivyo kama tunataka kupata muda zaidi kwenye siku yetu, hatua ya kuchukua
ni moja, kuacha kufanya baadhi ya vitu ambavyo tunavifanya sasa.
Kwenye hatua hii ya pili tunakwenda kujifunza jinsi ya kuacha kufanya yale
mambo ambayo siyo muhimu kwetu, kuanzia kwenye maisha yetu binafsi na
hata kazi zetu ili tuweze kupata muda zaidi wa kuishi maisha yetu kwa uhuru.
UNZALISHAI MZURI SIYO KUFANYA KILA KITU.
Watu wengi wamekariri kwamba ili uzalishe matokeo mazuri, basi lazima
ufanye mambo mengi, lazima kila wakati uwe bize na kazi zako. Lakini hili siyo
sahihi, kadiri unavyofanya mambo mengi, ndivyo na uzalishaji wako unapungua
pia, kwa sababu mengi kati ya hayo yanakuwa siyo muhimu na yanaishia
kukuchosha tu.
Ni vyema kuchagua yale machache muhimu na yanayozalisha matokeo bora na
kisha kuyafanya hayo na utaweza kupata matokeo mazuri na kupiga hatua
kubwa kwenye maisha yako. Ondokana na dhana ya zamani kwamba lazima
uwe unafanya mambo mengi ndiyo uonekane unazalisha kweli.
USAHIHI NA UFANISI.
Usahihi ni kufanya kile ambacho kinakusogeza karibu na lengo lako. Ufanisi ni
kufanya jambo kwa ubora na ustadi wa hali ya juu, iwe ni jambo sahihi au la.
Sasa dunia imekuwa inaendeshwa hivi, watu wanafanya kwa ustadi mambo
ambayo siyo sahihi kwao.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Unachopaswa kufanya wewe ni kuchagua kile kilicho sahihi kwako kufanya na


kisha kukifanya kwa ufanisi wa hali ya juu. Usikimbilie kufanya chochote kwa
ufanisi, kwa sababu haijalishi umefanya vizuri kiasi gani, kama kitu siyo sahihi
kwako kufanya, umepoteza muda na nguvu zako.
Katika kuweka vipaumbele vyako vizuri vya yale unayofanya, unapaswa
kukumbuka mambo haya mawili muhimu sana;
Moja; kufanya vizuri jambo ambalo siyo sahihi kwako hakulifanyi jambo hilo
kuwa sahihi.
Mbili; kuweka muda mwingi kwenye kufanya jambo hailifanyi jambo hilo kuwa
muhimu na sahihi kwako.
Kitu kimoja cha kujikumbusha kila mara ni kwamba kile unachofanya ni
muhimu kuliko jinsi unavyokifanya. Hakikisha unachofanya ni sahihi kwako
kabla hujakifanya kwa ufanisi.
SHERIA YA 80/20
Wilfred Pareto aligundua kwamba asilimia 80 ya matokeo inatokana na asilimia
20 ya juhudi zinazowekwa. Hii ina maana kwamba kuna juhudi chache ambazo
zinazalisha matokeo makubwa sana, huku juhudi nyingi zikizalisha matokeo
ambayo siyo mazuri. Kuelewa hili, angalia mifano hii;
Asilimia 80 ya faida kwenye biashara inatokana na asilimia 20 ya bidhaa na
wateja.
Asilimia 80 ya matokeo unayopata kwenye kazi, inatokana na asilimia 20 ya
majukumu unayofanya.
Sheria hii inatufundisha kitu kimoja muhimu sana, kwamba juhudi zote
tunazoweka hazifanani, kuna juhudi chache zenye matokeo makubwa na
juhudi nyingi zenye matokeo madogo.
Hivyo lengo letu ni kujua juhudi chache zenye matokeo makubwa na kufanya
hizo tu.
Kwenye biashara, kama unawahudumia wateja 10 na unaingiza faida ya laki
moja, basi jua wateja wawili kati ya hao kumi, wanakuingizia faida ya zaidi ya
elfu 80 na wateja 8 waliobaki wanakuingizia faida ya elfu 20. Je huoni kwamba
ukiacha kuhudumia wateja hao 8 wanaokuletea faida kidogo na ukahudumia
wateja 2 wanaokuletea faida kubwa utapunguza muda wako wa kazi na
kuongeza kipato chako pia?
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Kadhalika kwenye kazi, kama unafanya kazi masaa 10 kwa siku, masaa mawili
yanaleta matokeo makubwa kuliko masaa 8, na kama unatekeleza majukumu 5
kwa siku, jukumu 1 lina matokeo makubwa kuliko majukumu 4 yaliyobaki.
Hivyo ni wajibu wako kujua ni sehemu gani sahihi ya kuweka juhudi na muda
wako ili kupata matokeo bora.
KUWA ‘BIZE’ NI UVIVU.
Kama kila muda uko bize, maana yake wewe ni mvivu na huwezi kufanya
maamuzi sahihi kwako. Kwa sababu kama tulivyojifunza, maeneo machache
ndiyo yanayoleta matokeo makubwa. Hivyo kufanya mambo mengi ni dalili
kwamba huwezi kuchagua yale yaliyo sahihi kwako, na huo ni uvivu.
Uchapakazi ni kuchagua mambo machache yenye matokeo makubwa na
kutafanya hayo huku ukipuuza mengine yote. Uvivu ni kujificha nyuma ya
mambo mengi ambayo hayazalishi matokeo yoyote.
Usiwe mvivu, weka vipaumbele vyako sahihi kulingana na sheria ya 80/20 na
kisha toa matokeo mazuri.
SHERIA YA PARKINSON KWENYE MATUMIZI YA MUDA.
Tumeiona sheria ya Pareto (80/20) kwenye kuweka vipaumbele kulingana na
matokeo yanayozalishwa na hivyo tukiweza kuitumia, tutapunguza sana
majukumu yetu.
Ipo sheria nyingine nzuri sana ambayo tukiweza kuifanyia kazi tutapata muda
zaidi. Sheria hiyo ni ya Parkinson.
Sheria hii inasema kwamba jukumu huwa linachukua muda ambao
limepangiwa kufanyika. Kama una masaa mawili ya kufanya jukumu fulani, basi
litafanyika ndani ya masaa mawili, na kama una masaa nane ya kufanya
jukumu hilo hilo, pia litafanyika ndani ya masaa nane.
Na hii ndiyo sababu ambayo huwa inapelekea watu kuahirisha mambo,
wanapokuwa na muda zaidi wanaupoteza, lakini mwisho unapofikia ndiyo
wanasukumwa kuchukua hatua.
Ili kuitumia sheria hii kwa manufaa yako, jiweke muda mdogo wa kukamilisha
majukumu unayojipa. Kama jukumu umezoea kulifanya kwa masaa nane,
jipangie kulifanya kwa masaa manne, na utaona jinsi ambavyo utakamilisha
jukumu hilo ndani ya muda huo mfupi zaidi.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Kadiri unavyokuwa na muda mwingi wa kufanya jambo, ndivyo unavyopoteza


muda huo kwa mambo yasiyo muhimu. Lakini unapokuwa na muda mchache,
unautumia vizuri kwa sababu unajua huna muda wa kupoteza.
Anza kujibana wewe mwenyewe kwenye muda, jipe muda mchache wa
kukamilisha jambo na hapo utasukumwa zaidi kufanya kilicho sahihi na
kuachana na yasiyo sahihi.
MAJUKUMU MACHACHE, MUDA MFUPI.
Tukiziweka pamoja sheria ya PARETO na ya PARKINSON, tunapata mwongozo
mzuri sana kwenye matumizi sahihi ya muda wetu;
Moja; punguza majukumu yako kwa kufanya yale machache na yenye matokeo
makubwa (80/20)
Mbili; punguza muda unaojipangia kufanya majukumu yako ili usukumwe
kufanya yale muhimu tu (Parkinson).
Hivyo kwa kuchagua majukumu machache na kupanga kuyafanya ndani ya
muda mchache, utapata muda mwingi wa kuwa huru kwenye maisha yako, na
hapo utakuwa umenufaika sana na hatua hii ya pili.
Ili kukamilisha hili, hakikisha unachagua kabisa ni majukumu gani unakwenda
kufanya na kisha kujiwekea muda wa ukomo wa kufanya na kupanga muda
gani utayafanya na kufuata hilo. Usiianze siku yako kabla hujaipangilia, utaishia
kuipoteza siku hiyo na kuruhusu mambo yanayoonekana ni ya dharura kumeza
siku yako.
PUNGUZA TAARIFA UNAZOPOKEA.
Eneo jingine ambalo tunapoteza sana muda wetu ni kwenye kufuatilia taarifa
mbalimbali. Na hili limeshamiri sana zama hizi za mitandao ya kijamii, ambapo
jambo lolote linalotokea duniani linakufikia. Hivyo unajikuta unapokea taarifa
nyingi ambazo zinakuchosha na kukufanya ushindwe kufanya yake muhimu
kwako.
Hivyo ili kupata muda zaidi, punguza taarifa ambazo unazipokea. Chagua kuwa
mjinga kwenye baadhi ya maeneo, usitake kutokupitwa, yaani kujua kila
kinachoendelea. Badala yake chagua maeneo ambayo ni muhimu kwako na
yenye mchango kwa wewe kupiga hatua na ufuatilie hayo, mengine achana
nayo. Hii ni kwenye taarifa za kawaida unazopata na hata kwenye maarifa pia.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Habari nyingi unazofuatilia, vitabu vingi unavyosoma na hata makala na


mafunzo mengi unayopata, mengi yanakuwa hayana manufaa kwako, kwa
sababu unapokea bila kuchuja.
Kuanzia sasa, kabla hujapokea maarifa au taarifa yoyote, ichuje kwa vigezo hivi
vitatu.
Kigezo cha kwanza ni UHUSIKA, lazima maarifa au taarifa yawe yanahusika na
kile ambacho unafanyia kazi, yana mchango kwenye lengo unalofanyia kazi,
tofauti na hapo ni kupoteza muda wako.
Kigezo cha pili ni UMUHIMU, maarifa na taarifa unazopokea, pamoja na kuwa
zinahusika basi pia zinapaswa kuwa muhimu, ambazo zina mchango kwenye
kufika kule unakotaka kufika.
Kigezo cha tatu ni kuweza kuchukua HATUA, lazima maarifa na taarifa
unazopata, uweze kuchukua hatua kukufikisha kule unakotaka kufika. Kama
unapata maarifa na taarifa ambazo huwezi kuchukua hatua, unapoteza muda
wako.
Kabla hujakubali kupokea maarifa au taarifa jiulize je inaendana na
unachotaka, ni muhimu na kuna hatua unaweza kuchukua? Kama majibu siyo
ndiyo kwenye maswali yote matatu, basi achana na maarifa au taarifa hiyo,
inakupotezea muda wako.
ONDOKANA NA USUMBUFU.
Pamoja na kuchagua yale muhimu ya kufanya na kudhibiti maarifa na taarifa
unazopata, bado huwa kuna vitu unavyovifanya bila kujua ambavyo vinakuwa
usumbufu kwako. Ukiweza kuondoa vitu hivi, basi utaweza kuokoa muda wako
mwingi sana.
Kuna makundi matatu ya usumbufu kwenye maisha yako, ambayo unapaswa
kuyafanyia kazi ili usiendelee kupoteza muda wako.
Kundi la kwanza ni mambo yanayopoteza muda.
Haya ni mambo ambayo unapenda kuyafanya, lakini hata usipoyafanya hakuna
madhara yoyote yanayotokea. Mfano mzuri ni mikutano, mabishano, kuperuzi
mitandao, matumizi ya simu na barua pepe.
Kwa mambo haya chagua kuacha kuyafanya au yape muda mfupi wa kuyafanya
pale ambapo umeshakamilisha majukumu muhimu kwako.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Kundi la pili ni mambo yanayokula muda wako.


Kundi hili lina yale mambo ambayo unayafanya kwa kujirudia rudia kila wakati.
Mfano kusoma na kujibu barua pepe, kupiga na kupokea simu, kujibu maswali
ya wateja na hata kuandaa ripoti mbalimbali. Mambo haya usipoyatengea
muda wa kuyafanya, yanaweza kuijaza siku yako yote na kumaliza muda wako.
Hatua ya kuchukua hapa ni kutenga muda maalumu wa kufanya mambo hayo.
Mfano badala ya kusoma na kujibu email kila inapoingia, tenga muda wa
kusoma na kujibu email zote, mara moja kwa siku. Kadhalika kwenye simu na
mengine pia. Usiwe mtu wa kukatishwa kazi zako muhimu kwa mambo
ambayo ni ya kujirudia rudia, yatengee muda wa kuyafanya.
Kundi la tatu ni mambo ambayo umeshindwa kuwawezesha wengine.
Kundi hili lina yale mambo ambayo umewapa wengine wakusaidie kuyafanya,
lakini hujawawezesha kuyafanya kwa kujitegemea, hivyo kila wakati wanakuja
kwako kwa maswali na kuomba maelekezo zaidi.
Hapa unahitaji kuchukua hatua ya kuwawezesha watu kufanya maamuzi yao
wenyewe bila ya kukitegemea au kukuuliza wewe kila wakati. Weka kiwango
cha maamuzi ambayo mtu anaweza kufanya bila kukuuliza. Na kiwango cha juu
ambacho lazima uulizwe. Kwa sababu maulizo mengi ni kwa mambo madogo
madogo, ukiwawezesha wasaidizi wako, utapunguza kusumbuliwa mara kwa
mara na hivyo kuwa na muda zaidi.
WEKA SHERIA KWENYE MUDA WAKO.
Tumejifunza mengi kuhusu kupata muda zaidi kwenye hatua hii ya pili, kitu
kimoja muhimu sana unachoweza kuondoka nacho hapa ni hiki, weka sheria
kwenye matumizi ya muda wako na wengine wazijue ili wazifuate. Kama
hujaweka sheria au taratibu mbalimbali, watu wataendelea kupoteza muda
wako, na hata wewe mwenyewe utapoteza muda wako.
Baadhi ya sheria muhimu kuweka kwenye muda wako;
1. Zuia watu kuzoea kutumia muda wako watakavyo, kama hauna miadi na
mtu usikubali achukue muda wako.
2. Wafanye watu wajieleze kile hasa wanachohitaji kabla hujawapa muda
wako.
3. Epuka mikutano isiyo na ulazima na ile yenye ulazima ifanyike kwa muda
mfupi.
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

4. Majukumu yanayojirudia rudia yakusanye na kuyafanya kwa pamoja.


5. Unapokuwa kwenye kazi muhimu, usiruhusu watu kukusumbua.
6. Usijibu simu, meseji au barua pepe hapo kwa hapo kama siyo muhimu, na
nyingi siyo muhimu.
Hiyo ndiyo hatua ya pili ya kuelekea kwenye uhuru ambapo tumeifunza jinsi ya
kufuta yale yasiyo muhimu ili kuweza kuwa na muda zaidi.

HATUA YA TATU; IFANYE KAZI KUJIENDESHA YENYEWE (AUTOMATION)


Hatua ya tatu kwenye kuelekea kwenye uhuru wa maisha yako ni kuiwezesha
kazi yako kujiendesha yenyewe bila ya wewe kuwepo moja kwa moja.
Kikwazo cha kwanza kwenye uhuru wako ni wewe mwenyewe. Pale ambapo
kila unachofanya kinahitaji uwepo wako, unajizuia kuwa huru, kwa sababu
hutaweza kuondoka kwenye kazi hiyo.
Kama tulivyojifunza unahitaji uhuru wa muda, fedha na eneo, kwenye hatua ya
tatu unakwenda kujifunza jinsi ya kupata uhuru wa fedha, yaani kuweza
kuingiza fedha hata kama haupo kwenye kazi moja kwa moja, ili uweze kuwa
na uhuru wa eneo, uweze kusafiri bila ya kuwa na wasiwasi kwamba kazi au
biashara zako hazitakwenda.
Karibu tujifunze jinsi unavyoweza kupata uhuru wa kifedha kwa kuwezesha
kazi zako kujiendesha bila ya uwepo wako.
FUTA, TOA, GATUA.
Kutaka kufanya kila kitu peke yako ndiyo kunakukamisha usipige hatua na
kuifanya kazi au biashara yako ikutegemee wewe moja kwa moja. Siku ambayo
haupo kazi au biashara inaathirika.
Kuna mambo matatu ya kufanya kwenye kazi yako, kwanza kabisa orodhesha
majukumu yote ambayo unayatekeleza kila siku kwenye kazi au biashara yako,
kisha yagawe kwenye makundi haya.
Kundi la kwanza ni majukumu ya kufuta, haya ni yale unayopaswa kuacha
kuyafanya, kama tulivyojifunza kwenye 80/20. Kuna mengi unapaswa kufuta
kwa sababu hayana tija.
Kundi la pili ni majukumu ambayo unaweza kuyatoa kwa wengine, haya
unaweza kumpa yeyote akayafanya na kukupa matokeo. Hivyo tafuta watu wa

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

kuwapa majukumu hayo na wakupe matokeo, watu hawa huna haja ya


kuwaajiri, wao wanatekeleza unachotaka na kukukabidhi matokeo.
Kundi la tatu ni majukumu ambayo unayagatua kwa wengine, haya ni yale
majukumu ambayo unawapa watu ambao umewaajiri wakusaidie na hivyo
wanakuwa ni watu ambao wanaweza kutekeleza majukumu hayo bila ya wewe
kuwasimamia kwa karibu.
Lengo lako ni kuhakikisha kwamba hakuna majukumu yanayokutegemea wewe
moja kwa moja, hivyo hakikisha kila kinachopaswa kufanya, kuna mtu anaweza
kukifanya na anakifanya.
Kuna watu wengi ambao wapo tayari kukusaidia majukumu uliyonayo bila hata
ya kuwaajiri, teknolojia imerahisisha sana hili. Unaweza kuajiri watu
wakufanyie kazi hata kama wapo mbali na pale walipo. Muhimu ni kuyapangilia
majukumu yako vizuri na kisha kutafuta mtu sahihi wa kuyatekeleza.
NJIA TATU ZA KUFANYA BIASHARA ISIYOKUTEGEMEA.
Watu wengi wamekuwa wanapenda kufanya biashara, lakini wanakwama
kuanza kwa sababu wanajiambia hawana muda wa kufanya kila kitu. Lakini
sababu hiyo siyo sahihi, kwa kuwa kuna namna mbalimbali za kufanya biashara
hata kama huna muda wa kufanya kila kitu.
Hapa kuna njia tatu za kufanya biashara ambayo haitakutegemea moja kwa
moja.
Nia ya kwanza ni kuuza bidhaa ambayo tayari imeshatengenezwa na watu
wengine. Hapa kazi yako kubwa ni kutafuta soko tu kisha kupata oda, ambazo
utazituma kwa wauzaji wa bidhaa husika, wanawauzia wateja na wewe
unapata kamisheni yako. Unaweza kufanya hili bila hata ya kuwa na eneo la
biashara. Mtandao wa intaneti umerahisisha sana hili.
Njia ya pili ni kupata leseni ya kuuza bidhaa za wengine. Hapa unaomba nafasi
ya kutumia jina la biashara nyingine kuuza bidhaa. Unapewa leseni au kibali
cha kuuza bidhaa au kutumia jina la kampuni fulani kuuza bidhaa zao au zako.
Hapa unachohitaji ni kuweka mfumo sahihi tu na biashara inakwenda.
Njia ya tatu ni kutengeneza bidhaa yako mwenyewe. Na hili lisikutishe, huhitaji
kuwa injinia au mbunifu kuweza kutengeneza bidhaa yako mwenyewe, bali
unahitaji kuwa na wazo, kisha kuwapata watu sahihi wa kukusaidia
kutengeneza na wewe unawauzia wateja wako.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Utaona hapa njia zote tatu zinazungumzia bidhaa na siyo huduma, biashara
pekee unayoweza kuifanya na ukawa huru ni ya kuuza bidhaa. Biashara ya
huduma kama ushauri na nyinginezo, zinakuhitaji uwepo wako na hivyo huwezi
kuzifanya kwa namna ambayo utakuwa huru kabisa na muda wako.
BIDHAA RAHISI KWAKO KUZALISHA NA YENYE FAIDA NZURI.
Katika kutaka uhuru wa muda na fedha, kuna bidhaa ambayo unaweza
kuzalisha kwa urahisi na ambayo utaiuza kwa muda mrefu na kuendelea
kuingiza kipato hata kama hufanyi kazi moja kwa moja.
Bidhaa hiyo ni maarifa.
Ukizalisha maarifa, iwe ni kwa mfumo wa kitabu, video au sauti, unaweza
kuuza bidhaa hiyo kwa miaka mingi hata kama huandiki au kuandaa tena
maarifa hayo. Hivyo hii ni sehemu nzuri kwa kila mmoja kuanzia.
Usijiambie kwamba huwezi kuzalisha maarifa kwa sababu wewe siyo mtaalamu
au mwandishi au mengineyo. Unachopaswa kujua ni kwamba, kuna kitu
ambacho wewe unakijua au una uzoefu nacho na wengine hawajui kama
unavyojua wewe.
Hivyo unaweza kuwasaidia watu hao kupitia ujuzi au uzoefu ambao unao na
ukazalisha maarifa ambayo wengine watakuwa tayari kuyalipia na ukauza kwa
muda mrefu kulingana na uwezo wako wa kuwashawishi watu kununua.
NJIA TATU ZA KUZALISHA BIDHAA BORA YA MAARIFA.
Kama ambavyo tumejifunza, bidhaa za maarifa ni rahisi kwako kuzalisha na
utaweza kuziuza kwa muda mrefu, hivyo ni kitu unachopaswa kufanya.
Zipo njia tatu za kuzalisha bidhaa hizi za maarifa.
Njia ya kwanza ni kutengeneza maudhui wewe mwenyewe, hapa utahitaji
kufanya utafiti kupitia kusoma vitabu na kupata maarifa mengine, kisha
kukusanya pamoja yale maarifa ambayo yatamsaidia mtu unayemlenga.
Njia ya pili ni kukusanya maarifa yanayopatikana bure na kisha kuyapaki vizuri
na kuuza kwa wengine kwa njia ambayo ni bora. Haya ni yale maarifa
yanayopatikana bure kabisa, mfano ripoti mbalimbali za kiserikali na maandiko
ambayo hayana hatimiliki.
Njia ya tatu ni kuwatumia wataalamu kuandaa maudhui na wewe kuwalipa
kwa muda wao au kuwapa kamisheni kwa kila maudhui yanayouzwa. Mfano
unaweza kumchangua mtaalamu wa kitu fulani akaandika kitabu au
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

kutengeneza video za mafunzo na kisha wewe kumiliki na kusambaza bidhaa


hizo huku ukimlipa kwa makubaliano ambayo mliwekeana.
KABLA HUJAZALISHA BIDHAA KWA WINGI, FANYA MAJARIBIO.
Watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye biashara bila ya kufanya majaribio,
wanachofanya ni utafiti ambao huwa hauna majibu sahihi. Kwa mfano
ukimuuliza mtu kama atanunua kitu fulani, kwa sababu hataki kukukatisha
tamaa, atakuambia kwamba atanunua, lakini hapo hapo ukamwambia kitu
hicho unacho na anunue, hatanunua.
Hivyo badala ya kufanya utafiti wa kuuliza, fanya utafiti wa majaribio, kwa
kuzalisha kiwango kodogo cha bidhaa na kuanza kuuza kwa watu kupitia njia
mbalimbali. Kama watu watakuwa na mwitikio mzuri zalisha kwa wingi na uza
zaidi. Kama hawatakuwa na mwitikio mzuri jua sababu ni nini kisha fanya
marekebisho.
Usikubali kupoteza mtaji wako kwa kuzalisha bidhaa nyingi kabla hujafanya
majaribio kwa wateja wachache na kupata picha nzuri.
WAHUDUMIE WATEJA SAHIHI.
Watu wengi wanapoingia kwenye biashara, huwa wanafikiri kwamba kila mtu
lazima awe mteja wao. Hivyo wanakazana kukimbizana na kila aina ya wateja
wakiamini kuwa na wateja wengi ndiyo biashara kufanikiwa.
Unapaswa kurudi kwenye sheria ya Pareto (80/20) na kujua kwamba asilimia
80 ya faida unayopata, inatokana na asilimia 20 ya wateja wako. Hivyo wateja
wachache wanaleta faida kubwa.
Sasa utakuwa huru zaidi kwenye biashara yako kama utawahudumia wateja
wazuri wachache kuliko wengi ambao watakusumbua.
Wajibu wako ni kujua wateja wapi ni wazuri kwako na kuendelea nao na wale
ambao siyo wazuri kuachana nao, kwa lugha nyingine kuwafukuza.
Wateja wazuri kwako ni wale wanaojua wanachotaka, wanaojali thamani yake,
walio tayari kulipa kwa wakati na ambao hawana malalamiko mengi.
Wateja wasio wazuri na unaopaswa kuachana nao ni wale ambao hawajui
wanachotaka, hawajali thamani ya kitu, wanataka punguzo kila mara, hawalipi
kwa wakati na ni wasumbufu, kila wakati wanataka uwasaidie kitu kwenye kile
walichonunua kwako.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Wateja ni wengi, chagua kufanya kazi na wateja sahihi na achana na wale


wasio sahihi, kama unataka kupata uhuru wa muda na fedha.
WEKA MFUMO SAHIHI.
Mtandao wa intaneti na mitandao ya simu imejenga mifumo mizuri sana ya
kufanya biashara kwa uhuru wako huku ukiingiza kipato bila ya kujali uko wapi
au unafanya nini.
Chukua mfano huu, umeona kuna wazazi wengi wanahangaika na lishe kwa
watoto wao, na wewe ni mzazi ambaye ulihangaika sana na lishe, ukafanya
utafiti na kujua lishe sahihi kwa watoto, ukatumia kwa watoto wako.
Hapo unaweza kugeuza maarifa na uzoefu huo kuwa bidhaa ambayo unaweza
kuuza kwa wengine. Unaweza kuandaa kitabu kinachoelezea lishe kwa watoto
kisha kutengeneza tovuti ya kukiweka au kutumia tovuti za kuuza bidhaa
mtandaoni. Ukaweka namba ya kulipwa kupitia mitandao ya simu au njia
nyingine kama benki.
Kisha ukaweka mfumo ambapo mtu akishalipia, mtandao unamruhusu
kupakua kitabu hicho moja kwa moja. Ukishafanya kazi ya kuandaa kitabu na
kukiweka kwenye mfumo sahihi, kilichobaki wewe ni kutangaza kitabu hicho,
ambapo pia siyo lazima uwepo. Unaweza kulipia matangazo mtandaoni na
yakarushwa hata kama haupo mtandaoni.
Hivyo kinachofanyika ni matangazo yako yanaruka na kuwafikia wenye uhitaji,
wanakuja kwenye tovuti, wanakutana na kitabu, wanakipenda, wanabonyeza
kununua, wanaoneshwa jinsi ya kulipia, wanalipia na kisha wanapakua kitabu
na biashara imekamilika. Katika hatua zote hizo, hakuna hata moja inayohitaji
uwepo wako, lakini fedha inaingia kwenye akaunti yako.
Unaona jinsi ilivyo rahisi, sasa unaweza kufanya kwa jambo lolote unalojua au
ambalo una uzoefu nalo. Muhimu ni wewe kuweka mfumo sahihi na kisha
kuacha mfumo huo ukufanyie kazi wewe.
Kwenye hatua ya tatu tumejifunza jinsi ya kufikia uhuru wa kifedha, kwa
kutengeneza mfumo wa kuiwezesha kazi au biashara yako kuendelea kufanyika
hata kama haupo moja kwa moja.

HATUA YA NNE; KUPATA UHURU WA ENEO (LIBERATION)


Baada ya kupata uhuru wa muda kwa kufanya yale muhimu na kuachana
yasiyo muhimu, kisha kutengeneza uhuru wa kipato kwa kuiwezesha kazi au

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

biashara yako kujiendesha bila ya wewe kuwepo, hapo sasa una nafasi ya
kuweza kuwa popote unapotaka kuwa. Hulazimiki tena kuwa kwenye kazia au
biashara yako muda wote, kwa sababu inaweza kujiendesha yenyewe.
Hatua ya nne kwenye kupata uhuru wa maisha yako ni kuwa na uhuru wa
eneo, yaani kutokulazimika kuwa eneo moja, kuwa huru kwenda popote
unapotaka kwenda kwa wakati unaotaka kwenda.
KUKOSA UHURU WA ENEO NI UMASIKINI.
Kukosa uhuru wa eneo, yaani kulazimika kuwa eneo moja ambapo huwezi
kusafiri au kwenda unapotaka ni umasikini, haijalishi una fedha au mali kiasi
gani. Uhuru wa kweli ni kuwa huru kwa eneo pia, kama unataka kusafiri
unafanya hivyo bila ya kuwa na kikwazo chochote.
KUPATA UHURU KWENYE KAZI.
Kama tulivyojifunza, mpango huu wa kupata uhuru unawafaa watu wote, yaani
walioajiriwa na waliojiajiri. Lakini kwa walioajiriwa, wanahitaji kupata uhuru wa
eneo kwanza kabla hawajapata uhuru wa kifedha.
Na aliyeajiriwa anaweza kufanya hivyo kwa kuangalia jinsi anavyoweza
kutekeleza majukumu yake ya kazi bila ya kuwa eneo la kazi. Watu huwa
wanafanya kazi masaa 8 kwa siku wakiwa kwenye eneo la kazi, lakini ukiangalia
kwa umakini, muda halisia ambao mtu anafanya kazi hauzidi masaa mawili.
Muda mwingine huwa unapotelea kwenye vikao, kwenye mapumziko ya chai,
chakula, kwenye kubishana au kusubiriana kwa mambo mbalimbali.
Hovyo kwa kuijua kazi yako na kujua majukumu ambayo unapaswa
kuyatekeleza, kazi nyingi zinaweza kufanyiwa nyumbani au sehemu nyingine
kwa msaada wa mtandao wa intaneti. Japo siyo kazi zote, kuna kazi ambazo
lazima mtu awepo eneo la kazi, lakini sehemu kubwa ya kazi, mtu anaweza
kuifanya nje ya eneo la kazi.
Na hivi ndivyo makampuni mengi duniani yanafanya, kuepuka gharama za
kuendesha ofisi, yanaruhusu watu kufanyia kazi zao majumbani, hivyo
wanapewa majukumu wanayopaswa kutekeleza na muda wa kutekeleza na
watu hao wanakuwa huru muda gani wafanye kazi.
Kama mwajiriwa hiki ndiyo kitu unachopaswa kukitengeneza kwenye ajira
yako, kuangalia namna unavyoweza kutekeleza majukumu yako ya kazi bila ya
kuwa eneo la kazi na kisha kumshawishi bosi au mwajiri wako akupe nafasi ya
kujaribu hilo. Nenda kwake ukiwa na mpango kamili, ukionesha jinsi gani
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

utatekeleza hilo na manufaa ambayo yatapatikana. Ukipewa nafasi ya kujaribu


hili, basi itumie vizuri ili iwe na manufaa na uweze kuendelea na utaratibu huo.
KAZI AMBAZO HAZIFAI KUOKOA.
Siyo kazi zote zinakupa nafasi ya kuweza kuwa na uhuru wa eneo, kazi nyingine
zimepinda kiasi kwamba huwezi kuziokoa, na hapo ndipo unapopaswa kufanya
maamuzi sahihi.
Unapaswa kutengeneza njia nyingine ya kukuingizia kipato ili upate uhuru wa
kuondoka kwenye kazi hiyo inayokubana. Kama kazi inakunyima muda kabisa
na lazima uwepo eneo la kazi kuifanya, hupaswi kuifanya muda mrefu, maana
inakufanya kuwa mtumwa zaidi.
Badala yake fanya kazi hiyo kwa muda mfupi, ukiitumia kama sehemu ya
kusaidia wakati unajenga biashara yako ya pembeni, ikishakuwa vizuri unaacha
kazi yako na kuendelea na biashara yako ambayo utakuwa umeijengea msingi
sahihi wa kutokukuhitaji wewe muda wote.
KUSTAAFU KWA VIPINDI.
Moja ya njia za kutumia uhuru wa eneo ni kusafiri kwenda maeneo mbalimbali
kama njia ya mapumziko. Kama hilo haliwezekani basi unaweza kutumia njia
nyingine ambayo ni kustaafu kwa vipindi.
Kwa njia hii, unachagua kujipa mapumziko ya muda mrefu kwenye eneo tofauti
ka kipindi fulani, kati ya mwezi mmoja mpaka miezi sita. Hapo biashara zako
zinaenda kama kawaida na wewe unafanya yale unayopenda kufanya.
Muhimu ni upate muda wa kuwa pale unapotaka kuwa na kufanya kile
unachotaka kufanya.
Hiyo ndiyo hatua ya nne ya kufikia uhuru wa maisha yako, kuwa na uhuru wa
eneo, kutokulazimika kuwa eneo moja kwa sababu ya kazi au biashara,
ukiweza kufikia hatua hiyo una uhuru wa kweli.
Lakini huo siyo mwisho, kuna tatizo moja...

HUO UHURU UNAOUPATA UNAUTUMIA KUFANYA NINI?


Kuna jambo moja ambalo huwa linaumiza wengi, hasa wale wanaoingia bila ya
kujua. Wengi kwa kuzoea kuwa kwenye kazi muda wote, wanapoondoka
kwenye kazi wanapata msongo. Wanajikuta wapo wenyewe, hawana watu wa
kuongea nao muda wote wa siku. Na hata mtu anapokwenda kwenye

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

mapumziko siku za kwanza huwa zinakuwa za furaha, lakini baadaye mtu


anazoea na kugundua kwamba siyo furaha muda wote kama walivyofikiri.
Watu wanapopata muda mwingi ambao hawafanyi kazi, ndipo maswali ya
msingi na ya kifalsafa yanaibuka ndani yao. Maswali kama nini maana ya
maisha, maisha yangu yana kusudi gani, kwa nini nipo hapa duniani ndiyo
yanapata nafasi kwenye akili yako. Unapokuwa umetingwa na kazi maswali
haya hayapati nafasi, ila unapokuwa huru maswali haya yanapata nafasi
kubwa.
Hivyo Tim anashauri tuwe na namna ya kukabiliana na utupu ambao
tunautengeneza baada ya kupunguza kazi. Na tim anashauri tufanye vitu
vitatu;
MOJA; KUENDELEZA VIPAJI VYAKO.
Kila mtu ana kipaji, lakini kutingwa na kazi na maisha kunawafanya wengi
kukosa muda wa kuendeleza vipaji vyao. Hivyo unapopata uhuru wa maisha
yako, ndiyo muda wa wewe kuendeleza vipaji vyako.
Kumbuka yale mambo ambayo ulikuwa unapenda kuyafanya sana ukiwa
mtoto, kumbuka mambo ambayo unapenda kuyafuatilia hata kama hulipwi,
hayo ndiyo mambo ambayo unapaswa kuyafanya unapokuwa na uhuru.
MBILI; KUHUDUMIA WENGINE.
Unapokuwa huru una nafasi kubwa ya kuwahudumia wengine. Na zipo njia
nyingi za kufanya hivyo. Unaweza kuwasaidia wale walio kwenye mazingira
magumu, unaweza kujihusisha na uboreshaji wa mazingira au huduma
nyingine za kijamii kama elimu na afya. Na pia unaweza kutoa misaada kwa
wale wenye uhitaji.
Kwa vyovyote vile, tumia uhuru wako kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora
zaidi na utazidi kufurahia uhuru ulioupata.
TATU; JIFUNZE ZAIDI.
Kujifunza ni kitu ambacho unapaswa kufanya kila siku, bila ya kusema
umeshajua kila kitu. Unapokuwa huru una nafasi nzuri zaidi ya kujifunza, siyo
tu kupitia usomaji wa vitabu, bali pia kusafiri maeneo mbalimbali na kujifunza.
Ukiwa una uhuru wa fedha, muda na eneo, unaweza kwenda popote duniani
na kujifunza, unaweza kuhudhuria makongamano mbalimbali na unaweza
kutengeneza mtandao wako na watu mbalimbali.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Muhimu ni kuhakikisha uhuru unaoupata kwa kuondoa kazi au biashara yako,


kuna kitu kingine kinaziba pengo lililotengenezwa. Usipokuwa na kitu cha
kuziba pengo hilo, maisha yako yatakuwa ya hovyo licha ya kuwa na uhuru. Na
tuna mifano ya wengi ambao maisha yao yaliharibika baada ya kupata uhuru,
kwa sababu hawakuwa na jukumu linalowasukuma. Wewe jua mapema ni kipi
utafanyia kazi kabla hata hujapata uhuru wako ili uhuru huo usiwe laana
kwako.

HITIMISHO.
Umejifunza mambo muhimu sana kupitia uchambuzi huu wa kitabu cha THE 4-
HOUR WORKWEEK, umejifunza hatua nne za kufikia uhuru kamili wa maisha
yako na jinsi ya kuzifanyia kazi.
Sasa kazi ni kwako kwenda kuyaweka kwenye matendo ili uweze kupiga hatua
na kufanikiwa kwenye maisha yako. Kumbuka haya yote yanawezekana ila
yanahitaji uweke mipango yako mwenyewe na ujipe muda wa kutengeneza
uhuru huu. Japo mwishoni utakuwa huru, lakini mwanzoni lazima uweke kazi
hasa kwenye kujenga misingi ya biashara ambayo itaweza kujiendesha bila ya
wewe. Muhimu ni kuchagua kuyaishi maisha yako na kuacha kuiga maisha ya
wengine.
Kuendelea kupata chambuzi za kina za vitabu na vitabu vilivyochambuliwa,
jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kwa kufungua
www.t.me/somavitabutanzania
Kupata vitabu mbalimbali vya kujisomea tembelea www.somavitabu.co.tz

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007

You might also like