You are on page 1of 14

ANTIDIUS NSIGA

www.antidius-nsiga.com

KAZI HII INAJUMUISHA YAFUATAYO:

• Maana ya usairi kwa mujibu wa wataalam mbalimbali,


• Aina za mashairi;

(a) mashairi ya kimapokea

(b) mashairi ya kisasa

• Kufanana kwa mashairi ya kimapokeo na ya kisasa,


• Kutofautiana kwa mashairi ya kimapokeo na ya kisasa,
• Hitimisho.
• Marejeo.

USHAIRI.

Wataalamu mbalimbali wameeleza maana ya ushairi wa kiswahili, lakini mawazo yao

yamefungamana katika sehemu fulani na kuofautiana katika baadhi ya maeneo. Wataalamu

karibu wote kwa pamoja wanaamini kuwa shairi lazima liwe na:

• mpangilio mzuri wa maneno,

• lugha inayoeleweka, na

• lugha yenye kuleta maana kwa hadhira iliyokusudiwa.

Aidha wataalamu hawa kwa upande mwingine wanatofautiana katika baadhi ya maeneo.

maeneno hayo ni pamoja na:

1
• mpangilio wa urari wa vina na mizani,

• mabeti, na

• kibwagizo au bahari.

Kutokana na tofauti hizi, tunapata aina mbili ya mashairi yaani mashairi ya kimapokeo na

mashairi ya kisasa. Wataalam nao wapo wanaounga mkono mashairi ya kimapokeo na wale

wanaounga mkono mashairi ya kisasa kama ifuatavyo:

(a).WANAMAPOKEO

Hawa ni washairi wa jadi wanaoshikilia kuwa ili tungo fulani iweze kuingia katika

kundi la mashairi, ni lazima tungo hiyo ifuate sheria au kanuni fulani kama vile urari wa vina,

mizani , idadi ya mishororo katika beti (mishororo mine kila ubeti),ambazo huitwa arudhi.

Baadhi ya wana mapokeo ni Mnyampara, Shaban Robert, na Mayoka.

Mnyampala (1970), anasema “Ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kale,

ndicho kitu kilicho bora sana katika maongozo ya dunia kwa kutumia maneno ya mkato,

lugha nzito na yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa mizani na vina maalum kuwa ushairi”.

Mayoka (1984) anasema: “Ushairi ni mtungo wa kisanaa ulio na mpangilio maalum

wa lugha ya mkato ambayo ndani yake ina vina, urari wa mizani na muwala maalum

ambavyo kwa pamoja huwa na fani na maudhui yahusuyo hisi fulani au tukio juu ya maisha

ya mtu au watu wa mazingira na wakati maalum”.

(b)WANAMAPINDUZI

Hawa ni washairi wa kisasa wanaoamini kuwa ili tungo fulani iweze kuingia katika

kundi la mashairi, si lazima tungo hiyo izingatie arudhi kama vile urari wa vina, mizani, idadi

ya mishororo katika beti na mengine mengi. Kundi hili husisitiza kuwa la muhimu katika

2
tungo siyo sheria au kaida hizi bali ni ujumbe au maudhui aliyokusudia mtunzi kwa hadhira

yake. Baadhi ya wana usasa ni pampja na Pr. Kezirahabi, Pr. Mlokozi, Pr. Kahigi, Wangari na

Mwai.

Mlokozi na Kahigi (1979) wanasema “Ushairi ni sanaa iliyopambanuliwa kwa

mpangilio maalum wa maneno fasaha yenye muwala kwa lugha ya mkato, picha, au sitiari

katika usemi, maandishi au mahadhi ya wimbo ili kuelekeza wazo au mawazo, kufunza au

kuelezea tukio au hisi fulani kuhusu maisha au mazingira ya binadamu kwa njia inayogusa

moyo”.

Kezirahabi (1976) anasema “Ushairi ni tukio, hali au wazo ambalo limeoneshwa

kwetu kutokana na upangaji mzuri wa maneno fasaha yenye mizani kwa kifupi ili kuonesha

ukweli fulani wa maisha”.

Kwa ujumla tunasema ushairi ni tungo ya kisanaa wenye mpangilio maalumu wa

lugha ya mkato katika usemi, maandishi, wimbo unaoelezea wazi juu ya mawazo, hisia au

tukio juu ya maisha na ambayo hufuata utaratibu wa urari na muwala maalum unaoheshimu

na kuzingatia kanuni za utunzi wa mashairi unaohusika.

Mashairi ya kimapokeo na mashairi ya kisasa, kwa pamoja kuna baadhi ya mambo ya

msingi yanayofanana. Hoja zifuatayo zinaelezea baadhi ya mambo na sehemu za msingi

ambayo hupatikana katika mashairi ya kisasa na yale ya kimapokeo.

Mashairi ya kimapokeo na ya kisasa yote ni tungo za kubuni zinazoelekeza maisha ya

jamii kisanaa. Kwa ujumla shairi lolote lile ni utungo ambao hubuniwa na mtunzi kuelezea au

kutoa mawazo fulani kuhusu jamii au kitu fulani. Tungo hizi hutungwa kwa ufundi au ustadi

wa hali ya juu ili kugusa mawazo na hisia za walenga. Ufundi unaotumika kupanga mawazo

3
na kuteua lugha katika tungo hutumia sanaa ya kipekee kulingana na hitaji, kusudi pamoja na

ujuzi wa mtunzi juu ya kazi husika na walengwa wa kazi hiyo.

Aina zote hutumia maneno machache kuwakilisha dhana pana mno. Mashairi hutumia

maneno au lugha teule zilizoundwa kisanaa kamavile tamathali za semi, na mbinu nyingine

za kisanaa kwa njia yenye mvuto ambayo haimchoshi msomaji au msikilizaji. Mfano, katika

“Elimu jamii na chemsha bongo”, iliyoandikwa na Charles Mloka, shairi la “Lifuti yako ya

maneno”(shairi la kimapokeo) uk.20 ubeti wa pili, mshairi anasema:

“Heri nende na miguu, kuliko lifuti yako,

Heri ningojee tuu, daladala toka boko,

Lifutiyo roho juu, nikipanda huna cheko,

Binamu sipandi tena, lifutiyo ya maneno”.

Katika ubeti huu, mwandishi ametumia maneno machache kuelezea athari ya misaada toka

mataifa ya kibepari kwa nchi za ulimwengu wa tatu.

Aina zote hutumia picha au taswira zenye uwezo wa kutoa maelezo kamili. Matumizi

ya picha na taswira hukusudiwa zaidi kumfanya msomaji au msikilizaji kufikiri kwa mapana

juu ya kilichoandikwa au kilichozungumzwa, kuifanya kazi kuwa ya jamii pana, kuepusha

migogoro ya kimasilahi kati ya mtunzi na tabaka la juu, na kuifanya kazi kuwa na mvuto kwa

wasomaji na wasikilizaji pia. Aidha yapo baadhi ya mashairi ambayo hutumia lugha ya wazi

pia. Mfano katika mashairi ya ‘matunda ya azimio’ yaliyoandikwa na Sengo na wenzake,

katika shairi la 12 “Adhabu gani tuwape” (shairi la kimapokeo) uk.29, ubati wa 2, mshairi

anasema:

4
“Adhabu gani tuwape, wenye kosa la kunyonya

wanyonyao kama kupe, wagande wafe kunyonya

hawaachi japo kope, vipi tutavyowaonya

adhabu gani tuwape,wanyonyaji Tanznia?”

Taswira zilizojitokeza katika ubeti huu ni;

1. kunyonya- ikimaanisha kudhulumu,

2. kupe- ikimaanisha mafisadi.

3. Kope- ikimaanisha kipato kidogo.

Pia katika Elimu jamii na chemsha bongo kwa mashairi, iliyoandikwa na Charles Mloka,

shairi la Arobaini ya simba (shairi li kisasa) uk.43, ubeti wa kwanza, msahairi anasema:

“Hicho kipigo cha simba, wanyama kimewashitua,

Simba na kote kutamba, kinyonga kamuumbua,

Kamtegeshea gamba, angani kalinyanyua,

Simba kadhani mgomba, nyumbani unapumua,

Kumbe kombora la komba, masalale! Likauwa,

Simba na wote umwamba, kabaki ameduwaa,

Ngebe zote za kutamba, zikabaki mshumaa,

Simba kapachikwa mimba, mme hajamtambua,

Arobaini ya simba, mamba waweka matanga”.

Katika ubeti huu, taswira zilizojitokeza ni kama:

1. Arobaini ya samba ni tukio la septemba 11, 2001 kupigwa kwa jengo la kibiashara

la kimataifa nchini Marekani.

5
2. Simba ikimaanisha Taifa la Marekani,

3. Kinyonga ikimaanisha vikosi vya kigaidi,

4. Wanyama ikimaanisha mataifa mengine ya kibepari, na

5. Mamba ikimaanisha mataifa yanayopata misaada toka Marekani.

Aina zote hufungamana na hisia kwani hugusa moyo wa msomaji. Mashairi ni

mawazo ya mtunzi kwa ujumla kuhusiana na hali fulani katika jamii. Ili kuirekebisha hali

hiyo au kuleta mabadiliko, mtunzi lazima atengeneze kazi itakayogusa hisia na mioyo ya

walengwa wa kazi yake. Kufaulu kwa mshairi katika kuirekebisha jamii husika kupitia kazi

yake ndiko kunakoonesha ni kwa jinsi gani mshairi amefanikiwa kugusa mioyo na hisia za

walengwa wa kazi yake.

Aina zote za mashairi huelezea hisia za watu kutoka ulimwengu halisi wa kila siku.

Karibia mambo yote yanayozungumziwa na washairi ni yale yaliyomo katika jamii na

pengine ni uzoefu wa maisha ya kila siku. Mfano, mwandishi anaweza kuzungumzia masuala

ya kijamii kama vile elimu, afya, na dini, masuala ya kiuchumi, kisiasa au kiutamaduni

ambayo kwa ujumla hufungamana na maisha ya kila siku ya jamii hiyo. Mfano, katika Elimu

jamii na chemsha bongo kwa mashairi iliyoandikwa na Charles Mloka, shairi la Udini na

Ukabila, uk.13, ubeti wa 3, mshairi anasema:

“Mimi muisilamu, mwenzangu mkristo,

Joni na mimi Adamu, wote wa Mungu watoto.

Tutaitwa marehemu, kifika siku ya wito,

Hakuna mtu muhimu, sote tutakula moto,

Kama sote tu wamoja, kwanini twabaguana?”

Ubeti huu unazungumzia migogoro ya kidini ndani ya jamii kati ya waisilamu na wakristo.

6
Aina zote za mashairi hutumia lugha ya mkato na yenye mnato. Kwa ujumla mawazo

ya mwandishi katika shairi huelezewa kwa ufupi na kwa muhtasari ambao hubeba mawazo

yote ya mwandishi katika kazi husika. Aidha udondoshwaji na ufupishwaji wa baadhi ya

maneno au sehemu ya neno (ukiushi) hufanywa ili kupunguza wingi wa maneno na kufanya

muhtasari wa yale yanayokusudiwa kuzungumzwa katika shairi. Mfano, Matunda ya azimio

iliyoandikwa na Honero na wenzake, shairi la Hizi ni fanaka zetu myaka kumi ya uhuru,

uk.54, ubeti wa 27, mshairi ansema:

“Elimu sasa ni nyingi, hakika imepanuka,

Miaka mine si mingi, mkoloni aloweka,

Myaka saba msingi, watoto kuelimika,

Hizi ni fanaka zetu, myaka kumi ya uhru”.

Mshairi ameweza kufupisha maneno kama ifuatavyo:

1. Myaka badala ya miaka,

2. Mine badala ya minne,

3. Aloweka badala ya aliyoweka, na

4. Myaka saba msingi badala ya miaka saba ya elimu ya msingi.

Aina zote ni tanzu za ushairi zenye lengo la kufikisha ujumbe au fundisho fulani

katika jamii. Pamoja na kazi nyingine, mashairi hufanya kazi ya kuionya, kuelimisha na

kuikosoa jamii. Yapo mambo mbalimbali ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni

yanayokabili jamii nyingi. Mashairi ya kimapokeo na ya kisasa huweza kusifia ama

kupongeza mafanikio yaliyopatikana au kukosoa kasoro zilizopo ama zinazojitokeza katika

Nyanja hizo za maisha katika jamii ili kuunda jamii bora zaidi. Mfano, katika “Elimu jamii

na chemshabongo kwa mashairi” ya Charles Mloka, shairi la WANAFUNZI (shairi la kisasa)

uk.11, ubeti wa 1, mshairi anasema;

7
“Hebu nieleze Juma, uonavyo kwa hakika,

Vipi sasa taaluma, sekondari inashuka,

Wazazi tunalalama, vijana mnaanguka,

Wanafunzi!”

Katika ubeti huu mwandishi anazungumzia suala la kuporomoka kwa taaluma miongoni mwa

wanafunzi. Aidha katika Diwani ya Mloka, shairi la “Utamaduni”(shairi la kimapokeo) uk.34

ubeti wa 1, mshairi ansema;

“Palipo na watu hai, hapakosi tamaduni,

Hapo ndipo panadai, sanaa za kila fani,

Aghalabu pana rai, za hisi zetu moyoni,

Utamduni sauti, ya maisha ya jamii”.

Mshairi anazungumzia suala la utamaduni kama kiini cha maisha ya jamii yoyote ile.

Pamoja na kufanana kwa mashairi ya kimapokeo na mashairi ya kisasa, bado kuna

tofauti zinazojibainisha kati ya mashairi haya.Utofauti huu unajibainisha kama ifuatavyo;

Ukongwe. Katika umri, mashairi haya yanatofautiana. Mashairi ya kimapokeo ni

makongwe zaidi kuliko mashairi ya kisasa. Tangu miaka ya 850-323 BK, Plato aliweka

msimamo juu ya kazi ya sanaa (ushairi) akisema kuwa lazima ifuate sheria maalum ambazo

kimsingi ni msingi mkuu wa mashairi ya kimapokeo. Sheria na taratibu hizi zilikuja

kupingwa kati ya miaka ya 1680-1750 na Aristotle ambaye kimsingi alikuwa akimkosoa

mwalimu wake na ndio ukawa mwanzo wa mashairi ya kisasa (mashairi huru) ambayo kwa

namna ya pekee kati ya miaka ya 1969 mpaka 1970 baadhi ya wanafunzi wa chuo kikuu cha

Dar es salaam na ambao pia walikuwa watunzi wa mashairi,n mfano; Pr. Mlokozi, Pr. Kahigi,

na wengine waliyaunga mkono mashairi haya ya kisasa.

8
Mashairi ya kimapokeo hufuata idadi maalum ya mizani (8+8 kwa kila mshororo), hii

ikiwa ni kaida ya msingi katika mashairi ya kimapokeo. Kwa mfono; katika diwani ya mloka

iliyoandikwa na Charles Mloka, shairi la “Alimu wa Kiswahili” uk. 37 ubeti wa 1, mwandishi

anasema;

“Kujua lugha ilipo, tutazame ushairi,

Pamoja na lile jopo, la watunga mashairi,

Hakika tujue hapo, pana kila utajiri,

Ulimi mtoa neno, hifadhi kinywa vizuri”.

Katika ubeti huu, kwa kila mshiroro kuna mizani 16 (8+8). Kwa upande wa mashairi ya

kisasa si lazima kufuata utaratibu wa mizani 16 kwa kila ubeti. Mizani zinaweza kupungua au

kuzidi. Mfano; shairi la ‘siasa’ katika ‘Elimu jamii na chemsha bongo kwa mashairi’, uk.25,

ubeti wa 1, mshororo wa 1;

“Siasa soma, cha watu chao kilio”.

Katika mshororo huu kuna mizani 13 (5+8).

Mashairi ya kimapokeo huzingatia urari wa vina yaani vina vya kati na vya mwisho.

Mashairi haya yana vina vya kati na vina vya mwisho vyenye ulinganifu. Kwa mfano, katika

Diwani ya mloka, iliyoandikwa na Charles Mloka, shairi la ‘samaki wakasirika’(shairi la

kimapokeo) uk. 75 ubeti wa 1 mshairi ansema:

“Samaki hao samaki, wanatoka baharini,

Wameshikwa na hamaki, wakimbilia sokoni,

Wanakwenda kuwacheki, ndugu zao wa majini,

Samaki wakasirika, hawataki kuuawa”.

9
Katika shairi hili tunaona vina vya kati ni ‘KI’ Na vina vya mwisho ni ‘NI’. Katika mashairi

ya kisasa si lazima kufuata utaratibu wa vina vya kati na vya mwisho. Mfano, katika diwani

ya mloka, iliyoandikwa na Charles Mloka, shairi la ‘Mtu Aliyefikiri’ (shairi la kisasa) uk 9

ubeti wa 2, shairi linasomeka hivi:

“Maisha ya mwanadamu, ni sawasawa na gari,

Linalopita sehemu, yenye njia ya hatari,

Tazama kila kukicha, watu hawakai chini.......”

katika shairi hilo vina vya kati ni ‘MU na CHA’ na vina vya mwisho ni ‘RI na NI’ hivyo basi

vina vya kati havifanani vyote na vile vya mwisho pia.

Mashairi ya kimapokeo huwa na muundo ambao ni rahisi kufuatilia ukilinganishwa

na mashairi ya kisasa na hivyo huweza kuimbika kwa urahisi. Hii ni kutokana na matumizi ya

vina na mizani. Matumizi ya vina na mizani katika mashairi, hulifanya shairi liwe na ladha na

mvuto linapoimbwa na kusikilizwa au kuandikwa na kusomwa. Mfano, katika Diwani ya

mloka ilyoandikwa na Charles Mloka, shairi la “samaki wakasirika” uk.75 ubeti wa 4

mwandishi anasema;

“Dagaa kachachamaa, lini atasoma shule,

Anasema kunyamaa, kwamuongezea ndwele,

Leo akata rufaa, madai yaende mbele,

Samaki wakasirika, hawataki kuuawa”.

Mashairi ya kisasa pamoja na baadhi ya mashairi hayo kufuata utaratibu wa vina na mizani

lakini ni magumu kuimbika kutokana na kuwa na mishororo mingi ambayo huweza

kumchosha anyeyaimba au kuyasoma. Mfano; katika diwani ya Mloka, shairi la

“mwanadamu na maisha” (shairi la kisasa) uk.18, ubeti wa 1 na wa 2 kwa kila ubeti una

10
mishororo 12, na ubeti wa 3 una mishororo 18. Katika ubeti wa 1, mshairi anaandika;

“Mmea unapokua, huifurahia mvua,

Lakini siposogea, hulisingizia jua,

N’ambie ulivyoota, hata maji ukapata,

N’ambie ulivyosota, hata watu wakakata,

Uliamini ni Mola, ndiye kaupa chakula,

Ulikubali kabila, haliishi bila mila,

Mwanadamu kadhalika, hukua hufurahika,

Huupenda uhakika, wa nyota yake kufika,

Umri wa kuridhisha, huhitaji kujitwisha,

Hapo akiufikisha, huona kafanikisha,

Maisha yake hupenda, ni mazuri yakienda,

Na siyo yenye kupinda, hayo daima huponda”.

Mashairi ya kimapokeo huwa na urari wa mishororo (mishororo mine kwa kila ubeti),

kwa ujumla mashairi ya kimapokeo huwa na mishororo minne kwa kila ubeti. Mfano; katika

Diwani ya mloka, iliyoandikwa na Charles Mloka, shairi la ‘samaki wakasirika’(shairi la

kimapokeo) ubeti wa kwanza;

“Samaki hao samaki, wanatoka baharini,

Wameshikwa na hamaki, wakimbilia sokoni,

Wanakwenda kuwacheki, ndugu zao wa majini,

Samaki wakasirika, hawataki kuuawa”.

Ubeti huu una mishororo minne. Katika mashairi ya kisasa si lazima ubeti uwe na mishororo

minne, huweza kuwa na mishororo pungufu ya minne au hata zaidi ya minne. Mfano, katika

Elimu jamii na chemsha bongo kwa mashairi, iliyoandikwa na Charles Mloka, shairi la ‘sina

mbone!’ uk.17, ubeti wa 1, lina mishororo mitatu;

11
“Mwana kogela chinyala, kolonga kabule ng’anda,

Nemitondo kwa bang’ala, kuchiro kwake Luanda,

Sina mbone!”

Mashairi ya kimapokeo huwa na mtiririko maalum (muwala) wa mawazo toka ubeti

hadi ubeti. Wazo linalotoka katika ubeti wa kwanza huendelezwa katika beti zinazofuata.

Mfano, katika matunda ya azimio, shairi la “Bora kujitegemea” (shairi la kimapokeo) uk. 34,

shairi lina beti 8. Ubeti wa 1 unaanza kwa maneno “Hodi hodi uwanjani, mimi ningali kijana,

na ubeti wa mwisho unaanza kwa maneno “Beti nane nimefika, kalamu sitaishika”. Utaratibu

huu hauzingatiwi sana katika mashairi ya kisasa.

Mashairi ya kimapokeo huwa na idadi maalum ya vipande kwa kila mshororo. Kwa

kawaida katika mashairi ya kimapokeo kila mshororo huwa na vipande viwili vyenye mizani

nanenane. Mfano, katika diwani ya mloka, shairi la utu ni nini? Uk 23, ubeti wa kwanza,

mshairi anasema;

“Utu na ubinadamu, ni kama yai na kuku.

Utu ni ile nidhamu, mola aliyokhuluku,

Ubinadamu ni damu, ya utu wa kila siku,

Utu wowote wa mtu, ni kuwajali wenzake”

Mashairi ya kisasa hayazingatii sana idadi ya vipande kwa kila mshororo. Mashairi haya

huweza kuwa na kipande kimoja, vipande viwili, na hata vitatu kwa kila mshororo. Mfano

mzuri ni katika shairi la “Moyo” lililopo katika Wamitila (2005) kama ilivyonukuliwa

kwenye ubeti ufuatao:

“Moyo waniambia ota, kuwa mwizi usiote, siwe kaini,

Moyo waniambia kata, mirija yote ikate, mizizini,

Moyo waniambia teta, penye dhuluma patete, andikoni,

12
Moyo waniambia woga, ndiyo mwanzo wa maafa”.

Katika ubeti huu, kipande cha kwanza huitwa ukwapi, kipande cha pili huitwa utao, na

kipande cha tatu huitwa mwandamizi.

Pamoja na kufanana na kutofautiana kwa aina zote mbili za mashairi yaani mashairi

ya kimapokeo na mashairi ya kisasa, kwa pamoja yamekusudiwa kuburudisha jamii,

kuhamasisha jamii, kukuza sanaa na ukwasi wa lugha, kuliwaza, kuelimisha, kuonya,

kutahadharisha, kusifia mtu au kitu, na kukemea mambo yanayoenda kinyume na maadili ya

jamii.

13
MAREJEO;

Honero, L. N, Ngole, S. Y. na Sengo, T. Y. (1980) Matunda ya Azimio. TUKI. DSM

Mayoka , J. M. (1984) Mgogoro wa ushairi na Diwani ya Mayoka. Dar es salaam:

Tanzania Publishing House.

Mloka, C. (2002), Diwani ya Mloka. Mkuki na Nyota Publishers LTD. Dar es salaam.

Mloka, C. (2004), Elimu jamii na chemsha bongo kwa mashairi. Mkuki na Nyota Publishers

LTD. Dar es salaam.

Mnyampala, M. (1970) Diwani ya Mnyampala, Dar es salaam, Nairobi na Kampala: East

African Literature Bureau.

Mulokozi, M. M na Kahigi, K.K (1979), Kunga za ushairi na Diwani yetu, Tanzania

Publishing House:Dar es salaam.

Mulokozi, M na Kahigi. K (1995), Malenga wa bara. Dar es salaam University Press.

Wamitila, K. (2005) Tamthilia ya maisha, Narobi: Vide Muwa.

14

You might also like