You are on page 1of 63

SOMO: 1

Njia 9 za Kutangaza Biashara Yako Bila Pesa

Matangazo ni swala muhimu kwa kila biashara. Tatizo linatokea pale ambapo
biashara inashindwa kumudu gharama za matangazo, hasa matangazo ya
gharama kubwa.

Naamini wewe kama mjasiriamali unafahamu kuwa kuna wakati bajeti ya


biashara inakuwa imebana. Hivyo swala la kujitangaza linakuwa na
changamoto.

Fuatilia makala hii kwa karibu ili nikufahamishe njia 9 unazoweza kuzitumia
kutangaza biashara yako bure au kwa gharama nafuu sana.

1. Tumia tovuti
Tovuti au blog ni njia rahisi na ya gharama nafuu ya kujitangaza. Ikiwa una
blog au tovuti ambayo inaidadi nzuri ya watembeleaji, unaweza kuweka
tangazo la biashara yako hapo na likaonekana kwa watu wengi zaidi.

2. Tumia mitandao ya kijamii


Kama ilivyo wenye njia ya blog, vivyo hivyo unaweza kutumia mitandao ya
kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram n.k. ili kujitangaza.

Kumbuka hivi leo karibu kila mtu anatumia mitandao ya kijamii. Hivyo
kutangaza biashara yako kupitia kurasa au akaunti zako za mitandao hii ni
rahisi na utawafikia watu wengi zaidi.
3. Tengeneza vifungashio au zawadi ndogo
Siyo lazima uwe na pesa nyingi ndipo utoe zawadi au huduma ya vifungashio
vyenye chapa yako. Unaweza kubuni na kuchapisha vifungashio vyenye jina
na maelezo mafupi kuhusu biashara yako ili kujitangaza.

Unaweza kutoa zawadi ndogo kama vile kalamu au shajara (diary) vyenye
maelezo ya biashara yako.

4. Tengeneza kadi za kibiashara na vipeperushi


Unapopewa kadi ya kibiashara (business card) au kipeperushi lengo lake
hasa ni kujitangaza. Unaweza kutengeneza kadi za kibiashara pamoja na
vipeperushi vyenye maelezo mafupi kuhusu biashara yako.

Naamini njia hii ni nafuu sana kuliko kuweka tangazo kwenye televisheni
wakati wa habari.

5. Kuwa wakala wa biashara kubwa


Kuwa wakala wa biashara kubwa ni njia moja nzuri ya kujitangaza na
kuongeza wateja. Mara nyingi biashara kubwa huwatangaza mawakala wao
katika matangazo yao ya gharama kubwa.

Hivyo, kwa kuwa wakala wa biashara au kampuni kubwa kama vile


makampuni ya simu, bima, dawa, pembejeo, au fedha; utakuwa umepata
nafasi ya kutangazwa bure kabisa.

6. Hudhuria semina na makongamano


Njia nyingine nzuri na rahisi ya kujitangaza ni kwa kuhudhuria semina,
makongamano au sehemu zenye mikusanyiko.

Uwapo katika maeneo haya, hakikisha unatafuta angalau nafasi ya kutoa


salamu katika maeneo haya, ukipewa nafasi ya kuzungumza taja tu hata jina
la biashara yako kwani ina maana kubwa sana. Unaweza kuvaa pia mavazi
yenye maelezo au matangazo ya biashara yako.
7. Jitolee au toa misaada
Naamini mara kadhaa umewahi kuona wafanyakazi wa kampuni au biashara
fulani wakitoa misaada au hata kujitolea kufanya kazi kama vile usafi wa
mazingira.

“Hakuna chakula cha bure kwenye uchumi.”


Je ni nini hasa msingi wa swala hili? Kama wanauchumi wa kale
walivyotangulia kusema kuwa hakuna chakula cha bure kwenye uchumi, vivyo
hivyo matendo ya kujitolea au msaada yana lengo fulani.

Mara nyingi makampuni au biashara fulani zinapotoa misaada waandishi wa


habari hurekodi na kutangaza habari hiyo. Hii ni njia nzuri sana ya
kujitangaza.

8. Endesha shindano
Nani asiyependa kushinda? Naamini hata wewe unapenda kushinda zawadi
fulani.

Ili ushinde unatakiwa kununua bidhaa au kusambaza habari kuhusu biashara


fulani, je kwa njia hii hujaitangaza biashara hiyo? Naamini utakuwa umefanya
hivyo tayari.

Unaweza kuendesha shindano dogo lenye zawadi za kawaida kama vile


mikoba, vocha za simu, vinywaji, kalamu au hata bidhaa unazouza. Kwa njia
hii utajitagaza kwa gharama nafuu kabisa.

9. Toa elimu au ushauri bure


Kama kuna elimu au ushauri fulani unaoweza kuutoa ambao unaendana na
biashara yako; fanya hivyo sasa.

Kwa njia hii utafahamika na kuwafikia watu wengi zaidi na hivyo kuitangaza
biashara au huduma yako kwa urahisi na kwa gharama nafuu kabisa.
Hitimisho

Kufanikiwa katika kitu chochote kunahitaji mikakati sahihi na ubunifu. Naamini


umeona jinsi ambavyo unaweza kutumia njia mbalimbali kujitangaza kwa bei
nafuu au bure kabisa.

Naamini hutoumiza tena kichwa kufikiri njia za kupata pesa nyingi kwa ajili ya
matangazo ya gharama kubwa.

SOMO: 2

Mbinu 10 za Kuongeza au Kuvutia Wateja Kwenye Biashara

Haijalishi huduma au bidhaa yako ni kubwa kiasi gani, biashara yako


haitazalisha pesa kama wateja hawatakuwa tayari kununua bidhaa au
huduma yako. Hakuna wateja, hakuna biashara.

Tatizo la kukosa wateja hukabili sana biashara ndogo, na hata kusababisha


biashara hizo kufa. Siyo kwamba wateja hawapendi kununua bidhaa za
biashara hizi, bali tatizo kubwa ni mbinu duni za kujitangaza na masoko.

Katika makala hii nitakueleza mbinu 10 rahisi na za gharama nafuu ambazo


unaweza kuzitekeleza na ukaongeza au kuvutia wateja zaidi kwenye biashara
yako.

1. Lugha nzuri
Katika mambo yanayowapotezea wafanyabiashara wengi wateja ni lugha
mbaya kwa wateja. Hakuna mteja anayependa kupokelewa au kujibiwa
vibaya.

Hakikisha unazungumza na wateja wako kwa namna bora ambayo wataona


unawajali, unawathamini na kuwaheshimu.
Mimi mwenyewe ninapenda kwenda kwenye biashara ambayo wahusika
wana lugha nzuri; huwa nawashauri pia rafiki zangu kwenda kwenye biashara
za aina hiyo. Hivyo hakikisha unatumia mbinu hii ili kuongeza wateja.

2. Huduma au bidhaa za bure


Wateja wengi wanapenda vitu vya bure au zawadi. Siyo lazima ufanye jambo
kubwa la bure ili kuwavutia wateja; hata jambo dogo tu linaweza kuwavutia
sana.

Ili kuwavutia wateja unaweza kutoa huduma au vitu vya bure kama vile
kalamu, mifuko, shajara (diary) au hata maji ya kunywa. Kwa njia hii
utawavutia wateja wengi zaidi.

3. Punguzo
Punguzo ni njia bora sana ya kukabiliana na ushindani wa kibiashara na
kupata wateja. Ikiwa mwenzako anauza sabuni kwa shilingi 2,100, wewe uza
2,050. Unaweza usipate faida kubwa kwenye bidhaa moja lakini utapata faida
kubwa kwenye mauzo ya jumla.

Kwa mfano ikiwa faida kwenye sabuni hapo juu ni sh. 100, muuzaji wa
kwanza akauza sabuni 5 kwa sh. 2,100 atapata faida ya sh. 500.

Lakini wewe ukauza sabuni 20 kwa sh. 2,050 utapata faida ya sh. 1,000. Je
huoni kuwa umeuza na kupata faida zaidi kutokana na kuvutia wateja wengi
kupitia punguzo? Weka punguzo sasa.

4. Shindano
Siyo lazima uwe na pesa nyingi ndipo uweze kuendesha shindano. Unaweza
kuendesha shindano lenye zawadi ndogo kama vile vocha, kalamu, mikoba,
shajara au hata vinywaji.

Kwa njia ya kuweka shindano watu wengi watavutiwa kununua bidhaa au


huduma zako ili wawe washindi. Unaweza pia kuweka bidhaa au huduma
zako kama kitu cha kushindaniwa badala ya zawadi nyingine.
5. Anzisha tovuti au blog
Watu wengi hawafahamu umuhimu wa tovuti au blog. Wengi hufikiri kuwa ni
mahali pakuweka matangazo ya watu wengine ili wakulipe.

Ukweli ni kuwa blog au tovuti ni muhimu sana kwa ajili ya kuongeza wateja
kwa njia ya kutangaza biashara yako.

Ukiwa una blog nzuri yenye watembeleaji wa kutosha, unaweza kuitumia


kutangaza na kuuza bidhaa zako wewe mwenyewe na ukajipatia pesa nyingi.

6. Tumia mitandao ya kijamii


Kama ilivyo kwa blog na tovuti, vivyo hivyo mitandao ya kijamii inaweza
kutumiwa kuzalisha pesa nyingi.

Ikiwa unataka kuongeza wateja, basi wafahamishe watu kupitia mitandao ya


kijamii juu ya huduma au bidhaa zako. Hakikisha wanazielewa na kuweza
kuzifikia kwa urahisi.

7. Matangazo
“Biashara ni matangazo.”
Biashara nyingi hupuuza nafasi ya kujitangaza ili kuongeza wateja na hatimae
kupata faida zaidi. Siyo lazima utumie njia za gharama kubwa kujitangaza
kwani zipo njia nyingi sana.

Unaweza kutumia mitandao (rejea mbinu ya 5 na 6), vifungashio, saini ya


barua pepe (email signature), card ya utambulisho wa biashara (busness
card), vipeperushi n.k.

8. Toa misaada
Je umeshawahi kujiuliza kwanini biashara na kampuni nyingi hutoa misaada
mbalimbali? Je ni kwa kuwa wana pesa za ziada au wanawapenda sana wale
wanaowasaidia?
Ni wazi kuwa hii ni mbinu nzuri sana ya kujitangaza na wala si vinginevyo.
Kwa njia ya kutoa misaada wateja huongezeka zaidi kwani watu huifaahamu
biashara husika, pia huichukulia kama biashara inayowajali zaidi.

Kumbuka siyo lazima utoe misaada mikubwa au ya pesa nyingi. Unaweza


kutoa hata bidhaa zako au huduma yako kama msaada kwa watu au taasisi
fulani.

9. Lenga changamoto
Watu wananunua bidhaa au huduma fulani ili itatue changamoto zao. Hivyo
kuendesha biashara isiyolenga changamoto za wateja haitapata soko.

Hebu fikiri mtu anaanzisha duka la kuuza dawa za Ebola Kenya au Tanzania,
je atapata wateja kweli? Ni wazi kuwa hatapata wateja kwani tatizo la Ebola
kwa Tanzania na Kenya ni dogo sana.

Hivyo ili kuongeza wateja hakikisha unakuwa mbunifu na kulenga


changamoto na mahitaji ya wateja.

10. Shirikiana na biashara au kampuni kubwa


Hebu fikiri kampuni kama Vodacom au Airtel wakikutaja kwenye matangazo
yao kuwa wewe ni wakala wao; je unafahamu ni nini kitatokea? Moja kwa
moja utafahamika zaidi pamoja na kile unachokifanya na utaongeza wateja
zaidi.

Kumbuka kushirikiana na kampuni au biashara nyingine kubwa hukufanya pia


uaminike zaidi kwa wateja.

Hitimisho

Naamini sasa umeona jinsi unavyopoteza wateja na faida bila sababu yoyote
ya msingi. Fanyia kazi mbinu jadiliwa hapo juu nawe kwa hakika utaweza
kuongeza wateja na hatimaye kupata faida zaidi. Je wewe unatumia mbinu
gani kupata wateja?
SOMO: 3
Jinsi ya Kuanza Biashara na Mtaji Mdogo

Watu wengi wamekuwa wakitamani kuanza biashara lakini wanafikiri namna


ya kuanza kwani mtaji wao ni mdogo sana.

Usiogope; kuwa na mtaji mdogo au kutokuwa nao kabisa sio mwisho wako wa
kutimiza malengo yako.

“Usilie juu ya kile ambacho huna; tumia vizuri kile ulichonacho.”

Reginald Mengi
Zipo mbinu mbalimbali ambazo zinaweza kukuwezesha kufanya biashara
hata kama utakuwa na mtaji mdogo. Tafadhali fuatilia hoja jadiliwa hapo chini
kwa ufafanuzi zaidi.

1. Kuwa mbunifu
Moja kati ya mambo ambayo yatakusaidia sana kwenye kuanza biashara kwa
mtaji mdogo ni ubunifu. Kwa njia ya ubunifu utaweza kushinda biashara na
bidhaa zilizoko sokoni kwa urahisi zaidi. Unaweza kufanya haya yafuatayo:

 Chagua wazo la biashara unalolipenda na kuliweza vyema. Hili litakusaidia


kukabili changamoto vyema.
 Angalia tatizo au uhitaji uliopo sasa na uutatue kwa bidhaa au huduma yako.
 Panga bei vizuri; unaweza kuweka bei ambayo ni tofauti kidogo na bidhaa au
huduma ambazo tayari ziko sokoni ili uwavutie wateja.

Kwa kufanya mambo yaliyoelezwa hapa juu utaweza kukuza biashara na


mtaji wako kwa muda mfupi zaidi.

2. Anza na unachokijua
Unapokuwa na mtaji mdogo huhitaji kuhusisha mambo mengi mageni au
yanayotegemea sana watu wengine kwa kuwa huna pesa za kuyagaramia.
Kwa mfano kama unaanzisha biashara ya ushonaji basi anza kutengeneza
mavazi yale unayoyaweza kwa kutumia vifaa ulivyonavyo; kwa njia hii
utajenga mtaji wako kisha baadaye utaweza kuajiri wengine watakao
kuwezesha kutengeneza aina nyingine zaidi.

Unapofanya kile unachokijua gharama huwa haziwi kubwa sana kwani ni kitu
unachokimudu mwenyewe.

3. Waambie watu unachokifanya


Waambie watu unachokifanya kwani hili litakuwezesha kupata wateja na
kufahamika. Watu wakijua unachokifanya watatamani kukifahamu zaidi; hili
litakuwezesha kupata wateja na kuongeza mtaji wako.

Usiogope kueleza kuwa unafanya biashara ya mboga, chakula, duka dogo la


bidhaa n.k. Kwani hujui unaemweleza atakuwa nani kwenye biashara yako.

Ukiwa na marafiki kwenye mitandao ya kijamii waeleze pia juu ya kile


unachokifanya.

4. Epuka gharama zisizokuwa za lazima


Kwakuwa bado una mtaji mdogo jitahidi kuepuka garama zisizo za lazima
kama vile ofisi ya kifahari, matangazo ya gharama kubwa n.k.

Kuwa na matumizi mazuri ya fedha hasa kwa mambo ya msingi tu. Watu
wengi wameshindwa kwenye biashara kwa sababu wameanza biashara kwa
mbwembwe za matumizi badala ya huduma bora zenye ubunifu.

5. Fanya kazi kwa bidii


Kamwe huwezi kuona mafanikio kama hutofanya bidii. Kumbuka wewe ni
mjasiriamali anayeanza hivyo ni lazima ufanye bidii ili soko litambue kuwa upo
pia unaweza.

Tumia muda vizuri, pia hakikisha unatoa huduma yenye ubora wa hali ya juu
kwa bei ambayo wateja wataweza kuimudu. Jitese kwa muda mfupi kwa
kipindi cha kuweka msingi wa biashara yako kwani hata kipindi cha kupanda
katika kilimo huwa ni cha taabu.

6. Tumia rasilimali na fursa zilizopo


Njia nyingine itakayokuwezesha kuanza biashara ukiwa na mtaji mdogo ni
kutumia fursa zilizopo. Kumbuka kuwa huwezi kutengeneza fursa kama
huwezi kutumia fursa zilizopo.

Tumia fursa kama vile mitandao ya kijamii ili kujitangaza. Pia unaweza
kutumia udhaifu uliopo katika biashara nyingine za watangulizi wako kama
fursa kwani unaweza ukarekebisha udhaifu huo kupitia biashara yako.

Zipo pia fursa za mikopo yenye masharti nafuu ambayo itakuwezesha


kuongeza mtaji wako. Kumbuka unahitaji kutumia mkopo kwa makini kwani
utahitajika kuurudisha pamoja na riba tena kwa wakati.

7. Jali wateja
Kujali wateja katika biashara ni jambo muhimu sana kama unataka kuona
matokeo chanya. Siku zote ninapenda kusema “wateja hufugwa”. Wateja
hufugwaje? Hufugwa kwa huduma nzuri.

Waheshimu wateja wako pia hakikisha unatimiza na kumaliza haja zao katika
ubora wa hali ya juu. Kumbuka siku zote mteja huja kwanza kabla ya pesa;
hivyo usitangulize pesa kabla ya huduma nzuri kwa mteja.

Ukilifanyia kazi hili utaweza kukuza biashara na mtaji wako kwa muda mfupi.

Hitimisho

Zilizojadiliwa hapa ni mbinu saba zitakazokuwezesha kuanza biashara na


mtaji mdogo. Usiogope unaweza hata kama una kiasi kidogo sana cha fedha.

Thubutu, nza, fanya bidii, weka nidhamu, mtangulize Mungu na hakika utaona
mafanikio chanya katika biashara yako.

“Anzia ulipo.Tumia ulicho nacho. Fanya unachoweza.


SOMO: 4

Makosa 15 Ambayo Kila Mjasiriamali Anatakiwa Kuyaepuka

Kuanza biashara kutoka kiwango cha sifuri siyo kazi rahisi. Kama mjasiriamali
utakutana na changamoto nyingi. Hili haliwezi kuwa tatizo ikiwa uko tayari
kujifunza kutokana na makosa na kufahamu njia za kuyaepuka huko mbeleni.
Hivi ndivyo wajasiriamali wengi wanavyojifunza na kukua. Unapokuwa
kwenye biashara ni lazima ufahamu makosa ambayo yanaweza kuathiri
biashara au uwekezaji wako; ili ujitahidi kuyaepuka ama kuyapunguza kadri
iwezekanavyo. Ni dhahiri kuwa wajasiriamali wengi wamekwama kutokana na
kupuuzia au kutofahamu makosa haya 15 ambayo hata wewe unatakiwa
kuyafahamu na kuyaepuka.

1.Kujifanya unafahamu kila kitu


Usijifanye unajua kila kitu, hasa kama ndiyo umeingia kwenye ulimwengu wa
kibiashara. Kwanini? Kwa sababu kuendesha biashara ni kujifunza na kupata
uzoefu. Jitahidi kujifunza na kujijengea uzoefu kupitia maarifa mbalimbali ili
uweze kuendesha biashara yako vyema kama mjasiriamali.

2. Kuanza biashara bila miundombinu


Ni dhahiri kuwa wengi husema “mwanzo ni mgumu” lakini ni lazima
utengeneze miundombinu kadhaa. Unapoanzisha biashara kama mjasiriamali
jitahidi kuweka miundombinu kadhaa ya muhimu kwanza kabla hujaanza
kufanya biashara. Kuendesha biashara kunahitaji vifaa na rasilimali kadha wa
kadha ambazo ni muhimu ziandaliwe kabla. Miundombinu hii inaweza
kuhusisha mtaji, vifaa muhimu, ofisi ndogo ya kuanzia, n.k Kumbuka hivi ni
vile vitu vya msingi tu na siyo mbwembwe zisizokuwa na msingi.

Soma pia: Jinsi ya kuanza biashara na mtaji mdogo.

3. Kuchagua mshirika asiyefaa


Awali ya yote, siyo lazima kuanza biashara kwa ushirika wa mtu mwingine.
Kama umejiandaa vyema unaweza kumudu kusimamia na kuendesha
biashara yako vyema bila tatizo. Lakini kama unahisi ni muhimu kuwa na
mshirika basi chagua mshirika ambaye mnaendana kifikra. Huyu
atakuwezesha na kukuunga mkono na kukusaidia kutimiza malengo na
maono yako. Lakini ukichagua mshirika siyefaa ni dhahiri atakuzamisha.

4. Kutazama mafanikio pekee


Biashara yako au mradi hauwezi kukua ikiwa mipango yako haibadiliki. Wewe
kama mjasiriamali unatakiwa ufikiri kwa upana unapokuwa unafanya
maamuzi. Kutazama tu mafanikio bila kuzingatia ubora wa huduma ni
kujizamisha majini wewe mwenyewe. Ni dhahiri kuwa kuzingatia kumudu
kuwa na ubora wa huduma pamoja na ukuaji wa biashara ni jambo zuri zaidi.

5. Kutaka wateja wakutafute


Je ni kweli kuwa unataka wateja wakutafute na wakati soko limejaa
wajasiriamali wengine na huduma? Hapana! Kama unataka kukuza msingi
wako wa wateja ni lazima uwe pale ambapo wateja wapo. Kwa kufanya hivi
watakutambua na kununua huduma au bidhaa yako.

6. Kupuuza nafasi ya teknolojia


Wajasiriamali wengi wa Kiafrika wanadhani kuwa teknolojia ni kwa ajili ya
wazungu au kampuni kubwa. Haijalishi ni biashara au mradi gani unaoufanya
ni lazima uzingatie nafasi ya teknolojia. Teknolojia iko kila mahali; hivyo ni
vyema ukatumia teknolojia kama vile intaneti kutangaza, kuuza, na hata
kuwasiliana na wateja wako.

7. Matumizi mabaya ya fedha


Watu wengi hawana matumizi mazuri ya fedha hasa wao binafsi. Tatizo hili
limekuwa pia likijitokeza pale mtu anapotakiwa kusimamia na kutunza pesa za
mradi au biashara. Wengi huishia kuzitumia kwenye mambo yao binafsi au
kwa mambo ambayo hayana tija kwa kampuni au mradi. Ni lazima uwe na
nidhamu ya pesa kama mjasiriamali ili uweze kuiwezesha biashara yako
kukua; tambua hii ni pesa ya mradi au biashara na si ya matumizi yangu
binafsi.
8. Kujipanua bila mipango
Wajasiriamali wengi huwa wana mawazo makubwa na mazuri lakini
wanakosa mikakati na mipango mizuri ya kuitekeleza. Unafungua mradi fulani
leo na unafanikiwa ndani ya muda mfupi, nawe bila hata kujenga msingi imara
wa kiuchumi na rasilimali nyingine unakimbilia kufungua mwingine au tawi. Hili
ni kosa ambalo limeua maduka mengi yanayoanzishwa na wajasiriamali.
Jifunze kujiandaa na kuweka misingi imara pale unapotaka kupanua au
kuongeza mradi wako ili ule wa awali usife.

9. Kutokuajiri wafanyakazi wenye uwezo


Kama ni lazima kuajiri watu basi epuka kosa hili ambalo mara nyingi
wajasiriamali hulifanya kwa huogopa garama za kuajiri watu wenye uwezo
kwa ajili ya kufanya nao kazi. Ni dhahiri kuwa “rahisi inaumiza”; hivyo ni
vyema ukaajiri hata mtu mmoja bora kuliko kuajiri watano wenye uwezo duni.
Ukizingatia hili utajikuta unapata matokeo stahiki kutoka na kile ulichowekeza.

10. Kupuuza maoni ya wateja


“Mteja ni mfalme”; je unalifahamu hili? Wajasiriamali wengi hupuuzia maoni ya
wateja bila kujua kuwa maoni ya wateja ndiyo huwawezesha kujirekebisha na
kuweza kuwapa wateja wao kile wanachokihitaji. Kosa hili lisiposhughulikiwa
litakupotezea kiasi kikubwa cha wateja na kuleta matokeo mabaya kwenye
biashara au mradi wako.

11. Kuacha fursa zipite


Wajasiriamali wengi hupenda kungojea mazingira yawe mazuri bila hata kujali
fursa zinazopotea. Ni dhahiri kuwa hakuna mtu atakaye kutengenezea
mazingira unayotaka; ukiona fursa itumie na mambo yatakaa vyema mbele ya
safari. Inawezekana fursa unayoiona leo kesho isiwepo tena.

12. Kukataa ushauri wa kitaalamu


Kila kitu kizuri kinahitaji maarifa stahiki ili kiweze kutokea. Ni dhahiri kuwa
wajasiriamali wengi wanafanya kosa la kupuuza ushauri wa kitaalamu katika
kazi zao kwa kuona kuwa hauna nafasi. Kwa mfano kama unafuga kuku au
unalima mazao fulani kwanini usimwite mtaalamu wa kilimo au mifugo ili
akushauri? Ni dhahiri kuwa ukipata ushauri wa kitaalamu utakuwa mwenye
tija zaidi.

13. Kutokwenda na soko


Mjasiriamali mzuri ni yule anayefahamu kuwa kwa sasa soko linataka nini. Ni
lazima uweze kuepuka kosa la kutokutazama mahitaji ya soko, ili uhakikishe
mauzo ya bidhaa au huduma yako hayaathiriki. Kwa mfano zamani watu
walinunua zaidi kuku walio hai, lakini leo soko la kuku waliochinjwa ni kubwa
pia; kwanini wewe bado unauza tu kuku walio hai? Ni dhahiri ukitazama
mfano huu utaona jinsi kosa hili linavyowaathiri wajasiriamali wengi katika
maeneo mbalimbali.

14. Kushindwa kubaini wateja lengwa


Ni lazima wewe kama mjasiriamali uwabaini wateja wako ili huduma au
bidhaa yako iuzike. Kwa mfano umetengeneza dawa ya kuua mbu, kisha
unaiuza mikoa ya baridi badala ya mikoa yenye joto (kwenye mbu wengi); ni
dhahiri kuwa hutoweza kupata wateja wa bidhaa yako sawa sawa. Chukua
hatua leo watafute na uwafuate wateja sahihi wa huduma au mradi
unaoufanya.

15. Mbinu duni za masoko


Maswala ya masoko ni taaluma kamili ambayo watu hujifunza katika shule na
vyuo mbalimbali. Hivyo ni muhimu wewe kama mjasiriamali kutokupuuzia
taaluma hii kwani ndiyo itakayokuwezesha kubaini njia bora na sahihi za
kuuza huduma au bidhaa yako. Hakikisha mbinu za masoko unazifahamu
vyema tena zinaendana na soko husika la bidhaa yako. Hakikisha pia mbinu
zako zinabadilika kulingana na mazingira na hali ya soko.

Neno la Mwisho: Maarifa sahihi ni msingi wa kufanya vitu kwa ubora. Ni


dhahiri kuwa makosa mengi yaliyoelezwa hapa yanatokana na ukosefu wa
maarifa stahiki ya ujasiriamali. Nakushauri ujifunze kila siku ili kupanua uwezo
na uzoefu wako wa kiujasiriamali. Pia usisahau kuweka kwenye matendo yale
yote unayojifunza.
SOMO: 5

Kanuni 15 za Ujasiriamali Ambazo ni Lazima Uzifahamu

Ikizingatiwa kuwa upatikanaji wa ajira umekuwa wa shida sana, watu wengi


hujikuta wakiwa na chaguo la kuwa wajasiriamali pekee kwenye maisha yao.

Wengi hutamani au hata kujiingiza kwenye ujasiriamali, lakini siyo wote


wanaofanikiwa kutokana na kutokufahamu kanuni muhimu za ujasiriamali. Ni
wazi kuwa ili uanzishe kitu chochote chenye mafanikio, ni lazima ufahamu
kanuni za kukifanya kitu hicho jinsi ipasavyo.

Ikiwa wewe ni mjasiriamali, au unataka kuwa mjasiriamali, basi fuatilia makala


hii ili nikufahamishe kanuni 15 za ujasiriamali.

1. Kuwa mtatuzi wa matatizo


Ujasiriamali ni zaidi ya kupata pesa, ni lazima kwanza utatue changamoto ya
mtu ndipo utaweza kupata pesa kutoka kwa mtu husika. Ni muhimu
ukafahamu kanuni hii kama mjasiriamali kwani hutojikita kutafuta pesa bali
utajikita kutatua matatizo ya watu.

Kwa mfano kama kuna tatizo la upatikanaji wa mboga katika mji au eneo
unalokaa, ikiwa wewe utaleta mboga katika eneo hilo ni wazi kuwa watu
watakupa pesa ili uwape mboga. Hivyo ni muhimu kila mara ukatafuta
changamoto ukaitatua, nawe bila shaka utapata pesa za uhakika.

“Pesa ni matokeo ya kutatua shida ya mtu”

2. Kuwa na maono
Hakuna ujasiriamali bila maono. Kuwa mjasiriamali bila maono ni sawa na
kuendesha gari isiyokuwa na usukani. Maono katika ujasiriamali
yatakuwezesha kukuongoza ufanye nini na kwa muda gani. Ni lazima ujiulize
kuwa unataka kuwa nani, lini na unataka kufanya nini baadaye? Jonathan
Swift alisema maono ni sanaa ya kuona kile ambacho wengine hawaoni. Ni
lazima uwe na lengo na ufanye bidii kulifikia.
“Wajasiriamali waliofanikiwa ni wale walioweza kubadili maono
yao kuwa uhalisia”

3. Chagua washirika au timu sahihi


Wakati mwingine utahitaji kufanya kazi na watu au mtu fulani. Ni muhimu
kuwa makini wakati wa kuchagua washirika au timu ya kufanya nayo kazi ili
kuhakikisha maono yako hayakwamishwi. Kamwe usichukue mtu tu kwa
kigezo kuwa ni rafiki au ndugu yako, bali chukua mtu ambaye unaamini
anaweza kufanya kitu chenye tija kwa ajili ya kufanikisha malengo yako kama
mjasiriamali.

4. Toa huduma au bidhaa yenye tija


Hivi leo sokoni kuna bidhaa na huduma nyingi ambazo ni za aina moja, lakini
siyo zote zinafanya vizuri. Hii ni kutokana na baadhi ya bidhaa au huduma
kutozingatia kuwa na tija kwa wateja wake. Ikiwa unatengeneza bidhaa au
huduma fulani hakikisha itakuwa na manufaa makubwa na ya uhakika kwa
wateja wako.

Kwa mfano nimewahi kuona vitafunwa vilivyoandaliwa katika mazingira duni


na kuwa na dosari mbalimbali kama vile marashi, vipande vya nywele,
mchanga n.k. Ni wazi kuwa bidhaa za namna hii zitakosa wateja kutokana na
kuwa na ubora duni.

Kila mara kumbuka kuwa ushindani ni mkubwa, hivyo jitahidi kuongeza tija na
ubora wa huduma na bidhaa zako.

5. Fahamu na jali wateja


Ikiwa wewe ni mjasiriamali, basi futa mawazo kuwa wateja wanakuhitaji
wewe. Fahamu kuwa wewe kama mjasiriamali, ndiye unaye wahitaji wateja ili
ukuze biashara au huduma yako. Hakikisha mambo haya kuhusu wateja:

 Fahamu wanataka nini.


 Sikiliza maoni na ushauri wao.
 Hakikisha unakamilisha mahitaji yao.
 Tumia lugha nzuri na rafiki kwa wateja.
 Mfanye mteja aone unamthamini.
 Mfanye mteja aone kuwa umetanguliza huduma kabla ya pesa.

Naamini kwa kufanya hivi utaweza kujijengea msingi mzuri wa wateja kwa ajili
ya huduma au bidhaa zako kila siku.

6. Tumia pesa vyema


Changamoto ya matumizi mabaya ya pesa inawakabili watu wengi kuanzia
kwenye matumizi yao binafsi ya pesa. Watu wengi wanapata pesa lakini
zinaisha bila ya kufahamu wamezitumiaje au wamefanya kipi chenye tija.

Ni wazi kuwa matumizi mazuri ya pesa ni kanuni muhimu sana kwa


mjasiriamali, kwani kwa njia hii utaweza kukuza biashara yako kila siku.
Jifunze kufahamu hii ni pesa kwa ajili ya nini, na uitumie kwa mambo ya
msingi pekee. Epuka tabia za kibadhirifu na anasa. Ikiwa biashara au
uwekezaji wako ni mkubwa, basi unaweza kumwajiri mtu aliye na taaluma ya
utunzaji na usimamizi wa pesa.

Unaweza pia kujifunza wewe mwenyewe jinsi ya kutunza na kutumia pesa


vyema; unaweza pia kutumia programu za bure za kompyuta kama vile Wave
app kutunza mahesabu yako.

7. Jifunze kusema hapana


“Hapana” ni jibu dogo lakini lenye manufaa makubwa. Ikiwa wewe ni
mjasiriamali ni muhimu kuzingatia kanuni hii ya kusema hapana kwani
itakutenga na mambo au mipango isiyokuwa na ulazima.

Kuna watu, mipango, vitu au hata tabia ambazo zinaweza kukuathiri vibaya
sana kwenye ujasiriamali wako. Hivyo kusema hapana kutakuepusha kwa
kiasi kikubwa na mambo haya.

8. Usipuuze nafasi ya teknolojia


Tunaishi kwenye ulimwengu wa sayansi na teknolojia, hivyo wewe kama
mjasiriamali huwezi kujitenga nao. Kwa kupitia teknolojia kama vile simu na
mtandao wa intaneti, unaweza kuwafikia watu wengi zaidi na kuongeza
mauzo ya huduma au bidhaa zako.
Hakikisha wewe kama mjasiriamali unakuwa karibu na wateja wako ili kutatua
shida na mahitaji yao; pia hakikisha unajifunza mbinu bora za kufanya
biashara kupitia mtandao.

9. Fahamu soko
Kanuni mojawapo ya kuongeza mauzo yako kama mjasiriamali ni kulifahamu
soko vyema. Hakikisha huduma au bidhaa unayoitoa inakidhi mahitaji na
inafika kwenye soko stahiki.

Kwa mfano ikiwa wewe ni mzalishaji wa mayai, lakini eneo ulilopo soko ni
duni, basi tafuta eneo jingine ambalo soko la bidhaa hii ni nzuri. Ikiwa wewe
huwezi kwenda, unaweza kutafuta mtu kwenye eneo lenye soko zuri
akakuuzia bidhaa yako na ukampa gawio fulani.

Kwa kufanya hivi utaweza kulenga soko na kujiongezea faida zaidi wewe
kama mjasiriamali.

10. Ongeza maarifa


Kwanza nikupongeze kwa kusoma makala hii, ni wajasiriamali wachache
sana ndiyo hupenda kusoma makala na vitabu mbalimbali ili kuongeza
maarifa. Ni muhimu sana kila mara ukajizoesha kujiongezea maarifa, hasa ya
ujasiriamali pamoja na kile unachokifanya; hili liitakuwezesha kuwa na tija na
kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Unaweza kusoma vitabu, majarida na tovuti
mbalimbali (kama fahamuhili.com) ili kuongeza maarifa yako.

11. Jifunze kutokana na makosa


Moja ya kanuni inayozingatiwa na wajasiriamali waliofanikiwa ni kujifunza
kutokana na makosa. Makosa ni shule nzuri sana kwa kila mtu hasa
wajasiriamali. Ikiwa uliwekeza ukapata hasara, basi jifunze nini hasa kilikuwa
chanzo cha hasara ili mbeleni uweze kukiepuka. Usikubali kukwamishwa na
makosa, bali yawe ni hamasa kwako ya kuendelea mbele zaidi.

“Uzoefu ni kufanya makosa na kujifunza kutokana na makosa


hayo”
Bill Ackman

12. Jifunze kwa waliofanikiwa


Watu wengi wameshindwa kufanikiwa kwenye maisha yao kwa sababu
wanajifunza kwa walioshindwa. Walioshindwa wana maneno mengi, hasa ya
kukatisha tamaa kama vile hili haliwezekani, hili linahitaji pesa nyingi sana,
mimi lilinishinda, linachosha, lina faida ndogo, kuna wengi wanaolifanya, fulani
alishindwa n.k.

Wewe kama mjasiriamali, epuka watu hawa na ujifunze kwa waliofanikiwa,


fahamu walitatua vipi changamoto walizokabiliana nazo pamoja na mipango
waliyoitumia hadi wakafika hapo walipo.

13. Tumia muda vizuri


Hakuna mtu mwenye zaidi ya saa 24 duniani; lakini mwingine muda
unamtosha wakati mwingine analalamika muda haumtoshi. Ni wazi kuwa
mpangilio au matumizi mabaya ya muda ndiyo husababisha changamoto hii.
Wewe kama mjasiriamali ni muhimu ukaondoa mambo yasiyokuwa na
ulazima kwenye ratiba yako. Tambua ni kitu gani ni cha muhimu zaidi na
ukifanye kwa wakati.

14. Weka vipaumbele


Wewe kama mjasiriamali, ni muhimu kuzingatia kanuni hii ya kujiwekea
vipaumbele; vipaumbele vitakuwezesha kubaini ni kipi kianze na ni kipi kifuate
kutokana na umuhimu wake.

Kwa mfano ikiwa kuna wateja walipata shida kupata huduma au bidhaa yako,
maliza kwanza swala hili kabla ya kuendelea kuweka jitihada za kuuza bidhaa
mpya. Kwa kufanya hivi utaweza kufanya mambo kutokana na umuhimu
wake, jambo ambalo litakuwezesha kukua.

15. Usikate tamaa


Ni wazi kuwa katika safari ya ujasiriamali utakutana na changamoto
mbalimbali. Jambo la msingi ni kukumbuka kanuni hii kuwa usikate tamaa.
Tumia changamoto kama chachu ya kukuhamasisha kufanya bidii zaidi na
usirudi nyuma.

Changamoto zipo leo na kesho lakini keshokutwa hazitakuwepo tena; jambo


unalotakiwa kufanya ni kutazama lengo lako na kufanya bidii kila kukikucha
kuzikabili changamoto husika ili ufikie lengo lako.

“Siri ya mafanikio yetu ni kutokukata tamaa”

SOMO: 6
Mambo ya Kuzingatia Kabla ya Kuchagua Jina la Biashara

Uteuzi wa jina la biashara ni hatua muhimu kama ilivyo kwa jiwe la pembeni
katika nyumba. Watu wengi wamekuwa hawatilii maanani mambo muhimu ya
kuzingatia wakati wa kuchagua jina la biashara au kampuni.

Nimekuwa nikishuhudia makapuni mengi yakitumia majina ya ajabu ajabu


yasiyoendana na biashara zao. Kwa sehemu kubwa kufanikiwa na kujulikana
kwa biashara yako kunategemea jina la biashara yako.

Fuatana nami katika makala hii ambayo nitakueleza mambo kadhaa ya


kuzingatia kabla ya kuchagua jina la biashara.

1. Uhusiano wa jina na bidhaa au huduma


Je unafahamu kwamba jina la biashara linatakiwa liakisi huduma au biashara
unayoifanya? Ni jambo jema kutumia jina linaloakisi kile unachokifanya. Kwa
mfano jina kama vile “Samelctro” lifaa kwa kampuni ya vifaa vya kielektroniki,
“Pamba LTD” lifaa kwa kampuni ya upambaji au mavazi.

Itakuwa ni jambo la kushangaza kutumia “Samelctro” kwenye mavazi au


kutumia “Pamba LTD” kwenye vifaa vya kielektroniki. Ukizingatia hili mapema
utaweza kuitambulisha bidhaa au huduma yako vyema kwa kupitia jina la
biashara yako.
2. Jina fupi linalovutia na kueleweka
Uchaguapo jina la la biashara au kampuni yako kaa chini tafuta jina fupi lenye
mvuto na linaloeleweka.

Usitumie majina magumu na marefu kama vile “matunda bora ya shamba”,


“rextymyshoes” “mauaborasana”, “John Noe na Rose Mewa Beauty Saloon”,
n.k. Chagua jina fupi linalovutia ambalo pia ni rahisi kwa watu kulikumbuka.

3. Zingatia mahitaji ya kimtandao


Katika swala hili nimeshuhudia watu wengi wakichukua majina ya biashara au
kampuni bila kujali swala la matumizi ya mtandao. Kwa mfano mtu anaweza
kusajili kampuni inayoitwa hope, smart, green nk.

Majina haya huwezi kuyatumia kwenye mtandao kwani tayari yameshatumika


katika mambo mengi sana; hapa hutoweza kupata huduma kama vile anwani
ya tovuti au baruapepe inayoendana na jina la kampuni yako.

Hivyo basi tumia huduma kama vile (Whois) kutazama kama unaweza kupata
anwani ya matandao inayoendana na jina la kampuni au laa.

Kumbuka haina maana kampuni kuitwa Moja LTD halafu ikawa na tovuti
inayoitwa “http://mbili.com”; hapa utapoteza watu, hawataweza kuifikia tovuti
yako vyema.

4. Upekee
Kama nilivyoeleza katika hoja zilizopita hapo juu ni muhimu kuhakikisha
unabuni jina lenye upekee kwa ajili ya biashara yako. Epuka kutumia majina
yanayofanana na majina mengine.

Kumbuka zipo shereia za kimataifa zinazolinda majina ya kibiashara (Brands)


za kampuni mbalimbali; majina kama vile Microsofti, Thetoyota, Delli,
Vodacomu n.k yatakupelekea kuingia kwenye mgogoro wa kisheria na
makampuni husika kwani majina haya yanalandana sana na majina ya
kampuni zao.
5. Zingatia mahitaji ya baadaye
Inawezekana jina la kampuni au biashara linalofaa leo lisifae tena kwa ajili ya
biashara yako baadaya ya miaka mitano. Hivyo ni vyema kuchagua jina
ambalo utadumu nalo katika kampuni yako.

Kwa mfano mtu akiita kampuni yake 3GNetworks au 4GNetworks, baada ya


mika mitano 3G na 4G kwenye jina hazitakuwa za maana tena kwani
tutakuwa tayari tuna teknolojia mpya za 5G n.k.

Hivyo ni muhimu kuzingatia kuwa jina unalolichagua leo litakufaa pia kwa
upanuzi na matumizi ya baadaye ya biashara yako.

Hitimisho

Kwa kuhitimisha ninapenda kukushauri kuzingatia umakini na utafiti wa


kutosha katika kuchagua jina la biashara yako. Hakikisha kama unahusisha
watu wengine katika machakato huu wawe ni wale wanaoilelewa vyema
biashara au kampuni yako.

SOMO: 7
Fahamu Njia 8 Unazoweza Kuzitumia ili Kupata Mtaji

Nifanyeje nipate mtaji? Nina wazo zuri lakini sina mtaji? Haya ni maswali
ambayo nimekuwa nikiulizwa sana na wasomaji wa Fahamuhili.com, pamoja
na watu wengi ninaokutana nao kwenye maisha ya kila siku.

Kutokana na sababu hii, nimeona ni vyema niandae makala ambayo itajibu


maswali ya wasomaji wangu pamoja na wale wote wenye maswali kama
haya.

Ingawa mtaji siyo kigezo pekee cha kufanikiwa kwenye biashara au mradi
unaoufanya, mtaji unabaki kuwa kiungo muhimu sana katika kutekeleza wazo
fulani au mradi kwa ufanisi. Kwa kuwa watu wengi huanzisha miradi au
biashara kwa lengo la kupata pesa, huwa vigumu sana kuwa na pesa za
kutosha kuanza utekelezaji wa wazo hilo.

Karibu ufuatilie makala hii kwa karibu nikushirikishe njia 8 unazoweza


kuzitumia ili kupata mtaji wa kutekeleza wazo lako.

1. Akiba binafsi
“Mtu anayeweka akiba, ni mtu anayewaza kuhusu kesho.”
Mara kadhaa nimekuwa nikieleza kuwa kuweka akiba kuna manufaa
kemkem, ikiwemo kupata uwezo wa kuwahi fursa mbalimbali na kuzifanyia
kazi kwa wakati.

Hivyo basi, unaweza kutunza kiasi fulani cha pesa katika kipato chako
hatakama ni kidogo, ili uweze kupata mtaji wa kuanzisha biashara au mradi
wako.

Kumbuka! Usitake kuanza biashara na mtaji mkubwa sana kwani kuna hatari
ya kuupoteza, jega mtaji wako kidogokidogo; unaweza kuanza na mtaji wa
shilingi 10,000 lakini baadaye ukakua na kuwa mamilioni ya pesa.

2. Kubadilisha mali na vitu binafsi


Nimewahi kukutana na watu kadhaa wakilalamika kuwa hawana mtaji, lakini
ukiwachunguza sana utagundua kuwa wamezungukwa na mitaji mikubwa
wasiyoitambua.

Hakuna haja yoyote ya kuwa na simu, televisheni, Kompyuta, na nguo za


thamani kubwa wakati hauna mtaji wa kutekeleza mradi wako.

Unaweza kuuza vitu vyote ambavyo ukivikosa hutokufa ili uweze kupata mtaji;
kumbuka uwekezaji ni muhimu kuliko maisha ya kifahari na anasa.

Ikumbukwe kuwa ukiwekeza utaweza kutengeneza pesa nyingi zaidi na


kumudu kununua vitu vingine bora zaidi huko mbeleni.
3. Ndugu na marafiki
Ikiwa una mahusiano mazuri na ndugu zako, wanafamilia au marafiki, kwanini
unaona shida kuwaomba wakuwezeshe kupata mtaji?

Andaa wazo vizuri, tafuta watu au marafiki wakaribu watakaokuamini,


waombe wakuwezeshe kupata mtaji na uwaahidi utaurejesha mapema kadri
uwezavyo ili wakuamini.

Faida za mtaji au mkopo kutoka kwa marafiki na ndugu:

 Mara nyingi hakuna riba.


 Hakuna masharti na vigezo vigumu.
 Upatapo shida katika biashara au mradi wako ni rahisi ndugu kukuelewa.

Kumbuka! Usicheze na mtaji wa biashara au mradi kwa kuwa umeupata


kutoka kwa ndugu au marafiki; pia kumbuka kuwa mwaminifu kutimiza
mapatano ili wakati mwingine usaidike.

4. Taasisi za kuwezesha wajasiriamali


Hivi leo kuna taasisi na mashirika mbalimbali yanayotoa mitaji ya fedha na
vifaa kwa wajasiriamali mbalimbali ili waweze kutekeleza mawazo yao.

Baadhi ya taasisi hizo ni:

 Small Starter
 Africa Connekt
 Iesc

Hivi leo kuna taasisi na mashirika mbalimbali yanayotoa mitaji ya fedha na


vifaa kwa wajasiriamali mbalimbali ili waweze kutekeleza mawazo yao.

Fuatilia vyombo mbalimbali vya habari pia jiunge na vikundi vya wajasiriamali
wengine ili zitokeapo fursa za mitaji uweze kuzifahamu na kuzitumia.
5. Mikopo ya taasisi za kifedha
Hivi leo ziko taasisi kedekede zinazotoa mikopo kwa ajili ya watu mbalibali;
hivyo, mikopo kutoka kwenye taasisi za kifedha inaweza kutumiwa kama mtaji
mzuri sana wa biashara.

Hata hivyo nimekuwa nikiwashauri wajasiriamali wengi hasa wachanga


kutokupendelea njia hii, ikiwa hawajaweka mikakati sahihi ya kutumia na
kurejesha mkopo husika.

Hakikisha kama unataka kutumia njia hii kupata mtaji wa biashara au mradi
wako, umejipanga vyema na unafahamu wazi njia na mbinu utakazozitumia
kurejesha mkopo wa taasisi husika hata kama mambo yatakwenda mrama.

6. Ubia au uwanahisa
Katika dunia yetu ya leo, wapo watu wengi wenye fedha lakini hawajapata
mahali pa kuwekeza fedha zao; wengi huwa na pesa nyingi lakini hawana
muda wa kuanzisha na kusimamia biashara au mradi.

Unaweza kutumia mbinu hii kupata mtaji, kwa njia ya kuingia ubia au
uanahisa na mtu au watu wengine wenye mitaji wanaotafuta mahali
pakuiwekeza.

Kwa mfano unaweza kumfuata mtu mwenye pesa na ukamwomba


akufungulie biashara au mradi; kisha utampa asilimia fulani ya faida ya
biashara au mradi huo kwa kipindi fulani hadi utakapokuwa umereejesha mtaji
wake na kiasi fulani cha asante au riba.

7. Mali kauli
Najua umeshajiuliza ‘mali kauli’? Ndiyo, mali kauli ni njia nyingine bora kabisa
unayoweza kuitumia kupata mtaji wa biashara kwa kutegemea uaminifu wako.

Zipo biashara kubwa zenye mali nyingi lakini zina mzunguko mdogo katika
eneo husika; lakini inawezekana wewe unafahamu mahali ambapo mali hizo
zikiuzwa zitauzika vizuri. Unachopaswa kufanya ni kuchukua mali kwenye
biashara husika na kwenda kuziuza kisha unarejesha fedha ya mauzo ya
bidhaa husika na yule mwenye biashara atakupa gawio fulani kwa kazi hiyo.
Ikiwa utakuwa mwaminifu na kufanya kazi hii kwa bidii, ndani ya muda mfupi
utapata mtaji wa kuanzisha biashara yako mwenyewe ambayo imetokana na
kuuza mali za biashara nyingine kubwa kwa kuaminika tu (mali kauli).

8. Mashindano
Je, unajua kuna watu wametoka kimaisha kutokana na mitaji waliyoipata
kutokana na mashindano mbalimbali?

Hivi leo, yanaendeshwa mashindano mbalimbali hasa yale yenye lengo la


kuibua wajasiriamali wenye mawazo mazuri lakini hawana mtaji. Mfano Mzuri
ni Shindano la 3N lililokuwa likiendeshwa na hayati Regnald Mengi lenye
lengo la kuwaibua vijana wajasiriamali.

Hivyo basi, unaweza kushiriki mashindano haya, na ukaibuka mshindi na


ukajipatia mtaji wa kutosha kutekeleza wazo lako. Kumbuka kuweka nidhamu
kwenye pesa unayoipata kwenye mashindano; kwani kutokana na kupatikana
kwake bila kutarajia; inaweza kutumiwa vibaya na ikapotea.

Hitimisho

Naamini hadi kufikia hapa umepata mwanga wa ni njia gani unaweza kuitumia
ili kupata mtaji kwa ajili ya kutekeleza wazo au mradi wako.

Napenda kukukumbusha kuwa mtaji siyo kila kitu na wala siyo kiasi cha pesa;
bali usimamizi na mikakati sahihi kwenye kile unachaokifanya vitakuwezesha
kukuza mtaji wako na kufikia malengo yako.

SOMO: 8

Sifa 10 Ambazo Kila Mjasiriamali Anatakiwa Kuwa Nazo

Kwa hakika ujasiriamali ni chaguo muhimu sana kwenye karne hii ya sasa ili
kujipatia kipato. Hivi leo kuna wajasiriamali wengi waliofanikiwa na wengine
hawajafanikiwa.
Kwa hakika wajasiriamali waliofanikiwa wanafahamu na wanaziishi sifa za
wajasiriamali bora. Ni wazi kuwa huwezi kuwa mjasiriamali bora wakati una
sifa za mwajiriwa.

Ili kuwa mjasiriamali ni lazima kuzifahamu na kuziishi sifa za mjasiriamali.


Karibu nikufahamishe sifa 10 za mjasiriamali.

1. Mwenye malengo
Malengo ni mwongozo wa kukuwezesha kufanikisha jambo lolote. Kuwa na
malengo ni sifa muhimu ambayo kila mjasiriamali anapaswa kuwa nayo. Je
umeamua kuwa mjasiriamali kwenye nini? Kwa ajili ya nini?

Malengo yatakuongoza ufanye nini, wapi lini na kwa ajili ya nini. Bila malengo
utafanya mambo bila mwongozo wowote na ni vigumu kufanikiwa.

2. Nidhamu
Nidhamu ni sifa muhimu kwa mjasiriamali kwani itamtenga na mambo mengi
yasiyokuwa na umuhimu. Ni lazima mjasiriamali awe na nidhamu ya maswala
kama vile matumizi ya muda pamoja na pesa.

Kila mjasiriamali anapaswa kujinyima na kukataa vitu vyote ambavyo


havimwezeshi kufikia malengo yake.

3. Ujasiri na uthubutu
Ujasiri na uthubutu ni sifa muhimu sana kwa mjasirimali ili aweze kutekeleza
malengo yake. Ujasiriamali ni swala linalohitaji ujasiri na uthubutu wa
kuchukua maamuzi magumu hata kama kuna changamoto au hatari kadha
wa kadha.

Huwezi kuwekeza pesa zako kwenye mradi au biashara yoyote kama


hutokuwa na ujasiri na uthubutu. Ujasiri na uthubutu hautaruhusu hofu na
mashaka ya kushindwa au kupata hasara vikutawale.
4. Ubunifu
Ubunifu humtofautisha mjasiriamali mmoja na mwingine. Unahitaji ubunifu ili
ubuni wazo la pekee ambalo litakupa matokeo mazuri. Wajasiriamali wengi
hawana ubunifu ndiyo maana wanakwama.

Kwa mfano mjasiriamali mmoja akianzisha biashara ya kuuza maandazi, basi


wengine 20 wataiga. Ni lazima mjasiriamali uwe na ubunifu utakaokuwezesha
kufanya mambo yenye tija.

5. Uvumilivu
Kila jambo lina changamoto zake. Ujasiriamali una changamoto nyingi
ambazo zinahitaji uvumilivu ili kuzimudu.

Hivyo basi, sifa ya kuwa na uvumilivu ni muhimu sana kwa kila mjasiriamali
anayetaka kufanikiwa. Haijalishi umepata hasara au unakutana na
changamoto nyingi kiasi gani, ni muhimu kuvumilia.

6. Bidii
“Mafanikio huja kwa wale ambao wanafanya bidii kubwa
kuyatafuta.”

Henry David Thoreau


Bidii ni msingi wa kufanikiwa kwenye jambo au shughuli yoyote. Ni muhimu
kukumbuka kuwa mjasiriamali ni mwajiri (boss) wake yeye mwenyewe. Hivyo
ni muhimu kujituma na kufanya kazi kwa bidii bila kusukumwa na mtu yeyote.

7. Kupenda anachokifanya
“Fanya unachokipenda na pesa zitafuata.”

Marsha Sinetar
Watu waliofanikiwa sana duniani, wanafanya kile wanachokipenda.
Unapofanya kile unachokipenda ni rahisi kufanikiwa kwani utakifanya kwa
moyo, bidii pamoja na kutokata tamaa.

Kila mjasiriamali anatakiwa kuhakikisha kuwa anafanya kitu anachokipenda ili


aweze kufikia malengo yake.

8. Kuishi na watu vizuri


Kila mjasiriamali anahitaji watu wengine ili kufanikisha malengo yake ya
ujasiriamali. Kuishi na watu vizuri ni sifa muhimu kwa mjasiriamali kwani
itamjengea soko zuri pamoja na nguvu kazi bora.

Hakuna haja ya kudharau au kutenga watu bila sababu. Usijenge chuki au


ugomvi usiokuwa na sababu kati yako na watu wengine. Kumbuka kuwa watu
ndio chanzo na msingi wako wa kupata faida.

9. Mwenye kupenda kujifunza na mtafiti


Katika swala zima la ujasiriamali, kutafiti na kupenda kujifunza ni tabia
muhimu sana. Kila mjasiriamali anatakiwa kuwa na sifa hii ili aweze kujifunza
na kutafiti njia na mbinu mbalimbali ambazo zinaweza kumfanya mwenye tija
zaidi.

Ni muhimu kukumbuka kuwa kuna wakati mjasiriamali anatakiwa kukaa chini


kutafiti na kujifunza mambo mbalimbali ambayo yatamwezesha kufanikiwa
kwenye kile anachokifanya.

10. Kujifunza kutokana na makosa


Kama ulivyowahi kusikia mara kadhaa kuwa makosa ni shule muhimu kwa
kila mtu, ndivyo ilivyo pia kwa mjasiriamali.

Mjasiriamali anapaswa kuwa na sifa ya kupenda kujifunza kutokana na


makosa ili asiyarudie tena mbeleni na wala si kuyaogopa au kuyakimbia.

Kama uliwekeza pesa zako zikapotea, basi usiache ujasiriamali bali baini ni
nini kilisababisha ukapoteza pesa zako ili ukiepuke mbeleni.
Neno la mwisho

Naamini ukiwachunguza vyema wajasiriamali waliofanikiwa utabaini kuwa


wana tabia hizi zilizoelezwa hapa. Ni muhimu wewe kama mjasiriamali
kuhakikisha unajitahidi kuwa na tabia zilizoelezwa hapa ili ufikie malengo
yako.

SOMO: 9

Njia 10 Zitakazokuwezesha Kutumia Pesa Vyema


Je, huwa unajisikia vibaya unapohitaji pesa kwa ajili ya matumizi yako lakini
unajikuta mifuko yako ni mitupu? Haijalishi unapata pesa kiasi gani, swala la
matumizi mazuri ya pesa ni jambo muhimu; hili litakuwezesha kuwa na kitu
wakati wa uhitaji.

Watu wengi wanapata pesa lakini si wote wanaoweza kuzitumia vyema.


Wengi hujikuta wakizitumia kwenye mambo na mipango ambayo mwishoni
haiwaletei tija katika maisha yao.

Naamini ungependa kuwa na matumizi mazuri ya pesa; sasa fahamu njia 10


zitakazokuwezesha kutumia pesa vyema.

1. Weka bajeti
Ni rahisi kusikia watu wakilalamikia bajeti za serekali na kuzikosoa lakini wao
wenyewe hawana bajeti zao binafsi. Unawezaje kukosoa bajeti ya serekali
wakati ya kwako mwenyewe imekushinda? Fikiri tofauti; tambua umuhimu na
jinsi ya kujiwekea bajeti. Bajeti yako binafsi itakuwezesha kufahamu mapato
yako, mambo gani muhimu unayotakiwa kuyafanya na yatakugharimu kiasi
gani cha pesa. Kwa kufanya hivi utaweza kutafuta na kutumia pesa kulingana
na bajeti uliyojiwekea na kuokoa pesa ambazo zingepotea bila sababu.
2. Panga manunuzi kabla
Ni muhimu kupanga manunuzi yako kabla ya kwenda sokoni au dukani. Hili
litakuwezesha kubainisha nini unachotakiwa kununua na kwa gharama gani.
Unapokwenda sokoni au dukani bila kupanga manunuzi yako ni rahisi
ukanunua vitu ambavyo hukuvipanga. Unaweza kuorodhesha vitu katika
kipande kidogo cha karatasi pamoja na bei zake ili uwe ni mwongozo wako
katika manunuzi.

3. Weka vipaumbele
Kuna mahitaji mengi kwenye maisha ya mtu; lakini kuna yaliyo muhimu zaidi
kuliko mengine. Jifunze kubainisha mambo ya muhimu zaidi ili uanze
kuyatengea pesa kwanza. Kwa mfano maswala kama vile eilimu, uwekezaji,
kodi ya nyumba, chakula, ni baadhi tu ya mambo muhimu kuliko gari, pombe,
simu pamoja na mambo mengine ya anasa. Ukijifunza kuwa na mtazamo wa
kutambua vipaumbele utaweza kutenga na kutumia pesa kwenye mambo ya
muhimu kwanza.

4. Tumia kidogo kuliko unachopata


Ni rahisi kutumia kuliko kutafuta; hivyo si jambo la kustaajabisha ukajikuta
unapata elfu tano kwa siku lakini unatumia elfu saba. Maana yake hapa
unatengeneza deni mahali la shilingi elfu mbili kila siku. Inawezekana unakula
akiba au faida katika kile unachokifanya. Jifunze kutumia kidogo kuliko kile
unachokipata ili uweze kutunza pesa kwa ajili ya wakati wa uhitaji.

5. Tumia vitu (huduma) vyema


Kuna huduma kadha wa kadha tunazozihitaji kila siku katika maisha yetu
kama vile maji, umeme, gesi, simu n.k. Mara nyingi watu hushindwa kutumia
huduma au vitu hivi vyema na kujikuta wakijiongezea gharama za maisha
zisizokuwa na sababu ya msingi. Mambo unayoweza kuzingatia katika swala
hili:

 Epuka tabia kama vile kuacha taa zikiwa zimewashwa hata wakati wa
mchana bila sababu. Punguza matumizi ya pasi, redio na hata televisheni. Pia
unaweza kununua taa zinazookoa umeme yaani energy servers.
Unaweza ukaokoa maji kwa kutumia maji ya mvua au toka chanzo kingine
badala ya kutumia maji ya bomba kwa kila kitu.

 Punguza matumizi ya gesi kwa kuzima jiko pale lisipokuwa na uhitaji. Hakuna
haja ya kupasha maji moto kila wakati huku unaweza kuogea maji ya baridi au
uvuguvugu.
 Epuka kupiga simu zisizokuwa na ulazima kwani kwa kufanya hivi unapoteza
pesa bila sababu. Jiunge kwenye vifurushi (bundles) vya muda mrefu kuliko
vya siku moja ili uweze kupata muda wa kutosha kutumia vyema muda wako
wa maongezi.

6. Tafuta punguzo
Mara nyingi vitu huuzwa kwa punguzo, hivyo ni vyema ukanunua vitu kwa
punguzo kuliko kununua kitu katika bei halisi ili kupuguza gharama. Naamini
unafahamu kuwa yapo maduka yanayouza aina fulani ya shati kwa shilingi
laki tatu, lakini shati hilo hilo linauzwa kwa shilingi elfu kumi na tano duka
jingine. Sasa kwanini usinunue kwenye hili duka la pili linalouza shati kwa
shilingi elfu kumi na tano? Epuka sifa na ufahari usiokuwa na sababu, tafuta
na nunua vitu kwa punguzo ili kuokoa pesa ambazo zingepotea bila sababu.

7. Linda afya yako


Kutokana na watu kutojali wala kufahamu umuhimu wa kuwa na afya njema,
wengi wamekuwa wakitumia gharama zisizokuwa na sababu kwenye
matibabu. Kuna hatua kadhaa unazoweza kuzitumia kujilinda na maradhi
yasiyokuwa na sababu kama vile kula chakula bora pamoja na kuzingatia
kanuni za afya kama vile usafi. Chukua hatua mapema ili usipoteze pesa zako
hosipitalini kila siku kutibu maradhi ya tumbo au malaria ambayo ungeweza
kuyazuia.

8. Acha tabia badhirifu


Kuna tabia kadha wa kadha ambazo watu wengi hawazijui kama ni moja kati
ya tabia badhirifu. Tabia kama vile Kuvuta sigara, pombe, unywaji wa soda,
ulaji wa pipi, kulipia michezo ya kompyuta, kukodisha filamu, kamari n.k ni
baadhi tu ya tabia badhirifu. Unaweza kuepuka tabia hizi na kuokoa kiasi
kikubwa cha pesa ambacho kinapotea bila sababu.
9. Rekodi matumizi yako
Kwenye suala la kutunza kumbukumbu binafsi hasa za kipesa ni suala gumu
kwa watu wengi. Lakini ni vyema ukajifuna kutunza kumbukumbu za matumizi
yako ili hatimaye uweze kufahamu jinsi ulivyotumia kipato chako. Kwa
kufanya hivi utaweza kubaini ni wapi ambapo hukutumia pesa zako vyema na
utaweza kujirekebisha wakati mwingine.

10. Weka akiba


Mara ngingi watu hujitetea kuwa hawawezi kuweka akiba kwa kuwa hawana
kipato kikubwa. Ukweli ni kuwa kuweka akiba siyo kuwa na kipato kikubwa
bali ni maamuzi pekee. Fahamu kuwa kuna wakati chanzo chako cha kipato
cha sasa kinaweza kukauka; hivyo kuwa na akiba kutakuwezesha kukidhi
mahitaji yako kwa wakati ambao huna kipato cha uhakika au cha kutosha.
Unaweza kufanya mambo yafuatayo:

 Andaa bahasha nne (1. Kuwekeza, 2. Matumizi ya lazima, 3. Akiba 4. (Jambo


lingine muhimu linalohitaji pesa)
 Gawa kila unachokipata na kukiweka kwenye bahasha hizo nne. Kumbuka
bahasha zote zinatakiwa kupata mgao; bahasha ya nne inaweza kuwa
chochote kulingana na matumizi yako, Mf. Ada za Shule, Malipo ya Bima, n.k.
 Tumia pesa kulingana na bahasha. Bahasha ya akiba ni kwa ajili ya baadaye.
Pia bahasha ya kuwekeza ni kwa ajili ya miradi na uwekezaji utakaofanya
baadaye.

Naamini kwa kufanya hivi utaweza kupangilia pesa zako vyema na hatimaye
kujiwekea akiba.

Neno la mwisho: Pesa siyo kila kitu katika hii dunia, lakini ina nafasi kubwa
sana. Hivyo ukitaka kuwa na utawala mzuri katika maisha yako ni vyema
ukaimarisha misingi ya matumizi yako ya pesa. Epuka tabia za kitoto au za
watu wasiokuwa na busara, ambao hula au kutumia kila wanachokipata.
Naamini njia hizi 10 zilizoelezwa hapa zitakupa mwanzo mzuri wa matumizi
ya pesa.
SOMO: 10

Njia 8 za Kuokoa Mafuta Unapoendesha Gari


Ni wazi kuwa gari linahitaji mafuta ili kusafiri toka sehemu moja hadi nyingine.
Lakini swali ni je, unaweza kutawala kiwango cha mafuta kinachotumika?
Ndiyo, unawea kutawana kiwango cha mafuta na kupunguza garama za
matumizi ya mafuta zisizokuwa na ulazima.

Kama unapenda kuokoa kiasi cha mafuta yanayopotea bila sababu ya msingi
katika gari lako, basi tumia njia hizi 8 zifuatazo.

1. Kabili upepo
Unapoendesha gari upepo hukinzana na gari; hivyo kadri gari linavyokinzana
zaidi na upepo ndiyo pia unavyotumia mafuta mengi zaidi. Hivyo basi,
usipende kuweka mizigo juu ya gari kwa nje (carrier) au kufungua vioo kwani
kutasabisha ukinzani zaidi kati ya gari na upepo.

Kwa kukabili upepo vyema utapunguza ukinzani na kuokoa mafuta ambayo


yangetumika kukabili ukinzani huo wa upepo.

2. Punguza mwendo
Hakuna haja ya kukimbia wakati huna jambo la haraka unaloliwahi; pia
hakuna haja ya kukimbia ili uwe mbele ya gari linalofuata.

Kufanya hivi kutakupotezea kiasi kikubwa cha mafuta bila sababu yoyote ya
msingi. Endesha mwendo wa wastani kama hakuna ulazima wa kuchochea
mwendo na kupoteza mafuta mengi bila sababu.

3. Zingatia Matengenezo
Gari linahitaji matengenezo ya mara kwa mara. Kutofanyia mifumo kama vile
injini na magurudumu matengenezo kwa wakati kutakufanya kupoteza kiasi
kikubwa cha mafuta.
Unahitajika kuhakikisha mafuta lainishi (oil) yapo katika hali nzuri na katika
kiwango cha kutosha katika injini yako. Pia unatakiwa kukagua ujazo wa
magurudumu ya gari lako; kwani kadri gurudumu linavyokuwa na ujazo
mdogo, ndivo linavyohitaji mafuta mengi zaidi kulizungusha.

4. Punguza uzito
Kadri gari linavyokuwa na uzito mwingi ndivyo linavyohitaji mafuta zaidi
kuliendesha. Ikiwa hakuna haja ya kuongeza uzito usio na sababu kwenye
gari basi upunguze.

Hakuna haja ya kubeba mizigo na vifaa usivyovitumia mara kwa mara kila
ufanyapo safari. Jitahidi kupunguza mizigo isiyo ya lazima katika gari lako ili
kuokoa matumizi yasiyo ya lazima ya mafuta.

5. Zingatia matuta
Matuta huwekwa katika barabara ili kutawala mwendo. Hivyo kufunga breki
ghafla mara ukutapo tuta na kuchochea mwendo ghafla baada ya tuta
kutakufanya utumie kiasi kikubwa zaidi cha mafuta.

Unaweza kupunguza mwendo taratibu na kuuongeza taratibu mara ufikapo


kwenye matuta ili kuokoa kiasi cha mafuta kinachopotea.

6. Zima kiyoyozi
Ufanyaji kazi wa kiyoyozi (AC) katika magari mengi hutegemea nishati
inayozalishwa na kifaa kiitwacho Alternator ambacho huzalisha umeme kwa
msaada wa injini ya gari.

Hivyo basi, kuwasha kiyoyozi kutahitaji mafuta zaidi ili kuendesha kifaa hiki
kiitwacho Alternator. Inashauriwa kuwasha kwa muda au kuzima kiyoyozi pale
ambapo hakina ulazima ili kuokoa matumizi ya mafuta yasiyo ya lazima.
7. Tumia kiongeza mwendo vyema
Matumizi mazuri ya kiongeza mwendo (Accelerator), kutakuokolea kiasi
kikubwa cha mafuta mara uendeshapo gari. Mambo ya kuzingatia katika
swala hili:

 Ongeza mwendo (Accelerate) taratibu. Kuongeza mwendo au kukanyaga


mafuta kwa kasi kutasabisha utumizi mkubwa zaidi wa mafuta.
 Usikanyage kiongeza mwendo (Accelerator) hadi mwisho. Unapokanyaga
kiongeza mwendo hadi mwisho unasababisha matumizi makubwa sana ya
mafuta. Hivyo kupelekea upotevu wa mafuta usiokuwa na ulazima.

8. Punguza matumizi ya gari


Njia bora zaidi na yenye matokeo makubwa katika swala la kuokoa mafuta
katika gari ni kupunguza matumizi ya gari. Kakuna haja ya kwenda kila mahali
kwa kutumia gari.

Unaweza kutembea kama sehemu ya mazoezi au hata ukatumia usafiri


mwingine kama baisiketi au hata daladala.

Hitimisho

Zilizojadiliwa hapa ni njia anuwai zitakazokuwezesha kuokoa mafuta


unapoendesha gari. Ni dhahiri kuwa kupunguza matumizi ya mafuta ni jambo
linalowezekana ikiwa utafanyia kazi hoja jadiliwa hapo juu, ikiwemo
matengenezo ya gari kwa wakati pamoja na uendeshaji sahihi.

SOMO: 11
Mambo Matano Muhimu ya Kuzingatia Kabla ya
Kuomba Mkopo

Kutokana na kipato cha watu wengi kutokutosheleza mahitaji yao, hujikuta


wakilazimika kukopa. Wapo waliofanikiwa sana kwenye mipango yao
kutokana na mikopo, lakini wapo pia waliofilisika kutokana na mikopo.
Kwa hakika swala la mikopo linahitaji umakini mkubwa pamoja na mipango na
mikakati stahiki ili lisije likakuingiza kwenye madeni yasiyokwisha.

Ikiwa una mpango wa kukopa, basi fahamu mambo matano muhimu ya


kuzingatia kabla ya kuomba mkopo.

1. Bainisha uwezo wako wa kifedha


Ili upate na utumie mkopo vyema, ni muhimu ufahamu uwezo wako wa
kifedha. Ikiwa uwezo wako wa kifedha ni shilingi milioni moja, ukikopa mkopo
wa bilioni 1 hutoweza kuupata wala kuurejesha.

Hakikisha unatathimini kipato chako pamoja na uwezo wako wa kutumia pesa


ili usije ukatumbukia kwenye madeni.

2. Andaa mpango wa matumizi na marejesho


Watu wengi hushindwa kupata mkopo au kurejesha mkopo kutokana na
kutokuwa na mpango mzuri wa matumizi na urejeshaji wa mkopo.

Hakikisha kabla ya kukopa unaandaa mpango mzuri na unaotekelezeka na


namna utakavyotumia pamoja na kurejesha mkopo wako. Usikope ndipo
upange, bali panga ndipo ukope.

3. Fahamu kuhusu riba


Benki ni taasisi zinazofanya biashara ili zipate faida; benki hufanya biashara
hasa kwa kupitia mikopo. Ni muhimu kufahamu vyema kiwango cha riba
utakachotozwa kutokana na mkopo uliokopa.

Watu wengi wameingia kwenye matatizo makubwa baada ya kujikuta


wakikopa mikopo yenye riba kubwa sana. Hakikisha unafahamu riba
utakayotozwa na utathimini kama utaweza kuimudu.

4. Fahamu muda wa mkopo


Kadri mkopo unavyokuwa wa muda mrefu ndivyo na kiwango chake cha
kulipa kwa mwezi huwa kidogo. Hivyo ni muhimu sana kuchunguza muda wa
kurejesha mkopo ili uone kama unaweza kumudu kurejesha mkopo huo ndani
ya muda husika.

5. Fahamu gharama nyingine za mkopo


Mara nyingi mikopo huambatana na gharama nyingine kama vile gharama ya
kuchakata mkopo, gharama ya kurejesha mapema zaidi, gharama ya
kujiondoa mapema, n.k.

Ni vyema ukafahamu gharama hizi ili uone kama utazimudu vyema. Hakikisha
waraka wa mkopo unaopewa unausoma na kuuelewa vyema kabla ya
kuidhinishiwa kupokea mkopo ili kuepusha matatizo yoyote mbeleni.

Neno la mwisho

Kwa hakika mikopo imewasaidia wengi lakini pia imewafilisi wengi kutokana
na kutokufahamu mambo ya muhimu ambayo wangepaswa kuyazingatia
kabla ya kuomba mkopo.

Hakikisha hukopi pesa kwa ajili ya matumizi ya anasa au yasiyokuwa ya


msingi kwani utatumbukia kwenye madeni makubwa yasiyolipika.

SOMO: 12
Mambo ya Kuzingatia Ili Kuchagua Kichwa Kizuri cha
Kitabu

Swala la uandishi wa vitabu ni swala linalohitaji kuzingatia hatua kadhaa


muhimu. Moja kati ya hatua hizi ni uchaguzi wa wazo au kichwa cha kitabu.

Haijalishi ni kitabu cha kifasihi au kisicho cha kifasihi, utahitajika kuchagua


kichwa kizuri au bora cha kitabu chako.

Ikiwa wewe ni mwandishi au unajiandaa kuwa mwandishi wa vitabu, basi


fahamu mambo ya kuzingatia ili kuchagua kichwa kizuri cha kitabu.
1. Fanya utafiti
Utafiti ni msingi mkuu wa kupata kichwa kizuri cha kitabu. Ni muhimu kufanya
utafiti katika vitabu au makala nyingine mbalimbali zinazohusiana na kile
unachotaka kukiandikia. Unaweza kuzingatia haya wakati wa utafiti:

 Fanya utafiti kwenye vitabu vilivyochapishwa pamoja na vile vilivyoko kwenye


mtandao wa intaneti ili kubaini kama kichwa unachokitaka kimeshatumiwa na
mtu mwingine. Hili litakuepushia mgogoro wa hati miliki au kuwachanganya
wasomaji.
 Baini aina ya vichwa vya vitabu vinavyopendwa na wasomaji unaowalenga.
 Fahamu vichwa vya vitabu vya waandishi wengine vinavyopendwa au kuuzwa
zaidi.
 Kama unaukurasa wa mtandao wa kijamii au blog, basi tafuta maoni ya
wasomaji wako juu ya kichwa cha kitabu wanachokipenda au kukihitaji.

Ukizingatia haya utaweza kupata msingi mzuri wa kuchagua kichwa kizuri cha
kitabu.

2. Fahamu wasomaji wako


Ili uweze kuandika kitabu ambacho kitakuwa bora na kukubalika kwa
wasomaji wako, ni lazima uandike kitu kinachowalenga vyema.

Huwezi kuandika kitu kinachowalenga wasomaji wako ikiwa huwafahamu


vyema. Kwa mfano kama wasomaji wako ni vijana basi chagua kichwa
ambacho kitapendwa na vijana, vivyo hivyo kama unaandikia wazee au
watoto hakikisha unawalenga vyema.

3. Chagua kichwa kinachovutia


Usichague kichwa cha kitabu ambacho ni alimradi kichwa, bali chagua kichwa
ambacho kila atakayekiona atatamani kununua au kusoma kitabu hicho.

Tumia ubunifu wako kama mwandishi ili uteke fikra na hisia za msomaji
kupitia kichwa cha kitabu chako.

Kwa mfano unaweza kuandika kitabu cha kuwafundisha watu jinsi ya kuwa
matajiri na ukatumia vichwa hivi:
i. Jifunze jinsi ya kuwa tajiri

ii. Jinsi ya kuwa tajiri ndani ya mwezi mmoja

Ni ukweli usiopingika kuwa kichwa cha pili kinavutia zaiidi na kitanunulika


zaidi.

4. Usichague kichwa kipana sana


Jambo lingine unalotakiwa kulizingatia ili upate kichwa kizuri cha kitabu ni
kuepuka kuchagua au kutumia kichwa kipana sana. Hakikisha kichwa
unachokichagua ni kifupi na kinaeleweka vyema.

5. Chagua kichwa kinachosadifu maudhui


Naamini umewahi kuona vichwa vya vitabu vya kifasihi ambavyo nje
vinaeleza kitu kingine na ndani vinaeleza kitu kingine — jina la kitabu
halisadifu yaliyomo ndani.

Pamoja na sababu kuwa hii ni mbinu mojawapo ya waandishi wa kifasihi hasa


ya kuepuka migogoro kati yao na watawala au wahusika walioguswa kwenye
kitabu; jambo hili linapaswa kuepukwa.

Hakikisha kichwa cha kitabu chako kinasadifu yaliyomo ndani ya kitabu chako
ili ufikishe ujumbe vyema kwa hadhira lengwa.

Hitimisho

Ni vyema kukumbuka kuwa unapokosea kwenye kuchagua kichwa cha kitabu,


utakuwa umeshashindwa pia kwa kiasi kikubwa kwenye kitabu chako.

Hakikisha unapata muda wa kutosha wa kufanya utafiti wa kina kabla


hujaamua kuchagua kichwa fulani kitumike kwenye kitabu chako.
SOMO: 13

Maswali 10 Muhimu ya Kujiuliza Kabla ya Kuacha Kazi

Wakati wengine wakitafuta kazi usiku na mchana, wengine wanatamani


kuacha kazi mara moja. Kutokana na sababu mbalimbali, swala la kuacha
kazi linawakabili watu wengi.

Mazingira mabaya ya kazi, matatizo ya kifamilia au kiafya yamekuwa chanzo


kikubwa cha watu kutamani au kutaka kuacha kazi.

Swala la kuacha kazi ni swala nyeti ambalo linahitaji utulivu na maamuzi


yenye kuhusisha utafiti na busara kubwa. Wengi huacha kazi kutokana na
misukosuko midogo na kujikuta wakiingia kwenye matatizo makubwa zaidi.

Ikiwa unataka kuacha kazi unayoifanya ili utafute nyingine au ujiajiri


mwenyewe, basi jiulize maswali haya 10 kabla ya kumpungia mwajiri wako
mkono.

1. Je unaacha kwa sababu sahihi?


Inawezekana umekaripiwa na mwajiri wako kutokana na kosa ulilolifanya,
swala hili limekukasirisha kiasi cha kutaka kuacha kazi. Je kweli madhara ya
kuacha kazi ni madogo kuliko yale ya kukaripiwa?

Hakikisha unatafakari kwa kina sababu inayokufanya uache kazi. Usiache


kazi kwa mambo madogo ambayo ungeweza kuvumilia yakapita.

2. Je ni wakati sahihi?
Kufanya jambo lolote nje ya wakati ni kosa kubwa. Hakikisha uamuzi
unaoufanya wa kuacha kazi ni kwa wakati sahihi.

Wakati sahihi hutegemea maandalizi ya maisha baada ya kuacha kazi; ikiwa


bado hujajiandaa au kuna mambo yatakayoharibika kutokana na wewe
kuacha kazi, basi subiri kwanza.
3. Chanzo kingine cha kipato ni kipi?
Inawezekana kazi unayotaka kuiacha ndiyo chanzo chako cha kipato. Je
utapata wapi fedha kwa ajili ya matumizi yako wakati utakapokuwa umeacha
kazi?

Nimeshuhudia watu wakiomba kurudi kwenye kazi zao za zamani kutokana


na kutokujiandaa katika eneo la kipato. Hivyo hakikisha una chanzo kingine
cha uhakika cha kipato kabla ya kuacha kazi.

4. Je uko kwenye tasnia gani?


Inawezekana unalenga kutafuta kazi sehemu nyingine baada ya kuacha kazi;
je tasnia au uwanja unaoufanyia kazi ukoje? Je kuna watu wengi sana? Je
uwezo wako katika tasnia ukoje?

Kuacha kazi bila kufikiri juu ya maswala haya kunaweza kukufanya usipate
kazi tena. Inawezekana wapo watu tele wanaotafuta kazi kama yako, hivyo
kuiacha ni kuipoteza daima.

5. Je utapata kazi nyingine au utafanya nini?


Usiache kazi kabla ya kufahamu kama utapata kazi nyingine au utafanya nini.
Hakikisha unafahamu kazi utakayoifanya au kama utajiajiri mwenyewe uwe
tayari umeshaweka mikakati sahihi.

Kuacha kazi bila kujiuliza swali hili kutakuweka kwenye hali ngumu.

6. Je utapata stahiki au haki zako?


Kuna stahiki ambazo mtu anazipata mara amalizapo utumishi wake kwa
mujibu wa sheria. Je ikiwa utaacha kazi utapata stahiki zako kama vile mafao
ya uzeeni?

Hakikisha huachi kazi katika mazingira yatakayokusababisha upoteze


mishahara au mafao yako ambayo ungepaswa kulipwa.
7. Je familia inakubaliana na msimamo wako?
Ikiwa una familia ni muhimu ukawashirikisha juu ya uamuzi wako wa kuacha
kazi ili nao watoe msimamo wao.

Kuacha kazi bila kushirikisha familia kunaweza kukuweka katika mgogoro au


sitofahamu kubwa kati yako na familia yako. Je familia ilikuwa inategemea
kazi yako? Je kipato cha familia kitakuwaje? Je watakuwezesha vipi
utakapokuwa huna kazi?

8. Je walioamua mamuzi kama yako wakoje?


“Ningejua huja mwishoni.”
Wengi huacha kazi wakidhani mambo yatakuwa rahisi, baada ya kuacha kazi
hujikuta wakiwa kwenye hali ngumu.

Chukua muda uwatumie watu wengine walioacha kazi kama shule yako ya
kujifunza. Je maisha yao yakoje? Yamekuwa mazuri au mabaya? Tafakari
vyema kabla ya kuchukua hatua.

9. Je una akiba ya kutosha?


Akiba ni muhimu kwa ajili ya kukusaidia wakati ambao huna kipato kwa ajili ya
kutunza mahitaji yako. Hakikisha umebainisha matumizi yako ya fedha na
kuhakikisha unaweza kuyakidhi kwa akiba uliyo nayo.

Usiache kazi bila kuwa na kiasi cha uhakika cha akiba itakayokusaidia wewe
na wale wanaokutegemea.

10. Je unaweza kuruhusiwa kurudi kazini?


Kuna wakati mtu anajutia uamuzi wake. Hakikisha kabla ya kuacha kazi
umefahamu kama unaweza kuruhusiwa kurudi kazini ikiwa mambo
yatakwenda vibaya.
Ni muhimu pia kuhakikisha kuwa huachi kazi kwa shari bali unaacha kwa
amani ili ukitaka kurudi ufikiriwe. Kumbuka! Unaweza pia kuomba likizo ndefu
isiyokuwa na malipo (secondment) badala ya kuacha kazi kabisa.

Neno la mwisho

Swala la kuacha kazi ni swala ambalo likifanyika bila kutafakari na kujiandaa


vyema linaweza kuleta matatizo makubwa. Hivyo jiulize maswali tajwa hapo
juu kwa makini, na uhakikishe umeyajibu vyema kabla ya kuacha kazi.

Unaweza pia kuuliza watu wengine waliokutana na changamoto kama zako


wakupe njia ya kuzikabili badala ya kuacha kazi.

Je bado unataka kuacha kazi? Je una majibu ya maswali haya?

Yale tunayoyawaza na kuyatafakari kwenye fikra zetu yana nafasi kubwa


sana kwenye maisha yetu. Ikiwa tunataka kufanikiwa basi ni lazima tufikiri na
kutafakari juu ya kufanikiwa.

“Tunakuwa kile tunachofikiri”

Earl Nightingale
Vivyo hivyo ikiwa tunahitaji kuhamasika kufanya mambo mbalimbali maishani,
ni lazima tusome, tusikilize, tutazame na hata tutafakari vitu
vitakavyotuhamasisha.

Karibu nikufahamishe nukuu 50 (quotes) ambazo zitakuhamasisha katika


maswala mbalimbali unayoyafanya maishani mwako.

1. “Chochote ambacho akili ya binadamu inaweza kuumba


na kufikiri, inaweza kukikamilisha pia.”

Napoleon Hill

2. “Njia ya kuanza ni kuacha kuzungumza na kuanza


kutenda.”

Walt Disney
3. “Usiruhusu jana itawale sana leo.”

Will Rogers

4. “Kama unafanyia kazi kitu kinachokusisimua na


unachokijali kweli, hauhitaji kusukumwa. Maono yako
yatakusukuma.”

Steve Jobs

5. “Kufahamu haitoshi, ni lazima tuweke kwenye matendo,


Kutamani haitoshi, ni lazima tufanye.”

Johann Wolfgang

6. “Tunatengeneza hofu tunapokaa bila kufanya kitu.


Tunaishinda hofu kwa matendo.”

Dr. Henry Link

7. “Ikiwa unafikiri unaweza au huwezi, uko sahihi.”

Henry Ford

8. “Mtu mwenye kujiamini ndani yake, anapata kujiamini kwa


wengine.”

Hasidic Proverb

9. “Fanya kile unachoweza kwa vyote ulivyonavyo, popote


ulipo.”

Theodore Roosevelt

10. “Akili ni kila kitu. Unavyofikiri ndivyo unavyokuwa.”

Buddha
11. “Muda mzuri wa kupanda mti ni miaka 20 iliyopita.
Lakini muda mwingine mzuri wa pili ni sasa.”

Chinese Proverb

12. “Muda wako ni mdogo, usiupoteze kuishi maisha ya


mtu mwingine.”

Steven Jobs

13. “Kushinda siyo kila kitu, lakini kutaka kushinda ni kila


kitu.”

Vince Lombardi

14. “Huwezi kuvuka bahari kama huna ujasiri wa kuacha


kuona ufukwe.”

Christopher Columbus

15. “Kisasi kizuri ni mafanikio makubwa.”

Frank Sinatra

16. “Kuna njia moja tu ya kuepuka kukosolewa: usifanye


kitu, usiseme kitu na usiwe chochote.”

Aristotle

17. “Anzia ulipo. Tumia kile ulichonacho. Fanya kile


unachokiweza.”

Arthur Ashe

18. “Anguka mara saba simama mara ya nane.”

Japanese Proverb
19. “Mlango mmoja wa furaha ukifungwa, mwingine
unafunguliwa, lakini mara nyingi tunautazama sana ule
uliofungwa na kushindwa kuona ule uliofunguliwa kwa ajili
yetu.”

Helen Keller

20. “Kila kitu kina uzuri wake, lakini siyo kila mtu anaweza
kuuona.”

Confucius

21. “Changamoto zinafanya maisha yavutie na kuzishinda


ni kufanya maisha kuwa na maana.”

Joshua J. Marine

22. “Kama unataka kujiinua mwenyewe juu, mwinue


mwingine juu kwanza.”

Booker T. Washington

23. “Ili kufanikiwa, shauku yako ya mafanikio ni lazima iwe


kubwa kuliko hofu yako ya kushindwa.”

Bill Cosby

24. “Kila siku ninajitahidi kufanya vizuri zaidi kuliko nilivyo


fanya jana.”

Reginald Mengi

25. “Mtu ambaye hajawahi kufanya kosa hajawahi kujaribu


kitu chochote.”

Albert Einstein
26. “Mtu anayesema hawezi kufanya hatakiwi kumwingilia
mtu anayesema ninaweza kufanya.”

Chinese Proverb

27. “Haujachelewa kuwa ambaye ungeweza kuwa.”

George Eliot

28. “Unakuwa kile unachoamini.”

Oprah Winfrey

29. “Jenga ndoto zako wewe mwenyewe, la sivyo mtu


mwingine atakuajiri kujenga zake.”

Farrah Gray

30. “Ota ndoto kubwa na dhubutu kushindwa”

Norman Vaughan

31. “Badili kufikiri kwako na utakuwa umebadili ulimwengu.”

Norman Vincent Peale

32. “Andika kitu chenye manufaa kusomwa au fanya kitu


chenye manufaa kuandikwa.”

Benjamin Franklin

33. “Njia pekee ya kufanya kazi nzuri ni kupenda kile


unachokifanya.”

Steve Jobs

34. “Ikiwa unaweza kuliota, unaweza kulifanikisha.”

Zig Ziglar
35. “Ndoto zetu zote zinaweza kutokea ikiwa tuna ujasiri wa
kuzifuata.”

Wale Disney

36. “Usilie juu ya kile ambacho huna; tumia vizuri kile


ulichonacho.”

Reginald Mengi

37. “Mambo mazuri huja kwa watu wanaosubiri, lakini


mambo bora huja kwa wale wanaoondoka na kwenda
kuayachukua.”

Hajulikani

38. “Fursa hazitatokea, unatakiwa kuziunda.”

Chris Grosser

39. “Usijaribu kuwa mtu wa mafanikio, bali jaribu kuwa mtu


wa thamani.”

Albert Einstein

40. “Akili kubwa hujadili mawazo, akili ya wastani hujadili


matukio, akili ndogo huzungumzia watu.”

Eleanor Roosevelt

41. “Ikiwa hauthamini muda wako, hata wengine


hawatauthamini. Acha kupoteza muda na vipaji vyako
sasa – anza kuvifanyia kazi”

Kim Garst
42. “Mtu mwenye mafanikio ni yule anayeweza kujenga
msingi imara kwa kutumia matofali yaliyotupwa na
wengine.”

David Brinkley

43. “Usiinue sauti yako, boresha hoja yako.”

Hajulikani

44. “Ninaamini kwamba ujasiri pekee mtu yeyote


anaouhitaji ni ujasiri wa kufuata ndoto zako mwenyewe.”

Orarah Winfrey

45. “Fursa zina aibu, zinakusubiri uzikimbilie.”

Reginald Mengi

46. “Ubunifu unatofautisha kati ya kiongozi na mfuasi.”

Steve Jobs

47. “Hofu ni mojawapo ya adui mkubwa kwa mafanikio.”

Reginald Mengi

48. “Wengi wetu hatuishi ndoto zetu kwa sababu tunaishi


hofu zetu.”

Less Brown

49. “Hatua ya mwanzo ya mafanikio yoyote ni matamanio.”

Napoleon Hill

50. “Baadaye inamilikiwa na wale wote wanaoamini


kwenye uzuri wa ndoto zao.”
Eleanor Roosevelt
Naamini umehamasika na kufurahia nukuu hizi za hamasa. Ni wazi kuwa kila
kitu kinaanza kwenye fikra zetu – tunavyowaza ndivyo tunavyokuwa.

SOMO: 4

Mambo 7 ya Kufanya Kabla ya Kuanzisha Kampuni au


Biashara

Inawezekana una wazo zuri sana la biashara na unatamani kulitekeleza


haraka kadri iwezekananavyo. Pengine umeajiriwa katika taasisi au ofisi fulani
na unashauku kubwa ya kuacha kazi ili uweze kuanzisha kampuni au
biashara yako.

Kabla hujafanya maamuzi yoyote ni vyema ukae chini na utafakari mambo


kadhaa ambayo yatakuwa na manufaa makubwa kwako.

Katika makala hii nitakueleza mambo 7 muhimu ambayo utahitajika kuyafanya


kabla ya kuanza biashara yako.

1. Chagua wazo la biashara vyema


Katika eneo ambalo watu wengi hukosea wakati wanapoanzisha kampuni au
biashara ni uchaguzi wa wazo la kibiashara.
Unapochagua wazo baya au usilolimudu, ni wazi kuwa hutoweza kulitekeleza
na kupata faida. Hakikisha wazo unalolichagua unalimudu vyema pia
linatekelezeka.
Epuka kuchagua wazo pana sana au kuchagua wazo kwa sababu mwingine
analifanya. Kwa kuwa wewe unaanza ni vyema ukachagua wazo
unalolipenda, kulimudu vyema na linaloweza kukupa faida.
Soma pia: Mambo 5 ya Kuzingatia Kabla ya Kuchagua Wazo la Biashara.
2. Fanya utafiti
Kabla ya kuacha kazi yako au kile unachokifanya ili uanzishe kampuni yako,
ni vyema ukafanya utafiti wa kina juu ya biashara utakayofanya.

Mambo ya kufanyia utafiti ni:

 Elewa biashara yako na huduma utakayotoa


 Fahamu wateja wako
 Fahamu ushindani
 Wafahamu watu utakaofanya nao kazi
 Fahamu njia bora ya mauzo ya bidhaa au huduma yako

3. Andaa mpango wa biashara


Baada ya kufanya utafiti, sasa weka wazo au mpango wako katika karatasi.
Mpango huu utakuwezesha kukuongoza katika kufikia malengo yako.

Kimsingi mpango wako wa biashara utajumuisha mambo kama vile:

 Mwonekano wa jumla wa kampuni


 Muundo wa utawala
 Ufafanuzi/Maelezo ya kampuni
 Malengo, Maono na mikakati
 Maelezo juu ya soko na tasnia unayoingia kufanya biashara
 Uendeshaji
 Mpango wa matumizi ya fedha
 Pamoja na taarifa nyingine za msingi zinazohusiana

4. Bainisha chanzo cha fedha


Ni lazima kubaini chanzo cha fedha utakazozitumia kuanzisha biashara au
kampuni yako. Je fedha hizo zitatokana na mkopo, akiba yako au msaada?

Kumbuka uendeshaji wa kampuni unahitaji fedha kwa ajili ya shughuli


mbalimbali kama vile matumizi ya ofisi, usafiri, malipo ya huduma, mishahara
n.k. Ni vyema kulishughulikia hili mapema ili usije ukakwama katika biashara
yako.
5. Bainisha muundo wa kampuni au biashara
Unatakiwa kubainisha muundo wa biashara au kampuni yako kabla
hujaianzisha. Je kampuni au biashara yako itakuwa ni ya shirika, ubia au
binafsi?

Unapochagua muundo zingatia yafuatayo:

 Ugumu wa uendeshaji kwa kila mfumo.


 Gharama za uendeshaji.
 Kodi.
 Sheria na vibali.
 Manufaa ya muundo husika.
 Mtaji.

Unapozingatia haya hakika utaweza kuchagua muundo wa kampuni au


biashara wenye tija zaidi kwako.

6. Tafuta ofisi
Watu wengi wamekuwa wakianzisha kampuni kwa mazoea bila kuzingatia
kuwa ofisi ni muhimu kwa biashara au kampuni zao. Tafuta ofisi utakayo
mudu gharama zake, pia yenye kukidhi mahitaji ya kampuni au biashara yako.

Kama utaamua kufanyia kazi nyumbani, basi hakikisha unatenganisha


mambo binafsi na yale ya ofisini. Kumbuka kuepuka kuchagua ofisi ya
kifahari au ya gharama kubwa bila sababu ya msingi.

7. Bainisha changamoto
Changamoto zipo kila mahali; hivyo yakupasa kuzifikiria kabla ya kuanza
kampuni au biashara yako. Kama unajidanganya kuwa utafanya biashara bila
kukutana na changamoto yoyote unajidanganya.

Zitambue changamoto mapema ili uweze kuweka mikakati mapema ya


namna utakavyo pambana nazo.

Hitimisho:
Naamini makala hii imekupa mwongozo juu ya mambo unayotakiwa
kuyafanya kabla ya kuanzisha kampuni au biashara yako. Naamini ukiyafanya
haya utaweza kuanzisha kampuni au biashara itakayokuwa na mafanikio
makubwa.

SOMO: 15

Faida 10 za Kunywa Maziwa Usizozifahamu


Maziwa hufanya mambo mengi mazuri kwa ajili ya afya yako. Wataalamu
wa afya na wauzaji wa maziwa wamekuwa wakieleza faida kadha wa
kadha za kunywa maziwa. Je umewahi kujiuliza hasa ni faida gani hizo
zitokanazo na unywaji wa maziwa?
Ni wakati wako sasa wa kujiuliza kwa kina juu ya faida zitokanazo na unywaji
wa maziwa. Fuatana nami katika makala hii nikueleze faida 10 zitokanazo na
unywaji wa maziwa.

1. Hujenga na kulainisha ngozi


Je unamfahamu Cleopatra? Cleopatra alikuwa ni malikia wa Misri
anaesadikiwa kuwa mzuri sana. Inaaminikia uzuri wa Cleopatra ulitokana na
tabia yake ya kuogea maziwa mara kwa mara.

Hivyo basi, ni wazi kuwa, vitamini na virutubisho vilivyoko katika maziwa ni


muhimu kwa ajili ya ngozi bora. Ni vyema kunywa angalau bilauri moja ya
maziwa kila siku.

2. Huimarisha meno
Maziwa ni chanzo bora cha madini ya kalisiamu, hivyo basi maziwa ndicho
kitu halisi kinachohitajiwa na meno yetu. Pia maziwa huzuia kutoboka na
kuoza kwa meno. Kalisiamu hufyonzwa na miili yetu kukiwa na vitamini D;
hivyo jitahidi kunywa maziwa kwani maziwa huwa na vitamini D.
3. Huimarisha mifupa
Ni ukweli usiopingika kuwa watoto wanahitaji kunywa maziwa ili kuimarisha
ukuaji wao. Ni kweli pia watu wazima wanahitaji kunywa maziwa ili kulinda na
kuimarisha mifupa yao dhidi ya magonjwa kama vile udhaifu wa mifupa
(osteoporosis). Maradhi haya huzuiliwa kwa kalisiamu ipatikanayo kwenye
maziwa na ambayo hufyonzwa kutokana na uwepo wa vitamini D.

4. Kujenga misuli
Maziwa yana mchango mkubwa katika ukuaji wa misuli. Hili ni kutokana na
protini zinazopatikana katika maziwa. Wanariadha wengi hunywa maziwa
baada ya mazoezi, hii ni kwa ajili ya kuupa mwili virutubisho vya kutosha kwa
ajili ya kujijenga tena. Maziwa huzuia maumivu ya misuli pamoja na kurudisha
ute ulipotea kwenye misuli wakati wa kazi mbalimbali.

5. Kupunguza uzito
Utafiti unaonesha kuwa wanawake wanaokunywa maziwa hupunguza uzito
zaidi kuliko wale wasiokunywa. Inashuriwa kunywa maziwa wakati wa chakula
cha jioni au unapokula matunda. Pia maziwa yanaweza kutumiwa kama kileta
hamu ya kula yaani appetizer.

6. Huondoa msongo wa mawazo


Hebu fikiri juu ya vitamini na virutubisho vilivyoko kwenye maziwa; hivi
huweza kuondoa msongo. Baada ya kazi nyingi za siku, inashauriwa kunywa
angalau bilauri (glass) moja ya maziwa ya uvuguvugu. Hili litakusaidia
kukuondolea msongo katika misuli na neva zako za fahamu.

7. Huzuia maumivu wakati wa hedhi


Wanawake wengi wanakabiliwa na maumivu wakati wa hedhi. Maziwa
yamedhibitishwa kuzuia na kupunguza maumivu haya kwa kiasi kikubwa.
8. Huongeza nguvu za mwili
Je unaishiwa nguvu mapema au kuchoka sana? Kama jibu ni ndiyo, unahitaji
virutubisho vilivyoko kwenye maziwa. Hivi vitaupa mwili wako nguvu mpya na
kukufanya kuwa mwenye nguvu na furaha siku nzima.

9. Huondoa kiungulia
Kiungulia huwasumbua sana watu wengi. Kiungulia husababishwa na asidi
zipatikanazo tumboni. Hivyo maziwa (ambayo si mgando) hutengeneza
utando maalumu tumboni ambao hupambana na asidi hizi.

Kwa hiyo nywaji wa maziwa (ambayo si mgando) utakusaidia kupambana na


tatizo la kiungulia ndani ya muda mfupi.

10. Hupambana na maradhi mengine


Kwa miongo kadhaa tafiti zimebaini kuwa maziwa huzuia magongwa kadha
wa kadha. Magonjwa hayo ni kama vile shinikizo la damu na kiharusi.
Inaaminika pia maziwa hupunguza lehemu (cholesterol) mwilini na kuongeza
uwezo wa macho kuona. Baadhi ya watafiti wameeleza kuwa unywaji wa
maziwa huzuia ania fulani za saratani.

Hitimisho

Yaliyozungumziwa hapa ni faida 10 za kunywa maziwa. Naamini umebaini


kuwa maziwa yana manufaa mengi sana kwa ajili ya afya yako zaidi ya haya
yaliyotajwa. Ni jambo jema kujizoesha kula vitu vya asili, kwani ndivyo
huhitajiwa zaidi na mwili wa mwanadamu. Jizoeze kunywa angalau bilauri
moja ya maziwa kila siku kwa ajili ya afya ya mwili wako.

SOMO: 16

Makosa 8 ya Kuepuka Kabla na Wakati wa Kujenga Nyumba


Nyumba ni hitaji muhimu kwa watu wote. Kila mmoja anatamani na ana ndoto
za kununua au kujenga nyumba nzuri na ya kisasa. Ni kweli kuwa ujenzi wa
nyumba unahitaji rasilimali nyingi hasa fedha.

Pamoja na gharama hizi za ujenzi wa nyumba bado watu wengi wamekuwa


wakishindwa kupata nyumba nzuri huku wakiwa tayari wamepoteza kiasi
kikubwa cha pesa. Ni wazi kuwa yapo makosa mbalimbali yanayosababisha
hali hii yakiwemo yale ya ukosefu wa elimu pamoja na uzembe wa aina
mbalimbali.

Karibu ufuatilie makala hii ili uweze kufahamu makosa 8 unayoweza


kuyaepuka wakati wa kujenga nyumba ili hatimaye uwe na nyumba bora.

1. Kutozingatia kanuni za kununua kiwanja


Watu wengi hawafahamu mambo muhimu ya kuzingatia wakati wanaponunua
kiwanja. Hivyo hujikuta wakiingia katika matatizo mbalimbali kama vile
kuvunjiwa nyumba zao, kujenga kwenye maeneo mabaya kama matindiga na
mikondo ya maji. Ni muhimu kuhakikisha mambo yafuatayo kabla na wakati
wa kutafuta kiwanja cha kujenga nyumba:

 Kiwanja hakina umiliki zaidi ya mtu mmoja


 Kiwanja hakina mgogoro wa kisheria
 Kiwanja hakiko kwenye hifadhi ya barabara au mazingira
 Kiwanja kinafaa kwa ujenzi (Siyo tindiga, eneo la magadi, eneo la
maporomoko ya ardhi au mkondo wa maji)

Ukizingatia haya utaweza kupata kiwanja kizuri kwa ajili ya kujenga nyumba
bora kwa ajili ya matumizi yako.

2. Uchaguzi duni wa ramani


Mara nyingi mtu humwita fundi na kumwambia kuwa “nataka unijengee
nyumba ya vyumba vitatu”. Fundi anapouliza ramani yako iko wapi wao
husema we angalia tu nzuri alimradi iwe ya vyumba vitatu. Hili ni kosa kubwa
sana kwani husababisha watu wengi kujengewa nyumba ambazo
hawazipendi.
Ramani nzuri kwa fundi inaweza isiwe nzuri kwako na familia yako. Zingatia
uchaguzi wa ramani kwa makini kulingana na wewe unavyopenda, hili
litakufanya pia upende nyumba itakayojengwa.

Ramani mbaya.

3. Kutokufanya makadirio sahihi


Ni wazi kuwa umeona nyumba nyingi zikianzwa lakini hazimaliziki. Hili kwa
kiasi kikubwa linatokana na kufanya makadirio na maandalizi duni kabla ya
kuanza kujenga. Ujenzi wa nyumba unahitaji maandalizi mazuri hasa kifedha.
Ni muhimu kujiandaa vyema kabla ya kuanza ujenzi ili usikwamie njiani.

Mambo unayoweza kufanya:

 Weka makadirio ya gharama za ujenzi ili angalau uandae kiasi fulani cha
pesa.
 Nunua baadhi ya vifaa kabla. Unaweza kununua mchanga, mawe, kokoto,
nondo, mabati n.k. Ili kupunguza matumizi ya pesa wakati wa ujenzi.
 Weka mipango ya kutunza mahitaji yako mengine ya pesa kabla ya kuanza
ujenzi. Kwa mfano ada za shule, kodi mbalimbali, chakula n.k.
 Punguza matumizi yasiyokuwa ya lazima kabla na wakati wa ujenzi.
Ikumbukwe kuwa pesa nyingi zitahitajika kwenye ujenzi.

4. Kutokubainisha mahitaji
Mahitaji ya nyumba hutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine. Hivyo ni
vyema ukabainisha mahitaji yako kwa nyumba husika. Nimeshuhudia watu
wakijenga nyumba na kuzivunja ua kuzifanyia marekebisho kila mwaka
kutokana na kutobainisha mahitaji yao mapema.

Kurekebisha au kuvunja na kujenga upya nyumba yako kutakupotezea kiasi


kikubwa sana cha pesa. Kwa mfano wengi hurekebisha nyumba zao ili
kuongeza vitu kama vile jiko, choo na bafu, milango, madirisha n.k. ambavyo
wangepanga mapema wangekuwa wameviweka mwanzoni.

5. Kutokuwaza mbeleni
Ni vyema kuwaza mbeleni kwani nyumba ni kitu utakachokitumia muda mrefu.
Ni vyema ukafahamu vitu na mahitaji utakayoyataka kwenye nyumba yako
kwa siku za mbeleni. Hili litakuwezesha kujenga nyumba utakayoitumia na
kuifurahia kwa muda mrefu zaidi.

Ni vyema pia ukawaza kuweka miundombinu ya kisasa kama vile umeme,


simu (intercom), nyaya za televisheni, Kiyoyozi, na hata Data. Hata kama
huna pesa za kuweka mambo haya unaweza kubuni nyumba ambayo
baadaye itaruhusu miundombinu hii.
Nyumba ya Kisasa

6. Kutumia mafundi duni


Wengi hupenda kuokoa gharama kwa kutumia mafundi wenye uwezo mdogo
ili wawalipe kwa bei nafuu. Ni wazi kuwa rahisi inaumiza. Jiande vyema kabla
ya ujenzi ili uweze kuitendea haki nyumba yako kwa kutumia mafundi bora
wanaoimudu kazi yao vyema. Kutumia mafundi bora kutakufanya kupata pia
kazi yenye ubora.
Ngazi
zilizokosewa.

7. Kupuuza kanuni muhimu za ujenzi


Ujenzi una kanuni zake mbalimbali ambazo ni vyema zikazingatiwa. Kutokana
na uelewa mdogo, watu wengi hawazingatii kanuni muhimu za ujenzi kama
vile kumwagilia maji yakutosha pamoja na kujenga nyumba kulingana na
muda.

Nimeshuhudia nyumba nyingi zikivunjika kutokana na kujengwa haraka


haraka bila kutoa muda wa kutosha kwa nyumba kukomaa na kustahimili
uzito. Pia nimeona watu wakipuuzia umuhimu wa kunyesha sehemu
iliyojegwa kwa maji mengi; ni muhimu kunyesha vyema eneo lililojengwa
kwani “uimara wa saruji ni maji”; unaweza kunyesha angalau kwa siku saba
asubuhi na jioni.

Nyumba iliyoporomoka kutokana na kupuuza kanuni za ujenzi.


8. Matumizi ya vifaa duni
Kama nilivyoeleza katika maelezo yaliyotangulia, uhaba wa fedha huwafanya
watu wengi kufanya kazi duni. Hivi leo kuna vifaa mbalimbali vya ujenzi, lakini
si vyote ni bora. Kwa mfano, hakuna haja ya kununua kitasa kinachovunjika
baada ya mwezi au vigae vinavyofubaa. Kwa kufanya hivi utapoteza pesa
nyingi kwa kununua vifaa hivyo mara kwa mara. Jibane, jipange ufanye kitu
cha uhakika.

Hitimisho

Ni wazi kuwa ujenzi wa nyumba ni shunguli pevu inayohitaji kutulia, moyo na


maandalizi stahiki. Hakuna kitu kinachoshinda nia na mipango mizuri.
Naamini kwa kuyaepuka makosa tajwa hapo juu utaweza kujenga nyumba
bora, salama na ya kisasa kabisa.

You might also like