You are on page 1of 3

VITENGUZI VYA SWAUM (1)

NA BIN HAJJ IBRAHIMU

Ndugu msomaji leo katika Makala yetu hii tutazungumzia mambo yanaharibu
funga ya mtu, lakini ni vizuri tukafahamu kwanza maana ya kufunga kwa sababu
kutofahamu maana ya kufunga pia kunapelekea mtu kuharibu swaumu yake bila
kujua au kunapelekea pia mtu akadhania amefunga lakini kumbe ameshinda tun a
njaa kutwa nzima.
Tunapozungumzia swaumu au kufunga tunamaanisha kwamba swaumu ni Ibada
ambayo hutekelezwa kwa kuanzia kwa kutia nia ya kumuabudu Allah Ta’ala kwa
kujizuia na kula na kunywa nav yote vyenye kufunguza (kujizuia kwa) kuanzia
kuchipuza kwa Alfajiri ya kweli ambayo ni Alfajiri ya pili mpaka muda wa kuzama
jua (Magharibi). (Ash-sharhul Mumtih,Jz 6 uk298)
Ndugu msomaji kwa maana hiyo ya swaumu tulioielezea tambua ya kwamba kama
mfungaji atafunga swaumu ya Ramadhwani bila ya kutia nia ya kufunga basi mtu
huyo atakuwa hana swaumu bali ameshinda njaa tu hata kama amejizulia na kula
na kunywa na mengine yote yanayofunguza ambayo tutayataja. Vile vile kama
mfungaji hatazingatia muda wa kuanza kufunga yaani Alfajiri ya kweli au wengine
huitambua kwa alfajiri ya pili basi mtu huyo hana swaumu, na alfajiri ya kweli au
ya pili maana yake tunakusudia ni ni kubainika kwa weupe wa Alfajiri, na huo ni
weupe wa pili ambapo wakati wa Swalah ya Asubuhi huwa umeingia kama
alivyosema Allah “Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa
alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Swawm mpaka usiku…) (Quran
2:187)
Wengine hutambua alfajiri ya kweli au ya pili kwa kusubiria kusikia adhana ya pili
japo adhana si kipimo cha kukitegemea kwa asilimia mia moja kutokana na muda
wa adhana hiyo ya pili unatofautiana kutoka msikiti mmoja Kwenda mwengineo
au kutoka mji mmoja Kwenda mwengine japo wengi wao hufuata mafundisho na
maelekezo ya Mtume (Rahma na amani zimshukie juu yake) katika hadithi
alioipokea swahaba Ibn 'Umar (Radhi za Allah zimshukie) ambaye amesema:
"Mtume (Rahma na amani zimshukie) alikuwa na waadhini wawili; Bilaal na Ibn
Ummi Maktuum, kuna siku akasema,Hakika Bilaal anaadhini usiku adhana ya
kwanza, basi kuleni na kunyweni hadi atakapoadhini Ibn Ummi Maktuum”. (Imam
Bukhar na Muslim)
Ndipo hapo pakapatikana Alfajiri mbili ambapo ya kwanza ni ile Alfajiri ya adhana
ya kwanza ambapo wakati wa Mtume iliadhiniwa na bilaali na hiyo bado
hakujakucha na unaweza kula na kunywa au hata kufanya tendo la ndoa na mkeo
ama alfajiri ya pili au ya kweli ni ile inapoadhiniwa adhana ya pili ambapo wakati
wa zama za Mtume (rahma na amani zimshukie) ilikuwa ikiadhiniwa adhana yake
na Swahaba Ibn Ummi Maktuum, na hii adhana ndio inaashiria kumekucha nah
apo ni haramu kula na kunywa kwa yule aliyetia nia ya kufunga kutokana na
kuingia kwa ibada ya swaumu.
Mpendwa msomaji baada ya kufahamu maana ya swaumu sasa moja kwa moja
tuingie kwenye vitenguzi vya swaumu ambapo leo tutaanzia na kitenguzi cha kula
na kunywa.
Kula na kunywa ndani ya muda wa swaumu
Kula au kunywa kwa kukusudia ndani ya muda wa swaumu kunabatilisha swaumu
ya mtu, na Ushahidi wa hili ni neno la Allah Subhanahu wa Ta’ala, “Na kuleni na
kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku..”)
Quran 2:187 utaona kwa aya hii imeruhusu ni mubaha (ruhsa) kula na kunywa
mpaka pale itakapoingia alfajiri ya pili ambapo aya inakomelea ruhsa yake kwa
maana si ruhsa kula na kunywa baada ya kuingia alfajiri ya pili hivyo muislamu
aliyetia nia ya kufunga kisha akala kwa kukusudia au akanywa kwa kukusudia
kuanzia muda huo au muda wowote baada ya huo au baina ya alfajiri ya pili na
kabla ya kuingia magharibi basi mtu huyu hana swaumu. Kwa mfano mtu akatia
nia ya kufunga kisha muda wa saa kumi na mbili asubuhi akala au akanywa au
muda was aa kumi na mbili kamili au hata muda wa kubakia dakika moja kuingia
magharibi ikawa yeye ni mwenye kula au kunywa kwa makusudi basi mtu huyu
imebatilika swaumu yake.
Ufafanuzi wa namna ya kula na kunywa
Bila shaka ni maarufu kwamba Kula na kunywa maana yake ni kuingiza kitu
tumboni kwa njia ya kupitia chakula yaani kooni ambapo ndipo tumebainisha
kwamba kunabatilisha swaumu ya mtu ikiwa atafanya hivyo kwa kukusudia ndani
ya muda wa swaumu.Lakini mfano, je mtu akiingiza chakula au kinywaji kwa
kupitia tundu za pua? Bila shaka huyu nae swaumu yake imebatilika vile vile atie
maji kuosha pua yake kisha uoshaji wake ukapitiliza mipaka hatimae maji
yakaingia tumboni kupitia tundu la pua bila shaka amefungua lau kama maji yale
hayaathiri chochote basi Mtume (Rahma na amani) asingemuamuru swahaba kwa
kumwambia na uoshe pua yako kwa sana (kupitiliza) ispokuwa kama utakuwa una
swaumu (yaani usioshe tundu za pua ukapitiliza mpaka maji yakaingia tumboni)
(Sunan At-Tirmidhiy)
Ufafanuzi wa vitu vinavyobeba maana ya chakula
Kama tulivyotangulia kusema kwamba kula na kunywa kunabatilisha swaumu
lakini pia ifahamike kuna vitu si chakula lakini vinahesabika kuwa ni chakula
navyo pia vinaingia katika kundi la kufunguza, mfano, mtu akachomwa drip la
maji ya kumuongezea nguvu,drip la kumuongezea damu,au sindano kwa maana ya
kuchoma iwe mbadala ya chakula au kunywa hivi vyote hubatilisha swaumu
ispokuwa sindano mfano ya kutibu ugonjwa mfano, Malaria au sindano za kinga
hizi hazibatilishi japo ni vizuri zikatumika muda wa usiku.
Hukmu ya mwenye kubatilisha swaumu yake kwa kula au kunywa kusudi
Ama mwenye kula na kunywa kwa kukusudia huyu swaumu yake imebatilika na
hukmu yake huyu ni kuja kuilipa hiyo swaumu tu pasi na kulipa kafara lolote, na
hii ndio kauli ya ulamaa wengi katika madhehebu ya Imam Shaafiy na Hambali na
ndio kauli alioshikamana nayo Sheikh Swaaleh Al Othaymiin (Al Majimouh Al
Fataawa, Imam An Nawawiy, Jz 6 Uk 329)
Sababu za Mtu huyu kuhukumiwa ailipe swaumu ni (Qiyaas) yaani imechukuliwa
kutokana na kipimo cha mtu ambaye ni mgonjwa au msafiri yaani ikiwa mgonjwa
au msafiri japo wana dharura ya kufungua lakini bado wameamriwa kufungua na
kuja kuilipa funga hiyo siku nyengine hivyo hivyo basi kwa mtu ambaye
amefungua kwa kusudi kwa kula au kunywa ni aula kwake naye kulazimika
kuilipa siku hiyo alioifungua pasi na udhuru.
Vile vile mtu huyu aliyefungua kwa kusudi atawajibika kujizuia na kula na kunywa
siku nzima mpaka kuingia kwa magharibi na hii ni muongozo utokao kwa
wanachuoni wa madhehebu nne, Hanafiyyah,Maalikiyyah,Shaafiiyyah na
Hambaliyyah, kwa maana ya kwamba mfano, Mtu amefungua kwa kusudi muda
wa saa nne akanywa chai basi mtu huyu atawajibika baada yah apo kujizuia na
kula na kunywa mpaka muda wa magharibi japo kuwa swaumu yake
ilikwishabatilika tayari.
Ama yule ambaye amefunga kisha akala au kunywa lakini si kwa kukusudia labda
alijisahau akapitiwa basi huyu swaumu yake haibatiliki kutokana na Ushahidi wa
hadithi iliyopokelewa na swahaba Abii Hurayrah (Radhi za Allah zimshukie)
amesema, Mtume wa Allah (Rahma na amani zimshukie) amesema, “mwenye
kunga kisha akala au akanywa kwa kusahau basi aikamilishe swaumu yake kwani
Allah ndiye aliyemlisha na kumnywesha” (Imam Bukhar na Muslim).
Kwa Ushahidi huu unabeba aina yoyote ya chakula au kinywaji mtu akakila kwa
kusahau pasi na kukusudia au hata maji yakapita kupitia puani pasi na kukusudia
bila shaka swaumu ya mtu huyo haikubatilika
Tutaendelea kubainisha vitenguzi vyengine InshaaAllah

You might also like