You are on page 1of 3

UFALME WA MUNGU UPO WAPI?

Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.
Bwana Yesu aliwajibu Wayahudi kwamba,
“Baadhi ya Mafarisayo walimuuliza Yesu, “Ufalme wa Mungu utakuja lini?” Yesu akajibu,
“Kuja kwa ufalme wa Mungu si kitu unachoweza kuona. Watu hawatasema, ‘Tazama ufalme wa
Mungu uko hapa’ au ‘Ule pale!’ Hapana, Ufalme wa Mungu upo hapa pamoja nanyi.”.[ Luka
17:20-21 TKU].”
Kupitia jibu la Yesu kwa Mafarisayo ni kwamba ufalme wa Mungu upo kati yao lakini
Mafarisayo hawakuuona bali walizidi kuutizamia mbele, na katika mawazo yao walifikiri ufalme
huo ni kuifanya Israeli kuwa taifa kubwa duniani. Na walikuwa na mioyo migumu, na Yesu
aliongea nao kwa mifano lakini hawakuelewa. Yesu aliwambia wanafunzi wake kwamba,
“Akasema, Ninyi mmepewa kuzijua siri za ufalme wa Mungu; bali wengine kwa mifano, ili
wakiona wasione, na wakisikia wasielewe. [Luka 8:10].”
Hivyo Yesu alikuwa anajiongelea mwenyewe mbele ya Wayahudi kwa mifano kuwa ufalme wa
Mungu upo kati yao, ambao yeye ameuleta kati yao na kazi zake zinajionesha machoni pao. Na
Wayahudi walimshtumu kuwa anatumia nguvu za giza, akawajibu kwamba,
“Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.
[Mathayo 12:28].”
Hivyo nguvu za Roho Mtakatifu na kazi zake za uponyaji wa maradhi na kutoa mapepo
yaliyokuwa yanatesa wanadamu, zilijidhihirisha kwa Yesu, na nguvu hizo zilibainisha kuwa
ufalme wa Mungu umekuja na wenye nguvu ndio watauteka. [Mathayo 11:12]. Na hapo Yesu
hakumaanisha nguvu za mwili bali nguvu ya nia na Imani; Lakini Wayahudi walidumu
kutoamini na kumkataa Yesu, na Bwana Yesu akwaambia Neno gumu sana.
“Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa
lingine lenye kuzaa matunda yake. [Mathayo 21:43].”
Hilo taifa lingine, ni taifa la waaminio, wale ambao wana nguvu ya nia na Imani katika Kristo
Yesu Mwana wa Mungu. [1 Petro 2:9,10]. Ambao ni wazao halisi wa Ibrahimu kwa njia ya
Imani ambao ni Wakristo walio warithi sawasawa na ahadi. [Wagalatia 3:29]. Wayahudi wenye
mioyo migumu yenye kutoamini walikatwa katika ufalme na mahali pao ikachukuliwa na
wamataifa wenye kuamini, hivyo na wewe uliye katika ufalme usijivune pia usije katwa kama
wao. [Warumi 11:20].
Yesu aliwaagiza wanafunzi wake wautangaze ufalme wa Mungu, kuutangaza ufalme wa Mungu
ni kumtangaza Yesu kwa nguvu za Roho Mtakatifu na kupooza watu maradhi yao. [Luka 9:2].
Na Mitume waliutangaza ufalme wa Mungu kwa nguvu na kuponywa maradhi kiasi cha
Wayahudi na Serikali ya Herode ikatetemeka na Herode akatafuta kumwona Yesu. [aya 7-9]. Na
kutangaza ufalme wa Mungu ni kuhubiri Injili. [Luka 9:6]. Ambayo inawapa watu toba na
msamaha wa dhambi. [Marko 1:15; Mdo 5:31]. Yesu alisema,
“Akawaambia, Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia;
maana kwa sababu hiyo nalitumwa. [Luka 4:43].”
Mitume walimshuhudia pia kwamba.
“habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye
akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa
maana Mungu alikuwa pamoja naye. [Matendo ya Mitume 10:38].”
Habari njema ya Ufalme maana yake ni INJILI YA UFALME, na Biblia inasema, “Kwa maana
siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa
Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.” [Warumi 1:16]. Hivyo Injili inahusika na kila nafsi
kuanzia Myahudi na Mmataifa, hakuna injili mbili, ni ile ile habari njema ambayo ilitufanya
wawili kuwa umoja kwa kubomoa kiambaza cha kati kinachotutenga. [Waefeso 2:14].” Ni
uweza wa Mungu huletao wokovu na uponyaji, na tunaupata uwezo huo ndani yetu kwa njia ya
IMANI, maana pasipo Imani haiwezakani kumpendeza Mungu. [Waebrania 11:6].
Mitume baada ya Yesu kuondoka walihubiri sana ufalme huu, maandiko yafuatayo yanashuhudia
hilo.
“Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu
Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake. [Matendo ya Mitume 8:12].”
“Wakiisha kuagana naye siku, wakamjia katika nyumba aliyokaa, watu wengi sana, akawaeleza
kwa taratibu na KUUSHUHUDIA UFALME WA MUNGU, akiwaonya MAMBO YAKE
YESU, kwa maneno ya sheria ya Musa na ya manabii, tangu asubuhi hata jioni. AKIHUBIRI
HABARI ZA UFALME WA MUNGU, NA KUYAFUNDISHA MAMBO YA BWANA YESU
KRISTO, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu. [Matendo ya Mitume 28:23,31].
Hivyo kuhubiri Ufalme wa Mungu bila mambo yake Yesu ni kuhubiri Injili tupu isiyo okoa,
maana hakuna wokovu katika mwingine isipo kuwa Bwana Yesu. [Mdo 4:12]. Maana Yesu
ndiye asili yote ya ufalme wa Mungu. Kwahiyo ukihubiri fundisho lolote lisilo kwa jinsi ya
Kristo hiyo itakuwa ni Injili nyingine, na mwisho ni kujipatia laana. [Wagalatia 1:8,9].
Na Ufalme wa Mungu umegawanyika mara mbili ingawa ni mmoja, ambao ni.
1. Ufalme wa neema
2. Ufalme wa utukufu
Ufalme wa Neema.
Ni utawala wa Neema katika mioyo ya waumini kwa njia ya Imani, utawala huu upo duniani
ndani ya watu kwa njia ya Imani na ujazo wa Roho.[1 Yohana 3:24,4:13]. Na kiti cha enzi cha
Mungu, kiti cha neema kimeondolewa pazia la kutukinga, hivyo wote wanaweza kumwendea
Mungu moja kwa moja kwa ujasiri kwa damu ya Yesu mpatanishi ili wapate neema na rehema
kwa mahitaji. [Waebrania 4:16]. Ufalme huu unapaswa kutangazwa kwa nguvu zote, kwa sauti
kuu, maana ndio Injili ya Milele. [Ufunuo 14:6,7]. Na siri ya kuingia katika ufalme wa Neema ni
kumwamini Yesu na kuzaliwa mara ya pili kwa maji na Roho. Yesu anasema,
“Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi
kuuingia ufalme wa Mungu. [Yohana 3:5].
Na Ufalme huu watu wanapaswa kuufurahia kuanzia sasa, Mtume anasema, “Maana ufalme wa
Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu.[ Warumi
14:17].” Haki, Amani na furaha katika Roho Mtakatifu, hayo mambo si ya baadae, yaani ‘ya
wakati ujao’ ni mambo tunayopaswa kuwa nayo sasa. Haki tayari tunayo kwa njia ya Imani,
Amani tayari tumeshaachiwa, na furaha tunayo tayari kwa njia ya ujazo wa Roho Mtakatifu
ndani yetu. [Tazama, Warumi 3:24, Yohana 14:27; Mdo 9:31]. Kama hujisikii kuwa na vitu hivi
sasa, jipeleleze na fanya matengenezo.
Ufalme wa Utukufu
Huu utawala bado hujafunuliwa, na utakapofunuliwa kwa utukufu waaminio ndio watakao ng’aa
kwa utukufu na kubadilishwa kuwa kama Yesu, [1 Yohana 3:2], ila wale walio upuuza ufalme
wa Neema, watakuwa na kilio na kusaga meno na maangamizo. Biblia inasema,
“Malaika wa saba akapiga baragumu, pakawa na sauti kuu katika mbingu, zikisema, Ufalme wa
dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atamiliki hata milele na
milele. [Ufunuo 11:15].
Ufalme huu utaziondoa falme zote za dunia hii na kuziangamiza kabisa na kusimama waziwazi.
Biblia inasema hivi.
Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao
hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi
zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele. “Na ufalme, na mamlaka,
na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; ufalme
wake ni ufalme wa milele, na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii. [Dan 2:44; 7:27].
Je waovu watapata nafasi ya pili?
Biblia inasema hakuna kitu kama hicho, wasio mkubali Yesu wote wataangamizwa kwa
maangamizo ya milele.
“Kwa kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi;na kuwalipa ninyi
mteswao raha pamoja na sisi; wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni
pamoja na malaika wa uweza wake katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao
wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu; watakaoadhibiwa kwa
maangamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake;yeye atakapokuja
ili kutukuzwa katika watakatifu wake, na kustaajabiwa katika wote waliosadiki katika siku ile,
(kwa sababu ushuhuda wetu ulisadikiwa kwenu). [2 Wathesaloniki 1:7-10].”
Mungu akubarikie sana unapofanya maamuzi ya kumpokea huyu Yesu kuwa Bwana na
Mwokozi wa maisha yako, maana wakati huu karibu. Wito ni kuamini Injili. [Marko 1:15].

You might also like