You are on page 1of 2

DOMINIKA YA TANO

SOMO LA KWANZA Ayubu 7:1-4,6-7


"Hivi nazidi kusumbuka nahangaika hadi mapambazuko."
Somo katika kitabu cha Ayubu
Ayubu alisema: Je, mtu hana kazi ngumu duniani? Hatumiki kama mtu wa mshahara?
Kama mtumwa anayetamani kivuli kidogo; kama mfanyakazi anayetazamia mshahara
wake, ndivyo nami napata miezi ya usumbufu na kupewa siku za mateso. Nilalapo
kitandani najisemea: kutakucha wakati gani? Nikiamka naona kwamba jioni inakawia!
Hivi nazidi kusumbuka nahangaika hadi mapambazuko. Siku zangu hupita upesi kama
chombo cha mfumaji; hupita bila matumaini. Kumbuka ya kwamba uzima wangu ni
pumzi tu; macho yangu hayataona furaha tena.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA Zaburi 147:1-2, 3-4, 5-6 (K. tazama 3a)
K. Msifuni Bwana, yeye anawaponya waliovunjika moyo.
au: Aleluya.

Jinsi gani ni vema kumwimbia Mungu wetu sifa;


kwa maana kwapendeza, na yastahili kumsifu yeye.
Bwana anaijenga Yerusalemu,
anawakusanya Waisraeli waliotawanyika. K.

Yeye anawaponya waliovunjika moyo,


na kuvitibu vidonda vyao,
ameiweka idadi ya nyota,
anaziita zote kwa jina. K.

Bwana wetu ni mkuu na mwenye nguvu nyingi,


hekima yake haina kikomo.
Bwana huwategemeza wanyonge,
huwaangusha waovu mpaka chini. K.

SOMO LA PILI 1 Wakorintho 9:16-19, 22-23


"Ole wangu nisipoihubiri Injili."
Somo katika barua ya kwanza ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho
Ndugu zangu: Nikiihubiri Injili, sina sababu ya kujisifu. Wajibu huo nimetwikwa. Ole
wangu nisipoihubiri Injili. Maana nikifanya kazi hii kwa hiari, nitatuzwa. Lakini
nisipoichagua mwenyewe, nimekabidhiwa madaraka tu. Hapo tuzo yangu ni nini? Ni hili:
nihubiri Injili bila kudai kitu, wala kutumia haki yangu ninayopewa na Injili. Maana
hivyo nina uhuru kwa wote, naweza kujifanya mtumishi wa watu wote, nipate kuwavuta
wengi zaidi. Kwa watu dhaifu nalikuwa dhaifu, nipate kuwavuta wadhaifu. Nimekuwa
yote kwa wote, nipate kuwaokoa walau baadhi yao kwa namna yoyote. Hayo yote
nayafanya kwa ajili ya Injili, nipate kuwa mshiriki wake.
Neno la Bwana.

SHANGILIO LA INJILI Mathayo 8:17


K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Kristo mwenyewe amejitwika udhaifu wetu, amechukua magonjwa yetu.
W. Aleluya.

INJILI Marko 1:29.19


"Aliwaponya wengi walioshikwa na magonjwa mbalimbali."
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule: Yesu alipotoka kwenye sinagogi, alikwenda mara pamoja na Yakobo na
Yohane katika nyumba ya Simoni na Andrea. Hapo mkwewe Simoni alikuwa amelala
kitandani akishikwa na homa. Mara wakampasha habari ya hali yake. Akamkaribia,
akamshika mkono na kumwinua. Mara moja homa ikamwacha na akawatumikia.
Ilipofika jioni, baada ya kuzama jua, walimletea wagonjwa wote na waliopagawa na pepo
wabaya. Mji mzima walikusanyika mlangoni pake. Akawaponya wengi walioshikwa na
magonjwa mbalimbali. Akatoa pepo wabaya wengi, wala hakuwaruhusu kusema, kwa
kuwa walimjua. Asubuhi na mapema, kabla ya kupambazuka, aliamka, akaondoka, na
kwenda mahali pa nyika ili kusali. Simoni na wenziwe wakamtafuta na walipomwona,
wakasema, "Watu wote wanakutafuta." Akawaambia, "Twendeni mahali pengine katika
vijiji vya jirani, nipate kuhubiri huko pia. Hiyo ndiyo nia ya kuja kwangu." Basi
alitembea nchi yote ya Galilaya akihubiri katika masinagogi yao na kuwatoa pepo
wabaya.
Injili ya Bwana.

You might also like