You are on page 1of 11

29 MACHI 2024

IJUMAA
KATIKA MATESO YA BWANA

Adhimisho la Mateso ya Bwana

SOMO LA KWANZA Isaya 52:13—53:12

Somo katika kitabu cha Nabii Isaya.


Tazama, mtumishi wangu atafanikiwa, atatukuzwa, atainuliwa na
kusifiwa sana. Kama vile watu wengi walivyoogopa walipomwona,
kwa sababu uso wake ulikuwa umeharibiwa, kupita ule wa
mwanadamu, ndivyo hivyo mataifa mengi watashtuka; mbele yake
wafalme watasimama kimya; kwa kuwa wataona jambo
wasiloambiwa, na kutafakari kitu kisichosikika bado. Ni nani
aliyesadiki habari tuliyoisikia? Na mkono wa Bwana ulifunuliwa kwa
nani? Kama mche, alikua mbele yetu, kama mzizi katika nchi kavu;
hakuwa na umbo la kuvutia jicho, wala uzuri wa kutuvutia kwake.
Alichukiwa na kuepukwa na watu, mtu wa mateso, ajuaye huzuni,
sawa na wale ambao mbele yao twafunika nyuso zetu, alidharauliwa
na kufedheheshwa. Hakika, aliyachukua mateso yetu, na alijitwika
huzuni zetu. Sisi lakini, tulidhani ameadhibiwa na Mungu, na
kupigwa naye, na kuteswa. Ila aliumizwa kwa sababu ya makosa yetu
alipondwa kwa ajili ya maovu yetu. Aliibeba adhabu iletayo uzima
juu yetu, tumeponywa kwa vidonda vyake. Wote kama kondoo,
tulitangatanga, kila mmoja akienda njia yake; basi, Bwana ameweka
juu yake yeye maovu yetu sisi sote. Alionewa vikali sana,
akanyenyekea wala hakufunua kinywa chake; kama mwanakondoo
anayepelekwa machinjoni, na kama vile kondoo anyamazavyo mbele
yao wakatao manyoya yake, vivyo hivyo hakufumbua kinywa chake.
Alishikwa kwa nguvu na kuhukumiwa; ni nani atasimulia maisha
yake? Kweli, walimwondoa kutoka nchi ya walio hai, aliuawa kwa ajili
ya makosa ya watu wake. Walimpa kaburi pamoja na waovu, na
pamoja na matajiri katika kifo chake, ingawa hakutenda ukatili
wowote wala haukupatikana udanganyifu wowote kinywani mwake.
Bwana ametaka kumwumiza mtumishi wake kwa mateso
amemhuzunisha; amefanya maisha yake kuwa sadaka ya malipo ya
dhambi, naye ataona uzao wake, ataishi siku nyingi, nayo mapenzi ya
Bwana yatatimia kwa mikono yake. Kwa ajili ya mateso
aliyoyavumilia; yeye ataona mwangaza, atajaliwa mema; kwa
maarifa yake, mtumishi wangu mwema atatakasa watu wengi, yeye
atajitwika maovu yao. Ndiyo maana, nitamgawia sehemu kati ya
wakuu wa watu, atagawanya nyara pamoja nao walio hodari, sababu
alijitoa mwenyewe hata kufa akahesabiwa pamoja na wakosao,
akajitwika dhambi za wengi na kuwaombea wakosaji.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.

ZABURI YA KUITIKIZANA Zaburi 31


K. Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.
Nakukimbilia wewe, ee Bwana; nisiaibike milele.
Uniopoe kwa haki yako.
Mikononi mwako naiweka roho yangu;
uniokoe, ee Bwana, Mungu wa kweli. K.

2
Kwa adui zangu wote nimekuwa dharau,
kwa majirani wangu kitu cha kuogofya,
kitisho kwa rafiki zangu.
Wale wanionao njiani, wananikimbia.
Nimesahauliwa kama mtu aliyekufa;
nimekuwa kama chombo kilichovunjika. K.

Mimi lakini nakutumaini, ee Bwana;


nasema, “Wewe ndiwe Mungu wangu.”
Maisha yangu yamo mkononi mwako;
uniponye na mikono ya adui zangu
na wadhulumu wangu. K.

Umwangazie mtumishi wako uso wako;


uniokoe kwa wema wako.
Muwe hodari, mpige moyo konde,
enyi wote mnaomtumainia Bwana. K.

SOMO LA PILI Waebrania 4:14-16; 5:7-9

Somo katika barua kwa Waebrania.


Ndugu zangu: Kwa kuwa tuna kuhani mkuu aliyekwisha penya
mbingu, ndiye Yesu, Mwana wa Mungu, tuyashikilie maungamo
yetu. Maana hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuonea huruma
udhaifu wetu, kwani yeye alijaribiwa kama Sisi katika mambo yote,
ila hakutenda dhambi. Basi, tukikaribie kiti cha neema kwa
matumaini, ili tujaliwe huruma na neema na msaada wakati wa
shida. [Yesu] alipoishi duniani alimtolea sala na maombi kwa kilio na
machozi yeye aliyeweza kumwokoa katika mauti, akasikilizwa kwa

3
sababu ya uchaji wake. Ingawa ni mwana alijifunza utii kwa njia ya
mateso. Alipokamilika, alikuwa chimbuko la wokovu wa milele kwa
wote wanaomtii.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO LA INJILI
K. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
K. Kristo Yesu alijinyenyekeza mwenyewe, akawa mtii mpaka
mauti, yaani mauti ya msalabani. Kwa sababu hiyo Mungu
alimtukuza, akampa jina lipitalo kila jina.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.

INJILI Yohane 18:1—19:42

M — Msomaji
W — maneno ya Watu mbali mbali
 — maneno ya Yesu
M. Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo yalivyoandikwa na Yohane.
M. Wakati ule: Yesu aliondoka pamoja na wafuasi wake, kwenda
ng'ambo ya kijito Kidroni, pale palikuwa na bustani, akaingia
yeye na wafuasi wake. Kadhalika Yuda, yule aliyemsaliti, alijua
mahali pale, kwa maana mara nyingi Yesu alikusanyika huko
pamoja na wafuasi wake. Basi, Yuda alipokea kikosi cha askari na
walinzi waliotumwa na makuhani wakuu na Mafarisayo, akaenda

4
huko, walishika mienge, na taa, na silaha mikononi. Yesu akijua
yote yatakayompata, akatoka, akawaambia,
 “Mnamtafuta nani?”
M. Wao wakamjibu,
W. “Yesu Mnazareti.”
M. Yesu akawaambia,
 “MIMI NDIYE.”
M. Yuda aliyemsaliti alisimama pamoja nao. Alipowaambia, “MIMI
NDIYE,” walirudi nyuma, wakaanguka chini.
Akawauliza tena,
 “Mnamtafuta nani?”
M. Wakasema,
W. “Yesu Mnazareti.”
M. Yesu akajibu,
 “Nimekwisha kuwaambia ya kwamba MIMI NDIYE. Basi, ikiwa
mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.”
M. Hayo alisema, ili neno lake litimie, yaani: “Sikumpoteza hata
mmoja wa hao ulionipa.” Basi Simoni Petro alikuwa na upanga,
akauchomoa, akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata
sikio la kulia. Na yule mtumishi jina lake ni Malko. Yesu
akamwambia Petro,
 “Rudisha upanga alani mwake. Je, nisinywe kikombe alichonipa
Baba?”
M. Hapo kikosi cha askari na jemadari wake na walinzi wa Wayahudi
walimkamata Yesu, wakamfunga, na wakampeleka kwanza kwa
Anasi. Maana huyo alikuwa mkwewe Kayafa, naye alikuwa
kuhani mkuu wa mwaka ule. Kayafa huyo ndiye aliyewapa
Wayahudi shauri kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya taifa.
Petro na mfuasi mwingine wakamfuata Yesu. Huyo mfuasi
mwingine alijulikana na kuhani mkuu, akaingia pamoja na Yesu
katika ukumbi wa kuhani mkuu. Lakini Petro alisimama nje

5
karibu na mlango. Basi, yule mfuasi mwingine, aliyejulikana na
kuhani mkuu, akatoka akasema na mngoja mlango, akamleta
Petro ndani. Kijakazi huyo aliyekuwa mngoja mlango,
akamwambia Petro,
W. “Je, wewe si mmojawapo wa wafuasi wa mtu huyu?”
M. Naye akasema,
W. “Si mimi.”
M. Watumishi na walinzi walisimama huko na walikuwa
wamewasha moto wa makaa, maana kulikuwa baridi nao
wakaota moto. Na Petro pia alisimama nao akiota moto. Kuhani
mkuu akamhoji Yesu juu ya wafuasi wake na mafundisho yake
Yesu akamjibu,
 “Mimi nilisema wazi wazi mbele ya wote. Siku zote nilifundisha
katika sinagogi na hekaluni wanapokutana Wayahudi wote, kwa
siri sikusema neno. Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale
waliosikia niliyowafundisha. Bila shaka wanajua niliyosema.”
M. Aliposema hayo, mmoja wa mlinzi aliyesimama karibu alimpiga
Yesu kofi akisema,
W. “Wamjibu hivyo kuhani mkuu?”
M. Yesu akamjibu,
 “Kama nimesema vibaya, ushuhudie huo ubaya; bali kama
nimesema vema, mbona unanipiga?”
M. Hapo Anasi alimpeleka hali amefungwa kwa Kayafa, kuhani
mkuu. Simoni Petro alisimama huko akiota moto. Basi,
wakamwuliza,
W. “Je, wewe si mmoja wa wafuasi wake?”
M. Naye akakana, akasema,
W. “Si mimi.”
M. Mtumishi mmoja wa kuhani mkuu, ndiye jamaa wa yule
aliyekatwa sikio na Petro, akasema,
W. “Je, mimi sikukuona pamoja naye bustanini?”

6
M. Petro akakana tena. Mara hapo jogoo akawika.
Kutoka kwa Kayafa walimpeleka Yesu praitorio. Kulikuwa
nsubuhi mapema. Wenyewe hawakuingia praitorio, wasije
wakajinajisi, maana walitaka kuila Pasaka.
Basi, Pilato akawaendea nje, akasema,
W. “Mnaleta mashtaka gani juu ya mtu huyu?”
M. Wakajibu, wakamwambia,
W. “Kama huyu asingekuwa mtenda maovu tusingemleta kwako.”
M. Pilato akawaambia,
W. “Haya! Mchukueni ninyi, mkamhukumu kwa sheria yenu.”
M. Wayahudi wakamjibu,
W. “Sisi hatuna ruhusa ya kumwua mtu,”
M. Hivyo maneno aliyoyasema Yesu kuonyesha namna ya kifo chake
yalipata kutimia. Basi, Pilato akaingia tena katika praitorio,
akamwita Yesu, akamwuliza,
W. “Je, wewe u Mfalme wa Wayahudi?”
M. Yesu akajibu,
 “Unasema hivi kwa nafsi yako, au ni watu wengine waliokupa
habari yangu?”
M. Pilato akajibu,
W. “Ni Myahudi mimi? Ni taifa lako na makuhani wakuu waliokuleta
kwangu. Umefanya nini?”
M. Yesu akajibu,
 “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu
ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu
wangenipigania, nisije nikatolewa kwa Wayahudi. Lakini ufalme
wangu si wa hapa.”
M. Basi Pilato akamwambia,
W. “Wewe u mfalme, basi?”•
M. Yesu akajibu,

7
 “Wewe unasema ya kuwa, mimi ni mfalme. Nia ya kuzaliwa mimi
na nia ya kuja ulimwenguni mimi ndiyo nishuhudie ukweli. Kila
aliye wa ukweli husikia sauti yangu.”
M. Pilato akamwuliza,
W. “Ukweli ni nini?”
M. Baada ya maneno hayo, alikwenda tena nje kwa Wayahudi,
akawaambia,
W. “Mimi sioni kosa kwake. Lakini kuna desturi kwenu niwafungulie
mfungwa mmoja kwa Sikukuu ya Pasaka. Je, mwataka
niwafungulie mfalme wa Wayahudi?”
M. Wakapiga kelele na kusema,
W. “Si huyu, bali Baraba!”
M. Na Baraba alikuwa mnyang'anyi. Hapo Pilato alimtwaa Yesu,
akampiga mijeledi. Nao askari wakasuka taji la miiba, wakamtia
kichwani, wakamvisha joho la zambarau, wakamjongea,
wakisema,
W. “Salaam, mfalme wa Wayahudi!”
M. Wakampiga makofi. Kisha Pilato akaenda tena nje, akawaambia,
W. “Tazameni, ninamleta nje, mpate kutambua ya kuwa sioni kosa
kwake.”
M. Hapo Yesu alitoka nje amevaa taji la miiba kichwani na lile joho
la zambarau. Pilato akawaambia,
W. “Mtazameni mtu!”
M. Makuhani wakuu na watumishi walipomwona, walipiga kelele,
W. “Msulibishe! Msulibishe!”
M. Pilato akawaambia,
W. “Mchukueni ninyi wenyewe, mkamsulibishe. Kwa maana mimi
sioni kosa kwake.”
M. Wayahudi wakamjibu,
W. “Sisi tuna sheria, na kwa kadiri ya sheria hiyo amestahili kufa
kwa sababu amejidai kuwa Mwana wa Mungu.”

8
M. Pilato aliposikia hayo, akazidi kuogopa, akaingia tena praitorio,
akamwambia Yesu,
W. “Umetoka wapi?”
M. Yesu hakumjibu. Pilato akamwuliza,
W. “Husemi nami? Hujui ya kuwa nina mamlaka ya kukufungua, na
nina mamlaka ya kukusulibisha?”
M. Yesu akamjibu,
 “Usingekuwa na mamlaka yoyote juu yangu mimi, kama
usingepewa kutoka juu. Kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi
mwako ana kosa kubwa zaidi.”
M. Toka hapa, Pilato akajaribu kumfungua; lakini Wayahudi
wakapiga kelele wakisema,
W. “Ukimfungua huyu, wewe si rafiki wa Kaisari. Kila mtu ajifanyaye
mfalme anamuasi Kaisari.”
M. Pilato aliposikia maneno hayo akamleta Yesu nje na akaketi
katika kiti cha hukumu, mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au
kwa Kiebrania, Gabbatha. Ilikuwa siku ya maandalio ya Pasaka,
mnamo saa sita. Akawaambia Wayahudi,
W. “Tazameni, mfalme wenu!”
M. Nao wakapaza sauti,
W. “Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe!”
M. Pilato akawaambia,
W. “Je, nimsulibishe mfalme wenu?”
M. Makuhani wakuu wakajibu,
W. “Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.”
M. Hapo Pilato alimtoa kwao ili asulibiwe. Nao wakamchukua Yesu,
naye mwenyewe alichukua msalaba njiani toka mjini mpaka
mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania Golgotha.
Huko wakamsulibisha, na pamoja naye wengine wawili, mmoja
kushoto na mmoja kulia, na Yesu katikati. Pilato akandika hati,
akaiweka juu ya msalaba. Ilikuwa imeandikwa, “Yesu Mnazareti,

9
Mfalme wa Wayahudi.” Wayahudi wengi walisoma hati hiyo,
maana aliposulibiwa Yesu palikuwa karibu na mji; lugha ya hati
ilikuwa Kiebrania, Kilatini, na Kigiriki. Makuhani wakuu wa
Wayahudi wakamwambia Pilato,
W. “Usiandike, ‘Mfalme wa Wayahudi,’ bali ya kwamba alisema,
'Mimi ni Mfalme wa Wayahudi.’”
M. Pilato akajibu,
W. “Niliyoandika nimeyaandika.”
M. Baada ya kumsulibisha Yesu, askari waliyachukua mavazi yake,
wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu moja. Pia
walichukua kanzu; nayo kanzu ilikuwa nzima bila mshono, yaani
mfumo mmoja toka juu mpaka chini. Basi, wakaambiana,
W. “Tusiipasue, afadhali tuipigie kura na hivyo kuamua itakuwa ya
nani,”
M. kwa namna hii yalitimia Maandiko yasemayo: “Waligawanya
nguo zangu, wakalipigia kura vazi langu.” Hayo ndiyo waliyofanya
askari.
Karibu na msalaba wa Yesu walisimama mama yake, na ndugu
wa mama yake, Maria mke wa Klopa, na Maria Magdalena, Basi,
Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye mfuasi
aliyempenda, alimwambia mama yake,
 “Mama, tazama mwanao.”
M. Kisha akamwambia mfuasi,
 “Tazama mama yako.”
M. Toka saa ile mfuasi huyo alimpokea nyumbani kwake. Baada ya
hayo, Yesu akijua ya kuwa yote yaliyotakiwa kwa kutekeleza
Maandiko yametimia, akasema,
 “Naona kiu. ”
M. Huko kulikuwako chombo kilichojaa siki. Basi, wakalowesha
sifongo katika siki, wakaipachika kwenye mwanzi, wakakigusa
kinywa chake. Baada ya kuipokea siki, Yesu alisema,

10
 “Yametimia.”
M. Akainama kichwa, akatoa roho.

Wote wanakaa kimya kwa muda mfupi.

M. Siku ile ilikuwa siku ya kuandaa Pasaka. Kwa hiyo Wayahudi


walimwomba Pilato, waliosulibiwa wavunjwe miguu na
kuondolewa, ili miili yao isikae msalabani siku ya Sabato, kwa
maana Sabato ile ilikuwa sikukuu kubwa. Basi, askari wakaja,
wakamvunja miguu yule wa kwanza na wa pili waliosulibiwa
pamoja naye. Lakini walipomjia Yesu na kumwona amekwisha
kufa, hawakumvunja miguu, ila askari mmojawapo alimchoma
ubavu kwa mkuki, mara ikatoka damu na maji. Aliyeona hayo,
ameyashuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya
kuwa anasema kweli, ili ninyi pia mpate kusadiki. Maana hayo
yametendeka, ili andiko litimie lisemalo: “Hatavunjwa mfupa
hata mmoja.” Tena andiko lingine lasema: “Watamtazama yule
waliyemchoma.” Baada ya hayo, Yosefu wa Arimathea, ndiye
mfuasi wa Yesu, lakini mfuasi wa siri kwa kuwaogopa Wayahudi,
alimwomba Pilato ruhusa auondoe mwili wa Yesu. Pilato
akampa ruhusa. Basi, akaenda, akauondoa mwili wake. Akaja
Nikodemo, yule aliyemwendea Yesu mara ya kwanza usiku,
akaleta mchanganyiko wa manemane na udi, yapata ratili mia.
Kisha wakautwaa mwili wa Yesu, wakaufunga sanda ya kitani
pamoja na manukato, kama ilivyo desturi kwa Wayahudi kuzika.
Pale aliposulibiwa palikuwa na bustani, na katika bustani
kulibuwa na kaburi jipya, ambamo hajazikwa bado mtu. Basi
humo ndani wakamweka Yesu kwa sababu ya Maandalio ya
Pasaka yo Wayahudi, na kaburi lilikuwa karibu.
M. Injili ya Bwana... Sifa kwako Ee Kristu.

11

You might also like