You are on page 1of 5

HOTUBA YA MHE. DKT.

MOHAMMED GHARIB BILAL, MAKAMU WA


RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE
KONGAMANO LA KITAIFA KUHUSU WATOTO WALIO KATIKA
MAZINGIRA HATARISHI, UKUMBI WA MWL. JULIUS NYERERE,
DAR ES SALAAM, TAREHE 18 FEBRUARI 2015

Mhe. Dkt. Seif Seleman Rashid (Mb)


Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii;
Waheshimiwa Mawaziri mliopo;
Mhe. Said Mecky Sadick
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali;
Waheshimiwa Mabalozi wa Nchi mbalimbali;
Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Wawakilishi wa Wadau mbalimbali;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Waheshimiwa Wakurugenzi wa Halmashauri;
Ndugu Wanahabari;
Ndugu Wananchi;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu
mwingi wa rehma kwa kutupa uzima na afya njema, na kuweza kukusanyika
hapa katika Kongamano hili muhimu. Nitumie nafasi hii pia kukushukuru
wewe binafsi Mhe. Dkt. Seif Seleman Rashid, na uongozi mzima wa Wizara

wa Afya na Ustawi wa Jamii, kwa heshima kubwa mliyonipa, kunialika


kufungua kongamano hili.
Mheshimiwa Waziri;
Shughuli ya leo ni muhimu na imekuja wakati muafaka kwa kuwa Taifa letu
bado linakabiliwa na ongezeko la watoto walio katika mazingira hatarishi
pamoja na matukio ya ukatili, unyanyasaji, utelekezaji na unyonyaji dhidi ya
watoto. Hivyo tuna kila sababu kukaa na kuumiza vichwa, ili kupata namna
bora ya kuondokana na matatizo haya katika jamii yetu.
Ndugu Washiriki wa Kongamano;
Mabibi na Mabwana;
Nchi yetu kama zilivyo nchi nyengine za Kusini mwa Jangwa la Sahara
imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na janga la UKIMWI, umaskini, migogoro ya
kijamii, ukatili na unyanyasaji. Matatizo haya yamesababisha ongezeko
kubwa la watoto walio katika mazingira hatarishi kutokana na kudhoofika
kwa mifumo ya kijamii ya utoaji huduma katika ngazi ya familia. Taarifa za
tafiti na chambuzi mbalimbali zinaonesha kwamba wapo watoto milioni 2.5
ambao ni yatima kutokana na janga la UKIMWI (TDHS 2010). Matokeo ya
zoezi la utambuzi wa watoto walio katika mazingira hatarishi uliofanyika
katika halmashauri 111, unaonesha kuwa wapo watoto 897,913 wakiwemo
wasichana 422,019 na wavulana 475,894 wanaoishi katika mazingira
hatarishi (Taarifa ya utambuzi hadi 2013).
Vile vile Utafiti wa Hali ya Ukatili na Unyanyasaji (VAC 2009) uliofanyika
Tanzania, umeonesha kuwa watoto watatu kati ya 10 wa kike, na mtoto
mmoja kati ya saba wa kiume, wamefanyiwa ukatili wa kingono kabla
hawajafikisha umri wa miaka 18. Utafiti huo umeonesha pia robo ya watoto
wote wa kiume na wa kike, wamefanyiwa ukatili wa kimwili kabla ya kufikisha
umri wa miaka 18. Takwimu hizi zinatuonesha kwamba watoto wetu hawako
katika hali ya usalama jambo linaloathiri makuzi na maendeleo yao na Taifa
zima kwa ujumla kwa sababu watoto ndio Taifa la kesho.
Ndugu Washiriki wa Kongamano;
Mabibi na Mabwana;
Hali ya watoto wetu nchini hairidhishi kwa kuwa watoto walio wengi na hasa
wale walio katika mazingira hatarishi wanakumbwa na vidokezo vya hatari
katika umri mdogo. Vidokezo hivyo ni pamoja na afya duni, lishe duni, malezi
duni ndani ya familia au kaya, watoto kuishi na kufanya kazi mitaani,
kukinzana na sheria, vitendo vya ukatili kama vile kubakwa, kupigwa,
kutumikishwa nk. Watoto hawa wako katika hatari zaidi ya kuathirika katika

makuzi yao kimwili kiakili na kisaikologia jambo ambalo si jema kwa


maendeleo na maisha yao ya baadae. Vilevile watoto wengine wanapoteza
maisha na wengine wanapata ulemavu wa kudumu, kwa mfano wale
wanokatwa sehemu za viungo vyao kutokana na imani potofu zilizopo katika
jamii. Nafarijika sana kuona kwamba mmetambua umuhimu wa
kuwashirikisha watoto katika Kongamano hili ili wao wenyewe waweze
kuzungumza yale yanayowasibu. Rai yangu ni kwamba, ujumbe
utakaowasilishwa na watoto hawa, upewe kipaumbele na mapendekezo yao,
yaingizwe katika mikakati ya utekelezaji wa mpango huu.
Ndugu Washiriki;
Mabibi na Mabwana;
Serikali yenu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanya jitihada kubwa
katika kukabiliana na hali ya ongezeko la watoto walio katika mazingira
hatarishi pamoja na matukio ya ukatili na unyanyasaji wa watoto. Hata hivyo
utekelezaji wa jambo lolote haukosi changamoto. Nimearifiwa kwamba zipo
changamoto kadhaa zinazokabili utekelezaji wa mradi huu ambazo ni;
Uhaba wa rasilimali, Jamii kutoona umuhimu wa kusaidia malezi, Matunzo na
ulinzi kwa watoto walio katika mazingira hatarishi, Kiwango cha umaskini
katika ngazi ya familia/kaya, Majanga mbalimbali ukiwemo UKIMWI, Wazazi
kutengana na kuvunjika kwa ndoa pamoja na baadhi ya mila na desturi
zenye madhara. Yote haya yamesababisha kuwepo ongezeko la watoto
wanaoishi katika mazingira hatarishi na matukio ya unyanyasaji na ukatili
kwa ya watoto.
Ndugu Washiriki;
Mabibi na Mabwana;
Wito wangu katika kukabiliana na changamoto hizi, nawaomba wadau
mbalimbali waendelee kushirikiana na kusaidia Serikali katika kuandaa na
kutekeleza miradi mbalimbali ya Malezi, Matunzo, Ulinzi na Usalama kwa
watoto. Nitumie nafasi hii pia, kupongeza mashirika na taasisi ambazo kwa
njia moja ama nyingine, zimekuwa mstari wa mbele kusaidia miradi
mbalimbali ya kuboresha maisha ya watoto wetu. Kipekee, napenda
kushukuru mashirika yafuatayo kwa misaada yake mbalimbali ikiwemo ya
fedha na utaalamu. Mashirika hayo ni pamoja na; Shirika la Kimataifa la
Kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Masuala
ya Wanawake (UN Women), Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID),
Abbot Fund, Save the Children, Plan International, World Vision, European
Union, Catholic Relief Service pamoja na wadau wengine wote ambao
wanashirikiana na Serikali katika kutekeleza mipango mbalimbali ya
kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi tangu mwaka
2000. Napenda pia kuwapongeza Viongozi na watendaji katika halmashauri

zote za Tanzania Bara kwa kazi wanayoifanya ya usimamizi na utekelezaji wa


Mpango wa Huduma kwa Watoto Walio Katika Mazingira Hatarishi. Hongereni
sana, ongezeni bidii, msirudi nyuma.
Ndugu Washiriki;
Mabibi na Mabwana;
Naamini kwamba tumekusanyika pamoja katika Kongamano hili ili kuweza
kutafakari kwa pamoja hali ya watoto walio katika mazingira hatarishi hapa
nchini. Hivyo mijadala yenu katika siku tatu hizi ichambue na kuangalia
mambo yafuatayo;
1.

Majukumu ya kila mmoja wenu katika kuboresha hali ya


malezi, matunzo na ulinzi kwa watoto hao,

2.

Hali ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Watoto


Walio katika Mazingira Hatarishi (2013 2017) na namna
ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza,

3.

Kutumia vyombo vya habari katika kutoa hamasa na


mafunzo kwa umma juu ya umuhimu wa malezi na ulinzi wa watoto,
4.
Kuandaa mikakati endelevu ya kuimarisha upatikanaji wa
rasilimali kwa ajili ya huduma kwa watoto walio katika mazingira
hatarishi, na

5.

Uimarishaji wa mifumo ya ulinzi na usalama kwa watoto.

Ndugu Washiriki wa Kongamano;


Mabibi na Mabwana;
Kongamano la leo litupe fursa ya kutambua kwamba jukumu la kulea,
kutunza na kulinda watoto wetu ni letu sote, hivyo kila mmoja wetu
anapaswa kuendelea kutekeleza wajibu huu muhimu kwa kasi zaidi na
kuhakikisha kuwa masuala ya watoto hawa, yanapewa kipaumbele na
kuingizwa katika mipango ya maendeleo katika ngazi zote. Ni imani yangu
kwamba washirika wetu wa maendeleo, watazidi kuunga mkono juhudi zetu
za kuboresha maisha ya watoto walio katika mazingira hatarishi. Napenda
pia niwakumbushe viongozi wa wizara mbalimbali kwamba tunao wajibu wa
kutekeleza matamko tuliyojiwekea wakati wa Uzinduzi wa Mpango Kazi wa
Pili wa kitaifa wa Huduma kwa Watoto Walio katika Mazingira Hatarishi na

Uzinduzi wa Matokeo ya Utafiti wa Hali ya Ukatili na Unyanyasaji kwa Watoto


nchini.
Ndugu Washiriki wa Kongamano;
Ndugu Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Kwa kuhitimisha hotuba yangu, natoa wito kwa wananchi wote kila mmoja
wetu awajibike ipasavyo katika suala zima la kulea na kutunza watoto wetu
ipasavyo. Sisi sote tuna jukumu la kuhakikisha kwamba watoto wetu
wanaishi katika hali ya usalama na wanalelewa na kukuzwa katika maadili
mema.

Baada ya kusema hayo, kwa heshima kubwa na taadhima natamka kwamba;


Kongamano la Kitaifa la Watoto Walio Katika Mazingira Hatarishi,
limefunguliwa rasmi.
Nawatakia majadiliano mema. Tuwajibike Kuwalinda Watoto Wetu
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

You might also like