You are on page 1of 7

1

Sehemu ya kwanza

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

Katika kaya ya Muthithi, paliishi mwanamume mosi na ahali wake. Mwanamume huyo aliitwa Koga.
Alizimbua riziki yake kwa kuwatekea wakazi maji. Naye mkewe alichuuza maandazi na vitakataka
vingine katika chete ya Muthithi. Licha ya pato lao dogo, waliishi kwa furaha na buraha. Ni bayana
kuwa, binadamu hapati vyote wala hanyimwi vyote. Siku ayami zilipita kitambo waja hao wabarikiwe
na mtoto. Ni miujiza ya Mola kuwa ndoa yao ilidumu katika kipindi hicho. Wavyele wa Koga walikuwa
wemempa himizo na sindikizo amtaliki mkewe na kufunga pingu za maisha na mke mwingine. Mke
ambaye angewazalia wajukuu. Koga naye hakuyumba, alisimama tisti. Yeye alizidi kumwomba Mola na
kusubiri. Nalo la wahenga likatimia mcha Mungu si mtovu na subira huvuta heri!

“Washauri” wengi walikosa uso Susia alipopata mimba kisha akajifungua. Nia zaombovu ziligonga
mwamba. Lakini watu ni ngamba hawakosi la kuamba. Ghafla walizusha uvumi mwingine. Ulikuwa
uvumi usiokuwa na msingi wowote. Uvumi ulioongozwa na chuki na kijicho. Eti Susia alikuwa na
macho ya nje na mtoto wao alikuwa mtoto haramu. Yote hayo hayakuwavunja moyo Susia na kipenda
roho chake. Badala yake, hayo yaliimarisha mahaba yao. Ndoa yao ilinawiri na kushamiri. Kweli ndoa
hufungwa mbinguni. Wadaku wale walisalimu amri. Walibwaga silaha. Waliona kazi yao ilikuwa sawa
na kufumbatia maji iwapo si kujaribu kukimbizana na upepo. Naam, naye Mungu hamwachi binadamu
wake. Kaba, mwanao Susia na Koga, aliinukia kuwa mtoto mwenye bidii, adabu na mwajibikaji.
Shuleni akawa na kichwa chepesi. Matendo na maneno yake yakawa ni ya kupigiwa mfano.

Licha ya uhawinde wa wavyele wake, yeye alijifunga nira curriculumni. Aling’amua bayana kuwa ngazi
ya kupandia na kuondoka katika lile lindi la umaskini ilikuwa ni elimu. Daraja la elimu aidha
lingemvusha hadi ng’ambo ya pili, ng’ambo ya ufanisi. Alizidi kujifunga kibwebwe. Alielewa kuwa,
mtaka cha mvunguni sharti ainame na papo kwa papo kamba hukata jiwe. Si ajabu basi katika mtihani
wa darasa la nane, alipata maksi za juu sana. Nacho chanda chema huvishwa pete. Alipata mdhamini wa
curriculum yake ya shule ya upili. Kamwe hakugeuka kuwa mgema ambaye anaposifiwa tembo hulitia
maji. Aliongeza bidii zake maradufu. Vilevile, hakujigeuza kuwa punda ambaye fadhila zake ni mashuzi.
La hasha! Alikuwa kijana mwenye shukrani sana kwa mdhamini wake. Nusu muongo baadaye, kijana
Kaba alijiunga na chuo kikuu.

Swahili www.priorityhometuition.co.ke
2

Huko chuoni, maisha yalikuwa tofauti sana. Vishawishi vya kila nui vilikuwa tumbi nzima. Mbwamwitu
kwenye ngozi za kondoo walikuwa wengi. Hata hivyo yeye hakujigeuza kuwa maji yafuatayo mkondo.
Alikuwa na mikakati yake imara. Ingawa waambao waliamba mwenye njaa hana miko, Kaba alisimama
imara kama chuma cha pua licha ya telezi na utepetepe tele wa maisha. Aliyaepuka mambo ya anasa
kama ukoma. Alielewa fika kuwa anasa hunasa nayo raha ikipita hugeuka na kuwa karaha. Alifuzu
chuuo kikuu na kuajiriwa na shirika moja la kimataifa. Mbali na hayo aliendelea na curriculum na
kupata shahada ya uzamili. Mshahara wake ukawa wa kutajika, nyumba ya fahari na gari la kukodolewa
macho. Kumbe bidii hulipa na zito hufuatwa na jepesi!

Maelezo ya msamiati

• siku ayami – siku nyingi

• simama tisti – simama imara, kutoogopa

• kichwa chepesi – kuwa na uwezo wa kuelewa mambo haraka

• karaha – balaa, -enye kuudhi

1. Ni kweli kusema Koga na mkewe:

A) Walikuwa matajiri wa mali.

B) Walikuwa maskini wasiokuwa na furaha.

C) Waliishi kwa furaha na utulivu.

D) Walikuwa na watoto wengi.

Swahili www.priorityhometuition.co.ke
3

2. Ni nani hasa waliomtaka Koga amwoe mke mwengine?

A) Susia.

B) Wakweze Koga.

C) Mavyaa na bavyaa wa Susia

D) Majirani

3. ... binadamu hapati vyote wala hanyimwi vyote... Ni nini maana ya kifungu hiki kulingana na
taarifa?

A) Koga na mkewe walikosa mtoto lakini waliishi kwa furaha

B) Koga na mkewe walikosa furaha kwa kumkosa mtoto.

C) Koga na mkewe walikosa furaha lakini wakampata mtoto.

D) Koga na mkewe walikuwa na furaha licha ya kutopata utajiri.

4. Ni nini maana ya kubwaga silaha?

A) Kukubali kushindwa.

B) Kuanguka.

C) Kushinda vitani.

D) Kukasirika.

Swahili www.priorityhometuition.co.ke
4

5. Ni zipi sifa za Kaba kwa mujibu wa makala haya.

A) Maskini mzembe.

B) Kijana mwerevu, mwenye ari na uajibikaji.

C) Kijana mwepesi na mwenye macho ya nje.

D) Kijana pweke.

6. Ni yapi yangemkwamua Kaba kutoka biwi la umaskini?

A) Elimu

B) Ujanja

C) Wepesi

D) Wazazi

7. Kwa nini Kaba alimpata mdhamini?

A) Hakuwa na wazazi.

B) Hakuwa na pesa.

C) Alikuwa amefeli.

D) Wazazi hawangeweza kumlipia karo licha ya kufua dafu katika mthani.

Swahili www.priorityhometuition.co.ke
5

8. Kamwe hakugeuka kuwa mgema ambaye anaposifiwa hulitia tembo maji. Mwandishi anakusudia
nini?

A) Kaba alianza kutumia tembo.

B) Kaba alizidi kujibidiisha.

C) Kaba alianza uvivu.

D) Kaba alingiliwa na tabia ya maringo.

9. Ni nini maana ya kujifunga kibwebwe?

A) Kuwa na bidii.

B) Kufungwa grezani.

C) Kupongezwa.

D) Kupata msaada.

10. Ni methali ipi haifai kuyaelezea maisha ya Kaba?

A) Penye nia ipo njia.

B) Akufaaye kwenye dhiki ndiye rafiki

C) Dhamira ni dira.

D) Uzuri wa kuyu ndani mabuu.

Swahili www.priorityhometuition.co.ke
6

Sehemu ya pili

Translate this text to Swahili.

Roald Dahl's parents were from Norway, but he was born in Wales on 13 September 1916. The family
used to spend the summer holidays on a little Norwegian island, swimming, fishing and going by boat.
When Roald was four years old, his father died, so his mother had to organise the trip alone for herself
and her six children.

After school, Roald Dahl did not go to university, but applied for a job at the shell company, because he
was sure they will send him abroad. He was sent to East Africa, where he got the adventure he wanted;
great heat, crocodiles, snakes, and safaris. He lived in the jungle, learned to speak Swahili and suffered
from malaria. When the second world war broke out, he went to Nairobi to join the Royal Air force. He
was a fighter pilot and shot down German planes but got shot down himself. After six months in hospital
he flew again [15]

Sehemu ya tatu

Kwa miaka ayami, wimbo wa uhifadhi wa mazingira umekuwa vinywani mwa wengi. Kila kukicha
tukaelezewa tujiepushe na ukataji ovyo wa miti. Tukahimizwa na kuelimishwa kuwa iwapo tutaikata
miti, basi tuipande mingine papo hapo. Tulielezwa tele kuhusiana na utumiaji mbolea asilia ambayo
haina madhara katika udongo wetu. Hatukukosa wosia na nasaha kuhusiana na mbinu mwafaka za
kilimo ili kuepuka au kuzuia mmomonyoko wa udongo. Lakini yote hayo, wengi wetu tuliyatemea mate.
Ikawa ni sawa na kumwashia kipofu taa. Ni sawa na kumpigia mbuzi gita. Tulishauriwa kutoichafua
mito yetu lakini tukaigeuza kuwa mabomba ya uchafu.

Ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wawekezaji wakielekeza mifereji ya maji taka kutokaviwandani
mwao hadi mitoni au maziwani. Si ajabu tena kuona mifereji kutoka vyooni ikielekezwa hadi mitoni.
Isisahaulike maji ya mito yiyo hiyo yanatumiwa na binadamu, mifugo, ndege na wanyamapori. Ukizuru
mitaa yetu, utashangaa kuona kuwa, nusura katika kila sehemu wazi, imegeuzwa kuwa biwi la takataka.
Mirundiko ya takataka inayonuka fee imesimama kwa aibu kila mahali. Ni aibu na fedheha yetu hiyo.
Kivuli hicho cha fedheha kinatuandama popote tuendapo licha ya kujiita wastaarabu na wajuaji.

Swahili www.priorityhometuition.co.ke
7

Matokeo ya hayo yote ni masaibu tele yanayotufuata. Hatuachi kulalamika kutokana na maradhi ya kila
aina. Tutaepukaje maradhi ilhali baadhi ya mboga tunazotumia hunyunyiziwa maji ya takataka! Maradhi
yatokanayo na uchafuzi wa hewa limekuwa jambo la kawaida aushini mwetu.

Mikurupuko ya ndwele kama vile kupindupindu si jambo geni maishani mwetu. Kweli usaha hunuka.
Nayo majuto ni mjukuu mwishowe huja kinyume. Uhaba wa chakula ni tisho kubwa kwetu. Kutokana
na mbinu mbovu za kilimo, mashamba yetu yanazidi kushindwa kutosheleza mahitaji yetu. Mito yetu
nayo inazidi kukauka. Viumbe vya majini vinazidi kudidimia. Kisa na maana, misitu inazidi kudidimia
nayo mito inazidi kuchafuliwa. Mingi yao inaweza kuitwa mito ya sumu. Maafa hayo yote yanatokana
na miaka mingi ya mzaha. Mzaha dhidi ya mazingira yetu. Mambo ambayo yanastahili kuchukuliwa
kwa uzito ufaao tukayadhararisha. Nayo matokeo ndiyo haya. Maafa yanayotishia sio maisha yetu tu
bali na ya vizazi vijavyo. Yafaa tuchukue hatua mwafaka, imara na za dharura. Tuirejeshe hali ya
zamani ili tuweze kufurahia mandhari yetu.

Maelezo ya msamiati

• miaka ayami – miaka mingi

1. Fupisha ufahamu huu chini ya vichwa vifuatavyo. [15]

i. Mbinu za kuhifadhi mazingira

ii. Uchafuzi wa mazingira

iii. Madhara ya uchafuzi wa mazingira.

Sehemu ya nne.

Insha

Endeleza insha ifuatayo na uifanye iwe ya kuvutia:

• Giza lilikuwa limechukua milki ya viumbe wote duniani. Nyota zilitoa mwanga hafifu na mwezi
ulikuwa ushatua. Katika giza hilo... [30]

Swahili www.priorityhometuition.co.ke

You might also like