You are on page 1of 102

Mawe 12 ya Kuweka Msingi

wa Maisha ya Mwamini

D. K. DAVIS
Mawe 12 ya Kuweka Msingi wa Maisha ya Mwamini
Copyright 2023 © D. K. Davis

HAK I Z OT E ZI ME HI FA DH IW A

Hakuna sehemu ya chapisho hili inayoweza kunakiliwa,


kuhifadhiwa katika mfumo wa kurejesha, au kusambazwa, kwa
namna yoyote au kwa njia yoyote, kielektroniki, mitambo, kunakili,
kurekodi au vinginevyo, bila idhini ya maandishi ya mwandishi.

Tufuatilie zaidi
https://harufuyauzima.org

Imechapishwa na:

ISBN:

Harufu ya Uzima

Dodoma, Tanzania

+255713816586
D. K. DAVIS

Yaliyomo

Utangulizi .............................................................................. iv

Karibu kwenye Familia .........................................................13

Kweli za Kiumbe Kipya ........................................................ 22

Namna Mpya ya Kuishi ........................................................ 30

Kufanywa Upya Ufahamu Wako .......................................... 38

Roho Mtakatifu .................................................................... 47

Urithi wetu katika Kristo ..................................................... 55

Kusudi la Mungu Kwetu....................................................... 62

Nafasi Yetu Kwa Mungu....................................................... 69

Mwenendo wa Imani............................................................ 75

Ukuaji wa Kiroho ................................................................. 81

Kuwa Mshirika wa Kanisa .................................................... 88

Uvunaji wa Nafsi .................................................................. 93

Hitimisho: Kuwa Makini na Ujenzi Wako ........................... 99

Kuhusu Mwandishi ............................................................. 101

iii
MSINGI WA MWAMINI

Utangulizi

Hakuna jengo kubwa na imara lililojengwa juu ya


msingi dhaifu. Ni busara kusema, maisha ya juu na mazuri
unayoyataka, yanahitaji msingi imara, wenye kina kirefu. Ili
kitu kisimame imara, kinahitaji msingi imara: miti mikubwa
inahitaji mizizi mikubwa ya kuishikilia; jengo kubwa la
ghorofa linahitaji msingi wenye kina na imara, na maisha bora
na mazuri ya Kikristo yaliyojawa udhihirisho wa manufaa ya
kile tulicho nacho ndani ya Kristo, yanahitaji msingi mzuri wa
kiroho.

Ikiwa unataka kuacha alama ya kudumu na yenye


manufaa, ni hekima kujenga nyumba au kazi yako njema juu
ya msingi imara. Katika Mathayo 7:24-27, Bwana Yesu
anawaita wapumbavu wale wanaopuuza umuhimu wa msingi,
na wenye akili wale wanaojali na kuzingatia msingi wakati wa
ujenzi.

Mtume Paulo, mkuu wa wajenzi mwenye hekima,


alipewa neema na Mungu ya kuuweka msingi wa maisha ya
kikristo. Kwake tunajifunza mengi kuhusu Ukristo. Katika 1
Wakorintho 3: 6-9, aliandika:

6 Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye


kukuza ni Mungu.

7 Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali


Mungu akuzaye.

iv
D. K. DAVIS

8 Basi yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni wamoja,


lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa
na taabu yake mwenyewe.

9 Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu;


NINYI NI shamba la Mungu, ni JENGO LA MUNGU.

Wakristo ni shamba na jengo la Mungu; watumishi wa


Mungu, yaani, mitume, manabiii, wainjilisti, wachungaji na
walimu hufanya kazi pamoja na Mungu katika kupanda na
kujenga.

Katika mstari wa 9, Biblia inasema, "Ninyi ni shamba la


Mungu, ni JENGO LA MUNGU". Kila jengo ili liwe imara
linahitaji msingi imara. Ikiwa sisi ni jengo la Mungu, basi ni
muhimu kwetu kuzingatia msingi ambao tunajengwa juu yake.

Katika Zaburi 11:3, swali la kuamsha fikira linaulizwa:


"Kama misingi ikiharibika, Mwenye haki atafanya nini?"
Jibu ni Hakuna, bali kujenga msingi mwingine.

Swali hilo ni kwa ajili ya wenye haki, yaani, wale


waaminio; kwa kuwa hakuna mwenye haki wala mtakatifu
asiyeamini. Hii ina maana, hata WENYE HAKI wanaweza
kuharibikiwa misingi yao, ikiwa haikujengwa vyema.

Je! Yeye hakusema, kwenye Zaburi 82:5 kwamba:


"Hawajui wala hawafahamu, hutembea gizani; Misingi yote
ya nchi imetikisika". Kutembea gizani katika uonevu wa adui,
hutokana na msingi iliyotikiswa ama kuharibiwa. Mstari wa 7
anaendelea kusema, "Lakini mtakufa kama wanadamu,

v
MSINGI WA MWAMINI

Mtaanguka kama mmoja wa wakuu." Matokeo ya msingi


ulioharibika ni mauti, aibu na mateso kutoka kwa adui.

Mchukue Lazaro masikini kama mfano: Biblia inasema,


aliishi maisha ya haki, na baada ya kufa alikwenda mbinguni;
na kuonekana kifuani mwa Ibrahimu. Lakini, maisha yake
hapa duniani yalijaa mateso na maumivu, kwa sababu msingi
wake ulikuwa umeharibika. Ingawa alikuwa mwadilifu,
hakutembea katika baraka za wenye haki (utajiri na
utoshelevu), kwa sababu alikosa msingi imara kwenye eneo la
fedha na mali (Soma Luka 16:19-31).

Huu ni ukweli: Mahangaiko mengi wanayokabiliana


nayo wakristo ni kwa sababu udhaifu na ubovu wa misingi yao.
Wakristo wengi hawakujifunza kabisa mafundisho ya msingi
ya imani, na wengine walifundishwa mafundisho potofu
yasiyo na kweli kamili ya Neno la Mungu.

KWELI SITA (6) KUHUSU MSINGI

1. Maisha Yako ni Udhihirisho wa Msingi Wako


wa Kiroho

Jinsi unavyoishi (mwenendo na tabia yako), ulipo na


unapoelekea kimaisha, panaamuliwa na msingi ulionao. Jinsi
unavyofikiri, unavyozungumza, unavyoomba, unavyotoa;
jinsi unavyoabudu na kusifu ni kielelezo cha malezi yako ya
kiroho, msingi wako.

vi
D. K. DAVIS

Msingi wako wa kiroho unatoa picha ya jinsi maisha


yako yatakavyokuwa baadae.

2. Unajenga Juu ya Mafundisho ya Msingi


Uliyofundishwa

Ni rahisi kuamini kitu, kuliko kutoamini kile


ulichokiamini hapo awali. Hivyo, ni muhimu sana kujifunza
mafundisho sahihi wakati wa kuweka msingi.

Wengi wamefundishwa kimakosa, na hivyo kuteseka


kwa muda mrefu katika mambo wanayopaswa kushinda na
kuishi juu yao. Hivyo, wengi hufa kabla ya wakati wao, huishi
maisha ya laana, wako katika vifungo, kamwe hawajawahi
kuwa huru kutoka katika dhambi zao za zamani, kwa sababu
ya mafundisho yasiyo sahihi.

3. Msingi Unakupa Mwelekeo

Utaenda pale ambapo msingi unakuelekeza. Unaweza


kutabiri hali ya maisha ya mtu, na jinsi maisha yake yatageuka
kuwa, kwa kuzingatia msingi wake.

Msingi unakuelekeza; unakupa njia ya kufuata


maishani. Bila msingi hakuna matarajio wala maono. Imani
yako inaongozwa na msingi wako; unavutia vitu kwako sawa
na msingi ulionao.

vii
MSINGI WA MWAMINI

4. Msingi wako Unafafanua Mipaka Yako

Huwezi kujenga zaidi ya msingi wako; ukihitaji kujenga


zaidi, inakupasa kuongeza msingi. Watu wengi wameacha
mambo mazuri, kwa sababu hayaendani na misingi yao.

Kwa mfano, wengine hawaamini katika uponyaji na


miujiza; walifundishwa katika mafundisho yao ya msingi
kuwa zama za uponyaji, ishara na miujiza zilikwisha pita
zamani, kipindi cha mitume.

Isipokuwa kwa kuuharibu msingi mbaya wa namna hii,


daima watu wa jinsi hii watakuwa na kikomo cha kupokea
kilicho bora kutoka kwa Mungu: ishara, ajabu na miujiza.

5. Msingi Unakupa Uhakika wa Kuinuka

Huwezi kujenga juu zaidi ya msingi wako. Kadiri


unavyotaka maisha yako yawe mazuri, ya juu na yenye
matunda, msingi wako lazima uwe wa kina na wenye nguvu.

Unapotazama juu unakotaka kujenga, angalia chini jinsi


msingi wako unapaswa kuwa.

6. Msingi Unahakikisha Uthabiti wa Jengo

Wewe ni thabiti kama msingi wako. Wakati hali ngumu


za maisha zinakuja kwako, utabaki umesimama imara ikiwa
msingi wako ni imara.

Msingi hukupa kusimama imara katika nafasi yako siku


za uovu, siku za kujaribiwa kwako.

viii
D. K. DAVIS

PAULO, MKUU WA WAJENZI

Katika kitabu cha Wakorintho wa kwanza, sura ya 3


kuanzia mstari wa 10 mpaka wa 15, mtume Paulo anatupa
maelezo mazuri kuhusu msingi:

10 Kwa kadiri ya NEEMA YA MUNGU NILIYOPEWA,


mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye HEKIMA,
NALIUWEKA MSINGI, na mtu mwingine ANAJENGA JUU
YAKE. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu
yake.

11 Maana MSINGI mwingine hakuna mtu awezaye


KUUWEKA, isipokuwa ni ule ULIOKWISHA KUWEKWA,
yaani, YESU KRISTO.

12 Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo,


dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani
au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri.

13 MAANA SIKU ILE itaidhihirisha, kwa kuwa


yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe
UTAIJARIBU kazi ya kila mtu, ni ya namna gani.

14 Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata


thawabu.

15 Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye


mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto."

ix
MSINGI WA MWAMINI

Msingi wetu ni Kristo; Yeye ndiye msingi wetu thabiti.


Kadiri unavyomjua, na kufahamiana Naye, ndivyo msingi
wako unavyozidi kuwa na kina na wenye nguvu.

Mistari ya hapo juu tunaonywa kuhusu mitihani na


majaribu yatakayokuja kupima kile tunachokijenga juu ya
msingi wetu. Tunajenga kwa kujifunza, hivyo, daima angalia
na hakiki mara kwa mara jinsi unavyojenga juu ya msingi,
ambao ni Kristo.

Tunapata wapi Mawe ya Kujengea?


Biblia, Nyaraka

Waefeso 2:20-22 inasema,

20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii,


naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni.

21 Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na


kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana.

22 Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa


maskani ya Mungu katika Roho.

x
D. K. DAVIS

Namshukuru Mungu kwa neema aliyonipa kukusanya


na kuwasilisha kwako maarifa haya yaliyokuja kwako kama
Mawe 12 ya Kuweka Msingi wa Maisha ya Mwamini,
kupitia kitabu hiki chenye msukumo mzuri wa Roho
Mtakatifu.

Ninaomba usomapo kitabu hiki, Roho Mtakatifu


akufundishe na kukuelezea zaidi ya yale ambayo ningeweza
kueleza kwa maandishi.

Maisha yako yajawe utukufu na matunda baada ya


kupokea kweli hizi za ajabu; uangaze zaidi na uongezeke
katika neema na amani; miujiza, ishara na maajabu vikufuate
unapojifunza, kuamini na kuupokea ujumbe huu, katika Jina
la Yesu Kristo.

Amina!

xi
MAWE 12 YA KUWEKA MSINGI
WA MAISHA YA MWAMINI

D. K. Davis
JIWE LA 1

Karibu kwenye Familia

Mwanadamu amepotea, hana tena uhusiano mzuri na


muumba wake, baada ya kumtenda dhambi bustanini. Yeye
na uzao wake wote wanawekwa chini ya utawala wa dhambi;
wamefungwa na nguvu za giza. Lakini, Mungu amejaa rehema
na fadhili, anadhihirisha upendo wake mkuu kwa
kujipatanisha na mwanadamu kwa kufa, kuzikwa na kufufuka
kwa mwanawe Yesu Kristo.

Sasa wokovu unapatikana kwa watu wote. Kupitia


mahubiri ya injili, unashuhudiwa na Roho Mtakatifu kutubu.
Unapata uzoefu sawa na mwana mpotevu; unasema moyoni
mwako: "Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na
kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako;
sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa
watumishi wako" (Luka 15:18-19).

Lakini, unapokikaribia kiti chake cha neema na rehema


kwa ujasiri na moyo wa toba, Mungu anakuona kwa mbali na
kwa huruma nyingi, anakukimbilia, na kukuangukia shingoni
mwako, na kukubusu sana. Baada ya kutubu, Anazungumza
na watumishi Wake: yavueni mavazi yake machafu, mvikeni
mavazi safi na bora zaidi, mvike pete ya familia mkononi
mwake na viatu miguuni mwake.

13
Habari kuu ya furaha inatangazwa mbinguni: “Fanyeni
karamu, enyi mbingu, na wote wakaao katika nyumba ya
Mungu; kwa maana aliyekuwa amekufa sasa yu hai tena;
alikuwa amepotea, naye amepatikana.” Malaika wote
wanafurahi na kusherehekea.

Kisha kutoka kwenye kiti cha enzi, Mfalme wa Utukufu


akasema: KARIBU KWENYE FAMILIA MWANANGU

(Huu ni mfano wa kile kilichotokea ulipompokea Yesu


kama Bwana na Mwokozi wako)

FAMILIA YA MUNGU

“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika


watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake”

Yohana 1:12

Tofauti na dini nyingine, ukristo ni Imani pekee


inayokuingiza kwenye mahusiano, mahusiano ya kifamilia ya
Baba na mwana. Huu ni ukweli wa Agano Jipya. Mungu
alimtoa mwanawe pekee, ili kwa kumwamini na kumpokea,
upewe haki na uwezo wa kufanyika mtoto wa Mungu.

14
MWANA NA MTUMWA

Kuna tofauti kubwa kati ya mwana na mtumwa. Mwana


ni mrithi, mtumwa ni mwangalizi wa vitu vya mwana; mwana
ana uhusiano na babaye, mtumwa yuko kwa ajili ya malipo
(faida yake binafsi sio uhusiano); wana wanafanya kazi
pamoja na Baba yao, na tayari wana kibali, watumwa hufanya
kazi ili kupata kibali.

Ulipomwamini Bwana Yesu, ulifanyika mwana na si


mtumwa. Jione hivyo na husiana na Mungu kama mwana ili
uweze kufaidika na haki zako za uwana.

KUZALIWA KATIKA FAMILIA MPYA

Wokovu si tu kuepushwa na hukumu ya milele


inayokuja, bali kuingizwa katika familia, Familia ya Mungu.
Huu ni ubora wa Ukristo; unatofautisha Ukristo na dini
nyingine zote.

Mtume Paulo aliandika juu ya kile ambacho Mungu


alifanya katika kutuokoa: "Naye ALITUOKOA katika nguvu
za giza, akatuhamisha na KUTUINGIZA katika UFALME
WA MWANA wa pendo lake" (Wakolosai 1:13). Tuliokolewa
ili kuingia katika ufalme Wake kama wana na binti zake.

Hili ndilo lilikuwa kusudi la Mungu tangu mwanzo.


Alitaka tuwe katika daraja lake; tuwe na uzima na asili yake ya
Kiungu. Biblia inasema, "Maana wale aliowajua tangu asili,
aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa

15
Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni
mwa ndugu wengi" (Warumi 8:29).

KUZALIWA MARA YA PILI

“Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu


iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu
lenye uzima, lidumulo hata milele.”

1 Petro 1:23

Mtume Petro kwa Roho anazungumzia juu ya wokovu


wetu kama uzoefu mpya wa kuzaliwa mara ya pili. Yesu
alituokoa msalabani kwa kifo chake, akilipa adhabu kamili ya
dhambi zetu; kufufuliwa kwake kutoka kwa wafu,
kulimaanisha kuzaliwa kwake mara ya pili. Tulikufa ndani
yake alipokufa pale msalabani, na kuzaliwa mara ya pili ndani
yake, alipofufuliwa kutoka kwa wafu.

Mtume Yakobo pia anaandika katika Waraka wake


kuhusu kuzaliwa kwetu mara ya pili: "Kwa kupenda kwake
mwenyewe alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama
limbuko la viumbe vyake" (Yakobo 1:18). Tumezaliwa mara
ya pili kwa Neno na kwa Roho Mtakatifu.

Kuzaliwa mara ya pili kunahusisha roho yako, si mwili


wako. Wakati mmoja, Yesu akimjibu Nikodemo kuhusu
kuzaliwa mara ya pili alipouliza, “Awezaje mtu kuzaliwa,
akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya
pili akazaliwa? (Yohana 3:4). Alijibu, “Kilichozaliwa kwa

16
mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho” (Yohana
3:6).

Kuzaliwa mara ya pili ni uzoefu wa kiroho, si wa kimwili.


Baada ya kuzaliwa mara ya pili, roho yako, wewe halisi
unaumbwa upya, lakini mwili wako unabaki kama ulivyokuwa.
Maana yake, hakuna mabadiliko ya nje ya kimwili
yanayotokea pale unapoamua kumpokea Bwana, ila kwa
hakika roho yako hufanywa upya kabisa.

MUNGU, BABA YETU

Baada ya kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo,


alimtambulisha Mungu kwetu kama Baba yetu. Haikuwa
hivyo katika Agano la kale; katika agano jipya, Mungu
anatambulishwa kwetu kama Mungu wetu na Baba yetu.
Tazama mazungumzo aliyokuwa nayo Bwana na Mariamu nje
ya kaburi.

Yohana 20:14-17,

14 Naye akiisha kusema hayo, akageuka nyuma,


akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu.

15 Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini?


Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza
bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe,
uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa.

17
16 Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka,
akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (Yaani, Mwalimu
wangu).

17 Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa


kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu
ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni
Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.

Katika mstari wa 17, alisema "...Ninapaa kwenda kwa


Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni
Mungu wenu." Asante Mungu, alituleta katika familia Yake.
Sasa tunabeba Jina lake, Yeye ni baba yetu. Sisi ni watoto
wake, Yesu akiwa mzaliwa wa kwanza katika familia hii mpya.
"Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili
wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe
mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi" (Warumi
8:29). Yeye ni mzaliwa wa kwanza miongoni mwa sisi ndugu
wengi tuliomwamini. Haleluya!

YESU, MWANA WA MUNGU

Baada ya ubatizo wake, "na tazama, sauti kutoka


mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu,
ninayependezwa naye" (Mathayo 3:17). Mungu
alimtambulisha kama mwanawe.

Baada ya hapo, Bwana Yesu,

18
- Aliishi, alitembea, na kuzungumza kama mwana wa
Mungu

- Hakuwa na wasiwasi wala woga juu ya yale


yatakayotokea kesho (Mathayo 6:25-34)

- Alimjua Baba yake, na alikuwa na ujuzi wa kile


ambacho Baba angeweza kufanya kupitia Yeye (Yohana 6:46)

- Alizungumza na Mungu katika sala kama mwana wake


(Yohana 11:41)

- Alijua kile angeweza kufanya kwa uwezo na nguvu


alizopewa na Baba yake (Yohana 11:43)

Faida za kuwa Mwana

1. Mwana hushiriki tabia za asili za babaye

"Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za


thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa WASHIRIKA
WA TABIA YA UUNGU, mkiokolewa na uharibifu uliomo
duniani kwa sababu ya tamaa." (2 Petro 1:4)

1 Yohana 3:9 inasema, "Kila mtu aliyezaliwa na Mungu


hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake;
wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa
kutokana na Mungu."

19
2. Mwana ni mrithi wa Babaye

- Anaendeleza kile baba yake ameanza

- Anamiliki anachomiliki babaye

- Anaishi ili kumpendeza baba yake

"Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa


sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi;
warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam,
tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye"
(Warumi 8:16-17).

Mwana anarithi nini?

Yote aliyo nayo Babaye.

(Angalia zaidi katika Sura ya sita)

UPENDO WAKE KWETU

Ninapenda kile ambacho Roho huwasilisha kwa Kanisa


kupitia Mtume Yohana katika Waraka wake wa kwanza Sura
ya 3 mstari wa kwanza na wa pili. Anasema, "Tazameni, ni
pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana
wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu
haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. Wapenzi,
sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado

20
tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa,
tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo."

Katika mstari wa 2 anasema, "Wapenzi, sasa tu wana


wa Mungu..." Sisi ni viumbe wapya wenye uzima na asili ya
Mungu. Sisi ni wa aina moja na Mungu; tuna uzima wa milele
katika roho zetu. Haleluya!

21
JIWE LA 2

Kweli za Kiumbe Kipya

"Hata IMEKUWA, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa


KIUMBE KIPYA; ya kale yamepita TAZAMA! Yamekuwa
mapya."

2 Wakorintho 5:17

Ukristo upo katika ufunuo wa Kristo ndani yako na


wewe ndani yake. Maandiko hapo juu yanazungumza juu ya
utambulisho wetu mpya kama wakristo. Unasema, mtu akiwa
ndani ya Kristo Yesu amekuwa kiumbe kipya. Hii ina maana,
yeye ni aina mpya ya kiumbe, mwenye uzima na asili ya mpya
kabisa, tofauti na asili ya kibinadamu aliyokuwa nayo hapo
mwanzo. Ni upya wa roho sio wa mwili. Mwili unabaki vile vile
baada ya kuzaliwa mara ya pili, lakini roho ambayo ni wewe
halisi, inakuwa mpya. Mkristo si kama wanadamu wengine,
Yeye ni mtoto wa Mungu. Haleluya!

Katika Ukristo kuna upya wa maisha; sio maisha


yaliyofanyiwa matengenezo au maisha yaliyoboreshwa, bali
maisha mapya. Ni kama vile mtoto anapozaliwa: yeye ni mtu
mpya kwenye sayari ya dunia, asiye na historia wala maisha
ya kale. Maisha ya mtoto huanza pale anapozaliwa.

Vivyo hivyo, kwetu sisi wakristo, maisha yetu huanza


pale tunapompokea Yesu kama Bwana na mwokozi wetu;
tunazaliwa mara ya pili kwa Neno na Roho (1 Petro 1:23,

22
Yohana 3:6). Biblia inasema, maisha ya kale yamepita,
TAZAMA! yamekuwa mapya; ikimaanisha kuwa mtoto wa
Mungu hana muunganiko tena na maisha ya kale, bali maisha
mapya, mazuri na yaliyojawa na ukuu; haya ndio unapaswa
kuyaona na kuyatarajia.

Cha kusikitisha ni kwamba baadhi ya wakristo


hawajawahi kufundishwa hivi. Wanaishi katika utumwa wa
dhambi zao zilizopita; hawajawahi kuwa huru kutoka kwenye
hatia za makosa yao ya zamani. Hatia ya dhambi na
kushindwa daima inaharibu imani yao kwa Mungu, na kuwa
kizuizi cha imani yao; wanajiepusha na Mungu, na wengine
wanatubu daima dhambi zao za zamani, ambazo zinaonekana
kuwa hazijasamehewa kamwe.

Mtoto wa Mungu, wewe ni mtu mpya katika Kristo.


Maisha yako yalianza ulipompokea Yesu kama Bwana na
mwokozi wako. Achana na yaliyopita, tazama na weka mkazo
kwenye maisha yako mapya ndani ya Kristo.

KUSHINDA HATIA

Mtume Paulo anaandika kwenye barua yake ya


kwanza kwa Wakorintho, sura ya 6 kuanzia mstari wa 9:

9 Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi


ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati
hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu,
wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,

23
10 wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala
watukanaji, wala wanyang’anyi.

11 Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii;


lakini MLIOSHWA, lakini MLITAKASWA, lakini
MLIHESABIWA HAKI katika jina la Bwana Yesu Kristo, na
katika Roho wa Mungu wetu.

Ndiyo, ni kweli kwamba sote tulimtenda Mungu


dhambi, na hivyo kupungukiwa na utukufu Wake (Warumi
3:21). Lakini, Yesu alikuja kuchukua adhabu kamili ya dhambi
zetu zote. Alikufa kwa ajili ya kila mtu pale msalabani; kabla
ya kifo chake msalabani, alisema, 'imekwisha'. Alimaliza kazi
ya kutuokoa; tumeokolewa kutoka kwenye adhabu ya dhambi
(moto wa milele) sisi tunaomwamini.

Katika mstari wa 9 na 10 hapo juu, Paulo anasema


baadhi ya waamini katika Kanisa la Korintho walikuwa
wamefanya dhambi nyingi na mbaya sana hapo kale, kama
vile: udhalimu, uasherati, kuabudu sanamu, uzinzi, ufiraji,
ulawiti, wizi, kutamani, ulevi, utukanaji na unyang’anyi.
Mstari wa 11 anasema habari njema: "LAKINI, mlioshwa,
lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la
Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu."

Haijalishi umewahi kufanya dhambi gani na zenye


ukubwa upi hapo awali, ulipokuja ndani ya Kristo ulioshwa,
ulitakaswa na kuhesabiwa haki. Sasa, wewe ni mtu mpya; ya
kale yamepita, furahia maisha yako mpya ndani ya Kristo, na
andika historia mpya ya maisha yako.

24
Hebu tuangalie kwa kina maneno haya matatu:
MLIOSHWA, MLITAKASWA NA MLIHESABIWA HAKI.

● KUOSHWA

Katika agano la kale, damu za mafahari (wanyama)


hazikuweza kuwaondolea dhambi wale waliohitaji utakaso,
bali dhambi zao zilifunikwa kwa muda wa mwaka mmoja na
baada ya hapo kumbukumbu lake lilikuwepo.

Waebrania 10:1-4 inasema,

1 Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema


yatakayokuwa, wala si sura ya mambo hayo, kwa dhabihu
zile zile zinazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wote
kuwakamilisha wakaribiao.

2 Kama ndivyo, je! Dhabihu hazingekoma kutolewa;


kwa maana waabuduo, wakiisha kusafishwa mara moja,
wasingejiona tena kuwa na dhambi?

3 Lakini katika dhabihu hizo liko kumbukumbu la


dhambi kila mwaka.

4 Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi


kuondoa dhambi.

Kesi hiyo ni tofauti katika Agano Jipya. Baadhi ya


mawazo na mitazamo lazima ifanywe upya, kwa kuwa bado
kuna Wakristo wenye mtazamo huo ulioelezwa kwenye mstari

25
wa pili: wanajiona kama watenda dhambi hata baada ya
kuoshwa na kutakaswa kwa damu ya Yesu.

Agano Jipya

Damu ya Yesu Kristo ilitosha kabisa kuondoa dhambi; si tu


kusamehe dhambi bali kuiondoa isiwepo wala kumbukumbu
lake. Kwa sababu ya damu ya Yesu, ni kana kwamba hujawahi
kutenda dhambi yoyote ile. Mungu hana rekodi ya dhambi
zako za kale.

Waebrania 8:10-13 inasema,

10 Maana hili ndilo AGANO nitakaloagana na


nyumba ya Israel Baada ya siku zile, asema Bwana;
Nitawapa sheria zangu katika nia zao, Na katika mioyo yao
nitaziandika; Nami nitakuwa Mungu kwao,

11 Nao watakuwa watu wangu. Nao


hawatafundishana kila mtu na jirani yake, Na kila mtu na
ndugu zake, akisema, Mjue Bwana; Kwa maana wote
watanijua, Tangu mdogo wao hata mkubwa wao.

12 Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, Na


dhambi zao SITAZIKUMBUKA TENA.

13 Kwa kule kusema, AGANO JIPYA, amelifanya lile


la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kianzacho kuwa kikuu
na kuchakaa ki karibu na kutoweka."

Mungu amesamehe dhambi na maovu yako yote,


hatakumbuka tena. Yeye ni Mungu mwaminifu, unaweza

26
kuamini Neno lake. Hakumbuki dhambi zako zilizopita, na
hatakumbuka kamwe.

Umeoshwa, umekuwa safi.

● KUTAKASWA

Hii ina maana, tulitengwa kwa ajili ya Mungu;


tumewekwa na kuandaliwa kimaalumu kwa ajili ya matumizi
ya Bwana. Ni kama vile tunavyotenga (kuweka wakfu)
vyombo na vifaa vinayotumika kanisani: tunaviweka tayari
kutumiwa na Mungu.

Utakaso ndio unaoifanya miili yetu kuwa hekalu la


Roho Mtakatifu. Imewekwa tayari kutumiwa na Mungu.
Biblia inasema, "Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la
Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?"
(1 Wakorintho 3:16).

Wakolosai 1:21-23 inasema,

21 Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa,


tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya,
amewapatanisha sasa;

22 katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili


awalete ninyi mbele zake, WATAKATIFU, WASIO NA
MAWAA WALA LAWAMA;

23 MKIDUMU TU KATIKA ILE IMANI, hali


mmewekwa JUU YA MSINGI, mkawa imara;

27
MSIPOGEUZWA NA KULIACHA TUMAINI LA INJILI
mliyosikia habari zake, iliyohubiriwa katika viumbe vyote
vilivyo chini ya mbingu; ambayo mimi Paulo nalikuwa
mhudumu wake.

Hii ni hali yetu mpya mbele za Mungu: sisi ni


WATAKATIFU,WASIO NA MAWAA WALA LAWAMA.

● KUHESABIWA HAKI

Kuhesabiwa haki ni kutangazwa kuwa asiye na hatia.


Ni kama vile haujawahi kufanya kosa lolote wala uovu wowote
ule. Haki ndiyo ikupayo amani na Mungu. Haki hutupatia
uwezo wa kusimama mbele za Mungu bila hisia ya dhambi,
hatia, au hali ya uduni. Warumi 5:1 inasema, “Basi tukiisha
kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani
kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo”.

Biblia inasema kwamba hapo kwanza tulikuwa wafu,


bila Mungu duniani, wenye dhambi na maadui wa Mungu,
lakini sasa tumehesabiwa haki, tuna amani na Mungu.
Haleluya! Sasa Mungu ni Baba na rafiki yetu kwa kuwa
tumehesabiwa haki na Yeye mwenye haki.

Jifunze zaidi:

Waefeso 2:1-3, 12-18)

28
SISI NI HAKI YAKE

Sio tu kwamba tunatangazwa kuwa hatuna hatia, bali


tumepewa asili ya Mungu (haki yake na uwezo wa kufanya
mambo mema).

2 Wakorintho 5:21, "Yeye asiyejua dhambi alimfanya


kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya
Mungu katika Yeye." Asili ya dhambi imeondolewa ndani
yetu, sasa tunayo asili mpya ya haki na utakatifu wa kweli.

Pia, Yohana anaandika katika pumzi hiyo hiyo: "Kila


mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu
uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi
kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu" (1 Yohana 3:9).

29
JIWE LA 3

Namna Mpya ya Kuishi

"...Tazama! Yamekuwa mapya"

2 Wakorintho 5:17

Kila kiumbe ana mfumo wake wa kuishi; kila kiumbe


huishi sawa sawa na uzima alionao. Samaki ana mfumo wa
maisha tofauti na kondoo; na kondoo huishi tofauti na
mwanadamu; vivyo hivyo mwanadamu wa kawaida ni tofauti
na kiumbe kipya ndani ya Kristo. Wewe ni kiumbe kipya ndani
ya Kristo, una namna mpya ya kuishi.

1 Wakorintho 3:1-3 inasema,

1 Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi


kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu
wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika
Kristo.

2 Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa


kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi,

3 kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya


mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si
watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi
ya kibinadamu?

30
Baada ya Wakorintho kupokea ujumbe wa injili na
kuuamini (kuzaliwa mara ya pili), walionekana kutokua;
walibaki katika hali ya uchanga kiroho. Watoto wachanga
wanafafanuliwa kwa tabia zao: ni watu wenye tabia za mwilini
(wanaendeshwa zaidi na mambo ya mwilini kuliko yale ya
rohoni); tena wanaenenda kwa jinsi ya kibinadamu. Wanaishi
kama wanadamu wengine wasioamini. Haipaswi kuwa hivyo!

Kuna namna mpya ya kuishi, sio kama wanadamu


wengine wasioamini. Sisi ni viumbe wapya, tuna aina mpya ya
maisha sawa sawa na uzima tulioupokea. Tabia zetu, mawazo
yetu, jinsi tunavyozungumza, utamaduni wetu, jinsi
ulimwengu unavyotupokea na jinsi tunavyoitikia na
kuhusiana na ulimwengu ni tofauti; tunapaswa kuishi kama
wana wa Mungu hapa duniani.

Bwana wetu Yesu alitupa mfano wa namna ya kuishi


kama wana wa Mungu ambayo ni tofauti na bora kuliko
wanadamu wengine.

- Alifanya miujiza, ishara na ajabu nyingi sana

- Alizungumza na vitu (miti, upepo, maji) vikamsikia na


kumtii

- - Alitembea juu ya maji

- Aliwashibisha maelfu ya watu kwa mikate mitano na


samaki wawili

Yesu, Bwana wetu alitupa mfano kamili wa jinsi


tunapaswa kuishi.

31
Kutoka kwenye andiko letu hapo juu, tunaona tabia za
aina mbili: tabia ya mwilini na tabia ya rohoni.

TABIA YA MWILINI

Kuwa na tabia za mwilini ni kuishi maisha


yanayotawaliwa na hisia: kile unachokiona, kusikia, kunusa,
kuonja, na kugusa.

Mwanadamu ni kiumbe anayeishi katika ulimwengu


wa aina mbili kwa wakati mmoja; ulimwengu wa kiroho na
ulimwengu wa mwili. Ulimwengu wa kimwili unahitaji hisia
zako ili ufanye kazi ipasavyo duniani; lakini maisha ni ya
kiroho, unaishi kutokea rohoni.

TABIA YA ROHONI

Hizi ni tabia zinazodhihirika nje kutokea rohoni. Ni


udhihirisho wa utu wako wa ndani; ni maisha yanayotawaliwa
na kuongozwa na Roho Mtakatifu.

Kila kitu kinachoonekana na kisichoonekana


kiliumbwa na Mungu ambaye ni Roho, maana yake
ulimwengu wa roho ndio chanzo cha ulimwengu wa mwili.
Ulimwengu wa roho ni bora kuliko ulimwengu wa mwili.

Tumeitwa kuishi kutokea ulimwengu wa roho,


ulimwengu usioonekana. Hiyo ni kumaanisha, kiumbe kipya

32
ameitwa kuishi maisha ya juu na bora kuliko maisha ya
wanadamu wa kawaida.

Katika, 2 Wakorintho 5:7 tunapata maelekezo ya


namna ya kuenenda kama viumbe wapya: “(Maana
twaenenda kwa imani, si kwa kuona)." Kuenenda kwa imani
ni kuishi kutokea rohoni (Waebrania 11:1).

ASILI YETU MPYA

Katika anguko la Adamu na Hawa katika bustani ya


Edeni, dhambi iliharibu kila kitu kizuri kuhusu mwanadamu,
na dhambi iliposhughulikiwa kila kitu kilirejeshwa katika
uzuri wake.

Tabia njema ambayo Mungu alikuwa ameiweka ndani


ya mwanadamu iliharibiwa na dhambi; kwa hivyo, ilimbidi
Mungu amtume Yesu, na kupitia na kwa imani yetu Kwake
tupokee asili mpya, asili ya namna ya Mungu.

Akizungumza na Kanisa la Waefeso, Roho anasema;

Waefeso 4:22-24

22 MVUE KWA HABARI YA MWENENDO WA


KWANZA UTU WA ZAMANI, unaoharibika kwa kuzifuata
tamaa zenye kudanganya;

23 na mfanywe wapya katika ROHO YA NIA zenu;

33
24 MKAVAE UTU MPYA, ulioumbwa kwa namna ya
Mungu katika HAKI NA UTAKATIFU WA KWELI.

Utu wetu mpya umeumbwa katika haki na utakatifu


wa kweli.

Pia, Mtume Petro kwa Roho Mtakatifu anasema,

1 Petro 1:13-16,

13 Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa


na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema
mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo.

14 Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa


zenu za kwanza za ujinga wenu;

15 bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi


nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;

16 kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu


kwa kuwa mimi ni mtakatifu.

HAKI NA UTAKATIFU WA KWELI

Mitume wote wawili, Paulo na Petro kabla ya


kuzungumza juu ya kutembea kwetu katika haki na utakatifu;
wote wawili wanazungumza juu ya ufahamu na akili (nia).
Akili inadhibiti vitendo na mazungumzo yako. Ikiwa akili yako
imetakaswa kwa Neno la Mungu, matendo, mawazo na usemi
wako vinakuwa safi.

Akili yako haikuzaliwa mara ya pili pale ulipoamini;


inafanywa upya kila mara ujifunzapo Neno la Mungu.

34
(Tutaona zaidi kwenye sura inayofuata)

Roho Mtakatifu kupitia Paulo anatujulisha hili kuhusu


utu wetu mpya ndani ya Kristo.

Warumi 6:6 inasema,

6 MKIJUA NENO HILI, ya kuwa utu wetu wa kale


ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike,
tusitumikie dhambi tena

Anaendelea kusema katika mstari wa 11 mpaka 14

11 Vivyo hivyo ninyi nanyi JIHESABUNI KUWA


WAFU kwa dhambi na walio hai kwa Mungu katika Kristo
Yesu.

12 Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu


ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake;

13 wala msiendelee kuvitoa viungo vyenu kuwa


silaha za dhuluma kwa dhambi; bali jitoeni wenyewe kwa
Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa
Mungu kuwa silaha za haki.

14 Kwa maana dhambi HAITAWATAWALA ninyi,


kwa sababu hamwi chini ya sheria, bali chini ya neema."

(Warumi 6:11-14)

Kuna mikazo miwili katika mstari wa 6 na wa 11 hapo


juu: 'mkijua neno hili' na 'jihesabuni'.

35
Baada ya kupokea ujuzi wa asili yako mpya ya
utakatifu na haki ndani ya Kristo, unapaswa kujihesabu kuwa
mfu kwa dhambi na uliye hai kwa mambo ya haki tu.

Dhambi haitutawali, kwa sababu hatuko chini ya


sheria, bali chini ya neema.

Napenda ufahamu wa Mtume Yohana, anasema, "Kila


mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu
uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi
kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu" (1 Yohana 3:9).

Ni ukweli ulioje!

Je, Wakristo wanaweza kutenda dhambi?

Ndiyo, wanaweza kutenda dhambi, lakini hilo


haliendani na asili yao mpya ndani ya Kristo. Haiendani na
namna yetu mpya ya kuishi.

Ufanye nini utendapo dhambi?

Tubu na pokea msamaha kutoka kwa Mungu.

Anasema, "Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni


mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na
kutusafisha na udhalimu wote" (1 Yohana 1:9).

Pia,

"Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ILI


KWAMBA MSITENDE DHAMBI. Na kama mtu akitenda

36
dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye
haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa
dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote" (1
Yohana 2:1-2).

MAISHA YA MAFANIKIO

3 Yohana 1:2 inasema, "Mpenzi naomba ufanikiwe


katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho
yako ifanikiwavyo."

Mungu anataka tufanikiwe katika mambo yote, na


tuwe na afya kadiri roho zetu zinavyofanikiwa. Kitu chochote
kinyume na hiki hakitoki kwa Mungu.

Mungu wetu anajali kuhusu mafanikio yetu ya kimwili,


afya na maisha yetu ya kiroho. Yeye ni mwenye upendo na
anayejali. Mafanikio na ustawi ni namna yetu mpya ya kuishi.

HALELUYA!

37
JIWE LA 4

Kufanywa Upya Ufahamu


Wako

KUMBUKA: Nitumiapo maneno ‘nia’, ‘ufahamu’, ‘akili’ au


‘fikira’ katika sura hii ninamaanisha kitu kimoja.

Katika sura iliyotangulia, tuligusia kidogo kuhusu


kufanywa upya kwa akili (ufahamu); kufanywa upya nia ni
zaidi ya yale tuliyogusa kuhusu dhambi. Inaenda mbali zaidi
kumsaidia mtu kufurahia manufaa ya wokovu.

Mtu anaweza kuzaliwa mara ya pili, lakini ikiwa na


wakati nia (ufahamu) wake haujafanywa upya, anaweza kuwa
mwathirika wa hali za maisha (uonevu wa adui) kama yule
ambaye hajazaliwa mara ya pili.

Kufanya upya ufahamu wako ni muhimu. Huamua


ubora wa maisha yako.

Ufahamu unashikilia uwezo wa mawazo, utambuzi, na


shukrani, na unawajibika kwa uchakataji wa hisia, na
kusababisha mitazamo na vitendo.

KUGEUZWA NIA (UFAHAMU)

Warumi 12:1-2 inasema,

38
1 Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake
Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya
kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.

2 Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali


MGEUZWE kwa KUFANYWA UPYA NIA ZENU, mpate
kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya
kumpendeza, na ukamilifu.

Haya ni maagizo kwa 'ndugu', watu waliozaliwa mara


ya pili. Hii inamaanisha, kuzaliwa mara ya pili haimaanishi
kuwa akili yako imefanywa upya. Kuzaliwa mara ya pili ni
uumbaji mpya wa roho ya mwanadamu, si akili au mwili.
Ufahamu unapaswa kufanywa upya kwa Neno la Mungu.

Aliyezaliwa mara ya pili anapaswa kugeuzwa kwa


kufanywa upya nia, ili aweze kuyahakiki mapenzi ya Mungu
yaliyo mema, ya kupendeza, na makamilifu.

Upya wa akili sio shughuli ya siku moja; ni shughuli ya


kila siku unapoendelea kusoma na kutafakari Neno la Mungu;
hapo ndipo unapobadilishana mawazo, mtazamo, matamanio,
nia, hamu, imani na mapenzi kwa ajili Yake.

“Utatembea ndani au nje ya mapenzi ya Mungu


kulingana na jinsi akili yako ilivyobadilishwa kwa
Neno la Mungu.”

39
Ni kwa kufanya upya nia yako:

- Utajua na kuthibitisha kuwa uko katika mapenzi


kamili ya Mungu
- Unaweza kuishi katika utimilifu wa kile Mungu
amekupa kufanya katika Kristo Yesu
- Unaweza kuelewa utambulisho wako mpya katika
Kristo kama kiumbe kipya

MCHANGANYO MKUBWA

Ni mchanganyo mkubwa kuzaliwa mara ya pili,


mwenye roho mpya, lakini akili (ufahamu) ule ule wa zamani.
Maisha yako hayawezi kuonyesha tofauti kubwa ya kimatokeo
ikiwa nia (ufahamu, akili) yako haijabadilishwa kwa kufanywa
upya kwa Neno.

TAI ALIYEJIONA KUWA KUKU

Hadithi inatolewa,

Wakati tai akiwa mdogo sana, alianguka kutoka


kwenye usalama wa kiota chake. Mfugaji wa kuku
akamuokota tai huyo, akamweka shambani, na kumlea
kwenye banda la kuku kati ya kuku wake wengi. Tai alikua
akifanya yale ya kuku, akiishi kama kuku, huku akijiona na
kuamini kuwa yeye ni kuku.

40
Sote tunajua tai ni tofauti sana na kuku. Lakini kwa
vile tai huyu anafugwa kati ya kuku na anaamini ni kuku,
ataishi maisha ya kuku, hatafurahia kamwe faida za kuwa tai.

Jinsi hadithi hii ilivyo kweli, inaelezea maisha ya


wakristo wengi; wengi wanaishi kama wanadamu tu wa
kawaida (wasioamini), ilhali wao ni viumbe wapya wenye
Mungu ndani yao.

Ni lazima nia zetu zifanywe upya ili tuweze kuishi


kikweli katika utimilifu wa kile ambacho Mungu ametufanya
kuwa. Ama sivyo, tutaishi maisha ya chini na kuku, wakati
Mungu alikusudia tupande na kuishi juu zaidi na tai wengine.

ELIMU YA DUNIA DHIDI YA ELIMU YA KIROHO

Elimu ya Dunia: Hii inahusisha, elimu ya wazazi, elimu ya


shule, vyuo vikuu, elimu ya mtaani na mifumo mingine ya
elimu ya kidunia.

Elimu ya Kiroho: Hii inatokana na Neno la Mungu pekee.


Biblia ndio yenye maandiko pekee ya kweli ya elimu ya Kiroho.

Akili zetu kwa muda mrefu zimelishwa taarifa za


kidunia, kiasi kwamba wakati mwingine ni vigumu kwetu
kuamini juu ya uwezekano wa mambo ya kiroho.

Kwa mfano: Elimu ya dunia inafundisha kwamba


ugonjwa fulani hauwezi kuponywa, mtu akipatwa nao lazima

41
afe. Lakini, hiyo si kweli kulingana na Neno la Mungu.
Tunajua kwa Neno kwamba, magonjwa yote yanaweza
kuponywa kwa Jina la Yesu.

Ni muhimu kwako kujiweka chini ya kanisa au


huduma yenye msingi mzuri wa mafundisho ya Biblia, ili
ufanywe upya akili yako kwa mafundisho yanayofundishwa
hapo. Hili ni zuri kwa malezi yako ya kiroho.

MAOMBI YA PAULO

Haya ni maombi ya Mtume Paulo kwa Wakolosai,

Wakolosai 1:9-11

9 Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia,


hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe
maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu
wa rohoni;

10 mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana,


mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema,
na kuzidi katika maarifa ya Mungu;

11 mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya


nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila
namna na uvumilivu pamoja na furaha"

Unaweza pia kujiombea maombi haya kwa ajili ya


maendeleo ya akili yako. Kwa kufanywa upya akili yako, hapo
ndipo utazaa matunda kwa kila kazi njema.

42
AKILI ZA MWILI VS AKILI ZA KIROHO

Biblia inazungumza juu ya nia ya mwili na nia ya roho.


Nia ya mwili ni nia ambayo imejikita katika mambo ya kimwili.
Mwisho wake ni kifo. Nia ya roho ni mawazo yaliyowekwa
kwenye mambo ya Kiroho. Mwisho wake ni uzima na amani.

Hii inatofautisha watoto wachanga katika Kristo na


Wakristo waliokomaa: mtu ambaye akili yake imeelekezwa
kwenye mambo ya kidunia (ya kimwili) mambo ambayo
hayana faida za kiroho ni mtoto mchanga, na mtu
anayezingatia mambo ya kiroho amekomaa.

Warumi 8:5-14 inasema,

5 Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri


mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri
mambo ya roho.

6 Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho


ni uzima na amani.

7 Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu,


kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.

8 Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza


Mungu.

9 Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu,


ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu
awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.

43
10 Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa
kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya
haki.

11 Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu


katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo
Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali
ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.

12 Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili


tuishi kwa kufuata mambo ya mwili,

13 kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya


mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya
mwili kwa Roho, mtaishi.

14 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa


Mungu, hao ndio wana wa Mungu."

TAFAKARI NENO

Tunafanywa upya ufahamu (akili) zetu kwa kutafakari


Neno la Mungu.

Kile ambacho kutafakari kunafanya kwa akili zetu ni


kama vile ambavyo mmeng'enyo wa chakula unafanya kwenye
miili yetu.

Chakula kimebeba virutubisho mbalimbali muhimu


kwa ajili ya afya ya miili yetu. Lakini chakula
kisipomeng'enywa na kuingia katika mifumo mingine ya

44
mwili hakiwezi kuwa na faida kwa mwili. Maana, mfumo wa
mwili (mmeng'enyo) hukivunja vunja chakula ili kupata
virutubisho na kisha mwili huondoa uchafu

Neno la Mungu ni chakula, hatulipokei na kulikariri tu.


Bali, lazima limeng'enywe kwa kulitafakari ili lizalishe imani
na nguvu ndani yako inayoweza kukupa matokeo unayohitaji.

Mungu alimwambia Yoshua siri ya kuifanikisha njia


yake na kustawi sana, alisema, "Kitabu hiki cha torati
kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake
mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na
maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo
utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi
sana" (Yoshua 1:8).

Mahali pengine anasema, katika Zaburi 1:1-3,

1 Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio


haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala
hakuketi barazani pa wenye mizaha.

2 Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na


sheria yake huitafakari mchana na usiku.

3 Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando


ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.

Maadamu wewe ni mtoto mchanga katika kuelewa


mambo ya kiroho, huwezi kufurahia manufaa yote ya kile

45
Kristo amekupa au kukufanyia. Hivyo, ni muhimu kwako
kufanya jitihada za kukua kiroho kwa kugeuzwa nia yako.

Urithi wetu katika Kristo...

46
JIWE LA 5

Roho Mtakatifu

Kabla ya kuzungumza juu ya urithi wetu katika Kristo,


ni muhimu kwetu kujadili japo kwa ufupi nafsi ya tatu ya
Uungu, Roho Mtakatifu.

Yeye ndiye anayeshuhudia pamoja na roho zetu ya


kuwa sisi tu watoto wa Mungu

Pia, Yeye ndiye dhamana ya kupata yote yale Mungu


aliyowaahidia watu wake. Imeandikwa: "Ndiye aliye arabuni
ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa
ya utukufu wake" (Waefeso 1:14).

ROHO MTAKATIFU

Roho Mtakatifu sio moshi, nguvu, msisimko, ubaridi


au moto, msukumo au wingu fulani, wala Yeye si njiwa. Yeye
si kitu; Yeye ni Mungu.

Roho Mtakatifu ni Nafsi ya tatu ya Uungu. Yeye ni


Mungu; ni Roho wa Mungu. Yeye sio mdogo kwa Baba au Yesu;
Yeye ni mmoja pamoja nao.

Roho Mtakatifu amefunuliwa kwenye kitabu cha


Mwanzo kama mtendaji wa kazi za Uungu; anatenda kazi hizo
hata sasa.

47
ROHO MTAKATIFU NI NANI?

Ni nani mwingine angeweza kumtambulisha Roho


Mtakatifu vizuri zaidi kuliko Yesu Kristo, Bwana wetu?

Katika vitabu vya injili, anamtambulisha Roho


Mtakatifu kwa wanafunzi wake kabla ya kifo chake na baada
ya kufufuka kwake.

• Ni Msaidizi Mwingine

Yohana 14:15-17 inasema, "Mkinipenda, mtazishika


amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa
Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho
wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa
kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi
mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani
yenu."

Jinsi Yesu alivyo, ndivyo Roho alivyo. Yesu alikua


msaidizi, ndivyo Roho alivyo msaidizi kwetu. Yeye ni Roho wa
Kristo; ni Yesu asiye na mipaka katika utendaji wake.

• Ni Mwalimu na Mkumbushaji wetu

Yohana 14:26 inasema, "Lakini huyo Msaidizi, huyo


Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu,
atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote
niliyowaambia."

48
• Ni Shahidi wa Yesu

Yohana 15:26 inasema, "Lakini ajapo huyo Msaidizi,


nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli
atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia."

• Ni Kiongozi katika Kweli

Yohana 16:7-13 inasema, "Lakini yeye atakapokuja,


huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli
yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe,
lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo
atawapasha habari yake."

ZAIDI KUHUSU MSAIDIZI

Neno ‘msaidizi’ limetumika mara nyingi kumuelezea


Roho Mtakatifu. Ni neno linalotokana na Neno la kiyunani,
‘parakletos’ lenye maana ya yule anayeenda pamoja na wewe
(anayetembea pamoja nawe).

Tafsiri ya Amplified Classic Bible katika mstari wa 26


wa kitabu cha Yohana sura ya 14 inasema, “Lakini huyo
Mfariji (Mshauri, Msaidizi, Mwombezi, Mtetezi, Mtia nguvu,
mkamilishaji), huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba
atampeleka kwa jina langu [katika nafasi yangu,
kuniwakilisha na kutenda kwa niaba yangu],

49
atawafundisha mambo yote. Naye atawakumbusheni yote
niliyowaambia."

Katika tafsiri hii ya AMPC tunapata ufafanuzi mpana


zaidi kumhusu Roho Mtakatifu. Neno la kiyunani ‘parakletos’
limefafanuliwa katika maana saba, kama nitakavyozielezea
kwa ufupi hapo chini.

1. MSAIDIZI WAKO

Roho Mtakatifu ni uhakikisho wa msaada wako. Roho


Mtakatifu huweza kukusaidia mwenyewe ama kumtumia mtu
yeyote kukusaidia.

"Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na


vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema,
Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata
twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa;
Mwanadamu atanitenda nini?" (Waebrania 13:5-6).

2. MFARIJI

Anatoa faraja, furaha, tumaini, na amani; hutufanya


upya na kutuburudisha pale tuchokapo.

"Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu


Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote; atufarijiye
katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio
katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa
na Mungu. Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo

50
yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa njia
ya Kristo." (2 Wakorintho 1:3-5)

3. MSHAURI

Anajua mambo yote; ni mshauri mzuri. Ushauri wake


wapita hekima zote za kibinadamu.

Mara nyingi ametushauri, na kwa kutokumjua wengi


wameishia kusema: nilipokua kwenye changamoto nilipata
wazo fulani, nilipata machale, nilisikia uzito fulani moyoni au
nilisikia kitu kinaniambia

Imeandikwa, "Nitakufundisha na kukuonyesha njia


utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama"
(Zaburi 32:8). Hii ni kazi ya Roho Mtakatifu.

4. MTETEZI

Yeye ni mtetezi wako mahali unapoonewa.


Anasimama kukutetea na sio kukuhukumu; wanadamu
wanaweza wakakuhukumu na kukuchoka; Roho Mtakatifu ni
mtetezi wako, hatakuacha milele.

Yeye ndiye mtetezi wetu. Anatulinda sisi na sio


mshtaki wetu.

"Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa


kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu,
na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini

51
mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu
wetu, mchana na usiku" (Ufunuo 12:10).

Tunaposhitakiwa na Ibilisi, Roho Mtakatifu hututetea.

5. MWOMBEZI

Anatuombea kupitia watu; haombi Yeye kama Yeye


bali humtumia mwamini mmoja kumwombea mwingine
kupitia kunena kwa lugha.

"Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa


maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho
mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.
Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa
kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu."
(Warumi 8:26-27)

6. MTIA NGUVU

Huwezi ukawa dhaifu ukielewa namna ya kushirikiana


naye katika kazi Yake, maana yeye ndiye atutiaye nguvu pale
tunapochoka.

"Kwa hiyo nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina


lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa,
awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake,
kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika
utu wa ndani." (Waefeso 3:14-16)

52
7. MKAMILISHAJI WETU

Hataacha tuishie njiani, mahali tunapokwama Yeye


hutuhuisha upya. Yeye huwa karibu nasi kutupa msaada
wakati wa uhitaji.

"Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi


mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema.
Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu
asemaye ndani yenu." (Mathayo 10:19-20)

USHIRIKA WA ROHO MTAKATIFU

"Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu,


na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote."

2 Wakorintho 13:14

Ili uone utendaji wote huo wa Roho Mtakatifu


maishani mwako ni lazima ujifunze kutembea katika ushirika
Naye.

Ili kuwa na ushirika Naye unapaswa,

- Kumfahamu na kumtambua kwenye kila ufanyalo

- Kuzungumza Naye mara kwa mara

- Jifunze kuisikia sauti Yake

53
- Shiriki pamoja Naye katika maombi na kujifunza Neno la
Mungu

Haya ni machache sana katika mengi kumhusu


Roho Mtakatifu. Jifunze zaidi kumhusu kwa kusoma
vitabu na kusikiliza mafundisho yanayomhusu.

54
JIWE LA 6

Urithi wetu katika Kristo

"Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya


kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu
warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo;
naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa
pamoja naye"

Warumi 8:16-17

Unapofanyika mtoto wa Mungu, huhisi au kupata


ushahidi wowote wa kimwili; bali ushuhuda wa Roho
Mtakatifu rohoni mwako. Kuna uhakika katika roho ya kila
mtu ambaye amezaliwa mara ya pili, kwamba yeye ni mtoto
wa Mungu; hakika hii ni kwa Roho Mtakatifu, kwa maana
yeye hushuhudia pamoja na roho zetu.

Kuwa mtoto wa Mungu peke yake, ni jambo KUBWA.


Ndiyo maana Mtume Yohana anashangazwa na upendo wa
Baba, Anasema, “Tazameni, ni pendo la namna gani
alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo
tulivyo…” (1 Yohana 3:1). Ni sifa ya ajabu ya upendo wa Baba
kwetu. Alitupa haki ya kuwa watoto wake.

Lakini, si tu kwamba Mungu alitufanya kuwa watoto


wake, alitufanya warithi; warithi wake, warithio pamoja na
Kristo. Biblia inasema, "na kama tu watoto, basi, tu warithi;
warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam,

55
tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja
naye" (Warumi 8:17).

WARITHI PAMOJA NA KRISTO

Akiwa bado duniani, Yesu alituonyesha ina maana


gani kuwa mtoto wa Mungu, wakati huo huo alionyesha ni
nini kuwa mrithi, mnufaika wa urithi.

Alifikiri, alizungumza, alitembea na kuishi kama


mrithi wa Mungu. Alikuwa anatawala kila kitu duniani; vitu
vyote vilivyo hai na visivyo hai, vinavyoonekana na
visivyoonekana, vya kiroho na vya kimwili vilimwitikia na
kumtii.

Angalia kauli hizi alizotoa.

Moja, "Maana kama vile Baba alivyo na uzima


nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na
uzima nafsi yake" (Yohana 5:26).

Alikuwa na uhakika wa kufanana kwake kwa asili na


uzima na Babaye, kwa sababu alikuwa mtoto wa Mungu. Hii
pia ni kweli kwetu, kwani sisi ni wa asili na uzima sawa na
Mungu; sisi ni watoto wa Mungu.

Mbili, "Na yote aliyonayo Baba ni yangu; kwa hiyo


nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na
kuwapasheni habari" (Yohana 16:15).

56
Ni kauli ya ujasiri iliyoje! Kauli ya mtu ambaye ana
uhakika na ufahamu kamili wa kile anachosema. Anasema,
"YOTE ALIYO NAYO BABA NI YANGU".

Basi, ikiwa sisi ni warithi wa Mungu, warithio pamoja


na Kristo; basi yote aliyonayo Baba ni yetu. Maana yake, dunia
yote na ukamilifu wake ni mali yetu kwa urithi: dhahabu,
almasi, ardhi, nyumba, mashamba, vyanzo vya maji, nyota,
sayari na vyote ni vyetu.

Kila kilicho cha Mungu ni chetu kwa urithi. Hii ni


kubwa sana kwa akili zetu za kibinadamu! Inaweza tu
kueleweka kwa ufunuo wa Roho Mtakatifu.

URITHI WETU NI NINI?

- Ni vyote alivyonavyo Mungu, Baba.

Mrithi ana haki ya kuwa na kile alichonacho baba yake.


Kwa hiyo, urithi wetu ni yote aliyo nayo Mungu, Baba yetu.

Biblia inasema,

"Basi, mtu ye yote na asijisifie wanadamu. Kwa


maana vyote ni vyenu; kwamba ni Paulo, au Apolo, au Kefa;
au dunia, au uzima, au mauti; au vile vilivyopo sasa, au vile
vitakavyokuwapo; vyote ni vyenu; nanyi ni wa Kristo, na
Kristo ni wa Mungu" (1 Wakorintho 3:21-23).

2 Petro 1:3 inasema, "Kwa kuwa uweza wake wa


Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa,

57
kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema
wake mwenyewe."

SI KWA MATENDO

Urithi wetu si kwa matendo yetu mazuri, ni kwa


sababu ya kuzaliwa kwetu upya. Tulifanywa warithi pale
alipotuzaa mara ya pili kwa Neno na Roho Mtakatifu.

Ilihitaji tu kuamini na kupokea Ubwana wa Yesu


maishani mwetu, ili tuwe warithi wa Mungu.

URITHI WAKO

Ni muhimu kufahamu hili, kuwa mrithi na kumiliki


urithi wako ni mambo mawili yenye michakato tofauti. Kuwa
mrithi inahitaji uzaliwe tu kwenye familia; kumiliki urithi
wako kuna mchakato wake pia.

Kama ilivyo kwa wazazi wa duniani, huwapa watoto


wao urithi wanapofikia kiwango fulani cha ukomavu; ndivyo
ilivyo pia kwa Mungu.

Biblia inasema, "Basi, nasema hivi: Mrithi, akiwa


bado mtoto, hawi tofauti na mtumwa ingawaje mali yote ni
yake. Wakati huo wote yuko chini ya walezi na wadhamini
mpaka wakati ule uliowekwa na baba yake' (Wagalatia 4:1-
2 BHN).

58
Wakati ule uliowekwa na Baba, haufungwi kwenye
muda wa kibinadamu bali umefungwa kwenye ukuaji wa
mtoto. Mtoto akifikia kiwango fulani cha ukomavu anaweza
kuaminiwa na kupewa kiwango fulani cha urithi. Lakini,
wakati wote mrithi awapo mtoto hana tofauti na mtumwa
ingawaje mali yote ni yake.

Ni muhimu sana kwako mwana wa Mungu kukua kila


siku; kila hatua unayopiga katika ukuaji wako inakufungulia
mlango wa umiliki wa urithi wako.

JINSI YA KUBADILISHA URITHI WAKO KUWA


MILKI YAKO

1. UFAHAMU

Kujua ni kumiliki. Huwezi kumiliki usichokijua. Hili ni


la msingi, linaanza na ufahamu wako wa wewe ni nani katika
Mungu, na fursa ulizo nazo ndani Yake.

Katika Waefeso 1:17-18, Roho Mtakatifu anatuonyesha


kwamba tunahitaji kutiwa nuru katika macho ya mioyo yetu
ili tufurahie urithi wetu: "Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo,
Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo
katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru,
mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa
utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo"

Pia, katika Matendo 20:32, "Basi, sasa nawaweka


katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake,

59
ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao
wote waliotakaswa." Ufunuo wa Neno, kupitia ufahamu
hukupa urithi.

2. UKIRI WA IMANI

Baada ya kusoma Neno na kugundua urithi wako


katika Kristo, unaumiliki kwa maneno yako yaliyojaa imani.

Kwa mfano, Biblia inasema waziwazi kuwa, “kwa


kupigwa kwake mliponywa”; kwa hiyo ugonjwa
unaposhambulia mwili wako, unapaswa kuitikia kwa maneno
yaliyojaa imani. Unasema, “Katika jina la Yesu Kristo,
ninakataa kuwa mgonjwa, haipatani na urithi wangu nilio nao
katika Kristo. Afya ni yangu, na uzima ni wangu kwa Jina la
Yesu Kristo.”

3. POKEA KWA SHUKURANI

Urithi tayari umetolewa, lazima upokewe; sio


kuombewa, kulipiwa au kufanyiwa kazi. Tunaupokea kwa
imani, kwa kushukuru.

Wakolosai 1:12-13 inasema, "mkimshukuru Baba,


aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu
katika nuru. Naye alituokoa katika nguvu za giza,
akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa
pendo lake."

60
#UNASEMA

Baba mpendwa asante, neema ni yangu, afya ni yangu, furaha


ni yangu, utajiri ni wangu. Ninaongezeka, ninainuka,
ninaangaza kwa Jina la Yesu Kristo.

61
JIWE LA 7

Kusudi la Mungu Kwetu

Mungu wetu ni Mungu wa kusudi. Anauona mwisho


wa jambo wakati anaanza. Kulikuwa na kusudi la kuumbwa
kwa mwanadamu wa asili; kuna kusudi la uumbaji wa kiumbe
kipya.

Maisha huwa na maana pale mtu anapojinyenyekeza


ili kutimiza kusudi la Mungu. Safari ya maisha huanza kwa
kugundua kusudi la Mungu, na kisha huendelea kwa
kulitimiza.

Mungu alikuwa na kusudi la jumla kwa Adamu na


uzao wake. Pia, kuna kusudi kwa uzao mpya ndani ya Kristo.

KWA ADAMU NA UZAO WAKE

Mungu alipomuumba Adamu na kumweka bustanini,


alieleza kusudi lake: "Mungu akasema, Na tumfanye mtu
kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa
baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote
pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.
Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa
Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke
aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia,
Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale

62
samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe
chenye uhai kiendacho juu ya nchi" (Mwanzo 1:26-28).

Mungu alikuwa na mpango; mpango wake ulimweka


mwanadamu kuwa msimamizi wa vyote alivyoviumba.
Alimpa utawala juu ya samaki wa baharini, na ndege wa
angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye
kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mwanadamu akawa
kiumbe bora zaidi aliyeumbwa na Mungu, mwenye sura na
mfano ule ule wa Mungu.

Lakini mwanadamu alipoteza nafasi yake alipomkosea


Mungu. Nafasi inapopotea, kusudi haliwezi kutimia kwa
urahisi. Mamlaka aliyokuwa nayo mwanadamu yalipotea kwa
shetani. Ibilisi akawa mungu wa dunia hii, si kwa mamlaka
yake bali mamlaka ambayo Adamu alipoteza.

Lakini Mungu alikuwa na mpango wa urejesho.


Alikuwa na Yesu akilini, Adamu wa mwisho (1 Wakorintho
15:45). Kupitia Yeye, angeanzisha uzao wa viumbe wapya,
ndani ya Kristo.

Ndivyo Paulo anaandika: "Hata imekuwa, mtu akiwa


ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita
tazama! Yamekuwa mapya" ( 2 Wakorintho 5:17 ).

Kiumbe kipya ana kusudi bora zaidi. Haleluya!

63
KWA KIUMBE KIPYA

Biblia inasema,"Nasi twajua ya kuwa katika mambo


yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao
katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa
kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili,
aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa
Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni
mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao
akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na
wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza" (Warumi 8:28-
30),

Mstari wa 28, anasema, "Maana wale aliowajua


tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na
mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza
miongoni mwa ndugu wengi." Kisha, inaendelea mstari wa
29 kusema, "Na wale aliowachagua tangu asili, hao
akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na
wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza."

Mungu alituchagua, akatuita, akatuhesabia haki kwa


kusudi la kututukuza. Mwisho ni kututukuza. BIBLIA YA
AMPLIFIED inaeleza zaidi, “...Akawatukuza [akiwainua
kwenye hadhi ya mbinguni].” Haleluya! Tumeinuliwa katika
hadhi ya mbinguni.

Bwana wetu Yesu, katika maombi yake katika Yohana


sura ya 17 mstari wa 22, alisema: "Nami utukufu ule ulionipa
nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja."

64
Kiumbe kipya anapaswa kuishi maisha yaliyojaa
utukufu. Ili Mungu atukuzwe kwa maisha hayo.

“Kusudi letu ni kumtukuza Mungu kwa maisha yetu.


Tuliumbwa kwa utukufu wa Mungu”

Utukufu ni nini?

Utukufu wa Mungu unamaanisha, “Kila kitu Mungu


Alicho na kila kitu Alicho nacho”, hekima yake yote, nguvu,
ukuu, utajiri, uweza, mamlaka, ubora, na utakatifu wake.” (Na
Abraham John, Mwanzilishi wa Maximum Impact
Ministries)

Tumeumbwa ili kuonyesha jinsi Alivyo, na vile


Alivyonavyo. Tunapaswa kuonyesha hekima, nguvu, ukuu,
utajiri, uweza, mamlaka, ubora, utakatifu na haki Yake kwa
maisha yetu mbele za watu wote.

Kumbuka Maneno ya Yesu katika Mathayo 5:14-16,


Alisema, "Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi
kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa
na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo
yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru
yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona
MATENDO YENU MEMA, WAMTUKUZE Baba yenu aliye
mbinguni" (Mathayo 5:14-16).

65
Tunapaswa kumpa Mungu utukufu kwa maisha yetu,
kwa matendo yetu mema.

NURU ni matendo yetu mema. Matendo mema ya afya,


utoaji, mafanikio, ustawi, amani, furaha, upendo, haki na
utakatifu wa kweli.

Mungu hatukuzwi katika dhambi, umaskini,


magonjwa, udhaifu, maumivu, mateso, kushindwa na mambo
mengine yanayofanana na hayo. Mungu hatukuzwi katika
mambo mabaya; kwa sababu ubaya haumuelezei jinsi Alivyo
au vile Alivyo navyo. Mungu wetu ni Mungu mwema; tunaishi
kuonyesha wema wake mbele za watu wote.

Mungu hutukuzwa kwa mafanikio yetu, ustawi, ukuaji,


ushindi, ripoti nzuri, matokeo chanya, furaha, shangwe na
maongezeko tuliyonayo.

Jinsi Petro, Mtume anaelezea jambo hili, "Bali ninyi ni


mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa
milki ya Mungu, MPATE KUZITANGAZA FADHILI zake
yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya
ajabu" (1 Petro 2:9).

Sisi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu,


na watu wa milki ya Mungu, kwa kusudi hili: kutangaza fadhili
zake yeye aliyetuita tutoke gizani tuingie katika nuru yake ya
ajabu.

66
BIBLIA YA AMPLIFIED inatoa mwanga zaidi juu ya
hili: "Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa
lililowekwa wakfu, mlionunuliwa na Mungu, watu wa pekee,
mpate kuzitangaza kazi za ajabu, mpate kuonyesha wema
na ukamilifu wake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie
katika nuru yake ya ajabu" (1 Petro 2:9).

JINSI YA KUISHI MAISHA YA AINA HII

Kwanza, ruhusu na itie moyo huduma ya Roho


Mtakatifu ndani yako. Roho Mtakatifu ndiye anayeyapamba
maisha yetu; Anayapa maisha yetu rangi nzuri na za kuvutia.

Biblia inasema, "Kwa maana ndiye Mungu atendaye


kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa
kulitimiza kusudi lake jema" (Wafilipi 2:13).

Pili, jisalimishe kwa Neno la Mungu. Jifunze Neno,


litafakari na liweke moyoni mwako na kisha litendee kazi.
Kuwa na fanya yote ambayo Neno linasema juu yako. Neno
limejaa utukufu, litayapa maisha yako utukufu.

2 Wakorintho 3:18, "Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa


utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo,
tunabadilishwa tufanane na mfano huo huo, toka utukufu
hata utukufu, kama vile utukufu utokao kwa Bwana, aliye
Roho."

67
Tunapoendelea kulitazama Neno la Mungu, kama
katika kioo, tunabadilishwa tufanane na sura ile ile kutoka
utukufu hadi utukufu, kama vile kwa Roho wa Bwana.

Hakuna aliyejitoa kikamilifu kwa Neno la Mungu


aliyebaki vile vile. Utukufu na uzuri wa Mungu lazima
uonekane maishani mwake.

Ishi kutimiza kusudi la Mungu. Mtukuze Mungu kwa


maisha yako; ruhusu nuru yako iangaze mbele ya watu wote,
wayaone matendo yako mema, wamtukuze Baba yako aliye
mbinguni.

68
JIWE LA 8

Nafasi Yetu Kwa Mungu

Nafasi yako huamua mamlaka yako. Cheo chako


huamua ushawishi wako wenye kuleta mabadiliko. Kwa
mfano, nafasi ya urais ndiyo huamua mamlaka na ushawishi
alionao rais katika taifa.

Ni muhimu kuelewa nafasi yako katika Mungu kabla


ya kutenda kazi. Biblia inatangaza kwamba Mungu alitupa
nafasi katika Kristo; ndani yake tumeketi mkono wa kuume
wa Mungu Baba, juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka,
na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, si katika
ulimwengu huu tu, bali na ule ujao pia (Waefeso 1:21).

Pia, alitufanya kuwa Wafalme na Makuhani, ili


tumiliki juu ya nchi. "Hata alipokitwaa kile kitabu, hao
wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne
wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao ana
kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo
ni maombi ya watakatifu. Nao waimba wimbo mpya
wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na
kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa,
ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila
na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na
makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi"
(Ufunuo 5:8-10).

69
Mpango wa Mungu kwa mwanadamu ulikuwa, na
bado ni kutawala juu ya dunia: samaki wa baharini, na ndege
wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye
kutambaaa kitambaacho juu ya nchi ( Mwanzo 1:26).

Lakini, Adamu alipofanya dhambi, Alipoteza mamlaka


yake kwa Shetani. Kila kitu kiliingizwa kwenye hali ya utumwa
na uharibifu. Mpaka sasa viumbe bado viko katika utumwa
vikingojea udhihirisho wa Wana wa Mungu.

"Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa


shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu. Kwa
maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa
hiari yake, ila kwa sababu yake yeye atiyevitiisha katika
tumaini; kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa
huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie
katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu" (Warumi
8:19-21).

Hakukuwa na ubatili katika chochote alichoumba


Mungu. Uumbaji wote wa Mungu ulikusudiwa uishi milele,
katika uhuru mtukufu wa Mungu. Mwanadamu (Adamu)
aliwekwa kuwa msimamizi juu ya viumbe vyote vya Mungu;
baada ya kupoteza mamlaka yake kwa shetani, shetani akawa
kama mungu kwa kila kitu kilichowekwa chini ya
mwanadamu. Tangu wakati huo, viumbe vyote viliwekwa
chini ya utumwa, vikaingizwa katika hali ya kuharibika.

70
DHAMBI - MAUTI

Biblia inasema, "Kwa maana mshahara wa dhambi


ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika
Kristo Yesu Bwana wetu" (Warumi 6:23). Baada ya dhambi
kuingia duniani, kifo kilitawala viumbe vyote.

"Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti


ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao
wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki,
watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo"
(Warumi 5:17).

Asante Mungu kwa ajili ya Yesu Kristo!


Tumekombolewa kutoka kwenye utawala wa kifo.

Baada ya anguko, mwanadamu na vitu vyote vilikuwa


chini ya utawala wa kifo: shetani katika utendaji wa kifo.
Utawala wa mauti ulileta uharibifu kwenye kila kitu: ndiyo
sababu vitu vinaisha (vinazeeka), ndoa zinakufa, biashara
zinafirisika na kufungwa, umasikini na magonjwa vinazuia
hatma za wengi.

Kuna hisia ya kifo katika kila kitu ambacho bado


hakijakombolewa. Hii ndiyo sababu ya vitu kutokudumu.
Lakini, Mungu alikusudia kila kitu alichokiumba kidumu.

71
TUNATAWALA

"…zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile


kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule
mmoja, Yesu Kristo"

Warumi 5:17

SASA, tuko kwenye kiti cha utawala pamoja na Yesu


Kristo. Badala ya kifo, tuna neema na haki ya kutawala katika
uzima kwa mmoja, Yesu Kristo.

Bwana alituambia tuhubiri injili kwa kila kiumbe


(Marko 16:15). Injili ni ujumbe wa uzima; huwapa uhai wote
wanaoupokea. Kwa njia ya injili viumbe vyote vinakombolewa.
Kwa imani katika injili: wagonjwa wanaponywa, maskini
wanatajirika, wanyonge wanaimarishwa, ndoa
zinathibitishwa kwa upendo, biashara zinakua na kuongezeka
na vitu vinadumu.

Mtoto wa Mungu, unao uzima wa Mungu ndani yako.


Vuvia uzima kwa vyote vinavyokuhusu kwa kunena Neno la
Mungu juu yao. Zungumza Neno juu ya huduma yako, fedha
zako, watoto wako, biashara yako, shamba lako, elimu yako,
ndoa yako na kazi yako, navyo vitawekwa huru.

72
MUHTASARI

NAMNA YA KUTAWALA MAISHANI

1. KUELEWA NAFASI YAKO KWA MUNGU

Biblia inasema, "Akatufufua pamoja naye,


akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho,
katika Kristo Yesu" (Waefeso 2:6).

Hapa ndipo tulipoketi, "... mkono wake (Mungu) wa


kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme
wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina
litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao
pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe
kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo
mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote
katika vyote" (Waefeso 1:20-23).

2. TUMIA MANENO

Kuwa mwangalifu kwa kile unachozungumza, kwa


sababu kile unachosema kitaathiri hali ya maisha yako.

USIZUNGUMZE kifo, kushindwa, magonjwa,


mahangaiko, kushindwa, kukosa, na mambo mengine yote
usiyopenda kuyaona maishani mwako.

Ongea tu kile unachotaka kuona,"Kwa kuwa neno la


mfalme lina nguvu; naye ni nani awezaye kumwambia huyo,
Wafanya nini?” (Mhubiri 8:4).

73
3. TUMIA JINA LA YESU

Wote walio ndani ya Kristo, tumepewa haki ya kufanya


kazi kwa Jina la Yesu; tunatenda kwa niaba yake hapa duniani.

Unapotumia Jina la Yesu, unafanya kazi kwa mamlaka


yake. Yesu alisema, "... Nimepewa mamlaka yote mbinguni
na duniani" (Mathayo 28:18).

Jina la Yesu liko juu ya Majina yote katika nyanja zote


tatu: mbinguni, duniani na chini ya dunia: "Kwa hiyo tena
Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo
kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya
mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi
ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa
Mungu Baba" (Wafilipi 2:9-11).

74
JIWE LA 9

Mwenendo wa Imani

Ukristo ni maisha ya imani. UKRISTO NI IMANI.

Tunaanza kwa imani, na kuendelea katika imani.


Tunakua katika imani; tunafanya mambo yote kwa njia ya
imani: iwe maombi, sifa, ibada, au utoaji wetu kwa Bwana.

Mungu ni Roho. Sisi pia, ni roho katika miili ya


wanadamu; ili tuweze kuunganishwa na kuwasiliana na
Mungu ambaye ni Roho, ni lazima tutumie imani. Imani ni
kiunganishi kati ya ulimwengu wa mwili na ule wa roho;
ulimwengu unaonekana na ule usioonekana.

Kama Wakristo, maisha ya imani ndiyo namna yetu


mpya ya kuishi. Hatuishi tena kulingana na maagizo ya mwili
(hisia), lakini roho. Kuishi katika roho ni kuishi kwa imani;
kwa maana imani ni bayana ya mambo yasiyoonekana.

MWENENDO WA IMANI

"Lakini MWENENDO wenu na uwe kama INAVYOIPASA


INJILI YA KRISTO, ili, nikija na kuwaona ninyi, au
nisipokuwapo, niyasikie mambo yenu, kama mnasimama
imara katika roho moja, kwa moyo mmoja
MKIISHINDANIA IMANI YA INJILI"

Wafilipi 1:27

75
Kama wakristo, tuna namna yetu ya kuishi; sio kama
Ulimwengu. Biblia inatangaza wazi kwamba kuenenda kwetu
ni kwa imani; kuishi katika roho.

Lakini, haiwezekani mtu kuenenda kwa imani


asipolijua Neno la Mungu; kwa maana imani ya Kikristo huja
tu kwa Neno la Mungu.

IMANI NA NENO

"Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa


neno la Kristo"

Warumi 10:17

Wakati wengine wanategemea mapokeo na uzoefu


mwingine wa kibinadamu kama chanzo chao cha imani; imani
ya kweli ya Kikristo huja tu kwa Neno, si vyanzo vingine
vyovyote.

Tunamshukuru Mungu kwa Neno! Ni mwongozo wetu


wa maisha. Inatuonyesha sisi ni nani kama Wakristo, jinsi
tunavyopaswa kuishi maisha yetu, na Mungu wetu ni nani
hasa.

Neno la Mungu ni hitaji la lazima kwa maisha ya


Mkristo. Kama vile isivyowezekana mtu kuishi bila chakula,
haiwezekani kuishi maisha ya kiroho (maisha ya kikristo) bila
Neno la Mungu. Yesu, Bwana wetu alitangaza:
"...Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila
neno litokalo katika kinywa cha Mungu" ( Mathayo 4:4 ).

76
Uzima unatoka kwa Mungu, na Mungu ameweka
uzima huo katika Neno Lake. Unapolichukulia Neno la
Mungu kwa uzito, maisha yako yanageuka kuwa ya utukufu.

MAANDIKO

"Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa


mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa
kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa
Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila
tendo jema."

2 Timotheo 3:16-17

Maandiko yote yameandikwa chini ya uvuvio wa Roho


Mtakatifu kwa kusudi la kutufanya wakamilifu,
tuliokamilishwa katika matendo yote mema. Neno peke yake
lina uwezo wa kukufanya kuwa mkamilifu, ikiwa unajitoa
kikamilifu kwake.

Biblia ni kifaa cha Mungu, chenye manufaa na faida


kwa mafundisho, maonyo, maongozi, na mafunzo ya
kimaadili. Faida zote hizi nne zinapaswa kuchukuliwa kutoka
kwenye Neno, lakini wengine hutumia Neno pale tu
linapojibu uhitaji wao.

Wengine hujifunza Neno ili kupata maelekezo tu,


lakini pale Biblia inapowaonya makosa yao hawataki kusikia.
Wengine hutaka mafundisho ya aina fulani kwenye Biblia kwa
sababu ya uhitaji walionao wakati huo, lakini Biblia

77
imekusudiwa kukukamilisha katika nyanja zote. Kipimo
kimoja hakiwezi kukukamilisha.

Unaposoma Neno la Mungu kuwa tayari kwa ajili ya


mafundisho, maonyo ya makosa, maongozi na kuadabishwa
katika haki.

Kumbuka hili: Hatusomi maandiko ili tu kuchukua


kile tunachotaka kwa manufaa yetu ya kimwili. Tunasoma ili
kupokea maagizo kutoka kwa Bwana: yeye ni Bwana,
anatuamuru kufanya kile anachotaka kwa ajili yetu.

Kila siku uliyonayo katika ulimwengu huu mzuri,


tenga muda fulani wa kujifunza Neno la Mungu. Fanya
kusoma na kutafakari Neno kuwa mtindo wa maisha, sio tukio
linalotokea wakati wa uhitaji. Hii itakusaidia kukuza imani
yako.

Kwa waamini wapya: Usomaji wa Biblia ndio


unaokuza imani yako na kukupa ukomavu kama mkristo.
"Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini
maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kukulia
wokovu" (1 Petro 2:2).

Kutembea ndani ya na kuishi kwa Neno ni mwenendo


wetu mpya wa maisha (kutembea kwa imani).

78
KAZI YA IMANI

"Maana twaenenda kwa imani, si kwa kuona"

2 Wakorintho 5:7

NINI MAANA YA KUTEMBEA KWA IMANI?

Kama mkristo, moja ya somo la msingi la kujifunza ni


kuenenda kwa imani.

Mtoto anapozaliwa, huzaliwa akiwa na miguu kamilifu,


lakini ingawa miguu ni kamilifu, hawezi kutembea mpaka
ajizoeze kuitumia. Mkristo aliyezaliwa mara ya pili ana imani,
kwa maana hakuna anayeweza kuzaliwa mara ya pili bila
imani, lakini ili imani yake ifanye kazi inapaswa kuzoezwa.

Imani ni miguu yako ya kiroho; kadiri unavyojifunza


Neno, ndivyo inavyokua na kuongezeka; kadiri unavyolitenda
Neno la Mungu, ndivyo unavyokuwa na nguvu zaidi. Jifunze
kulitumia Neno kwa kuliweka katika matendo ili likuzalie
matokeo.

Mstari wetu wa ufunguzi katika sura hii, unatuambia


kwa maneno rahisi maana ya kutembea kwa imani. Unasema:
"Maana twaenenda kwa imani, si kwa kuona." (2
Wakorintho 5:7).

‘Si kwa kuona’ ndiyo maana ya kuenenda kwa imani.


Hatutembei kwa hisia [kile tunachoona, kugusa, kuhisi,
kusikia, kuonja au kunusa].

79
Kataa kutembea kwa yale uliyojifunza kwa hisia zako,
na jizoeze kutembea kwa maelekezo ya Roho Mtakatifu
kupitia Neno.

Kuenenda kwa imani ni mwenendo wa kikristo;


maana yake ni kutembea katika Neno ambalo ni Roho.

80
JIWE LA 10

Ukuaji wa Kiroho

Ukuaji ni moja ya sifa ya kiumbe hai. Mwanadamu


huzaliwa, hukua hatua kwa hatua hata kufikia ukomavu.
Ndivyo ilivyo kwa Mkristo, ulipompokea Yesu kama Bwana na
Mwokozi wako, ulizaliwa mara ya pili; ukawa mtoto mchanga
kiroho, anayepaswa kukua hata kufikia ukomavu.

Ukuaji ni wa muhimu sana. Hebu fikiria mama


aliyezaa mtoto ambaye haonyeshi ishara yoyote ya ukuaji; na
baada ya kama miaka minne mtoto hawezi kutembea,
kuzungumza, au kuelewa kama anavyopaswa au hata kula
vyakula fulani ambavyo mtoto wa miaka minne angekula.

Pasipo kukawia, mama huyu angechukua hatua za


haraka kumpeleka mtoto wake hospitali, ili aonane na daktari,
kwa kuwa hali ya mtoto siyo ya kawaida. Mtoto baada ya
kuzaliwa akiwa mwenye afya, anapaswa kukua. Ikiwa hakui
inavyopaswa, anapaswa kuangaliwa kwa ukaribu zaidi,
pengine ana shida kubwa inayosababisha hilo.

Cha kusikitisha, huu ni uzoefu wa Wakristo wengi.


Kuna waliookoka miaka mingi iliyopita, lakini hawakukua au
hata kusikia chochote kuhusu ukuaji na ukomavu. Na wengine
hudhani kwamba idadi ya miaka ambayo wamekuwa katika
Ukristo inaashiria ukomavu wao, lakini hiyo si kweli. Mtu
anaweza kuwa na miaka 50 katika wokovu, na bado akawa
mtoto katika mambo ya rohoni.

81
Katika Ukristo, nambari ya miaka haimaanishi kukua
au kukomaa, bali ujuzi, ufahamu, hekima, imani na uzoefu wa
kiroho humaanisha hivyo.

Niruhusu nikuambie kwa ujasiri jambo hili: ni jukumu


lako kukua kiroho; sio jukumu la Mungu wala kiongozi wako
wa kiroho. Kwa hiyo, kusudia na fanya maamuzi ya
kimakusudi ya kukua katika mambo ya rohoni.

Katika sura hii, nitashiriki nawe baadhi ya mambo


yatakayokusaidia kukua kiroho.

1. CHAKULA CHA KIROHO

Chakula ni hitaji la msingi kwa maisha ya wanyama,


kama Neno la Mungu lilivyo kwa maisha ya kiroho. Neno la
Mungu ni chakula cha kiroho. Unapoelewa hili, utalichukua
Neno la Mungu kwa uzito na umuhimu linalostahili.

Niulize tu, Unaweza kuishi kwa muda gani bila


chakula? Na nini kingetokea kwako ikiwa ungefanya hivyo? Je,
unaweza kuishi bila chakula?

Kuhusianisha mambo ya kimwili na ya kiroho: jambo


lile lile linaloweza kutokea mwilini mwako usipokula chakula,
linaweza kukutokea rohoni ukikosa Neno la Mungu. Hii ndiyo
sababu baadhi ya Wakristo ni dhaifu rohoni na hawafanyi kazi
ipasavyo, kwa sababu hawalichukulii Neno la Mungu kwa
uzito.

82
Yesu, Bwana wetu alisema hivi kuhusu Neno: “Mtu
hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika
kinywa cha Mungu" (Mathayo 4:4). Neno ni uzima kwa
Mkristo, unapojifunza Neno ndivyo unavyoishi zaidi.

Petro Mtume mkuu, kuhusu ukuaji wa kiroho


alitumiwa na Roho kuandika: "Kama watoto wachanga,
waliozaliwa sasa, yatamanini maziwa ya kiroho
yasiyochanganywa na kitu kingine chochote, ili kwa hayo
mpate kukua katika wokovu" (1 Petro 2:2 NEN).

Neno ‘yatamanini’ kwenye mstari wetu hapo juu


linatupa wajibu. Mungu amesema tutamani na kuwa na njaa
ya Neno, kama vile mtoto mchanga aonavyo njaa ya maziwa
ya mama yake. Tamaa ya Neno haiji yenyewe tu,
unailazimisha kimakusudi itokee. Ikiwa huna njaa ya Neno
(maziwa ya akili), Mungu hatakulazimisha kusoma.

Ukitaka kukua kiroho, Neno ni la msingi na mahali


pako pa kuanzia kwa ukuaji na ukomavu wako.

2. MAZOEZI YA KIROHO

Baada ya kusoma Neno, ni muhimu kwako kulifanyia


kazi. Hebu fikiria mtu ambaye anakula tu bila kufanya
mazoezi; atakua mkubwa tu asiye na nguvu wala uimara
wowote.

Ukijifunza Neno la Mungu tu bila kulifanyia kazi,


utakuwa mwenye maarifa mengi, ila asiye na matokeo ya

83
kuonyesha. Hili si zuri hata kidogo: kujua kitu bila kuwa na
nguvu ya kukidhihirisha. Hii ndiyo sababu Yakobo alisema,
“Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali
mkijidanganya nafsi zenu” (Yakobo 1:22). Unajidanganya
nafsi yako pale unapokuwa msikilizaji wa Neno asiye mtendaji
wa kile amesikia.

Bwana Yesu alifafanua hili kwa ukali zaidi. Alisema,


"Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye,
atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake
juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo
zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko
lake likawa kubwa" (Mathayo 7:26-27).

Kuhusu mtendaji wa Neno, Alisema: "Basi kila


asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa
na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya
mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo
zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana
misingi yake imewekwa juu ya mwamba" (Mathayo 7:24-
25).

Biblia ni mwongozo wa mafundisho; kitabu cha


mwongozo wa vitendo, kitabu cha kufanya ili uishi; si kitabu
cha hadithi.

Ukuaji wa kiroho unategemea jinsi unavyofanyia kazi


kweli za kiroho. "Bali hadithi za kizee, zisizokuwa za dini,
uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa. Kwa maana
kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini
utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya

84
uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye" (1
Timotheo 4:7).

Utauwa unaweza kufafanuliwa kama ‘maisha ya


nidhamu’ au ‘mazoezi ya kiroho’.

Jifunze zaidi:
2 Timotheo 3:16-17, Waebrania 5:12-14

3. MAOMBI

Maombi ni mazoezi ya Kiroho. Kama nilivyoandika


huko nyuma, kwa anayetaka kuwa na afya njema, ni muhimu
kwake kula na kufanya mazoezi.

Maombi ni fursa kubwa tuliyopewa na Mungu. Ni


mahali petu pa kuwasiliana na Mungu; mahali pa kumjua na
kuunganishwa Naye zaidi katika ushirika na Roho wake. Pia,
ni mahali ambapo tunadhihirisha imani yetu. Na, kupitia
zoezi hili tunakuza imani zetu na kuzifanya kuwa imara.

Kuhusu ukuaji wa kiroho, kunena kwa lugha ni kweli


iliyothibitishwa ambayo hutusaidia kukua na kujengwa zaidi
katika utu wa ndani.

1 Wakorintho 14:4, "Yeye anenaye kwa lugha


hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa."

85
Yuda 1:20, "Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya
imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho
Mtakatifu"

Ikiwa unasoma kitabu hiki, na bado hujaweza kunena


kwa lugha, unaweza kumwomba Mungu akupe zawadi hiyo ya
thamani, au nenda kwa Mchungaji wako au mtumishi wa
Mungu yeyote wa kweli na umwombe akuombee. Ni muhimu
sana kuomba katika roho.

4. HUDUMA YA ROHO MTAKATIFU

Roho Mtakatifu ndiye mlezi wetu, tulikabidhiwa


kwake na Bwana Yesu mwenyewe. Ana huduma ya kutulea
hata tutakapofikia ukamilifu wetu. Kupitia huduma Yake ya
mafundisho na maongozi hutufikisha kwenye ukomavu.

Kuna mengi ya kuandika juu ya Roho Mtakatifu, lakini


nafasi na wakati haviwezi niruhusu kufanya hivyo. Lakini,
ninakutia moyo katika Jina la Yesu ujifunze zaidi juu ya Roho
Mtakatifu kupitia vitabu na mafundisho yanayomhusu.

Yohana 14:26 inasema, "Lakini huyo Msaidizi, huyo


Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu,
atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote
niliyowaambia."

Yohana 16:13 inasema, "Lakini yeye atakapokuja,


huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli
yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe,

86
lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo
atawapasha habari yake."

5. KUWA MSHIRIKA WA KANISA LA MAHALI

Hii itakuwa sura yetu inayofuata.

87
JIWE LA 11

Kuwa Mshirika wa Kanisa

"Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa


jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao"

Mathayo 18:20

Kanisa ni mwili wa Kristo—watu wote wanaokubali


zawadi ya Kristo ya wokovu na kufuata mafundisho ya Kristo.
Ni zaidi ya jengo. Katika Biblia, neno “kanisa” halimaanishi
jengo. Humaanisha watu—watu wanaomfuata Yesu Kristo.

Kanisa la Yesu Kristo ni familia yake hapa duniani. Ni


mfumo wa kimuundo ambao Mungu aliuumba kwa ajili ya
kuzaa na kulea watoto Wake hata wafikie ukomavu.

Kila mtoto anayekuja katika ulimwengu huu, anakuja


kupitia familia ya watu wawili, baba na mama. Mungu aliweka
mfumo huo ili kusaidia malezi ya mtoto. Baba na mama
humlea mtoto mpaka kufikia ukomavu wake, kwa kutumia
maarifa, uzoefu walio nao, na mifumo iliyopo [shule, vyuo na
vyuo vikuu].

Ndivyo ilivyo kwa kanisa. Kanisa ni familia ya Mungu


ambapo watoto wa Mungu hulelewa ili kuwa kila kitu
ambacho Mungu anataka wawe. Mtoto asiye na familia
huteseka kwa mambo mengi na hukosa mambo mengi katika
ukuaji wake, na hilo linaweza kuathiri jinsi atakavyokuwa

88
awapo mtu mzima. Vivyo hivyo kwa mtu ambaye si mshirika
wa kanisa lolote, anaweza kupata mateso mengi na kukosa
mema ya Mungu yaliyoandaliwa kwa ajili yake.

Baada ya kuzaliwa mara ya pili, ni muhimu na lazima


kutafuta kanisa ambapo utalelewa na kujifunza kuhusu
Ukristo.

UTARATIBU KANISANI

Waefeso 4:11-16, inasema:

11 Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine


kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine
kuwa wachungaji na waalimu;

12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata


kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;

13 hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani


na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu
mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu
wa Kristo;

14 ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku


na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila
ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.

15 Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata


tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.

89
16 Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na
kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya
utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate
kujijenga wenyewe katika upendo.

Kuna utaratibu kanisani; ni Mungu aliyeweka


utaratibu huo. Aliwaweka wengine kuwa mitume, wengine
manabii, wengine wainjilisti, wengine wachungaji na waalimu.
Hatujaitwa wote kwenye ofisi hizi; ni baadhi tu walioitwa na
kutangulia mbele ya wengine wanaowafuata.

Katika mstari wa 12, anaeleza kusudi la utaratibu wa


kanisa: “kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi
ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe"
(Waefeso 4:12).

Mungu alikusudia kanisa liwe mahali ambapo


watakatifu wake wanakamilishwa (wanakua) na kutayarishwa
kwa ajili ya kazi ya huduma, ya kulijenga kanisa. Kanisa
lazima likue na kuongezeka hapa duniani kabla Bwana wetu
hajarudi. Tumepewa sehemu ya ujenzi, na tunashiriki ujenzi
kwa kuwashirikisha wengine habari njema za wokovu.

Mstari wa 14, Anaelezea lengo la kanisa: "ili tusiwe


tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na
kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa
ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu." Na mstari wa 15,
Anamalizia: "Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua
hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo."
Ukuaji na ukomavu ndio lengo.

90
KWANINI KANISA NI MUHIMU?

1. Ukuaji wa kiroho

Kanisa ni kwa ajili ya malezi yetu. Kanisa humsaidia


mkristo kukua mpaka ukomavu kamili, ili aweze kufurahia
manufaa kamili ya Ukristo wake.

2. Uwajibikaji

Kwa kuwa, katika kanisa tunanyenyekea chini ya


mamlaka (viongozi) ambao Mungu amewaweka,
tunafundishwa kuwajibika kwa yote ambayo tumepewa
kufanya.

Biblia inasema, "Watiini wenye kuwaongoza, na


kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho
zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye
hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa
ninyi” (Waebrania 13:17),

3. Kunoa karama na wito

Kanisa ni mahali pa kunoa na kutumia vipawa


ambavyo Mungu ameweka ndani yako. Kanisa linakupa nafasi
ya kutumia karama uliyonayo, kwa kuwa vipawa na karama ni
kwa ajili ya manufaa ya Kanisa.

1 Wakorintho 14:26-27,

26 Basi, ndugu, imekuwaje? Mkutanapo pamoja, kila


mmoja ana zaburi, ana fundisho, ana ufunuo, ana lugha,
ana tafsiri. Mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga.

91
27 Kama mtu akinena kwa lugha, wanene wawili au
watatu, si zaidi, tena zamu kwa zamu, na mmoja na afasiri."

4. Uvunaji wa Nafsi

Hiki ndicho Bwana Yesu alituachia tufanye hapa


duniani. “Akawaambia, ENENDENI ulimwenguni mwote,
mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe” (Marko 16:15).

92
JIWE LA 12

Uvunaji wa Nafsi

Katika Kitabu cha Marko sura ya 16 na mstari wa 15,


Yesu Bwana wetu alilipa kanisa agizo; jambo la lazima
kufanya. Alituamuru sisi (tunaomwamini), kuihubiri Injili
kwa kila kiumbe.

“Akawaambia, ENENDENI ulimwenguni mwote,


mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe”

Marko 16:15

Haya si maagizo waliyopewa mitume, wachungaji,


manabii, waalimu na wainjilisti pekee; ni amri iliyotolewa kwa
wote wanaomwamini na watakaomwamini Yesu. Ikiwa
unamwamini Yesu, umeamriwa kuhubiri habari njema za
wokovu kwa wengine, ili nao wapate nafasi ya kuamini.

Matendo 1:8, Biblia inasema: "Lakini mtapokea


nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi
mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika
Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi."

Wewe ni shahidi wa Yesu hapa duniani. Shahidi ni mtu


aliyeona tukio, na ana ujuzi unaotokana na kutazama au kuwa
na uzoefu wa kitu husika.

93
Mara tu unapompokea Yesu kama Bwana wako, na
kuona upendo na huruma yake ni uzoefu wako wa kwanza;
mabadiliko ya maisha na mambo mengine ya ajabu
anayokufanyia hukufanya kuwa shahidi wake.

Kila mtu ambaye amekutana na Bwana anao


ushuhuda; ushuhuda huo hukupa haki ya kuwa shahidi wake.

Biblia ni kitabu chenye rekodi za shuhuda mbalimbali.


Ni hati iliyoaminika itumike katika kuhubiri Habari Njema za
Yesu Kristo: Yeye ni nani, alifanya nini na atafanya nini.

MOYO WA MUNGU

Kwenye nafsi za watu ndipo moyo wa Mungu ulipo.


Mungu "anataka watu wote waokolewe, na kupata kujua
yaliyo kweli" (1 Timotheo 2:4). Hili ni takwa lake: watu wote
waokolewe. Neema yake bado inapatikana; Alilipa gharama
kupitia kifo cha Yesu Kristo msalabani, kwa ajili ya watu wote
waliokuwepo, waliopo na watakaokuja baadaye katika
ulimwengu huu.

Wokovu wa wanadamu ni jambo muhimu sana kwa


Mungu. Ndiyo maana alilipa gharama kuu: mwanaye wa
pekee kufa kwa ajili yetu.

Kusudi la Yesu Kristo linatangazwa katika Luka 19:10:


"Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa
kile kilichopotea." Hili ni kusudi linaloendelea hata sasa. Yesu

94
alifanya sehemu yake, na mwili wake-kanisa bado linaendelea
na utume huu, kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.

Kwa nini Kanisa bado liko hapa duniani?

Sote tunakubali kwamba mbinguni ni mahali pazuri


zaidi kuliko duniani. Basi, kwa nini Mungu hatupeleki
mbinguni mara tu tunapoamini?

Ni kwa sababu bado kuna idadi kubwa ya watu ambao


hawajasikia injili ikihubiriwa kwao. Uko hapa duniani
kuhubiri injili ya Yesu Kristo kwa huyo kaka na dada aliye
karibu nawe.

Mungu ametuamini mimi na wewe kwa kazi hii kubwa.


Kila nafsi ni muhimu kwake; haijalishi mtu huyo
anaonekanaje au anatafsiriwa vipi na wengi duniani. Yesu
alisema, "Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa
ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya
wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu"
( Luka 15:7 ). Injili ni kwa ajili ya wenye dhambi.

Unaweza sema, ‘mimi sijui jinsi ya kuhubiri.


Nifanye nini?’

Ni rahisi sana kuhubiri injili. Kumbuka habari ya


mwanamke msamaria, alikutana na Yesu kisimani, naye Yesu
akamhudumia. Baada ya kuhudumiwa, hakuwa na mengi ya

95
kusema kumhusu Yesu, lakini alikuwa ameshuhudia jambo
fulani kutoka kwake.

Yohana 4:28-29, inasema;

28 Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake,


akaenda zake mjini, akawaambia watu,

29 Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote


niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?

Maneno machache tu, "Njoni, mtazame mtu


aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda" yalitosha
kushawishi mji mzima kumfuata. Hauhitaji maneno mengi ya
ushawishi kuhubiri injili, maneno machache pamoja na
utendaji wa Roho Mtakatifu yanatosha kuwaokoa watu.

Yohana 4:39-42 inaendelea kueleza,

39 Na katika mji ule Wasamaria wengi


walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke,
aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote
niliyoyatenda.

40 Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi


akae kwao; naye akakaa huko siku mbili.

41 Watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno


lake.

42 Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini,


wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi

96
tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye
Mwokozi wa ulimwengu.

Kupitia nguvu za Roho Mtakatifu, unaweza kuwavuna


wengi. Roho wa Mungu ndiye anayewashuhudia mioyoni
mwao, si maneno yako mengi au machache.

Ni muhimu ujiandae katika maombi kabla ya kwenda


kuhubiri injili, ili kuchochea utendaji wa Roho Mtakatifu, na
kuharibu vizuizi vya adui mioyoni mwa watu. Unapoomba,
injili inapata mlango wa wazi mioyoni mwa watu.

Kuwaleta watu kwa Yesu Kristo ni rahisi sana;


unaweza kufanya hivyo. Fuata Neno tu.

KUAMINI NA KUKIRI

“Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni


Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu
alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo
mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata
kupata wokovu”

Warumi 10:9-10

Kuamini na kukiri ni mahitaji mawili ya wokovu.


Hakikisha mtu huyo unayemhubiria, anaamini moyoni
mwake kufa, kuzikwa na kufufuka kwa Bwana wetu, kisha
amkiri Yesu Kristo kwa kinywa chake kama Bwana na
Mwokozi wake binafsi. Haya tu ndiyo matakwa ya Kibiblia
kwa wokovu wa wanadamu.

97
SALA YA WOKOVU

“Eh Bwana Mungu, naamini kwa moyo wangu wote katika


Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Naamini alikufa kwa
ajili yangu na Mungu alimfufua katika wafu. Naamini yu hai
leo. Ninakiri kwa kinywa changu ya kuwa Yesu Kristo ni
Bwana wa maisha yangu kuanzia leo. Kupitia Yeye na Ndani
ya Jina Lake, Ninao uzima wa milele, nimezaliwa mara ya pili.
Asante Bwana, kwa kuiokoa nafsi yangu! Sasa mimi ni mwana
wa Mungu. Haleluya!”

MTAMBULISHE KWA KANISA

Baada ya kufanya yote, msaidie mwamini mpya


kupata kanisa linalofaa ambapo atakutana na wakristo
wengine wa imani moja naye, ili aweze kukua katika mambo
ya Mungu. Ikiwezekana mpeleke kule unakoabudu wewe
mwenyewe.

Weka ahadi ya kufanya kazi hii ya Mungu ungali


duniani. Upo duniani kwa sababu hii. Utakuwa na sababu ya
kuishi mara tu unapojitoa kufanya kazi ya kuhubiri injili.

98
Hitimisho: Kuwa Makini na
Ujenzi Wako

Ujenzi ni mchakato, unahitaji uwekezaji wako wa nguvu,


muda na rasilimali. Wavivu hawajengi; wapumbavu
wanadharau msingi, wangependelea kujenga nyumba zao juu
ya mchanga. Lakini, kamwe kanuni na mifumo haiwezi
kudharauliwa au kupuuzwa, kwa kuwa ndizo huamua
matokeo yanayofuata.

Naamini umeandaliwa vyema kupitia kitabu hiki, kwa


ajili ya ujenzi wa msingi wako imara. Tayari umepokea mawe
12 ya kuweka msingi; sasa unaweza kujenga kutoka hapo hadi
maisha ya juu unayotaka katika Kristo.

KUWA MTENDAJI WA NENO

Soma maneno ya Bwana Yesu kwa makini, ni maagizo


maalum ya ujenzi. Anasema,

Mathayo 7:24-27,

24 Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na


kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga
nyumba yake juu ya mwamba;

25 mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma,


zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake
imewekwa juu ya mwamba.

99
26 Na kila asikiaye maneno yangu asifanye,
atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake
juu ya mchanga;

27 mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma,


zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa
kubwa.

Kujenga ni kutendea kazi Neno la Mungu, na si kusikia


au kusoma tu. Hekima ni kutendea kazi maarifa uliyonayo.

Naamini umepokea hekima nyingi; hujasoma tu kitabu,


utatenda pia, kwa hiyo hekima itajulikana kuwa na haki kwa
kazi zake ndani yako.

Mungu akubariki wewe, wapendwa wako na wote


utakaowashirikisha kweli hizi ulizozipata katika kitabu hiki.

Amen!

100
Kuhusu Mwandishi

D. K. Davis ndiye mwandishi wa kitabu hiki kizuri


cha Mawe 12 ya Kuweka Msingi wa Maisha ya
Mwamini; kwa neema ya Mungu ameitwa kama
mchungaji mwenye karama ya ualimu; sehemu kubwa ya
lengo lake linahusisha kuwaandaa waamini kusikia,
kujua na kumfuata Mungu katika uzoefu wao wenyewe
kila siku. Anafundisha Neema ya Mungu katika kweli, na
kuwajulisha watu wote ulimwenguni Upendo wa Kristo
upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, huku
akilidhihirisha Neno la Mungu kwa Nguvu za Roho
Mtakatifu katika ishara na miujiza.

101
HONGERA KWA KUSOMA

Kwa mawasiliano Zaidi:

Simu: 0713816586

Barua pepe: d.k.davis@harufuyauzima.org

102

You might also like