You are on page 1of 4

DOMINIKA YA 23 YA MWAKA “A” WA KANISA

Ndugu wapendwa katika Kristo, neno la Mungu tulilolisikia leo linatufungua macho juu ya
uhalisia unaotokea katika kila jumuiya ya kikristo. Ni kwa namna gani tunadili na mtu
ambaye ametukosea, ni kwa namna gani tunadili na ndugu yetu ambaye ana tabia ambazo si
za kawaida, ni kwa namna gani tunadili na mdhambi. Somo la kwanza na somo la Injili
yanatukumbusha juu ya wajibu wetu wa kumrudisha mdhambi katika njia sahihi.

Nabii Ezekiel katika somo la kwanza anatualika tuwe kama walinzi wa wenzetu, kumzingatia
mwanajumuiya mwenzetu ambaye ametukosea, ambaye amefanya kosa ambalo linaharibu
uhusiano kati ya wanajumuiya. Na lengo la kumzingatia mtu huyo si kumuhukumu, bali ni
kumrudisha tena mtu huyu kumrudisha tena katika njia sahihi.

Injili inatupatia hatua za kufuata katika kumrekebisha mwenzetu ambaye ametukosea. Injili
inatutahadharisha juu ya unafiki, kuwasema wengine pembeni. Kristo kupitia Mwinjili
Mathayo anatufundisha kumfuata mtu na kumweleza ukweli, si kumnyooshea vidole tu.

Somo la pili kutoka waraka wa mtume Paulo kwa warumi linaeleza juu ya upendo,
tunakumbushwa kuwapenda wenzetu, na sehemu ya upendo kwa ndugu zetu ni
kuwasahihisha ndugu zetu kila muda anapokosea. Na kwa kuwa upendo ni utimilifu wa
sheria, niwaalike tuutafakari Zaidi juu ya upendo ambao Kristo anauzungumzia.

Katika injili ya Yohane 13:34 tunasikia Yesu akiwapa wafuasi wake amri mpya, mpende
jirani yako kama nilivyowapenda. Hiyo ni amri mpya. Tujiulize, ni nini kipya katika amri
mpya ya mapendo? Katika agano la kale Mungu aliwaambia wasraeli, mpende jirani yako
kama unavyojipenda mwenyewe. Lakini katika amri mpya, mpende jirani yako kama mimi
nilivyowapenda. Kwamba kielelezo cha kupenda si kujipenda tena bali ni kama Yesu
alivyotupenda, kielezo cha kupenda ni Kristo mwenyewe. Kristo ambaye anatupenda pamoja
na udhaifu wetu, pamoja na udhambi wetu, pamoja na mapungufu yetu. Upendo ambao
unconditional love. Kristo msalabani anatuambia, nawapenda na nimekufa kwa ajili yenu
hata kabla ya kuja kwenye Misa hii, nawapenda na nimekufa kwa ajili yenu hata kabla ya
hujaenda katika kiti cha kitubio. Na ni upendo huu ambao Kristo anatualika kuuonesha kwa
wenzetu.

Kristo katika injili ilivyoandikwa na Yohane 14:23 anatuambia, yeyote anayenipenda, huzitii
amri zangu. Upendo ni utii. Tunaweza endapo tunapenda, na utii hudhihirisha ni kiasi gani
Page 1 of 4
unapenda. Bila shaka kuna wanandoa hapa, kama mnakumbuka wakati wa ndoa yenu,
mwanaume alimpa mwanamke ahadi, kwamba nitakutunza wewe pamoja na watoto ambao
Mungu atatupa, lakini kabla ya kuweka ahadi hii, mwanaume huweka ahadi ya upendo kwa
mwanamke, nah ii ina maana kwamba hayo yanaweza kutendeka endapo unampenda.

Ndugu zangu, Upendo ni kutenda, upendo hufanya kila kitu kuwa amri. Mt. Augustino
anasema, penda nawe utaweza kufanya kila kitu. Kwake yeye Upendo ni hamu ya kuona
mpendwa yupo na hali njema. Chochote ambacho mpendwa anahitaji, ni amri kwa mpenda.

Upendo ambao unazungumziwa katika maandiko matakatifu dominika ya leo hasa katika
somo letu la pili, si upendo kwa wale wanaotutendea mema tu, ni upendo ambao unatajwa
pia katika injili ilivyoandikwa na mwinjili Mathayo 5:44, “wapendeni adui zenu, watendeeni
mema wanaowaudhi” Kufuata mashauri haya tunaweza kusema ndio ugumu wa kumfuata
Kristo ndio ugumu wa kuwa mkristo. Kuwapenda adui zetu ni jambo gumu ila ni habari
njema. Ni habari njema kwa sababu tukisema kinyume cha haya, wengi wetu wangekuja
hewani na kuhuzunika, kwa mfano tungesema Kristo amesema waueni adui zenu, na mwisho
wa Misa padre aseme, Misa imekwisha nendeni mkawae adui zenu zenu na mlipize visasi
kisawasawa, bila shaka wote mtahuzunika na kushikwa na butwaa kwa sababu si habari
njema kuuana, ingawa ni jambo rahisi kulipiza kisasi.

Ndugu zangu, kumpenda adui si kuwa na hisia nzuri kwake kwa sababu upendo si hisia, bali
upendo ni zaidi ya hisia. Upendo ni kutenda, si kuhisi. Upendo ni kwamba hata kama sijisikii
kufanya, nitafanya kwa sababu ninapenda, na hata kama ninajisikia kufanya, sitafanya kwa
sababu sipendi. Na hivyo Kristo anapotuambia wapendeni adui zenu, si kushikilia
kutawaliwa na hisia juu ya mtu aliyekuumiza, bali ni kutamani mema juu yake na
kumuombea mema kwa ajili yake. Ndivyo kuwapenda adui zetu, ndivyo kuwatendea mema
wanaotuchukia. Kumbe basi inawezekana kuendelea kumpenda mtu hata kama hatujisikii
vizuri juu ya matendo yake.

Nelson Mandela, Raisi wa kwanza wa Afrika Kusini aliyefungwa kwa miaka mingi kwa
sababu za kisiasa aliulizwa na raisi Clinton, “bila shaka uliteseka mno gerezani, je, ulipokuwa
ukitoka katika gereza, ulipokuwa unaliacha eneo la gereza, hukutoka na hisia za maumivu,
chuki na kisasi dhidi ya wale waliofanya maisha yako magumu?” Nelson Mandela alijibu,
nilipokuwa natoka katika gereza langu, nipatwa na hisia hizo, tena kali zisizoelezeka. Lakini
nilipokuwa nakaribia geti kuu la gereza, nilihisi uhuru ambao kwa muda mrefu nimesubiri
Page 2 of 4
kuupata na kuuishi, hivyo nikaamua kuziacha hisia zangu za maumivu, chuki na kisasi, kwa
sababu nisipofanya hivyo, nitabaki mfungwa maisha yangu yote. Hili ndilo Baba Mtakatifu
Yohane Paulo wa Pili analisema wakati akihojiwa baada ya kupigwa risasi na Ali Agca,
aliyedhamiria kumuua, aliulizwa, “kwa nini uliamua kumsamehe mtu aliyetaka kukuua?
Baba mtakatifu alijibu, “ninamsamehe kwa sababu naamini kuwa mtu asiyeweza kusamehe
ni mfungwa aliyefungwa na historia.” Yohane Paulo wa pili na Nelson Mandela
wanatufundisha kwamba, kama unataka moyo wako kuwa huru, msamehe adui zako. Kama
unataka kuwa na usingizi mtamu usiku, msamehe unayelala naye kitanda kimoja.

Kwa kawaida watu ambao tunaona ugumu kuwasamehe si tu adui zetu, ni marafiki zetu wa
karibu tunaowapenda na kuwathamini, ambao kwa namna moja wametuumiza. Lakini
pamoja na maumivu hayo, tunatakiwa kuendelea kuwapenda na kuwathamini kama Kristo
anavyotuambia, wapendeni adui zenu, watendeeni mema wanaowaudhi. Mtu mmoja aliwahi
kusema, “tunaposhindwa kusamehe, tunaharibu au tunapunguza uwezo wetu wa kupenda”.

Ndugu zangu, kuwasamehe wale waliotuumiza ni namna ya kutangaza uhuru wetu, kwamba
hatudhuriwi na ubaya ambao watu wanatutendea. Kusamehe si ishara ya kushindwa au
unyonge au udhaifu, bali ni ishara kwamba tupo imara, ni ishara kwamba hatumpi nguvu mtu
kuziendesha dhamiri zetu, tabia zetu na hisia zetu. Mtu anayeweza kusamehe ni mtu ambaye
anaweza kuishikilia na kuitunza dhamiri yake kwa sababu matendo yake hayaendeshwi kwa
uzuri au ubaya ambao anafanyiwa.

Kuweka kinyongo na kushindwa kusamehe ni sawa na kunywa sumu huku ukiamini kwamba
itamuua adui, tamaa ya kuwateketeza adui zetu, huteketeza uzuri wa roho zetu, nikujiteketeza
sisi wenyewe. Tunatakiwa kuwasamehe wengine kwa sababu Kristo anataka tuwe kama yeye,
tuwe kama Baba yake, tuwe wenye huruma, kwamba hatakama aliteswa na kusalitiwa na
marafiki zake wa karibu, aliendelea kuwapenda, na kwa kufanya hivyo anatueleza kwamba
moyo wake upo huru kana kwamba hakuna mtu anayeweza kuendesha hisia zake na tabia
yake. Hii ndiyo njia ya kuwa na furaha, ndiyo njia ya kupata baraka.

Kwa kuwa kusamehe ni jambo gumu, tuombe neema ya Mungu tuwe na moyo huru, tuwe na
tamaa nzito ya kuwasamehe wale waliotuumiza. Kusamehe ni kugumu mno na wakati
mwingine haiwezekani, lakini ni kwa neema ya Mungu tutaweza kuwasamehe hata wale
ambao wametuumiza na kuwa wema si kwa wale tu ambao wanatutendea wema bali hata
kwa wale ambao wanatuudhi, na kwa kufanya hivyo tunakuwa kama Kristo, tunakuwa kama
Page 3 of 4
Baba, ambaye anaruhusu Mwanae afufuke kwa ajili ya wote, wema na wabaya, kwa sababu
upendo wake ni kwa kila mmoja wetu, na anatutaka sisi kuwa na upendo wa namna hiyo kwa
sababu ndiyo njia pekee ya kuwa na furaha na amani katika maisha yetu.

Frt. B.A. Rochus


10/09/2023
Parokia ya Mt. Benedikto Abate
Visiga

Page 4 of 4

You might also like