Nukushi: +255- S.L.P. 9223 2122617/2120486 11483 DAR ES Baruapepe: ps@moha.go.tz SALAAM
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Zimekuwepo taarifa za kuingia nchini kwa wahamiaji haramu kupitia mpaka wetu na Nchi ya Kenya. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara yake ya Uhamiaji inawahakikishia Watanzania kwamba hatua kali za kisheria zinachukuliwa dhidi ya raia wote wa kigeni wanaoingia nchini kinyume cha Sheria za Uhamiaji na nchi yetu.
Kimsingi hakuna raia yeyote wa kigeni anayeruhusiwa kuingia
nchini kwa kisingizio cha kuja kufanya kazi, biashara au Uwekezaji bila kufuata Sheria na taratibu za Uhamiaji, na kwamba wote wanaokiuka Sheria hizo watarudishwa makwao mara moja. Ni jambo lisilokubalika mtu atoke nchini kwake bila kibali cha kufanya kazi Tanzania kwa madai kwamba alishatuma maombi ya kibali husika na amekuja kusubiri majibu ya kibali hicho akiwa Tanzania. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi haitavumilia ukiukwaji huu wa sheria za nchi na kwamba kila raia wa kigeni anayekusudia kuingia nchini ahakikishe ana kibali cha kuingia nchini na anafanya kazi ambayo ndiyo aliyoiombea kwenye kibali chake.
Yapo matukio ya raia wa nchi jirani, hususan katika mipaka ya
Kenya na Uganda ambapo kutokana na hali ya muingiliano wa kiuchumi na kijamii, raia wa nchi zetu, wamekuwa wakivuka mipaka pande zote kufuata huduma mbalimbali, Hii pia inachangiwa na mapungufu katika usimamizi wa alama na maeneo ya wazi ya mipaka yetu. Hali hii inapelekea baadhi ya wananchi wetu kutumia mwanya huo kuwatengenezea raia wa kigeni mazingira ya kuingia nchini bila kufuata taratibu au hata kutumiwa katika biashara haramu ya kusafirisha binadamu. Tahadhari inatolewa kwa Watanzania wote ambao wamekuwa wakiwapokea raia hao wa kigeni na kuwahifadhi, kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi ikiwemo ile Sheria ya usafirishaji haramu wa binadamu.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara yake ya
Uhamiaji imeanza kuchukua hatua ili kuweza kushughulikia suala hili. Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dk. Anna Makakala, tayari ametembelea baadhi ya maeneo ya mipaka yetu hususani kijiji cha Jasini wilayani Mkinga mkoani Tanga ili kujionea hali halisi na kutoa Maelekezo ya hatua za kuchukua kudhibiti hali hiyo kwa mujibu wa Sheria, kwa kuwa eneo hilo linaonyesha kuwa na muingilino baina ya nchi ya Kenya na Tanzania kwa muda mrefu.
Wizara itaendelea na Mashauriano na Mamlaka nyingine zenye
dhamana ya Kusimamia alama za mipaka ya nchi yetu kwa kuwa tatizo hili la muingiliano wa wananchi wa pande zote lipo kwenye mipaka mingi ya nchi.
Imetolewa na Christina R. Mwangosi Kaimu Msemaji Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 4 Agosti 2017