You are on page 1of 18

See discussions, stats, and author profiles for this publication at: https://www.researchgate.

net/publication/337543122

Mchango wa Waandishi wa Kazi za Kubuni katika Uendelezaji wa Kiswahili

Article  in  Eastern African Literary and Cultural Studies · November 2019


DOI: 10.1080/23277408.2018.1529851

CITATIONS READS

0 5,027

1 author:

Ernest Sangai Mohochi


kibabii University
12 PUBLICATIONS   6 CITATIONS   

SEE PROFILE

All content following this page was uploaded by Ernest Sangai Mohochi on 09 September 2020.

The user has requested enhancement of the downloaded file.


Eastern African Literary and Cultural Studies

ISSN: 2327-7408 (Print) 2327-7416 (Online) Journal homepage: https://www.tandfonline.com/loi/real20

Mchango wa Waandishi wa Kazi za Kubuni katika


Uendelezaji wa Kiswahili

Ernest Sangai Mohochi

To cite this article: Ernest Sangai Mohochi (2019) Mchango wa Waandishi wa Kazi za Kubuni
katika Uendelezaji wa Kiswahili, Eastern African Literary and Cultural Studies, 5:3-4, 223-238, DOI:
10.1080/23277408.2018.1529851

To link to this article: https://doi.org/10.1080/23277408.2018.1529851

Published online: 25 Nov 2019.

Submit your article to this journal

Article views: 337

View related articles

View Crossmark data

Full Terms & Conditions of access and use can be found at


https://www.tandfonline.com/action/journalInformation?journalCode=real20
EASTERN AFRICAN LITERARY AND CULTURAL STUDIES
2019, VOL. 5, NOS. 3–4, 223–238
https://doi.org/10.1080/23277408.2018.1529851

Mchango wa Waandishi wa Kazi za Kubuni katika


Uendelezaji wa Kiswahili
Ernest Sangai Mohochi
Chuo Kikuu cha Rongo

IKISIRI MANENO
Makala hii ililenga kuchunguza mchango wa waandishi wa waandishi wa kazi za kubuni;
kazi za kubuni katika uendelezaji wa Kiswahili. Hili ushawishi wa kijamii; athari;
lilichochewa na ukweli kuwa waandishi ni miongoni mwa uendelezaji wa Kiswahili;
wanafunzi; walimu
makundi muhimu katika ukuzaji wa lugha, mengine
yakiwa: wanaisim, walimu, watafiti, wachapishaji, na
wapenzi wa lugha. Hata hivyo, waandishi wa vitabu
kuhusu maswala mbalimbali ya kinadharia, pamoja na
uendelezaji wa lugha na fasihi yake ndio wametajwa zaidi.
Mchango wa waandishi wa kazi za kubuni haujaangaziwa
sana. Madhumuni mahsusi ya makala hii yalikuwa
kuchanganua nafasi ambayo waandishi wa fasihi ya
Kiswahili wameipa lugha hii katika kazi zao, pamoja na
jinsi ambavyo nafasi hiyo inachangia katika ukuzaji wa
lugha hiyo. Aidha, maelezo yametolewa kuhusu jinsi
wamechangia kuwaathiri wasomaji wao kuhusu umuhimu
wa Kiswahili. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya
ushawishi wa kijamii inayoshikilia kuwa watu maarufu
wana ushawishi mwingi unaowawezesha kuwaathiri
wengine katika jamii. Waandishi wana sifa hizo na hivyo
wanaweza kuathiri misimamo na mielekeo ya wasomaji
wao kuhusu umuhimu wa lugha ya Kiswahili. Data
ilikusanywa kwa kusoma kazi za kubuni za waandishi
watatu wa fasihi ya Kiswahili walioteuliwa maksudi:
Shaaban Robert, Wallah bin Wallah na Ken Walibora,
pamoja na hojaji iliyotolewa kwa wanafunzi 40 na walimu
8 katika Chuo Kikuu cha Rongo. Vilevile, kazi za waandishi
hao ziliteuliwa maksudi. Matokeo ya utafiti huu
yameonyesha kwamba waandishi hawa wameipa lugha ya
Kiswahili nafasi ya kipekee kama sehemu ya maudhui
katika kazi zao, na wamewachora wahusika wapenzi wa
Kiswahili wanaokitetea Kiswahili, ambao wanawaathiri
wahusika wenzao. Isitoshe, waandishi hawa wameathiri
msimamo wa wanafunzi na walimu wa Kiswahili kuhusu
Kiswahili kutokana na nafasi wanayokipa katika kazi zao.
Makala inahitimisha kuwa, kwa mujibu wa nadharia ya
ushawishi wa kijamii, waandishi ni kundi muhimu katika
jamii lenye ushawishi mkubwa na wanapoendelea
kuithamini lugha ya Kiswahili, watawaathiri wengine wengi
kuwa na msimamo kama huo.

WASILIANA Ernest Sangai Mohochi smohochi@gmail.com © 2019 Informa UK Limited, trading as Taylor & Francis Group
Eastern African Literary and Cultural Studies is co-published by NISC Pty (Ltd) and Informa Limited (trading as Taylor & Francis Group)
224 E. S. MOHOCHI

Utangulizi
Lugha ni kitu ambacho daima huhitaji kushughulikiwa kwa namna mbalimbali ili
kukiwezesha kutekeleza majukumu yake katika jamii. Hili linachangiwa kwa kiasi
kikubwa na ukweli kuwa lugha hubadilika kwa mpito wa wakati. Ili hili liweze kufa-
nyika kunahitajika juhudi za maksudi kutoka kwa wadau mbalimbali. Miongoni
mwa watu muhimu katika mchakato huu ni waandishi. Makala hii imelenga
kundi hilo la wadau lakini kwa kujikita zaidi katika waandishi wa kazi za fasihi,
huku mjadala ukiegemezwa kwenye nadharia ya ushawishi wa kijamii. Makala
imetangulizwa na mjadala mfupi wa dhana ya ushawishi kwa kuwarejelea wataa-
lamu wachache miongoni mwa wale ambao wameizungumzia. Sehemu ya pili
imemulika athari au ushawishi walio nao waandishi katika jamii. Hii imefuatiwa
na maelezo ya mchango wa waandishi wa fasihi katika uendelezaji wa lugha ya
Kiswahili, ikiwa ni pamoja na uchambuzi wa kazi mahsusi za waandishi watatu
wa fasihi ya Kiswahili ili kuonyesha ni jinsi gani wamekipa Kiswahili nafasi
muhimu katika kazi zao. Inatarajiwa kuwa jambo hili linaweza kutoa hamasisho
na kuchangia kupendwa zaidi kwa lugha hiyo. Pia, maoni ya wanafunzi na
walimu wa Kiswahili kuhusu mchango wa waandishi wa kazi za kubuni katika uen-
delezaji wa Kiswahili umejadiliwa.

Nafasi ya Ushawishi wa Kijamii


Dhana ya athari ama ushawishi imeshughulikiwa na wataalamu wengi, hasa wana-
saikolojia jamii. Mmoja wa wataalamu hao ni Friedkin (1998) ambaye ameizun-
gumzia kwa mtazamo wa saikolojia ya kijamii huku akiegemeza mawazo yake
katika uchanganuzi wa kimuundo jamii. Miongoni mwa mambo muhimu ana-
yoyajadili ni lile la tofauti zilizopo baina ya wanadamu. Kwamba mbali na zile
tofauti zilizozoeleka kama vile jinsia, dini, kazi au taaluma, binadamu hutofautiana
kwa kuzingatia nafasi ama nyadhifa zao katika jamii. Aidha, katika muundo wa
jamii, ni kawaida kabisa kuwa na tofauti mbalimbali. Katika mchakato wa
maisha, kutokana na muundo wa jamii, wahusika huathiriana katika mahusiano
mbalimbali. Upo wakati wanapokubaliana na pia wakati ambapo wanakosa kuku-
baliana. Kwa hivyo, katika mtagusano wa watu katika nafasi tofauti za kijamii, kuna
michakato kadhaa ya kuathiriana na kushawishiana inayoibuka. Ni kawaida kwa
watu kubadilisha ama kuchukua mielekeo ya wengine ambao wanahusiana kwa
namna moja au nyingine. Hili linatuwezesha kutambua kuwa katika mahusiano
yetu kuna hali ya kushawishi na kushawishiwa. Zaidi ya hayo, inaelezwa kuwa
katika hali ya kushawishi na kushawishiwa, watu wanaanza jitihada za kuthibiti
mazingira yao ya kijamii kwa kubadili mielekeo na maoni ya wanaohusiana nao
(Friedkin, 1998). Inakuwa kawaida kwa watu kufanya hivyo ili kukubaliana na
watu wanaowachukulia kuwa muhimu kwao. Katika hali hii, swala la ushawishi
wa watu muhimu katika jamii linakuwa la msingi kwani huchangia misimamo
na mielekeo ya wengi kuhusu mambo kadhaa.
EASTERN AFRICAN LITERARY AND CULTURAL STUDIES 225

Mbali na hayo, katika nadharia anayoifafanua ya ushawishi wa kijamii, Friedkin


(1998) anasema kuwa ni lazima tutambue mchango wa mtu binafsi katika mcha-
kato huu wa ushawishi. Kwamba lazima mhusika ana maoni na msimamo wake
kama mtu binafsi ambao sharti uzingatiwe katika mjadala wa kinachofanyika
katika mtagusano wa kijamii. Fauka ya hayo, anatongoa misingi mitatu katika ush-
awishi wa mtu mmoja kwa mwingine: mshikamano, mfanano, na umuhimu. Kwa
hivyo, ili maoni ya A yaweze kumuathiri B ni lazima B awe na ufahamu kuhusu
hayo maoni ya A kwanza. Baada ya hapo, uwezekano wa A kumshawishi B utate-
gemea umuhimu na thamani ya maoni ya A kwa B.
Katika mazingira ambamo wahusika wana mshikamano, kuna mahusiano ya
mara kwa mara na uwezekano mkubwa wa wahusika kuathiriana. Aidha, itokeapo
kuwa kuna mfanano wa maoni baina ya wahusika, uwezekano wa kuathiriana ni
mkubwa hata kama mara nyingi hilo ni swala ambalo hawalijui wala kulifikiria.
Katika hali kama hii, ni kawaida kumsikia O akisema “mimi ni kama P, hivyo nita-
tenda na kuamini afanyavyo P” ama “nataka kuwa kama P, na nitakuwa kama P
zaidi nikitenda na kuamini afanyavyo P” (Friedkin, 1998:71, akirejelea maoni ya
Deurkheim 1933; Dahrendorf 1959 na Hechter, 1987). Kuhusu msingi wa tatu,
wahusika wanaochukuliwa kuwa muhimu katika kundi wana nafasi kubwa zaidi
ya kuwashawishi wenzao wakilinganishwa na wanaochukuliwa kuwa na
umuhimu mdogo.
Kimsingi, watafiti wamegundua kuwa baadhi ya watu huwa muhimu na huwa
na ushawishi kuliko wengine katika kikundi (Goldsmith, 2015). Ukweli huu haud-
hihiriki kwenye kikundi tu bali hubainika vilevile katika jamii pana. Mjadala wa ush-
awishi unahusisha sana swala la namna binadamu hufanya maamuzi: je, ni uamuzi
wa mtu binafsi ama anabadilisha maoni na msimamo wake ili uoane na athari
inayotarajiwa kutoka kwa wengine na jamii? Mayhew (1997) anasema kwamba
ushawishi ni kuathiri matendo ya wengine kwa kuwabembeleza. Hakuna matu-
mizi ya nguvu au vitisho, ama ahadi za malipo bali rasilmali huwa ni za kijamii.
Kwingineko, maelezo ya muda mrefu ya ushawishi yamehusishwa na kuwepo
kwa hadhi, uwezo, mali na nafasi. Katika mantiki hii, wenye sifa hizo wana
nafasi kubwa zaidi ya kuwashawishi wengine; wanakuwa viongozi au wanaotoa
maoni yanayofuatwa katika jamii. Misimamo na maoni yao hukubalika kwa
urahisi zaidi katika jamii. Mayhew (1997) pia anadai kuwa hata kama hakuna matu-
mizi ya nguvu na vitisho, lazima kuna hali ya kueleza maoni na msimamo wa mtu
ili wengine waweze kushawishika na kutenda kwa namna maalum. Ni jinsi gani
waandishi wa kazi za kubuni wanavyoshawishi wanajamii kwa kuzingatia nadharia
hii ya ushawishi wa kijamii? Jambo hili linashughulikiwa katika sehemu inayofuata.

Athari ya Waandishi katika jamii


Kwa jumla, waandishi wana athari na ushawishi mkubwa sana katika jamii. Ni
kutokana na maandishi mbalimbali, mengi yakiwa matokeo ya utafiti, ambapo
jamii nyingi zimepata kuendelea. Uandishi ni njia moja muhimu sana
226 E. S. MOHOCHI

inayochangia katika kubadilishana na kupitisha maarifa kutoka kwa kizazi kimoja


hadi kingine, na kutoka jamii moja hadi nyingine. Ni maandishi yanayofanikisha
sekta nzima ya elimu. Aidha, uandishi ni njia moja muhimu sana katika uhifadhi
wa utamaduni na amali mbalimbali za jamii, hasa kwa kuzingatia kuwa utamaduni
wa masimulizi unaendelea kupotea. Uhifadhi wa utamaduni uliokitwa katika
vitabu na makala, au katika hali ororo kwenye mitandao mbalimbali, na njia nyin-
ginezo za kiteknolojia ndio unaendelea kutawala. Ughaibuni, waandishi kama vile
Spencer, Milton na Shakespeare waliendeleza sana Kiingereza, huku Pushkin na
Tolstoy wakisaidia sana kuikuza lugha ya Kirusi kwa kuzitumia lugha hizi katika
maandishi yao ya kifasihi (Ngugi Wa Thiong’o, 1986). Athari ya Shakespeare
katika lugha ya Kiingereza ni kubwa kiasi cha kutambulika kwa “Kiingereza cha
Kishakespeare”. Wengi wanatarajia waandishi wa lugha za Kiafrika kufanya vivyo
hivyo kuhusu lugha za Kiafrika.
Katika muktadha wa bara la Afrika, waandishi wamechangia sana katika uende-
lezaji wa lugha za Kiafrika kwa kuziweka katika maandishi. Hapo awali, hili lilijito-
keza kuwa muhimu katika swala la dini wakati wamishenari waliposhirikiana na
wenyeji wachache kutafsiri maandishi matakatifu katika lugha za Kiafrika. Kule
kuziweka lugha za Kiafrika katika maandishi tu kulizipa hadhi fulani na kuziweka
katika kundi la lugha zenye maandishi. Mbali na sekta ya dini, lugha mbalimbali
za Kiafrika zilianza kupata nafasi katika maandishi yasiyo ya kidini. Katika
mantiki hii, kuna waandishi wengi ambao wamechangia katika uendelezaji wa
uandishi katika lugha ya Kiswahili kwa sababu lugha hii imetumika katika macha-
pisho mengi.
Hata hivyo, ikumbukwe kuwa katika miaka ya nyuma, waandishi wengi wali-
pendelea matumizi ya lugha ya Kiingereza na lugha nyingine za kigeni kwa
madai kuwa hilo liliwawezesha kuwafikia wasomaji wengi zaidi. Ngugi wa
Thiong’o ni mwandishi mmoja ambaye tangu hapo alijitokeza wazi na kutetea
umuhimu wa matumizi ya lugha za asili badala ya zile za kigeni. Katika Decolonis-
ing the Mind (1986), Ngugi anataja kuwa baada ya kuandika Petals of Blood (1977)
alisitisha matumizi ya lugha ya Kiingereza katika uandishi wake wa kazi za kubuni.
Aliendelea kuzalisha maandishi mengine katika lugha hiyo lakini kitabu hicho
Decolonising the Mind (1986), kilitarajiwa kuwa cha mwisho katika Kiingereza. Alia-
hidi kutumia Kiswahili na Kikikuyu tu katika kazi zake za baadaye, huku akiamini
kuwa kupitia kwa taaluma ya tafsiri bado mawazo yake yangewafikia wengi.
Mjadala wa lugha mwafaka katika uandishi wa fasihi ya Kiafrika uliwashughu-
lisha wengi. Kutokana na athari ya ukoloni na ubeberu, Waafrika walikuwa wame-
jenga tabia ya kupendelea vilivyo vya kigeni zikiwemo lugha, huku wakibeza za
kwao. Ngugi (1986), kwa mfano, analalamikia mtindo wa kuigawa Afrika kwa
misingi ya lugha za kigeni, uliochangia kuundwa kwa makundi ya nchi za Kiafrika
zinazozungumza Kiingereza, Kifaransa au Kireno. Anaiendeleza hoja hiyo kwa
kumtaja Chinua Achebe kama mmoja wa waandishi mashuhuri waliokiri kuwa
kuna usaliti wa namna fulani kwa Waafrika kutumia lugha za kigeni badala ya
zao lakini akadai kwamba hakuwa na namna nyingine ila kutumia lugha hiyo ya
EASTERN AFRICAN LITERARY AND CULTURAL STUDIES 227

Kiingereza. Mwandishi mwingine ambaye aliukubali ubeberu wa lugha ya kigeni


na kuusifia kwa uwezo wake ni Leopold Sedar Senghor aliyeihusudu lugha ya
Kifaransa (Ngugi, 1986). Senghor alishikilia kuwa lugha ya Kifaransa ilikuwa
lugha nzuri sana iliyompa mwandishi fursa ya kuyaeleza mawazo yake kikamilifu
na kuyawasilisha kwa umma mpana.
Hata hivyo, si wote walioukubali ubeberu huo wa kiisimu. Kulingana na Ngugi
(1986), waandishi kama vile Obi Wali na David Diop walipinga hali hiyo na kueleza
kwamba lugha pekee ya Mwafrika aliye huru kutumia kueleza utamaduni wake na
hisia zake ni lugha zake za asili. Diop, kwa mfano, aliamini kuwa matumizi ya Kiin-
gereza, Kifaransa na Kireno yangekuwa ya muda tu kabla ya lugha za Kiafrika
kuchukua nafasi zake.
Hadi miaka ya hivi karibuni, swala la lugha mwafaka ya waandishi wa Kiafrika
kutumia kuandika kazi zao linajadiliwa. Kwa mfano, Aboh (2015) amelizingatia
kwa kutumia mfano wa hali ya Nigeria. Anadai kwamba kulazimisha watu
wenye asili tofauti kujumuika na kujenga nchi moja pamoja na mabadiliko
katika hali ya maisha yameifanya lugha ya Kiingereza kuwa lugha ya kila kitu
nchini humo. Aidha, Aboh (2015) anarejelea mjadala wa muda mrefu ulio na
pande mbili kuhusu swala hili. Kwa upande mmoja kuna watu kama Wole
Soyinka, ambaye mwaka wa 1975 alipendekeza matumizi ya Kiswahili, na
upande wa pili una watu kama Chinua Achebe, ambaye haoni ubaya wa kuende-
lea kutumia lugha ya Kikoloni-Kiingereza. Afrika Mashariki, kuna lugha ya asili ya
Kiswahili ambayo imezalisha kazi nyingi zinazoeleza changamoto za maisha
yetu na hatua mbalimbali za kuzikabili. Ni muhimu kuikuza na kuitumia huku
wanaopendelea Kiingereza nao wakiwa huru kuandika katika lugha hiyo, lakini
wakumbushwe kila mara kuwa wananchi wa kawaida hawafaidi maandishi
katika lugha za kigeni.
Je, waandishi wa kazi za kubuni za Kiafrika wametoa mchango gani katika jiti-
hada za kuhakikisha kuwa lugha za Kiafrika zimeendelea kukuzwa na kuchukua
mahali pa za kigeni kama alivyoamini Diop? Swali hili linashughulikiwa katika
sehemu inayofuata kwa kutumia mfano wa fasihi ya Kiswahili. Halikadhalika,
maelezo yametolewa kuhusu mbinu za ukusanyaji wa data iliyojenga msingi wa
maandalizi ya makala hii.

Mbinu za Utafiti
Mwandishi alipitia kazi mbalimbali za waandishi wa Kiswahili na kueleza mchango
wa kazi hizo katika uendelezaji wa lugha ya Kiswahili. Katika kufanya hivyo, kundi
la kwanza linahusu kazi za waandishi wa awali ambao walichangia sana ukuzaji wa
fasihi ya Kiswahili. Sehemu ya pili ilihusisha usomaji wa kina wa kazi mahsusi za
waandishi watatu na kuonyehsa zinavyochangia ukuzaji wa Kiswahili katika
ujenzi wa maudhui. Kazi zilizorejelewa ni za Shaaban Robert, Wallah Bin Wallah,
na Ken Walibora. Kazi zao zinazozungumzia Kiswahili ziliteuliwa maksudi na kuja-
diliwa katika makala hii. Aidha, hojaji ilitumiwa kupata data kutoka kwa wanafunzi
228 E. S. MOHOCHI

wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Rongo pamoja na walimu wa chuo hicho na
shule jirani katika kaunti za Migori na Kisii, magharibi mwa Kenya. Walimu wa
shule jirani waliotumiwa ni wale ambao hufunza Kiswahili kama walimu wa
muda katika Chuo kikuu cha Rongo. Lengo kuu la kutumia hojaji lilikuwa
kupata maoni ya walimu na wanafunzi kuhusu nafasi ya kazi za kubuni katika uen-
delezaji wa Kiswahili, pamoja na athari ya waandishi wa kazi hizo katika maswala
ya ukuzaji wa Kiswahili. Kwa jumla, wanafunzi arobaini na walimu wanane
walishiriki katika utafiti huu. Walimu na wanafunzi walioshiriki ni wale ambao wali-
patikana chuoni Rongo wakati wa kufanyika kwa uchunguzi huu.

Mchango wa Waandishi wa Kubuni katika Uendelezaji wa Kiswahili


Pamoja na mchango wa kiuandishi, waandishi wa kazi za kubuni wamechangia
katika uendelezaji wa lugha ya Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika kwa njia
nyinginezo. Kwa mfano, msimamo wa Ngugi wa Thiong’o uliibua mjadala wa
muda mrefu kuhusu swala hili. Tunaporejelea lugha ya Kiswahili, mchango wa
kwanza kabisa wa waandishi wa kazi za kubuni unatokana na uchapishaji wa
kazi nyingi za kubuni katika lugha ya Kiswahili. Hapa tutataja kazi kadhaa, tukianza
na zile zilizotokana na fasihi ya awali ya Kiswahili iliyoibuka kutokana na mahu-
siano ya awali ya Waswahili na jamii za nje ya Afrika. Kundi hili lina kazi kama:
Utendi wa Tambuka; Al Inkishafi (1980), Takhmisa ya Liyongo, Utenzi wa Mwanaku-
pona, na Mashairi ya Muyaka (1979). Kipindi kingine kilihusisha waandishi kama
Walter Mbotela, Henry Kuria, Graham Hyslope, na Gerishon Ngugi. Baada ya
hapo waliibuka magwiji wa fasihi ya Kiswahili, hasa kipindi cha baada ya uhuru,
kama Shaaban Robert, Euphrase Kezilahabi, Ebrahim Hussein, Abdilatiff Abdalla,
Mugyabuso Mulokozi na wenzao kutoka Tanzania Bara, pamoja na Said Ahmed
Mohammed, Mohammed Suleiman Mohammed, na Mohamed Said Abdala
kutoka Visiwani waliochangia kazi nyingi za kutajika. Nchini Kenya walikuwepo
waandishi kama vile Chacha Nyaigoti Chacha, Jay Kitsao, Rocha Chimerah, na
Kithaka wa Mberia.
Baadaye, kukaibuka kizazi kingine cha waandishi kama Ken Walibora, Kyalo
Wamitila, Mwenda Mbatiah, John Habwe, na Timothy Arege, miongoni mwa
wengine. Awali, maandishi mengi ya kazi za kubuni yalitoka Tanzania lakini
kuanzia miaka ya tisini waandishi kutoka Kenya walizalisha kazi nyingi sana. Waan-
dishi hawa wote wamechangia sana katika kuiendeleza lugha ya Kiswahili kwa
sababu ya kuongeza mavuno katika ghala la maandishi katika Kiswahili, na kwa
kuangazia maudhui mbalimbali katika kazi zao. Kwa kufanya hivyo, hadhira ya
wasomaji wa kazi za kubuni za Kiswahili inaendelea kupanuka kwani wasomaji
tofauti huvutiwa na uandishi wa watu maalumu pamoja na mada maalumu zina-
zoshughulikiwa na waandishi hao. Kwa mfano, tunaposoma riwaya ya Kuli ya
Shafi Adam Shafi au tamthilia ya Kilio cha Haki ya Al Amin Mazrui, tunabaini hali iliyo-
wakumba wafanyakazi wa kawaida katika enzi za ukoloni ulioandamana na
EASTERN AFRICAN LITERARY AND CULTURAL STUDIES 229

unyanyasaji kwa wenyeji, hususan wanyonge katika jamii. Kupitia kwa njia hii, fasihi
inatekeleza majukumu kadhaa likiwemo lile la kuangazia historia ya jamii zetu.
Tukizingatia kuwa fasihi ina mchango mkubwa pia katika kufunza na kupanua
ufahamu wa lugha maalumu, ni wazi kuwa waandishi hawa wamesaidia pia katika
ufundishaji wa Kiswahili. Kwa mfano, mwandishi wa makala hii aliitumia kazi ya
Ken Walibora ya Ndoto ya Amerika (2001) pamoja na riwaya ya Tumaini (2006)
ya Clara Momanyi katika ufundishaji wa Kiswahili kwa wanafunzi wa kigeni
nchini Marekani. Walimu wengi wa Kiswahili nchini Marekani na maeneo
mengine ughaibuni hutumia kazi mbalimbali za fasihi katika madarasa yao,
hasa kwa wanafunzi wa viwango vya pili na tatu. Ingawa kumekuwa na mjadala
wa muda mrefu miongoni mwa wataalamu kuhusu umuhimu wa fasihi katika
ufundishaji wa lugha, kinachoaminika ni kuwa fasihi husaidia si katika kipengele
cha kuwapa wanafunzi fursa nzuri ya kuelewa mengi zaidi kuhusu utamaduni
wa jamii tu, bali vilevile kuwafahamisha namna mwafaka za kuelezea hisia mba-
limbali. Aidha, fasihi hukuza zaidi matumizi yao ya miundo mbalimbali ya
kiisimu wanayoisoma. Hali hii haibainiki katika mafunzo kwa wanafunzi wa
kigeni tu. Hata katika muktadha wa Kiswahili hapa Afrika Mashariki, usomaji wa
kazi nyingi za kubuni huwasaidia wanafunzi kupanua msamiati wao wa lugha
pamoja na miundo tofauti ya matumizi ya lugha hiyo.

Kiswahili kama Mada Muhimu katika Kazi za Fasihi


Wapo waandishi wa kazi za kubuni ambao wameangazia umuhimu na nafasi ya
Kiswahili katika jamii kwa njia ya moja kwa moja katika kazi zao. Mchango wa
waandishi hawa ni wa kipekee kwa kuwa huishughulikia lugha ya Kiswahili
kama mada kuu katika utunzi wao, hususan kwa kuipa nafasi muhimu katika
maudhui ya kazi zao.
Mwandishi wa kwanza tutakayemrejelea katika kundi hili ni Shaaban Robert
ambaye aliizungumzia wazi wazi lugha ya Kiswahili katika shairi lake la “Titi la
Mama”.
Titi la mama litamu, hata likiwa la mbwa,
Kiswahili naazimu, sifayo iliyofumbwa,
Kwa wasiokufahamu, niimbe ilivyo kubwa,
Toka kama mlizamu, funika palipozibwa,
Titile mama litamu, jingine halishi hamu.

Lugha yangu ya utoto, hata sasa nimekua,


Tangu ulimi mzito, sasa kusema najua,
Ni sawa na manukato, moyoni mwangu na pua,
Pori bahari na mto, napita nikitumia,
Titile mama litamu, jingine halishi hamu.

Mwandishi anaisifu lugha ya Kiswahili kwa sababu ya uzuri wake na kusema kuwa
wasioifahamu atawaelimisha kwa njia ya kuimba ili kuisifu lugha hii adhimu.
230 E. S. MOHOCHI

Aidha, anaeleza jinsi ambavyo imemkuza tangu akiwa mtoto hadi sasa ambapo
anaizungumza kwa urahisi katika utu uzima. Inamwezesha sasa kutekeleza shugh-
uli zake zote popote aendapo. Kwa sababu hiyo anailinganisha na manukato.
Labda muhimu zaidi ni kibwagizo kisemacho ‘titile mama litamu, jingine halishi
hamu’. Tukitafakari kauli hii tunaona kuwa kwa kumithilisha lugha ya Kiswahili
na titi, Robert anaonesha umuhimu wake kwetu. Hakuna mtu anayeweza
kupinga, kwa mafanikio, umuhimu wa titi la mama kwa mtoto. Ingawa wapo
ambao siku hizi hawataki kuwapa wana wao titi, ati kwa sababu kunyonywa
kutayaharibu matiti, wataalamu wamesema kuwa hakuna kiwezacho kuchukua
nafasi ya maziwa ya mama kwa mtoto. Isitoshe, twaweza kuangalia uamuzi wa
kutumiwa kwa mfano wa mbwa kwa mapana zaidi. Katika jamii ya wanyama,
mbwa hana hadhi kubwa sana. Wapo wanyama wanaoheshimiwa zaidi, lakini
kwa mwana mbwa hakuna jingine liwezalo kuchukua mahali pa titi la mama.
Vivyo hivyo, japo zipo lugha nyingine, tukumbuke kuwa ni lugha zetu tu
ambazo zinaweza kutimiza hamu. Kwa maana hiyo, kwetu sisi Kiswahili ndiyo
lugha tuwezayo kuitumia kutekeleza shughuli zetu na kuleta maendeleo. Inatubidi
kuiendeleza ili vizazi vijavyo viweze kuendelea kulinyonya titi la mama na kupata
uhondo wake.
Wallah Bin Wallah katika shairi lake “Tutukuze Kiswahii”, linalopatikana katika
diwani ya Malenga wa Ziwa Kuu (1988) ameijadili nafasi muhimu ya Kiswahili
katika jamii. Anatanguliza kwa kusema kuwa atakayoyasema ni ya ukweli. Mion-
goni mwa mambo mengi anayoyaeleza ni kuwa: lugha ni kitu kinachotoa
heshima kwa nchi; ni muhimu kwa watu wote, wakubwa kwa wadogo; ukosefu
wake waweza kukwamisha mambo mengi; Mungu alitubariki Afrika Mashariki
kutupa Kiswahili hivyo tukisambaze, huku na ughaibuni; ni muhimu kisemwe na
kutumiwa kwa ufasaha unaostahili, na juhudi za urekebishaji wa pale palipohari-
bika zifanywe kwa umoja. Kibwagizo chasema ‘Kiswahili kitukuzwe, kwani lugha
ya Taifa’. Shairi hili lilitungwa katika muktadha wa Kenya ambapo wakati huo
Kiwahili kilikuwa ni lugha ya taifa tu. Hata hivyo, yasemwayo na mshairi yanahusu
eneo letu zima la Afrika Mashariki lililo kitovu cha lugha hii. Ni wajibu wetu kuki-
tukuza Kiswahili. Shairi hili lilikuza sana lugha ya Kiswahili na kuathiri msimamo wa
watu kuhusu Kiswahili. Hili lilibainika zaidi wakati idhaa ya redio na runinga ya KBC
(Kenya Broadcasting Corporation) ilipolitumia kutanguliza vipindi vya Lugha Yetu.
Shairi hili liliimbwa kwa mahadhi mazuri na kufahamika kote nchini.
Mwandishi mwingine katika kundi hili ni Ken Walibora. Katika riwaya yake ya
Siku Njema (1996) lugha ya Kiswahili imepewa nafasi muhimu sana na mwandishi.
Awali ya yote, majina ya wahusika wake wengi ni majina yanayohusiana na Uswa-
hili. Haya ni pamoja na: Zainabu, Msanifu Kombo, Salim, Vumilia Binti Abdalla,
Selemani, Bakari, Rashidi, Amina, Zawadi, na Athman. Pia, jina la mhusika mkuu,
lililofahamika zaidi ya hilo Msanifu, la Kongowea Mswahili ni moja kati ya
majina hayo. Pili, amewasawiri baadhi ya wahusika wake kama watu ambao
wanaipenda na kuithamini sana lugha ya Kiswahili. Kwa mfano, Zainabu
Makame, mama yake Kongowea. Mama huyu alikuwa mwimbaji na mtunzi
EASTERN AFRICAN LITERARY AND CULTURAL STUDIES 231

hodari sana wa mashairi ya taarab. Ni mwimbaji aliyejulikana na kupendwa sana


ndani na nje ya Afrika Mashariki. Alifahamika kwa umaarufu wake wa uimbaji
katika kundi la Mbelewele Taarab mjini Tanga.
Sifa na umaarufu wake unafafanuliwa na wahusika mbalimbali katika riwaya hii.
Mwanawe, Kongowea, anaeleza bayana umahiri wa mama huyu katika utunzi wa
mashairi. Aidha, Kongowea anaonesha jinsi Zainabu alivyopenda sana mashairi.
Ifuatayo ni mifano ya kudhihirisha hilo: “Mama alikuwa na mazoea ya kusoma
tungo za washairi farisi. Ndiposa haikumwia vigumu kutunga na kuimba
nyimbo za taarab zilizowapa watu pumbao. Alikuwa ashiki mkubwa wa lugha
ya Kiswahili na ushairi wake, nami nadhani sitakosea sana kusema kwamba alinir-
ithisha mwelekeo huo.” (uk. 1-5). Mbele kidogo kuna maelezo haya, “wakati mwin-
gine aliniomba nimwimbie au nimsomee shairi moja au mawili kutoka kwenye
Sauti ya Bara, diwani aliyoipenda kama asali.” (uk. 11). Alipoaga dunia, wapenzi
wa muziki wa taarab walihuzunika mno kutokana na kumpoteza mtunzi na mwim-
baji mahiri wa fani hii ya muziki wa Kiswahili. Mazishi yake yalihudhuriwa na watu
wengi ajabu.
Umahiri wake ulifafanuliwa vyema katika gazeti la Baraza. Habari za kifo chake
ziliandikwa chini ya kichwa cha habari ‘WAPENZI WA TAARAB WAMZIKA MWIM-
BAJI HODARI’. Mbali na kueleza wingi wa watu waliohudhuria mazishi hayo na
kutoa sifa kem kem kwa marehemu Zainabu, gazeti lilisema yafuatayo (uk. 15-
16), “ … kwa wapenzi wa taarab wa mbali na karibu, kifo kimewapiga pute
johari adimu na thamani … Naye Zainabu Makame ameacha nyayo zake katika
safu za waimbaji na watunzi hodari.”
Isitoshe, Kongowea alipofika Mombasa katika safari yake ya kumtoroka Sele-
mani Mapunda na kumsaka babake, alikaribishwa nyumbani kwa Rashid. Siku
ya kwanza tu katika nyumba hiyo, Rashid, ambaye hakujua wakati huo kuwa
Zainabu alikuwa mamake Kongowea, alicheza wimbo mmoja wa taarab wa
Zainabu Makame kwenye kinanda chake. Baada ya wimbo kuisha Rashid alikiri
hivi (uk. 63), “Basi mwanamke huyu alikuwa akiimba kweli … Looh! Kifo ni
mwizi mkubwa wa kuiba kila kilicho bora.” Katika barua yake kwa kijana wake Kon-
gowea, babake alisema yafuatayo kuhusu mamake, “Mamako Zainabu Makame
tulikutana zamani sana … Alikuwa mutribu aliyeghani nyimbo za taarab kwa
lahani taanusi” (uk. 132). Ni wazi kutokana na hayo yote kuwa Zainabu alikuwa
na kipawa cha kipekee katika fani yake. Aidha, ni wazi kuwa aliwaathiri wengi,
kama vile mwanawe Kongowea, Rashid. Aidha, ilivyodhihirika kwenye gazeti
baada ya kifo chake, aliwaathiri wengi katika jamii.
Mzazi mwenzake Zainabu, yaani babake Kongowea, pia alijihusisha na shughuli
za Kiswahili. Alipompata babake mwishoni mwa msako wake, Kongowea aligun-
dua kuwa Juma Mukosi alikuwa mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu hapo
zamani kabla hajajiuzulu na kuhamia Kitale, mji mdogo ulioko bonde la ufa kule
Kenya. Aidha, alipokutana na Zainabu Makame mjini Mombasa, alikuwa katika
harakati za utafiti kuhusu lahaja ya Kimvita ilhali Zainabu alikuwa anaendelea
na shughuli za uimbaji wa taarab. Vilevile, Kongowea alibainikiwa kwamba
232 E. S. MOHOCHI

babake, Juma Mukosi, ndiye Amuj Isokum, mwandishi wa diwani maarufu ya Sauti
ya Bara, ambayo aliipenda sana mamake na yeye mwenyewe, na iliyokuwa inafun-
dishwa kwenye shule ya kina Alice na mwalimu Nambuye Pilipili. Kutokana na sifa
hizo za wazazi wake, hasa kuhusiana na lugha ya Kiswahili, si ajabu kuwa Kongo-
wea naye aliibuka kukipenda na kukienzi Kiswahili kweli kweli.
Mwandishi ametumia mifano mingi kuonyesha mapenzi aliyokuwa nayo Kon-
gowea kwa lugha ya Kiswahili; mapenzi ambayo yalisababisha yeye kuja kuitwa
Mswahili, jina ambalo lilikuwa maarufu na kuchukua nafasi ya jina lake halisi,
Msanifu Kombo. Mapenzi ya Msanifu Kombo kwa lugha ya Kiswahili yalianza
mapema sana katika maisha yake. Mwenyewe anasema hivi, “Nilipojua kusoma
nilijikusuru kuzisoma tungo adhimu za Kiswahili nilizopata kukumbana nazo, vita-
buni na magazetini” (uk. 5). Katika ukurasa unaofuata anasema wazi, “Waama,
mambo yanayohusiana na Kiswahili na Uswahili yamenitamia kwa miaka mingi.
Niliwahusudu wazee wengi wa Tanga kwa umahiri wao katika Kiswahili na
kunga zake za ushairi.” Kwa sababu hiyo, Msanifu alipenda kukaa na wazee mba-
limbali ili aweze kupata maarifa kutoka kwao. Vilevile, alipendelea kusoma vitabu
mbalimbali vya Kiswahili katika maktaba ya umma ya Tanga, jambo analodai lilim-
wezesha kukijua Kiswahili vizuri zaidi ya hirimu zake wengine.
Akiwa katika shule ya msingi, alitunga hadithi “Kongowea Mswahili” ambayo
ilichukua nafasi ya kwanza katika mashindano ya shule za msingi mkoani
Tanga. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa jina lake la Kongowea Mswahili akiwa
darasa la sita. Kutokana na weledi alioonyesha shuleni, hasa katika somo la Kiswa-
hili, wenzake walianza kumuita bingwa wa Kiswahili, ingawa yeye binafsi haku-
jiona ama kujichukulia kuwa bingwa. Kongowea alipoletewa habari kuwa
anaitwa na mamake aliyekuwa katika hali mahututi, alikuwa kwenye maktaba
ya umma akisoma Kamusi ya Kiswahili iliyoandikwa na Dr. Ludwig Krapf (uk. 11-12).
Halikadhalika, baada ya kusoma nakala ya gazeti iliyokuwa na habari kuhusu
kifo na mazishi ya marehemu mamake, Kongowea anatoa kauli inayodhihirisha
kuwa hakipendi tu Kiswahili kwa sababu alikijua, bali alikithamini kiasi cha kujali
ni jinsi gani kinavyotumiwa na wengine. Anamsifu mwandishi wa habari ile kwa
sababu ya matumizi mufti ya lugha ya Kiswahili, jambo ambalo anakiri ni nadra
sana katika magazeti mengi ya Kiswahili. Anasema kuwa “waandishi wa habari
na vitabu wanayo dhima ya kuwafundisha wasomaji wao ufasaha na umbuji uta-
kikanao … Mtu anayepima ubora wa Kiswahili kutokana na kile akisomacho katika
magazeti yetu hana budi kukihukumu kuwa lugha dufu na pungufu” (uk. 17). Ken
Walibora amejitokeza na kujibainisha kuwa ni mwandishi anayekithamini Kiswahili
na kuhimiza hali ya kukiendeleza kwa kufuata kaida na kanuni mwafaka za lugha
hii adhimu kwa kupitia kwa kauli za wahusika wake mbalimbali kama vile Kongo-
wea katika Siku Njema, na Amani katika Kidagaa Kimemwozea. Aidha, yeye amefa-
nya kazi katika sekta ya habari kwa muda mrefu, kwa hivyo hali anayoizungumzia
hapa anaielewa barabara.
Kongowea Mswahili pia alikuwa mtunzi wa mashairi ya Kiswahili. Baada ya
mazungumzo ya muda mrefu na Mjomba wake, Kitwana Makame, kuhusu
EASTERN AFRICAN LITERARY AND CULTURAL STUDIES 233

uamuzi wake wa kuhama kutoka Tanga, Kongowea alikosa usingizi na akaamua


kutumia muda huo kutunga ubeti ufuatao:

Naambe ambaye amba, atakaye badiliko


Ajaponifunga kamba, nisiende nitakako
Nayo njia nitatamba, kule Kenya nende huko

Ulipofika wakati wake kutoka Tanga, miongoni mwa vitu vichache alivyovibeba
katika mkoba wake ni vitabu vitatu: cha hadithi kilichoitwa Shani Kubwa; diwani
ya Sauti ya Bara, pamoja na kamusi ya Kiwahili. Uamuzi huu ni dhihirisho
kuhusu nafasi ya Kiswahili katika maisha yake. Alipoishi na Rashid mjini
Mombasa, alipenda kutumia muda wake wa ziada kwenda katika maktaba ya
umma kusoma vitabu. Aidha, aliandika hadithi fupi na mashairi, baadhi ambayo
yalitokea katika magazeti ya Baraza na Taifa Leo. “Hapana shaka niliandika mno,
lakini ilikuwa kazi iliyonipa furaha isiyomithilika. Niliipenda. Nilipenda kuchangia,
japo kwa akali ndogo, utukufu wa lugha ya Kiwahili.” (uk. 74).
Alipofika Kitale na kupata makazi katika kasri la Bi Mercy MacDonald, Mswahili
aliendelea kutunga mashairi na kuyapeleka magazetini, na mengi yalisomwa na
watu katika Baraza na Taifa Leo. Hali hii ilichangia umaarufu wake na kujulikana
na watu wengi kama vile mwalimu wa shule alikosomea Alice, Bintiye Bi Mercy.
Mwalimu wa Alice aliomba kuonana naye wakati Alice aliomba msaada wa
kuchambua diwani ya Sauti ya Bara. Mwalimu Nambuye alimwalika Kongowea
Mswahili kuzungumza na wanafunzi wake kuhusu Kiswahili. Awali alisita sana
ama kumsaidia Alice au kwenda shuleni kwao lakini hatimaye, kutokana na
mapenzi yake kwa Kiswahili, akakubali maombi yote mawili. Haya yalifanyika
baada ya shairi lake, “m’baguano” kupata nafasi ya kwanza katika mashindano
ya utunzi wa mashairi nchini Kenya. Kuhusu mwaliko wa kwenda shuleni kutoa
hotuba, alisema hivi, “ … nitakuja. Nitakuja tu kwa sababu ya utukufu wa Kiswa-
hili.” (uk. 120).
Akijiandaa kwa hotuba yake shuleni Kongowea alisoma vitabu vingi, baadhi
akiwa ametoka navyo Tanga na vingine alivyovinunua mjini Kitale. Mwenyewe
anasema kuwa yalikuwa mazoea yake kununua vitabu vya Kiswahili. Ni wangapi
kati ya walimu na wataalamu wengine wa Kiswahili wawezao kusema kuwa
wana mazoea ya aina hiyo? Japo wapo, si wengi sana. Katika hotuba yake, ‘Mata-
tizo yanayoikabili lugha ya Kiswahili’, Mswahili alieleza mengi muhimu kuhusu Kis-
wahili kabla ya mhusika Kazi Kwisha kuivuruga hotuba yake. Kongowea alitaja
wazi uzuri na umuhimu wa Kiswahili kisha akalalamika kuwa, kwa kiasi kikubwa,
ni sisi wenyewe ambao hatuelekei kukitambua, kukithamini na kukiendeleza
kwa dhati Kiswahili. Aliwatambua na kuwasifu wageni kutoka nje, kama vile:
Lambert, Dr. Krapf, F. Johnson, na Prof. Wilfred Whiteley kwa mchango wao
mkubwa katika kutafiti na kuandika mambo mengi kuhusu Kiswahili. Aliwatanaba-
hisha wasikilizaji wake kuwa jukumu la kuiendeleza lugha hii tukufu ni letu sisi
sote, tuwe wa pwani ama wa bara. Analalamika kuwa waandishi wa Kiswahili
hawana soko kubwa kwa sababu watu hawapendi kusoma vitabu vya Kiswahili.
234 E. S. MOHOCHI

Isitoshe, hata wataalamu wa Kiswahili wanasoma zaidi vitabu vya Kiingereza.


Anasema wazi kuwa adui mkubwa wa Kiswahili ni wewe na mimi. Wangapi wana-
weza kupinga maoni hayo ya Kongowea kwa dhati? Huo ni ukweli unaopaswa
kutufikirisha na kutuzindua ili tubadili mielekeo yetu kuhusu lugha ya Kiswahili.
Kazi hii ya Ken Walibora ilikuwa na ushawishi mkubwa sana miongoni mwa
wapenzi wa fasihi ya Kiswahili, hasa nchini Kenya. Riwaya ya Siku Njema iliteuliwa
kusomwa na kutahiniwa katika mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne, yaani KCSE
(Kenya Certificate of Secondary Education), jambo ambalo lilipanua umaarufu
wake. Wanafunzi wengi waliokisoma kitabu hicho shuleni wanakiri kuwa riwaya
hii ilichangia sana wao kulipenda somo la Kiswahili. Wanaosoma Kiswahili katika
vyuo vikuu hadi sasa hufurahia sana kuijadili na kuirejelea ili kutoa mifano
katika mijadala yao darasani.
Aidha, katika riwaya yake ya Kidagaa Kimemwozea, Ken Walibora ameendeleza
hali ya kuipa lugha ya Kiswahili nafasi muhimu katika uandishi wake wa kazi za
kubuni. Mosi, kazi hii ina majina kadhaa ya Kiswahili na Uswahilini. Haya ni
pamoja na Amani, Imani, Nasaba Bora, Bi. Zuhura, Mashaka na Madhubuti. Mwan-
zoni mwa riwaya mapenzi yake kwa lugha ya Kiswahili yanabainika kutokana na
msimamo unaolezwa na Amani kuhusu matumzi ya kilugha cha mjini cha sheng
alichozoea kukizungumza mhusika DJ. Anapokieleza anataja wazi kuwa kinakera
na anashangazwa na hali ya siku hizi ya wazee nao kujiunga na kundi la wakitu-
miacho na kuharibu sarufi ya Kiswahili. Msimamo wake unaelezwa hivi: “ … .
Hata hivyo, ana itikadi bado kwamba kilugha hiki dufu ni tishio kwa uhondo na
umilisi wa lugha” (uk. 5). Vilevile, tunaelezwa jinsi Mwalimu Majisifu alivyojipatia
sifa kutokana na umahiri wake katika utunzi wa kazi za fasihi. Ingawa baadaye
tunapata kuelewa hali halisi kwamba alikuwa anafanya njama za kuiba miswada
ya watu, ni bayana kuwa mwandishi anaonyesha kuwa mtu anaweza kufahamika
na kuinua hali yake ya kimaisha kutokana na utunzi wa kazi za fasihi ya Kiswahili.
Isitoshe, Majisifu aliipenda lugha na kupania kuitumia ipasavyo. Si ajabu alijulikana
kama Askari Polisi wa Sarufi kwa mazoea yake ya kukosoa wote waliovunja kanuni
za sasufi ya Kiswahili.
Amani alikuwa mtunzi msifika, tena mwenye kipawa cha hali ya juu. Alipenda
ushairi na kila mara alipokumbana na kadhia kubwa, alizieleza hisia zake kwa
kutumia utanzu huo. Hili linawekwa wazi anapomtungia marehemu mamake
shairi (uk. 33), alipotunga ubeti baada ya kifo cha Uhuru (uk. 110), na alipomwan-
dikia Mwalimu Majisifu ujumbe wa kishairi baada ya ukweli kuhusu mswada wake
kuwekwa wazi (uk. 143). Vilevile, nafasi muhimu ya Kiswahili katika jamii inajito-
keza kupitia kwa mazungumzo ya wahusika wawili katika ule mkutano mkubwa
wa kusherekea Sikukuu ya Wazalendo huko Sokomoko. Mmoja wao anaona
kuwa ingekuwa bora iwapo Mtemi Nasaba Bora angelisoma hotuba iliyotafsiriwa
katika Kiswahili badala ya Kiingereza ambacho waliohudhuria wengi hawakukie-
lewa (uk. 70). Anajibiwa kuwa anafanya hivyo kwa kufuata mfano wa Mtukufu
Rais wa Tomoko. Huu ni ukweli unaodhihirika hata leo ambapo wananchi wengi
huhudhuria mikutano na kusikiliza hotuba kisha wakarudi nyumbani bila ya
EASTERN AFRICAN LITERARY AND CULTURAL STUDIES 235

kuelewa kilichozungumziwa katika hotuba husika. Ukiwauliza kilichosemwa hawa-


takujibu na sababu kubwa ni matumizi ya lugha isiyoeleweka na wengi. Fauka ya
hayo, katika kazi hii, mwandishi ameonyesha kukerwa na tabia ya kuiba miswada
ya waandishi wa kazi za kubuni, jambo linaloonyesha namna anavyothamini
juhudi za waandishi na mchango wao, na kusikitikia wizi wa jasho lao.
Ken Walibora pia shairi la hivi karibuni, ambalo halijachapishwa, liitwalo “Lugha
Bora”. Katika shairi hili, mshairi anazungumza na Kiswahili kupitia kwa mbinu ya
uhaishaji na kusema angependa kukituma. Anakisihi kiwe imara, na kukitahadhar-
isha na maadui zake, kama vile wazungu weusi ambao wanakikwamiza kwa
kukosa kukitunza. Kwanza kabisa, anataka kiende kwa Kiingereza na kukifaha-
misha kuwa yeye si mtumwa wake tena na ameishakitema. Pili, kiende kwa
Kidachi na kukieleza kuwa manufaa yake ni kwa Wadachi lakini huku Uswahilini
hakina cheo. Baada ya hapo, anataka kiende kwa Kireno na kubainisha kuwa
kwa hakika Kiswahili kinakishinda kwa mambo mengi, kwa hivyo Kireno wala
hakina ushindani. Vivyo hivyo kikienda Uarabuni kifahamishe Kiarabu kuwa kwa
sasa kimepaa mno na wala hakilingani na hicho Kiarabu. Mwisho kiende Uchina
na kupasha habari Kichina kuwa hakikiogopi kamwe. Kiswahili kina ukwasi usio
kifani katika kufanikisha utunzi na wala hakistahili kubezwa na kutemewa mate.
Katika shairi hili la “Lugha Bora”, Walibora analinganisha Kiswahili na lugha
nyingine kubwa ulimwenguni, na maoni yake ni kuwa Kiswahili hakijapungukiwa
na chochote. Kwa hakika, msimamo wake ni kuwa kinazipiku hizo lugha nyingine.
Anakubali kuwa hizo nyingine ni muhimu kwa hao wazizungumzao, hivyo kuele-
kea kutuasa nasi kutokuwa Wazungu Kasoro rangi, bali tusimame imara kukienzi
na kukiendeleza Kiswahili, lugha yetu adhimu.

Maoni ya Wanafunzi na Walimu kuhusu Mchango wa Waandishi


Pamoja na mapitio ya maandishi ya waandishi waliorejelewa katika makala hii,
mwandishi vilevile alipata data kutoka kwa hojaji fupi ambayo ilijazwa na
walimu pamoja na wanafunzi wa Kiswahili. Walimu walioshiriki ni wanane wanao-
fundisha Kiswahili katika kaunti za Migori na Kisii, ambao pia ni walimu wa muda
wa Chuo Kikuu cha Rongo. Walimu hawa wote ni wanafunzi wa shahada ya
uzamili ama ya uzamifu katika chuo hicho. Mwalimu mmoja wa Chuo Kikuu cha
Rongo pia alishirikishwa. Vilevile, wanafunzi arobaini wa shahada ya kwanza
katika Kiswahili na katika Elimu walishiriki. Wote wamesoma kozi za isimu ya Kis-
wahili na fasihi yake. Kwa kuzingatia kigezo cha jinsia, miongoni mwa walimu kuli-
kuwa na wanawake wanne na wanaume wanne. Kundi la wanafunzi lilikuwa na
wanawake ishirini na nne na wanaume kumi na sita.
Hojaji iliyotumika ilikuwa na maswali saba yaliyonuiwa kupata habari kuhusu
nafasi ya waandishi wa kazi za kubuni katika kuiendeleza lugha ya Kiswahili.
Maswali yalikwa ya wazi ambayo yalimpa mhusika fursa ya kutoa maoni yake.
Swali la kwanza liliwaongoza kutoa taarifa kwa kutaja waandishi watatu wa fasihi
ya Kiswahili wanaowapenda zaidi, lengo likiwa kutaka kujua iwapo kuna waandishi
236 E. S. MOHOCHI

wanaowachangamkia na kuwathamini. Jumla ya wandishi kumi na tisa walitajwa.


Miongoni mwao, wawili walitajwa zaidi ya mara ishirini, mmoja mara kumi na
tisa, na wengine wote chini ya mara kumi. Watatu waliotajwa zaidi ni Ken Walibora
(ishirini na sita), S.A. Mohamed (ishirini na sita), na E. Kezilahabi (kumi na tisa).
Katika swali la pili, washiriki walitakiwa kutoa sababu za kuwapenda waandishi
waliowachagua. Swali hili lilinuiwa kuonesha kama kuna sababu ambazo zinato-
kana na mchango wa waandishi hao katika ukuzaji wa Kiswahili. Sababu zifuatazo
zilitolewa: wanashughulikia mambo muhimu na ibuka yanayotokea katika jamii
(kumi na saba); ukwasi wa lugha na ubunifu wa hali ya juu (kumi na moja); matu-
mizi mazuri ya lugha inayovutia (kumi); lugha inayoeleweka (sita); maswala ya
wanawake kupewa nafasi (tano), na kuimarisha msomaji kilugha (tatu). Majibu
manne kati ya haya sita yanahusu lugha moja kwa moja.
Pia, waliulizwa swali lifuatalo: unadhani waandishi wa fasihi wana mchango
wowote katika uendelezaji wa Kiswahili? Thelathini na mbili walisema kuwa waan-
dishi wana mchango ilhali wawil walisema hawana. Wengine hawakujibu swali
hilo. Swali lililofuata liliwataka waliosema kuwa waandishi wana mchango
waeleze waandishi wanavyochangia katika hilo. Majibu yalitolewa hivi: kuimarisha
lugha na kufanya wengi kuipenda (kumi na sita); kukuza ubunifu wa waandishi
chipukizi na wasomaji (kumi na tatu); matumizi ya msamiati mpya (saba); kusaidia
wasomaji kukuza lugha kwa kutumia msamiati unaokuza ujuzi na umilisi wao wa
lugha (kumi); na kuwasilisha maarifa mapya. Hapa inabainika kuwa kati ya majibu
matano, manne yanahusiana na swala la lugha.
Swali la tano lilihusu kueleza kama kuna mwandishi ambaye ameathiri mielekeo
na msimamo wao kuhusu lugha ya Kiswahili. Watoa taarifa ishirini na nne walisema
ndiyo na tisa wakasema hapana. Wengine hawakujibu swali hilo. Waliosema ndiyo
waliombwa kueleza walivyoathiriwa na mwandishi waliyemtaja. Majibu yalionesha
kuwa waandishi wanawaathiri kwa namna zifuatazo: kuwafanya wakipende Kiswa-
hili zaidi (kumi); kutambua umuhimu wa Kiswahili (saba); kuwachochea kuandika
kazi za fasihi (nne), kukosa kuelewa na hivyo kuanza kuchukia Kiswahili (moja). Hati-
maye, waliulizwa kutoa maoni ya kijumla kuhusu mchango wa waandishi. Wengi
wao walirudia hoja zilizokwishatolewa hapo juu kama vile, umuhimu wa waandishi
kuendelea kukuza msamiati, kuwamotisha waandishi chipukizi, kusambaza msa-
miati mpya na hivyo kukuza lugha ya Kiswahili. Kimsingi, linalobainika hapa ni
kuwa wanafunzi hawa wanawatambua waandishi wa kazi za kubuni kama wadau
walio na mchango mkubwa katika ukuzaji na uendelezaji wa lugha ya Kiswahili.
Hali haikuwa tofauti sana katika kundi la walimu. Kuhusu waandishi watatu wa
Kiswahili wanaowapenda zaidi, waandishi kumi walitajwa. Waliotajwa mara
nyingi ni: Ken Walibora (sita), S.A. Mohamed (tano), na Katama Mkangi na Euphrase
kezilahabi waliotajwa mara tatu kila mmoja. Adam Shafi alitajwa mara mbili, na
wengine watano wakatajwa mara moja. Sababu za kuwapenda waandishi hao zili-
tolewa pia ifuatavyo: wanashughulikia maswala ya kihalisia yanaoikumba jamii
(saba); mtindo wao mzuri wa uandishi (tano); ubunifu wao pamoja na ukwasi wa
lugha wa hali ya juu (tatu); kulimulika swala la nafasi ya wanawake (mbili); matumizi
EASTERN AFRICAN LITERARY AND CULTURAL STUDIES 237

ya lugha inayoeleweka (mbili), na utetezi wa Kiswahili sanifu (moja). Kinachobainika


hapa ni kuwa majibu manne kati ya sita yanalenga lugha moja kwa moja.
Walimu wote wanane walijibu swali la tatu kwa kukubali kuwa waandishi wana
mchango katika uendelezaji wa Kiswahili. Walisema wanachukua msimamo huo
kwa sababu waandishi hao wanachangia msamiati mpya katika lugha (nne),
wanaimarisha lugha na kuwafanya wengi kuipenda (tatu), wanakuza ubunifu wa
waandishi wanagenzi (tatu), na huwasaidia wasomaji kukuza uwezo wao wa
lugha (tatu). Walimu wote walikubali kuwa kuna mwandishi ambaye amewaathiri.
Walikiri kwamba wameathiriwa kwa njia tofauti kama vile: kukuza matumizi yao ya
lugha (tatu), kumakinika zaidi katika matumizi yao ya Kiswahili (mbili), kuanza
kujiingiza katika bahari ya utunzi wa fasihi (mbili), kugundua kuwa Kiswahili ni
lugha yenye umuhimu mkubwa katika jamii (mbili), na kukipenda zaidi Kiswahili
pamoja na fasihi yake (moja). Kuhusu maoni yao ya jumla kuhusiana na
mchango wa waandishi walikuwa na majibu yale yale: wanakuza Kiswahili
(tano); wanachonga vipawa vya waandishi wengine (tatu); kuchangia msamiati
(mbili), na kuinua hadhi ya Kiswahili (moja).
Walimu na wanafunzi wa Kiswahili walioshiriki katika utafiti huu wanakubaliana
kwa kiasi kikubwa kuwa waandishi wa kazi za fasihi wanatoa mchango mkubwa
katika uendelezaji wa Kiswahili. Pia, wana athari kubwa kwa wasomaji wao, na ni
wadau muhimu katika mchakato mzima wa ukuzaji wa lugha. Kwa kuzingatia
mawazo yanayotolewa katika nadharia ya ushawishi wa kijamii, waandishi hawa ni
wadau muhimu wa kushirikiana na makundi mengine yanayohusika kwani wana
umaarufu unaoweza kuchangia maendeleo endelevu ya lugha ya Kiswahili.
Waandishi wamedhihirisha mchango wao katika uendelezaji wa Kiswahili, na
athari yao kuhusu hili katika jamii kwa njia zifuatazo: uamuzi wa kukitumia katika
maandishi yao hivyo kuchangia kwenye hazina ya maandishi ya Kiswahili; kuifanya
lugha ya Kiswahili na umuhimu wake katika jamii kuwa sehemu ya maudhui
wanayoyajadili; kuwasawiri wahusika mbalimbali wanaodhihirisha mapenzi kwa
lugha ya Kiswahili na wanaopata ufanisi maishani kutokana na lugha hiyo; kuchan-
gia katika ufundishaji wa lugha kwani kazi za fasihi ni malighafi muhimu katika
taaluma hiyo, na kuwamotisha waandishi chipukizi. Wahusika wa kazi za Ken Wali-
bora, kama vile Zainabu Makame, Juma Mukosi, Amani, na Kongowea, miongoni
mwa wengine, wanaathiri wahusika wenzao na kuwafanya watambue umuhimu
wa lugha ya Kiswahili. Waandishi wote watatu wanaathiri wasomaji wao kuitizama
lugha ya Kiswahili kama silaha muhimu katika maendeleo ya kibinafsi, ya kitaifa, na
ya kieneo. Pia, maoni ya walimu na wanafunzi yametufunulia ukweli kuwa wasomaji
wa kazi za fasihi huathiriwa na kazi hizo kwa namna mbalimbali.

Hitimisho
Makala hii imelishughulikia swala la mchango wa waandishi wa kazi za kubuni
katika uendelezaji wa lugha ya Kiswahili kwa kujikita katika nadharia ya ushawishi
wa kijamii. Sehemu ya mwanzo imeeleza dhana ya ushawishi wa kijamii. Kimsingi
238 E. S. MOHOCHI

imebainishwa kuwa katika maisha yetu ya kila siku, kuna hali nyingi za kuathiriana
baina ya wanajamii. Wapo wanaotuathiri na tunaowaathiri. Mtagusano wetu ume-
jengeka kwenye mahusiano ya kuathiriana. Mjadala wa nafasi ya waandishi katika
jamii, hasa waandishi wa fasihi, umeshughulikiwa. Kwa jumla, imefafanuliwa kuwa
maandishi na waandishi huchangia sana katika maendeleo ya jamii. Hii ni kwa
sababu waandishi huyaweka maarifa katika hali ya kuweza kuwafikia watu
wengi zaidi na hivyo kutoa elimu na burudani miongoni mwa mambo mengine.
Mjadala uliegemea pia mchango wa waandishi wa kazi za kubuni katika uende-
lezaji wa Kiswahili. Makala imejikita katika uchanganuzi wa kazi za waandishi
watatu ili kudhihirisha jinsi waandishi wanavyochangia katika kuikuza lugha.
Katika kulishughulikia hili, makala imezingatia aina mbalimbali za mchango wao
kama waandishi wa kazi za fasihi ya Kiswahili.
Sehemu ya mwisho imejadili maoni ya walimu na wanafunzi wa Kiswahili kuhusu
mchango wa waandishi wa kazi za kubuni katika uendelezaji wa Kiswahili. Imebai-
nika kuwa waandishi wa kazi za kubuni wana umaarufu katika jamii, ambao huwa-
fanya kuwa na ushawishi mkubwa sana. Kutokana na hilo, wana uwezo wa kuathiri
watu wengi. Wanapotokea kuwa watetezi wakubwa wa lugha ya Kiswahili na kuji-
husisha katika uandishi wa kazi katika lugha hiyo na wanaposhiriki katika shughuli
nyingine za kuiendeleza, wanakuwa mawakala muhimu wa lugha yenyewe.

Marejeleo
Abdulaziz, H.M. (1979). Muyaka: 19th Century Popular Swahili Poetry. Nairobi: EAEP.
Aboh, R. (2015). “Talking” Igbo, “Writing” English: Nigerianism in the Concubine, katika A.
Odebunmi & J.T. Mathangwane (wh.), Essays on Language, Communication and Literature in
Africa. Newcastle-upon-Tyne: Cambridge Scholars Publishing. Iliyopakuliwa kutoka from
https://ebookcentral.proquest.com/lib/rucke-ebooks/detail.action?docID = 4648739
Friedkin, N.E. (1998). A Structural Theory of Social Influence. Cambridge: Cambridge University
Press.
Goldsmith, E.B. (2015). Social Influence and Sustainable Consumption. International Series on
Consumer Science, DOI 10.1007/978-3-319-20738-4_2
Mayhew, L.H. (1997). The New Public: professional communication and the means of social
influence. Cambridge: Cambridge University Press.
Mlamali, M. (1980). Al Inkishafi: Sayyid Bin Ali Bin Nasir. Nairobi: Longman.
Momanyi, C. (2006). Tumaini. Nairobi: Vide-Muwa Punlihsres.
Ngugi Wa T. (1986). Decolonising the mind: the politics of language African literature. Nairobi:
Heinemann Educational Publishers.
Ngugi Wa T. (1992). Petals of Blood. Nairobi: East African Educational Publishers.
Robert, S. (2016). “Titi la Mama”, Katika Jahadhmi’s anthology of Swahili poetry. Iliyorejelewa
kutoka http://www.mwambao.com/mashairi.htm
RUC, 01/09/16
Walibora, K. (1996). Siku Njema. Nairobi: Longhorn Publishers.
Walibora, K. (2001). Ndoto ya Amerika. Nairobi: Sasa Sema Publishers.
Walibora, K. (2016). “Lugha Bora”, Shairi ambalo halijachapishwa.
Wallah, B.W. (1988). “Tutukuze Kiswahili”, katika Malenga wa Ziwa Kuu. Nairobi: Heinemann
Kenya Limited.

View publication stats

You might also like