Professional Documents
Culture Documents
Uchanganuzi Matini
Uchanganuzi Matini
Kwa mujibu wa King’ei (2010), anafafanua muktadha kuwa ni ile hali inayotawala na kuelekeza
matumizi ya lugha inayozungumzwa. Kwa mfano mahali, wakati, hadhira na kusudio la
msemaji. Halikadhalika katika lugha ya mazungumzo wazungumzaji wengi hushawishika
kutumia aina fulani ya lugha kulingana na muktadha fulani ambao hutoofautiana na muktadha
mwingine. Hali hii inaonesha kuwa kuna mambo fulani ambayo huwafanya wazungumzaji wa
lugha wateue msamiati fulani katika mazungumzo yao unaolingana na muktadha walipo wakati
huo.
Hali kadhalika Msanjila na wenzake (2011), wanasema kuwa mawasiliano yanaweza kuwa
katika muktadha wa mazungumzo au maandishi, na matumizi ya lugha katika muktadha hubeba
mawasiliano kwa wanajamii. Vilevile SwahiliHub (26/6/2016), wakimrejelea Austin (1962),
wanasema kuwa ni muhimu kuhusisha matumizi ya lugha na muktadha wake wa kijamii kwani
lugha huwa na matumizi tofauti kama vile kutoa mapendekezo, kuahidi, kukaribisha, kuomba,
kuonya, kufahamiana, kuagiza, kukashifu, kusifu na kuapiza. Kwa ujumla tunaona kuwa
muktadha ni mazingira au hali ambamo tukio au jambo hutendeka.
Kamusi teule ya Kiswahili, (2013) matini ni maelezo kuhusu jambo lolote lile ambalo
limeandikwa au kunakiliwa. Kwa mfano, hotuba na magazeti.
Kwa mujibu wa Massamba (2009), anaeleza kuwa matini ni maelezo ya kitu ambayo ama
yameandikwa na mtu au yamenukuliwa na ambayo yamekusudiwa kutumiwa kwa maksudi
maalum.
Kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake, (1996) matini huweza kuainishwa kwa kufuatana na
mada, kwa kutumia kigezo hiki tunapata aina kuu tatu za matini ambazo ni matini za kifasihi,
kisiasa na kisayansi.
Kwa ujumla, matini ni wazo au mfulilizo wa mawazo ambao hujitosheleza kimaana na ambao
unahitaji kutafsiriwa. Kwa hivyo, matani yaweza kuwa neno, kirai, kishazi, sentensi aya au
kifungu cha habari.
Baada ya kufafanua kwa kifupi maana ya dhana zilizojitokeza katika swali hili, tunajikita
kwenye kiini cha swali ambapo tunapaswa kueleza umuhimu wa kipengele cha muktadha katika
kufanikisha mawasiliano kuwa bora na thabiti. Zifuatazo ni baadhi ya hoja zinazoshadidia
umuhimu wa kipengele hiki:
Husaidia kutambua mtindo unaofaa kuwasilishia ujumbe, wakati msemaji anatambua muktadha
na mazingira aliyomo, moja kwa moja atatambua ni mtindo upi autumie kuwasilisha ujumbe
wake kwa wasikilizaji au hadhira. Mwansoko (1994:22), anabainisha namna muktadha unaweza
kusaidia kutambua mtindo. Mfano, katika mtindo wa kitaaluma msemaji anaweza kuzingatia
utaratibu maalumu wa uandishi wa marejeleo ya vitabu, makala, magazeti na majarida. Kwa
mfano, uandishi wa rejeleo la kitabu ambacho kimeandikwa na mwanaisimu Bloomfield
unapaswa kuanza na jina la ubini, jina lake, mwaka, jina la kitabu, mahali kilipochapishwa na
wachapishaji. Hivyo, hata kwa wazungumzaji wa miktadha mingine kama ya dini au siasa,
mzungumzaji atatumia mtindo unaoendana na sehemu hiyo ya ibada au uwanja wa siasa.