You are on page 1of 26

NOVENA YA ROHO

MTAKATIFU
Sala na Nyimbo Kwa Siku
Zote Tisa

Kimetolewa na AckySHINE.com
Toleo Na: 4, 2016
Mhariri: Melkisedeck Leon Shine Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

YALIYOMO
MWONGOZO WA KUSALI NOVENA YA ROHO MTAKATIFU KWA
SIKU ZOTE TISA ........................................................................... 2
BAADHI YA NYIMBO KWA ROHO MTAKATIFU ............................... 2
NJOO WANGU MFARIJI ................................................................................... 2
NJOO ROHO MTAKATIFU ................................................................................. 2
UJE ROHO (SEKWENSIA) ................................................................................ 3
NJOO ROHO MTAKATIFU ................................................................................. 3
SALA ZA NOVENA YA ROHO MTAKATIFU ...................................... 4
SIKU YA KWANZA: IJUMAA - Roho Mtakatifu Anatufariji ...................................... 4
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA PILI: JUMAMOSI - Roho Mtakatifu
Anatusaidia Kueneza Injili ............................................................................... 6
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA TATU: JUMAPILI - Roho Mtakatifu
Anatufanya Kuwa Mitume ................................................................................ 8
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA NNE: JUMATATU - Roho Mtakatifu
Analiunganisha Kanisa .................................................................................. 10
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA TANO: JUMANNE - Roho Mtakatifu
Anawatakasa Waumini .................................................................................. 12
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA SITA: JUMATANO - Roho Mtakatifu Anatupa
Nguvu ........................................................................................................ 14
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA SABA: ALHAMISI - Roho Mtakatifu Anatupa
Hekima ....................................................................................................... 16
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA NANE: IJUMAA - Roho Mtakatifu Anatupa
Mwanga. ..................................................................................................... 18
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA TISA: JUMAMOSI - Roho Mtakatifu Anatupa
Mapendo ..................................................................................................... 20
LITANIA YA ROHO MTAKATIFU .................................................. 22
MWISHO WA KITABU ................................................................. 24
UJUMBE WA MHARIRI ................................................................................... 24

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 1


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

MWONGOZO WA KUSALI NOVENA YA ROHO MTAKATIFU KWA


SIKU ZOTE TISA

Ufuatao ni mtiririko wa Novena ya Roho Mtakatifu kwa siku zote tisa.

Kusali novena hii unaanza nia wimbo/nyimbo kisha unasali sala ya kila siku na
kumalizia na litania na Atukuzwe Baba….x3 kwa siku zote tisa.

BAADHI YA NYIMBO KWA ROHO MTAKATIFU


NJOO WANGU MFARIJI

/Njoo wangu Mfariji


Yako shusha mapaji
Roho Mungu njoo/

1. Hekima nishushie, Mungu nimfuatie, Roho Mungu njoo


2. Akili nijalie, imani nizidie, Roho Mungu njoo
3. Nieneze shauri, imani nizidie, Roho Mungu njoo
4. Nizidishie nguvu, nsifanye ulegevu, Roho Mungu njoo
5. Elimu nieleze, hakika niongoze, Roho Mungu njoo
6. Ibada niwashie, Peke nikupupie, Roho Mungu njoo
7. Uchaji nitilie, dhambi nizichukie, Roho Mungu njoo.

NJOO ROHO MTAKATIFU

/Njoo Roho Mtakatifu, shusha mapaji (kweli) niwe imara x2


Leta nuru ya mwanga wako, ifikie moyoni mwangu x2/

1. Roho mwenye hekima, Roho wa shauri na nguvu


2. Nipatie elimu nitambue nafsi yako
3. Nipatie ibada nikusifu daima milele
4. Roho mwenye uchaji washa moto wako wa mapendo

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 2


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

UJE ROHO (SEKWENSIA)

1. Uje Roho Mtakatifu, tuangaze toka mbingu, roho zetu kwa mwangao
2. Uje Baba wa maskini, uje mtoa wa vipaji, uje mwanga wa mioyo
3. Ee Mfariji mwema sana, ee Rafiki Mwanana, ewe raha mustarehe
4. Kwenye kazi u pumziko, kwenye joto burudisho, u mfutaji wa machozi
5. Ewe mwanga wenye heri, uwajaze waumini, neema yako mioyoni
6. Bila nguvu yako Wewe, mwanadamu hana kitu, kwake yote yana kosa
7. Osha machafuko yetu, panyeshee pakavu petu, na kuponya majeraha
8. Ulegeze ukaidi, pasha moto ubaridi, nyosha upotovu wote
9. Wape waamini wako, wenye tumaini kwako, paji zako zote saba
10. Wape tuzo ya fadhila, wape mwisho bila hila, wape heri ya milele.
11. Amina aleluya, amina aleluya, amina aleluya.

NJOO ROHO MTAKATIFU

1. Njoo Roho Mtakatifu, angalia zetu nyoyo, waletee neema nguvu, wakosefu
viumbevyo.
2. Majina yako Mfariji, shina la uzima pendo, wake Mwenyezi upaji, mafuta ya roho
moto
3. Ndiwe mnye mapaji saba, wa Mungu kuume mkono, mshika uhadi wa Baba, mtoa
kwa ndimi maneno
4. Angalo litung’arie, moyo kwa pendo tushushe, nguvu neema tujalie, wanyonge
wasabilitishe
5. Shetani mbali mkimbize, amani utupatie, tukufuate tuongoze, maovu utukingie
6. Baba Mungu tujulishe, pia Mwana tumkubali, Roho tukuungamie, mtokea wao
wawili.

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 3


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

SALA ZA NOVENA YA ROHO MTAKATIFU


SIKU YA KWANZA: IJUMAA - Roho Mtakatifu Anatufariji

Yesu alipokuwa akiagana na mitume wake, kabla ya kupaa mbinguni, aliwaambia


wasiondoke Yerusalemu mpaka hapo watakapokuwa wamempokea Roho Mtakatifu.
Aliwaambia: “Wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni, mtajazwa nguvu, nanyi
mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika nchi yote ya Yuda na Samaria,
hata kwenye mipaka yote ya dunia.” (Mdo.1:8)
Waliendelea kusali pamoja toka hapo Yesu alipopaa mbinguni mpaka siku ya
Pentekoste. Waliomba Roho Mtakatifu awashukie, awajaze na mapaji yake. Na baada
ya siku tisa Roho Mtakatifu aliwashukia hao kundi dogo nao wakawa chanzo cha Kanisa
lililopata kuenea duniani kote.
Siku hizo tisa za kusali zinaitwa NOVENA; na kila mwaka wakati huu, wakristu wakifuata
mfano wa mitume, wanasali muda wa siku tisa kabla ya Sikukuu ya Pentekoste.
Wanamuomba Roho Mtakatifu awashukie, awajaze nguvu na wingi wa mapaji yake.
Wakati huu wa NOVENA, Tunayo mengi ya kuliombea Kanisa na kujiombea sisi
wenyewe. Kwa hiyo tumuombe Roho Mtakatifu atusaidie kusali vema na kuomba yale
yote tunayohitaji kwa maslahi yetu ya roho na mwili.
Na kama mtume Paulo alivyowaambia wale waKristu wa kwanza, Roho Mtakatifu huja
kutufatiji katika udhaifu wetu. Basi tumuombe atufariji kwa sala hizi za NOVENA,
Atuwezeshe kusali na kuomba inavyotupasa kusali.

1. Ee Baba wa milele, tunakuomba umtume Roho Mtakatifu atushukie sisi taifa lako
awashe ndani yetu moto wa upendo wako.
W. Twakuomba utusikie.

2. Ee Baba mwema, tunakuomba utujalie faraja ya Roho Mtakatifu sisi wana tulio
katika dhiki na taabu nyingi mno hapa duniani.
W. Twakuomba utusikie.

3. Ulijalie Kanisa lako mapaji ya Roho wako Mtakatifu, liweze kutekeleza vema utume
wake wa kuhudumia watu wote hapa duniani.
W. Twakuomba utusikie.
4. Utujalie sisi kudumu katika NOVENA hii mpaka mwisho kama Maria na mitume
walivyodumu pamoja wakisali kabla ya Pentekoste ile ya kwanza.
W. Twakuomba utusikie.

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 4


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

5. Utujalie neema zote zinazohitajika ili tuweze kumshuhudia Kristu popote kwa
mwenendo na matendo yetu ya kila siku, tukiongozwa na Roho Mtakatifu.
W. Twakuomba utusikie

6. Uzijalie familia zote za wakristu neema na nguvu za Roho Mtakatifu tupate


kuendelea pasipo kuchoka katika sala na katika matendo mema siku zote.
W. Twakuomba utusikie

7. Ewe Roho Mtakatifu, uwajalie vijana wetu moyo wa ujasiri, wapate kulijenga kanisa
lako na kueneza utawala wako katika jumuia zetu za Kikristu.
W. Twakuomba utusikie.

TUOMBE;
Ee Mungu, uliye muumba wa vitu vyote, tunakuomba utusikilize kwa wema sala zetu
sisi taifa lako, utuongoze sote tufuate siku zote utaratibu wa mapenzi yako; naye
Roho Mtakatifu atutegemeze mpaka mwisho wa novena hii. Tunaomba hayo kwa njia
ya Kristu Bwana wetu.
W. Amina.

LITANIA YA ROHO MTAKATIFU … (soma hapo chini)

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 5


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA PILI: JUMAMOSI - Roho Mtakatifu


Anatusaidia Kueneza Injili

“Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika
utawala wa Mungu,” (Yn. 3:5).
Kanisa limepewa na Yesu ujumbe wa kuwaletea watu wote uzima mpya, uzima wa
Mungu. Yesu aliwaambia mitume wake: “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na
duniani. Nendeni basi mkawafanye watu wa makabila yote kuwa wafuasi wangu.
Wabatizeni kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Wafundisheni kuyashika
maagizo yote niliyowapeni. Nami nipo pamoja nanyi siku zote mpaka mwisho wa
nyakati (Mt.28: 18-20).
Sisi tuliobatizwa tumepata kuwa viungo vilivyo hai vya Mwili wa Fumbo wa Kristu; kwa
Kipaimara tumeimarishwa na kuthibitishwa na Roho Mtakatifu. Tumekuwa taifa teule.
Tumeshirikishwa ule ukuhani wa Kristu. Tumepokea ujumbe wa kueneza utawala wa
Mungu.
Tunapopokea Sakramenti, na hasa ile Sakmenti ya Ekaristi, tunalisha imani na
kuongeza mapendo, ambayo ni msingi wa utume wowote ule. Mapendo yanatuhimiza
kueneza utawala wa Mungu na kumpenda Yesu Kristu aliyekuja kuwakomboa
wanadamu wote.
Kila aliyebatizwa anao wajibu wa kueneza imani ya Mungu na utawala wake. Kwa hiyo
tumuombe Roho Mtakatifu atuwezeshe kutimiza wito huo.

1. Ee Baba wa mbinguni tunakuomba umpeleke Roho Mtakatifu aliangaze kanisa na


kuliongoza, liweze kuwafikishia mataifa yote habari njema ya wokovu.
W. Twakuomba utusikie

2. Ee Yesu Mkombozi wetu, umtume Roho Mtakatifu awahimize wakristu wapate


kutimiza wajibu wao wa kueneza neno lako popote duniani
W. Twakuomba utusikie

3. Ewe Roho Mtakatifu Mfariji, uamshe katika mioyo ya vijana wengi hamu ya
kupenda kulitumikia kanisa lako na kulihudumia taifa lako kwa uaminifu.
W. Twakuomba utusikie

4. Ewe mwanga wa mataifa , uwajalie wanafunzi wasikie sauti yako mioyoni mwao,
nawe unapowaita wasikose kuisikia sauti yako, wawe tayari kujitoa kwa ajili ya ndugu
zao.
W. Twakuomba utusikie.

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 6


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

5. Uwasaidie wazazi wawalee vema watoto wao; uwatie moyo katika wito wao,
wapate pia kuishiriki vema ile kazi ya kueneza neno lako kwa jirani zao.
W. Twakuomba utusikie

6. Ewe Roho Mtakatifu, uwasaidie wakristu wote kueneza habari njema ya wokovu,
kwa sala, kwa sadaka na kwa mifano ya maisha yao ya uchaji.
W. Twakuomba utusikie

7. Ewe mpaji wa mema, uwajalie waumini mapaji yako saba, wasichoke kulieneza
neno lako kwa hekima pasipo hofu.
W. Twakuomba utusikie.

TUOMBE;
Ee Mungu, unapenda watu wote waokoke, waifikie kweli yako. Tunakuomba uwapeleke
wafanyakazi walio wengi na wema katika shamba lako. Uwajalie kulihubiri neno lako
kwa imani kuu ili neno lako lienee na kupokewa na mataifa yote, wapate nao kukujua
wewe peke yako Mungu wao, Mungu wa kweli. Tunaomba hayo kwa nguvu ya Roho
Mtakatifu anayeliongoza kanisa lako sasa na milele.

W. Amina

LITANIA YA ROHO MTAKATIFU … (soma hapo chini)

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 7


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA TATU: JUMAPILI - Roho Mtakatifu


Anatufanya Kuwa Mitume

Bwana alisema kwa kinywa cha nabii Yoeli; “Katika siku zile za mwisho asema Bwana,
nitawamiminia binadamu wote Roho wangu. Watoto wenu, waume kwa wake,
watautangaza ujumbe wangu; vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota
ndoto….hata watumishi wenu watamiminiwa Roho wangu katika siku zile, nao
watautangaza ujumbe wangu. (Mdo.2:17-21)
Siku ile ya Pentekoste, bada ya Roho Mtakatifu kulishukia kanisa, mitume
waliwakumbusha watu maneno haya ya nabii Yoeli, na miaka mingi baadae, Petro
aliwaandikia barua Wakristu wa kwanza akawaambia; kila mmoja anapaswa kutumia
kipaji alichojaliwa na Mungu kwa faida ya wengine, kama vile wakili mwema wa zawadi
mbali mbali za Mungu. Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya
Mungu; anayetumikia anapaswa kutumikia kwa nguvu aliyojaliwa na Mungu ili katika
mambo yote, Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristu, ambaye utukufu na nguvu ni
vyake milele na milele (Pet 4;10-11).
Mtaguso wa Pili wa Vatikano ulitukumbusha jambo hilo hilo uliposema; “Roho Mtakatifu
anayetakasa taifa la Mungu kwa njia ya Sakramenti amewapa waumini mapaji ya pekee
na kumjalia kila mmoja kadiri apendavyo. Kwa hiyo kila mmoja amgawie mwenzake
kadiri ya vipawa alivyopewa, awe mgawaji mwaminifu wa neema ya Mungu, alijenge
kanisa zima katika upendo.
Tunao wajibu wa kutumia vipawa tulivyojaliwa na Roho Mtakatifu kwa manufaa ya
kanisa zima, na kwa faida ya watu wote. Tuunganike sote pamoja na wachungaji wote
katika kazi hiyo ya utume. Tumuombe basi Roho Mtakatifu atusaidie kutumia vema
vipawa vyake alivyotujalia.

1. Ewe Roho Mtakatifu uwape wakristu neema na nguvu za kutumia vema vipaji
ulivyowajalia kwa ajili ya kujenga kanisa lako popote duniani, kwa ajili ya wokovu wa
watu wote
W. Twakuomba utusikie

2. Utujalie sisi sote mapaji yako saba, tupate kukutumikia kwa uchaji
W. Twakuomba utusikie

3. Utujalie tuwe mitume wa kweli wa wenzetu, tushirikiane na wachungaji wetu katika


huduma za kuwaongoza watu wote na kuwafikisha mbinguni
W. Twakuomba utusikie.

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 8


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

4. Utujalie hekima na nguvu za kuwahudumia watu wote kwa mapendo ya kweli


yasiyo na kinyume
W. Twakuomba utusikie

5. Utujalie neema ya kumpenda Mungu kwa moyo wote na kuwapenda jirani zetu
kama tunavyojipenda wenyewe
W. Twakuomba utusikie

6. Utupe neema ya kulisikia neno lako na kulifuata, nayo mawazo yetu na matendo
yetu yafuate daima mwongozo wako mtakatifu
W. Twakuomba utusikie

7. Uwazidishie mapaji yako wale wote wanaotumia vyema vipawa vyao, uwarudishe
na wale wanaotumia vibaya rehema zako
W. Twakuomba utusikie

TUOMBE;
Ewe Roho Mungu ndiwe uliyewapa waumini vipawa vyako kwa kadiri unavyotaka.
Utujalie tuyapokee na kuyatumia vyema mapaji yako mengi kwa ajili ya utukufu wa
Jina lako na kwa ajili ya wokovu wa watu wote. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu
Bwana wetu.
W. Amina

Litania ya Roho Mtakatifu …. (soma hapo chini)

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 9


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA NNE: JUMATATU - Roho Mtakatifu


Analiunganisha Kanisa

“Atakapokuja huyu Roho wa kweli, atawaongoza kwenye ukweli wote” (Yn 16:13)
Baada ya kusema hayo, Yesu aliinua macho yake kuelekea mbinguni akasema “Mimi
nimekutukuza hapa duniani; nimeikamilisha kazi uliyonipa niifanye. Naomba ili wote
wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba Wewe ulinituma (Yn
17:4,21).
Nasi twamuomba Mungu Mwenyezi alijalie kanisa lake umoja wa kweli, awaunganishe
wakristu wa madhehebu yote katika zizi moja chini ya mchungaji mmoja.
Popote duniani watu wengi, makundi kwa makundi wanavutwa na neema hiyo ya
kuungana na kuufikia umoja wa Kanisa. Hata ndugu zetu waliotengana nasi wanazidi
kukubali mwongozo wa Roho Mtakatifu na kutaka kurudi katika nyumba ya Baba na
kuwa kundi moja chini ya mchungaji mmoja. Isitoshe, hata sasa tena twaweza kuona
kwamba kwa namna fulani wamejiunga nasi katika Roho Mtakatifu, naye Roho
Mtakatifu anafanya kazi ndani yao kumshuhudia hata kwa kumwaga damu yao.
Tena katika hao ndugu zetu waliojitenga, Roho Mtakatifu analisha katika mioyo yao ile
ya imani inayowaunganisha wafuasi wote wa Kristu. Tumwombe basi Mwenyezi Mungu
atujalie hima huo umoja wa Kanisa lake tunaouania mno.

1. Ee Yesu Bwana wetu wewe umetuombea kwa Mungu Baba tuwe itu kimoja kama
Wewe ulivyo kitu kimoja na Baba. Utujalie huo umoja, ili ulimwengu uone na kukiri
kwamba ndiwe Bwana na Mkombozi wa watu wote
W. Twakuomba utusikie

2. Ee Yesu utujalie moyo wa kulishika neno lako kwa uaminifu, wala usituache
kufuata njia zetu sisi wenyewe na kufarakana.
W. Twakuomba utusikie

3. Ee Yesu uliye Mchungaji wetu mwema, ondoa ndani yetu ile tabia ya utengano,
tupate kuwa sote kundi moja chini yako wewe uliye mchungaji wetu mmoja.
W. Twakuomba utusikie

4. Ee Yesu, uliye Mchungaji mkuu, uwajalie wachungaji wetu wawe siku zote na
upendo wa Jina lako, wasichoke kulichunga vema kundi lako hapa duniani na
kuliweka pamoja lisitengane
W. Twakuombaa utusikie

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 10


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

5. Ewe Roho Mtakatifu, uziangaze akili za watu wote, wapende siku zote kuishi kwa
amani, umoja na mapendano
W. Twakuomba utusikie

6. Ee Mungu, utufungulie …… wa muungano wako wa kweli sisi tulio ndugu katika


Bwana wetu Yesu Kristu.
W. Twakuomba utusikie

7. Utujalie mapatano na amani, tudumu tumeungana katika familia zetu, katika jimbo
letu na katika nchi yetu yote.
W. Twakuomba utusikie.

TUOMBE;
Ee Mungu, utuunganishe sisi kondoo wako tuliotawanyika, tuwe chini ya Mwanao
mpenzi, tupate sote kuushiriki ule utawala wako wa kweli na haki, utawala wa neema
na amani, utawala wa upendo wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu
W. Amina

LITANIA YA ROHO MTAKATIFU …. (soma hapo chini)

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 11


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA TANO: JUMANNE - Roho Mtakatifu


Anawatakasa Waumini

Walio wa Mungu watafuata yaliyo ya Mungu, na walio wa dunia hufuata yaliyo ya dunia,.
Ni mauti kutosheka na mambo yaliyo ya dunia. Uzima na faraja ya kweli hupatikana tu
katika mambo ya Mungu.
Kwa nguvu zetu sisi wenyewe hatuwezi kutenda lolote jema. Kuweza kwetu kwatoka
kwa Mungu, kwatoka kwa Yeye anayetupa kujua, kupenda na kutenda.
Mtu anapotenda dhambi, hawezi kuongoka ila kwa msaada wa Roho Mtakatifu, ndiye
anayempa mkosefu neema ya kutambua ubaya wa kosa lakena kuamua kuliacha. Ndiye
anayempa pia mkosefu kutambua uzuri wa neema aliyoipoteza na kumrudishia neema
hiyo. Ndiye anayempa nguvu za kuidumisha neema hiyo na kuiongeza.
Isitoshe, Roho Mtakatifu ndiye anayemuwezesha mtu kuwa na maendeleo katika
fadhila na utakatifu. Ndiye anayemjalia imani iliyo msingi wa maisha ya kiKristu. Ndie
anayetujalia akili ya kushika mafumbo ya dini yetu na kuishi imani yetu mpaka kufa.
Lakini imani peke yake haimtoshi mtu aokoke. Imani pasipo matendo haifai kitu; imani
bila matendo imekufa (Yak 2:28) Roho Mtakatifu anamuwezesha mtu kumuamini
Mungu na kumenda kuliko vitu vyote na kumpenda jirani kama kujipenda mwenyewe.
Ndiyo maana Roho Mtakatifu huitwa chanzo cha matendo yetu yote yaliyo mema. Basi,
tumuombe Roho Mtakatifu aitakase mioyo yetu sisi waumini wake, atuzidishie imani,
atuwezeshe kutenda matendo yaliyojaa imani.

1. Ewe Roho Mtakatifu, utudumishie imani, uyatakase mawazo ya mioyo yetu yafuate
daima maongozi yako na amri zako
W. Twakuomba utusikie

2. Uzigeuze nia zetu zipate kumuelekea daima Mungu


W. Twakuomba utusikie

3. Utuwezeshe kuelekea katika utakatifu na kutenda mema kwa imani siku zote za
maisha yetu
W. Twakuomba utusikie

4. Utuzidishie imani matumaini na mapendo, tuweze kushika kwa moyo thabiti yale
yote tunayofundishwa na kanisa lako takatifu
W. Twakuomba utusikie

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 12


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

5. Uiwashe mioyo yetu na moto wa mapendo yako, tupate kumpenda Mungu kweli na
kumpenda jirani yetu pasipo unafiki.
W. Twakuomba utusikie

6. Utusaidie tuishi vema kwa imani na matumaini siku zote za maisha yetu
W. Twakuomba utusikie

7. Utujalie kudumisha mioyoni mwetu ile neema ya utakaso tuliyoipata mwanzo


katika ubatizo wetu
W. Twakuomba utusikie

TUOMBE;
Ee Mungu, mbele yako mioyo yetu i wazi; wewe wayajua yote, wala hakuna siri
iliyofichika mbele yako. Uyatakase mawazo ya mioyo yetu kwa kutupelekea Roho
Mtakatifu, ili tuweze kukupenda na kukutukuza kama inavyostahili. Tunaomba hayo
kwa njia ya Kristu Bwana wetu
W. Amina

LITANIA YA ROHO MTAKATIFU … (soma hapo chini)

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 13


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA SITA: JUMATANO - Roho Mtakatifu


Anatupa Nguvu

“Nitamuomba Baba, naye atawapelekea Mfariji mwingine atakaye kaa nanyi siku zote”.
Katika maisha yenu hapa duniani tunahitaji mno kitulizo cha Mungu. Ni jambo la hekima
kutafuta kitulizo hicho kwa Mungu wala si kwa viumbe; maana kitulizo kinachopatikana
kwa viumbe hapa duniani hakidumu; bali kitulizo kitokacho kwa Mungu ni cha kudumu.
Roho Mtakatifu ndio kitulizo chetu cha kweli. Baba ndiye aliyetuumba, Mwana ndiye
aliyetukomboa, Roho Mtakatifu ndiye aliyetutakasa mioyo yetu na kutufariji.
Kazi ya Roho Mtakatifu sio tu kuwatuliza wale walio na huzuni, bali pia kuwapa moyo
wa kuvumilia taabu zozote kwa saburi.
Tunahitaji nguvu ya Roho Mtakatifu ili tuweze kuishi maisha mema ya kikristu. Katika
juhudi zetu za kumtumikia Mungu mara nyingi tunakutana na shida; naye Roho
Mtakatifu ndie anayetufariji kwa kutupa nguvu za kupambana na matatizo yote. Maisha
yetu hapa duniani yamejaa misalaba. Na misalaba hiyo hatuwezi kuichukua kwa nguvu
zetu wenyewe. Roho Mtakatifu ndie anayetupa nguvu za kuvumilia. Basi, tumuombe
aje kutufariji na kutupa nguvu za kuchukua msalaba wetu kwa saburi kila siku.

1. Ee Yesu Bwana wetu, tunakusihi Wewe na Baba mumtume Roho Mtakatifu atufariji,
awajalie kitulizo wale wote walio katika taabu na majonzi
W. Twakuomba utusikie

2. Ewe Roho Mtakatifu, uwafariji wale walio katika tabu za namna zozote ili waweze
kuvumilia kwa saburi mateso yao kwa faida ya Roho zao na roho za ndugu zao.
W. Twakuomba utusikie

3. Uwafariji wale walio wagonjwa, uwajalie afya ya roho na ya mwili


W. Twakuomba utusikie

4. Uwasaidie yatima, wajane na wote walioachwa, wasikose kupata siku kwa siku
mahitaji yao ya lazima
W. Twakuomba utusikie

5. Wajalie wale wote walio walegevu na wakosefu neema ya kuongoka na kurejea


hima katika amani ya upendo wako
W. Twakuomba utusikie

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 14


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

6. Uwaimarishe wale walio wema, uwajalie neema ya kudumu wasilegee katika


kutenda mema leo na kesho na siku zote za maisha yao.
W. Twakuomba utusikie

7. Utujalie nguvu za kutafuta na kudumisha amani ya kweli katika mioyo yetu na kati
ya ndugu zetu katika jumuia zetu za kikristu
W. Twakuomba utusikie

TUOMBE;
Ee Bwana Mungu wetu, tunakuomba neema ya Roho Mtakatifu ituangaze akili na
mioyo yetu na kutujaza nguvu ya upendo wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu
Bwana wetu.
W. Amina

LITANIA YA ROHO MTAKATIFU … (soma hapo chini)

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 15


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA SABA: ALHAMISI - Roho Mtakatifu


Anatupa Hekima

Hekima tunayopewa na Roho Mtakatifu si sawa kama hekima inayopatikana katika


ulimwengu huu.
Hekima ya Roho Mtakatifu ni ile Mtk. Paulo aliyowaambia Wakorintho ya kuwa; ni
hekima ambayo watawala wa dunia hii hawakuielewa; maana kama wangaliielewa,
hawangalimsulubisha Bwana wa utukufu. Lakini, ni kama yasemavyo maandiko;
mambo ambayo jicho halijapata kuyaona wala sikio kuyasikia mambo ambayo
binadamu hajapata kuyafikiria moyoni, hayo ndiyo Mungu aliyowatayarishia wale
wampendao (1Kor 2;8-9).
Mtk. Paulo alisema kama vile roho ya mtu ndiyo yenye kufahamu na kutambua yaliyo
ndani yake; hivyo pia Roho Mtakatifu ndiye anayefahamu mambo ya Mungu na
kutufumbulia sisi mioyoni mwetu.
Katika Sikukuu hii ya Pentekoste tunatazamia kumpokea Roho Mtakatifu. Yeye aliye
hekima ya Mungu atatufumbulia siri za Mungu na ukweli wake. Ndiye atakayeamsha
ndani yetu mapendo ya Yesu Msulibiwa, Mkombozi wetu. Ni yeye atakayetuongoza
kutenda mema na kuacha mabaya; tunahitaji sana Roho Mtakatifu katika maisha yetu
ya kila siku, tupate hekima ya kuchagua na kutenda daima yaliyo mema. Katika novena
hii tuzidi kumuomba Mungu atushushie Roho Mtakatifu, atujaze na hekima yake.

1. Ee Mungu, uwabariki viongozi wa dini na wasaidizi wao, wapate kutuongoza kwa


hekima na mapendo
W. Twakuomba utusikie

2. Ewe Roho Mtakatifu, utujalie hekima ya kutambua Mambo ya Mungu na


kuyatekeleza kwa uchaji
W. Twakuomba utusikie

3. Utujalie kuyajua mapenzi ya Mungu na kuyapokea kwa furaha


W. Twakuomba utusikie

4. Uamshe ndani yetu mapendo ya Yesu msulibiwa , utuwezeshe kutimiza vema


wajibu wetu kama wafuasi wa kweli wa Kristu Bwana wetu
W. Twakuomba utusikie

5. Utuwezeshe kuchagua daima yaliyo mema na kuyatekeleza, tupate kulijenga na


kulidumisha kanisa lako hapa duniani
W. Twakuomba utusikie

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 16


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

6. Utuepushe na mafundisho yoyote yaliyo na upotovu, utujalie hekima ya kuzidi


kutambua ukweli wako na mafundisho yako yaletayo wokovu
W. Twakuomba utusikie

7. Hekima ya Roho Mtakatifu ituongoze katika satfari ya maisha yetu hapa duniani,
tupate mwishowe kukurudi Wewe Muumba wetu uliye mwanzo wetu na mwisho wetu
W. Twakuomba utusikie

TUOMBE;
Ee Mungu, Baba wa utukufu, tunakuomba utupe Roho wako wa hekima, atuwezeshe
kukufahamu vema, atuongoze kuishi maisha yenye kukupendeza. Utusaidie
kupambana na matatizo ya maisha, tupate kuishi maisha mema hapa duniani na
mwisho tupate tunzo la heri na furaha yako huko mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia
ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.

LITANIA YA ROHO MTAKATIFU … (soma hapo chini)

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 17


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA NANE: IJUMAA - Roho Mtakatifu


Anatupa Mwanga.

Roho Mtakatifu anaangaza akili zetu tuweze kuona ukweli wa Mungu na kuufata. Bila
Roho Mtakatifu akili zetu zimo katika giza nene, wala hatuwezi kuona njia ya
kutuelekeza kwa Mungu.
Mungu alipoumba ulimwengu, dunia ilikuwa giza tupu, haina kitu. Mungu alisema; “Iwe
nuru”, ikawa nuru, Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema (Mwa 1;3-4) vivyo hivyo
akili ya binadamu bila nuru ya mwanga wa Roho Mtakatifu, ni tupu, ina giza, haiwezi
kuona mambo yanayotuelekeza kwa Mungu. Tukiwa na nuru ya Roho Mtakatifu tunaona
ukweli wa Mungu jinsi ulivyo.
Roho Mtakatifu anapoijia roho ya mtu, anaiangaza akili yake iweze kuona mambo
yanayofaa kwa wokovu. Naye akiisha kuiangaza akili ya mtu huimarisha utashi wake
na kumwezesha kuchagua daima yaliyo mema.
Roho Mtakatifu huiangaza akili iweze kuona ukweli. Kabla ya kuwaaga mitume, Yesu
aliwaambia kuwa atawapelekea mfariji mwingine atakayekaa nao siku zote. Roho wa
kweli ambaye dunia haiwezi kumpokea kwa sababu hawakumfahamu, lakini wao
mitume watamfahamu kwa maana atakaa nao siku zote. Yesu ametuahidi pia sisi Roho
huyo akae nasi.
Leo hivi duniani kuna uwongo na udanganyifu mwingi; kuna dhuluma, vita, na maovu
ya kila namna. Hii ni kwa sababu dunia haijamtambua bado Roho Mtakatifu na
kumpokea Yeye aliye mwanga wa dunia na asili ya kweli yote.
Mtaguso wa Pili wa Vatikano watambua ya kuwa Roho Mtakatifu anakaa katika kanisa
na katika mioyo ya waumini kama katika hekalu. Roho Mtakatifu analiongoza kanisa na
kulifanya liwe na umoja; analipamba na mapaji yake mabalimbali.
Tumuombe Mungu Baba ampeleke huyo Roho Mtakatifu katika kanisa lake, aliongoze
na kulilinda lisipate kutengana, bali lisaidie kueneza utawala wa Mungu popote duniani.

1. Ewe Roho Mtakatifu, utujalie kuona mwanga wa kweli yako na kuifuata


W. Twakuomba utusikie

2. Uwape waregevu neema ya kuirudia tena njia ya kweli yako


W. Twakuomba utusikie

3. Utuwezeshe sisi sote waamini wako tutembee siku zote katika nuru ya kweli yako
na sheria zako
W. Twakuomba utusikie

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 18


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

4. Utuangazie akili ya mioyo yetu tuchague daima yale yanayakupendeza


W. Twakuomba utusikie

5. Uwape mwanga wako viongozi wetu wa dini na serikali, wapate kutuongoza kwa
hekima na uchaji, wasisahau kamwe kwamba uwezo walionao unatoka kwa Mungu.
W. Twakuomba utusikie

6. Utupe mwanga wako tuwaone watu wote kama ndugu zetu. Tuishi kindugu na
kusaidiana kindugu
W. Twakuomba utusikie

7. Ewe Roho Mtakatifu ndiwe mpatanishi wa mioyo,; tunakuomba uondoe udhalimu,


uonevu, udanganyifu na maovu yote katika mioyo ya watu wote.
W. Twakuomba utusikie.

TUOMBE
Ee Yesu Bwana wetu, uliyesema “Pasipo Mimi hamuwezi kitu” umpeleke Roho
Mtakatifu atuangaze akili zetu, tupate kufahamu mapenzi yako na kuyatimiza kwa
imani na uchaji. Roho Mtakatifu atuongoze katika mambo yote, yeye anayeishi na
kutawala nawe pamoja na Baba daima na milele.
W. Amina

LITANIA YA ROHO MTAKATIFU … (soma hapo chini)

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 19


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA TISA: JUMAMOSI - Roho Mtakatifu


Anatupa Mapendo

Maandiko Matakatifu yanatuambia ya kuwa, Roho Mtakatifu, Nafsi ya Tatu ya Utatu


Mtakatifu, ndiye Upendo katika Baba na Mwana. Upendo hujieneza. Naye Roho
Mtakatifu aliye pendo lenyewe la Mungu, hupenda kujieneza na kujishirikisha nasi, na
kuwasha ndani yetu moto wa mapendo yake.
Roho Mtakatifu ndiye mwenye kutakatifuza roho zetu kwa neema ya utakaso. Neema
hiyo ni uzima wa Mungu, ndio huo upendo wa Mungu tunaoshirikishwa. Roho isiyo na
neema ya utakaso imetengana na Mungu, haina uzima wake, haina upendo wake, kwa
hiyo haiwezi pia kuwa na mapendo ya kweli ya jirani.
Ingawa tunaona ishara nyingi za watu kupendana kidugu hapa duniani, mapendo hayo
si mapendo ya kweli wala si kamili kama hayatokani na neema ya utakaso rohoni mwa
mtu. Kama hakuna neema ya utakaso ndani yetu, Mungu pia hayupo kati yetu.
Roho Mtakatifu anatuunganisha na Mungu katika upendo. Pasipo na mapendo hapana
mapatano, hapana masikilizano wala mwungano. Watu wanaopendana wanaungana na
kulingana katika fikra zao na nia zao. Roho Mtakatifu anayetutia mapendo rohoni na
kutuwashia moto wa mapendo, ndiye anayetuwezesha kuwa na mawazo ya namna
moja na nia moja.
Watu wanaopendana hupenda kukaa pamoja, kuishi pamoja na kusaidiana. Roho
Mtakatifu aliye chanzo cha mapendo ya kweli hutuweka pamoja katika Kanisa lake.
Hukaa ndani yetu, hukaa katika Kanisa na kuwasha moto wa mapendo yake ndani yetu.
Roho Mtakatifu anatuwezesha kukaa kwa amani nyumbani, kazini na katika jumuiya
zetu. Basi, tumwombe sasa Roho Mtakatifu atuongezee hayo mapendo yake ndani yetu.

1. Ewe Roho Mtakatifu, uwashe mioyoni mwetu moto wa mapendo yako, tupate
kuwapenda jirani zetu kama tunavyotaka kupendwa nao.
W. Twakuomba utusikie

2. Udumishe ndani yetu neema hiyo ya mapendo yako, tuwezeshe kuishi kwa amani
leo na siku zote za maisha yetu.
W. Twakuomba utusikie

3. Utujalie neema na nguvu za kutekeleza mema yote tunayokusudia kuyatenda siku


hii ya leo
W. Twakuomba utusikie

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 20


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

4. Uongoze nia zetu na maazimio yetu, yalingane na juhudi zetu za kutaka kuleta
mafanikio ya roho na mwili kati yetu
W. Twakuomba utusikie

5. Utubariki, ili baada ya maombi haya, tuwe na juhudi ya kutimiza vema zaidi wajibu
wetu wa kikristu kwa moyo mkuu
W. Twakuomba utusikie

6. Utuwezeshe kueneza mapendo na amani kati yetu na katika jumuiya zetu za


kikristu
W. Twakuomba utusikie

7. Utuwezeshe kuwa kweli chachu ya wema na mapendano kati ya watu, ili nao
wapate rehema zako kwa maombezi yetu.
W. Twakuomba utusikie.

TUOMBE;
Ee Mungu, tunakushukuru kwa neema ulizotujalia, hata tukaweza kuifanya ibada hii
ya Novena takatifu mpaka mwisho. Utujalie mema yote tuliyoomba; utusaidie
kutekeleza yote yale tuliyokusudia kutenda. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu
Bwana wetu.
W. Amina.

LITANIA YA ROHO MTAKATIFU … (soma hapo chini)

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 21


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

LITANIA YA ROHO MTAKATIFU


o Bwana Utuhurumie………Utuhurumie
o Kristu utuhurumie……..….Utuhurumie
o Bwana utuhurumie….. Utuhurumie
o Baba mweza wa vyote….. Utuhurumie
o Yesu Mwana wa Pekee wa Baba na Mwokozi wa Dunia……..Utuokoe
o Roho wa Baba na Mwana aunganishaye maisha ndani ya Baba na
Mwana………….Ututakatifuze
o Roho Mtakatifu……….Utusikie
o Roho Mtakatifu atokaye kwa Baba na Mwana…………..Njoo ndani ya mioyo yetu
o Ahadi ya Mungu Baba……………… Njoo ndani ya mioyo yetu
o Mionzi ya Mwanga kutoka Mbinguni……………… Njoo ndani ya mioyo yetu
o Mwandishi wa vyote vilivyo vizuri……………… Njoo ndani ya mioyo yetu
o Chanzo cha Maji ya Uzima……………… Njoo ndani ya mioyo yetu
o Moto utumikao daima……………… Njoo ndani ya mioyo yetu
o Muungano Mtakatifu……………… Njoo ndani ya mioyo yetu
o Roho wa ukweli na upendo……………………Utuhurumie
o Roho wa hekima na elimu……………………Utuhurumie
o Roho wa shauri na nguvu……………………Utuhurumie
o Roho wa akili na neema ya kumtumikia Mungu……………………Utuhurumie
o Roho wa neema na sala……………………Utuhurumie
o Roho wa amani na subira……………………Utuhurumie
o Roho wa usafi na uaminifu……………………Utuhurumie
o Kitulizo cha Roho……………………Utuhurumie
o Roho aletaye Utakatifu……………………Utuhurumie
o Roho uongozaye Kanisa……………………Utuhurumie
o Zawadi kutoka kwa Mungu juu Mbinguni……………………Utuhurumie
o Roho ajazaye ulimwengu……………………Utuhurumie
o Roho Mtakatifu…………………..tupe neema ya kuchukia dhambi
o Roho Mtakatifu…………………..njoo ufanye upya sura ya ulimwengu
o Roho Mtakatifu…………………..jaza roho zetu kwa mwanga wako
o Roho Mtakatifu…………………..ifuraishe mioyo yetu kwa sheria yako

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 22


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

o Roho Mtakatifu…………………..washa moto wa mapendo ndani yetu


o Roho Mtakatifu…………………..jaza mioyo yetu na hazina ya neema yako
o Roho Mtakatifu…………………..tufundishe kusali vyema
o Roho Mtakatifu…………………..tuangaze kwa nguvu zako za Ki-Mungu zitupatiazo
moyo wa kutenda daima yaliyo mema
o Roho Mtakatifu…………………..tuongoze Kwenye njia ya wokovu
o Roho Mtakatifu…………………..tuweze kufahamu yale ya muhimu tu
o Roho Mtakatifu…………………..tupe hamu ya kuitafuta fadhila yako
o Roho Mtakatifu…………………..tusaidie tuweze Kupata fadhila zote
o Roho Mtakatifu…………………..tupe uvumilivu tuweze kutenda yaliyo mema tu.
o Roho Mtakatifu…………………..tunaomba uwe zawadi ya uzima wetu
o Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia…………….Tushushie Roho
wako Mtakatifu
o Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia…………….jaza mioyo yetu
kwa mapaji yako ya Roho Mtakatifu
o Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia…………….tupe roho ya
hekima na neema ya kumsifu Mungu.
o Njoo Roho Mtakatifu uzijaze roho za waumini wako uwashe moto wa mapendo
yako ndani ya mioyo yetu (W)

TUOMBE
Ee Mungu Baba mwenye huruma tujalie Roho wako alete Mwanga kwetu ili apate
kututakasa na kuingiza ndani ya mioyo yetu Baraka za kuweza kutenda yale yaliyo
mema.

Tunaomba hayo kupitia kwa Mwanao Mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo, anbaye
anaishi na kutawala pamoja nawe katika Umoja wa Roho Mtakatifu. AMINA

Atukuzwe Baba…..x3

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 23


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

MWISHO WA KITABU
Tembelea ackyshine.com/vitabu Kupata vitabu na majarida mengine ya Dini. Kitabu Hiki
Kimehaririwa na Melkisedeck Leon Shine

UJUMBE WA MHARIRI

Kwa kuhitimisha, mpendwa katika Kristu, Mimi Melkisedeck


Leon Shine napenda kukupongeza kwa kuamua kufanya
safari hii ya kiroho kupitia kurasa za Kitabu hiki cha Novena
Ya Roho Mtakatifu.

Napenda kukwambia kwamba nakupenda sana, ninakutakia


mema, na daima ninamuomba Mungu kwa ajili yako. Ni
Maombi yangu kwa Mungu kwamba “yeyote asomaye
kitabu hiki Maombi yake yapate Kibali Mbele za
Mungu” Melkisedeck Leon Shine

Mpendwa Katika Kristo, Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu;


la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na
Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda
neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza
mwendo, niifikilie tuzo ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.
(Wafilipi 4:12-14)
Hivyo basi kwa unyenyekevu, naomba unifanyie kitendo kimoja cha wema: Tafadhali,
chukua muda wako wa dakika kadhaa kadiri utakavyopendezwa moyoni mwako
kuniombea Mimi Melkisedeck katika safari hii yangu ya Kiroho na kimwili, Mimi Binafsi
na Familia yangu. Wote tunamhitaji Mungu katika maisha yetu, na sala yako ni zawadi
ya thamani kwa roho yangu. Unaweza kunipa zawadi hiyo?

Mpendwa katika Kristu, Naomba Ukumbuke daima maneno ya Mtakatifu Paulo,


"Ombeni Bila Kukoma" (1 Wathesalonike 5:17). Kwa pamoja, tuendelee kujenga
imani yetu na kuungana na Mungu katika sala.

Natanguliza shukrani zangu za dhati kwako kwa kuniombea.


Mungu akubariki sana na akutimizie haja za Moyo Wako. Amina.

Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo
au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe
katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina.
Waefeso 3:20-21

Unaweza kunifahamu zaidi kwa kutembelea shine.tz kusoma profile yangu


au wasiliana nami kwa simu namba +255 757 310 426 Nitafurahi kusikia
kutoka kwako na kuungana na wewe katika safari yetu ya Kiroho.

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 24


Shine
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

Copyright © All Rights Reserved, Ackyshine

Mhariri: Melkisedeck Leon Shine www.ackyshine.com 25


Shine

You might also like