You are on page 1of 4

KIGOGOTO

Abdilatif Abdalla

Kujipurukusha kwangu kote nilikojipurukusha, hakukuniombea! Mwisho ikanibidi nisalimu


amri. Maana, chembelecho waliosema, Kifo kukimbizwa funza, chawekwa mahali gani?

Nami pia, kama wenzangu waliotoa maoni yao, mzee wetu Bwana Saadani Abdu Kandoro
alinijia na muswada wa kitabu hiki akiitacho Fasihi Sahihi, na akanitaka niuandikie kama
alivyonitamkia mwenyewe chochote ili upate baraka zako! Nikatambua kuwa mzee
wangu huyu asema nami kikuu. Na wavyele walisema, Nahodha mtaka chombo si mjinga wa
safari.

Kwangu mimi ndio imekuwa ni vigumu zaidi kulitimiza nililotakwa nilitimize. Haswa kwa
kuwa maji haya ni makuu nami; yamenipita kimo. Yaani sijihisabu kwamba nishafika
makasada ya kuwa nami ni muweza wa kuingia katika majadiliano ya mawango ya juu kama
yaliyomo humu. Hata hivyo, ikanibidi nijikusanyekusanye nipate kuandika hicho chochote.
Isipokuwa hizo baraka nina hakika sinazo!

Kama kitakavyoonekana, kitabu hiki kimegawanyika sehemu mbili. Sehemu kubwa, ya pili,
imekusanya mashairi juu ya mambo mbalimbali. Kama kitabu chake cha kwanza,1 mbali na
mashairi yake mwenyewe vile vile muna mashairi ya watunzi wengine. Kwa hivyo, wale
walio wapenzi wa mashairi, watafaidika na sehemu hiyo.

Na kabla ya sehemu hiyo, kuna sehemu ya nathari, ambayo imekusanya maoni ya Mwalimu
T.S.Y. Sengo, dibaji ya Mwalimu J.A. Ramadhani, na makala marefu ya mwandishi wa
kitabu hiki ambayo, katika jumla ya mambo yazungumzwayo humo ni Fasihi na mashairi.
Bali naona nitakuwa sahihi zaidi nisemapo kuwa madhumuni haswa yaliyokusudiwa makala
hayo ni kuzungumzia Fasihi. Sababu yangu ya kusemea hivyo ni kwamba roboo tatu nzima
za makala hayo zimetandwa na mjadala wa Fasihi. Pengine neno mjadala si mahali pake
kutumika hapa, kwa sababu katika makala hayo Bwana Saadani yuwasema pekee; hana wa
kumuaili. Lakini matumaini yangu ni kwamba mjadala huenda ukaanza baada ya wahusikao
kuyasoma mawazo ya mwandishi wa kitabu hiki juu ya Fasihi.

Jambo kubwa lijitokezalo katika makala yenyewe ni kwamba Bwana Saadani hakubaliani na
maana ya pili iliyopawa neno Fasihi; kwamba vyereje hata Fasihi kuwa na maana ya
tungo za kisanaa zitumiliwazo lugha ya maneno na hali kuna maana yake ya asili? Yeye
yuwadai kwamba, neno fasihi halitumiki mahali pengine popote isipokuwa katika maneno ya
lugha tu (msisitizo ni wangu). Kisha yuwatutolea ushahidi wa makamusi ambayo yatoa
maana moja tu (hiyo ya asili) ya neno fasihi. Kwa mfano, ametutajia Standard Swahili
English Dictionary, Standard English Swahili Dictionary (yote mawili yamepigishwa chapa
mwaka 1939), Kamusi ya Kiswahili, Munjid (ambalo ni kamusi la lugha ya Kiarabu), na
Arabic English Dictionary2.

Mpaka hapa, nakubaliana moja kwa moja na mzee wetu. Nakubaliana naye kwamba asili ya
neno fasihi ni lugha ya Kiarabu. Nakubaliana naye kuwa katika hiyo lugha yake ya asili, na
hata lilipoingia katika lugha ya Kiswahili, maana yake yahusiana na usafi, unyofu, utamkaji
sahihi na mpango mzuri wa maneno katika lugha. Pia nakubaliana naye kuwa mpaka hivi sasa

1
S. A. Kandoro, Mashairi ya Saadani, Mwananchi Publishers, Dar es Salaam, 1972.
2
Hava, J.G. ???, 19??

1
hakuna kamusi lolote la Kiswahili lililochapishwa ambalo lalipa neno fasihi zaidi ya hiyo
maana moja iliyotajwa. Lakini kukubaliana kwetu juu ya fasihi kwakomea hapa.
Tukiondoka hapa, twafarikana; na kila mmoja wetu yuwapita njia yake na kwa sababu zake.

Baada ya kuyasoma kwa makini makala hayo, imenipitikia kuwa yaonyesha kwamba, mosi,
nguzo aliyoishikilia mzee wetu ni kuwa neno la lugha ya kigeni litiwapo katika lugha
nyengine ni lazima libakishwe vile vile lilivyo katika hiyo lugha yake ya kwanza. Yaani, kwa
mfano, lisibadilishiwe maana wala lisiongezewe maana zaidi ya hiyo yake ya asili, au labda
hata matamshi yake yabakie vivyo hivyo. Mimi nami naona kuwa hiyo lugha ya pili ina kila
haki ya kulisarifu ili lilingane na haja na muundo wa lugha yake basi ikiwa ni kwa
kuliongezea maana au ni kulibadilishia matamshi.

Pili, yeye yuwachukulia kwamba kila aongezaye lake katika kuitafiti na kuikuza lugha au
kuyaongezea maneno maana ambazo ni tafauti na zile za asili, basi mtu huyo ni mvurugaji
wa lugha na ni mfujaji. Mimi naona kuwa mtu afanyapo hayo huwa hana madhumuni mabaya
bali nia yake huwa ni kutaka kuipeleka mbele hii lugha. Sikatai kwamba katika jitihada yake
hiyo, mtu hupata akateleza; na hapo matokeo ya jitihada yake yakaonekana kwamba
yamekwenda upogo. Bali nilikataalo ni kumtuhumu mtu huyo kuwa nia yake ilikuwa mbaya
tangu mwanzo, na kwa hivyo yuwafanya makusudi ili kuvuruga. Hainipitikii kuwa mtu kama
huyo lake ni kuwinda pazima ili kupatia pengo. Sidhani kama yuko awezaye kuhatirisha
kukifanyia hujuma Kiswahili hivi leo haswa hapa Tanzania baada ya kuwa lugha hii ina
majeshi yaongozwayo na majamadari kama Bwana Saadani Abdu Kandoro!

Tatu, hii nguzo ya kuwa madhali makamusi yote3 yana maana moja tu ya neno fasihi, basi
maana yoyote nyengine itakayovyaziwa neno hilo itakuwa yaichafua hiyo ya kwanza au
yalitoa neno hilo nje ya msingi wake, si nguzo madhubuti kwa sababu mbili:

Sababu ya kwanza ni kwamba makamusi yote hayo aliyoyatolea ushahidi Bwana Saadani, ni
ya zamani. Mawili kati ya hayo yana umri wa miaka thalathini na minane sasa, na hilo la tatu
lina miaka arubaini na miwili tangu lichapishwe. Kwa hivyo, makamusi hayo yamepitwa na
maendeleo ya lugha ya Kiswahili kwa miaka yote hiyo, na papo hapo ni kwamba si ya
kutegemewa tena kushuhudilia maana na matumizi ya baadhi ya maneno yaliyokumbwa na
mabadiliko yanayotokana na maendeleo makubwa ya lugha hii.

Na sababu ya pili yatokana na hiyo ya kwanza. Nayo ni kwamba hii maana ya pili ya neno
fasihi aipingayo mzee wetu haingeweza kuwamo katika makamusi hayo kwa sababu tokea
neno hili lipate hiyo maana ya ziada ni miaka tisia tu sasa. Na hivi leo, baada ya maendeleo na
ukuaji wa lugha hii, kuna maneno chungu nzima yatumikayo na ambayo ukiyatafuta katika
makamusi kama hayo huwezi kuyapata, au ukiyapata pengine yamebadilika maana au
yameongezeka. Basi ikiwa sababu ya kuikataa hii maana ya pili ya fasihi ni kwamba haimo
katika kamusi lolote, hoja hii hii yaweza kutumiwa kwa kusema kuwa na hayo maneno
mengine na maana nyengine zisizokuwamo katika makamusi pia nazo zisikubalike.

Baadhi yetu twafahamu kwamba chanzo cha hii maana ya pili ya neno fasihi kilianzia
mwaka 1968, wakati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilipoanza kufundisha - kwa Kiswahili
somo maalumu lihusianalo na fani ya tungo za Kiswahili za kisanaa4 - kama vile mashairi,
riwaya, tamthilia, na kadhalika. Kwa upande wa Kiswahili, somo hili lilikuwa ni jipya. Na
upya wake si kwamba ulitokana na sababu ya kuwa kabla ya hapo hakukuwa kukisomeshwa

3
Na hapa nayasemea makamusi yahusianayo na Kiswahili, kwa sababu neno hili sasa nalihisabu kuwa ni la
Kiswahili zaidi kuliko kuwa ni la Kiarabu, ingawa asili yake ni lugha ya Kiarabu.
4
Na katika shule za sekondari za Tanzania, somo hili lilianza kufundishwa katika mwaka 1970.

2
vitabu vya tungo kama hizo, bali upya huo ulitokana na namna ya ufundishaji wake. Twaweza
kusema kwamba hapo zamani tungo hizo zikisomeshwa kwa namna ya ufahamu, ambapo
huo mtindo mpya ulikuwa ni wa kuzishughulikia kwa mapana yake na kwa kuviangalia
vipembe vyake mbalimbali. Msitu ulivyokuwa ni mpya, na komba wakawa ni wapya! Mwana
huyu alipozaliwa, ikawa sasa ni lazima apawe jina. Lakini jina lake halikuwa rahisi hivyo
kupatikana. Na havilekei mtu aweze kupiga kite kisha ashindwe kumpa mwanawe jina.
Ndipo, baada ya majadiliano marefu, likapatikana hilo fasihi.

Kama tufahamuvyo, katika lugha ya Kiingereza, somo la namna hii laitwa Literature. Kwa
hivyo, katika miezi ya kwanza, kabla ya kupatikana hilo Fasihi, somo hilo likawa laitwa
kwa jina hilo hilo la Kiingereza; na hata baadhi ya istilahi zake zikabakia katika lugha ya
Kiingereza. Baada ya kitambo cha miezi kadhaa kupita, kukawa kumependekezwa majina
matatu ili mojawapo lishike mahali pa Literature. Majina yenyewe yalikuwa ni aadab5,
maandishi na fasihi.6 Ndipo kura ikaja ikaangukia kwenye hili jina la mwisho. Na hapa
ndipo alipo na vita napo Bwana Saadani. Vita vyake ni vya pande mbili.

Upande wa kwanza ni ule nilioutaja mwanzo: Kwamba neno Fasihi haliwezi kutumika kwa
maana nyengine zaidi ya ile yake ya asili. Upande wa pili ni kuwa, mbali ya kwamba haliwezi
kutwishwa maana ya ziada, kadhalika haliwi ni maana ya neno la Kiingereza, Literature.
Yuwasema mzee wetu,

Tafsiri ya Literature iwe kwa maana ya Fasihi si sahihi.

Na kabla ya hapo pia alikuwa amesema:

Wataalamu fulani walizungumzia neno Fasihi na Literature,


wakafahamisha dalili...na wakakubaliana Fasihi ni Literature.
Kwa kweli, lugha ya Kiswahili imefikia daraja ya kukuzwa,
kuenezwa kwa usafi sana, kuheshimiwa na kulindwa ili kiwe
ni chombo kisichochezewa ovyo.

Vile vile, kisha akatudondolea maana moja ya neno Literature. Katika Kiingereza, neno hili
lina maana tatu; na kila maana yaanza na neno maandishi.7 Yaani katika Kiingereza, neno
literature halitenganishiki na maandishi; bila ya maandishi hakuna literature. Lakini, kama
nilivyopata kusema mahali kwengine,8 ukweli ni kwamba sababu ya kuwa katika Kiingereza
neno literature likapawa maana hiyo na ikasisitiziwa maandishi, ilitokana na kuliendea
kinyume na kulitweza tabaka fulani la watu ambao hawakuwa na elimu ya kusoma wala
kuandika, na ikawapendelea wale walio katika tabaka la wasomi na watawala kwa sababu
historia ya fasihi ya Ulaya Magharibi ni historia ya fasihi ya tabaka la watawala.9 Na katika
hizo maana tatu za neno literature katika Kiingereza, maana moja tu ndiyo ihusianayo na
maandishi ya sanaa; na hizo maana zilizosalia zina maana ya maandishi yoyote yale.

5
Katika lugha ya Kiarabu, hili ndilo lenye maana ya Literature.
6
Kuhusu kuanzishwa kwa somo hili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pia tizama makala ya Farouk M.
Topan, An Approach to the Teaching of Kiswahili Literature, yaliyomo katika SWAHILI, Jarida la Chuo cha
Uchunguzi wa Lugha ya Kiswahili, Toleo la 38/2, Septemba 1968, kurasa 161-163.
7
Kwa mfano, tizama Hornby, A.S, Oxford Advanced Learners Current English Dictionary, Oxford University
Press, London, 1974, ukurasa 503.
8
Abdilatif Abdalla , The Position of Kiswahili Poetry in Modern East African Literature, (mhadhara
uliotolewa Chuo Kikuu cha Mainz, Ujerumani Magharibi, katika The Second Janheinz Jahn Symposium on
Modern East African Literature and Its Audience (Aprili 22-26, 1977).
9
Okot pBitek, African Cultural Revolution, Macmillan, Nairobi, 1973, uk. 20.

3
Lakini hili neno literature lilipotafutiwa la Kiswahili lake, na hatimaye likapatikana hilo
fasihi, halikuchukuliwa kwa misingi ile ile ya kwao. Yaani halikuchukuliwa pamoja na lile
wazo la kuwa ni lazima liambatanishwe na maandishi peke yake, bali lililozingatiwa zaidi
lilikuwa ni ule upeo wa sanaa itumiliwayo maneno basi haidhuru maneno hayo yawe
yameandikwa au ni ya kusemwa au kuimbwa. Vile vile, neno fasihi liliposhika mahali pa
literature halikukusudiwa likusanye na hizo maana mbili nyengine zisizohusiana na sanaa;
bali lilijivua nazo.

Kwa hivyo, ingawa twasema kuwa neno la Kiingereza liwezalo kufasiri neno fasihi kwa
maana ya sanaa itumiliwayo lugha ya maneno ni literature, lakini huwa hatuna maana ya
literature kwa maana zake zote. Yaonyesha kuwa mzee wetu, Bwana Saadani Abdu Kandoro,
hakuwa amelitaamali hili. Makosa kama haya ndiyo aliyoyafanya M.M. Mulokozi aliposema
kuwa:

Fasihi ni maandishi au habari yoyote ile katika lugha yoyote.


Fasihi ipo ya aina mbili: Fasihi ya kisanaa na fasihi ya kitaaluma.
Fasihi ya kisanaa inazo fani zake mbalimbali, mathalani ushairi,
michezo ya kuigiza, nyimbo, hadithi fupi na riwaya (hadithi ndefu
za kubuni). Fasihi ya kitaaluma huwa na maarifa ya taaluma
mbalimbali za elimu, kama vile historia, hesabu, kemia, siasa, n.k.10

Kutokana na mzee wetu kutolitaamali hilo, ndipo akahukumu kwamba neno fasihi ni
makosa kusimama mahali pa literature, na badala yake akapendekeza neno lunda.
Akatueleza pia kuwa neno lunda latokana na lugha za Kiyao na Kimwera, na kwamba
maana yake ni mkusanyiko wa habari zilizohifadhiwa mahali kwa ajili ya maelezo ya sasa na
baadaye Lau kama literature ikusudiwayo ni fasihi ingekuwa ni habari yoyote tu,
pengine pendekezo la mzee wetu lingefaa; bali mimi naona neno lunda lasadifu zaidi
kushika mahali pa neno historia.

Mimi ni miongoni mwa hao waliungao mkono neno fasihi kwa maana ya somo maalumu
lihusianalo na tungo za sanaa, kama vile mashairi, riwaya, tamthilia, tenzi, na kadhalika. Neno
fasihi lenye maana yake ya asili aliyoitaja mzee wetu, limevyaziwa maana ya pili. Hapana
ubaya kwa neno moja kupawa ziada ya maana, haswa kwa hii lugha yetu ya Kiswahili,
ambayo hata mzee wetu, Bwana Saadani, yuwakubali kuwa haina budi kukuzwa na
kupanuliwa matumizi yake.

Amma namshukuru mno Bwana Saadani Abdu Kandoro, na nampongeza kwa dharubu
aliyochukua na kwa jitihadi yake kubwa katika kuiendeleza mbele hii lugha. Majadiliano
kama haya husaidia sana katika kuongezana maarifa. Kwa hivyo, hii ni dalili nzuri.

Basi namalizia kwa kusema kuwa mzee wetu huyu pengine aliidunda ngoma ili kuusikiza
mlio. Lakini kwa vile alipoidunda alitwita tuushuhudie mlio wake, na kwa sababu haya
mambo nasi yametuvama hata tukashindwa kuusikiza tu huo mlio ila tukaunyakua mdundo,
basi ni matumaini yangu kwamba na kila mchezaji atakaousikia mdundo huu atajitoa ugani ili
tukeshe nayo hii ngoma.

Dar es Salaam
Agosti 9, 1977
10
Katika makala yake, Fasihi na Mapinduzi, yaliyomo katika Kioo cha Lugha, Toleo la 6, Jarida la Chama cha
Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 1976, uk 1.

You might also like