You are on page 1of 4

SIKUKUU YA MAMA BIKIRA MARIA MKINGIWA DHAMBI YA ASILI NA

MSIMAMIZI WA NCHI YETU YA TANZANIA


TAREHE 9 DESEMBA

Inapendekezwa kwa wale ambao hawataweza kushiriki maadhimisho ya


Misa Takatifu inayoadhimishwa Kawekamo au kwingineko kokote kwa lengo hili,
wasali kwanza Rozari Takatifu kwa nia ya kuombea nchi yetu ya Tanzania kisha
kusali sala zifuatazo. Kwa pale ambapo hakuna Askofu/Padre, Kiongozi wa sala
aongoze sehemu husika.

SALA YA KUIOMBEA TANZANIA


(Na Papa Mt. Yohani wa XXIII)
Askofu/Padre: Ee Mungu Mwenyezi wa milele, Baba wa mataifa yote na wa watu
wote, utuangalie kwa macho ya huruma sisi watu wako wa Tanzania
tunaohesabika kati ya mataifa ya dunia. Kwa baraka yako utuwezeshe kuishi
maisha mema iwapasavyo wana wa Mungu.
Kiitikio: Ee Bwana uibariki nchi yetu.

Askofu/Padre: Uwaangazie viongozi wetu, ili sheria wanazotunga, zilingane na


sheria zako Wewe uliyetuumba kwa ajili yako, tena zitusaidie kupata manufaa ya
maisha mema hapa duniani.
Kiitikio: Ee Bwana uibariki nchi yetu.

Askofu/Padre: Uwajalie watu wote paji lako la imani ya kuwa Wewe upo. Utupe
hekima ya kutafuta ukweli katika mambo yote, na kuishi kwa uaminifu katika amri
zako.
Kiitikio: Ee Bwana uibariki nchi yetu.

Askofu/Padre: Uwashe moto wa mapendo yako ya Kimungu mioyoni mwetu.


Mapendo hayo yatusaidie kushinda utengano, ushindani na chuki ya ukabila au ya
udini au utaifa.
Kiitikio: Ee Bwana uibariki nchi yetu.
Askofu/Padre: Utuunganishe sisi sote kwa mwungano wa kindugu, tupate kwa
msaada wa neema yako kuwa mmoja ndani yako wewe, Baba wa wote, na ndani
ya Mwanao.
Kiitikio: Ee Bwana uibariki nchi yetu.

Askofu/Padre: Ubariki taifa letu liweze kustawi na kushika amani na mataifa


mengine. Kiitikio: Ee Bwana uibariki nchi yetu.

Askofu/Padre: Uwaongoze viongozi wetu wote ili watimize wajibu na kazi zao
sawasawa.
Kiitikio: Ee Bwana uibariki nchi yetu.

Askofu/Padre: Wawasaidie raia wote kujipatia hali njema hapo walipo.


Kiitikio: Ee Bwana uibariki nchi yetu.

Askofu/Padre: Ututhibitishe tusishindwe kupambana na maovu yawezayo


kutufikia kutoka nje au ndani.
Kiitikio: Ee Bwana uibariki nchi yetu.

Askofu/Padre: Utufadhili sisi sote kufikia kipeo ulichotutayarishia, yaani kuwa raia
katika ufalme wa mbinguni, unapoishi na kutawala daima na milele.
Wote: Amina.

SALA YA KUIKABIDHI TANZANIA KWA BIKIRA MARIA


(Sala ya Mtakatifu Papa Yohane wa Pili)

Padre: Maria Mtakatifu, Mama wa Kanisa, Mama wa Binadamu wote Pamoja na


Mimi Yohane Paulo wa II, Halifa wa Mtume Petro, Sisi wanao wote wa Tanzania,
tunajiweka chini ya ulinzi wako wa upendo.

Wote: Mama Maria, utuombee sasa na saa ya kufa kwetu, Amina.


Padre: Kwa Moyo mmoja, leo na daima, tunajiweka upya mikononi mwako Kama
Mataifa machanga, Katika Bara hili la ahadi, Kwa matumaini mapya na matarajio
ya sasa na tunaomba msaada wenye nguvu yako, wewe mama wa Mkombozi na
Bwana wetu Yesu Kristo.

Wote: Mama Maria, utuombee sasa na saa ya kufa kwetu, Amina.

Padre: Mama wa Familia Takatifu ya Nazareti, ndiwe Mama wa “Kanisa la


nyumbani” Tunaomba msaada wako kwa ajili ya familia zote za nchi zetu. Utufariji
katika Mateso na Usumbufu; utuimarishe kwa neema zile zote zilizopamba maisha
ya familia yenu wewe Mama, Mwanao Yesu na mumeo Yosefu; yaani kwa neema
ya mwanga, faraja, utulivu na ujasiri.

Wote: Mama Maria, utuombee sasa na saa ya kufa kwetu, Amina.

Padre: Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu, kwa moyo wote tunakukabidhi pia
kanisa takatifu katoliki katika nchi zetu. Tunaweka chini ya ulinzi wako wewe Mama
mwajibikaji, kila Jimbo na kila Parokia ili waumini wote wanapokutana pamoja na
wachungaji wao, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, kwa Nguvu ya injili na adhimisho
la Sadaka ya Ekaristi Takatifu, Kanisa takatifu katoliki la Kitume, lake Yesu Kristo.

Wote: Mama Maria, utuombee sasa na saa ya kufa kwetu, Amina.

Padre: Kwa upendo wako wa kimama uwasimamie na kuwasaidia Maaskofu,


Mapadri na Watawa, waishi kikamilifu miito yao waliyopokea ndani ya Moyo wa
Kanisa, walitumikie Taifa la Mungu na waushuhudie ukweli na maadili ya kiroho ya
ufalme wa Kristo.

Wote: Mama Maria, utuombee sasa na saa ya kufa kwetu, Amina.

Padre: Kwa namna ya pekee, na kwa maombezi ya Mtakatifu Yohane Paulo wa II


(Papa) umkumbuke Baba Mtakatifu (…………), Maaskofu wote, Mapadri, na
Watawa wote ili wawe watumishi waaminifu na watangazaji hodari wa injili
Wote: Mama Maria, utuombee sasa na saa ya kufa kwetu, Amina.

Padre: Malkia wa Amani, sikiliza sala zetu tuombao Amani ya kudumu na


mshikamano thabiti katika nchi zetu na Afrika nzima. Utufundishe moyo wa
kusameheana na moyo wa kupatana yatokeapo mafarakano katika familia zetu,
Aidha katika masuala ya kijamii na kisiasa. Utujalie wote kujua namna bora ya
kumpokea na kumstahi kila mtu na kuaminiana kindugu; aidha moyo wa kufanya
kazi kwa bidii kwa maendeleo ya nchi zetu huku tumezingatia kila siku ujamaa
ndiyo haki na umoja.

Wote: Mama Maria, utuombee sasa na saa ya kufa kwetu, Amina.

Padre: Maria Mama yetu, Upokee tendo hili la kuziweka nchi zetu chini ya ulinzi
wako, na utujalie kupata hayo tunayoomba kutoka kwa moyo wa Mwanao, Bwana
wetu Yesu Kristo. Amina.

SALAMU MALKIA
Salamu Malkia, Mama mwenye huruma, uzima, tulizo na matumaini yetu, salamu.
Tunakusihi ugenini hapa sisi wana wa Eva. Tunakulilia tukilalamika na kuhuzunika
bondeni huku kwenye machozi. Haya basi, Mwombezi wetu, utuangalie kwa
macho yako yenye huruma. Na mwisho wa ugeni huu, utuoneshe Yesu, mzao
mbarikiwa wa tumbo lako. Ee mpole, ee mwema, ee mpendelevu, Bikira Maria.

Kiongozi: Utuombee, Mzazi Mtakatifu wa Mungu.


Wote: Tujaliwe ahadi za Kristo.

Tuombe:
Ee Mungu, makimbilio na nguvu yetu, uwaangalie kwa wema watu wanaokulilia;
na kwa maombezi ya Bikira Maria mtukufu asiye na kosa, Mzazi wa Mungu, na ya
Mtakatifu Yosefu, mchumba wake, na ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume wako,
na ya Watakatifu wote: usikilize kwa Huruma na wema sala tunazokutolea kwa
wongofu wa wakosefu na kwa uhuru na utukufu wa Kanisa, mama mtakatifu.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Amina.

You might also like