You are on page 1of 2

DOMINIKA YA NNE

SOMO LA KWANZA Kumbukumbu la Torati 18:15-20


"Nitawasimamishia nabii, nitamtia kinywani mwake maneno yangu."
Somo katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati
Musa aliwaambia wana wa Israeli, "Bwana Mungu wako atakusimamishia, kati ya
nduguzo, nabii kama mimi, msikilizeni. Ndilo neno hilo ulilomwomba Bwana Mungu
wako pale Horebu siku ile ya mkutano: 'Nisikilize tena sauti ya Bwana Mungu wangu
wala nisiangalie tena moto ule mkuu, nisife." Naye Bwana akaniambia: Hayo
waliyosema ni sawa. Nitawasimamishia kati ya ndugu zao nabii afananaye nawe,
nitamtia kinywani mwake maneno yangu naye atawaambia kila nitakachowaamuru.
Kama mtu hasikilizi maneno yangu atakayosema huyu kwa jina langu, basi mimi
mwenyewe nitamdai mtu huyu. Lakini ikiwa nabii anayethubutu kusema kwa jina langu
neno nisilomwamuru mimi, akisema kwa jina la miungu mingine, nabii huyu atakufa."
Neno la Bwana.

ZABURI YA KUITIKIZANA Zaburi 95:1 2,6-7, 7d 9 (K. 7d, 8a)


K. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msiifanye mioyo yenu kuwa migumu.

Njoni, tumpigie BWANA kelele za furaha;


tumshangilie mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele yake kwa shukrani,
tumfanyie shangwe kwa nyimbo na zaburi. K.

Njoni, tuabudu na kusujudu;


tumpigie magoti BWANA aliyetuumba.
Kwani yeye ni Mungu wetu,
sisi lakini ni watu wa malisho yake.
na kondoo wanaochungwa kwa mkono wake. K.

Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!


Msifanye mioyo yenu kuwa migumu kama huko Meriba,
kama baba zenu walivyokuwa siku ya Masa jangwani.
Waliponijaribu, baba zenu waliponipima;
ijapo walikwishaona matendo yangu. K.

SOMO LA PILI 1 Wakorintho 7:32-35


"Bikira huwaza mambo ya Bwana apate kuwa mtakatifu mwili na roho."
Somo katika barua ya kwanza ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho
Ndugu zangu: Nataka msiwe na shughuli. Asiye na mke anashughulikia mambo ya
Bwana, ampendeze Mungu. Bali aliye na mke hushughulikia mambo ya ulimwengu,
ampendeze mkewe. Huelekea huko na huko. Kadhalika mwanamke asiyeolewa au bikira
huwaza mambo ya Bwana apate kuwa mtakatifu mwili na roho. Lakini aliyeolewa
hushughulikia mambo ya ulimwengu huu, ampendeze mumewe. Nasema hayo kwa
kuwafaidia, si kwa kuwategea tanzi bali kwa kuwapa heshima ya kumtumikia Bwana
daima pasipo kuvutwa na mambo mengine.
Neno la Bwana.

SHANGILIO LA INJILI Mathayo 4:16


K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Watu wakaao gizani wameona mwanga mkuu. Wenye kukaa katika nchi na uvuli wa
mauti wameangazwa na nuru.
W. Aleluya.

INJILI Marko 1:21b -28


"Aliwafundisha kama mtu mwenye mamlaka."
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
[Katika mji wa Kapernaumu] Yesu aliingia katika sinagogi, akafundisha siku ya Sabato.
Watu walistaajabia mafundisho yake, kwa maana aliwafundisha kama mtu mwenye
mamlaka na si kama Waandishi. Ndani ya sinagogi yao alikuwapo mtu amepagawa na
pepo mchafu, akapaza sauti akisema, "Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja
kutuangamiza? Nakujua u nani, ndiwe Mtakatifu wa Mungu!" Yesu akamkemea akisema,
"Nyamaza! Umtoke!" Pepo mchafu akamtikisatikisa, akamtoka huku akilia kwa sauti
kubwa. Wote wakashangaa na wakaulizana, "Kitu gani hiki? Haya ndiyo mafundisho
mapya kwa mamlaka. Anawaamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii." Na sifa yake
mara ikaenea kila mahali katika ujirani wote wa Galilaya.
Injili ya Bwana.

You might also like