You are on page 1of 2

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 19
Aprili, 2016 amefungua rasmi Daraja la Kigamboni linalounganisha usafiri wa barabara kati
Kigamboni na Kurasini Jiji la Dar es salaam na amependekeza Daraja hilo liitwe Daraja la
Nyerere (Nyerere Bridge).
Sherehe za ufunguzi wa daraja hilo kubwa na la kipekee kwa Afrika Mashariki na Kati
zimefanyika kando ya daraja hilo upande wa Kigamboni na kuhudhuriwa na viongozi na
wageni mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Balozi wa China
nchini Tanzania Dkt. Lu Youqing, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi
Mhandisi Edwin Ngonyani, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) Mheshimiwa Antony Mavunde, Wabunge na Mameya
wa Jiji na Dar es salaam.
Ujenzi wa daraja hilo umehusisha nguzo mbili za pembezoni na mihimili miwili
inayoshikilia nyaya 36, na daraja zima lina urefu wa meta 680, upana wa mita 32, njia sita za
magari, njia mbili za watembea kwa miguu na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa
2.5.
Daraja hilo limejengwa kwa fedha za ndani na kugharimu jumla ya shilingi Bilioni 254.12
ambapo kati ya fedha hizo asilimia 60 zimetolewa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), na
asilimia 40 zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Kujengwa kwa Daraja hili kutaondoa kero ya msongamano wa magari na usafiri kwa wakazi
wa Kigamboni na wakazi wa katikati ya Jiji la Dar es salaam ambao walilazimika kutumia
kivuko (Ferry) ili kukatiza eneo la mkondo wa bahari ya Hindi ama kutumia barabara ya
kuzunguka kupitia Kongowe lenye urefu wa kilometa 52.
Daraja hilo limefanyiwa majaribio kwa kutumia Malori 44 yenye uzito wa tani 30 na
limethibitika kuwa na uwezo wa kubeba jumla ya tani 1,320 na hivyo linatarajiwa kusaidia
usafirishaji wa mizigo ya kutoka na kuingia katika bandari ya Dar es salaam.
1

Akizungumza katika sherehe hizo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli ameagiza vyombo husika vianze mchakato wa daraja hilo kupewa jina la
"Daraja la Nyerere" (Nyerere Bridge) ikiwa ni kuuenzi mchango mkubwa wa Hayati Baba
wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefanya kazi kubwa ya kuijenga Tanzania.
Aidha, Rais Magufuli amewapongeza wadau wote waliohusika kufanikisha ujenzi wa Daraja
hilo likiwemo Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na
Uchukuzi na wakandalasi kutoka China, na ametaka watanzania wajivunie daraja hilo
kubwa na lililojenga heshima kubwa kwa nchi.
Pia Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa vyombo vya habari vya Tanzania
kuitangaza vyema Tanzania na kuwa na uzalendo wa kweli kwa nchi yao badala ya kubeza
kazi nzuri zinazofanywa ndani ya nchi kwa manufaa ya watanzania.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Jiji la Dar es
salaam Bw. Wilson Kabwe na kuagiza vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi dhidi ya
tuhuma zinazomkabili za kusaini mikataba iliyosababisha serikali kupoteza mapato.
Dkt. Magufuli ametangaza uamuzi huo wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa daraja la
Kigamboni, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Paul Makonda kumueleza
kuwa amebaini upotevu wa shilingi Bilioni 3 uliotokana na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es
salaam Bw. Wilson Kabwe kusaini mikataba ya ukusanyaji mapato ya Kituo Kikuu cha
Mabasi Ubungo kwa kutumia sheria iliyopitwa na wakati, na pia ukusanyaji wa tozo za
uegeshaji wa magari ndani ya Jiji.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
19 Aprili, 2016

You might also like